Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 7, 2017

DUWA LA KUKU -8Wakati kijana ametoka nje, mzee mmoja akaona asipoteze muda, akasema;

'Ina maana hutaki kukiri kosa, wakati mkeo kasema kathibitisha hayo na kasema yeye ana ushahidi mpaka wa mkanda wa video,…sasa unataka nini mwanangu, unataka tuone madhambi yako, ayaonyeshe hapa mbele yetu,….’akasema baba yake.

 Mbaba akatikisa kichwa akionekana kusikitika,hakuna aliyejua dhamira yake ni nini..na machozi yalikuwa hayafutika machoni, na hakuna aliyejua kwanini aliyatoa hayo machozi.,machozi ambayo yalimuathiri sana kijana wake, kwa jinsi alivyoonekana akimuangalia baba yake kwa macho ya huruma.

‘Wazee wangu mimi sina cha kusema,….’akaanza kuongea na mara mlango ukafunguliwa na waliatarajia atakuwa kijana wao, lakini aliyeingia alikuwa mtu tofauti,…..

Tangia awali, walitaka kikao hicho kiishie kama familia, na hakukutakiwa mtu mwingine aje, walimuhusisha binti wa kazi kwa vile naye analifahamu hilo tatizo na kwa namna nyingine yeye ni mhanga wa hilo tatizo, …akachukuliwa na yeye kama miongoni mwa familia.

‘Haya tuyaongee kama familia, tuna imani kuwa hakutakuwa na mtu wa kuja kutuingilia, kwahiyo mtajua wenyewe jinsi gani akija mgeni mtaweza kumuomba kuwa aje siku nyingine au…mtajua wenyewe….’hiyo ilikuwa kauli yam zee walipoanza kuongea.

‘Hatutarajii kuwa na mgeni…’akasema mama mwenye nyumba.

Sasa mlangoni anaingia mgeni, na mgeni huyo sio mwanafamilia,…itakuwaje sasa….

Tuendelee na kisa chetu…

***************

‘Kiongozi umekuja,…’aliyesema hivyo, alikuwa baba mwenye nyumba, huku akimuangalia mgeni huyo kwa mashaka, hakutarajia ugeni huo, na hakujua kwanini mtu huyo amefika, lakini mgeni ni mgeni, hata kama hukumtarajia, na sasa keshaingia ndani mtafanyaje…

Wakasalimiana, na wazee nao wakawa wanamuangalia mgeni huyo kwa shauku, na kuona jinsi gani wenye nyumba watamuondoa, ili waweze kuendelea na kikao chao, na hawakujua ugeni huo una maana gani, hata mama mwenye nyumba, akawa anamuangalia mgeni huyo kwa namna ya kujiuliza….

‘Naona wote hamukunitarajia…, macho yenu yanaonyesha kila kitu, niwaombe radhi tu, kuwa nimefika, na ujia  wangu ni mguu wenu, na mguu wa kikao hiki…na nilishaambiwa kipo kikao, na niliombwa nije mapema, tuendelee nikiwemo, lakini mnajua tena, majukumu, ukitaka kulifanya hili kunatokea hiki,…na mtajiuliza ni nani kanialika niwepo kwenye hiki kikao… lakini ujio wangu umetokana na kijana wenu, alinipigia simu, ….’akasema na wote sasa wakatulia, maana kijana yupo nje, na yeye ndiye alitakiwa kuulizwa ni kwanini akafanya hivyo.

‘Kijana wenu aliwahi kidogo kunielezea tatizo fulani a humu ndani,…na leo akanipigia simu mapema sana, akanielezea mambo yalipofikia, ambayo sasa, amehisi yanaweza kuleta matatizo kwenye familia yake, …’akatulia.

‘Sisi ndio tunafunga ndoa, lakini mara nyingi wanandoa wanafikia kubaya, na badala ya kurudi kwa wale waliofungisha ndoa, wao wanachukua hasira na kuivunja ndoa hata bila ya kutushirikisha, na huenda wangelitushirikisha, tungeliweza kutatua tatizo,…’akatulia

‘Kijana anakiri kuwa kafanya kosa, kunielezea hayo, na hajui wazazi wake watamfikiriaje, lakini ameona hakuna jinsi nyingine ila mimi niwepo nije nishirikiane na mababu zake, kulitatua hili tatizo..aliniuliza je alichofanya ni sahihi kama kakosea basi, ninyamaze tu kimia…mimi nikimwambia, mimi ni kiongozi wa dini, na moja ya kazi zangu ni kuwasaidia waumini wangu, na sio waumini wangu tu, na hata wale wanaoamini kuwa mimi kama kiongozi wa dini nitaweza kuwasaidia…’akatulia.

‘Unajua kuna mambo mengine hayana matibabu ya kihospitali, lakini ni maradhi, ila hayatambulikanai kama maradhi, na mambo hayo hayana ujanja ujanja wa kibinadamu, na hayana ujanja ujanja wa kishirikina, au uganga wa kienyeji, matibabu yake ni ya kiroho..'akashiko sehemu ya moyo.

'Na kwa alichosema kijana japokuwa sio kwa uwazi,...naliona jambo hili linahitajia, dawa ya kiimani zaidi, ..kuzisafisha nafsi zetu zaidi,...ili dawa hiyo ya kiroho iweze kupenya ndani... unajua kuna mambo tupende tusipende, yanahitajia nguvu za mola wetu,...na  hatuwezi kufanikiwa kama hatujamfahamu mola wetu aliyetuumba, ambaye wakati mwingine anatupatia mitihani ya kutupima imani zetu, sasa kama huna imani ndio hapo unakimbilia kukufuru.....'akatulia, na kwa muda huo alikuwa bado kasimama.

‘Mimi kila siku napita hapo nje, nawasalimia, na kijana wenu huyu amekuwa ni mwanafunzi wangu, na najua hata kuja kwake hadi kuwa mwanafunzi wangu, ni kwasababu ya matatizo yaliyopo ndani ya familia yake,..hakuwahi kunieleza hayo bayana, lakini maswali yake mengi aliyokuwa akiniuliza yalijionyesha hivyo, ….kuwa kwenye familia yake kuna tatizo, sijui kama ni  kweli au si kweli..?’ akawa jana anauliza.

‘Ni kweli kiongozi, lakini hatukuwa tumefikia uamuzi wa kuyaweka matatizo yetu hadharani, tulitarajia kuyamaliza kifamilia tu…’akasema baba mwenye nyumba.

‘Safi kabisa, uwe na amani kuwa hilo tatizo limefika kwangu, na halitakuwa la hadharani, bali tatizo hilo litamalizwa ndani ya familia, na wanafamilia wenyewe, mimi nitakuwa kama mshauri wa imani, wa kuzisafisha nafsi zetu….’akatulia.

‘Karibu ukae…’aliyesema hivyo alikuwa mzee

‘Mimi naona raha nikiongea huku nimesimama…najihisi nipo kwenye majilisi yangu,…labda niwaulize, je nimewaingilia, na labda sihitajiki kwa sasa, maana ujio wangu nimeufanya kwa kushtukiza , baada ya kijana kufika kunipigia simu akionyesha yupo kwenye majonzi makubwa,..alikuwa kama analia kwa suati yake,  kwa vile anahisi baba na mama watafikia hatua ya kuachana, kitendo ambacho kwa kauli yake kitamfanya asiwe na amani tena hapa duniani…’akatulia

‘Mh…kwa vile umefika, na tunachotaka kukifanya hapa ni kuweka mambo sawa,..na itakuwa ni vyema ukitusaidia pia, kwani nyie mumejaliwa elimu hiyo ya dini, na ndoa ni nusu ya dini..sisi tulikuwa tukiangalia upande wa nusu nyingine, na sasa tunaona umefika basi utusaidia kwenye hiyo nusu nyingine ya upande wa dini..sisi wazee tunaona itakuwani heri kwetu….’akasema mzee.

‘Hewala…sasa labda mimi nikae, nisikilize muendelezo wake, na ikibidi na mimi nitaingilia katim niwie radhi wazazi wangu, maana wazee nyie ndio tunaowahitajia kutuongoza kwa kupitia hekima zenu…’akasema

‘Hapana, wewe sasa ingia moja kwa moja,..tunakuachia uongozi,...ila kwa kifupi ni kuwa wanandoa hawa wamefikia sehemu hawaaminiani tena..., na chanzo, kwa maelezo ya haraka ni kutokana na kuhisi kuwa huenda baba mwenye nyumba ana mahusiano na wafanyakazi wa ndani, ..naona niseme moja kwa moja hivyo, japokuwa tulikuwa hatujaingilia huko..kwa maoni na kauli ya mama mwenye nyumba ndio hivyo, yeye anahisi huenda mume wake anamsaliti,….’akasema mzee.

‘Anamsaliti kwa kupitia wafanyakazi wa ndani au sio…?’ akauliza kiongozi wa dini.

‘Sawa kabisa,…kwa kupitia kwa wafanyakazi wake wa ndani, hatujaweza kupata nyongeza kuwa ni kwa kupitia kwa wafanyakazi wa ndani tu au kuna wengine, ndio tulikuwa tunaelekea huko katika kudodosa dodosa, na kiukweli hatukutaka kuyafahamu yote hayo, tulipendelea kuwe na suluhu bila kupata mambo hayo kwa undani wake, haina haja, au sio mzee mwenzangu,…’akasema mzee na mzee mwingine akaongezea kwa kusema;

‘Ni kweli, jingine la ziada ni kuhusu hao wafanyakazi wa ndani, utaona hiki kiao kilikuw cha kifamilia, lakini humu yupo huyo mfanyakazi wa ndani, yeye kaingia humu moja kwa moja kwa vile, hao mabinti ni mayatima, wametokea kwenye familia zenye mitihani ya matatizo mbali mbali na kuwa wafanyakazi humu ilikuwa ni pamoja na kupata msaada awe kama mtoto wa familia, kwa namna moja au nyingine..’akafafanua huyo mzee mwingine.

'Oh...ni vizuri sana kama wanafamilia wengi wangelifanya hivyo , kila mwenye uwezi amchukue yatima, au wale wasiojiweza waweze kuishi nao, wawalipe kama wafanyakazi lakini pia wawachukulie kama watoto wao, hiyo ingeleta baraka kwenye maisha yetu, na mola angelikuwa radhi na sisi....'akasema kiongozi wa dini.

'Lakini sasa hilo limeleta mtihani...'akasema mzee na kiongozi wa dini akasema;

‘Basi vyema tuone tatizo hilo ni nini, au mumeshaliona taizo limetokea wapi...?' akauliza kiongozi wa dini.

'Sisi tulitaka tutumie hekima za uzee, tuachane na msigishano, wao kwa kila mmoja wapo, ajione kakosea, maana katika kudodosa dodosa tumeona madhaifi yapo kwa pande zote mbili, kuacha hilo la kutokuaminiana..lakini kwanini wasiaminiane, tumeona kwa haraka kuwa kuna matendo waliyaruhusu na huenda ikawa ndio chanzo...'akasema mzee.

'Mhh...lakini kwa vyovyote iwavyo, kuna hili la mayatima, hawa watu wana kosa gani, ...hapo naanza kupata kichefu chefu, labda tuendelee ....'akasema kiongozi wa dini.

'Kifupi hapa kuna tatizo, na ni nyeti kidogo,…kwanza ni tatizo la ndoa, lakini pili ni haki za mayatima, ni kwasababu hiyo, ndio maana na sisi kama wazee likatuvuta na sisi tufike hapa kwa haraka, kabla adhabu ya mungu haijafanya kazi, ….maana japokuwa sisi sio wataalamu sana wa imani za dini, lakini uzee wetu unatupa hekima ya kuliona jambo hili kuwa ni kubwa, kuliko wenyewe wanavyofikiria..

‘Mfanyakazi wa ndani ni sawa na mfanyakazi mwingine maofisini, lakini hawa wametunikiwa mtihani mwingine mkubwa wa uyatima, binti huyu hapa, baba na mama yake wamefariki, na zaidi, kama nilivyosikia hali yao ya kiuchumi ilikuwa mbaya, na ninaweza kudiriki kusema kuwa walikuwa kwenye kundi lile la masikini..sasa ije itokee wanatendewa madhila mengine kama hayo tuliyoyasikia, inaumiza sana….’akasema mzee

‘Mzee samahani, unaongelea kuhusu huyu binti …au kuna mwingine kauli yako inaonyesha kuwa sio binti mmoja au..?

‘Yupo mwingine, lakini hayupo hapa kwa sasa, ila tulimweka tayari afike akihitajika, ili kutoa ushahidi, ikibidi, …

‘Na yeye sifa zake ni hizi hizo..au ?’ akauliza kiongozi huyo.

‘Ndio..kabisa, nimewafuatilia maisha yao huko nyuma, nimegundua kuwa wote wapo hivyo hivyo…’akasema mzee

‘Mungu ni mkubwa….’akasema huyo kiongozi wa dini.

‘Sasa kwa ujio wako, tunakuomba uliangalie hili tatizo kwenye uwanja wako, hasa kwenye nusu yako imani ndani ya ndoa, kama mlivyotuambia ndoa ni nusu ya dini, …..au sio, sasa utusaidie hapo, tutalitatuaje hili jambo, maana lina utata mkubwa sana..baba mwenye nyumba mpaka sasa hajataka kukubali shutuma hizo, hatujui, ni kweli au si kweli, japokuwa mama ana ushahid mnzito sana…’akasema mzee.

‘Ushahid wa kivipi..?’ akauliza kiongozi wa dini.

‘Mama mwenye nyumba anasema yeye ana uhakika wa shutuma zake kwani ana ushahidi wa watu na mwingine upo kwenye vifaa vya kisasa, yaani ana video…’akaambiwa.

‘Mungu ni mkubwa….’akasema huyo kiongozi

‘Sasa sijui tuanze vipi, maana sisi tulifikia sehemu ya kumuomba baba mwenye nyumba, akiri kosa na atubu hayo makosa, ili mambo yaishe kwa amani…, ili tusipekenyue pekenyue mambo yao ya ndani, haina haja tujue kila kitu kilichotokea, haina haja tukajua siri zao za ndani, siri zao za kindoa,…tumemuomba mume mtu aliokoe hilo kwa kukiri kosa na kutubu, na kuomba msamaha yaishe…’akasema mzee.

‘Kwa namna hiyo kumbe mlishafika sehemu nzuri tu ya kuhitimisha hayo, ili na mimi nije kutoa maneno ya mungu, ili kuwaweka sawa, au sio.....'akasema na kumgeukia baba  mwenye nyumba na kusema;

'Kumbe kwahiyo baba mwenye nyumba ndio uwanja wako wa kukiri na kutubu, na hatimaye kumuomba mwenzako msamaha..kusameheana ni jambo jema sana, na hakuna kitu kibaya kama kukaa mkiwa na kinyongo, chuki, na visasi, hivyo ndio vinazidisha maradhi, maradhi ya moyo,..na shinikizo la damu, tusipende kufikia hapo, tuwe huru kusamehe, tuweze huru kuomba msamaha, na kwa kufanya hivyo, upendo utazidi, na neema za mola zitakuwa nyingi tu....sasa baba mwenye nyumba niambie...au wazee nimekwenda haraka kidogo…?’ akauliza kiongozi wa dini.

‘Ndio hivyo kiongozi, tuendelee…’akasema mzee, na kiongozi wa dini, akamgeukia tena baba mwenye nyumba, akamuuliza;

‘Je mkuu wa familia, upo tayari kwa hilo...?' akauliza

'Kwa lipi, la kukiri au kuomba msamaha...?' akauliza

'Kwa yote ..si mumeshamaliza au..?' akauliza

'Hapana labda umeshtukiziwa tu, hatujamaliza, ...'akasema

'Kwahiyo unataka kusema nini, kuwa  shutuma hizo sio za kweli, na hapo tayari kukiri kosa, ukatubu, na kumuomba mwenzako msamaha kuwa hutarudia tena, na mkayasahau yaliyopita mgange yajayo..kwa upendo na furaha, kwanini msifanye hivyo mkakumbukia enzi hizo, na watoto wakawa na amani, au mnafurahia hivyo watoto wanavyoumia, wakiwaona hamuishi kwa amani?’ akaulizwa baba mwenye nyumba.

Baba mwenye nyumba hakutaka hata kutulia sasa akasema ;

‘Hizo shutuma sio za kweli, na siwezi kukiri kosa ambalo sijalifanya, …sio haki na imeniuma sana kushutumiwa jambo ambalo silijui, na kwa vile limefikia hapo, mimi kama mume nataka kuusikia huo ukweli, auseme, maana sasa nahisi nataka kupandwa kichwani…’baba mwenye nyumba akasema nakuwafanya wazee wote wawili wagune.

Na mama mwenye nyumba akacheka, kicheko cha dharau fulani hivi, na mimi pale nilipokaa, nikawa najiuliza ni kwanini baba mwenye nyumba huyu afikie kusema hivyo, kwanini asikubali tu, mambo yakaisha na hizo shutuma na mambo yao ya ndani, yakafichika.

‘Oh, samahani kidogo, mimi nilijua mumeshafikia muafaka, mbona sasa yaonyesha ni kama vile tunaanza, wazee, mumelisikia hili, msije mkafukia fukia bora liende,, hili la shutuma, hili la kukiri kosa, naona bado haliwekwa sawa, ...kwa za baba mwenye nyumba au mimi nimekuja na kuchochea fitina...'akasema kiongozi wa dini.

'Hapana kiongozi sisi tulinza kumuhoji baba mwenye nyumba ili tuone msimamo wake, tukamweka sawa, na tulitajia kuwa tungelifikia muafaka, sasa naona imekuwa tofauti na muono wetu...'akasema mzee.

'Mnajua, watu sasa hivi wanapupia kwenye kusikiliza maneno ya kusikia, ...kauli za kusikia tu, watu wanachuklia kuwa ni kweli, ni hatari namna hii, sisemei hapa, au kuhusu hili, ila kiukweli kiuhalisia watu wanapenda sana kuhitimisha mambo yao kwa kauli za kusikia, ....tutahukumuwa kwa hili, sio vizuri usikie jambo na wewe ulihalalishe kuwa ni kweli....'akatulia.

'Naomba mnielewe hapa, sio kwamba nimesema hivi kwa veile eti hili tatizo ni la kusikia tu, hapana, natoa u kama angalizo kwetu sisi sote, na naomba hili angalizo lisije kuwa ni kikwazo cha kuusema ukweli, sawa mama mwenye nyumba....'akasema kiongozi.

'Mimi nimekuelewa sana, ndio maana kabla ya kulisema hili nilihakikisha kua nina ushahidi, na nilishafanya uchunguzi wa kutosha, ...sina shaka  na hilo...'akasema mama mwenye nyumba.

'Lakini baba mwenye nyumba, unasema hujafanya , na shutuma hizo zipo mbali na wewe, je mnataka kulimalizaje hili, maana kuna njia rahisi tu, ya kukubaliana na kupotezea hayo yaliyopita, nna ni heri kwenu,...'akasema

'Hapana, ..yeye kadai kuwa hana shaka na hilo, ina maana yeye anasema kuwa ana uhakika na shutuma zake, mimi nasema ni uwongo, hana uhakika, ni uzushi wa kusikia tu...siwezi kukubaliana nao,…’akasema baba mwenye nyumba.

'Wazee mbona ...kumbe ilikuwa bado hamjaafikiana, na naona kuna ugumu wa kukiri kosa, sasa tufanyeje...?' akauliza kiongozi


‘Ndio maana tunakuomba wewe utusaidi hapo..tulitaka tutumia nguvu za wazazi, maana sisi ni wazazi wao, tunaweza kuhukumu, na kutumia rungu letu la wazazi,  tukayamaliza kwa nguvu, lakini je itakuwa ndio mwisho wake..’akasema mzee

‘Mtakuwa hamjamaliza tatizo, kwa hali hii, mngeliondoka hapa huku nyuma watu wanashikana mashati, na zitakazoumia ni nyasi,…’akasema kiongozi wa dini

‘Sasa tusaidie…’wazee wakasema

***********

Kiongozi wa dini akamgeukia mama mwenye nyumba, na kusema;

‘Mama mwenye nyumba, na baba mwenye nyumba pia, katika mahusiano, ya mke na mume muwe makini sana, kwenye kutoa shutuma, …maana kama utamshutumu mwenzako kwa kosa ambalo hajafanya, ni dhambi kubwa sana , kwahiyo uwe makini sana,…na umakini huo utapatikana kwa nyie wawili kwanza kuelezana ukweli, kuwa mimi nakushuku hivi je ni kweli, na mwenzako ajitetee,..la sivyo, ndio tunapitia sehemu kama hizi…’akasema mkuu wa dini.

‘Lakini muwe makini sana kuchunga ndimi zenu, maswala kama hayo ya kushutumiana, na matatizo ya ndani kabisa ya ndoa, yasitoke nje, ikawa mnatanagaziana ubaya wenu kwa watu wengine, hilo ni kosa kubwa maaan hamjui ni nani atalipokea kwa wema, au kwa ubaya..sasa ni hivi, nikuulize wewe mama mwenye nyumba je una uhakika kuwa shutuma hizi ni kweli..?’ akauliza kiongozi huyo.

‘Nina uhakika….’akasema mama mwenye nyumba.

‘Mtihani….’akasema mzee mmojawapo.

‘Mtihani kweli…’akasema mzee mwingine.

‘Je hampo tayari, kusameheana bila ya kuingilia undani wa tatizo lenyewe, yaani kila mmoja akiri kosa, na amsamehe mwenzake, ili yashe, na muendelee na maisha ya ndoa kama kawaida, maana mengine yanatokea kama mtihani,na hapo ndipo shetani anapata mwanya wa kuleta fitina zake…?’akauliza kiongozi wa dini.

‘Mpaka ilipofikia hapa, hakuna kurudi tena nyuma, nataka ukweli ubainishwe la sivyo yeye akiri kosa, ili yaishe, lakini yeye kang’ang’ania kuwa sio kweli, ….mimi nilikuwa tayari kuyasamehe, lakini kwa hatua ilipofikia, mimi siwezi kusamehe tena,…kwasababu yeye anaona kuwa mimi ninamsingizia, nisimsingie ili iweje,….kwa hilo mimi sina jinsi , nitaanza kutoa ushahidi wangu, na kwsababu imefikia hapo, mimi nitajua la kufanya baada ya kutoa huo ushahidi wa kuonyesha uchafu wake…’akasema mama mwenye nyumba.

‘Unaona anavyonitishia, na ndio maana mimi sitaki kukubali kirahisi, najua ananitega,…ningelisema nikubali tu bora yaishe, lakini je ana dhamira gani baada ya hilo, kwa vile mimi namfahamu sana alivyo, basi mimi siwezi kukubali tu kwa nia ya kukubali, ili tu yaishe, hapana,..yeye sasa autoe huo ushaidi wake…nipo tayari kwa lolote lile…yeye si ana ushahidi autoe, ….’akasema baba mwenye nyumba akimkazia macho mke.

‘Kwa hali hiyo mpo tayari tuanze kuingilia mambo yenu ya ndani, ina maana mpo tayari mambo yenu ya ndani yawekwe hadharani, ujue baba mwenye nyumba mkeo kasema ana ushahidi wa watu na video, na watu watasema kwa vinywa vyao kwa hayo waliyoyaona au kutendewa, watu ni watu sio wote wenye nia njema kwenu, na video itadhirisha hata yale tusiyoyataka kuyaona,…huoni kuwa ni aibu kwako…?’ akaulizwa,

‘Ni aibu kama nilifanya, ni aibu kama shutuma hizo ni za kweli, lakini kama ni za kutengenezwa tu.., wenyewe mtajua la kufanya, ila kwa hatua hii basi na mimi nipo radhi nisikie huo ushahidi wake,……itakuwa ni vyema ili hatima ya haya yote ijulikane, mimi nashindwa kuelewa kwanini iwe hivyo, nimetoa machozi hapa, sikuweza kujizuia, maana mimi sijui hayo yametokea wapi, mangapi nimekuwa nikiyavumilia, ….sitaki kuongea mengi, ila namuomba mke wangu atoe huo ushahidi…’akasema.

‘Ndugu zanguni, maswala ya ndoa ni rahisi sana, kama wana ndoa wenyewe watakuwa radhi kukubaliana, na kukubaliana ni kuelezana mambo yao bayana, uzito unakuja pale kila mmoja anaposhikilia lake la moyoni, ubabe na kudharauliana vikatawala, na mambo hayo ya ubabe, na dharau, ni sumu ya ndoa, …niwaambie kitu, mwenyezi mungu alipanga hili la ndoa liwe ni raha kwa wanandoa…, kusaidiana na kuvumiliana iwe ni nyenzo ya kufikia malengo ya kimaendeleo, na hatima yake ni upendo, wenye kuleta neema,…sasa kama raha haipo na hakuna masikilizano ndoa zetu zitakuwa sio ndoa tena bali ni ndoana…’akasema kiongozi wa dini.

‘Mimi kwa kuliingilia hili kati…, sikupendelea hilo la kutoa ushahidi na kila kitu, nilitaka kwanza tuone chanzo cha tatizo, maana huko inawezakena ikawa ndio sababu kubwa sana, na haya mengine yakawa ni madhara ya hilo tatizo….ndugu zanguni, ndoa ni kati ya mke na mume wengine tunasaidia tu kuhakikisha wana ndoa wanafanikiwa kwenye malengo yao…, na tunashiriki kwasababu ya udugu, au ujirani mwema tu….nyie wawili ndio mnaoweza kuijenga ndoa yenu au kuibomoa ndoa yenu, na msikubali kamwe kuivunja ndoa yenu kirahisi hivyo….

‘Lakini imenisikitisha sana kuona kuwa ndoa yenu imevuka mipaka na kuvunja maagizo ya mwenyezimungu kuhusu kuwatendea wema mayatima, na kuwasaidia masikini, ..hapo mimi kama kiongozi wa dini, inabidi niliingilie kati na nione ni kwanini ikafikia huko, kwanini msiwaonee huruma hawa waliokutwa na mitihani hiyo, mayatima na masikini wametajwa sana kwenye vitabu vya mungu, kwanini, kwasababu wao kama wao hawakulipenda hilo, sasa tuziwaongezee mzigo, bali tuwasadie kuwapunguzia huo mzigo….’akatulia.

‘Je matatizo haya yalianzaje….?’ Akauliza na mama mwenye nyumba sasa akaomba yeye aanze kuongea, na baba mwenye nyumba naye akataka yeye aanza kuelezea..na kiongozi wa dini akasema;

‘Hebu kwanza tumsikia mlalamikaji, mama mwenye nyumba, yeye alianzaje kuliona hili tatizo, ili tuone kama ndio chanzo cha tatizo au la….’akasema kiongozi wa dini, na mama akaanza kuongea.

NB: Leo jamani  naishia hapa ili msabe-sabe vyema!

WAZO LA LEO:  Ni kosa kubwa kujiona wewe upo sahihi kwa kila jambo, na hata kama wewe ni kiongozi, au mkuu wa kaya, au bosi, inatakiwa uwasikilize na wengine waliopo chini yako, kuwa na wao wana mawazo gani kuhusiana na hoja au jambo linalizungumziwa. Kuna mambo ambayo sio ya kisayansi, ni mambo ya nadharia tu, mambo ambayo kila mtu ana hoja zake, ili kufikia lengo. Kama kiongozi uwe ni mwepesi kutoa uwanja wa mawazo, hata kma unajua hitimisho la mawazo hayo ni lipi. Usiwadharau wale waliopo chini yako, kwani ukiwapa nafasi ya kutoa mawazo, unakuwa umewashikirisha kwenye lengo, na kwenye utekelezaji kila mmoja atajiona anafanya kile alichokubaliana na wenzake.

Soma na hiki kisa, kilikuwa miongoni mwa visa vizuri sana:


http://miram3.blogspot.com/2014/01/mkuki-ni-kwa-nguruwe-65-mwisho.html

Ni mimi: emu-three

No comments :