‘Niambie mke wangu nipo tayari, kukubalia
lolote lile, najua nimekukosea sana mke wangu..., na sitaki niendelee kukukosea, nataka
nikuonyesha kuwa mimi ninakupenda sana mke wangu...’akasema baba mwenye nyumba
akitamani hata kupiga magoti.
Na mke wake ndio akaanza kuongea....
Tuendelee na kisa chetu...
'Wazee wangu, ni kweli mume wangu ana huruma
sana, nilimpenda tokea awali kwa tabia hiyo ya huruma na upole, kwasababu hata
mimi sipo mbali na yeye, na tabia hiyo ya huruma niliyokuwa nayo mimi ndiyo iliyonifanya niwe mbali na wazazi wangu !
Kwanini nasema hivyo, …kwasababu sijui ni
kwanini, wao kwa mtizamo wao, na siwezi kuwalaumu, ndio kawaida ya kibinadamu,
wao wanaamini madaraja ya maisha yapo kuwa kuna watu wa hali ya juu na wa hali
ya chini…na kwamba wao kwa vile wapo juu, kwa jinsi wanavyojiona wao hivyo, marafiki
wao wa kweli ni wale walio sawa na wao, na wale watakao-oa kwao wawe ni watu
wanaojiweza kama wao walivyo…
Kiukweli, sijui ni kwanini tupo hivyo,… kwangu
mimi hilo sikulipenda, hasa nikikutana na watu ambao hwakujaliwa kuwa na uwezo,
najua wengi sio kwa dhamira yao,…kiukweli mimi nikikutana na masikini, mayatima
watoto wa mitaani, naingiwa na moyo wa huruma, najiuliza ni kwanini wao wanateseka
hivyo, wakati kuna watu wana mali, wana uwezo uliopitiliza, …sijisifu ila kwetu
kwa wazazi wangu tuna kila kitu, tunakula na kusaza, wakati huo huo kuna watu
wanateseka…’akasema kwa uchungu.
Hapana mimi sikulifurahia hilo, kwanini
tumwage chakula, kwanini tubadilishe magari kama nguo, kwanini, tunaishi maisha
ya raha sana, wakati dunia hii ni ya kupita tu, sikupenda hiyo hali, mimi nikawa
kila siku naleta watoto wa mitaani, hapo nyumbani kwetu..nawapa chakula
nguo..nawasaidia,…, na hilo liliwakera sana wazazi wangu…sio kwamba nawateta
wazazi wangu, lakini wengi wenye uwezo wapo hivyo. Isjui kama nakosea!
Mimi nilipokutana na mume wangu, tukawa
marafiki, akanielezea maisha yake, nilijawa na huruma na mapenzi yakaanzia hapo,
…nilijua huyu ndiye wangu wa kufa na kuzikana, nilitamani kuwa na mume wa namna
hiyo, mwenye huruma na upendo, ambaye anawapedna wale wasiojaliwa kupata upendo
kwasababu ambazo zipo nje ya uwezo wao, kama mayatima na watoto wa mitaani,
tulikuwa mimi na yeye tunalijadili hili mara kwa mara….
Sasa haya yanatokea usoni mwangu,…yamenipa
fundisho fulani, kuwa sio vyote ving’aavyo ni dhahabu, sio kwamba wengine wote
wanaoteseka wana miyo mizuri, wengine ni kwasababu tu hawajaipata hiyo nafasi,…
mtu akipata hubadilika, huwezi kuamini kua ndio yule wa zamani…mimi sitaki
maisha hayo….’akasema
‘Lakini mke wangu mimi sijabadilika,…mbona
wanasingizia mambo ambayo sio ya kweli….’akajitetea mume wake,lakini yeye
hakumsikiliza, akaendelea kuongea kwa kusema;
'Ndio maana, sasa hivi nataka nipate muda wa kuyatafakari
haya yote, nahitajia muda wa kujipima wapi nilikosea, lakini pia, sitaki
kumkwaza mtu, sitaki kumuumiza mtu, sitaki mtu anione kuwa nafanya haya kwa
vile, hapana, maana sitaki nifanye mambo yenye kumkasirisha mola wangu.
'Ninajua maagizo ya mola wetu ni kusaidiana,
kutendeana wema, kujenga udugu wa kiukweli nk..lakini mitihan ikizidi sana mtu
hukengeuka, hujikuta akiingia kwenye dhambi bila kupenda, lakini pia sio vyema
kujilegeza na kusema nimeshindwa,..hapana mimi bado sijajishindwa,
naji….ninajibidisha ndio maana nikafikia maamuzi hayo ambayo nitayateleza ili name
nipate muda wa kujijongeza kwenye uhalisia.
Baada ya kuyasema haya, nataka niwaambie nini maamuzi
yangu, mume wangu hata kama una matatizo ya kiafya,…labda kama ipo hivyo,
siwezi kukubali tu, maana mimi sina kipaji hicho… au hata kama ulilogezewa kama
alivyodai huyo mdada maana wengi tunapenda kukimbilia huko, hata kama sio …hata
kama kuna njia mbadala, na njia sahihi nyingine, …mimi naamini kuwa mola wetu
anatujua sana sisi tulivyo…, ndio maana akatuelekeza njia hiyo, lakini ….hapa
nilipofika nasita, na inabidi tufanye hivyo….
Mume wngu, nimeipima nafsi yako, japokuwa sina
uwezi huo, ila kwa kile kidogo nilichojaliwa nacho nimekiona kuhusu wewe
ulivyo, japokuwa utapinga,… nafsi yako haijatulia, ina muwashawasha wa tamaa za
kimwili, kama walivyo wanaume wengi, nyie mnakuwa wa kwanza kutuchoka sisi
wanawake, hasa tukianza kuchujuka, ukubali usikubali ndio hivyo…’akasema pale
alipoona mume wake anataka kusema neno.
‘Ni kweli nyie wanaume hamzeeki, sisi wanawake
tunazeeka mapema, ule urembo wetu unatoweka, lakini kwani hayo ni mapenzi yetu,
kwanini mungu alifanya hivyo…najiuliza sana tu, na sio kwamba namlaumu mola
wetu,lakini majibu yapo, ndio maana nitachukua maamuzi hayo, na mtu asije
kuniona mimi ni mtu wa ajabu sana, hapana na mimi ni mwanadamu..
Nataka unielewe hapo mume wangu…, hata kama
utapinga na kujitetea vipi, hili nitakalo kushauri ulifanyie kazi, nilishalifanyia
kazi mimi akilini mwangu kwa uoni wangu, na nipo tayari kulibeba hili , japokuwa
moyoni nitaumia, sikupendelea iwe hivyo,… lakini mimi nayafanya haya kwa vile nakupenda
sana mum ewangu…’akatulia kidogo.
Mimi nayafanya haya kwa vile ninataka wewe
uzidi kuwa na furaha, lakini pia furaha yako isiwaumize wengine… sasa ni juu
yako kulifanya au kuliacha, nimefikia mamuzi hayo baada ya kupiti utafiti mmoja
ya wa njozi, mtu huyo kwa fikira zake na utafiti wake, yeye alisema, ndoto
nyingi tunazoota usiku, ni zile hisia zetu za matamanio yetu ya kila siku, kila
mtu anatamani kuwa hivi kupata kile hata kama uwezo huo hana,….
Mimi sio …mshirikina, na sipendi imani hizo,
ila….kuna mengine unayaona kuwa ni kweli hata bila kupitia huko,
Mtu anataka awe tajiri, au amuoe bint wa
sultan ili hali yeye ni masikini, ataota nini hapo , ni lazima usiku ataota
ndoto zake, kuwa kafanya hivi na vile akafanikiwa, hata kama haitawezekana kuwa
hivyo..maana mipangilio ya mweneyzimungu ina hekima zake, japokuwa sisi
hatulioni hilo.
Sasa kuna kitu nilikiwazia sana, ndoto kama alizosema kiongozi wetu wa dini ,
kuwa zipo …ndoto za matendo, ya kuwa uliwazalo mchana utakuja kuliota kwa
matendo usiku, hata kama mchana ulishindwa kulifanya, basi usiku unaweza
kulifanikisha kwa njia ya njozi, na unatenda kwa matendo, hii ni hatari eti…kwa
mfano , nachukulia tu kama mfano,…je ukimchukia mtu hadi kutamani afe, usiku
utafanyaje,..najiuliza tu ni nini hatima
yake, lakini mungu ni waajabu sana huwalinda waja wake, na haijatokea watu kama
hao wakafanya mabaya kiasi hicho cha kuua,… ila wanaweza kufanya madhambi kama
hayo aliyoyafanya mume wangu, hahaha hapo unajiwekea alama ya kuuliza…’akasema
Naombeni mnivumilie kwa maneno mengi, lakini
nina maana yangu hapo, ili kwa maamuzi yangu msije kuniona nimegeuka kuwa jiwe….
Mume mtu kusikia hivyo, akanyosha mkono kutaka
kupata ruhusu ya kuongea, na mkewe akamuangalia bila kusema neno, na yeye
akasema;
‘Mke wangu, usfikie kunuhukumu kihivyo,…yawezekana
nilifanya ndio, maana ushahidi si unao,…, yawezekana nina matatizo hayo,mimi
sijui....lakini ukizidi kuninyanyapaa, ujue nasikia vibaya sana, najiuliza hta
mimi, kwanini iwe hivyo, kwanini…hizi kwanini zinaumiza mke wangu…kama
tulishakubaliana yaishe, basi, yamekwisha, tuyasahau, na mimi nitajitahidi
kujirekebisha…’akasema.
‘Sikunynyapai, lakini ukweli lazima usemwe, na
ukisemwa kama hivi utakuwekea kumbukumbu ya kujihami kila ukikusudia kufanya
mabaya, ukikumbuka kikao kama hiki, maneno kama hayo, utaogopa,..ndio maana tumeusiwa
kukatazana mabaya na kuamrishana mema, nia ni nini, sio kuhukumu mtu hapo, sio
kujikweza, nia ni kujengeana kumbukumbu za kujihami…unielewe hapo, mimi nimesomea
ualimu na najua ni vipi niwafundishe watu…’akasema mkewe.
‘Ok, sawa, sasa unaonaje ukalisema hilo
ulilokusudia kulisema kwasababu kwa jinsi unavyorefusha maneno unanipa shikizo
la moyo, nashindwa kujua nini dhamira yako unaanza kuniogopesha hata mimi….’akasema
‘Ni kweli, hata mimi nilipata sana shida
kulifikiria hilo…na ni maamuzi magumu kama hayo kwangu mimi, kwa mtu kama mimi,
lakini sina jinsi, na…binti ataelewe tu, na ipo siku atakuja kunielewa kwa
hili, sasa hivi…itakuwa vigumu na huenda akaniona mtu wa ajabu sana.
‘Baada ya kuyawaza hayo yote, nimefikia
maamuzi haya, kuwa hivi sasa, nataka wewe mume wangu, umtafutia huyu binti,
sehemu ya kuishi, umtafutie chumba chake, kwa namna utakavyoweza wewe,
umuwekezee mradi kwa namna utakavyoweza wewe, na hata ukitaka mfunge ndoa, ili
uweze kwenda kwake kwa nafasi, bila kujiiba, si ulimtamani, si ulimpenda, sasa
nataka hilo usilifanye kwa kificho na mimi nipo radhi…’aliposema hivyo, mimi
nilishtuka, nikatoa macho ya kuogopa.
‘Unasema nini mke wangu, unataka kufanya nini,
kunifukuza humu ndani au.?’ Akauliza mume mtu akisimama.
‘Mume wangu mimi sijatamka hilo, na hata siku
moja, japokua niliwahi kutamka kwa hasira, kuwa utaondoka humu ndani, lakini
mimi sijafikia maamuzi ya kuwa tuachane kwa talaka, kutamka kuwa utaondoka humu
ni namna ya kukujenga uelewe wajibu wako, ninachotaka kwa hivi sasa ni wewe
usiwe mnafiki, uweze kuifurahisha nafsi na matamanio yako kwa uwazi,…sijui kama
bado sijaeleweka hapo, maana huyo
unayemfanyia hivyo yeye ni mwanadamu, kwanini umzalilishe na wakati ipo njia
halali, kwanini mfanye kwa siri wakati mnaweza kuifanya kwa dhahiri kwa halali…’akasema.
‘Mimi sijafikiria huko na siwezi kufanya hivyo…’akasema
mume mtu.
‘Hili nimelipanga hivyo, kwasababu gani, huyu
binti nilikabidhiwa mimi, na yupo mikononi mwangu, na mama yake keshafariki, ni
masikini na ni mjane, …na haya yametokea ndani ya nyumba yangu, ndani ya
mamlaka yangu, na mimi wakati mwingine ndiye wa kulaumiwa, huenda nimeshindwa
kumshibisha mume wangu, huenda…sasa hizi huenda….hapana, na zaidi waliomtendea
hayo ni familia yangu, tunahitajika
kuwajibika kwa hilo, lakini pia tunahitajika kuchukua tahadhari..ili yasije
kutokea tena makubwa zaidi ya hilo, maana chuki zinakuja kutokea, na chuki,
hahaha, zinaweza kuotwa usiku tukaja kuuana humu ndani….’akasema.
‘Kwahiyo, mume wangu kaa ufikirie hilo.., ila kwa
huyu binti kuanzia leo, naomba baba, wewe ndio tegemea langu, wewe mara nyingi
umekuwa ukinielewa, haya yakiendelea kufanyika, tukiendelea kumpa muda mume
wangu kuyafanikisha hayo, kwa jinsi yeye atakavyoona ni sahihi, ninaomba huyu
binti aje akae kwako..sikutupii mzigo, mimi bado nitaendelea kumsaidia kwa
kadri niwezavyo,..ila hili saa ni jukumu la mume wangu, sio mimi nitamsaidia,
ila nitahakikisha misaada hiyo inamfikia mlengwa…’akatulia.
‘Hapana mimi siwezi kulifanya hilo, kama
humtaki mtoto wa watu umrudishe huko ulipomchukulia, mimi huyu sijamleta mimi, …’akasema
baba mwenye nyumba.
‘Mume wangu uliahidi kuwa nitakachokisema
utakitekeleza, ahadi ni deni, sasa kazi ni kwako….’mke mtu akasimama.
‘Mke wangu unataka kwenda wapi hili
hatujakubaliana nalo, japokuwa nilikuahidi hivyo….’mume akaanza kulalamika.
‘Mimi nimemaliza, binti fungasha kile kilicho
chako, mtaondoka na baba yangu hii leo....nilishaongea naye hili kabla japokuwa
sikujua haya yatakuja kuwa hivi,…nimuomba kama kutatokea lolote kama hili,
niliwazia hivyo tu, basi huyu binti sio wa kutelekezwa, anahitajia njia
nyingine ya kumsaidia, na njia nyingine ndio hiyo..mume wangu usijivunge,
huyu binti umempenda…’akasema na watu
humo ndani wakataka kucheka,
‘Hapana mke wangu huko umefika siko…hapana, …hayo
ni mawazo yako…’akasema
‘Sisi tutaendelea kulijadi kama mke na mume,
lakini maamuzi yangu ni hayo, leo hii huyu binti ataondoka na baba, na ni
lazima wewe umtafutie njia ya kujikimu huyu bint, ndio ni mimi nimleta, lakini
sikumleta hapa li mumuzalilishe, na adhabu ya kuzalilisha watoto wa watu ni nini…au
hujui kuwa huyu naye ni mtoto wa watu…uwajibike kwa hilo..Baba nakuomba
unisaidie, sikutupii mzigo, naomba unielewe hivyo, tutazidi kuliongea hili na
kulifanyia kazi..’akasema akimuomba baba yake.
‘Aaah, mimi sina tatizo, kuna nafasi kubwa kule
kwangu, atakaa ila naomba iwe ni kwa muda, kama ulivyosema, mume wako
anahitajika kuwajibika, basi atawajibika, au sio mzee mwenzangu..?’ akasema
huyo mzee akimuangalia mzee mwenzake.
‘Eeeeh, yeye atajifunza kwa kupitia njia hiyo,
lakin hilo la kuoa, aah, sijui ni yeye mwenyewe, hapo kuna mtego, lakini kama
hajatulia, tutamsaidia vipi,..ila la kuoa bado sijaliafiki, ila kumuhudumia
huyo binti ni kazi yako mwanangu, na ushukuru kwa hilo, ni wapi utampata mke
mwenye hekima kama huyu…ila usije kulichukulia hili jambo kijuu juu, ikawa ndio
umepata nyumba ndogo,..huu ni mtihani kwako..kama ni kuoa uoe, sio nyumba ndogo,
…’akasema huyo mzee.
‘Nyumba ndogo hata mimi ndio siikubali, ndio
maana nimempa nafasi hiyo, kama anataka kumuoa, amuoe, tujue moja, na kama
hataki anajivunga huku nafsi inatamani, lazima huduma zimfikie huyu binti,, ni
dhamana tuliyokabidhiwa,..ichukulie hii kama ni adhabu kwako kwa kumzalilisha
binti wa watu, na jiulize je kama ulipana begu zikaota, itakuwaje, hapo
iliwazie kwa makini …huyu binti wa watu ana kosa gani, mim inaniuma sana
kuchukua hatua kama hii, lakini najihami, ..hili ni tatizo ..mume wangu
hajijuai tu..na kwa hili hata akija ndugu yangu wa kike humu ndani,, itabidi
nifikirie mara mbili tatu…’akasema.
‘Mke wangu umefikia huko, huniamini
tena…’akalalamika.
‘Sio swala la kuaminiana hapa, imetokea mara
ngapi, huyu ni binti wa pili unamfanyia hivyo, huo sasa ni ugonjwa, ni tatizo ulilo nalo, je akija mdogo
wangu wa kike na yeye ukimtamani, usiku itakuwaje, ….hahaha, sio kwamba nacheka
kwa furaha, lakini hili ni tatizo, na naomba mungu atujali tuwe kulipatia
ufumbuzi wake, bila kufanya makosa ….naogopa sana, tukitoka hapa tunakwenda
kumtafuta dakitari, na …jingine .nitafanya uchunguzi wangu, mungu akipenda, nitakuja kuwapa
matokea yake kama ni lazima…’akasema .
‘Mimi naona hapo tumemaliza…’akasema kiongozi
wa dini.
‘Tunakusikiliza wewe…’akasema mzee na baba
mwenye nyumba akamuangalia kiongozi huyo wa dini, kama vile anasubiria hekima
zake za kumuokoa kwa hilo.
‘Unajau hakuna kitu kigumu na rahisi kama
kutatua kesi ya wanandoa, lakini ugumu wake na urahisi wake unategemea na
wanandoa wenyewe,…mara nyingi, sisi tunatakiwa kuwasikiliza wanandoa, na ni
muhimu kila mmoja ukampa nafsi yake, mimi nimependa maamuzi ya huyu mama wa
nyumbani...'akasema
'Japokuwa baba wa nyumbani anaona ni gumu sana kwake.., lakini hebu
jaribu kulifanya kwanza kama mlivyokubalina hapa ili uone matokea yake, huenda
ni heri kwenu, na tumuombe mungu iwe hivyo, mimi naona utafanikiwa tu,,maana
binti wa watu akiendelea kukaa hapa, na haya yakiendelea kutendeka, ni dhambi
kubwa sana, kazi iliyobakia ni nyie watekelezaji, mzee, ondoka na huyo binti,
ili ulete amani kwenye hii ndoa, na..mambo yakikaa sawa, anaweza kurudi tena,
…’akasema kiongozi wa dini.
‘Lakini wazee wangu, mimi naliona hili kuwa halijakaa
sawa, naona kama mke wangu ananitega…’akasema mume wa familia.
‘Ni kazi yako sasa kuweka sawa hilo wewe ni
mume…liweke sawa lisiwe ni mtego kwako, uwe na hekima za kuitunza ndoa yako, na
hapo hapo,….uhakikishe huwaumizi wasio na hatia kama huyu binti wa watu,
inasikitisha sana kwa haya yaliyotokea, hili sasa lipo mikononi mwako….’akasema
kiongozi wa dini sasa akianza kuondoka.
‘Sawa, sina jinsi, nitafanya kama alivyotaka
mke wangu, lakini sio kwa kuoa,..mimi bado nampenda mke wangu, haya yaliyotokea
najua ni mtihani kwangu,…nitaanza
kuhangaika kumtafutia huyu binti sehemu ili aje kuishi na aanze maisha yake,
nitajitahidi kufanya hivyo, nab ado tutaendelea kulijadili hili mimi na mke
wangu, nawashukuruni sana wazee wangu…’akasema.
*****************
Mimi pale nikabakia nimeduwaa, sikujua ni nini
kipo mbele yangu, sikujua ni nini hatima yangu, sikujua naenda kukabiliana na
maisha gani huko mbele, lakini nikaona ni heri tu ,…maana kama hayo yaliyosemwa
ni kweli, kuwa na mimi kumbe ilikuwa sio ndoto, ..hapo nikajihisi kama
nimepakwa kinyesi, nilitamani nitoke pale nikaoge,…
Lakini pia nikaona ni heri niondoke hapo,
maana chuki zilishaanza kunijaa, kwa huyo baba mwenye nyumba, japokuwa kama
walivyosema sio dhamira yake, pia chuki kwa kijana wake, aliyejifanya mwema
kwangu kumbe usiku wananizalilisha,..
Moyoni nilimuomba mungu anisaidie, kama kuna
kosa kwangu, mimi sijui, ..namuomba mungu aniongoze kwenye njia sahihi, nisiwe
sehemu ya mitihani kwa watu…nikajikuta nalia, nililia lakini kwa kujificha, na
aliyenishtua ni baba wa mama mwenye nyumba.
‘Binti kajiendae tuondoke…’akaniambia, na
nilipoinua kichwa nilijikuta nipo na huyo mzee, wengine walikuwa nje wakiagana,
Baada
ya hapo nikafungansha kile kilicho changu, na tukaondoka na baba mkubwa wa mama
mwenye nyumba, machozi yalitoka sana nilipokuwa naagana na hawa watu, kwangu
mimi pamoja na haya yote, niliwaona kama wazazi wangu…
Mama mwenye nyumba akasema wakati naagana
naye,…
‘Unaondoka, sio kwamba nakufukuza, lakini pia
iwe ni fundisho kwako, najua kuna kitu umenificha, sasa ni juu yako, kama
uliona mume wangu ni mbora kwako, ukamtetea, badala ya kusema ukweli wote, sasa
utakuja kuona ukweli wa kusema ukweli, sikuombei mabaya, ila inatakiwa na wewe
ukaayanze maisha, ili ujue maisha yalivyo na changamoto zake, na najua, hakuna
baya lolote linaweza kutokea huko mbele.., ila likitokea usisite kuniambia, ila
lisiwe kuhusu mume wangu au kijana wangu, kwasababu mwenyewe umekiri kuwa
hawajakutendea mabaya,..sawa..kwaheri..
Sikuweza hata kumuangalia baba mwenye nyumba
machoni au kijana wake, sikuweza hata kuwasemesha, nilipitiliza hadi kwa mzee,
ambaye sasa ndiye atakuwa mafadhili wangu, na safari nyingine ya maisha
ikaanzia hapo…
NB: Tukutana kwenye sehem uijayo, je itakuwa
hitimisho la kisa hiki, au kuna muendelezo wake, ngoja nimuulize msimuliaji je
huko kulitokea nini…kwani wakati ananihadithia hilo, alikuwa kambeba huyo
mtoto, je huyo mtoto ni wa nani
WAZO LA LEO: Dhambi ni dhambi tu, hata ukitenda kwa siri, ni dhambi!!
Iweje tuwaogope wanadamu wenzetu, kwa kuchelea
kuonekana tukitenda madhambi yetu…, tukidhulumu, tukiwanyanyasa, na kuwadhulumu
haki zao mayatima na masikini…, tukiwanyanyapaa wasiojiweza na wazee kwa maneno
ya kejeli kama vile na sisi hatutakuwa hivyo, ..tukiwadhulumu wafanyakazi haki
zao, kwa vile sisi ni wamiliki au ni vingozi tuliopewa mamlaka hayo...nk
Tunasahau kuwa yule aliyetuumba anatuona, hata
kama tumejificha tukitenda hayo madhambi
, tukumbuke yeye aliyetuumba hana mapungufu tuliyo nayo sisi viumbe wake,
anayabaini yote, ya siri na ya dhahiri.
Tumuombe mola wetu atusamehe makosa yetu na
atuongoze njia iliyonyooka.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment