Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, July 12, 2017

DUWA LA KUKU--10


‘Wewe binti uliwahi kuniona nikiingia chumbani kwako usiku…?’


‘Hapana….’ akasema

Binti wa nyumbani akaulizwa na kuambiwa aseme ukweli, yeye akasema hakuwahi kumuona baba mwenye nyumba akiingia ndani , maana yeye huwa anakuwa na usingizi mnzito, japokuwa anakabwa na majinamizi….

Ushahidi huo ukaonekana hauna mshiko…na baba mwenye nyumba akapendekeza yule binti mwingine aitwe, ili atoe ushahidi, mimi niliona ni ajabu , kwanini baba mwenye nyumba awe anajiamini hivyo, inawezekana kweli hahusiki na hizo shutuma, lakini mama mwenye nyumba anadai ana video inayoonyesha tukio zima.

Tuendelee na kisa chetu….

***************
‘Huyu binti mwingine kakataa kuja, lakini sio kitu, tunaweza kuangalia shahidi mwingine, eti mke wangu.. tumuulize nani tena…au, labda kijana wetu , kama na yeye anaweza kuwa shahidi wako…’akasema baba mwenye nyumba,

‘Hapana, ….’akasema mama mwenye nyumba, na kuwafanya watu pale kushikwa na mshangao.

‘Kwanini hutaji kijana wako akahojiwa, yeye aliwahi kuingia ndani, au sio, yeye alikuwa karibu na huyu binti, na huyo aliyekuwepo hapa kabla, basi huenda kuna jambo analifahamu ,…’akasema kiongozi wa dini.

‘Sitaki kumuingiza mtoto wangu kwenye maswala haya ya kikubwa, nina uhakika hahusiki ni ujanja ujanja wa baba yake tu….’akasema mama mwenye nyumba.

‘Basi ngoja nihakiki jambo kwa huyu binti wa sasa kwanza, nataka nikuulize maswali tena machache…’akasema kiongozi wa dini akimuangalia huyo binti….na baadae akaanza kumuhoji…
.
'Mama amesema kuna siku alikukuta umepoteza faham chumbani kwake, ulikuwa ukifanya usafi au sio…?’ akaulizwa,

'Ndio…nilikuwa nfanya usafi nikagundua barua, nilipoisoma ndio nikapoteza fahamu…’akasema.

'Baba mwenye nyumba anasema alikufanyia huduma ya kwanza, ambayo ndio ilimfanya mama mwenye nyumba amuhisi mumewe vibaya…kwa maelezo niliyopewa, je kwa muda wote wakati baba mwenye nyumba anakufanyia huduma ya kwanza ulikuwa huelewi hicho anachokufanyia..?’ akaulizwa.

'Ndio, nilikuwa sielewi kabisa..…wala sijui alinifanyia nini,….’akasema.

'Sasa kwanini ulipozindukana ukakimbia…?’ akaulizwa

'Nilihisi anataka kunizalilisha..kwa vile …hata sijui, unajua mwanaume awe amekukalia juu hivi.., …inatisha, ndio maana nikakimbia….’akasema.

'Alikukalia juu kwa vipi…?’ akaulizwa

‘Alikuwa kapiga magoti, na kuniinamia, uso wake ulikuwa karibu na uso wangu, …ndivyo nilivyoona hivyo, na sikuelewa anataka kufanya nini, ..wazo lililonijia haraka ni labda alikuwa anataka kunifanyia kitu kibaya….’akasema.

‘Sasa kwanini uhisi hivyo, wakati huyo ni baba yako, ni sawa na baba yako…?’ akaulizwa.

'Kwa jinsi alivyokuwa kaniinamia…siweza kuwazia jambo jingine zaidi ya hilo, hata sijui kwanini niliwazia hivyo….’akasema.

'Yaonyesha humuamini baba yako, ..au kuna kitu kiliwahi kukutokea mpaka ukaogopa au?’ akaulizwa.

'Wanaume wote mimi siwaamini, mama aliniusia hivyo..anasema nisipende kuwa karibu nao kihivyo, maana ibilisi ni mkali ukiwa nao karibu na wao hawawezi kujizuia, kuingiwa na ushawishi mbaya…’akasema.

'Sio kwasababu ya hayo yaliyotokea humo ndani, au kuna jambo liliwahi kukutokea, la kukutia mashaka..?’ akaulizwa.

'Zaidi ni hayo majinamizi tu ..mmh, hakuna jambo lilinitokea,…mmmh, mimi sikumbuki zaidi….., ni hisia zilinijia tu hivyo…’akasema.

'Unahisi labda kuna mtu humu ndani anaweza kuhusika na hayo majinamizi au unaamini ni ndoto tu, au kuna mashetani…?’ akaulizwa.

'Hapana, sitakiwi kumuhisi mtu vibaya, na sijui nini, mashetani, hapan, mimi siyajui hayo, …kiukweli mimi sijawahi kutokea na vitu kama hivyo, nasikiaga kuna ndoto za majinamizi ,na dalili zake ni kama hizo, ..hivyo tu…’akasema.

'Chumba chako kipo karibu na kijana, na kijana anasema, mara nyingi amekusikia ukipiga kelele, je na yeye hujawahi kumuona akiingia chumbani kwako  usiku ukiwa umelala..?’ akaulizwa.

'Mhh, hapana, ..awali nilipofika kwenye nyumba hii, ndio yeye alikuwa akinielekeza mambo mengi ya humu ndani, kazi nk…ndio aliwahi kufika siku usiku siku za awali nilipoanza kazi… , nilipofungua macho, nikamuuliza nini kimetokea, amefuata nini ….akasema kanisikia nikipiga kelele, lakini haijatokea tena mimi kumuona akiingia ndani usiku…’akasema.

'Huhisi kuwa anaweza kuwa ndio yeye anayekufanyia hivyo usiku…?’ akauliza.

'Siwezi kumuhisi mtu yoyote vibaya, kama hajanifanyia, na kuhakikisha kuwa ndio yeye, kwangu mimi hayo yote nayaona kama ilikuwa ni ndoto tu…’akasema.

'Sasa ikitokea baya mfano umepata mimba utasemaje..nasema hili kwa vile umesikia mwenzako aliyekuwa hapa awali ilimtokea kama hivyo, akajikuta ana mimba…?’ akaulizwa.

'Mimba!... nitapataje hiyo mimba, hapana kwani ndoto  inaweza kumpatisha mtu mimba!, mmhh, mimi hata sijui...mimba mungu wangu! , iingiaje hiyo mimba....hata sijui…’nikasema sasa nikionyesha mashaka.

 'Ndio hivyo, usiposema ukweli, usije kumlaumu mtu , utafukuzwa humu ndani, na hakuna wa kukusaidia tena….’akaambiwa

'Sasa mlitaka mimi niseme nini zaidi, maana hivyo nilivyosema ndivyo nijuavyo, kama kuna zaidi mimi  namuachia mungu.
***************

‘Ngoja nimjaribu tena huyu binti mwingine labda aliogopa kupokea simu kwa vile yupo na mabosi wake….’akasema baba mwenye nyumba na kuanza kupiga simu tena, na safari hii binti akapokea na wakaanza kuongea na baba mwenye nyumba. Baba mwenye nyumba akaweka spika ya nje ili kila mtu asikie anachoongea na huyo binti, hakutaka ionekane kampanga huyo binti aje kuongea atakavyo yeye.

‘Samahani unaweza kufika hapa nyumbani mara moja…?’ akasema.

‘Nije kufanya nini, mizigo yangu nimeshaichukua, mimi siwezi kufika hapo nyumbani kwenu tena…’akasema.

 ‘Kwanini, ..hakuna tatizo lolote baya,  muhimu kuna kitu tunataka kukuuliza, tunakuomba tafadhali…’akasema na huyo binti hakujibu kitu akakata simu.

‘Siwezi kuja,….kwanza bosi wangu hataki niwe ninatoka toka ovyo, …’akasema

‘Basi tuongee hapa kwenye simu , tukuulize maswali mawili matatu utusadie….’akaambiwa

‘Hapana hata hivyo nimetoka nje kidogo simu ilipoita…, nasubiriwa ndani kuna kazi nafanya, kwaheri….’akakata simu.

‘Huyu bint naona hatuwezi kumpata kwa hivi sasa, nilitaka na yeye aje hapa ili aweze kuthibitisha hili, kwa kauli yake, ili tuyamalize haya mambo kwa amani, nitafurahi turejee maisha yetu ya kawaida, …’akasema baba mwenye nyumba.

‘Kwa hali kama hii sizani kama hilo litawezekana tena….’akasema mama mwenye nyumba.

‘Kwanini mke wangu, mbona hujaamini hilo, niamini mke wangu…unajua wewe ni hisia zako tu, lakini kiukweli sivyo hivyo kabisa, je uliwahi kuingia ndani ukaniona nikifanya lolote baya,..hujawahi, na mengine yote ni hisia zako tu….’akasema.

‘Tatizo lako, unajifanya mjanja sana, unaniona mimi sina akili, mimi sijui hawa mbinti umewapa nini,…hata sijui…na huyu binti angelisema ukweli, lakini nahisi kuna kitu umewafanyia, mpaka wanaogopa kusema ukweli,na huo usiku kuna kitu unawafanyia mpaka wanashindwa kuamuka,…’akasema mkewe.

‘Sasa huko nikunisingiziana uchawi, mimi nifawafanyie nini, na kwa ajili gani, kuna raha gani hapo…mke wangu, hivi na umri huu ninaweza kuanya kitu kama hicho…’akasema.

‘Sio uchawi, sio lazima uchawi, ila kuna jambo uliwafanyia hawa mabinti, haiwezekani itokee siku zote washindwe kuzindukana, na mimi mwenyewe nilikuona ukiingia huko chumbani kwao, …’akasema mama mwenye nyumba na kiongozi wao wa dini, akasema;

‘In maana uliwahi kumfuatilia, akienda huko chumbani kwa hao mabinti, hebu hapo kidogo, tuelezee ulivyomfuatilia na kumuona akiingia huko chumbani kwao na je ilitokea hivyo kwa mabinti wote wawili..?’ akaulizwa.

‘Siku ya kwanza, nilipoanza kumshuku, …’akasema huku akimuangalia mume wake.
************
‘Ilikuwa ni usiku, ghafla nikashtuka kutoka usingizi, nikajiona nipo peke yangu, nikajua mwenzangu labda kaenda kujisaidia, nikasubiria kama nusu saa sikumuona mwenzangu akitokea, nikaamuka na kuanza kumtafuta chooni, alikuwa hayupo, hapo nikaingiwa na mshaka, huyu mtu kaenda wapi..sikuwa na wazo jingine zaidi ya kuwa, labda katoka nje kuna tatizo.

‘Nikataka kuelekea nje, lakini wazo likanijia huenda kuna tatizo chumbani kwa huyo binti, maana tatizo hilo nilishalisikia kutoka kwa mtoto wangu, kuwa huyo binti huwa anapiga kelele usiku,…wazo hilo liliponijia nikaelekea huko chumbani kwa huyo binti….’akatulia

‘Wakati natoka sasa kuelekea huko, nikamuona mume wangu akitokea chumbani kwa huyo binti, na mimi kwa haraka nikajificha na kumuacha apite,..hakuniona, aknipita  na aliponipita tu mimi nikamfuata kwa nyuma hadi chumbani, yeye akapanda kitandani kulala, na kuanza kukoroma, kama vile hakujatokea kitu…’akasema.

‘Hukumuuliza kwa muda huo..?’ akaulizwa.

‘Hapana, sikumuuliza usiku huo, nilimuuliza asubuhi yake, na nikashangaa, akikataa kuwa hakutenda hivyo, nikaona ajabu sana, kwanini akatae, nilipombana sana, akasema, huenda alisikia sauti, maana huyo binti wakati mwingine huwa anapiga makelele, na aliposikia sauti za ukelele,ndio akaenda huko, kuangalia kuna nini,,….’akasema.

‘Sasa kwanini nimekuuliza mara ya kwanza ukakataa kuwa hukufanya hivyo…?’ nikamuuliza.

‘Aaah, unajua kichwa changu kina mambo mengi, nikiamuaka asubuhi huwa nawazia mambo ya kazini, nisamehe tu mke wangu….’akaniambia hivyo.

Kiongozi wa dini, akauliza swali jingine;
‘Na huyo binti ulipomuuliza na yeye  alisema nini..?’ akaulizwa.

‘Alisema hajui…maana alikuwa amelala, ila ni kweli yeye aliendelea kuota kukabwa,….na hajui zaidi…basi kwa vile sikuwa na mashaka sana siki hiyo,  sikutaka kudadisi zaidi, na hiyo ilikuwa siku ya kwanza kugundua hayo mambo kutoka kwa mume wangu, kuwa huwa usiku ana tabia ya kuelekea huko kwenye chumba cha mabinti…’akasema.

‘Je kuna siku nyingine ilitokea hivyo, na ilitokeaje, maana umesema hukuwa na wasiwasi na tukio hilo…?’ akaulizwa.

‘Kiukweli japokuwa sikuwa na wasi wasi na tukio hilo , lakini siku zilizofuatia niliamua kulala kwa kuvizia ili kama nitamuona mume wangu akitoka nimfuatie, au nikisikia kelele kwa huyo binti, mimi sasa ndio niende huko badala ya mume wangu…, lakini hutaamini, nikawa nashikwa na usingizi mnzito, najikuta nazindukana kukiwa ni asubuhi….’akasema.

‘Kwahiyo hukuwahi kumfuatilia na kumfumania mumeo wako, kama ni hivyo kumbe hisia zako ni za kuhisi tu, sio kweli kuwa uliwahi kumfamania mume wako..?’ akaulizwa.

‘Ipo siku moja, nilizindukana kama hivyo hivyo tena,…na nikakuta mume wangu hayupo kitandani, nikasema sasa nitaweza kuhakiki jambo hilo , kama sijachelewa…akilini sio kwamba nilikuwa simuamini mume angu, lakini kutokana na kisa cha mfanyakazi wa awali na yaliyotokea kwake, na tukio hilo lililotokea humo ndani kipindi hiki, nikawa naanza kujenga hisia hizo,…’akatulia.

‘Basi kwa haraka nikaamuka na kuelekea huko chumbani kwa binti, ni kweli kumbe alikuwa keshaingia huko ndani, ..nilipofika mlangoni, nikasikia kelele za kulalamika….’akatulia.

‘Sauti ya nani anayelalamika….?’ Akaulizwa

‘Nahisi ilikuwa ni ya binti,..sikuwa na uhakika sana… ni kama mtu anayeongea akiwa usingizi, ..’sitaki, mimi sitaki…niach, sitaki,…’.vitu kama hivyo…niliposikia sauti kama hiyo nguvu zikaniishia,…nikataka kufungua mlango,…nithibitishe huo ukweli, maana hapo akili ilikuwa kama sio yangu tena,..kwanini asema sitaki, niache, …ina maana kuna mtu kweli anataka kufanya kitu kibaya kwa huyo binti,na ni nani zaidi ya mume wangu…kwa haraka kwa hasira nikataka kufungua mlango,  na ile nashika kitasa, cha mlango, mlango ukafunguliwa kwa haraka…akatokea mtu…’akatulia .

‘Ni nani…mume wako…?’ akauliza.

‘Hapana alikuwa ni kijana wangu…!’akasema, na watu wakaonyesha uso wa mshangao.

‘Oh, kijana wako tena….?’ Akaulizwa na huyo kiongozi.

‘Ndio, kijana wangu, na aliponiona akanishika mkono na kuvuta pembeni, akaniambia…’

‘Huyo binti anapiga ukelele, na baba yupo ndani, anajaribu kumsaidia….’akasema.

‘Oh, mimi nikataka kwenda huko, ili nikasaidie, lakini kwa mshangao  kijana wangu akanizuia na kusema;

‘Hapana mama usiende huko, baba aliwahi kuniambia awali, kuwa mtu akiota ndoto kama hizo haitakiwi kumshtua, na akizindukana akiona watu ni wengi wamemjalia, mtu kam huyo anaweza kushikwa na presha, ..basi mimi nilipomuona baba yupo huko ndani, sikutaka kuwasumbua hata baba hajui kuwa nimefika huko na kuwaona, ….’akasema.

‘Umewaonaje..?’ nikamuuliza hivyo tu.

‘Baba alikuwa akijaribu kumtikisa kidogo huyo binti ili aweze kuamuke, lakini huyo binti alikuwa bado anaendelea kupiga kelele, anagala gala tu,…’akasema.

‘Kelele gani..?’ nikamuuliza
‘Kama anakabwa, anasema sitaki, niachie,…lakini sauti haitoki vizuri, ..kama yakujiuma uma …’akasema, na wakati tunaongea mara mume wangu akatokea huko ndani, na kuelekea chumbani, mimi nikamfuatilia hadi chumbani, na kumkuta ameshalala fofo…, ..kiukweli siku hiyo sikuwa na amani, kwasababu kumbe hata kijana wangu analijua hilo.

‘Ulipomuuliza kesho yake alisemaje?

‘Kama kawaida yake alidai kama ni kweli basi alikwenda huko, aliposikia kelele, na madhumuni ni kuangalia kuna nini kinachomfanya huyo binti apige makelele,…’akasema.

‘Alitamka  hivyo….’kama ni kweli,…’ kwanini asema hivyo, kama ni kweli….?’ Akaulizwa.

‘Ndio alitamka hivyo…, hata mimi nikajiuliza kwanini anasema hivyo, kama ni kweli, ina maana hakumbuki, ina maana gani, nikawa najiuliza sana, ndio nikajiwa na wazo hilo la kuweka video ya kurekodi matukio huko chumbani, nione ni nini kinachotokea maana kufuatilia usiku ilishindikana,kwasababu ya usingizi,..huwa mara zote nilizopanga nifuatilie, najikuta nimelala usingizi mnzito…’akasema.

‘Ukafanikiwa kufanya hivyo….?’ Akaulizwa.

‘Ndio..nilifanikiwa video ilichukua picha vizuri sana…japokuwa, ..kuna …mapungufu fulani, lakini nilichotaka kukiona nilikiona, kwa uwazi zaidi hawezi kukataa akiiona hii video….’akasema.

‘Muongo, …hiyo kanda ya video, itakuwa imetengezwa huko mitaani, sio kweli kabisa, je ilionyesha nini, kuwa mimi ndiye ninayewakaba hao mabint…?’ akauliza.

‘Ni zaidi ya kuwakaba,……ulikuwa unawazalilisha hao mabinti, kwa ushahid huu hapa…’akasema mama mwenye nyumba,a kionyesha hiyo kanda ya video alioyokuwa nayo.

‘Sikubaliani na hilo kabisa, na kwasabau hiyo itabidi uionyeshe hiyo kanda ya video, tuhakikishe, …siwezi kufanya lolote zaidi ya kuwakagua na kumtikisa tikisa ili azindukane….’akasema.

‘Sio kweli..nimeona kwa macho yangu ulichokifanya kwa huyo binti…, ni aibu mume wangu, sikupenda kulisema hili, au kulionyesha,  lakini sasa umenichefua, unataka nionekane mimi ni muongo, mbele ya wazazi wangu hawa,  wakati ni kweli….’akasema.

‘Mimi nipo tayari niione hiyo video,…ionyeshe….’akasema mume wake na mkewe akamuangalia kwa uso wa mshangao, na kusema;

‘Wewe…unataka nionyeshe huo uchafu wako mbele ya wazazi hawa,….’akasema mke wake.

‘Mimi najua hakuna kitu kama hicho ndio maana nataka uionyeshe, sijwahi kufanya kama anavyotamka yeye, ni uwongo mtupu,….’ Akasema.

‘Una uhakika kuwa kanda hiyo ya video inaonyesha kila kitu, ambacho kinadhihirisha kuwa mume wako ndiye anayafanya hayo…?’ akaulizwa

‘Ndio…niliiangalia mimi mwenyewe, nikarududia tena na tena….kiukweli baada ya kuiona hiyo kanda ya video, nikasema basi, ….yale mapenzi niliyokuwa nayo kwake, yakaondoka, na ikabakia chuki, nasema ukweli huo,chuki, sasa haivi namchukia huyu mwanaume …sizani kama hali hiyo ya zamani itarejea tena, sizani….’akasema.

‘Aonyeshe, …kama anavyodai ni kweli, aonyeshe, maana mimi sijafanya hivyo…, lini jamani, …hapana, huo ni uwongo,mke wangu una uhakika na hilo…usiseme kwa kujifurahisha, na usije ukadanganywa na mashoga kuwa utengeze kitu kama hicho ili kunizalilisha, …samahani sana, mke wangu kwa hilo mimi sikuamini….’akasema na wajumbe pale wakaangaliana, na ilikuwa kama hawakupendelea hilo tendo lifanyike, na mkuu wa dini, akauliza.

‘Je kama ikionekana ni kweli, utasemaje ..?’ akaulizwa baba mwenye nyumba.

‘Hakuna kitu kama hicho….sio kweli,…labda iwe ni ya kugushi, lakini kama ni kweli, ilichukua matukio ya ndani, mimi nina uhakika sikuwahi kufanya kitu kama hicho, …jamani mimi nimechanganyikiwa, hapana, mke wangu, tafadhali sema ukweli….’akasema jamaa.

 ‘Wewe unampenda mke wako?’ akaulizwa na kwanza akamuangalia mkuu huyo kwa mshangao, halafu akasema;

‘Sana tu, nampenda sana mke wangu, ni yeye tu na dhana zake potofu…’akasema na wazee na mkuu wa dini wakaangaliana na mkuu wa dini akamuuliza mke mtu.

‘Wewe unampenda mume wako..?’ akamuuliza.

‘Nimeshasema awali, mume wangu nilimpenda sana, na ningeendelea kumpenda, kama angekiri kuwa ana tatizo, lililomsukuma hadi kufanya tendo hilo, maana hata ukiangalia hiyo video, ni kama analazimishwa, …anakuwa kama sio yeye….’akasema
‘Mimi kwa uni wangu, naona sio vizuri kuonyesha kitu kama hicho mbele ya watu, lakini kama mume mtu unazidi kukataa, na mke unaona huo ndio ushahidi wako, basi hatuna jinsi, ila kwa ushauri wangu,..baba mkwe utuwie radhi, mimi na baba yake tutaangalia, na kama ni kweli tutakuthibitishieni huo ukweli…’akasema hivyo.

‘Sawa, ni vyema…’akasema baba mkwe.

‘Aaah, kwanini, mimi nataka wote tuone, ili tubainishe uwongo, mimi najua jinsi gani watu wanavyogushi video, wanachukua mapicha ya watu wengine wanawekeza vichwa, kwenye mapicha hayo,…nataka nije kumuumbua mke wangu,…’akasema baba mtu kwa kujiamini.

‘Hapana, ….mimi na huyu mfanyakazi wenu wa kazi za ndani tutatoka nje…’akasema na wakati wanajiandaa kutoka, mara mlango ukagongwa, na aliyeingia alikuwa yule bint wa kazi wa zamani

‘Mimi nimekuja kufuata muito wenu….’akasema

‘Oh karibu lakini tunakuomba usibirie nje kidogo…’akaambiwa.

‘Hapana mimi sina muda zaidi, ila nataka niseme ukweli, nimeona siwi na amani…’akasema.

‘Ukweli gani..?’ akaulizwa

NB: Bint anataka kumwaga radhi, au kuna jingine


WAZO LA LEO: Mwanadamu ana staha zake, ndio maana sehemu zake nyingine zinaitwa za siri, sio vyema kudhihirisha viungo hivyo vya siri kwa kila mtu, kwa kufanya hivyo unakiuka haki za binadamu. Wengi wamekuwa wakipiga picha za wengine na kuzituma mitandaoni, sio vizuri jamani,…Mwenyezimungu katuwekea mipaka, ya maumbile yetu..kuwa ni nani na nani wanatakiwa kuonana maumbile yao ya siri. Na kuyadhihirisha maumbile ya siri ya watu wengine huko ni kuzalilishana ni dhambi kubwa sana, tutakuja kuulizwa madhambi hayo siku hiyo ya hukumu, kwa kuwakosea wanadamu wenzetu…. Tuweni makini jamani.
Ni mimi: emu-three

No comments :