Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, June 23, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-56


‘Wewe ndio kawaida yako unapenda mizaha mizaha..soda umechelewa kuleta, na bado unanigandisha,….mimi nakwenda ndani, …’akasema huyo mdada akiwa kainamisha kichwa chini, na aliposimama mimi nikajitokeza,..tukawa tunaangaliana uso kwa uso,…

Unajua kushtuka, mimi nilishikwa na mshituko wa aina yake, …nikajikuta nimekodoa macho, …siamini ninachokiona mbele yangu,..kwa maana aliyekuwa kasimama mbele yangu sio mwingine, ni yule mpenzi wa facebook.

Mpenzi wa facebook,…aliyetaja tuonane na yeye nikajikuta makaburini na safari nyingine akanitokea tukapata ajali mbaya…nikaja kuambiwa huyo sio mtu ni shetani, mpenzi wa facebook, tuliyeambiwa ni mtu wa kutengeneza, akiambatishwa na nguvu za giza,..mpenzi wa facebook…oh, sasa huyu hapa yupo mbele yangu.

Tuendelee na kisa chetu…

******************
‘Oh, we-we ni na-niii…?’ nikamuuliza nikishikwa na kigugumizi, mimi sio muoga, lakini kwa hali hii nilijikuta nikishikwa na kigugumiza cha kutokuamini, ..huyu ni mtu au..na kama ni mtu , kwanini nikaambiwa kuwa huyo mtu hayupo katika hali ya kibinadamu.

‘Hahaha,…sasa hivi unajifanya kuwa umenisahau au?…’akasema na kuuliza hakutaka kuniangalia machoni tena, akawa kaangalia upande.

‘Mhh…sina uhakika na wewe, huenda ni mbinu zenu tena hizi …’nikasema.

‘Mbinu gani,… unakumbuka tuliahidiana nini mimi na wewe…, ukasema utakuja nyumbani, hukuwahi kufika,…. ukanidanganya, hiyo ndio tabia yako ya kuhadaa mabinti, eeh,…haya mimi nimekuja mwenyewe,…unasema eti, ni mbinu zenu na nani…?’ akaniuliza.

‘Oh, siwezi ku-kuamini, wewe ni kweli..hapana, ….msitake kunichanganya…’nikasema.

‘Wewe mwanaume, mbona unakuwa hivi, unajua mimi sikuzoea tabia hizo, mimi sio mtu wa…unajua nikuambie kitu,..kama umezoea kuwahadaa mabinti wengine mimi sio aina hiyo,…ina maana yale uliyokuwa ukiniambia kwenye facebook, ulikuwa unanivunga, eeh, ongea kama mwanaume..?’ akaniuliza, nikajaribu kumuangali.

 Oh ndio yeye, sura, ..oh,..jamani, huyo mdada wa facebook,.. katoka wapi, nilishaanza kusahau kuwa kuna mtu kama huyu, nikakumbuka walivyosema kuwa mpenzi wa facebook, walimtengeneza, ..au ni shetani, au…

‘Mbona mdogo wake, …..kaniambia nije huku nitakutana na dada yake..sasa nakutana na huyu mzuka, …sijui, au…hapana hapa kuna jambo, lisilo la kawaida,…’ niliwaza hivyo huku nageuka huku na kule,kumtafuta ndugu yake yule binti, lakini hakukuwa na dalili ya mtu mwingine hapo karibu.

‘Unaonekana una wasiwasi sana, kuna mtu mwingine unatarajia kukutana naye nini, nimekuvurugia dili yako au sio, sema ukweli, napoteza muda wangu,…?’ akaniuliza na mimi kwa haraka nikajibu;

‘Ndio…’nikasema

‘Ndio…msichana au sio, kama kawaida yako,..?’ akaniuliza

‘Mpenzi wangu, …mchumba wangu…’nikasema

‘Eti nini,….Hahaha, nilijua tu, nyie wanaume waongo, ina maana kuniambia kote kule kuwa unanipenda, ilikuwa ni hadaa tu, ukasema hata kulala, hulali kwa kiniwaza mimi, ukawa ukilala unalala na laptop pembeni, tunaangalia, …oh, kumbe ndivyo ulivyo eeh, sasa nimeshakujua…’akasema.

‘Sikiliza kwanza, kipindi hicho nilikuwa sijitambui , sijui ni kwanini, pili, sikujua mchumba wangu kama bado yupo,..nilijua keshaolewa,….au..kwahiyo sikuwa na uhakika, nilipokuona wewe, kwa vile ulikuwa unafanana naye nikajua nimepata badili yake,…’nikasema.

‘Hahaha, …..unanishangaza sana wewe mwanaume,..kwahiyo unataka kusema nini..?’ akaniuliza akionyesha kukasirika.

‘Nikuombe samahani tu, kwa vile mchumba wangu keshapatikana, na nilikuja hapa kwa ajili ya kukutana naye…’nikasema.

‘Una uhakika gani kuwa huyo mchumba wako, yupo tayari kuolewa na wewe, baada ya yote haya…una uhakika gani kuwa hajafahamu kuhusu mpenzi wako wa facebook,…, je nikikuambia nimeshajitambulisha kwake, kuwa mimi ndiye mchumba wako tuliyekutana naye kwenye facebook, utasemaje…hahaha, utakosa kote, halafu utakuja kujuta, …’akasema.

‘Hata kama ….mimi sitajali, ilimradi yupo hai, sitachoka kumsubiria, yeye ndiye chaguo langu, wewe ilitokea tu, na sielewi, maana nilisikia wewe sio halisi..lakini hata hivyo, nashukuru kwa kukutana na wewe, ili nikuambie ukweli, kuwa mimi na wewe basi, sitaki tena mawasiliano na wewe....nisamehe kwa yote, najua nitakuwa nimekuumiza sana, lakini…’nikasema nikitaka kuondoka.

‘Hebu subiri kwanza…unataka kwenda wapi, ..hunijui eeh, ulifikiri, wasichana weote ni wakuchezea, sasa nikuambie kitu, nitakufanya jambo hutalisahau..unasikia…’akasema akitaka kunisogelea, sikutaka aniguse, japokuwa sina imani na imani za mashetani, lakini hapo nilitaka kuwa na tahadhari, nakumbuka hayo yaliyotokea huko nyuma, nikawa nawazia huyo asije akawa shetani kaja kunighilibu.

Alipotaka kunigusa nikaruka mbali na yeye..nikasema;

‘Wewe mwanamke vipi…ina maana ..’nikasema;

‘Subiri , nikuonyeshe kuwa sio wote wana tabia hizo, nataka nikufunze adabu,….’akasema na mimi nikaanza kukimbia..huku nasema;

‘Samahani sana, …nielewe tu, mimi sikutaki tena, na kama unataka kunifanya nini, fanya, mungu atalinda na mashetani, na ubaya wake,  ….’ Nikawa nimeshamuacha mbali,

Na wakati, nipo mbali na huy binti,… mara kwa mbali nikasikia kelele za kushangilia, kelele hizo zilitokea mlangoni mwa nyumba ya hiyo familia ya mzee, kwanza nikajisikia vibaya, kuwa wataniona nimesimama na huyo msichana, kwahiyo nikazidi kukimbia mbali kama nataka kutoka nje ya geti.

‘Hahahaha…….’mara nikasikia mtu akicheka, akiwa anakuja usawa wangu, lakini sikutaka kugeuka, ila nilishajua huyo anayecheka ni nani, ..hicho ni kicheka cha mdogo wake, yule msichana wa kwanza wa huyo mzee.

Nikawa sasa nipo getini, nataka kufungua mlango wa geti nitoke nje,..huyu mdada akanijia na kuanza kuongea..huku bado anacheka,…nikawa sielewi kitu, na aliponikaribia akasema;

‘Umeonaeeh, huyo ndiye mpenzi wako wa facebook, sasa amua moja dada yangu au huyo mpenzi wako…’akasema

‘Kwanini umefanya hivyo..huyu shetani katokea wapi..?’ nikamuuliza

‘Hahaha, eti shetani, sinimesikia wewe haumini mambo hayo,….’akasema

‘Sikiliza, sasa naona umevuka mipaka hivi dada yako angeliniona nimesimama na huyo msichana, unafikiri angelijisikiaje,…na dada yako yupo wapi..?’ akaniuliza.

‘Hahaha….’akacheka, na akawa anaangalia kule mlangoni ambapo nilisikia sauti ya kushangilia, na sikutaka kugeuka kuangalia kule…nikasogea kama kutaka kuondoka, na kitu kikasema niangalie kule mlangoni kabla sijaondoka…kule niliona familia yam zee, wakiwa wamesimama, wakituangalia..

Hapo, sasa sikutaka kusimama tena nikavuta mlango, ufunguke niondoke kabisa eneo hili…na huyu mdada akageuka kuwafuta wenzake huku akicheka, na wakati sasa nimeshatoka nje, mara nikasikia sauti ya docta,…

‘Wewe, mbona unaondoka..?’ akaniuliza na mimi sikumjibu nilikuwa sasa nipo kwa nje, na docta akatoka na kunikabili.

‘Mbona unaondoka, kuna nini kimetokea..?’ akaniuliza.

‘Sijisikii vizuri,….’nikasema hivyo tu.

‘Unaumwa..au…lakini hata hivyo, huwezi kuondoka kienyeji hivyo, …nataka  kukuambia jambo…’akasema akinishika mkono ili anirudishe ndani.

‘Hapana docta, nielewe tu,…mimi siwezi kurudi tena huko ndani, sitaki kuendelea kuwepo tena eneo hili…, nimekutana na mambo ya ajabu huko..’nikasema.

‘Mambo gani…?’ akaniuliza akiniangalia usoni, nikakwepa kuangalia na yeye moja kwa moja, maana huyu docta anakipaji cha kukugundua unawaza nini mkiangalia moja kwa moja.

‘Hata siwezi kuamini,… hivi docta, si ulisikia mwenyewe, kuwa mpenzi wa facebook, ni vitu walitengeneza tu,…na wewe ukasema ni shetani, au sio..’nikasema na docta akaniangalia huku amejaa tabasamu usoni,  akasema;

‘Hebu nikuulize kwanza kabla sijajua ni nini lengo la swali lako, hivi kwa mfano kama huyo mpenzi wa facebook yupo kweli, utafanyaje..?’ akaniuliza.

‘Kwa vipi, kwanza nijue yupo kweli au hayupo..’nikasema.

‘Kwani wewe umekutana naye..?’ akaniuliza akionyesha mshangao.

‘Ndio…’nikasema.

‘Una uhakika…’akaniuliza.

‘Docta, akili yangu ni timamu, sizani kama imerudia kipindi kile cha kuchanganyikiwa…nina uhakika ndio yeye,  nimemuacha punde,…docta sielewi haya mambo, kuna nini hapa..’nikasema.

‘Nakuuliza tena, je kama huyo mpenzi wa facebook yupo upo tayari kuwa naye…?’ akaniuliza, na kunifanya nihisi kuwa docta anajua kinachoendelea, na ya kuwa wanataka kunipima kama kweli nampenda mpenzi wa facebook, au huyo mdada wa hapo nyumbani kwa mzee.

‘Docta unalifahamu jibu langu tayari, siwezi kuwa muasi kiasi hicho baada ya haya yote, sizani kama naweza kugeuka nyuma, nitakuwa sio binadamu mwenye utu, …hapana docta , huyo ni shetani, katokea wapi huyo mdada, au una fahamu haya mambo, mlionana naye wapi mkaamua kuchezea hivi…’nikasema.

‘Hahaha, sasa umeshaanza kuamini hayo mambo, naona akili yako imeshageuzwa, nilijua wewe ni imara, huwezi kutetemeshwa na mambo kama hayo, kwanza nikuulize una uhakika kweli huyo uliyekutana naye ni binadamu, maana unachozungumza hapa, hakipo, huyo mpenzi wa facebook, hayupo..…’akasema.

‘Docta, ina maana huaniamini.. nimekutana naye, nilikuwa naongea naye,..ndio yeye mpenzi wa facebook,....’nikasema.

‘Hebu twende huko ndani, ukanionyeshe,…’akasema
‘Docta,…nimemuacha ndani, na hajatoka, twende…’nikasema na tukaingia ndani tena, na kutembea hadi pale alipokuwa huyo mdada, hatukukuta mtu, au dalili za kuwepo mtu hapo.
‘Haiwezekani…ina maana ni shetani….’nikasema

‘Yupo wapi…?’ docta akaniuliza.

‘Docta,…kwa kauli yako wewe ulisema huyo msichana ni  shetani, na kwa kauli yao mbele ya mahakama wamesema walitengeneza msichana wa facebook, kuhadaa watu ili watimize lengo lao..basi huyo waliyemtengeza yupo mitaani, kama ni shetani basi lipo mitaani,…’nikashika kichwa.

‘Sikiliza mimi ni rafiki yako, niambie ukweli, je upo tayari kuwa na huyo binti, au la…?’ akaniuliza.

‘Binti yupi sasa..?’ nikamuuliza.

‘Niambie wewe…’akasema docta.

‘Docta kuna nini hapa..nahisi kuna mchezo mnanichezea, mimi sio mjinga kiasi hicho,..niambie ukweli docta, kwanza ile familia imetokezea pale mlango, ikawa kama inashangilia,walikuwa wanashangilia nini,…’nikasema na docta akacheka, halafu akasema;

‘Twende tukaage tuondoke maana utachanganyikiwa ..nataka nikakupe dawa za kusafisha akili yako, nahisi haupo sawa, mengine tutaongea huko…’akasema, na sikumbishia, tukaenda kuaga..lakini tukakuta familia wapo wanaongea na watu wengine na tusingeliweza kukatisha mazungumzo yao, na mimi nilijitahidi kuficha hisia zangu, na wao hakuna aliyeonyesha dalili za kutaka kunidadisi, ilikuwa kama kawaida tu.

*************
‘Twende…’akasema

‘Si tunaondoka au…?’ nikauliza

‘Hapana kabla ya kuondoka, kuna jambo nataka tulifanye kwanza…..wakati familia wanaagana agana na watu wengine ni lazima tuchukua nafasi hii, ni muhimu sana…’akasema.

‘Hapana docta, mimi sitaki kuongea na mtu mwingine, akili hapa haipo sawa…’nikasema.

‘Wewe usiharibu mambo, …’akasema na mimi nikamfuata tu kinguvu nguvu, hadi nje tena, na sasa ilikuwa sehemu nyingine iliyotulia, akasema;

‘Wew nisubiri hapa, nakuja….’akasema na docta akaondoka, na mara nikasikia mchakato wa kitu kinakuja,..kwanza nikahisi ni huyo huyo mpenzi wa facebook, moyoni nikawa namuomba mungu aniongoze, kama kweli mtu huyo yupo, basi anisaidie , na kama ni shetani aliharibu, lipotee kabisa…

‘Habari yako…’sauti ikanishtua, ni sauti ya dada mtu, hapo, nikajipa moyo, nikageuka, na sasa nikawa naangaliana na huyo mdada, msichana ambaye aliteseka kwa ajili yangu, msichana ambaye ilisadikiwa kuwa amekufa kwa ajili yangu..watu wakasema, amejiua kwa ajili yangu…lakini kama binadamu unajua tulivyo, unapokuwa unalinganisha mambo….nikawa namlinganisha na mpenzi wa facebook, sikuweza kupata jibu ni nani zaidi.

‘Oh, umekuja, unajua mdogo wako alisema upo kule,…’nikaanza kusema hivyo .

‘Kule wapi…halafu ikawaje…?’ akaniuliza.

‘Aah, tuyaache hayo nashukuru sasa nipo na wewe, na…nilitaka niipata nafasi hii, tuongee, mimi na wewe, ni docta kakutuma uje huku au..?’ akaniuliza.

‘Kwanza nijibu swali langu kule ulikutana na nani..?’ akaniuliza.

‘Mimi sijui mdogo wako ana maana gani, kanikutanisha na msichana ambaye sikutaka kabisa kukutana naye…’nikasema.

‘Msichana gani huyo…?’ akaniuliza

‘Aaah, nitashukuru kama hilo utaliacha kama lilivyo, mimi naomba tuongee ya kwetu, ndilo muhimu kwangu…’nikasema.

‘Ulikutana na mpenzi wako wa facebook, au sio..?’ akaniuliza.

‘Oh, ni nani kakuambia,…?’ nikamuuliza.

‘Haah, bado unaye kichwani,…’akasema na akaonyesha kama kukata tamaa, au…na mimi nikasema;

‘Mimi nijuavyo huyo msichana hayupo, ni hadaa tu walitengeneza kuninasa, sasa nashindwa kuelewa,..na hata hivyo, ..kama yupo basi ni hao wasichana wanaotafuta biashara tu, siwezi kamwe kujihusisha nao,..mimi nataka tuongee ya kwetu, mimi na wewe…naomba uniamini….’nikasema.

 ‘Sawa kama maongezi yako hayana shari karibu sana, mungu anajua zaidi yaliyopo moyoni mwako kuliko mimi,,..na pili docta kanichukua juu kwa juu kuja huku, nilijua nakuja kuonana na mdogo wangu , mara nakutana na wewe..’akasema.

‘Aaah, kwakweli …akili yangu, imeharibika, ..naomba unielewe tu, mimi nia na lengo langu ni kuongea na wewe, na sio huyo ..sheta-tani..’nikasema.

‘Mhh..kama akili yako haipo sawa, mimi naomba uende ukapumzike, usije ukaongea mambo bila kufikiria,na hata mimi nahitajia kupumzika, au sio, basi mimi naondoka…’akasema.

‘Hapana usiondoke, nataka tuongee ni muhimu sana…’nikasema’

‘Mimi siruhusiwi kukaa vichochoroni na wanaume, wazazi wangu wakiniona hivi hawatakuwa radhi  na mimi,..japokuwa mungu anajua ni nini kilichopo moyoni mwa kila mja wake…niambie ulichotaka kukisema, nakusikiliza…’akasema.

‘Mimi kwanza naomba radhi kwa yote yaliyotokea, kiukweli siku ile ulipofika sikuwa na mimi..’nikaanza kujitetea.

‘Siku ile ..ipi..?’ akaniuliza akionyesha uso wa mshangao.

‘Siku ile ulipofika nyumbani kwangu…najua ni muda sana umepita…lakini mimi naona kama ilikuwa jana…’nikasema.

‘Ok hayo yalishapita, kama ni hilo tu,  mimi nimeshakusamehe, kabisa, usiwe na shaka na hilo, mungu mwenyewe anajua ni kwanini ilitokea hivyo…’akasema.

‘Lakini nilitaka pia kukuelezea ukweli kwa jinsi ilivyokuwa siku ile, kuwa sio kweli kuwa yule msichana alikuwa ni mpenzi wangu,..alikuja na hadaa zake, na nakuhakikishia na mungu ni shahidi yangu, sikuwa na ajenda yoyote na yule bint,…’nikasema akaniashiria kwa mkono.

‘Nimeshakuambia, sitaki kusikia hayo tena, yameshapita, usisumbuke kujielezea, mimi nimeshajua kilichotokea, nimeshaambiwa kila kitu, usiwe na shaka na hilo….’akasema

‘Ni nani kakuambia..?’ nikamuuliza.

‘Na hilo tena, unataka kujua, hapana,hatukuongea ili nije kukuambia….’akasema.

‘Na …moyoni mwako umeniamini kuwa mimi sina tabia mbaya kiasi hicho..?’ nikamuuliza.

 ‘Haah,…nikuambe ukweli kutoka moyoni mwangu, kwa hali kama ile sio rahisi mtu kukuamini tena..unielewe tu hivyo..’akasema.

‘Mungu ni shahidi yangu, sina zaidi ya hilo, na sikutaka kusema hayo mbele ya watu, maana masikio ya wengi yangeliweza kubadili ukweli kuwa fitina,..nimeishi hivi hivi, sikutaka kuwa na mpenzi maana nilijua wewe ni chaguo langu, sikujua kuwa kuna jambo limetokea huku nyuma…’nikasema.

‘Sawa yamtokea mengi tu… na hayo yaliyotokea, yanaweza kubadili mstakabadli mnzima wa nafsi ya mtu, …na ni vyema ukawa muwazi, ..na hata hivyo ulichoniitia umeshaniambia au sio, ulitaka kuomba msamaha..mimi nimekusamehe, ..’akasema.

‘Sijaongea nilichotaka kuongea..’nikasema.

‘Unataka kuongea nini, mimi ningelikushauri, kama ulivyosema akili yako umetatizwa, ni bora urudi nyumbani utulia, ili uwe na uhakika na mambo yako, ..japokuwa sijui unachoataka kuniambia, lakini…..’akatulia.

‘Hapana siwezi kuondoka mpaka nikuambie ya moyoni mwangu,..sijaweza kuwa na rafiki wa kweli, …tangia tuachane mimi na wewe…’nikasema.

 ‘Una maana muda wote huo ulikuwa huna rafiki wa kike..?’ akaniuliza.

‘Rafiki,.?? Hahaha,….kwa maana ya rafiki, kuongea kupotezeana mawazo..siwezi kusema hakuna, lakini sijawahi kumtamkia mtu kuwa nakupenda, au nakutaka, ..siwezi kusema ni kwa ujanja wangu, hapana, nafsi wakati mwingine inatamani kutenda hisia za mwili, lakini haikuwahi kutokea,…lakini nashukuru mungu amekuwa akiniokoa kwa namna ya pekee, na hadi sasa simjui mtu moyoni mwangu, mwilini mwangu zaidi yako wewe…’nikatulia.

‘Mhh, ujue unaongea na nani,…mimi sina haja ya kuimbiwa mashairi, nakupenda, nakuota nakuota,…unasema hujawahi kumtamkia mtu kuwa nakupenda, je na huyo mpenzi wa facebook hukuwahi kumtamkia kuwa unampenda..?’ akauliza na kunifanya nishutike, nilishasahau kuwa kulikuwa na mtu kama huyo.

‘Ni nani kakuambia kuhusu huyo shetani,…’nikasema.

‘Leo hii huyo amekuwa ni shetani, au…?’ akaniuliza
‘Kiukweli sikuwahi kukutana na huyo mtu kabla, ni leo kwa mara ya kwanza.., ilitokea tu nikajuana naye kwenye mtandao wa facebook, na nikuambie ukweli, nilivutika naye kwa vile anafanana na wewe, awali nilijua ni wewe, na nilipoambiwa umefariki…basi tena, nikajua mungu kaniletea badili yake..na na kiukweli, ..’ nikasita.

‘Hahaha eti kafanana na mimi, una uhakika na hilo..?’ akaniuliza.

‘Mnafanana, fanana na yeye, kisura, hata kimwili, lakini sio, kitabia, wewe umemzidi sana kitabia, unajua mimi nilishamsahau huyo mtu, maana, hao watu wabaya…walisema walichukua sura yako, wakachanganya na sura ya mama yao…unajua tena, ni mambo ya kishetani, ya kunipumbaza akili…’nikasema.

‘Sasa si umeshamuona mbashara, niambie…au bado haupo sawa, ..huyo umemuona, sisi ni sawa na ndugu zako tupo tayari kukusaidia, umuoe…’akasema.

‘Eti nini…nimuoe,..hahaha, hunitakii mema, ..hivi kweli kama ungelikuwa ni dada yangu ungelinishauri kitu kama hicho..hapana, siwezi, ..mimi ninachotaka ni kukuoa wewe..narudia tena, mimi …’nikasema na akanikatisha kwa kusema.

‘Basi mimi nikushauri kitu, kwa nia njema, maana usije ukawa unaongea, kwa vile… huku akili yako ipo kwa mtu mwingine, utakuwa huna raha katika maisha yako ya ndoa,…pata kwanza muda wa kutosha wa kutafakari hilo,na ni vyema, ukamtafute kwanza huyo mpenzi wako facebook, ukae naye muongee, ujiridhishe,.. nikwa ushahuri wangu tu..’akasema.

‘Hapana, moyo wangu upo kwako,..ulipozindukana pale hospitali.., ukafunua macho yako, ulinifanya nihisi vingine kabisa..nakupenda sana, amini hilo, huyo alikuja kuighilibu nafsi yangu, sio aina yangu, kabisa...’nikasema.

‘Mimi namtegemea mungu peke yake, kama ni wewe , kama yupo mwingine nitampokea kama kweli mungu kapenda iwe hivyo..siwezi kukata kuwa kweli wewe uliutekea moyo wangu kwa mara ya kwanza, lakini ukauvunja kwa nyundo kubwa sana..nikabakia na jeraha kubwa.

‘Mhh, samahani kwa hilo, nisamehe sana, nielewe ndio maana nilitaka nikusimulie yaliyokuja kutokea hadi ikafikia pale, nisamahe, na nielewe…’nikasema, na yeye akaendelea kuongea wakati nami naongea.

‘Sasa kuja kujitibia hili jeraha..mmh.., sijui…ninachopenda kukuambia, ni kuwa uwe na subira nilitibu kwanza hili jereha moyoni mwangu na siku likipona,..na mungu akanielekeza kwako, basi.. nitakuja kwako kama siku ile…,au nitakutumia ujumbe wa maneno kwenye simu, ila usiharakishe kufanya lolote kwangu, mpaka mimi nikuarifu..sitaki kulazimishana,…tafadhali,..’akasema akitaka kuondoka.

‘Kwahiyo…’nikauliza.

‘Kwahiyo vipi tena, kwani hujanielewa… nakuomba uondoke hapa wasije kutokezea wazazi wangu ikawa ni sababu ya mimi kuwakosea tena wazazi wangu, nawapenda sana wazazi wangu..’akasema na mimi ikabidi niondoke tu.

**********
Baadae ndio nikakutana na docta akaniuliza ilikuwaje, sikutaka kumuelezea mengi, nikamwambia;

‘Aaah, binti kama kawaida yake,..anataka nimpe muda, …anasema nilimuumiza sana siku ile, kwahiyo anahitajia muda wa kutafakari..’nikasema.

Docta akasema;

‘Nimeongea na wazazi wa hao wasichana wawili, nikaamua kuwa mshenga wako japokuwa sio rasmi..nikawaambia kuwa mimi nachukua dhamana kwako, kama mshenga asiyerasmi, ila tutakuja tena, kama watanikubalia ombi langu,…
‘Oh docta…’nikataka kusema na yeye akanikatisha kwa kuendelea kusema;

‘Wakaniuliza nina maana gani, unajua wazazi wanakuwa makini sana kwa maswala yanayohusu watoto wao, wanaweza wakajua ni nini , na walijua ni nini nataka, lakini walihitajia uhakika, basi mimi nikawaambia, kama mjuavyo rafiki yangu alikuwa rafiki wa binti yenu kwa siri, na hakuwa na nia mbaya, sasa anataka kujibainisha kwenu kuwa yupo tayari kumposa binti yenu…hapo wakajifanya kushtuka, na kusema;

‘Mhh, hivyo….lakini mbona haraka hivyo, bint yetu bado hajatulia baada ya mikasa hii iliyotokea,… unajua tulijaribu kumuulizia hilo,…kama wazazi ikitokea kitu kama hicho, unapata ishara kuwa binti au kijana wako kakua na anahitajia mwenza, kwahiyo hatukusita kumuuliza , kuwa yupo tayari kuolewa kwa hivi sasa, akasema kwa sasa hataki kabisa mambo ya kuolewa..

‘Ehe, kwasasa unataka nini..usije kusema hivi na wakati una jingine,….’tukamuambia hivyo na yeye akasema;

‘Lengo langu kwa hivi sasa ni kusoma zaidi…, sasa nashindwa kukupatia jibu la haraka la ombi lenu, unielewe hapo, maana japokuwa sisi ni wazazi, lakini muhusika anahitajika kutupatia majibu yake, kabla hatujasema lolote…’akasema hivyo baba yake.

Mimi nikawaambia, ‘kama ni kusoma atasoma tu, anaweza akafanya hivyo akijulikana kuwa ni mchumba wa mtu, au akasoma baada ya ndoa, hilo halitazuia yeye kutimiza dhamira yake, mimi nachukua dhamana hiyo kuwa binti yenu hatapata shida,..atatimiza malengo yake bila wasiwasi, na kiukweli, huyo rafiki yangu na binti yenu, wanaivana, na sio mimi tu, hata wabaya wenu waliligundua hilo kuwa huyo hawa wawili nyota zao zinafanana, wakioana mambo mengi yataenda vyema.

‘Basi sisi tunaomba mtupe muda tutaongea na binti yetu akikubalia, sisi hatuna shaka na nyie…tumeshajiridhisha kwa hilo’

‘Oh, sasa mbona itakuwa shida,….’nikasema nikikumbuka kauli ya huyo binti kama angalizo kuwa nitakutumia ujumbe wa maneno kwenye simu, ila usiharakishe kufanya lolote kwangu, mpaka mimi nikuarifu..sitaki kulazimishana,…

‘Hakuna shida hapa, mimi nawapa siku kadhaa, wakiwa kimia, mimi mwenyewe nitakwenda huko rasmi…’akasema

Haikupita siku mbili, nikapokea ujumbe kwenye simu,..maneno machache tu, yakisema;

Nimeridhia ombi lako, japokuwa umevunja sharti langu….’aliandika hivyo tu.

‘Nimevunja sharti lake, oh, nilijua tu…docta kakurupuka mapema…’nikajisema hivyo.

Nilimuambia docta, na docta akasema hakuna haja ya kusubiria yeye atafuatilia taratibu zote kwa haraka, anafanya hivyo kwa vile anatarajia kusafiri nchi za nje…, kuna mualiko wa kwenda kujiendeleza zaidi na wenzake, na zaidi ni kuwa kapata kazi huko huko, kwahiyo yeye hatakuwepo hapa bongo mara kwa mara, atakuwa anakuja kwa likizo tu.

‘Sijui nitakaa huko kwa muda gani, ila tutakuwa tukiwasiliana, ..ndio maana nataka kabla sijaondoka, nihakikishe hili limefanikiwa,na zaidi, nilikuwa sitaki kuwalipisha hiyo familia pesa nyingi, lakini hutaamini kwenye lile jengo, litapigwa mnada, mke wa mzee, atapewa fungu lake, kwa yote yaliyotokea, na unajua tena wamiliki wote hawapo duniani…unakumbuka yule mtu aliyekuwa akiendesha hilo jengo, ndio yule mtaalamu, siku zile alijibadili,..na alikuja kugundulikana wakati wanampima maiti yake…’akasema.

‘Kuna kipindi walisema sio Mtanzania…’nikasema.

‘Ndio kwa jinsi alivyokuwa akifanya shughuli zake pale, alijulikana kabisa kuwa yeye sio mtanzania,…alijitahidi sana kufanikisha hilo, waliokuwa wanaufahamu huo ukweli ni hao washitakiwa wawili,…lakini yeye ni mbongo, na ana udugu fulani na hao washitakiwa wawili…

‘Duuh, kweli walicheza mchezo, japokuwa ulikuwa mchezo mbaya…’nikamwambia docta hivyo

 Basi docta akafanya kazi ya ushenga rasmi, hakutaka kumtafuta mtu mwingine… na akafanikisha kila kitu,..hatimaye nikafunga ndoa na huyo binti mkubwa wa mzee… nikaanza maisha kutoka sifuri, nilikuwa sina kitu, pesa aliyonipa docta niliitumia kwa mahari, na maandalizi madogo madogo, mke anaingia ndani, tunaanza kupiga mahesabu jinsi gani ya kuishi…hatukutaka kuishi kwa wazazi wake, au…hapana yeye na mimi tukakubaliana tukaze buti…!

‘Mungu ametusaidia sana, hatua kwa hatua, tunaanza kujiweka sawa, ..ndio maana umenikuta katika hii hali rafiki yangu, sikuwa hivi, unanifahamu sana, yote maisha, na yote ni kwasababu ya mpenzi wa facebook,….’akanimalizia kisa chake na alipotamka hayo maneno ya mwisho akacheka.

‘Sasa nikuulize kitu, huyo mpenzi wa facebook yupo kweli..?’ nikamuuliza.

‘Hahaha,…mpenzi wa facebook,..ni kweli yupo…hutaamini…’akasema.

‘Yupo wapi,….keshaolewa, mnaonana naye au ulipo-oa, ndio hamukuwahi kuonana naye tena..?’ nikamuuliza.

‘Hivi hujanielewa hadi hapo,..huyo mpenzi wa facebook, ni mke wangu…. unajua ni nini kilifanyika siku ile, …kumbe docta wakati anaongea na wazazi, mimi nipo nje, akataka kuwaridhisha, kwa kunitega, akawaambia ili wote wahakikishe kama kweli nampenda binti yao au huyo mpenzi wa facebook, basi wafanye jambo moja, kunipima..

‘Wakamuita binti, docta akamsomesha ni nini kinatakiwa kifanyike, kwanza binti alikataa , lakini wazazi wake waliposhinikiza akakubali,..kufanya hilo igizo, la kunipima mimi, ..mimi muda huo sijui lolote, sikuwahi kuongea na docta, kuwa nitajibu vipi,… basi docta kwa vile alikuwa na ule mtandao unaoweza kubadili sura kwa kuvalisha ngozi, akamvalisha huyo binti sura ya yule mpenzi wa facebook,…nia yao ni unipima akili yangu….

‘Kwahiyo ina maana…’nikataka kusema, na yeye akaendelea kusema;

‘Huyo mpenzi wa facebook, niliyemkuta pale, ni huyo huyo mdada, ambaye sasa ni mke wangu, alivalishwa hiyo sura, nia ni kunipima, kama kweli nampenda yeye au huyo mpenzi wa facebook, na nashukuru mungu niliweza kufanya yaliyowaridhisha wazazi na hata …mke wangu....umenielewa hapo.


Na ujue wakati naongea na huyo mpenzi wa facebook, wao walikuwa wakiniangalia kwenye laptop ya docta, mbashara…hata huyo binti hakujua kuwa tunaangaliwa.. ndio maana walipotoka pale mlangoni wakaanza kushangilia…sikujua wanashangilia nini, hata huyo binti hakujua hilo…, sikujua mdogo wake, alipojitokeza mbele yangu alikuwa na furaha gani..kiukweli ilikuwa ni kitendawili kwangu!


‘Oh, hongera sana, …mpe salamu shemu, mpenzi wako wa facebook, wa kweli…’nikasema na tukashikana mikono ya kuagana.

                      ***********Na hapa ndio mwisho wa kisa hiki*************


WAZO LA LEO: Sio kila king’aacho ni dhahabu, …na sio kila anayekuchekea ana nia njema na wewe…muhimu tuwe makini kwenye maamuzi yetu, tumuweke mbele muumba wetu, kwani yeye ndiye anayejua ya siri na ya dhahiri!

NB: Nawashukuruni sana nyote mlioweza kukifuatilia hiki kisa hadi mwisho..najua sio wote watafurahia kila kitu, lakini hivyo ndivyo nilivyoweza kuwakilisha hili tukio, ama kwa wale waliotaka kumuona au kuwasiliana na docta, ..huyo docta hayupo hapa nchini kwa sasa…

Ama kwa hiki kisa.., kama ni kizuri, basi tuelimike sote,  na ujumbe uliopo ndani ya kisa hiki uwe ni shule kwetu, …mojawapo ni kuwa tuwe waangalifu kwenye kutumia hii mitandao ya kijamii,..mumesikia mtanzania kafungwa huko nchi za nje,…na tujue ukweli kuwa,.. sio kila kitu unachokiona kipo kama kilivyo,tusiwe wepesi wa kutoa taarifa zetu zote,..au kuandika mambo kwa pupa, tuelewe tunachokifanya na faida na hasara zake, kabla ya kuandika au kuweka picha, na zaidi,…tusikurupuke, kutamani, kwani sio kila king’aacho ni dhahabu

Ni mimi: emu-three

No comments :