Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, June 21, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-55


Tulifika kwenye shughuli hiyo, tukakaribishwa kama wageni rasmi, na utambulisho wetu uliwafanya watu washangilie, tulielezewa kama wapiganaji tuliojitoa mhanga kuhakikisha tatizo hilo limekwisha, na mzee akasema akazidi kusheneza kwa kusema;

‘Siwezi kumlaumu yoyote kwa hili, mimi naliona kama mtihani katika maisha yangu na familia yangu, mimi sikujua ni nini kilitokea huko nyuma halikadhalika mke wangu,lakini niseme neno,…hivi tukiamua kila lililofanyika huko nyuma tuwe tunalipizana kisasi kweli kutakuwa na usalama…, basi tufike mahali tusema yaliyopita si ndwele tugange yajayo..’

‘Kwa wale tuliwakosea, tunawaomba sana msamaha, mtusamehe ….maana bila wao kutusamehe hatutakuwa na radhi mbele ya mungu, na sisi tumewasamehe wale wote tuliowakosea tukijua kuwa mwanadamu ana mapungufu yake mengi, kama mwanadamu, hatuwezii kuwa wakamilifu abadana.

Nitumie fursa hiii kuwashukuru sana wote, na nitakuwa mkosefu wa fadhila,kama sitwashukuru kipekee docta na msaidizi wake, wao wanakuwa ni sehenu ya familia, kwa jinsi walivyojitolea kupambana na hili jambo…mungu atawalipa zaidi kwenye maisha yao.

Kiukweli…, wapo wengi wa kushururu..wapo askari polisi wamefanya kazi kubwa sana na wote walihusika kwa namna moja au nyingine wote hao tunawashukuru sana…’akaongea na mke wake naye akaongea, akaomba msamaha kwa hayo yaliyowahi kutendwa na kizazi chao, akasema hayo yalikuwa huko, lakini kwa vile imefika hadi kwao, basi yeye anaomba msamaha kwa niaba ya wazee wake.

Baadae docta akapewa nafasi ya kuongea, na kabla hajaongea, akachukua mfuko, aliokuja nao,…

‘Ndugu zanguni,…mimi sio mrithi wa hivi vitu,..kuna vitu hapa ni mali ya hii familia, vitu hivi vimetumika kama kichocheo tu, ..ndivyo dunia ilivyo, watu wana chuki zao, wengine wana visasi vyao, wengine wan hula zao za shari tu, …na wengi wao hawataki kuyaonyesha hayo matatizo yao bayana, wanatumia miavuli fulani, kama kisingizio..

Ukichukulia mfano wa hili tatizo, waliotenda haya, wanadai, kuwa familia yao,… mama yao alidhulumiwa, ni sawa ilitokea hivyo, huko nyuma,…hayo yameongewa mahakamani, lakini tujiulize walidhulumiwa na nani,..je huyo aliyefanya hivyo yupo, ..hayupo, kwanini tuiumizeni familia nyingine ambayo haihusiki,..tinafanya makosa, inabidi kila mtu aubebe mzigo wake mwenyewe.

 ‘Hao watu, walikuja kutumia vifaa hivi vitatu kama sababu, kwanini walitumia hivyo,..ni njia ya kuficha maovu yao, ..binadamu wengine hurithi ubaya, wengine huja kuiga, wengine, wanatafuta upenyo tu..tujiulize yote haya matokeo yake ni nini, je baada ya kufanikisha hayo, kama utafanikiwa utaishi mielele, ..

‘Ndugu zanguni, tusitafute uchochoro wa kuonyesha hisia zetu, tusitumie visingizio hata vya imani zetu, kuonyesha makucha yetu, ikawa ni visingizio vya kutenda uhalifu kwa watu wasio na hatua mungu hatakuwa radhi na sisi, na hatuwezi kufanikiwa kamwe,  na mwisho wake ni fedheha tu.

Ama baada ya kuyasema haya, nitumie fursa hii kuvikabidhi hivi vifaa kwa wenyewe, wenyewe wanajua ni vitu gani,..na nini cha kuvifanya, ila, kama nilivyosema tusichukue mambo ya kurithi, ikawa ndio sababu ya kutekeleza matakwa yetu, tukatumia kama visingizio vya kukidhi tamaa za nafsi zetu, muhimu kwa jambo lolote hebu kwanza tulifanyie utafiti tuone faida na hasara zake, tujiulize kwanza je sisi wenyewe tukitendewa hivyo itatufurahisha,…

‘Hivi vifaa vinatakiwa vikabidhiwe kwa mama wa hii familia, yeye ndiye mrithi wa asili na yeye ndiye anayeweza kuamua lipi lifanyike kwa vifaa hivyo, wengine wakiamua kufanya lolote kwa vifaa hivi, wakiwa wanafahamu masharti yake, wata[ata shida sana, ndio maana wenzetu wakaamua kutumia njia ngumu ya kufanya makafara ya kumwaga damu za watu wasio kuwa na hatia…

Haitakiwi kuwakabidhi watoto kwa hivi sasa wakati mzazi wao ambaye ni mmoja wa warithi bado yupo, .. ‘akasema akiwageukia kuwaangalia hao mabint wawili.

‘Hao wenzetu, wao waliamua kuwatumia watoto moja kwa moja, baada ya kujua kuwa wakiamua kuwatumia wazazi, hawatafanikiwa kwa haraka, nayo ilihitajia makafara pia, ni shidaa…

‘Kwahiyo huyu mama ndiye sasa atakuwa na mamlaka ya hivi vitu, na akishavipokea, yeye ndio atakuwa na uhuru wa kuwakabidhi watoto wake, akitaka, au kuviuza..au..atajua mwenyewe…’akageuka kumuangalia huyo mama.

‘Natoa kama angalizo tu..linaweza kufuatwa au kuachwa, maana mimi sina mamlaka hayo,..hivi vitu ni nyeti sana kuliko watu wanavyofikiria, ni vya hatari sana kama vitafika mikononi mwa watu wenye tamaa mbaya, kama, ilivyotokea kwenye hilo kundi haramu, hapo bado walikuwa hawajavimilikisha kabisa…, mungu awasamehe madhambi yao, maana, kama wangevimiliki wakafanikiwa …muda huu tungeliongelea mengine, kwahiyo vitu kama hivi,...mimi sijui, ngoja  tumsikilize mama, ambaye ndiye mrithi halali atasemaje..

‘Tafadhali mama mrithi,….’akasema docta akimuashiria huyo mama, na huyo mama akasimama, kwanza akainama kidogo kwa mume wake, kama kumuomba radhi, au ruhusa ya kusimama na kuchukua jukumu hilo, na mume wake akatikisa kichwa kuashiria kuwa amekubali…

Mama Mrithi akasogea pale alipokuwa kasimama docta, na docta akachukua ule mfuko, na kuwa kama anamkabidhi huyo mama, huyo mama akawa kama anasita kidogo, na docta, akavaa kinga za mikononi, na kutoa kifaa kimoja, akamuonyesha na cha pili akamuonyesha halafu akaukung’uta ule mfuko, kuashiria kuwa hakuna kitu kingine, ndipo yule mama akaupokea,…lakini kabla ya kuupokea, kwanza akamuomba mungu ampe kinga, halafu, akasema;
‘Kwangu mimi, kama nilivyokataa kupokea kikombe cha wazee…watu wanaita mikoba.., na hiki pia mimi sikipokei, kwasababu gani, haya yaliyovifanya hivi vitu, sijui undani wake, na je nitawezaje kufanya hayo waliyokuwa wakiyafanya wao wakati sikuwahi kufundishwa au kuona wakifanya…lakini kwa vile kwa hali ilivyo inabidi nivipokee, ili sije ikawa kama alivyosema,….docta, vikaingia kwenye mikono yenye tamaa mbaya..’akatulia.

‘Nawaombeni watoto wangu mje hapa …’akasema akiangalia pale walipokuwa wamekaa mabinti zake, watu waliokuwemo wakawa wanawaangalia hao mabinti, wakikumbuki hayo waliyofanyiwa, hasa huyo mkubwa,

‘Hawa ni watoto wangu, hii ni sehemu ya familia yangu, sitamuita baba yao kwanza, maana haya mambo yana masharti yake, nisingelipenda mume wangu mpendwa akaingizwa kwenye mambo yasiyomuhusu,…kama ni kudhurika, nidhurike mimi mwenyewe..’akasema, na kila mtu akawa na hamu kujua ni kitu gani huyo mama anataka kukifanya.

Mabinti wale wawili wakafike pale mbele, na mama yao akawa anawanong’oneza jambo, na wao wakatikisa kichwa kukubali,.. baadae yule mdogo, akatoka kidogo, aliporudi alikuwa kaandamana na mtu akiwa kabeba pipa kubwa, ni aina yamapipa maalumu ya kuchomea taka-taka, na huyo mtu akalitua lile pipa,..

Yule mama akamuomba mungu wake akaomba kinga kutoka kwa mola wake kwa hili alilokusudia kulifanya, na kuomba radhi, kama atakuwa amekosea, lakini yeye kwake ameona ndio njia sahihi, na kama kuna madhara yoyote basi yampate yeye mwenyewe, kwa maamuzi hayo…

Alipomaliza kuomba hivyo, akageuka kumuangalia mume wake, na mume wake akatikisa kichwa kukubali, ..wenyewe walivyoangaliana walijuana ni nini wanachongea.

Akaingiza mkono kwenye ule mfuko na kutoa kifaa kimoja wapo akasema;

‘Hii hapa ni bastola, hii ni ishara ya nguvu, mamlaka, na dhamana ya kulinda utawala aliokabidhiwa kiongozi na raia zake...ndivyo ilivyokuwa dhamira ya watengenezaji, hivi vifaa kwa jinsi nijuavyo mimi, lakini ina upande wake wa pili, ni ishara ya umwagaji damu, vita, mabavu na udikiteta duniani,…’akatulia.

Ni kwanini ikawa na sehemu mbili, ni kwasababu utawala, ni mtihani, na mtawala anapimwa kwa hekima zake, sasa yeye akiwa muadilifu, anayewajali raia wake, hataweza kugeuza upande mbaya, atasimamia upande wa uadilifu, hekima, ..na kuwaongoza raia wake, kwa mujibu wa  sheria,..kinyume chake akipatikana mtawala mbaya, basi atatumia upande wa pili, ili aogopewe, huu upande wa pili kasimama shetani..nisingelipenda kuuelezea upande huu zaidi, maana ukiuelezea sana wale wenye vichwa dhaifu huingiwa na hamasa nao…

Sasa mimi kama marithi halali wa hiki kifaa.., kwangu mimi nasema iwe mwisho, na dunia iwe na amani,utawala, na mamlaka yake yarudi kwa raia wenyewe, wao ndio wakuamua ni nani mtawala wao, na wala usiwe ni utawala wa kurithiana tena, …’ akachukua ile bastola, akaiangalia, na kwa haraka  akaitumbukiza kwenye pia,…na yule mtu aliyeleta hilo pipa alijua ni nini cha kufanya.

Akawasha pembeni mwa lile pipa, na kukasikika mngurumo, kuashiria inafanya kazi, na haikupita muda,…akaashiria kwa kichwa kuwa tayari…akafunua, kukatokea moshi,..ulipotulia, akainamisha lile pipa ili watu waone, hakukuwa na kitu tena, kile kifaa kilikuwa kimeteketea kabisa.Yule mama akatoa kifaa kingine kwenye mfuko, hiki kilikuwa kidogo tu, akakishika mkononi.

‘Na hiki hapa,pamoja na udogo wake, ni kikubwa sana kwa matendo yake hasa katika dunia hii ya sasa,…huu..ni ufungua unaweza kufungua kifungo chochote, ikiwemo, nyumba, mitambo inayolindwa kwa kutumia mitandao, akiwemo mitandao yenyewe..’akatulia.

‘Ina maana gani, ina maana hata uweke neno gani la siri, hiki kifaa kinafungua, hii ni ishara ya pia kwa kiongozi muadilifu kuwa umepewa nchi, na nchi hiyo ina mipaka, ina masharti, mila na desturi zake, ina mali asili ina mali za watu, na watu wake, basi wewe funga nyumba hiyo..maana nchi ni mfano wa nyumba yako na familia yako, uhakikishe umefunga kila kitu ili nchi iwe salama… ukitumia alama ya ufunguo huu.

Ama kwa upande wake wa pili, ndio huo utapeli, wenzako wamezalisha, wenzako wamehifadhi vitu vyao, wewe unatumia kifaa kama hiki kupakenyua maisha ya wenzako, unaiba mali za wenzako, una-dhuluma,..huko ni kubaya hata kuelezea.

Sasa mimi kama mrithi halali wa hiki, nasema huu uwe ni mwisho, kila mwenye siri yake abakie na siri yake….na kila mwenye mali yake halali abakie na mali yake…na kila mwenye ujuzi wake, autumie ujuzi wake kwake yeye kwa manufaa yake yeye, na akitaka awasaidie na wengine lakini iwe kwa ridhaa yake,…’akatulia.

Mimi kama mrithi halali, nakiharibu hiki kifaa kwa manufaa ya vizazi vyetu ambavyo kwa hivi kwa mfano, wametawaliwa na mitandao, ..wanaweza kuangamizwa kama hiki kifaa kitaingia kwenye mikono mibaya, watu watatumia hiyo mitandao, na kuweka, mashetani ndani yake..msiona hii mitandao, mkafikiri ina mema yote..hapana, kuna mangapi mabaya yapo humo…kizazi kitaharibika kisipojua madhara yake..mapicha mabaya, yenye kuathiri akili za vizazi vyetu, hii ni moja ya kazi ya shetani..mungu atulindie vizazi vyetu..

Kwa haraka akakitumbukiza ule ufungua kwenye pipa, na gesi ikawashwa na kufanya kazi yake, ilichukua muda kidogo, kuliko ile ya kwanza, kuashiria kuwa kifaa hicho kina nguvu sana,..na hatimaye kikaharibiwa kabisa..

Alipomaliza hivyo, akageuka kumuangalia docta, na docta akageuka kumuangalia mzee wa familia, …na mzee wa familia akasimama.

‘Najua ni kwanini watu hawa wananiangalia mimi, …hahah, je nikikataa, eti jamani, mimi nimepewa hivyo vitu kama zawadi, hajalishi masharti yake,…lakini mm, docta kanishtua, kasema ukijua masharti yake ukakaa nacho,…utapata madhara, na mimi naogopa hayo madhara, hasa kwa familia yangu.

Ninacho kifaa chao kimoja,..nilipewa kama zawadi nikiwa jeshini..na sikupewa kifaa kimoja tu, nilipewa vifaa viwili, ile bastola na hivi viatu…’akaninama na kuvivua viatu alivuyokuwa kavivaa…na kuendelea kusema;

‘Kiukweli, kiatu na bastola, nilikaidhiwa mimi kama zawadi..na nisingelijua asili yake ningeliendelea kuvimiliki..lakini sioni umuhimu wake kwangu, hasa ukiangalia upande wa pili yake…naona sasa nikiwakilisha kifaa hiki kwa wahusika, na wenyewe watajua jinsi gani ya kufanya..akasogea pale na kumkabidhi mke wake hivyo viatu.

Mama alifanya hivyo, kama vingine…akisema

‘Nasikia kifaa hiki enzi hizo, mfalme, aliweza kuruka nacho usiku kukagua miliki yake, kuhakikisha hakuna madhara …kwa ufupi kifaa hiki kinawakilisha usafiri, miundo mbinu ya namna hiyo…na mengineo, ila kwa upande wa pili, kinawakilisha nguvu za giza,…’akatulia.

‘Najua umeshasikia watu wanatembea na ungo…basi kazi ya kifaa hiki kwa upande mbaya ndio hiyo,.. kifaa hiki usiku unaweza ukaruka nacho, ukafanya mambo yasiyompendezesha mungu, humo kuna shetani, . ..aah ni hivyo tu, nisiseme mengi..akaviangalia vile viatu, ni vizuri kwakweli …‘free size’..

Akakitumbukiza kwenye pipa,…mpaka vikaharibika kabisa,.. na ikawa ni mwisho wa hivyo vifaa vya ajabu,..na mwishowe shughuli hiyo kukaendelea shughuli nyingine za kisherehe, na mpaka ikafikia mwisho wa shughuli hiyo.
************
Baadae, wakati tunajiandaa kuondoka, mara docta akaitwa ndani, ..nilijua ni kwanini, docta alifanya kazi hiyo kwa makubaliano ya kuja kulipwa, kwahiyo ilibidi wakutane na familia hiyo waone watalipana vipi,..mimi sikupenda kuwepo, nikamuacha docta akaenda peke yake.

Wakati docta anaongea na hiyo familia  mimi nikatoka nje ya hilo eneo, nikawa napunga upepo,…nikiwaza mambo yangu, maana binadamu mawazo ni kawaida, sikutaka kuwazia sana maisha ya mbele, …na mara nikahisi kuna mtu anakuja nyuma yangu, sikuataka kugeuka, nilijua ni docta.

‘Shemeji,..samahani…nilikuwa nakutafuta huko ndani, kumbe uko huku, oh…’akasema na mimi niliposikia hivyo, tena nikiitwa shemeji, akili ikaanza kuwaza mengi, namuda huo akawa ameshafika pale nilipokuwa nimekaa, sikugeuka kumuangalia, akasema;


‘Kwanza nikushukuruni sana,..kwa hayo mliyotufanyia, tunashindwa hata la kusema, mungu mwenyewe ndiye atawalipa, ..na pia, aheri nimekuona peke yako, ili nitumie fursa hii kukuomba unisamehe..’sauti hiyo ilinifanya nigeuka kwa haraka,, kwanza hiyo kauli,sauti..

‘Mhh, kwanza nikuuliza kwanini unaniita shemeji..’nikasema kama nauliza

‘Kwani wewe sio shemeji yangu, najua, na nilijua ipo siku..mungu atawaunganisha wewe na dada, najua hayo yaliyotokea ilikuwa ni ..mitihani tu..su sio, au kuna mengine usije ukawa umeshampata mwingine,…niambie ukweli…’akasema

‘Unajua, hayo unayozungumza, shemeji, ..ilikuwa zamani, sasa hivi, huwezi jua, ..kwangu mimi, aah, siwezi kukudanganya, sijaweza kuwa na mtu..nipo kama nilivyo…’nikasema

‘Mambo si hayo…’akasema.

‘Sikiliza kwnza…’nikataka kuendelea kusema akanikatisha kwa kusema;
‘Sio sikiliza mimi namfahamu sana dada yangu anakupenda sana, na hata baada ya hayo yote bado anakupenda, ..lakini hawezi kukuambia hilo, ..tulikuwa tumetoka na ndada nje, tukawa tunaongea,…’akatulia.

‘Sawa…’nikasema

‘Na nikatoka pale nikikutafuta kule ndani sikujua upo huku nje,..’akasema

‘Unitafute kwa dhumuni gani labda..?’ nikamuuliza.

‘Nilitaka utumie nafasi hii, uongee na dada, muyamalize, kwa hivi sasa hajui kuwa nimekuja kukutafuta, ..ila kwanza uniambie ukweli wako kutoka moyoni, ..kama una mtu wako mwingine unitamkie hapa, na mimi nitajua jinsi gani ya kumalizana na dada, uwe muwazi, je unamtaka mpenzi wako wa facebook, au dada,…niamini..kwani sitaki mtu aje kumuumiza dada yangu tena..’akasema.

‘Eti mpenzi wangu wa facebook,ni nani kakuambia hilo, huyo mtu hayupo, ni geresha zao hao watu..…haaah,…je una uhakika kuwa dada yako atanisamehe..?’ nikamuuliza.

‘Kwani ulimkosea nini…?’ akaniuliza hivyo.

‘Oh, si ndivyo hata wewe uliwahi kusema hivyo..kuwa mimi ni chanzo cha hayo yote au…’nikasema.

‘Nilisema vile, …kwa vile sikujua,… sasa nimeujua ukweli…, hata familia yangu sasa ipo radhi na wewe… hata walipogundua kuwa wewe ulifumwa ukiwa na msichana mwingine, na ndio ikamuathiri dada…’akasema

‘Lakini mimi sasa sijawa tayari kuishi na mke, sina mbele wala nyuma, nimefirisika, nipo-nipo tu..nahitajia muda w kujijenga tena..kwa mfano kwa hivi sasa naishi kwa mgongo wa docta…’akasema.

‘Hilo la kuishi mtaishije, lisikutia shaka,labda uniambie ukweli kuwa akili yako bado inamuwaza huyo mpenzi wa facebook, ama kwa dada,… mimi namafahamu sana dada yangu kuna kipindi nilimuuliza je akimpata mume asiye na kitu akampenda itakuwaje, unajua aliniambia nini..?’ akaniuliza.

‘Sijui labda uniambie wewe..’nikasema.

‘Alisema hivi, yeye hajali mali, kwasababu mali ni majaliwa ya mungu unaweza kumpata mume mwenye mali akafirisika, au mali hiyo ikawa sio ya halali, ..lakini ukimpata mume mwenye upendo wa kweli hiyo ni mali tosha, haifirisiki, na ni halali hadi mwisho wa maisha yenu, na mume kama huyo mnaweza kujipanga mkajijenga na kufika mbali zaidi, maana ana upendo wa kweli…’akatulia kidogo.

‘Kiukweli....nilipenda maneno hayo ya dada…’akasema.

‘Kwahiyo hata wewe upo tayari kuolewa na mume yoyote, ilimradi umempenda, mkapendana..?’ nikamuuliza

‘Usiniulize ya kwangu, mimi nipo hapa kwa jili ya dada na wewe, na mpenzi wako wa facebook…’akasema.

‘Oh…hata sijui nisemeje, unajua naogopa hata kuja kuongea na dada yako nahis nilimkosea sana,…aah, haya, niambie, maana kama hilo litafanikiwa, sijui nitakushukuruje..’nikasema na hapo akasogea na kunyosha mkono, sikujua ana maana gani, nikatulia.

‘Nataka unishike mkono, kwa ishara ya ahadi..kuwa kweli utampenda dada yangu, utamlinda, mtakuwa naye kwa shida na raha…au kama moyo wako upo kwa mpenzi wa facebook, basi, hata huyo …sio mbaya, …’akasema na mimi kwanza nikasita, lakini baadae nikanyosha mikono yangu, ikaishika mikono yake,..nilipomuachia, akaruka juu na kusema.

‘Yeesss…’kwa nguvu sana, nikabakia nimeshangaa sikujua kabisa kuwa hilo lipo moyoni kwa huyu msichana, nilimuangalia alivyofurahi na mimi sasa nikaingiwa na shauku ya kukutana na huyo dada yake.

‘Kwani yupo wapi huyo dada yako..?’ nikamuuliza, na akaniashiria kwa mkono kuwa yupo upande wa pili wa nyumba, halafu akasema;

‘Nenda ..nenda…ila usichelewe ataondoka, nimemuambia nakwenda kuchukua soda ndani … mkimalizana naye utakuwa na jibu muafaka ….ni nani umpendaye…’akasema na kuondoka, na mimi nikatembea kuelekea hiyo sehemu, niliyoelekezwa, nikafika pale alipokaa,  alikuwa kainama, kashika simu, hakujua ni nani anakuja.

‘Na wewe bwana, …maana yake ni nini kunigandisha hapa nje muda wote huo, hizo soda ulikwenda kununua dukani,..mimi leo nataka kwenda kulala mapema, sitaki kusumbuliwa..umeshaleta, umeifungua kabisa..’akauliza na mimi nikakaa kimia.

‘Ndio kawaida yako..mimi sitaki mzaha hapa,...hata sitaki tena kuendelea kukaa huku nje...mimi nakwenda zangu ndani, …’akasema na aliposimama mimi nikajitokeza, uso kwa uso,…nikajikuta nashikwa na mshtuko mkubwa, maana aliyekuwa kasimama mbele yangu sio mwingine, ni yule mpenzi wa facebook…

NB: Haya naambie...naona imekuwa ndefu sana sehemu hii, nitamalizie sehemu ijayo, tuachane na kisa hiki.

WAZO LA LEO: Kutoa , kusaidia wengine ni mtihani, mtu anajiuliza hivi mimi mwenyewe maisha ndio haya ya kuunga unga, nitatoaje hiki kidogo, kumsaidia mtu mwingine....Tunasahau kuwa mpaji ni muumba wetu, na aliposema utoe usaidie wengine ana maana yake, kutoa huko inaweza ikawa ni sababu ya wewe kubarikiwa zaidi, …tukumbuke kuwa mkono utoao ndio unaopokea.

Kwa waumini wa dini ya kiislamu, tukumbue kutoa zakatul fitry.
Ni mimi: emu-three

No comments :