Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, June 19, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-54
Kesi iliahirishwa kwa jinsi hali ilivyojitokeza, washitakiwa hao muhimu wakakimbizwa hospitali wakiwa na hali mbaya kabisa,..na hakimu akasema kesi hiyo itaendelea kwa taratibu nyingine za kutambulisha ushahidi ambao hauwezi kusubiria, na kesi hiyo, itatajwa tena siku kadhaa mbele, na itategemeana na hali ya hao washitakiwa. Watu wakatawanyika kila mtu lake moyoni, wenye ndimi za kuongea hili na lile wakapata mwanya, na magezeti yakapamwa na vichwa vya kila namna.

Siku ya pili yake taatifa za majonzi zikasikika, washitakiwa wote wawili walisadikishwa kuwa wamefariki…, na docta mwenyewe alikwenda kuthibitisha hilo, alifanya hivyo, ili isije ikawa ni mbinu zao.

'Kweli wamefariki...na sijui kama kuna zaidi kwenye hii kesi, kwa vile ipo mahakamani, tutasubiria tusikie hakimu atasema nini...'akasema docta.

'Wanazikwa wapi...?' nikauliza

'Katika usia wa hao marehemu, walitoa maagizo kuwa pindi wakifariki, wanataka wazikwe karibu la mama yao,..'akasema docta

'Wapi huko...?' nikamuuliza

'Mhh, ni pale pale makaburini,...kiukweli watu wamehangaika sana kutafuta eneo hilo,..kaburi hilo lilitafutwa sana, na baadae likaja kugunduliwa sehemu ambayo haikutarajiwa, kumbe marehemu hao waliwahi kuligundua hilo kaburi..., wakalijengea, na mazishi yao tunatarajia yatafanyika kama walivyotaka,...'aksema docta.

'Mambo mengine...?' nikauliza


Tuendelee na kisa chetu….

***************

 Huku nyumbani kwa mzee, pamoja na hayo yaliyotokea huko mahakamani, kwao ilikuwa ni furaha, ni kama mgumba kapata mtoto, mimi ni mmoja wa watu walioalikwa,kwenye shughuli maalumu, ya kumshukuru mungu, na mambo mengine ya kifamilia. Sikupenda kwenda, kwani akilini nilikuwa na mawazo mengi sana, sijui kwanini.

‘Au unamuwaza sana mpenzi wa facebook..?’ akaniuliza docta.

‘Kwani nimuwaze wakati kumbe huyo sio mwanadamu, ila kiukweli docta, nahisi, anafanana fanana na huyo binti..'nikasema

'Kweli eeh, ni vizuri basi,...kwenye hiyo shughuli, nataka upate muda wa kuongea naye...'akasema docta.


'Mhh....sijui, naona bado mapema...'nikasema

'Huu ndio wakati muafaka,..chelewa chelewa utamkuta mwana sio wako...'akasema docta,

'Mhh, sijui kama atanisamehe....japokuwa siku ile , sijui ni shetani gani yule...na yule mwanamke nikimuona tena, ...sijui nitamfanya nini...'nikasema

'Hayo yamepita, ...ila niambie wewe unawaza nini,nimekuona huna raha kabisa...'akasema

'Hakuna kitu docta....'nikasema

‘Ninajua ni kitu gani unachokiwaza, lakini usijali, nakuhakikishia mambo yote yatakwenda vyema…’akasema docta.

‘Sidhani kama unaweza kuisoma nafsi yangu kihivyo, ujue docta hivi sasa, nina mambo mengi kichwani, ukizingatia kuwa shughuli hii nzima imenifanya nisiwe na kipato chochote, kwahiyo hata ikitokea lolote nitakuwa kama mtazamaji tu…’nikasema.

‘Ukumbuke wewe ni msaidizi wangu, upo kwenye ajira yangu, usijali..hilo ni moja ya jambo nililokuwa nikiliwazia, kuwa unawaza hivyo,…’akasema.

‘Na jingine…?’ nikauliza

‘Jingine litajitokeza hivi karibu, muda utasema sitaki nikuambie, kama unavyonijua , mimi huwa nafanya mambo baada ya vipimo…’akasema docta na kutabasamu.

Mimi nikazama kwenye mawazo yangu nilikumbukia tukio hili, baada ya mahakama...

************

 Ukumbuke, kuwa yule mzee kigagula aliniambia nihakikishe nimefanya yale aliyoniagiza kwa yule binti wa mzee ili aweze kuzindukana, tendo hilo kwa mujibu wa docta, nilitakiwa nilifanye mahakamani siku ile pale mahakamani, lakini kutokana na yaliyotokea, ikabidi zoezi hilo lisifanyike…ila docta na muendesha mashitaka walimfuata hakimu na kumuomba hilo zoezi likafanyikie hosp, mbele ya hakimu mwenyewe kama moja ya ushahidi.

Basi hakimu akakubali, na ndio maana akatangaza kuwa ushahidi mwingine ambao hauwezi kusubiria, utaendelea kufanyika kwa mujibu wa sheria, na tulipotoka tu pale tukaelekea huko hospitalini, wakiwemo mawakili wa utetezi,..

 Nilipofika pale, tulimkuta huyo binti kalala tu… , na docta akamweka sawa,..

‘Hebu mwekeni hivi, kama kakaa…’akasema docta,na akawekwa hivyo, alikuwa kalegea mwili mnzima..kama vile mwili hauna mifupa..anaangalia lakini hawezi hata kugeuza kichwa,..ile hali iliwafanya wazazi wake hasa mama kuanza kulia,..baba mtu akajitahidi na kuwa karibu na binti yake, akakaa pembeni yake akisaidia kumshikilia.

‘Kweli mwanangu atapona…?’ akauliza mama

‘Atapona , usijali….’akasema docta, na kuniangalia mimi, na mimi nikasogea pale karibu yao, nikiwa na kile kichupa tayari mikononi, nikautoa ule unga nikaushika mkononi, nikaongea yale maneno, na kuomba kwa mwenyezimungu amjalia huyo mgonjwa apone, na nilitamka hayo maneno ya kumuomba mungu kwa nguvu na wote wakaitikia ‘amin’…nikamrushia huyo mdada huo unga usoni, nikafanya kama nilivyoelekezwa..

Mdada huyo akafungua macho…akatikisa kichwa,apiga miayo…alikuwa kama mtu anayetoka usingizini, na alipoona watu wamemzunguka na yupo kitandani, akahisi mashaka kidogo, akafunga macho kama kuvuta kumbukumbu, halafu, akaangalia kama anajiuliza, na docta akasogea na kumfanyia mambo kadha wa kadhaa, …mimi nikasoge nyuma na kuiachia familia iendelee naye..

‘Anahitaji kuoga, na akiwa tayari, tutaweza kuongea naye…’akasema docta.

‘Baada ya zoezi hilo, binti akaanza kuhojiwa mbele ya hakimu, yeye ni nani, ilitokeaje, na yeye akaanza kuongea;

‘Mimi ninachokumbuka, ….ilikuwa nipo na ndugu yangu, baada ya kutoka sehemu, tuliyokwenda kumtembea rafki yangu mmoja,…’akasema na kukatisha.

‘Usijali, wewe endelea tu..’akaambiwa.

‘Nilipotoka huko kwa huyo rafiki yangu, nisingelipenda kumtaja,…’akasema

‘Sawa endelea….’akambiwa.

Nikawa sina raha , kuna mambo yalitokea, naomba nisiongelee kuhusu hayo…’akasema

‘Ni muhimu ukayaongelea maana yana taarifa ambazo tunahitajia kuzihakiki, je ni kweli yaliyosemwa na watu ‘akaambiwa.

‘Ah…sipendi kwakweli…taarifa gani kwani…?’akasema na kuuliza

‘Huyu hapa ni hakimu, nahakimu anataka kusikiliza ukweli wote, …’akaambiwa.

‘Hakimu..!!’ Hakimu wa nini…?’ akauliza

‘Yalitokea kwako, imekuwa ni kesi, na leo kaja kukuona, na angelipenda kusikia yote yaliyotokea kwako…’akaambiwa

‘Oh, kumbe mlishitaki, sawa..na huyo mtu kakamatwa…?’ akaulizwa

‘Ndio..ndio maana tunataka kusikia ukweli kutoka kwako, ..kasikilizwa yeye na sasa ni zamu yako…’akaambiwa.

‘Oh, haya…mimi nilipofika kwa huyo rafiki yangu, hatukuelewana, ikabidi niondoke, nikarudi kwa ndugu niliyekuwa nimemuacha mahali..’akasema

‘Hamukuelewana kwa vipi, ni muhmu sana hapo, tunakuuliza hivyo, kutokana na taarifa zilizojitokeza baadae, tunataka kuhakiki ukweli wa habari hizo..’akaambiwa.

‘Ni waulize kwanza ni habari gani hizo, …maana haya mengine ni mambo binafsi au , mimi sijui kulitokea nini, na haya maswali, na hakimu, aah, mnanichanganya..’akasema

‘Tutakuja kukufahamisha vyema baadae…ila kwa vile hakimu ana haraka, yeye anachohitajia kutoka kwako ni ukweli halisi , ulitokewa na nini hadi ikafikia hatua hiyo…. na ukweli huo utawekwa kwenye kumbukumbu za kimahakama…’akaambiwa, na binti yule akatulia, halafu akageuka kuwaangalia wazazi wake.

‘Wewe ongea ukweli mtupu, maana yote tunayajua sisi, lakini kuna mambo yalitokea na yanahitajia uhakiki, ukweli wako utasaidia kuweka mambo hayo sawa…ongea kila kitu, na wala usiwe na wasiwasi…’akaambiwa.

‘Haya, sawa kama wazazi wangu mpo tayari, ..ninachowamba mnisamehe, maana nilikiuka maagizo yenu, lakini ujue mimi ni msichana, na msichana wakati mwingine ndio hivyo, kuna kuhadaika, ..mimi nilihadika na mvulana, akaniahidi kuwa atanioa, na siku hiyo nilitaka kwenda kumpa jibu kuwa mimi nimekubali au la..kiukweli nilishamkubalia, kwahiyo nilitaka kumuambia hilo ili afuate taratibu , aje yeye au mshenga kujitambulisha nyumbani…’akaanza kuongea.

‘Nilipofika nyumbani kwake, nilikuta ….nilimkuta yupo namsichana mwingine, ..niliwahi kuambiwa kuwa rafiki yangu huyo ana msichana mwingine nikakataa, sasa siku hiyo ndio nikathibitisha, kwa macho yangu…’akasema

‘Uliwakuta katika hali gani…?’ akaulizwa.

‘Mhh..yule msichana ndiye aliyefungua mlango, akiwa kajitanda khanga moja tu, kwanza nikawa siamini, nikamuuliza huyo msichana, kuwa huyo rafiki yangu yupo wapi, akasema yupo chumbani, mimi nina shida gani na mchumba wake.

‘Mchumba wako..!?’ nikamuuliza kwa mshangao, akasema;

‘Ndio kwani wewe hujui…’akasema na mara nikasikia sauti ya rafiki yangu huyo akiuliza kutokea ndani,

‘Ni nani huyo,unayeongea naye..’akauliza hivyo,  na huyo msichana akasema;

‘Ni Malaya mmoja hivi, eti anakuulizia,..’akasema na huyo akajibu.

‘Mimi sina Malaya …kama ni Malaya mwambie aondoke zake…’akasema hivyo tu, kiukweli kauli hiyo iliniuma sana, lakini nikataka kuhakikisha hicho ninachokiona kina ukweli ndani yake, nikamuomba huyo msichana nionane na huyo mpenzi wake kama anavyodai kuwa ni mpenzi wake, yeye akasema;

‘Huwezi kumuona, kwanza umetukatishia sterehe zetu, pili unanipotezea muda wangu..’akasema na kufunga mlango…Mimi sikuwa na jinsi nikageuka na kurudi zangu, kwenda pale nilipokuwa nimemuaacha mdogo wangu.

Nahisi yeye aliponiona nilivyo, akajua kuna tatizo, hakuniuliza kitu..na wakati huo, nilihisi kichwa kikizidi kuniuma, ..maana nyumbani kwetu kulikuwa na matatizo mengi, hatulali usiku, ..aah, sijui ni mitihani gani, lakini mimi sikuijali, nilijua ni watu tu wanataka kutusumbua!

Basi tulipofika kwenye duka moja la madawa, nikamuambia mdogo wangu nataka kununua dawa za maumivu, yeye aliniambia ni bora twende hospitalini, mimi nikamwambia hapana, ..nataka dawa za kichwa, nikalale nyumbani..nilisema hivyo tu, sikutaka kuongea zaidi….kuna kitu kilikuwa kinavuta, ni hisia ambayo nilikuwa napigana nayo,..lakini..’akatulia

‘Ulikuwa unahisi vipi..?’ akaulizwa

‘Kwa mfano hata hiyo kununua dawa, mmh..nilitaka nifike nyumbani nilale tu, sikupendelea dawa, ila hiyo hali ikanivuta tu, niende kununua hiyo dawa…’akasema.

 Nilipofika pale dukani, kwenye hilo duka la dawa, muuzaji akaniambia niingie chumba kingine,..

‘Chumba kingine kwanini..?’ nikamuuliza

‘Dawa utapata huko usijali…’akasema

Basi mimi sikutaka kubishana naye sana, nikaingi ahicho chumba kingine..ni chumba cha dawa, lakini kimetengenishwa na viyoo, unaona sehemu fulani ya ndani kuwa ni chumba cha dawa, lakini sehemu kubwa huoni ndani, kumewekewa tinted..’akatulia kidogo.

 Muda ule nilianza kuhisi hasira, nikiwazia hayo ya nyuma, nikiwazia, …hilo nililolikuta kwa huyo rafiki yangu, lakini sikuwa na…yaani mpaka hapo nilikuwa sijaamini, kuwa ni kweli,..sijui nisemeje,….kuna hali ilikuwa inajijenga kichwani, sikupenda hiyo hali lakini ikawa inajichochea, ni kama mtu ananiambia;

‘Nilikuwambia huyo rafiki yako sio mtu mwema, unaona sasa, umemfuma moja kwa moja, unataka ushahidi gani tena,..dunia itakucheka,..ni bora ufanye kitu, …umkomoe huyo rafiki yako afungwe maisha…ni kitu kama hicho…hapana nikawa naikataa hiyo kabisa,..kwahiyo kichwani nikawa kama nahangaishwa na watu wanabishana….

 Basi huyo mtu aliponiambia niingie huko ndani, ..kwanza nikataka kumuambia sitaki tena hizo dawa, lakini hali ikaniambia nikachukue tu hizo dawa, ..nikatii, nikaingia ndani, kwenye hicho chumba, ilikuwa ni sehemu ya madawa pia, sikuwa na muda wa kujiuliza zaidi…

Ile naingia kwenye kile chumba, nikawa kama najiona …yaani kuna taswira imesimama mbele yangu, sawa sawa na mimi..kilichonifanya nijue kuwa sio taswira yangu ni pale nilipojaribu kuinua mikono, huyo..au hiyo taswira ilikuwa imesimama tu ikiniangalia,…akatabsamu, kama vile ananifahamu…

‘Uliona mtu au uliona taswira..?’ akauliza

 ‘Ni mtu…anafanana na mimi kwa kila kitu…hivi kweli huyo mtu yupo..?’ akauliza akigeuka huku na kule,..akawaangalia wazazi wake hakuna aliyemjibu, na yeye akaendelea kuongea.

‘Kiukweli, natamani nimuone tena, kwani ilikuwa kama najiangalia kwenye kiyoo, nguo, sura na kila kitu..najiuliza mpaka nguo …basi sikutaka lile lipite hivi hivi, kwa haraka nikataka kugeuka…

 Nikataka nigeuke nimuite mdogo wangu..ili aje ajionee na yeye,…., ooh, nilihisi mtu akinishika kwa nyuma, sijui aliniwekea nini puani, ...sikujitambua tena,..sijui nililala au ilikuwaje, lakini nahis ni kama vile mtu aliyepigwa sindano wakati anafanyiwa upasuaji…’hapo akatulia.

‘Kwahiyo muda wote ulikuwa hujui ni nini kinachoendelea, hadi leo hii..?’ akaulizwa

‘Naweza kusema hivyo,.ila kuna muda, ilikuwa…sasa sijui kuwa ni ndoto au ni, nini..kuna nakumbuka, hata sijui, …kuna watu walikuwa wakitoa damu..kiukweli siwezi kujua ..sikumbuki, ni hivyo tu..mpaka hivi sasa nazindukana, kwani,…muda gani nimelala…’akauliza

‘Ni muda kwakweli..lakini usijali, sasa hivi upo salama..na mengi utakuja kuambiwa, na usiwe na wasiwasi kabisa, tulitaka kuhakikisha hayo yaliyotokea je yana ukweli ..’akaambiwa.

'Labda nikuulize baada ya kumkuta huyo binti nyumbani kwa huyo rafiki katika hali kama hiyo, na maneno kama hayo,..aliyokuambia kuwa yeye ni mchumba wa huyo rafiki yako, ulijisikiaje…?’ akaulizwa

‘Mhh..wivu, hasira..lakini mimi niwaambie kitu kimoja, ..sijali, kama kapata mtu mwingine zaidi yangu, angeliambia tu, mimi ningelimuelewa, kabisa nisingelimlaumu sana, lakini siku ambayo natarajia nimpe kauli yangu kuwa nimemkubali ndio siku nakutana na hilo,..kiukweli niliumia, lakini yote ni mapenzi ya mungu, ningelifanyaje....maana hata hivyo, ilikuwa urafiki tu,…na yeye kama mwanaume alikuwa na uhuru wa kuchagua mtu mwingine, au sio…’akasema

‘Kwahiyo wewe hukufikia kutaka kunywa sumu, na ukanywa sumu kujiua,,?’ akaulizwa

"Kwann ninywe sumu,…mimi nani kawaambia kitu kama hicho,.. nijiue kwasababu ya mapenzi,..kwanini nifanye hivyo, hatukuwa tumefikia hatua ya kuwa labda keshaichumbia, ilikuwa bado mapema sana, hapana…hilo haliwezi kutokea kwangu hata siku moja, mungu anilinde…’akasema, na watu wakaangaliana, na yeye akasema;

 ‘ Hata hivyo, mimi sijaamini, nahisi huyo mdada alitaka tu ..lakini sawa sitaki kulifikiria zaidi, limeshapita basi kama kaamua hivyo, namtakia maisha mema, ….’akasema.

‘Kwanini hujaamini na wewe ulimkuta na mwanamke, na kwa hali hiyo…?’ akaulizwa.

'Mimi  namfahamu sana huyo mwanaume,...sio mtu wa kunifanyia hivyo mimi…nilitaka tu nimuone, nisikie kauli yake,…lakini huyo mdada hakuniruhusu, na nisingelilazimisha, unajua tena, kwanza pale nilienda kwa kujiiba, wazazi wangu hawatambui hilo….’akasema.

 'Kwahiyo wewe huna kinyongo na mchumba wako kutokana na tukio hilo, na kama akikuambia bado yeye yupo na wewe anataka muoane, upo radhi…?’ akaulizwa

'Aaah, hayo tuyaacheni jamani, nisingelipenda kuyalamba matapishi yangu, haina maana kwangu kwasasa..mimi naona..aah, hapana.., sitaki kujisumbua na mapenzi, kama mungu kapanga iwe hivyo basi, nimepokea hayo kama matakwa yake...na nitaendelea kumuomba mungu anipatie tu mume mwema, ni hilo tu…na sisi kama familia tuna matatizo mengi, yanahitajia kipaumbele, zaidi ya hilo..naombeni tafadhali kwa hilo , mliache kama lilivyo…’akasema

 'Ngoja kidogo, kuna kitu tunataka tukiweke sawa, Je unahisi hayo yaliyokukuta, mpaka ukapoteza fahamu ni sababu yake yeye,..?’ akaulizwa.

‘Kwanza sijui kama nilipoteza fahamu, mimi nilitaka nimfahamu huyo aliyenishika kwa nyumba akaniwekea kitu puani, huyo ndiye anastahiki kushitakiwa, alikuwa na dhamira gani,..huyo mtu, aah…kwanza ni nani huyo mtu.?’ akauliza

‘Huyo keshapatikana, ..ndio maana tunakuuliza tupate uhakika..’akaambiwa

‘Ni nani na alitaka nini kwangu..?’ akauliza sasa kwa sauti ya kukasirika.

‘Hayo utakuja kuambiwa muhimu kwasasa ni afya yako…unasikia, wewe tuliza kichwa, na hatua kwa hatua , utaambiwa kila kitu, usiwe na wasiwasi kabisa. Ama kwa maswala ya familia yako yote yameshawekwa sawa, hakutakuwa na matatizo tena..’akaambiwa.

‘Oh na nani…basi hizo ni habari nzuri natamani nimjue huyo aliyesaidia hilo,…natamani pia nirudi nyumbani, nimelala sana, kwani mimi naumwa, hapana ni usingizi tu, sijui, waliniwekea madawa gani…na hivi,…mdogo wangu yupo wapi…’akasema akigeuka kuwaangalia wazazi wake, na mara akakutana na sura yangu, akanitizama kwa muda, na mimi nikamuangalia tu.

‘Mdogo wako huyu alikuwa nje…’akasema mtu mmoja, na mdogo wake akawa anaelekea pale kitandani kuongea na ndugu yake, ila hali ya kukutana hawa mabinti wawili ilinifanya nihisi furaha moyoni kuwa hatimaye familia hii itakuwa na furaha tena..na sijui kama huyo binti ataweza kunisamehe..

Docta, akanisogelea na kuninong’oneza kitu sikioni, nikageuka kumfuata…


***********

Docta, alinishika mkono, tukatembea hadi nje halafu akasimama, na kusema;


‘Huu ni wakati wa familia, kuongea na binti yao, …ila nataka kujua kitu kimoja kutoka kwako.


‘Je sasa upo tayari kumuoa huyo binti, akikukubalia..?’ akaniuliza docta hilo swali, ilikuwa swali la kunishtukizia, na mimi nikabakia kimia kwa sekunde kadhaa…

Sikuweza kumjibu docta hilo swali, hadi leo tunaalikwa kwenda kwenye shughuli iliyoandaliwa na familia hiyo ya mzee....


NB: Nilijua nitamaliza leo, naona tusubiria sehemu nyingine ya kubainisha jabu langu na ni nini kitatokea kati yangu na huyo mdada, nikikutana naye mimi na yeye uso kwa uso,..


WAZO LA LEO: Mambo mengi hutokea katika maisha yetu, mazuri na mabaya, mengine yanaweza kutusumbua sana, mitihani juu ya mitihani, unaweza kufikiria labda kuna kitu,na wasio na subira watasema labda kuna mkono wa mtu. Tukumbuke kuwa sisi wanadamu matatizo, ni sehemu ya maisha yetu, na haya matatizo ni namna ya kutuweka sawa…na kutuvusha ngazi moja kwenda nyingine. Tusikate tamaa, tuzidi kujibidisha katika matendo mema, huku tukimuomba mola wetu, kwani baada ya dhiki huwa ni faraja. 

Ni mimi: emu-three

No comments :