‘Basi muondoeni huyo hiyo sura yake ya bandia tumgundue na
yeye ni nani, halafu tutaangalia kama tuna muda wa kumsikiliza na yeye …muhimu
tumfahamu na yeye ni nani, maana leo …’akasema hakimu, na kila mtu akawa na
hamasa ya kutaka kumjua huyo mtu naye ni nani..
Docta akafanya vitu vyake, akafanya kitu kwenye laptop yake,
na mara usoni kwa huyo jamaa, kukafutuka,
kama ilivyokuwa kwa mshitakiwa namba mbili,…na ikafunguka kama zipu, na docta
akafika pale mbele kumalizia hiyo kazi, lakini cha ajabu alipomkaribia huyo
jamaa, akafanya kazi ya kuondoa hiyo ngozi ya sura ya bandia…docta alipoiondoa,
kabla hajamaliza kabisa…,kwanza akasita akabakia kwa karibu dakika moja akiwa ameduwaa,….
Kuduwaa kile, kuliwafanya watu waingiwe na hamasa zaidi,
docta kaona nini mpaka ashikwe na butwaa, …na muheshimiwa hakimu akauliza;,
‘Vipi docta umeona nini…mbona umeshikwa na butwaa…?’
akaulizwa.
Docta hakujibu,..hakusema neno, akaivuta ile ngozi bandia,
na kutembea kurejea sehemu yake kwenye laptop,..akimuacha huyo mtu, ili kila
mtu ajionee yeye mwenyewe, …
Watu walijivuta…hata waliokuwa nje wanataka kuingia ndani,
askari nao kwa vile wana hamasa ya kuona wakajikuta wanaachia watu wanaingia…,
na wale wasio na simile, waliokuwa wamekaa, wakasimama ili wamuone vyema huyo mtu,
kwani sasa jamaa alikuwa anaonekana, japokuwa alikuwa kainamisha kichwa chini,…lakini
kwa anayemfahamu alishamtambua mara moja,…
Sasa kile kilichotokea kwa docta, kikawatokea na
wengine,..watu walibakia mdomo wazi, kwa mshangao, na tofauti na walivyofanya kwa mshitakiwa namba
mbili, ambapo watu walipiga kelele, kwa huyu sasa, watu walibakia kimia, kilichoongea
ni macho na midomo yao…macho yaliwatoka , na mdomo ukabakia wazi,..ni hisia ya
aina yeka!
Mbele kwa hakimu,…ndio ikatokea mpya, mara nyingi hakimu
anajitahidi sana kuficha hisia zake, lakini safari hii, …hakimu alishindwa
kujizuia, akafikia kusimama, na usoni, akaashiria kukunja uso, wa
kutokuamini,..akawa kama anasogeza shingo kuangalia vizuri, na alipohakikisha
alichokiona kuwa ni sahihi, akawageukia wenzake, wazee w baraza, wazee walikuwa
nao katika ile hali ya kushangaa..
‘Mungu wangu hii ni nini jamani…’akasema hakimu.
‘Ndio hapo mjionee, wenyewe, ni kwanini tuliamua ushahidi
huu uonekane mbele ya mahakama, kiukweli hatukutarajia hili, ila …tulitaka
muone jinsi watu wanavyobadilika wakivaa hizo ngozi, lakini sasa imekuwa zaidi
ya kubadilika,..tujionee wenyewe….’aliyesema sasa ni muendesha mashitaka.
‘Hii ….imenishitua sana…hebu inua kichwa watu wakuone vizuri….’akasema
hakimu, kidogo akionyesha lugha ya unyenyekevu, tofauti na ilivyokuwa kwa
mshitakiwa namba mbili!
Jamaa, mshitakiwa namba moja, alikuwa bado kainamisha kichwa
chini, taratibu akainua kichwa chake, na sasa akawa anawaangalia watu, na hapo
watu hawakuweza kujizuia, wakaanza kuzomea, kupiga kelele…na jamaa akaanza
kucheka, kule kuanza kucheka kwake, kukawafanya watu wakanyamaza, yeye
akaendelea kucheka, mpaka akawa anatoa machozi, halafu akabakia kimia,…
‘Ni ajabu kabisa…halafu unacheka…hivi unataka sisi
tukueleweje, hasa mimi ambaye ninakufahamu sana…lakini sio kukufahamu kwa tabia
hiyo, mimi kwangu wewe ulikuwa mwalimu, ulikuwa mzazi, ulikuwa…aah, siwezi hata
kuamini hii, ina maana na wewe upo kwenye kundi hilo haramu ..nasikitika sana…’akasema
hakimu, sasa akitaka hata kutoa machozi.
‘Unajua ni kwanini nacheka,…nacheka, kwa vile …hahahaha,
sikutarajia kuwa ipo siku na mimi nitaweza kusimamishwa hapa, nimezoea
kuwasimamisha wengine hapa,..sikutarajia kuwa nitakuja kuumbuliwa hivi, ..lakini
zaidi,..na kwa kuona watu walivyotoa macho ya kunishangaa, mnashangaa nini…eti,
mnaona kipi cha ajabu, kuwa mimi nami nimo,…jiulizeni mara mbili, kama
alivyotangulia kuongea mshitakiwa namba mbili, alisema nini….’akatulia
‘Mjiulize kwanza ni kwanini mtu kama mimi nikajiunga na
jambo kama hili..sio kitu kidogo, sio kitu rahisi…..sasa mimi ndio mimi, kwenye
sura yangu halisi,…mimi sina kawaida ya kuficha sura yangu…mbele ya watu kama
nyie, nina kawaida ya kuficha sura yangu nikiwa kazini ..kwenye kaz zetu…
‘Na ikitokea mmoja wapo akanitambua, basi hatanitambua tena…hataweza
kufungua mdomo wake tena…kwasababu gani, ..kwasabau sikutaka nijulikane mimi ni
nani, sikutaka,..nije kupata fedheha, kama fedheha, niliyoipata hii leo,
sikupenda nije kudhalilika tena nilishadhalilishwa sana, jamani tuliwakosea
nini wanadamu wenzetu....nilimuomba mungu sana, ikiwezekana aichukue roho yangu
kabla tendo hili halijatokea, lakini haikuwezekana..
‘Najua muda wangu kuishi bado upo...lakini nibado masaa
macheche tu..kwani kama ilivyotokea kwa wengine, kuwa wakiniona hawatapata
nafasi ya kuniona tena, sasa ni zamu yangu, mumeniona na hamtapata nafasi ya
kuniona tena, nikiwa napumua..hamtaamini hili, ila…ndivyo itatokea...’akageuza
kichwa kuangali kushoto na kulia, halafu akageuka kuangalia kule alipokaa yule
mama, …
Yule mama aliyekuwa kasimama kipindi kile, mshitakiwa namba
mbili anaongea sasa alikuwa kakaa, akionekana hana raha,…lakini kwa kuonekana
kwa huyu mshitakiwa namba moja, hata yeye, alijikuta akishikwa na bumbuwazi,
hakuna aliyetegemea hili kabisa,….na mama alipoona huyo mshitakiwa anamuangalia
yeye, akajua kuna neno kubwa linakuja tena dhidi yake, hakujua ni neno gani.
‘Najua wewe mama, una neno la kusema dhidi yangu, ukikumbuka
kuwa mimi ndiye niliyekuwa nikizimisha kesi zako zikifika kwangu, sasa umepata
jibu sahihi, kuwa ni kwanini ilikuwa hivyo….’akaanza kuongea.
‘Mimi ni hakimu wenu, nimekuwa nanyi kwenye mahakama hii kwa
muda mrefu sana, mnanifahamu kwa sera zangu, na mlikuja kushaangaa jinsi gani
nilivyoweza kuipiga dana dana kesi hiyo ya huyo mama,…kwa wajanja wangeliligundua
hili mapema kuwa kuna jambo, lakini hakuna alieyeweza kulifikiria hili..
‘Huyo docta, alinifanya nihisi kuwa kanigundua, lakini
baadae nikagundua kuwa hajanigundua,..na isingelikuwa uzembe wa …hawa jamaa..isingelikuwa
kukosea kwa huyo mtaalamu marehemu,…..na isingelikuwa huruma…..iliyonishika,
nikawaza mbali, na ..labda bado ingelikuwa kitendawili cha kunipata
mimi..lakini wanasema lililopangwa limepangwa, lazima litatokea..hapo akatulia
kidogo.
‘Najua hakimu, unataka nijitambulishe rasmi, nasita kukuita
muheshimiwa hakimu, maana wewe ulikuwa mwanafunzi wangu kikazi,mimi ni bosi
wako, maana nilikupokea, nili..kusaidia ukawa mzoefu, sasa leo unahitajika
kunihukumu mimi ni ajabu kabisa..sawa fanya kazi yako….’akasema.
‘Kwenye sheria hakuna mkubwa, …sasa hivi upo chini ya
mamlaka yangu, haya, tuambie rasmi wewe ni nani..?’ akauliza.
‘Mimi kwa jina ni…..(akataja
jina) halafu akaendelea, ‘ Na kwa
kikazi, mimi ni, hakimu,…hakimu mkuu wa mahakama hii, ambaye mnamfahamu sana, ndio maana wengi
mlitoa macho karibu ya kudondoka , kwa
mara ya mwisho mimi ndiye niliyekuwa nikisimamia hii kesi, nikaamua nikae
pembeni, maana nilishaona nikiendelea nayo mnaweza kunishuku.
‘Aaah,..nashukuru sana, kuwa leo, na mimi ni mshitakiwa,
nashukuru kuwa na mimi nitapata nafasi ya kuelezea, madhalimu
nili..yaliyonikuta hadi nikafikia hapa…’akasema kwa kusita sita, ilishaonekana
hayupo vizuri kiafya, tokea awali.
‘Kumbe ndio maana…’aliyesema sasa hivi ni yule mama, mke wa
mzee.
‘Kumbe ndio maana, hahaha,…ndio… wewe usiongee kabisa, maana
wewe ndiye chanzo cha haya yote, ..’akasema.
‘Na wewe unasema hivyo, mimi nilikufanyia nini kibaya wewe,
wewe ndiye mbaya maana kila kesi yangu ikitajwa unaipiga kalenda, ni kwanini..?’
akauliza huyo mama.
‘Nashukuru sana, kuwa ni wewe umeliuliza hilo swali badala
ya muendesha mashitaka, na mimi sitakwenda mbali sana, sitaongea sana,
maana,..muda sina..ila nikujibu swali lako kwa maelezo mafupi tu.
‘Hivi wewe uliposikia kuwa binti yako kafa kwa kunywa sumu,
na ukahisi kuwa hakuinywa sumu hiyo kwa kukusudia…, huenda alifanyiwa jambo
mpaka akafikia hatua hiyo, uliwazia kufanya nini moyoni mwako, kama kweli kuna
mtu alifanya hayo na ndio ikafikia binti yako kunywa sumu, sema ukweli wako..?’
akauliza.
‘Kwahiyo wewe ndiye ulifanya yote hayo..?’ akauliza mama.
‘Unajibu swali au unaniuliza swali…’akasema huyo mshitakiwa.
‘Nakujibu…’akasema huyo mama na watu wakacheka.
‘Na mimi nakujibu ..ndio, ni mimi ndiye niliyefanya yote
hayo..ni mimi nilitengeneza namna kufanya binti yako anywe sumu…ili afe, ili
tumchukue kama msukule kwa ajili ya kufanikisha lengo letu, unajua
tulifanyaje..’akatabasamu kidogo.
‘Mashetani wakubwa nyie….’huyo mama akasema kwa hasira.
‘Wewe unatuona hivyo, lakini nyie hamjioni…Mimi kama
mtaalamu wa kupanga mambo, kitaalamu..niliweza kulipangili hilo tukia kwa namna
yake,..kwanza kwa kuhakikisha kuwa kuna mfarakano kati ya binti yako na mchumba
wake wa siri, haya yalianza mapema sana….huyo mchumba wake wa siri, mpaka leo
hajui kuwa mipango ya yeye, kumpata mwanamke mwingine na kuweza kumuumiza
mpenzi wake wa siku nyingi..hiyo namna ilipangwa na sisi..hajui mpaka leo,
muulizeni..
‘Jamaa akakutaka na msichana tuliyemuandaa, akiwa na sura ya
mvuto, hakujua kuwa sura ile sio sura sahihi ya huyo binti, huyo binti alikuwa
ni kahaba tu, tulimsomesha, tukamtengeza, akajibu..na akaisambaratisha ndoa ya
wapendwa hao..na wengine tuuliotaka wafanyiwe hivyo, hiyo ndio kazi ya shetani,
kafarakanisha ndoa…’akatulia.
Siku mdada, binti yako anafika kwa huyo mchumba wake
akamkuta jamaa yupo na binti, ..ni nini alichokiona na ni nini kilichomfanya
atoke pale akilia, mtakuja kumuuliza yeye mwenyewe..ila lengo letu ilikuwa
ashikwe na hasira, na hiyo hasira iwe ni sababu ya tendo litakalofuata..
Binti alipotoka pale, akakutana na ndugu yake,
hawakuongea,..ndugu yake alihisi kuwa ni hasira, ni tabia ya ndugu
yake..hakujua kuwa ni sisi tulikuwa tunacheza na akili za dada yake..kuna muda
dada yake alitamka maneno,…’ni bora nife, ni bora nife..’ haya maneno
hakuyatamka yeye kwa kupenda,…yalitamka na mbinu zetu, huyo binti hana udhaifu
wa kufikia hapo, huyo binti ni jasiri sana, aliyemfahamu zaidi ni baba yake..
‘Haya, binti akafika dukani kununua dawa…muone hapo…, binti
alifika duka la dawa, wakaingia na ndugu yake, ndugu yake, akawa anakagua vitu
vingine vipodozi sijui.., huyo dada yake akawa anaongea na muuza dawa, muuza
dawa akamuambia ingie chumba kile, …hizo dawa atapewa huko…uone ilivyotokea…
‘Toka lini hizo dawa zikauzwa chumba hicho kingine, na
kwanini huyu ndugu yake hakuweza kulishutukia hilo, na kujiuliza ilikuwaje
hapo..akili zililala..mara nyingi watu hatuna tabia za udadisi,, hamna tabia ya
utafiti..kitaalamu,…, mara nyingi watu hukimbilia kwenye tukio, wakazusha mambo
yasiyothibitishwa kitaalamu,..lakini akili zetu hazichimbi ukweli wa jambo.
‘Yule mdada kwa muda huo alikuwa sio yeye, akaingia huko
alipoelekezwa, na huko, akakutana na mdada mwingine sura sawa sawa na ya kwake,
kama mtaweza kumrejesha kwenye hali yake, mtamuuliza hilo yeye mwenyewe, kama
atakuwa na kumbukumbu, maana huyo sijui....ila ninachotaka kuwaonyesha hapa ni
muone jinsi gani tulilipangilia hili tukio kitaalamu.
‘Mdada anaingia chumba alichoambiwa anamkuta pacha….sio
pacha wa kuzaliwa bali ni pacha wa sura, akashika na mshangao, ni kama
anajiangalia yeye kwenye kiyoo…na hakupewa muda, mimi nilikuwa nyuma ya mlango
nikasogea nikamweka kitambaa puani kutokea nyuma,na kitambaa hicho kilikuwa na
dawa ya kumlewesha na kumtoa fahamu za kibinadamu, na kutokea hapo akawa hayupo
kwenye hii dunia.
Yule mdada pacha wake, akatoka sasa akiwa kashika dawa, za
maumivu ya kichwa, akakutana na ndugu yake wakaondoka kurudi nyumbani…huyu sasa
alipewa aina fulani ya dawa, ni sumu, lakini sio sumu ya kuua moja kwa moja, ni
sumu ya kumuonyesha mtu kuwa amekufa..lakini akirudi kwetu kuna dawa tunampa
inaondoa ile sumu anarudi tena kwenye hali yake ya kawaida.
‘Binti kafa, bint kajiua..ikaenda zaidi kama tulivypanga,
..kajiua kwasababu mpenzi wake kamkana…na…huko hospitalini, kulikuwa na watu
wetu, vipimo vikaonyesha huyo binti alikuwa na mimba..hahaha, huyo binti hakuwa
na mimba,ila kwa mbinu zetu, tulimuwekea kitu, mtu akipima anaona kuwa ana
mimba, …lakini hakuwa na mimba,
‘Na zaidi binti wa huyo mama, hajawahi kutembea kimapenzi na
huyo mchumba wake, muulizeni mwenyewe, huyo msaidizi wa docta,..atawaambia,…na
uzushi huo unatokea wakati huyo binti ni marehemu, usoni mwa watu, kwahiyo
hakukuwa na mtu wakumuuliza ili aseme ukweli…, umbea ukasambaa, na lengo letu
likatimia, na mtu wetu tuliyemtaka sasa akawa mikononi mwetu…kazi ya kwanza
kubwa ikakamilika.
‘Unajua ni kwanini tulitaka kumpata huyu binti, kwanza ni
kwa ajili ya kisasi, hili lipo wazi, mtasema huyo binti anahusikanaje, sisi tulihusikanaje
mpaka tunaswekwa jela…,..lakini zaidi ni baada ya kutambua umuhimu wa hivyo
vifaa vitatu,..na zaidi matambiko yote, yalihitajia damu, na damu iliyohitajika
ilikuwa ya kutoka kwenye familia husika,..na damu hasa iliyohitajika ni ya huyo
binti, huyo binti alikuwa na …viasilia vyote vya mababu zake..
‘Kwahiyo kila tulipotaka kufanya tambiko, damu ya binti
ikawa inachukuliwa…mambo yanijipa, lakini..bado kuna jambo lilitakiwa
lifanyike,..kuvipata hivyo vitu vingine….bahati nzuri, yakatokea matukio
ambayo, yaliwezesha hivyo vifaa virudi huku kwetu, hilo hatukufanya sisi…na
hadi tunahangaika awali hatukujua kuwa vifaa hivyo vipo mikononi mwa huyo mzee,
baba wa hao mabint, mume wa huyo mama..haya yalitokea tu..ila sisi tukacheza
upande wetu, kuhakikisha kuwa, hivyo vifaa vinakuja kwetu…baada ya kuambiwa na
huyo ndugu wa huyo mama kuwa vifaa hivyo sasa vipi mikononi mwa mume wake.
Sasa kabla ya hayo, tuliambiwa kuwa ili hilo zoezi
likamilike, ni lazima atafuwe mtu,…mwenye damu sahihi, mwenye moyo..wa pendo kwa
huyo binti, awe ni vinasaba vinavyoendana na huyo binti…ni kazi kubwa kumpata
mtu kama huyo,
Tukabuni mbinu..kwa kutumia mtandao,kuanza kutafuta mtu kama
huyo, akili ya mtu akiona sura tu, anaweza kuhisi kuwa huyu nampenda, na hisia
hizo, zikienda mbali, bsi viasili hivyo vinakuwa vimeivana,..
Ilichukua muda kidogo, lakini baadae tukafanikiwa, mpenzi wa
facebook, akamnasa mtu,…na mtu aliyemnasa ni yule yule mpenzi wa zamani wa huyo
mdada, kumbe kweli,.. tukaja kugundua kuwa mpenzi wa binti, yule yule ana viasilia
sahihi, ..na zaidi watu hao wanapendana, na wakikutana wanaweza kuoana, hata
bila hata ya kutumia uchawi wetu..mungu atupe nini..
Tulipompata huyu mtu, tukaanza kazi ya kuingia kwenye kichwa
chake kwa kumtumia shetani,….tukamvuta tukawa sasa tunasoma hisia zake,..ni
uchawi , lakini uchawi wetu wa kisayansi,….tumeshampata sawa, sasa atajileta
vipi, ndio hapo sasa tukamtumia shetani wetu…mpenzi wa facebook..
‘Mtajiuliza shetani ataingizwaje kwenye mtandao, ..hahaha,
kwani shetani ni nani,..hapo tumieni akili zenu vyema, kwani shetani ni lazima
awe shetani kama shetani, au matendo ya mtu yanaweza kumfanya mtu akawa ni
shetani,… shetani anaweza akawa mtu kutokana na matendo yake, watu hufanya
mambo ya kishetani zaidi ya shetani mwenyewe…kwanini tushindwe kulifanya hilo…hilo
linafanyika hata bila kutumia uchawi..ni akili tu..
‘Mpenzi a facebook akatengenezwa akaingizwa kwenye facebook,
na bila kukosea, akakutana na mlengwa,…sura ikamvuta jamaa, na sisi tukawekeza
mambo yetu, jamaa akawa hoi..halali, hali, hanywi…huyu hajanyweshwa limbatwa, tunacheza
na akili yake tu,…huyu akawa kalogewa akawa anachati hadi kwenye usingizi ,
akiwa usingizini anakutana na sisi, tunazidi kumuharibu…mpaka leo mpenzi huyo
yupo kichwani kwa jamaa, muulizeni kama natania..
‘Mapenzi ni kitu cha ajabu sana, sisi tuliligundua hilo,
tukawa tunatumia madhaifiu hayoi ya kibinadamu ya kupenda .. kuwanasa watu
wetu, wangapi tuliwatengenezea ugoni,..ili tuwapate, ili waje kuogopa, maana
tukionyesha mapicha hayo mabaya ya ugoni wao, kwa wenza wao, watavunja ndoa zao…ni
ushetani ulitengezwa..na akili za watu hunaswa zaidi kwenye shetani huyo wa
mapenzi.
Mpenzi wa facebook, akafanya kazi, yake,…matukio yaliyofuata
sasa, ni michezo yetu, tukamuita, hadi makaburini, ambapo tulipanga tumnase,
lakini nyota ya huyu mtu, ..ogopeni sana mcha mungu, mtu anaweza kuwa mcha
mungu kutoka moyoni, lakini msimuone kama ni mcha mungu, anakuwa na imani kweli
ya mungu wake..hebu fikiria, tokea ashutumiwe kuwa yeye ndiye chanzo cha huyo
binti kuwa alimpa mimba, aliwahi kusema sijawahi kutembea na huyo binti…?.
‘Ni kwanini mpaka leo hajasema hivyo…hahaha, huyu ni mtu aliyeiva
kiimani, aliogopa kusema hayo, akamuachia mungu, ..muulizeni, kama nasema
uwongo, yeye alisema mungu wewe ndiye unajua ukweli wa haya yote, na siku huyo
mpenzi wangu ananifuma, sikuwahi kutembea na huyo mwanamke aliyenikuta naye,
ila sijui ilitokeaje…na mpaka leo najuta, je iweje nisingiziwe mimba,
..sitaweza kulisema hili kwa watu, nakuachia wewe mungu wangu…
‘Muulizeni hakuyasema haya akiwa peke yake akimuomba mungu
wake,..sasa huyu ni mcha mungu wa kweli, lakini usoni kwa watu hajulikani..na
hataki kujionyesha kihivyo, yeye aliweka kipaumbele chake cha kutokuogopa, na
hiyo ni pia ilimsaidia sana kama kinga zake ambazo, zilitufanya tushindwe
kumpata kwa haraka…, maana ili mashetani yetu yaingie kwenye akili za watu ni
mpaka..huyo mtu tumjaze hofu..huyu jamaa ana ujasiri wa ajabu, hajengeki na
hofu harakai,…’akatulia
‘Lakini sisa hatukata tamaa, tukawa tunamlewesha kwa namna
nyingine nyingine, na kama angeliwahi kuingia kwenye lile pango mapema,…kwa kupitia
lile kaburi, tungelishamaliza kazi yetu,..lakini haikuwezekana hivyo…na..na ok…’akashika
kifuani, kuashiria anahisi maumivu.
‘Tunamshukuru sana mzee Kigagula, mzee huyo ndiye
aliyetuwezesha mambo mengi ya nguvu za giza, lakini ikafika mahali, tukagundua
akiendelea kuwepo, nguvu zake za giza zitatugeukia na sisi, maana yeye kila
jambo kafara la mtu, kila jambo..kafara kafara, mpaka lini, tukaona huyu
hatufai tena, kwanza uhakika wa kuvipata hivyo vitu umeshakamilika, huyo mzee
wa nini, hakuwa na umuhimu kwetu, ….
‘Kwahiyo alipotuletea mtu wetu ndani ya pango, tukaona basi yeye,
arejee kwa mizimu yake, iliyokuwa ikimsubiria kwa hamu, hatukuweza kumlinda,
maana pamoja na mambo yake, sisi tuliweza kumlinda na mizimu yake ambayo
ilishataka kummaliza yeye mwenyewe kwa kuvunja baadhi ya masharti, ambayo
anayajua yeye mwenyewe.
‘Ndugu zanguni…haya mambo, hatukuyafanya kwa kupenda,
narudia, tena sio kila mtu anayefanya mabaya, ni mbaya, kuna wengine
wameshinikizwa, kutokana na madhila waliyokutana nayo,..watu wanateseka kizazi
kwa kizazi, watu wanateswa familia zao, kila siku watoto wanaumwa, wanapata
matatizo mbali mbali, wanafukuzwa shule, watoto wanafelishwa majina yao
yanachukuliwa na watu wengine, haya hamyaoni….
Wapo watu..wanafanyiwa mabaya mengi tu…wengine wanafungwa
hata bila kosa, na huko jela wanakutana na matatizo, huku nyuma familia zao
zinataabika, wananyang’anywa kila kitu, watoto wanaishia kuwa machokoraa,
wakati wazazi wake walikuwa na mali… na huyo mtu aliyewafanyia hivyo,yupo,
anatesa..anaishi maisha ya raha,..hivi wewe ukitoka huko jela utakuwa na moyo
wa jiwe wa kusamehe…sijui, labda sisi tuliumbwa na mioyo ya kishetani…’hapo
akatulia na hakimu alikuwa katulia tu.
‘Ndugu hakimu,…sijui kama nimeweza kuwajibu ni kwanini hata
mimi niliingia huko, sitaki kuelezea mengi kuhusu machungu niliyopitia,
yanaumiza, na nikianza kuyaelezea hapa, nahisi nitegeuka kuwa mnyama,…na kila
mara nikiwazia huko nageuka kuwa mnyama…ila wewe chukulia mfano mmoja tu,
ulizaliwa ukiwa kamili, mwanaume kamili, unafikia mahali watu wanakufanyia
mambo, mpaka unakuwa sio mwanaume kamili…unadhalilishwa, unaumizwa, nyie acheni…sitaki
niongee huko zaidi..
‘Ila nawaambieni hapa wazi wazi, walionifanyia hivyo, wote
waliyapata yale yale waliyonifanyia, mimi, ..na kama wangeliweza kuja kuongea
hapa, mungewaonea huruma, lakini inafikia mahali unajiuliza, ni nani
aliyesabisha haya yote, huyo nay eye, na kizazi chake inabidi wawajibike…ooh,
aaah…nahisi hapa..ndi-ndi… ndio nafikia mwisho..nahisi muda umefika,…’akashika
kifuani.
‘Kwahiyo wewe ulijiunga na kundi hilo kwa vile
ulizalilishwa, ..na sasa ni kwanini uilenge hiyo familia, ni kwanini, kwani wao
ndio walikufanyia hivyo…?’ akaulizwa, na jamaa akasema;
‘Una-una-jua ni kwanini nilicheka awali…hahahaha, nilicheka
kwa vile hata ndugu yangu mwenyewe hakuweza kunitambua mimi ninani, …, kwa jinsi
nilivyoweza kujibadili, mi-mi..eeh,..sina kawaida hiyo nikikutana naye…ananijua,
lakini ….mlinikamata nikiwa nimejibadili, sikuweza kupata nafasi ya
kutokelezea, alivyonizoea….’akashika kifuani, akaanza kuonyesha dalili zile
zile za mshitakiwa namba mbili.
‘Kwahiyo wewe ni nani…?’ akaulizwa.
‘Mi-mi.. ndi-ndi-ye pacha wa mshitakiwa namba ..mbili, huyo
ni pacha mwenza, na, na…ndio maana, ohhhhh…’akatoa maneno hayo na kuporomoka,
akadondoka chini.
NB: Mpaka hapo kisa
kimekwisha, yaliyobakia ni nini kilitokea baadae….tutaileta sehemu hiyo kama
sehemu ya kumalizia, kama mtapenda.
WAZO LA LEO: Sio kile mkosaji ni
mtenda makosa, wakati mwingine mtu hutenda kosa, kutokana na madhila
aliyoyapata, ndio maana wenzetu wazungu, mtu akitenda kosa lisilokuwa na
kawaida kwanza wanampima akili yake…Kwahiyo kwenye jamii, hasa kwa watoto wetu,
tusikimbilie kuadhibu tu, kushutumu tu, kutukana tu, tujaribu kuchunguza, na
kuwa washauri nasaha, huenda kosa hilo lina sababu yake muhimu. Tumuombe mungu
atujalie tuwe wenye tabia njema, kwani tabia njema, ndio huleta upendo, amani
na furaha kwenye maisha yetu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment