Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, June 16, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-52



‘Sasa nikuulize wewe unyejifanya kuwa sio ndugu yangu, unamfahamu huyo aliyembebesha mama yangu huo uja uzito, akamfanya akapatwa na hilo tatizo..?' akauliza akimgeukia huyo mama aliyesimama hatua chache mbele yake.

Huyu mama hakujibu, akabakia kimia..

 ‘Unashindwa kujibu eeh,…najua hutaweza kujibu, japokuwa uliwahi kusikia habari hiyo, kutoka kwa bibi yako ambaye alitaka kukukabidhi mikoba ya uganga,..bibi yako alikuwa mganga wa kienyeji, mkunga,..au sio…na ukweli ulivyo, hata wewe huwezi kuwa tofauti na wengine, hata wao walivyoulizwa waliogopa kujibu,…usijali, sio kosa lako,.. mimi nitajibu kwa niaba yako….’akasema na kutulia kidogo, halafu akasema;

Tuendelee na kisa chetu


*************


‘Huyo jamaa, huyo kidume, aliyembaka mama yangu, akamuumiza, kidonda kikatengeneza donda ndugu, alikuwa ni baba yako….’akasema kwa sauti.


‘Hapanaaah, wewe muwongo mkubwa..., walimzushia tu, sio kweli…’akasema huyo mwanamke.


‘Ni uwongo, ndivyo walivyosema kuwa alizusha, ndivyo ulivyoambiwa, je hata bibi yako alisema huo ni uwongo,,,,?' akauliza na huyo mama akabakia kimia.


'Sema ukweli, au ili uhakikishe hilo,... unataka ushahidi….nikutafutie ushahidi, nipeni ruhusa hiyo niwaletee ushahidi huo..., na ushahidi ni wa nini,... mimi nipo hapa, nipimeni ..siku hizi si kuna kipimo cha DNA, nipeni kama mimi sio damu ya huyo mzee,...na siku mkimapata huyo pacha wangu, na yeye mumpime kama sio damu ya huyo mzee..hayo sisi tulishayafanya, tukagundua kuwa ni kweli..


'Haya hilo labda ni zito, ..., waulizeni wazee waliokuwepo hapo, kama ni wachamungu wa kweli watausema ukweli….’akasema na mama yule alibakia kimia, na baadae jamaa akasema.


‘Huwezi kulikana hilo, na pia huwezi kulikubali hilo....'akatulia kama anampa nafasi huyo mama asema neno.

'Nyie mlijiona ni kizazi cha kifalme, watenda haki…lakini mali, …utajiri, cheo, hivyo vitu vina mitihani yake,…usoni kwa jamii, mtajifanya ni watu wema, lakini ukigeuka ukawapa watu mgongo, unawakebehi…sio kwa kunyali tu, hata kwa vitendo, gizani mnatenda madhambi makubwa tu, dhuluma....manadhulumu watu...'akatulia.

'Nikuulize wewe..., unafahamu baba yako alikuwa na watoto wangapi wa nje ya ndoa…wangapi, …huko mbele ya kadamnasi, anajinadi, kuwa ana mke mmoja, yeye ni muadilifu, ni kweli hayo,…hahaha, nyie watu nyie…je hayo sio kweli…?’ akauliza na yule mwanamama alibakia kimia.


‘Ndio alikuwa na nyumba ndogo nyingi, na hizo nyumba ndogo, washukuru,maana wao walitendewa haki, wakapewa walichopewa, je sisi tulipewa nini,…tulibakia kuwa watoto wa mitaani, chokoraa, tunazalilika, tunadhalilishwa, na ole wetu tungelionekana, ..mimi niliponea chupu chupu kuuwawa gerezani, maana ningelijulikana,..sijui…nitadhalilisha nyumba ya kifalme..namshukuru mungu….’akatikisa kichwa.


Sasa mumeelewa ukweli, na asiyeelewa, hataelewa tena,…mimi na pacha wangu tukazaliwa mayatima, tukakulia maisha ya uchokoraa,….baba yake huyu aliambiwa kutuhusu sisi akatukana, akasema hatutambui kabisa, unajua ni kwanini, kwasababu aliogopa fedhaha kuwa alizaa na kilema, mwanamke aliyembaka.


‘Wewe mwanamke hulijui hili, hukuwahi kusimuliwa hili…?’ akauliza tena na huyo mwanamke alibakia kimia.


‘Sitaki unijibu, maana sisi ni kizazi cha shetani, watoto tuliozaliwa kwa njia haramu, au sio,  ndivyo tulivyojulikana, hakuna aliyetafiti akajua huo uharamu ulitokana na nani, na dunia ndivyo ilivyo,….hakuna anyejaribu kuuliza ni kwanini tulifikia kufanya hivyo, watu wanafikiria kusudio letu ilikuwa vifaa hivyo vitatu,…


‘Sawa tulipogundua kuwa hivyo vitu vitatu, vina manufaa, tuliona ni kwanini tusivipate vije kutusaidia mbele kwa mbele..angalau na sisi tuje kurithi, makombo ya nyumba za kifalme…angalau….’


‘Lakini dhumuni letu kubwa..ilikuwa sio hivyo, sio kwamba sisi tulifanya hivyo,kama itikadi ya wachawi, japokuwa tulijifunza uchawi, nia yetu ililenga hiyo familia,...na tulipojua kuwa hivyo vifaa vinaweza kutusaidia huko mbele, basi tukatafiti zaidi …je tutafnyeje ili viweze kufanya kazi yake..’akatulia.


‘Oooh, mambo yakajileta, kumbe, ili vifanye kazi yake, vinahitajia mkono wa kizazi cha kifalme,..warithi halali, waliozaliwa ndani ya ndoa,..sio akina sisi,..tukajiuliza akina sisi tunawezaje kufifanya vifanye kazi..tukaambiwa, ni lazima kwanza vipitie kwenye hiyo mikono ya kifalme..hapo unafikiri tungelifanyaje…


‘Jiwe moja linaweza kuua ndege wengi tu…hapo ikawa tumepata namna ya kulifanikisha lengo letu,…tukamtumia huyo huyo ndugu yao wanayemtambua,…sura yake,..na utaalamu wake, maana na yeye alikuwa na kiutalaamu kidogo cha mambo hayo…lakini tukaona hana faida sana…tukamuwekeza kwenye mambo yetu, tukamfanya zezeta…..ili tuweze kutumia picha yake..’akasema.

‘Sehemu hii ya pili ndio nyie watu mumeishikilia sana, kuwa sisi ni wachawi, sisi tunahitajia hivyo vitu kwa nia ya kutawala dunia…propogada potofu, na sisi tukaona hiyo hiyo ndio itatusaidia kufanikisha lengo letu…maana hata tukiongelea yaliyompata mama, ni nani atakuamini tena..wakati yaliandikwa kuwa bibi alikuwa machwi, alitaka kumloga muheshimiwa, akafungwa…mama alikufa kwa kihoro cha kuumwa sijui…zambi za bibi yake zilimuandama..waliandika mengi..mungu anajua ….


 Mimi baada ya kutoka jela ya watoto, nikaanza kusoma, maana huko nilikutana na vichwa, vikanifunua akili kuwa elimu ndio silaha ya mambo mengi,..na ukiwa na elimu unaweza ukafanya mambo yango yakaenda kimpangilio…kiukweli nashukuru sana kwa hilo…


Kwahiyo,..nilipotoka jela,..nikaanza kusoma, na kusome kweli, sio kwa kubahatisha,, kumbe akili ya darasani nilikuwa nayo, kumbe ni kwasababu ya umasikini wetu, huna wazazi wa kutuongoza…huo ndio ukweli, wapo watoto mitaani, wana akili sana, wapo watoto vijijini wana akili sana, lakini watasoma wapi…nyie mnawaona watoto wa matajiri tu, wanaosoma shule za bei, mbaya, wanaonekana wana akili sana…


Sawa wana akili, lakini kwanini hamuangalii mazingira mtu anayotokea,..maisha, hali za kiuchumi,..nk…hamuwezi kufikiria, ni kwanini wao wakaonekana hivyo zaidi ya akina kayumba…nyie mnawapambaisha akina kayumba na hao…eti ni nani zaidi, mnachekesha kwakweli…


Huyu anakula vyema, analala vyema, ana vitendea kazi, huyo mwingine, hajui atakula nini, anaamuka asubuhi haijui chai….anatembea umbali mrefu, na bado eti unataka ashindane na huyo..., basi mngejaribu kutofautisha maksi zao, wa shule nzuri maksi zao ziwe juu, kuliko hawa ambao, ..ok, huko tupaache, maana dunia hii haina wema, haina usawa…


Niliposoma na kuligundua hili, kuwa dunia hii, watawala, matajiri, …sio kwamba nawachukia wtu hao…, nazichukia tabia zao, ..maana mali zao, wengi wao, sio za halali..ulizia chunguza, utaligundua hilo....mimi nilifanya uchunguzi huo kwenye mitandao, kwenye uchunguzi wangu, wakichawi, nikagundua mengi kuhusu matajiri..matajiri wengi ni washirikina, sio lazima aende kwa kigagula, wana namna zao, hivi ukimdhulumu mtu, wewe ni nani, wewe ni mchawi tu…hao matajiri hawawadhulumu wafanyakazi wao…wanakula dhuluma…sawa hayo tuyaache pia, tuje kwenye ajenda yetu.


Katika kuhangaika huko kusoma, maana wakati nasoma ndio nilikuja kumgundua huyo pacha wangu, nasoma huku nafanya uchunguzi, mimi ni nani, wazazi wangu ni nani… ndio nikakutana na huyo mama mkunga, aliyemzalisha mama yangu, na alishukuru sana kuonana na mimi…, maana alipewa kazi ya kuhakikisha ujumbe huo umefika kwangu.., alikuwa akiota kila siku akiulizwa je kawakilisha hupo ujumbe kwa watoto …


‘Nyie mlizaliwa mapacha…’akaniambia


‘Eeeh, hivyo, … sasa mwenzangu yupo wapi..?’ nikamuuliza


‘Mimi sijui..nimewatafuta sana, lakini kwa vile nimekupata wewe, basi, ujumbe utafika, na siku ukimpata mwenzako utamsimulia, maana ya mungu mengi, nipo hai leo, sijui ya kesho…’akasema

Basi huyo nesi wa wakati huo, akanisimulia, mimi ni nani, wazazi wangu walikuwa ni ni nani, ..na aliposimulia kumuhusu mama,….kiukweli nililia sana..hebu fikiria unasimuliwa kitu kama hicho kwa mara ya kwanza, utakuwaje…nililia..nililia…we acha tu…mama hajawahi kuninyonyesha, mama hajawahi kunipakata, mama, hajawahi..lakini familia ya kifalme, inapita na magari….inaneemeka,…na eneo letu wamelichukua…niilihisi hasira,..hapo hapo roho yangu ikabadilika.


‘Unajua nilipotoka jela..nilianza kuwa mcha mungu, mpole…nikaona elimu ndio kila kitu, niwe mtu mwema,…sawa hayo niliyapokea, lakini hili lilipofika kwenye kichwa changu, nikaona kumbe….nilianza kubadilika, roho yangu ikajenga chuki….sijui niwalezeje nilivyojisikia!


‘Sawa labda mimi ni shetani, labda mimi…sio sawa na wangine, ndio maana nililichukulia hilo juu kwa juu, kwa hasira na chuki za kwa vile sisi ni kizazi cha umasikini, mtoto wa mitaani, yatima, asiye  na baba wala mama….labda..kwa vile sisi ni kizazi haramu, labda…


‘Sikuishia hapo, nikawa nauliza watu mbali mbali, lakini nikiwa nimeficha sura yangu, sikutaka nijulikane mimi ni nani, na siku baada ya siku ndio nikakutana na pacha mwenza, kumbe siku ile nilipotoka hapo kwa huyo mama mkunga, na yeye alikuja siku ya pili yake kwenye hiyo nyumba, akakutana na huyo mama mkunga, ….


Kumbe yeye alishapitia sehemu nyingine, akiutafuta ukweli,  na huko ndio wakamuelekeza  kwa huyo mama mkunga,…yeye alishafika mpaka kwa hao madocta kabla yangu,….maana mimi niliwahi kwa huyo mama mkunga, baada ya kuelekezwa na mzee mmoja ambaye aliwahi kumfahamu huyo mama yangu,…na nilipotoka hapo ndio nikaelekea kwa hao madocta,..nia ni kuupata huo ukweli.


‘Sasa ndugu yangu tufanyeje..?’ nilimuuliza ndugu yangu tulipokutana, sikuwa na nia y akujua yeye aliishije…’akatulia.


‘Unauliza jibu…’alinijibu hivyo, nakumbuka sana kauli yake hiyo,.. akilini nikawa nachemka kwa hasira.


‘Lakini ndugu yangu tuyafanye haya mambo, kama wasomi, kwanza tumaolize shule, tupate kazi, na wakati huo huo, tunatafuta njia sahihi,…tuje tufanye jambo ambalo dunia itakuja kutukumbuka…’nikasema na ndugu yangu akasema.


‘Sawa kabisa, mimi nilikuwa na wazo hilo hilo, cha kwanza ni elimu, cha pili ni kutafiti namna gani bora ya kulifanya hili jambo, liwe na manufaa kwetu, lakini hapo hapo tuweze kulipiza kisasi, na kuhakikisha mali zetu zimerejea mikononi mwetu.na kuhakikisha kuwa..dunia iinakuja kututambua sisi ni nani….’akasema na tukashikana mikono.


‘Kila mmoja alikuwa kivyake kwenye kutafuta elimu,maisha, kazi nk....mpaka tukahitimu, mimi nikajiunga na jeshi la polisi, kama dhamira yangu ilivyonituma, nilijua huko nitajua mambo mengi tu, nitaweza kutumia silaha, nitaweza kujilinda, ..na mwenzangu,naye akajiendeleza kivyake, hatukuwa tunakutana, mara kwa mara, mtandao ndio ulikuwa ukutukutanisha, hatukutaka kabisa watu waje kutufahamu,, mtu asiniulize huyo pacha wangu ni nani…eeh siwezi kuwaambia, sio kazi yangu..’akatulia.


‘Katika pilika pilika za kutafuta namna bora ndio nikakutana na ndugu wa huyu mwanamke, huyo anamfahamu maana mama yake alikuwa mtu wa watu…wenye nazo, sio…siwalaumu, ni kweli, kila ndege hutua kwenye mti aupendao, au sio…mimi, nikajenga urafiki na huyu mtu, ilitokea tu, tukawa tumeelewana, na yeye alikuwa na chuki zake,..unajua tena, hata mkiishi vipi, bado kuna mambo mtakuwa mnapishana..huyu, aliona kuwa kwenye familia zao, wao walitengwa kidogo…


Akaja kunisimulia,kuwa …kwenye kizazi chao, kuna babu yao, alikimbilia nje, na vifaa vitatu…bastola ya ajabu, iliyotengezwa na mikono ya shetani…upande mmoja, na upande mwingine, mnajua wenyewe, na kuna viatu vya ajabu, vina historia yake kubwa iliyofanya hadi viatu hivyo vifike kwa huyo mfalme wa enzi hizo…lakini kizazi cha huyo mwanamke…


Kubwa lao, ambalo tuliliona sisi ni jema kweti ni ufunguo-malaya, ufunguo wenye maajabu ya aina yake, ufunguo huo ulitengezwa enzi hizo, lakini kinamna ambayo unayoweza kuuingiza kwenye komputa, au mlango unatumia..digital,..ukafungua…yaani..hapo nikasema, hiki ndio kinafaa, hivyo vingine tutakuja kuvipata, lakini kwanza tukitumie hiki…


Hapo, nikaanza kusomea komputa kiundani, na mwenzangu pia, alifanya hivyo kivyake vyake..…tukaja kukutana na mzungu mmoja, ambaye ni mwanamazingaumbwe…anajulikana sana, akatufundisha mambo mengi ya ajabu, pesa inaongea, …akatuelekeza kwa docta mmoja bingwa, anayeweza kubadili sura kwa kutumia komputa…muone ilivyokuwa ajabu, moja linazaa jingine kwa manufaa ya mpango wetu.

Kuna mengi hapo yalifanyika, lakini haina haja kuyasimulia, ila ili kazi ifanyike ni lazima kuwe na mkuu, tukawatafuta watu mbali mbali waliofaa kuwa nasi, wakashirikiana nasi, walioweza wakaendelea mbele, ambao walikuja kutusaliti, tukawamaliza,..maana ukimuacha keshajua siri ya mambo yetu, …ni lazima amalizwe.


Wengi walimalizwa, na mkaja kutukamata mimi na huyu ….ambaye, mtakuja kumfahamu wenyewe,kwani ndiye alikuwa ..tulichagua kuwa bosi wa shughuli hizo, kwani aliweza kucheza vyema kwenye kazi yake.


Mimi na ndugu yangu, yeye, hakuhusika sana, ndani ya kundi, tuliona awe hivyo,…sisi wengine ndio tulicheza sana na mambo hayo,…maana tulishahitimu, tuliweza kujigeuza tupendavyo, kwa kutumia komputa, tuna ujuzi wa nguvu za giza, tukasema sasa tuanze kazi…mtu wa kwanza kuwa majaribio yetu…., alikuwa kaka wa huyu mdada….tukamwekeza mambo, akawa mtumwa wetu..


Tukaona kama kuna mtandao, kama kuna namna mtandao unaweza kuwasiliana dunia nzima,kwanini tusigundue jambo, kwa kutumia nguvu za giza…maana sisi ni wachawi, lakini wa kisasa,..wachawi wenye kutaka maendeleo..lengo ni maendeleo, ajenda ni kulipiza kisasi…


Tukaoana kwanza tujijenge, tuwekeze …tutafanyaje, wakati hatuna mtaji…haaa, eti hatuna mataji, ufunguo wa ajabu unafanya nini…ufunguo huo ulitufanya tuwe matajiri, tuliutumiaje, siwezi kuwaambia,……hiyo ni siri yetu..ila una nguvu za giza, upande mmoja, ..yaani nguvu za shetani, na upande wa pili, una mambo ya halali…ambayo, mnayataka nyie…manaojifanya malaika,…au sio……ok..tuyaache kama yalivyo!


Awali hatukuwa na hamasa sana na hivyo vitu vingine viwili, maana maisha yalituendea vyema tu…lakini mara tukaja kukutana na huyo mzee kikagula….huyo ndiye alitutia hamasa, ya vitu hivyo vingine, umuhimu wake kwenye dunia ya gizani, na nguvu za kiutawala,..mzee huyu alikuwa mkali sana wa mambo ya giza,…tulimlipa pesa nyingi sana, akaja kutufundisha mambo ya msukule..uchawi wetu wa kiaafrika, hauna maana ni kutesa wengine, sisi tuliutaka uwe na maana…


‘Tuliutaka uwe wa maana..katika mpango wetu wa kulipiza kisasi…tulifanya mambo mengi hapo, ili kufanya majaribio mbali mbali…tuliweza kuingia kwenye majumba ya watu watu wamelala, hawajui sisi tupo humo ndani..ni mambo ya ajabu, acheni tu…tulifanya hayo katika utafiti, sisi lengo letu sio kuwaumiza watu wengine, ..walioingia kwenye mtego wetu kwa bahati mbaya, watusamehe tu…


Tulipojiunga na huyo mzee, tukajikuta tunafanya mambo mengine ambayo sio lengo letu,…ilibidi tufanye hivyo..ili kukamilisha baadhi ya mambo, ilibidi tufanye makafara, kama alivyotufundisha huyo mzee kikagula,. Ili tuweze kuja kufanikisha lengo letu.na kuvipata hivyo vifaa vingine..ambavyo vilitakiwa virejee kwa maadui zetu.


‘Huyu mzee, hatukumuambia moja kwa moja sisi ni nani, kama aligundua, basi aligundua kivyake,..ila tulimuulizia historia ya vifaa hivyo vitatu, historia ya huyo mama aliyekufa peke yake kwenye nyumba, alitusimulia kama alivyosimuliwa …maana na yeye ni wa siku nyingi eneo hilo, na mwisho wake akatufichulia siri la hilo pango…



Hapo, sasa tukaona tumeweza…maana hilo pango..msilione hivyo, ndani kwa ndani kuna maajabu mengi sana, kuna mashetani…humo ndani, yanahitajia damu za watu…kuna mizuka, …sisi tukishirikiana na huyo mzee, tuliweza kuyamiliki hayo..mashetani, wakawa ni watumwa wetu…


Tukawekeza humo ndani, tukatumia pesa nyingi kupajenga vyema humo ndani, huwezi amini, humo ndani kuna vyumba vingi tumejenga,…lakini tuwatahadharishe, humo ndani ukiingia uwe umejiweza..vinginevyo hutatoka,…waliojaribu kuingia humo wamepotea moja kwa moja…sio sisi tuliowapoteza, ni mazingara ya humo ndani…, ila mzee anajua ni kwanini..tunajua ni kwanini lakini siwezi kuwaambia..


Mimi kwenye maisha yangu ya kazi, …nikaja kuwa bosi, nilifanya tu, ili dunia isije kuniona mtu wa ajabu, anayeishi maisha mazuri bila kazi, nilifanya kwasababu ilikuwa ni sehemu niliyoweza kupata taarifa ya mambo mengi, na kama tulifanya mambo yetu, niliweza kuyazimisha kiaina….na yule aliyekuja akajaribu kuchokonoa anga zetu, nikajua jinsi gani ya kumdhibiti…


Na najua muna hamu sana y akumfahamu pacha wangu,..yeye kama kawaida yake alikuwa na kazi yake, yeye, kama nilivyosema hakuwa moja kwenye moja shughuli zetu, yeye tulihakikisha anakuwa nje kabisa na mambo yetu,..siwezi kuwaelezea zaidi kumuhusu yeye, …siku mkimkamata atakuja kuwasimulia mwenyewe.


Mfano wa watu kama hao , ambao walijaribu kuingilia anga zetu ni huyo mpelelezi, hakuwa na maana kwetu sana…alijiingiza kwenye anga zetu, na hatukuwa na jinsi, kwanza tulimuonya kwa namna mbali...kupitia kwa familia yake, hakutuelewa, pili tukaona labda tumuwekeze kinamna, afaidi matunda ya kazi yetu, lakini akawa mkaidi...alikiona cha mtema kuni...


Mimi nilikuja kuwa mkuu wa kituo hapo, na nikiwa humo niliweza kugundua mengi yaliyokuwa yamejificha, na humo nikawa nauhakika wa hicho kilichotokea kwa mama yangu, sikuwa na shaka tena, nikaongea na pacha, na yeye akasema hana shaka na hilo, kwani keshachunguza vya kutosha, kwahiyo kazi ikabakia ni moja, kwanza kuhakikisha tumevipata hivyo vifaa, na huku tunaigaragaza familia husika.

Na-na-natumai hadi hapo mumeupata ukweli, nahis muda wangu umefika, sizani kama nina umri tena...'akasema hivyo, alikuwa kama anaona vitu visivyoonekana.


'A-a-ama kwa jinsi gani tulimtengeza mpenzi wa facebook, kwanza mjue kuwa huyo ni miongoni mwa mipango yetu ya kulipiza kisasi….huyo tulimuwekeza kwenye mtandao, akawa anawatokea watu..huo ni mmoja wa miujiza tulioweza ku-u-ufanya..ukafanikiwa, na tukaweza kumnasa mtu muhimu sana..mwenye damu inayokubalika kwenye kufanikisha mambo...

'Hi-hi...'akawa kama anahisi kitu akashika kifuani, upande wa kushoto, na muendesha mashitaka akauliza;


‘Kabla hujaendelea huko, huyo pacha wako ni nani…?’ akaulizwa.


‘Huyo pacha wangu…'akasema huku anaangalia mbele, kama anaona kitu.

'O..pacha wngu, mmmh, mimi sijui yupo wapi,..na hata kama ningelijua, nisingeliweza kuwaambia,…hicho ni kiapo chetu, siwezi kukuvunja, najua mtataka kunilazimisha au kumlazimisha huyo mwen--nzangu. mliyemkamata..la-lakini,..yeye au mimi hakuna anayeweza kusema huyu yupo wapi, msijisumbue.


'Huyu si ndio pacha wako...?' akaulizwa na huyu mshitakiwa akageuka kumuangalia, akacheka, kicheko chenye maumivu, akasema;


'Mimi ..sijui...hiyo sura kwanza ni ngeni kwangu...pili, yeye, sio rahisi kupatikana, hamuwezi kumkamata kirahisi hivyo....'akasema


'Tafadhali,,… huko msinilazimishe, mimi au huyu... kabisa, siwezi kuwaambia,..hiyo ni kazi yenu kumtafuta, …mtafuteni huko, alipo, hata mimi sijui kwa hivi sasa yupo wapi..., hata hivyo, nahisi afya yangu sio nzuri, niliyowaambia ndio niliyojaliwa kuwaambia, siku mkimpata huyo mwenzangu, ataweza kuwasimulia, yaliyobakia,....’akasema.


‘Haya endelea kuhusu mtandao, mlitengeneza mabinti, na mkamtengeneza mpenzi wa facebook, je huyu ni nani, yupo kweli au ni shetani,….kama watu wanavyodai…?’ akaulizwa.


‘Hahahaa, hivi hamuamini, mimi sina uhai tena...muda wa hukumu yangu umeshafika...na mengine mtakuja kuyasikia, sio kwangu tena...ila niwaambie kitu,…….aah, niwaambie kitu….’ghafla akatulia, alikuwa kama kaona kitu mbele yake, macho yakamtoka,…mara akashika kifuani upande wa kushoto, akawa anainama….kiukweli alionekana anahisi maumivu, awali tulihisi kuwa labda ni mbinu zake, labda…anaigiza lakini tulipoona jasho linamtoka, macho yamemtoka, ..tukajua ana tatizo,…docta akamsogelea, akampima, na kusema;


‘Jamaa yupo kwenye hali mbali, presha ipo juu sana….’akasema na haraka madakitari wengine wakafika, na kuanza kumpa huduma ya kwanza, lakini haikusaidia, jamaa akawa kwenye hali mbaya, akapoteza fahamu…


Muheshimiwa hakimu, akasema;


Huyo apelekwa hospitalini,…chini ya ulinzi mkali …sasa japokuwa muda umekwenda sana, tunaye mshitakiwa namba moja,….’akasema hakimu.


‘Muendesha mashitaka unataka kusema nini kuhusu huyo mashitakiwa…?’ akauliza hakimu.

‘Kama alivyokuwa mshitakiwa namba mbili, naye alijibadili sura…kwahiyo na yeye tunaomba tuweze kumuondoa sura ya bandia, ili ajitokeze kwa sura yake ya asili..mpaka sasa hatujajua yeye ni nani….’akasema muendesha mashitaka

‘Na yeye alikuwa mshirika wa huyo mshitakiwa namba mbili…?’ akauliza


‘Ndio muhesimiwa hakimu, lakini kila mmoja alikamatwa kivyake…’akasema muendesha mashitaka.


‘Basi muondoeni hiyo sura yake ya bandia tumgundue na yeye ni nani, halafu tuaangalia kama tuna muda wa kumsikiliza na yeye …’akasema hakimu, na kila mtu akawa na hamasa ya kutaka kumjua huyo mtu ni nani..


Docta akafanya vitu vyake, na mara usoni kukafutuka, kama ilivyokuwa kwa mshitakiwa namba mbili, na docta akafika pale mbele kumalizia hiyo kazi ya kuondoa hiyo ngozi ya sura ya bandia…docta alipoiondoa, kabla hajamaliza, akabakia ameduwaa,….ilichukua dakika moja kaduwaa..


‘Vipi docta umeona nini..mzuka…?’ akaulizwa, watu sasa wakiwa na mashaka, wakikumbuka alivyofanya mshitakiwa namba mbili na ghafala akazidiwa.


 Na docta hakujibu, akaivuta ile ngozi bandia kutoka kwa huyo mshitakiwa namba moja, na sasa akawa kasimam mtu mwenye sura yake kamili, na alipoonekana ...


Oooh,….hapo, kila mtu alibakia mdomo wazi….na hata hakimu alijikuta akisimama, hakuamini macho yake macho yakamtoka pima, na kubakia mdomo wazi…

NB: Kumbe mambo bado…

Labda huyu ataelezea ukweli kuhusu mpenzi wa facebook….ngoja tuone itakuwaje!

WAZO LA LEO: Kila mtu ana mipango yake mingi…nitafanya hiki, na kile, …ndio maisha yetu yalivyo, na ni vyema tukawa na utaratibu huo, wa kuwa na mipango mizuri ya kimaisha,…lakini je ni wangapi wanaweka mipango ya maisha baada ya hapa duniani..maisha ambayo ndio marefu zaidi, hatujui yatachukua muda gani


Maisha ya hapa duniani, ni ya muda mfupi tu, kila mtu na umri wake, lakini hayo ya kudumu, ni nani analiwazia hilo, .! Tumuombe mola wetu atupe maisha mema hapa duniani, na kesho akhera..Tumuombe mola utujalie katika mpango yetu, tuweze kuwa na mipango mizuri ya kutusaidia hapa duniani na kesho akhera.

Ni mimi: emu-three

No comments :