Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, June 8, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-45


Docta alikuwa anamfuatilia mpelelezi na alipoona kafika kwenye huo mlango, akatumia mbinu za kumsaidia, kwa kumfanya mtu wao..yaani,  askari wa mkuu-msaidizi..ajifanye kama anatoka nje, na alijua mpelelezi atachuku nafasi hiyo na kuingia ndani…

‘Ngoja nione lengo la huyu jamaa, mpelelezi, nahisi kuna kitu anakifuatilia, ngoja tumuone kitaalamu,…’akasema docta akiendelea kumfuatilia mpelelezi.

Mpelelezi, alipoingia ndani, cha kwanza alichotaka kukifanya, ni kwenda kwenye kile chumba alichowahi kumuona yule mdada, alipofika alishangaa kukikuta kipo wazi, kwa tahadharai akaingia ndani na kuanza kukagua, kwanza kwa macho, pili kwa vitendo, kwa kuchunguza sehemu zote kama anaweza kupata lolote la muhimu,  na alipohakikisha kuwa hakuna kitu kinachoweza kumsaidia, akageuka kutaka kuondoka, na mara akasikia watu wakiongea..

Sauti hizo ziliashiria kuwa huenda watu hao wanataka kuja kwenye chumba hicho, na yeye kwa haraka,akatafuta sehemu, akajificha, na kusubiria…

Haikuchukua muda, mara hao watu wakaingia, kwanza walisimama mlangoni wakishangaa, halafu wakaingia ndani…walikuwa watu wawili;

‘Yupo wapi huyo mdada mwenyewe….’akauliza mtu wa kwanza, japokuwa walikuwa wamevalia vito usoni vya kuficha sura yao, lakini mpelelezi akawagundua, ni akina nani,…akasubiria kuona lengo lao ni nini;

‘Alikuwa humu, huoni jinsi palivyowekwa vyema, maana huyo ni malikia, huyo ndiye , bila yeye bado hivyo vitu visingeliweza kufanyakazi kama itakiwavyo..’akasema mzee

‘Sasa yupo wapi, mzee, ….mimi naona una lako jambo, ….’akasema huyo anayeonekana ni kijana, na huyo mzee akasema;

‘Subiri kwanza,…..’mzee akasema na kupiga simu, nahisi alikuwa akiulizia

‘Vipi, mtaalamu msaidizi, mbona vyumba vipo wazi, na hapa alipokuwa mdada, hakuna mtu, mimi nilitakiwa kuja kumaliza kazi, sasa nitafanyaje kazi….eeh, unasema haiwezekani, sasa itakuwaje…’akauliza na akawa anasikiliza

‘Hilo halina shida…niamini, lakini hata vikipatikana, vitakuwa havina maana,…kwahiyo, unasema, anakuja, ….ohooo, ngoja kwanza, mimi nijuavyo, anapokuja kukutana na mtu fulani, mtu huyo, hataweza kumuona tena, ndio zake, sasa kama anakuja huku, anakuja kuonana na nani..na mimi…haaa, kama hanijui, atajiua sasa…tutaona,…maana bila mimi hakuna kitakachowezekana….’akasema

Baadae mzee, akakata simu, na kuanza kuongea , hapo akasahau kuwa ana mtu ambaye hakutaka afahamu undani wake;

‘Huyu mtu najua,..kwa tamaa zake, anataka kunitumia, animalize, lakin sitakubali, atajua kuwa kaingi anga za nani..haiwezekani, nimejitolea na kuhatarisha maishayangu kwa ajili yao…huku wangekujuaje….sasa…kwanini lakini…’akashika kichwa.

‘Mzee kwani imekuwaje…’kijana akasema akimshangaa mzee, kwani alimuona uso ukimbadilika ghafla, akawa  mweusi kupitiliza, na ikawa kama jasho linamtoka.

‘Sikiliza, huyo jamaa anakuja yeye mwenyewe, sio kawaida yake, na huyo jamaa akija, ….kazi yake ni kuua, yaani, mfano akija kwako, kwa vile hataki afahamike, akishamaliza hicho alichokujia, wewe anakumaliza…ndio maana hadi leo hakuna anayemfahamu, hata mmoja kati yetu…’akasema

‘Hata huyo kiongozi aliyekamatwa, hamfahamu…?’ akauliza.

‘Huyo yawezekana …anamfahamu lakini hata yeye anadai hamfahamu..’akasema

‘Na uchawi wako umeshindwa kumfahamu yeye ni nani….?’ Akauliza
‘Utaalamu wangu hauwezi kutambua hayo…huyo kakamilika,….anajigeuza kma kinyonga sio mtu wa kawaida, ulaya anakwenda kama nyumbani kwake,….kiongozi anasafiri sana, lakini huyo …kazidi…’akasema

‘Anasafiri kwa hivi hivi au kwa uchawi wake…?’

‘Kwahivi hivi, leo anaweza kusafiri kwa sura hii kesho nyingine, sio mtu wa kawaida, mimi simuwezi, ndio maana namuogopa, vinginevyo, ..ningelishamaliza hii kazi peke yangu…’akasema.

‘Kwahiyo anakuja kuvichukua hivyo vitu, ..unitume mimi nivichukue halafu kwa ujinga wako umkabidhi huyo mtu, mbona sikuelewi mzee, kama hivyo vitu vina faida, na unajua kazi yake ni nini, kwanini umpatie huyo mtu, maana picha ninavyoiona hapa ni kuwa, mimi utanituma, sijui kwa vipi, nitakwenda kuvileta hivyo vitu, ...mtaniua, hlafu ukishamkabidhi huyo mtu hivyo vitu, atakuua,na wewe,.’akasema huyo kijana

‘Sikiliza, sasa…nimeshajua la kufanya, wewe ..tufanye hivi, kabla hajafika, eeh, tuhakikishe tumeshavipata hivyo vitu, tukishavipata akija tu, tunam-maliza, unaonaje wazo langu…lakini haiwezekani, sio rahisi kwa huyo mtu, hapa tunaongea anatusikiliza huko alipo…keshajiandaa…’akasema huyo mzee akiangalia huku na kule.

‘Unajua mzee, hilo wazo lako sio baya…, ila sasa, mimi siwezi kukubali kufanya huo uchawi wako, kabla sijamuona huyo binti,..hilo ndilo lilikuwa sharti letu muhimu,…kwanza nimuone huyo mdada, mengine hayo yatafuta baadae…si ndivyo tlivyokubaliana,awali…’akasema kijana.

‘Sikiliza, ..niamini mimi, huyo mdada hajafa…’akasema

‘Sasa yupo wapi..?’ akauliza

‘Katoka,..najua hii ni kazi ya docta, kawashinda hao watu wa mitandao, akafungua milango yote, na watu wote waliokuwa humu ndani wametoka,..walinzi na watu muhimu wote wamekamatwa, ..ndio maana huyu ‘mkuu, ‘ kaamua kuja mwenyewe kumalizia kazi, na atakachofanya …ohoo, sijui,….’akatulia

‘Atafanya nini bwana,…mzee tusipoteze muda, huyo mdada tutampataje maana sijakuelewa hadi hapo, kutoka kwetu huko ilikuwa ajenda ni hii, sasa umenihadaa, na mimi siwezi kuendelea kukaa hapa ni lazima niondoke,…kabla huyo jamaa yako hajafika, …’akasema

‘Huwezi kuondoka,…usijisumbue kwa hilo…..’akasema huyo mzee, na kijana akamuangalia huyo mzee, hakusema neno hapo na huyo mzee, akasema

‘Ndio maana nilihisi hali sio ya kawaida, mizimu ina jambo, lakini kwa hivi sasa siwezi kuongea nayo, ni vigumu sana leo,..sijui nitafanya nini….’akatulia.

‘Sasa kama unamfahamu huyo mtu, kuwa ni mbaya kihivyo, ni kwanini mnamuahangaikia yey, ..eti aje kuchukua madaraka, nyie watu mpoje, kwanini usingelishirikiana na polisi,…ukamaliza kazi, wewe si mtu wa serikali, kwanini ufanye mambo kama haya, nikushauri kitu,…wakati ni huu, wakuonyesha sehemu yako ya pili ya undamilakuwili,..’akasema kijana.

‘Kijana chunga maneno yako..hunijui mimi…’mzee akasema

‘Nakujua sana mzee, nimeshakujua wewe ni nani,…..nisingelikujua nisingelikubali kuja hadi huku, wewe ni ndumilakuwili, msailiti…’akasema

‘Tatizo lako hujui  tu…hunijui, hujui kuwa mimi naweza kuja usiku ukiwa umelala nikakufanyia mambo na hujui …’akasema

‘Sasa unapata fadia gani, mimi si nimelala, ..fanya ufanyalo, …sijui, sina fahamu hizo, wewe ndio unajisumbua,na mwisho wa siku utaangamia, makaburi yenu yatajaa mijoko, mtakufa huku mnanuka, mtaoza mkiwa wazima…adhabu zeni ni nyingi sana, sijui kwanini hamumuogopi mungu….’akasema kijana.

‘Tunamuogopa sana, lakini hayo …ni mambo ya kurithi tu, na ukishaingia unakuwa huna ujanja wa kutoka, kutoka kwake, labda ufe….’akasema.

‘Mzee,..tuspoteze muda, …mimi nitakusaidia jambo moja, wewe si unavitaka hivyo vitu, sasa kwanza ungekuwa umenihakikishia kuwa huyo mdada yupo hai, ningelifanya utakavyo, uvipate hivyo vitu.., lakini sasa..kumbe unakwenda kuwatupia mbwa mwitu,….hata sikuelewi…mzee, kwa mtaji huo sizani kama nitakuamini….’akaambiwa

‘Kijana nilikuambiaje tokea awali, mimi nauma na kupulizia, nia ilikuwa kuwapata hawa watu, nipate na kula yangu, nina maisha mazuri nyumba,..unaona, nikihiajai pesa napewa, japokuwa ..oh, sina raha, ni maisha ya shida,..’akasema akionekana mnyonge.

‘Hamna akili ndio maana, kwanini ulikubali..’akasema.

‘Kijana, wewe una akili sana, unajua hilo wazo…lakini anatusikia,…hilo la kusema eti tushikiane na polisi, ni wazo zuri,…,lakini hivyo vitu,…mimi nimeshafungamana navyo,visipopatikana na mimi nitakuwa matatani…nitaangamia,….ndio tatizo la haya mambo…’akawa sasa akionyesha dhahiri kuwa keshaanza kuogopa
Kukasikika sauti, kitu kama kimedondoka, wote wakatega sikio..

‘Umesikia mzee, ndio mizimu hiyo….’kijana akasema akitega sikio.

‘Mhh…hiyo sio mizimu, kuna kitu….’akasema huyo mzee akikagua kwa macho.

‘Hebu kwanza nieleze ulivyofanya, …kuhusu mdada, na inatakiwaje..?’ akaulizwa kijana akionyesha kutokujali , lakini mzee akawa anaendelea kutafiti kwa macho,

‘Nahisi kuna mtu humu ndani…’mzee akasema.

‘Mzee hakuna mtu,..wasiwasi wako tu, …hebu niambie, uliingiaje kwenye anga za hawa watu….?’ Akaulizwa na mzee akamuangalia kijana, halafu akasema;

‘Mimi ni mtaalamu wa mambo ya msukule, ..walinihitajia sana, kama nilivyokuambia awali..nia yao, niwasaidie utaalamu huo, wachangenye na utaalamu wao wa kidigitali kama walnavyouita, kwa ahadi kadha wa kadha..mimi nikaona hakuna shida, maana walitega kwa mambo fulani fulani, nisipowasaidia, basi, wataniumbua,…’akatulia

‘Wajanja sana,mpaka mzee ukakubali kuwasaidia,…sawa kwahiyo ukawasaidia nini hasa, kuwafundisha tu huo utaalamu, au kuna mambo mlikuwa mnafanya na wao,…?’ akauliza.

‘Kuwasaidia sio jambo dogo, kulihitajika kila mara wakitaka kufanya jambo lao linalohitajia mambo yangu wananiita, kama wanataka labda kuwapata maadui zao au kuna watu muhimu wanaowahitajia,basi wananiita, napata mapesa mengi tu, lakini unajua tena mapesa yao ni kishetani, unapata leo keshi huna kitu….’akasema

‘Na wewe ndio uliwasaidia kuhusu hivyo vitu…?’ akauliza

‘Hivyo vitu…ndio, bila ya mimi wasingelijua wpi vilipokuwa, bila ya mimi wasingelijua nhivyo vitu vinatakiwaje, vifanyiwe nini,…nimewasaidia sana, lakini tatizo hawa watu hawana rafiki wa kudumu, ukifikia muda hawakutaki wanakumaliza….nio sera yako!’akasema kwa sauti ya chini.

‘Aaah, mimi sijaelewa jinsi gani ulivyofanya hadi ukaligundua hilo, wapi vilivyo, na vifanyweje…’akasema huyo kijana.

‘Mambo ya giza..hayo, siwezi kukuelezea ukaelewa,…ila mimi niliweza kuipata historia yote ya hivyo vitu…ni mambo ya kale sana, lakini mpaka sasa yanafuata mkono wa kizazi husika, nikawaelezea namna itakiwavyo…na awali, ilikuwa hivyo vifaa vifike kwa mama wa huyo binti,..kufauta mila zake, yeye akivishika, anamkabidhi huyo binti yake..hivyo ndivyo ilitakiwa awali…sasa mimi nikafanya mambo ya na mizimu…tukabadili badili wee, lakini kwa makafara makali…’akatulia

‘Makafara ya kuua watu…au si ndio hivyo?’ akauliza

‘Inabidi…mambo hayo , sio mchezo..niliwaambia lakini, hawakusikia, nia yao ni kuhakikisha hivyo vitu vinapatikana, hawakujali tena maisha ya watu…, unaona humu ndani, hiki chumba ndipo nilikabidhiwa kila kitu, na ..hata sisi kufika hapa,… ilipangwa na mambo yote yangelimazikia humu ndani kama mambo yangeenda vizuri, mdada akiwepo, na wewe ungeliletwa hapa na kazi ingelimalizika…docta ndiye kaharibu, huyu docta huyu…ole wake…’akachuchumaa.

‘Sasa mzee, jiamini, wewe si kigagula,…manachukua watu usiku, mna..wafanya nini sijui wanaonekana wamekufa kumbe bado…hilo siamini,…labda kidogo nimuone huyo mdada, akiwa hai, hapo nitaweza kukuamini…’akasema.

‘Tatizo lako wewe, hujaamuka bado,…’akasema

‘Sasa mzee, kwanini wakutishe watu wengine, nasikia nyie mnaweza kujigeuza paka,..akija huyo jamaa akitaka kukuua, unajigeuza paka, au ni geresha zenu,…hahaha, watu wengine bwana…’akasema kijana kama mzaha.

‘Unasema nini, unajua wewe kijana, usitake tukaanza kukosana, sikiliza, wewe hujui hatari iliyopo mbele yetu, humjui huyo mtu, hujui kabisa kinachokusubiria wewe, na hata mimi .., ogopa, kukutana na huyo mtu…wengine wanamtania kwua ni izraili,..maana akija kwako, unahesabu siku, …’akatulia.

‘Iziraili, nyie watu mnakufuru sana….’akasema kijana.

‘Ndio maana nasema wewe hujajua hatari iliyopo mbele yako…’akasema

‘Na wewe je…..’akasema

‘Unasikia…’mzee akatega sikio, akiwa makini kusikiliza

‘Mimi sisikii kitu mzee, kuna nini, labda ni mizimu yako mzee, au…..?’ akauliza

‘Tutafuta sehemu nyingine,..hapa tupo wazi sana, mtu akiingia mlangoni tutangulie kwanza kumuona, na kujiandaa, ..na nahisi  huyo mtu keshaingia tayari ndani ya hili pango la kuzimu, ,..….’akasema huyo mzee, sasa akimvuta huyo kijana ili wajifiche…

‘Mzee, mungu ndiye wa kuogopwa, kama kufa kwa kupitia kwa huyo mtu,basi, mungu ndiye kapanga hivyo, hilo halina mjadala,..mimi, mzee, simuogopi huyo mtu yoyote, wa kunitishia maisha, namshukuru mungu kwa hilo, siogopi hata ukiwa kigagula, unasikia, …muhimu nimpate huyo mdada, na wewe nakupatia vitu vyako hiyo ndio dili, na huyo mtu akija, …polisi watapapambana naye, ..ni kitu kidogo tu mzee…kwanini unaogopa…’akasema

‘Unajua hata wakati nafanya kazi ya kukuzimisha wewe,  nilipata shida, sana,..wewe na huyo binti nyota zenu zina nguvu sana,…ilibidi tupata makafara mengi tu,.. lakini mimi mtaalamu wa mambo hayo, hatimaye nilifanikiwa,,…sasa nashangaa unavyojinadi hapa, kama ningelitaka kukumaliza…ilikuwa ni kazi rahisi tu, lakini mnahitajika bado…’akasema mzee.

‘Msingeliweza mpaka siku ifike mzee.., kama siku  imefika,hakuna mwenye ujanja wa hilo, na hata wewe kama siku yako imefika, basi ujue huyo jamaa akija anakumaliza tu, muhimu, ni kujitahidi, nikushauri mzee, wangu, unajua tumezoeana sana, japokuwa ..kiukweli mimi siwapendi watu wa aina yenu,..washirikina,…siwapendi kabisa, lakini kwa hili nitakusaidia, ilimradi tu, nimpate, ok, nimuone huyo binti ambaye alikufa kimazingara yenu…’akasema.

‘Hahahahaha, kijana, eti utanisaidia, kweli asiyejua ni kama mtu kwenye usiku wa giza, unafikia kutamka hivyo kuwa utanisaidia mimi…hahaha, wewe unajua ni kitu gani kinakuja mbele yako, we acha utani,..lakini ngoja nikuambie jambo,..mimi nataka ukavichukua hivyo vitu, sasa hivi kabla huyo jamaa hajafika…’akasema.

‘Sasa mzee kama wewe una uwezo huo kwanini unitume mimi si unakwenda wewe mwenyewe unavichukua na kurudi tu….?’ Akauliza

‘Mtu anayeweza kufanya hivyo…kuvichukua huko vilipo ni wewe , wewe uliyeweza kuvichukua kutoka kwenye mikono ya yule mtu, ndio huyu huyo anayeweza kwenda kuvichukua huku vilipo na kuvirejesha kwake..huyu auliyevichukua kwake,..kuna masharti hapo,mwingine akifanya hivyo, sizani kama atafanikiwa…’akasema

‘Kwasababu gani…?’ akauliza

‘Mazindiko yake…tangia awali yameshavunjwa, na haitafanikiwa mpaka hayo …yaani wewe ukavichukue, na kuvirejesha hapa…nikuambie kitu, hii ni siri, sikutakiwa nikuambie,…wewe ndiwe uliyatakiwa ..umuoe huyo binti, na ukimuoa, yale makutano yenu yanabariki ile nguvu ya vile vifaa, vikiwa mikononi mwenu…sikutakiwa niwaambie hili mpaka uvilete kwanza…’akasema.

‘Sawa mimi sina shida, kwa maana mimi sina umuhimu wa hivyo vitu… muhimu wangu mkubwa ni huyo mdada, sasa nikuulize kitu, nyie,mnasema mlinifahmu mimi kabla, mkanitafuta kwa nguvu za giza, …haiji akilini, maana aliyeniltea mimi huku ni docta, huyu docta ni nani kwenu…’akauliza.

‘Docta..ni msaliti tu…huyo achane naye, ..atajuta kuzaliwa, ila nguvu zilitumika ili wewe uje, kuna mambo tulifanya yakutokee, hadi ukavutika..huko kote ulikuwa unazunguka tu, tulikutafuta kwa kupitia mtandao, wa facebook, ndio tukaweza kukupata ..unajua kuna watu wana nguvu za asili za ulinzi wao,…wewe ni mmojawapo, lakini hatimaye ukaingia kwenye himaya yetu..huyo msaliti ndio akaharibu…’akasema

‘Kwahiyo docta mnamfahamu sana..?’ akauliza

‘Kumfahamu ni baada ya kujitokeza,…mimi nilikuwa simjui…ila hawa watu walipomlisha kwenye mtandao, wakamgundua kuwa yeye ni nani…kiasili ni mtu wa huku huku..yeye, alitakiwa awe mshirika, …wa nguvu za giza, lakini alikataa, huko alipokuwa, angelijiunga, angelikuwa na sisi, hata akiwa huko, si tunakutana…’akasema

‘Oh, kwahiyo, …mimi najiuliza ni kwanini na yeye avitake hivyo vitu, wakati anafahamu hana urithi navyo, au..?’ akauliza

‘Hatujui dhamira yake ni nini, ,..nahisi na yeye kwa vile ana asili fulani na hivyo vitu, yawez\ekana kagundua namna ya kuvifanya vifanye kazi, kwa kupitia utaalamu wake, lakini kwa vyovyote vile, ili viweze kufanyakazi,ni lazima vipitie, kwa huyo dada,akivipata huyo mume atakayemuona ndiye anaibeba ile nguvu yake, lakini sio mume tu, inatakiwa awe na nyota kama ya kwako…nikuulize kitu, wewe docta hajawahi kukuambia  umuoe huyo mdada,..najua atakuwa alikuambia hivyo…?’ akauliza.

‘Mdada yupi sasa..? maana si wapo wawili….’akauliza

‘Kama huyo wa kwanza alijua kuwa kafariki ni lazima alikushauri umuoe huyo mwingine, je hajawahi kukuambi ukamuoa binti, wa huyo mzee, ?’ akauliza…na kijana hakujibu kitu

‘Ndio maana docta hataki kukuachia, na sisi hatutaki kumuachia huyo mdada…tunapambana kwa nguvu za asili, na utaalamu wa kisasa…’akasema

‘Mnapambana wewe na yeye au…?’ akaulizwa

‘Hapana, wao..mimi sinimekuambia wamenialikatu…kwa ahadi kuwa akifanikiwa na mimi nitawekezwa kwenye uongozi na masilahi…mimi ninawasaidia kuwaonyesha nguvu za giza,kwa vile nazifahamu…kiukweli ninazo hizo nguvu,..kutoka kwa mababu, lakini sihitaji sana hizo nguvu.., nafanya kwa vile mizimu inanitaka nifanye hayo, na wakati mwingine ni lazima nitoe makafara , ..unajua, tuyaache hayo mazungmzo, maana masikio yapo mengi, …’akasema
Kukapita kitambo cha ukimia, na huyo mzee akasema;

‘Haya mambo yakiisha salama, nitakufundisha kidogo haya mambo yalivyo….’akasema mzee.

‘Unataka na mimi niwe mchawi, ..hapana mzee…mimi hapana, hayo ni yenu, mimi nitafanya hicho mnachotaka tu , ili  nimpate huyo binti, basi..’akasema.

‘Hahaha, …ushaingizwa baba,… huna jinsi, vinginevyo, mauti yatakuandama, ..ni mambo machache tu, yakikamilika huna jinsi, …ila wewe, una bahati kuwa, bila wewe na huyo binti haya mambo hayawezi kukaa sawa, ..ndio maana mpaka sasa mpo hai..vingnevyo, ndugu yangu, …haaa, ..’akatulia akiangalia saa yake.

Mara kukasikika sauti ya mtu anakuja

‘Nahisi ndio huyo anakuja..’mzee akasema
NB: Mazungumo ya huyu kijana na mzee, yamekuwa marefu, nia ni kufichua mambo mengi yaliyokuwa na utata ndani yake, natumai sasa kila kitu kipo wazi.


WAZO LA LEO: Inapotokea mtu na mtu mkasigishana ni vyema, mkavuta subira, badala ya kukimbilia kutukanana, na kuanzisha zogo, hadi kupigana. Kwenye zogo na kutukanana, shetani anapata mwanya wa kuweka vishawishi vya chuki,  na matokeo yake, wandugu, marafiki, jamii, zinafikia kukosana kabisa. Wakati mwingine ni heri kwetu, kama mtu utajishusha, na hata kuonekane mjinga, ilimradi mwisho wa siku mje kupatana,…ni ujasiri wa kuishinda nafsi, ili kukwepa mfarakano, na visasi visivyoisha. Tumuombe mola wetu atupe subira, na atujalie nafsi zetu zisijawe na hasira za haraka zenye kuleta migongano na chuki kwenye mahusiano yetu, baina ya mtu na mtu.
Ni mimi: emu-three

No comments :