Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, June 1, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-41



 Ni kituo cha polisi ambapo ndipo mama, mke wa mzee alipowekwa kwa usalama wake, na akiwa miongoni mwa washitakiwa,….na bint alipofika hapo akaomba kiongea na mama yake, na mama yake akaitwa,  mama alipofika tu kwa binti yake, kwanza alionyesha macho ya kushangaa, halafu akasema…

‘Umekuja kunitoa, au una habari gani au umetumwa tena na hao watu…?’.

‘Mama sijajaja kwa hayo yote, ila nina…eeh usahuri tu…, kwa hali iliyopo sasa ni bora ukae huku huku…., watu sasa hivi wanauliwa ovyo…kuna mtu jana kauliwa ..akiwa na msaidizi wa docta, na huyo msaidizi wa docta kaponea chupu chupu, kuwawa na hao watu, nasikia wameanzisha operesheni ya kuwamaliza wote ambao wanaona ni hatari kwao ….’akasema

‘Mhh…nani huyo aliyeuliwa, safari hii.?’ Akaulizwa binti na mama yake.

‘Yule wakili wao mkuu,…yule waliyemualika kutoka nchi ya jirani….’akasema

‘Duuh, hapo sasa nimeamini…’ mama akasema akionyesha uso wa huzuni.

‘Umeamini nini mama…?’ binti akauliza akiwa na shauku .

‘Unamfahamu huyo wakili wao ni  nani…?’ akauliza.

‘Aaah, hapana mama,….ni mtu mgeni sana machoni mwangu,  kwani yeye ni nani huyo..?’ akauliza.

‘Wakimkagua vyema…watamgundua…’akasema mama

‘Kwa vipi, nasikia ni mtu wa nchi jirani wanafanya mpango wa kumsafirisha au siivyo hivyo…’akasema binti.

‘Itafanyika hivyo lakini …hatafikishwa huko…itakuwa danganya toto…’akasema mama

‘Kwa vipi mama, kwani askari, hawafahamu…lakini mama kwanini..huyasemi hayo kwa polisi, uwasaidie, nahisi unajua mengi…’akasema binti.

‘Huyo, …wakiweza kuondoa, hiyo ngozi yake ya juu, watamgundua,….mmh..’mama hapo akasita na kusema hivi
‘Aaa tuyaache…, ngoja yawarudie wao wenyewe, maana ni yeye aligundua mambo hayo yote…, ni yeye..mungu amsamehe tu,…’akasema mama.

‘Sijakuelewa mama…’akasema binti, na mama akawa kama hajamsikia akaendelea kuongea;

 ‘Huyo alijiona yeye ni yeye mbele ya wenzake, akafufua mambo yaliyopita, akawajaza wenzake upepo, sasa kipo wapi, sisemi kufa kwake ni …kutokana na madhambi yake, maana kila mtu atakufa, lakini…umauti wake,, na sijui,huko kaburini itakuwaje, anayejua ni mungu mwenyewe,…yeye alijua akifanya mambo yake hatauliwa, na wenzake.

‘Huyo, alijiona yeye ni mtaalamu, ..ni kweli alikuwana kipaji kikubwa sana, kama angetulia akafanya mambo ya haki ,…angelikuwa mbali sana, lakini, tamaa…ana tamaa sana,..ana damu ya kichwi…nisimseme sana, lakini ndio hivyo, damu hurithiana…’akasema

‘Mhh…’binti akaguna hivyo.

‘Bibi yangu aliwahi kuniambia ..tuwe mbali na hao watu, japokuwa ni ndugu zetu, kipindi hicho mimi ni mdogo, …baba yake babu alio wake wengi kwa vile alikuwa kiongozi , alikuwa mfalme wa eneo letu..kipindi hicho maeneo yaligawanywa ki makabila, au kiukoo, …mambo ya kale hayo..nimesimuliwa tu…’akatulia

‘Sasa kati ya hao wake, mmojawapo, alikuwa kigagula kweli…aliwachezea sana wenzake, na bahati nzuri mume wake akamgundua, …na alichomfanyia huyoo mwanamke anajua yeye mwenyewe, lakini alishazaa naye, alishakuwa na kizazi chake, na kizazi chake ndio hiki kinasumbua watu,…’akatulia mama.

‘Kwahiyo mama unataka kusema nini…?’ binti akauliza

‘Ninachotaka kusema ni hivi,…huyo wakili, sio wakili tu, ana kipaji cha mambo mengi, kama ninavyohisi ndio sahihi, basi, huyo mtu..na atakuwa ndio yeye maan yeye hujigamba kuwa anaweza kujibadili kama kinyonga, anaweza kuishi mataifa mengi akiwa na kazi tofauti tofauti, ..sijui ni nani…wanajua wao wenyewe, lakini pia,…aah..’hapo akatulia

‘Binti yangu, ngoja nisikuambie mengi, …ila kama ndio huyo, yeye alijua kuwa kwa utaalamu wake, wenzake watamuogopa, hakumjua huyo mtu anayemtumia yupoje,..yeye, au wao wanafahamu kuwa siri ikitoka ikajulikana kwa serikali, hawataweza tena kumiliki hivyo vitu, hawataweza tena, kuwa watalawa,..kwahiyo msaliti, kama wajuavyo wao, dawa yakee ni kuuwawa,  hawajali kuua, kama wanahisi huyo mtu,atafichua siri ya kundi lao, watamuua tu, hata awe nani….’akasema mama

‘Kwahiyo unahisi huyo wakili alikuwa ni nani,…?’ akauliza bint.

‘Huyo mtu ana dhambi nyingi sana,…na nilijua mwisho wake utakuwa hivyo, nilikuwa na hasira naye, ..nilitaka kumtaja pale mahakamani, ili haki itendeke, lakini akanizuia, akanitishia, aliongea mambo ambayo,..sio kwamba naogopa, alkini nachelea usalama wa familia yangu,….we acha tu…’akasema mama

‘Au ndio huyo mkuu wao au..?’ akauliza binti.

‘Huyo…hapana nielewe huyo, sio huyo mkuu wao,… mimi huyo mkuu wao wala simjui, ila mimi namfahamu huyo ndugu yangu ambaye kaingia ubia na huyo mkuu wao…kwa vile huyo mkuu wao, atamlinda, hadi afanikiwe, wanajuana wameahidiana nini, kuwa labda huyo ndugu yangu akifanikiwa, akapata utawala, badi huyo mkuu atakuwa nani,..ndio hivyo…na huyo mkuu wao ni mkuu kweli,..hajulikani, haonekani…!

‘Sasa kama ni mkuu, kwanini ndugu yako atayarishwe kuwa mtawala wakivipata hivyo vitu, kwanini huyo mkuu asiwe ndiye mtawala mtarajiwa…?’ akauliza

‘Wana maana yao,…na ni kwasababu ya hivyo vitu, haviwezi kwenda kwa mtu baki vikafanya kazi, lazima viwe mikononi mwa damu ya utawala wetu….’akasema mama, na kabla binti yaka hajaulizwa swali jingine mama akasema;

‘Sasa huyo, …kama ndio yeye, huyo alikuwa  mtu wa karibu sana na mkuu, …nahisi huyo mkuu alishagundua kuwa huyo jamaa atakuja kumtaja…akaona ni bora am-malize mapema…’akasema

‘Kwahiyo yeye alikuwa kama nani kwenye hilo kundi…?’ akauliza

‘Huyo marehemu ehe…?...Mimi sijui cheo chake hasa, au ana wadhifa gani,…maana mambo yao ni ya siri sana,…nimejitahidi sana kufanya uchunguzi wangu kwa kujiweka karibu na wao, lakini sio kazi rahisi, ila ninavyohisi  huyo wakili nahisi anaweza akawa ndio huyo wanayemuita mtaalamu wao mitambo…’akasema.

‘Kwanini…?’ akauliza.

‘Kwasabu huyo mtaalamu wao, anafahamu sana mambo mengi , ikiwemo mambo ya sheria,…nilishamsikia akiongea, akiwaelekeza watu wao kuhusu kipi kifanyike na kipi kisifanyike kwa mujibu wa sheria,..pamoja na hayo anafahamu sana utaalamu wa mitambo, komputa,..na zaidi anafahamu hata mambo ya giza…yeye ni kama mashine ya kundi hilo, …

‘Basi atakuwa ndio yeye mkuu wao mama…wamemuua, kwa vile labda kuna mmojwapo anataka kuchukua cheo chake…’akasema binti

‘Hapana, sio yeye…huyo sio huyo mkuu wao,…kama angelikuwa ndio huyo mkuu wao ni nani alitoa amri huyu auwawe…ina maana kuna mtu mwingine mwenye mamlaka zaidi ya huyo. Huyo  alikuwa akitumika tu, bado yupo huyo mkuu,..sasa hapo sijui huyo mkuu ni nani,…ila kwa kuuwawa huyo mtu, basi tena,.hilo kundi halitakuwa na nguvu sana…. ni nani ataweza kuliendesha hilo li mashine lao,..’mama akatulia kama anawaza jambo.

‘Si atachaguliwa mwingine, watakuwa na mbadala wake..’akasema binti.

‘Mhh, hata sijui kama wataweza kujiendesha wenyewe bila ya huyo mtu..lakini kwa vile wanavyodai…kama alivyoniambia kaka…, nia yao ni kupata vitu wanavyovitafuta, wakivipata basi kazi imekwisha, yeye atakuwa mtawala wa aina yake,…hizo ndizo ndoto zake…’akasema mama.

‘Vitu gani hivyo mama..?’ akauliza bint.

‘Binti yangu usitake kujua mengi, mambo mengi humo yamevikwa ushirikina, …na sitaki familia yangu ije kujihusisha na mambo kama hayo, ndio maana nimekuwa msitari wa mbele kupambana na hawa watu…’akasema

‘Vitu hivyo vina namna mbili, wema upande mmoja na ubaya upande wa pili. Upande wa wema, ukiwa mtawala utakuwa na hekima, utaongoza watu kwa uadilifu, utaishi maisha ya kawaida, hupendi uheshimiwa, kutukuzwa, ni..maisha ya kawaida ya kiongozi muadilifu,ila hutakuwa tajiri sana, ni kawaida tu…’akatulia

‘Lakini sasa upande wa pili yake ni upande wa ubaya, upande  huo una giza, una ushirikina, una kila aina ya mambo mabaya unayoyafahamu hapa duniani,…na  zaidi una utajiri mkubwa sana, na zaidi unahitaji kumwaga damu , ukichagua upande huo, utakuwa kiongozi wa kuogopewa kama kitu gani sijui…sasa mtu mwenye tamaa, ni rahisi sana kuchagua upande huo wa utajiri…’akatulia na binti akamuangalia sana mama yake halafu akamuuliza;


‘Mama,..hebu  niambie ukweli, wewe sio mmoja wao…na kwanini ukajiunga huko, na kwanini usimwambie baba mambo kama hayo, huyo ni mume wako alihitajia kuyafahamu hayo,…?’ binti akauliza.

‘Sio rahisi kama unavyofikiria wewe..yeye ni mume wangu ndio, lakini mambo kama hayo sikustahiki kumuambia, ..maana kwanza yalishapita, na kama angelijua kuwa mimi ni kizazi cha huo ukoo…labda angesita kunioa…’akasema

‘Ina maana ukoo wenu ulikuwa mbaya, wa wachawi..?’ akauliza

‘Kama nilivyokuambia, ukoo wetu ulikuwa wa kifalme, alikuwepo mtawala muadilifu,…akaoa wake wengi sifa ya kiongozi ni pamoja na kuwa na wake wengi, mifugo mingi, ardhi , na nguvu… ndio kizazi chetu kilikuwa hivyo,,..lakini mtawala huyo, alioa, kati ya wake zake, .. Kikagula!

Mke huyo, alifanya mambo makubwa ya kumfanya mtawala huyo kuogopwa zaidi..na ndiye aliyemuelekeza mtawala huyo kugeuza vifaa hivyo upande wa pili, eti ili wazidi kuogopwa duniani, na kuteka maeneo mengine..mtawala huyo alikuw hajui kabisa siri y aupande huo pili....na ujue, mkitenda mambo mema, ikatokea jambo moja baya, linaharibu mambo yenu yote mazuri..huyo mama alikuja kufanya ukoo wetu utambulikane vinginevyo…’akasema

‘Oh…kwahiyo..’binti akataka kuuliza swali jingine na mama akamkatili na kusema;

‘Binti yangu nimeshakuambia usitake kutaka kujua mambo mengi, ambayo yanaweza kukuharibia, ustahimilivu wako,..unaweza ukaingizwa huko kwa tamaa, ukisema labda nijaribu,..kwa makamo yenu ya ujana, ni rahisi sana kuvutika, kujaribu, lakini kwa utu uzima wetu, tunajua kuwa kuna mambo hayatakiwi kujaribiwa,…sasa, ..usitake kabisa kujua mambo yao, …namuomba mungu sana, mambo hayo yaishilie mbali, …sitaki kabisa nyie mje kujiingiza..’akasema.

‘Bado mama hujanisaidia, maana kama ni kuingia huko tumeshaingizwa na kuhatarisha maisha yetu kwa vitu ambavyo hata hatuna utaalamu navyo na wala haatuvijui..sasa tumekuwa, na kwa vile tumeshaumizwa, sasa tuna haki  kujua, kwanini iwe hivyo, kwanini ni sisi tu…mama niambie ukweli, inavyoonekana wewe unafahamu hayo mambo yote na wahusika wake…?’ akauliza

‘Binti, ..nielewe ninachokuambia, sitaki ubishi wako wa kitoto, wewe sasa ni mkubwa wa kufahamu kile ninachokuambia, …hayo mambo ni mabaya, yana ushetani ndani yake, na ushetani wake una mvuto zaidi ya upande wake wa wema,…aah, hata sijui kwanini yamerejea huku kwetu, yalitakiwa yabakia huko huko kwao, mimi nilikuwa sijui…lakini ..huyo ndugu yangu…’akatulia akiangalia huku na kule.

‘Huyo ndugu yako, huyo ndugu yako ni nani, na yupo wapi…?’ akauliza binti…na mama akatulia kama vile anaogopa kuongea kitu, na binti alivyoona hivyo akasema;

‘Mama nafahamu unaogopa kuniambia ukweli, kuwa ukiniambia ukweli na wewe utauwawa, lakini niamini mama, sisi ni wacha mungu, wewe mwenyewe ulitufundisha hivyo, tumuamini mungu na kumtegemea yeye, sasa mbona unafanya kinyume chake…unaogopa kufa, au? Akauliza binti.

‘Binti yangu mimi ni mama yako,…nimeishi umri mrefu zaidi yako,nafahamu ubaya na uzuri wa kila jambo, nafahamu kipi cha kusema na kipi cha kunyamaza kwa masilahi ya familia, mimi nina bahati kuwa nimebahatika kuwaona mababu, wakiwa kwenye uzee wao,…na mimi nimekutana na mambo mengi mabaya na mazuri, …mimi nimekubeba tumboni mwangu miezi tisa, nimeteseka sana katika uzazi wenu…’akatulia kidogo.

‘Kwahiyo binti yangu nielewe,…sipendi yale mateso ya uzazi yawe yanajirudia rudia tumboni mwangu,…mwanangu hujajua uchungu wa mwana kwa mama yake, hujui jinsi gani mama anavyojisikia pale anapoona mwanae anapata shida,…we acha tu…’mama akasema, na kauli hiyo ikamfanya bint anywee…

‘Mama naelewa hilo, sina nia ya kukufanya wewe uteseke, ila mimi natafuta njia ya kulikwepa hilo na kuhakikisha wazazi wangu mpo salama, nikilijua hilo jambo, hata mimi nitaweza kujilinda, na kuwalinda nyie wazazi wangu…hivi sasa mnaumwa, na sijui chochote,…nitasema nini, nitawalindaje wazazi wangu…tunajikuta sisi watoto kati kati ya matatizo ambayo hata hatujui yameanzia wapi…tuna haki ya kufahamu mama…’akasema binti.

Mama alimuangalia sana binti yake, na machozi yakaanza kumlenga lenga, akatikisa kichwa na kusema;

‘Hapana binti yangu, sio wewe….sitaki, sitaki…naona hili jambo acheni tufe nalo, sitaki mje kujihisi ni …washiriki, au warithi wa mambo kama hayo..mimi nilikataa, na ningelikubali..oh, sijui..ingelikuwaje…, mungu mwenyewe ndiye kanisaidia, sasa iweje na mimi nije kuwaingiza nyie kwenye uchafu huo…’akasema.

‘Kwahiyo mama kumbe mambo hayo ni uchafu, ni uchawi, ..una maana kusema wewe ulikabidhiwa mambo hayo, ..wewe mwenyewe umesema upande mmoja una mazuri, sasa kwanini uogope…’akasema


‘Najua mtihani wake..hapo tu umeshaingia na tamaa, kuwa upande mmoja ni mnzuri, utakusaidia nini, hata kama ni mnzuri, kwanini uingie kwenye tamaa ya mambo ambayo..kwanini usimtegemee mungu wako utegemee vitu kama hivyo, ni ushirikina mtupu..ndio maana sitaki viendelee kuwepo., nikiwa hai…’mama akasema

‘Najua ni nini kitakuja kutokea kama utajiingiza kwenye mambo hayo, najua uta-taka kupigania haki yenu ambayo sasa inataka kutawaliwa na ndugu zenu ambao wanaona wana haki navyo kwa vile wao ni wanaume, lakini sisi, nyie wenye haki navyo, ni wanawake,…’hapoa katulia kidogo, halafu akasema;

‘Enzi hizo,…wanawake walikuwa na haki zao, lakini inapofika kwenye utawala, kama mke ndiye mrithi, akishaolewa haki hiyo anaichangia na mume wake ..na huyo mume anatakiwa awe ni mume muadilifu, walijua wenyewe jinsi gani ya kumpata mwanaume wa namna hiyo, sasa sio kizazi chenu hiki cha sasa!

‘Sasa hao ndugu zangu, wameshaambiwa kuhusu hivyo vitu, lakini hawajui ukweli wake, kuwa kuna sehemu  mbili ya hekima na uadilifu, na ili uipate sehemu hii ni lazima uwe na haki, ya kuvirithi hivyo vitu, hiyo haki hawana, ila kuna sehemu hiyo ya pili, ya nguvu, ..uongozi na utajiri,..lakini inahitajia makafara ya damu….umeona hapo kulivyo na mtego…’akasema mama.

Huyo ndugu yangu..ambaye ndiye chanzo cha haya yote, yeye anafahamu ukweli wote tofauti na ndugu hao wengine…, na anajua kuwa ili hivyo vitu vifanye kazi ni lazima vipitie mikononi mwangu,..mwenye haki , maana mama,..yaani huyo bibi wa kipindi hicho alikuwa ndiye mama yetu sisi…kwahiyo hivyo vitu ilibidi vipitie mikononi mwetu sisi kwanza…’akatulia.

‘Kama …hatuna sifa za uongozi, basi unavikabidhi kwa ndugu wengine wenye sifa hizo,…kuna namna yao, …sasa wao walitaka vikishapitia kwangu mimi eti nivikabidhi kwao, kwa vile mimi ni mwanamke.

Lakini pia nyie mpo, bado nyie ni wanawake,..basi kwa njia nyingine, ukitaka haki, nyie mlitakiwa mvipate kutoka kwangu, halafu muolewe na waume waadilifu, ndio nguvu iwepo, wasiwasi wangu ni kuwa je mtawapata waume wema, wenye kubakia upande huo wa hekima, uongozi wa uadilifu, asiye na tamaa…hapo  ..ndio mtihani wake. Ndio maana nilitaka hivyo vitu vipotee kabisa visije kuleta mabalaa…’akatulia mama.

‘Sasa kwanini wao wanavihitajia, wakati wao sio warithi halali..?’ akauliza

‘Ukumbuke wao ni waovu  kiasili, na wao wanataka kuchagua upande ule wa pili, ule hauhitaji sana,…haki, ..na mlolongo wake, wenyewe ni wa tamaa, utawala,.utajiri, nguvu, na madaraka,..ukiwa navyo ukachagua upande huo, wewe ni kiongozi wa imla,…kutoa amri,..lakini ili ufanikiwe huko…damu itamwagwa,..ndio wanaita makafara….hata hivyo, bado itahitajika damu yenu, nyie warithi halali, ili nguvu ihamie kwao…wao kiasili wameshaingizwa kwenye ushirikina huo, na wameshajua kuwa vitu hivyo vipo, na kuvipata kwake ndio hivyo…

‘Mama…’akasema

‘Si umetaka nikuambie, haya ukweli ndio huo…niambie, sasa utafanyaje hapo, maana ukiviachia hivyo vitu vitaenda kubaya, na ubaya utakuja kukuangamiza hata wewe kama alivyoangamia dada yako, kwa vile damu yenu ni muhimu sana ili vitu hivyo vifanye kazi,..na ukivichukua wewe kwa mfano, je una uhakika gani kuwa utapata mume muadilifu..una uhakika gani kuwa….ni mtihani mwanangu..ndio maana mimi nilitaka nivipate, nijue nitafanyaje…’akasema

‘Ukivipata utafanyaje…?’ kauliza

‘Kwa vipi tena ..na wakati huyo …kaka keshavipata….’akasema mama

‘Nakuuliza mama je nikivipata hivyo vitu nikakuletea utavifanyaje..?’ akauliza binti.

‘Nitajua la kufanya..mume wangu ni muadilifu, lakini..sikutaka kumuambia chochote kuhusu vitu hivyo, ..angaliweza kubadilika,…mume wangu ana haki na hivyo vitu , lakini kama vilivyo, bila ya kuwa na nguvu yoyote ya asili,..maana alivipigania akavipata kwa njia halali, lakini je ningelimuambia kuhusu uasili wake..wasi wasi wangu ulikuwahivyo..

'Ina maana ulikuwa humuamini baba...?' akauliza binti

'Sio swala la kumuamini , ni swala la kuitanguliza mbele familia,..mimi ni mama natakiwa niyaone hayo yote..maana sote sisi ni wanadamu, siwezi kuijua nafsi ya mtu mwingine hata akiwa mume wangu..anaweza akatekwa na ibilisi akabadilika, wangapi yamewatokea hayo,…maana dunia hii ina mitihani...'akasema

'Lakini mbona vikaja mikononi mwake...huoni kuwa mungu ametaka kukuonyesha kuwa mume wako ni mwema...'binti akasema

'Sasa hapo sio mimi, na kwa muda huo , hata alipovileta bado nilikuwa sina mawazo navyo, sikuwa nafahamu kuwa ndivyo hivyo bibi alivyoviongelea....ndio maana, hata nilipojua kuwa ndio hivyo, nikataka aendelee kuwa navyo, bila ya yeye kujua undani wa hivyo vitu,...'akasema

'Una uhakika kuwa baba hajui undani wa hivyo vitu....'akauliza binti.

'Sizani kama anafahamu hayo, hayo ni mambo ya ndani ya kifamilia, na ni ya zamani sana...ila kama vingendelea kuwa kwake..nisingelikuwa na mashaka maana nina uhakika vilikuwa kwenye mikono salama…hadi siku muafaka ikifika, na mimi ningelijua nifanyeje..’akasema mama.

‘Kwahiyo mama, …ulijuaje kuwa baba kavipata hivyo vitu…?’ akauliza.

‘Nilikuja kuambiwa na kaka..huyo ndugu yangu wa kambo.., kuwa anahisi kuwa mume wangu keshavipata hivyo vitu akawa ananishawishi nimpe ili avitumie yeye kama mimi sitaki kuvitumia....nikakumbuka bibi alivyoniasa kuwe niwe makini na hicho kizazi,japokuwa yeye aliamua kumkabidhi huyo ndugu yangu huo mkoba, maana alikuwa tofauti na ndugu wengine, ..'akasema

'Kwanini saa wewe hukutaka kuuchukua huo mkoba, kwani ulikuwa wa uchawi...?' akauliza

'Hapana sio uchawi..ni utaalamu wa kitiba..na..na mambo hayo ya kurithi, kuna mambo unatakiwa kuyafanya, kila muda fulani, mimi nayaona kama ni mambo ya kishirikina tu...'akasema.

'Sasa kwanini bibi yako huyo hakutaka kuyaacha kama yalivyo, akafa na vitu vyake...?' akauliza

'Kuna masharti...sijui lakini,lazima kuna sababu...kuwa hana jinsi, ni lazima kumkabidhi mtu mwingine...na hakupenda kumkabidhi huyo kaka yangu, japokuwa alikuwa ni mtu mwema kipindi hicho, aliniambia huyo hafai, hawaaminiki, na niwe makini nao..'akasema

‘Kwahiyo kwa namna nyingine ilitakiwa hivyo vitu vije kwenu...kwako, hakukuwa a mtu mwingine zaidi yenu, au sio...,au ni lazima kwa mke wa kwanza, na mtoto wa kwanza, hata awe mke au mwanaume,,…au sio?’ akauliza

‘Ndio hivyo…sijui ..lakini nahisi ndio hivyo….’mama akasema akionyesha hakupenda sana kuyaongelea hayo mambo, lakini hakuwa na jinsi .

‘Sasa yeye, huyo ndugu yako aligunduaje…?’ akaulizwa

‘Atakuwa aliambiwa na …bibi..au..hata sijui..bibi aliyetaka kutuachia mkoba mimi nikakataa, huenda yeye alimuelezea..katika kukabidhiana huo mkoba, ndio maana alipoupokea tu, akasafiri…na akawa ni mtu wa kuja na kuondoka…’akasema.

‘Nahisi huko ndio akaja kuambiwa, …kuwa mume wangu anavyo hivyo vitu..na ukumbuke kulikuwa na ufunguo huo wa jabu, alishaupata, na siri za ufunguo huo ni kuwa ukiupata ufunguo huo wa ajabu, inakuwa ni namna ya kuweza kufungua kujua mambo mengine ya dunia, ya watu, yaliyojificha, kufungua vitu vyote vyenye vitasa nk…’akatulia

Na sasa kwenye enzi hizi za digitali, ufunguo huo, unaweza kufungua password yoyote ile..nk, lakini ndugu yangu huyo awali hakuwa mtaalam sana, alihitajia mtu anayejua utaalamu wa kisasa,.. ndio akampata huyo marehemu, huyo ndio akawa kichwa chake…sasa keshavipata hivyo vitu vingine, hahitaji mtu kama huyo tena..nahisi ndio maana akaamua kumuua,..’akasema mama.

‘Oh, mama, kwanini usingeliwaambia polisi au watu wanaoweza kutusaidia kama docta..’

‘Hahaha, docta….hahaha,… docta, huyo humjui tu, huyo, ni ndugu kutoka kizazi cha bibi miongoni mwa wanawake wa huyo mfalme wa enzi hizo, lakini yeye hatoki kizazi cha huyo bini Kigagula, ila kulikuwa na mwanamke wa huyo mfalme aliyekuwa na kipaji cha uganga, ..’akasema

‘Ulimjuaje…?’ akauliza.

‘Mimi ni kama mrithi wa kifalme, kuna vitu vinanijia kwenye njozi..siwezi kujua zaidi, ila nilikuja kumgundua tu, na siku niliongea naye, akakubalia, kuwa huenda, hakutaka kunifichulia,..nahisi anaonyesha kuwa na tamaa na hivyo vitu,…anavihitajia ili kukamilisha mambo yake, najua akivipata hivyo, atakuwa docta wa aina yeka…maana hivyo vitu vina siri nyingi zaidi ya utawala,..kama atakuwa mwema kama alivyokuwa mama yake,..lakini …, ‘mama akasema.

‘Kwahiyo akivipata hivyo vitu..huwezi jua, anaweza kutafuta namna yake na yeye maana ana damu ya kifalme, japokuwa sio mrithi halali, ila akighilibiwa, anaweza kutumia upande wa pili,, …na ndio maana alitoka kote huko mbali kuvitafuta hivyo vitu, na alishajua njia yakuvipata hivyo vitu ni kupitia kwa..msaidizi wake..’akasema

‘Msaidizi wake kwa vipi, yeye ni nani kwetu…?’ akauliza

‘Yeye anatokea ukoo, ambao kwetu sisi ni haki kuolewa au wao kuoa kwetu, ulitambulikana sana, enzi hizo..ukoo huo ndipo alipotokea mama wa huyo docta, tatizo lao moja…hawaaminiki sana…hata hivyo ukoo wao ulikuja kuwa mbaya baadae, …kuna mambo yalitokea, kwa huko kuchanganya changanya, kuoa huku na kule…’akasema

‘Sasa mama nikuulize kitu, Je huyo docta akivipata hivyo vitu itakuwaje…?’ akauliza

‘Mungu wangu …, hata sijui…huyo mtu haaminiki,…kuna jambo jingine sikukuambia, ni kuwa hivyo vitu vikienda kwingine, basi … kizazi chetu, kitakuwa ndio mwisho wake, yaani wewe hutazaa tena, ndio basi tena..ndio maana unaona hatuna watoto, kwa vile vitu hivyo havipo kwetu, tumejaliwa watoto wawili tu…, na huyo mmoja ndio basi tena, umebakia wewe, sasa wewe utakuwa huzai tena,..mimi kwakweli sijui kwanini haya mambo yapo hivi..ndivyo alivyoaniambiwa...’akasema.

‘Uliambiwa na nani..?’ akauliza bint.

‘Huyo kaka, …. hata bibi..aliwahi kuniambia hivyo..lakini hakunifafanulia , sikujua ni kutoka kwenye hizo siri  za hivyo vitu,…bibi huyo hakunitajia waziwazi, ..kwa vile nilikataa kuupokea huo mkoba…ila mengi alimuambia huyo kaka yangu’akasema.

‘Kwahiyo mama kumbe ..natakiwa nivipiganie hivyo vitu kwa nguvu zote, ili vije mikononi mwako, na wewe utajua jinsi gani ya kuvifanya, kama ni kuviharibu….au ..vyovyote utakavyo…nimeshajua hilo, haina haja ya kuniambia zaidi….na ni uhakika vitarudi mikononi mwako mama, labda nife..’akasema binti.

‘Unaona sasa, unataka kuharibu, mimi sijasema hivyo, kumbe..oh, sasa hili ni balaa, kwanini nimekuambia haya…’mama akasema.

‘Mama..tuyaache hayo,…..naona muda umekwisha, unamuona yule askari anavyotutizama,…’akasema bint akionyesha tabasamu kama vile kafanikiwa kupata kitu ..lakini mama akawa hana raha kabisa!

‘Ndio hayo ambayo yalinifanya nisiwaambie haya mambo, nilijua tu, nyie kizazi cha sasa hamna subra, mna pupa pasi na kutafakari, pasi na kufanyia tafiti, huwezi kukurupuka tu, bila kuhakiki, mtaharibu, badala ya kujenga…sasa unachotaka kufanya kitanifanya na mimi nianze kuumwa kama baba yako..uvumilivu na uhodari wangu wote wa kujiamini, sasa umeshaniondoka, sijui kwanini nimekuambia haya…’mama akasema sasa akionyesha kuchoka.

Akafika askari na kusema muda umefika, na mama akasema

‘Naomba muda kidogo, kuna mambo nataka kuyamaliza na binti yangu…’mama akasema sasa akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa.

‘Mama usijali…usiwe na wasiwasi kabisa na mimi…, sitafanya kitu zaidi ya kufuata malezi yenu mema, niamini mama, na kuna kitu kingine ninataka kukihakiki, nikipata uhakika wake, basi…’binti akasema sasa akianza kuondoka..

‘Kitu gani tena hicho bint yangu,..mbona unataka kunimaliza kabla ya muda wangu.

‘Nimegundua kuwa dada hajafa….’akasema.

‘Eti nini…wewe acha ujinga huo, ni nani kakuambia hivyo…’akasema.

‘Kama haya uliyoniambia ni kweli,….basi ..kweli dada hajafa, …na mimi ni lazima niupate huo ukweli…’akasema binti.

‘Kutoka kwa nani..?’ akauliza mama sasa akionyesha kuishiwa nguvu uso ulishaingia uwoga, ambao hajawahi kuwa nao kabla.

‘Kwa huyo huyo ndugu yako…’akasema.

‘Wewe mtoto wewe , hivi kwanini nimekuambia mambo hayo…mungu wangu, na huyo mtu utamuona wapi,…unajua unachotaka kukifanya ni kama vile mbwa anavyojipeleka kwenye kinywa cha chatu, mungu wangu nimefanya nini jamani…nakuomba tafadhali…’mama akasema lakini binti huyo alishaondoka.

Na kwa mbali akamuona docta akija, akiwa kaongozana na mkuu!
NB: Ngoja niishie hapa nisije kuchanganya mambo, maana naona mambo mengi yananijia

WAZO LA LEO: Matatizo yakizidi sana unaweza kufikia sehemu mtu ukasema, ‘mungu wangu hivi mimi , ni hivi mpaka lini…’ ni kauli ya kukata tamaa, lkn haitakiwi kukata tamaa, ‘hivi mpaka lini’ iwe ni changamoto ya kujaribu njia mbadala ya halali…na mola atatusaidia,…tuzidi kumuomba mola wetu,atujalie subra na kuongoza kwenye njia halali za kupata kipato chetu, atujali tupate riziki ya halali…Aamin.
Ni mimi: emu-three

No comments :