Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, June 24, 2017

DUWA LA KUU...1 (Utangulizi)


Kuna mambo mengine ukihadithiwa unaweza kusema ni hadithi tu, au ni visa tu vya kutunga tu na wengine wanasema wewe unayaandika haya, umesaidia wangapi....kweli tuone tusiseme, kweli tumeona , tumesikia, tusiseme tukae kimia tu kwa vile hatuwezi kusaidia,..mimi naona kusaidia tuliojaliwa nako ndio huku kusema, kuyaelezea yale mabaya yanayotokea, huenda ikawa ndio sabau ya watu kubadilika...

Na haya wengine hawaamini,...kutokana na mitizamo mbali mbali...lakini hakuna aliyeomba,..labda tusuibiria, yatukute ndio tutaamini maana ndio hulka zetu, tunaamini kwa mifani, tunasaidiki kwa kuona, na ndio maana mabeberu wanatunga uwongo, ili kutupumbaza akili zetu, si ndivyo tunataka kwa mifano ndivyo wanadamu tulivyo,  …watu wanafikia hata kutokumuamini mwenyezi-mungu kiukweli kutoka moyoni, wanaamini tu mdomoni, mpaka wapatwe na mitihani mikubwa ndio utamsikia mtu akisema mungu wangu nisaidie.

Wakati naliwazia hili, nikakumbuka kisa cha binti, ambaye alikuwa mfanyakazi wa ndani, ambaye wakati ananihadithia kisa hiki, alikuwa kambeba mtoto mgongoni, sasa ni mama mlezi,…hajui watakula nini, lakini hajakata tamaa!
Nilimuangalia yule mtoto aliyembabe, akahisi ninataka kusema nini, akatangulia kusema;

‘Sasa nina huyu mtoto, lakin mpaka sasa sijajua baba yake ni nani…’akasema

‘Kwanini, kwani huyu mtoto ulimpataje..?’ nikamuuliza.

‘Mungu ndiye shahidi yangu kwa kauli hiyo…, maana hata niongee nini, ni nani atanisikiliza, nimejionea nijinyamazie tu…, na kuna kipindi nilitaka kwenda mahakamani, lakini nilichokipata nikasema basi tena.., nimuachie mungu japokuwa duwa la kuku halimpati mwewe….’akasema aionyesha uso w majonzi.

‘Kwanini usinisimulie kisa cha matatizo yako, huenda ikawa ni sababu sio kwako wewe tu, bali na iwe ni sababu ya wengine kuliona hili jambo kwa ukweli wake, kutoka kwako, maana kwa hivi sasa watu hawalijua au sio..kama ulivyosema,…, na wanasema mengi ..si ndio hivyo, watu si wanasema mengi ambayo sio sahihi kuhusu huyo mtoto..?’

‘Ni kweli, na sitaki tena kuwaambia lolote nimewaacha waongee tu, lakin siri ya matatizo haya nayafahamu mimi mwenyewe, na nimeamua, nitahangaika na huyu mtoto, mpaka atakua mkubwa.., na ipo siku ataniuliza baba yangu ni nani, ndio hapo nitampa jibu ambalo hatalisahau..’ilikuwa kauli ya huyo mdada, aliyekuwa mfanyakazi wa ndani.

‘Haya niambia ilikuwaje, …huyo mtoto ulimpataje, na baba yake ni nani..?’ nikamuuliza.

‘Hivi uniamini….Nimeshakuambia baba yake mimi simjui,..hadi hii leo, sio kwamba naongea hili kwa kuogopa kumtaja, hapana, naongea hivi kwa vile kiukweli simjui hasa baba wa huyu mtoto ni nani….mungu mwenyewe ndiye anayemfahamu, na huenda kafanya hivi ili iwe mtihani kwangu na kwa hao walionifanyia hivi…’akasema.
‘Hao waliokufanyia hivyo, ina maana ni wengi, labda samahani,..walikubaka..au..?’ nikauliza

‘Walinibaka!!…Mhh,…hata sijui…nakuambia simjui,…na ..oh, tuyaache tu…’akasema

‘Sawa labda unisimulia ilikuwaje,..’nikasema, na yeye akaniangalia machoni, halafu akatizama chini, baadae akasema;

‘Naogopa sana kulisimulia hili,…nilitaka nije kumsimulia huyu mtoto akikua,…najua yeye atakuja kuniamini, wengine hawataki kuniambi…waliniona ni Malaya…niliipata kwa …wapiga debe , kama alivyosema huyo mama na mumewe….’akasema

‘Mama yulee, aliyekuchukua kwa mama yako na mumewe au sio…?’ nikamuuliza

‘Ndio….hata huwezi kuamini…yaani ni watu wema kabisa,…ukiwaona wakiongea hivi, huwezi amini, na hata mimi sikuamini hilo mpaka siku …ulipotokea huu mtihani…’akasema.

‘Sasa naanza kupata picha…huyo baba huyo anaweza kuwa baba wa huyu mtoto au sio..?’ nikauliza.

‘Hapana….siwezi kumuhukumu huyo baba wa watu..sijui, kama ningelijua ningelimtaja, kwanini nimfiche..lakini mama alinifundisha kitu, nisiwe muongo, na nisiseme jambo kama sina uhakika nalo,….’akasema

‘Sawa, ….nimekuelewa.

‘Mimi nitakusimulia, kisa hiki, ..nimekusikia sana kwa jinsi gani unavyoandika visa vyako vya kuwasaidia watu kama mimi, nitakusimulia kwa sharti moja, usije kunitaja jina langu, au la hao walionitendea hivi..’akasema.

‘Hilo usijali,…’nikasema.

Kwanza akaanza kulia,…mmh, nikajiuliza kwanini tena, baada ya kuongea anaanza kulia, na nikaona nimuache kwanza alie..huenda itasaidia kumuondoa hicho kilichopo moyoni mwake, baadae akatulia, na kusema;

‘Jana alinitokea mama yangu, akaniuliza kwanini sijafanya alichotaka nikifanye…’akaanza kusema hivyo.

‘Oh, alikutokea mama yako mzazi, kwa vipi..?’

‘Mimi ni yatima, sina baba wala mama, baba yangu alifariki zamani kidogo, na baadae akaja kufariki mama, na tangia nianze matatizo mama amekuwa akinitokea, akitaka nilipize kisasi kwa haya yaliyotokea kwangu na kwake, lakini mimi mtu kama mimi nitafanya nini…’akasema.

‘Kwa vipi mama yako akutokee wakati alishafariki, … hizo si ndoto tu, ..’nikasema.

‘Ni ndoto tu eeh!.. hahaha,..wewe unasema tu kwa vile haijawahi kukutokea,…na kuna mambo aliwahi kunitokea akaniagiza, nikayafanya, na ikafanikiwa, nilitaka ku…..itoa hii mimba, akanizuia, kwa namna ya ajabu kabisa, siwezi hata kuamini..’akasema.

‘Unazidi kunipa hamasa ya kukisikia hiki kisa, …hebu tuanzie awali kabisa, ilivyoanzia, tuanzie, eeh, huko kwa wazazi wako ilikuwaje.

‘Nitaanzia, pale nilipoagana na mama yangu,..huko kijijini, siku ambayo alikuja, mama mmoja, yeye, ni mwenyeji huko kijijini kwetu…ila wao  mungu amewajalia kuwa na uwezo, wamejaliwa kuwa na maisha mazuri, huko kijijini na huku mjini halikadhalika, ..’akatuliza.

‘Basi huyo mama akaja kwa mama yangu kiwa hai, …huko kijijini tunajulikana sisi kama masikini wa mwisho ..hata ndala hatuna, nilikuwa natembea peku peku nikipita kuomba mitaani…, na siku alipofika huyo mama ndio alininunulia ndala,..nashukuru, kwani alininunulia ..sio ndala, kwangu nilikiona kama kiatu cha ufahari.., kwangu mimi nilikiona cha thamani kubwa sana, haijawahi kutokea au kuvaliwa kwenye huu mguu wangu…na alimnunulia mama pia.

‘Sasa mama nani hii,… nimekuja kukuomba jambo, najua nyie mpo wawili tu, na huyu binti ndiye anakusaidia sana…lakini hata akikaa hapa pembeni yako, anakusaidia nini, …’akasema akinitupia jicho.

‘Ndio hivyo, kuomba omba, mitaani, anachokipata ndio riziki yetu tutafanyaje…’akasema.

‘Na hivi kile kishamba chenu vipi..?’ akauliza huyo mama.

‘Watu wanakitaka, …lakini tukikiuaza si ndio basi tena,baba yake huyu binti yangu, alisema tusikiuze, kije kumsaidia huyu binti yetu,..lakini inafikia mahali hatuwezi,..hapa naumwa, sina pesa ya dawa, ni huyu binti apite pite mitaani akiomba ndio ..nipate dawa..’akasema kwa unyonge.

‘Sasa  sikiliza, je huyu binti akiondoka,…nataka akawe mfanyakazi wangu wa ndani, na atakuwa akikutumia pesa za matumizi , unaonaje..?’ akauliza.

‘Oh, jamani…mimi nitaishije,..lakini kama atanitumia pesa za matumizi,..si bora , kuliko kuomba omba hivi, sipendi kuomba, inaniumiza sana, lakini nitafanyeje… basi ni heri…..’akasema akiniangalia mimi, sikuamini kama mama angelikubali hivyo, walishafika watu wengi akawakatalia, sijui huyu mama alikuwa na bahati gani.

‘Mimi nitakusaidia dawa, na nitakuachia pesa za matumizi, kwa siku kadhaa.. na vyakula nimekuja navyo, nitakuachia, unga, maharage, ..na mchele kidogo, vya kukusaidia siku kadhaa,..angalau uweze kupata chochote wakati, huyu binti akiondoka, na kila mwisho wa mwezi huyo binti yako atakuwa akikutumia chochote alichokipata, unaonaje..?’ akauliza.

Mama yangu alipoambiwa hivyo, akampigia magoti, huyo mwanamke, kwa kumshukuru, na kweli akapewa vyakula, na pesa, na usoni mama alionyesha ile furaha yake, ambayo sijawahi kuiona, japokuwa hiyo furaha yake,  ilikatika pale aliponiona sasa naondoka machoni kwake, aliniangalia kwa macho ya huzuni,..macho ambayo nayakumbuka hadi leo,…macho ya kuniaga macho ambayo, yananijia kila mama akinitokea,…’akasema.

‘Yaani mama, sitakuona tena, zaidi ya kunijia kama ndoto…mpaka leo nakuambia siamini..nahisi kama mama yangu yupo huko kijijini ananisubiria…’akasema.

Hapo huyo mwanadada akawa analia, na mtoto wake , ni mdogo tu wa kukaa, hajaanza kutembea akawa anamfuta machozi, kile kitendo cha mtoto mdogo kama yule kumuonea mama yake huruma na kumfuta machozi, kilifanya hata mimi machozi yanilenge lenge., dunia hii jamani, kwanini…we yaache tu.

‘Sikujua kuwa siku ile mama ananiaga, na machozi yanamtoka, akiniambia binti yangu nenda, maana huenda ndivyo mungu alivyotupangia, nenda ukijua kuwa mimi mama yako nipoje, hapa nilipo ni masikini wa kutupwa…wa mfano,  na sina thamani yoyote  hapa kijijini, ..na kila mtu akitaja umasikini ananifananisha na mimi.

‘Binti yangu, huko unapokwenda ni mji wa watu una mitihani mingi …,..sijui hawa watu wapoje, mimi nimeona uende nao tu,  lakini moyo wangu unasita, nahisi,unakwenda kwenye mitihani ya maisha, kwa umri uliofikia, wanadamu wasio wema, wanaweza kukutia kwenye majaribu, ,,ila wewe nenda tu, muhimu mungu wako muweke mbele.

‘Sisi hatukuomba tuwe masikini,..likumbuke hilo, …ila umasikini upo, na sisi ndio zawadi yetu, usije ukaenda huko ukinilaumu mimi, kuwa mama, wazazi wangu ni uzembe wao….mimi nina imani kuwa umasikini wetu, sehemu yetu ya maisha, na mungu ndiye aliyotupangia…..

‘Kila siku nalia…kwanini sisi…maisha yetu ndio hivyo, tokea baba yako, atutoke, kila kitu kimeondoka, na maisha yetu yamekuwa,..ya jana ni bora kuliko ya leo..leo hii kwa mara ya kwanza tutaweza kula chakula cha kujipikia wenyewe…nataka nikupikie na mimi, ule chakula alichokupikia mama yako…’akasema.

‘Hapana hatuwezi kusubiria, yeye atakula huko mbele…’akasema huyo mwanamke.

‘Mwanangu usije kunisahau,..na safari ni hatua, sijui itakuwaje huko mbele, sijui itakuwaje ukiondoka nikabakia peke yangu, sijui…maana hata hicho kidogo tulichopata, kuna wengine wanakitamani, unakumbuka jana walituibia ile ndoo tuliyopewa, yaani hata sisi masikini wanatuibia,..’akasema .

‘Basi mama inatosha mimi sitakusahau mama yangu, nakupenda sana mama yangu..’nikasema na yule mwanamke alikuwa akinisubiri…niende yeye sasa alishatangulia kwenye gari lake.

Mama, akanishika mkono, akaniangalia machoni, akasema;

‘Kwaheri mwanangu,..nahisi kama sitakuona tena…’

‘Kwanini unasema hivyo mama…’nikasema sasa nikiingiwa na wasiwasi.

‘Kwaheri mwanangu…’akasema na kuondoka kuingia kwenye kibanda chetu, ambacho kilikuwa mbavu za mbwa.
.
Basi nikaingia kwenye gari la huyo mama, kwa mara ya kwanza kuingia kwenye gari, nikawa nahangaika kumuangalia mama, lakini mama hakutoka nje, na ikawa mwisho wa kuonana na mama yangu.

Kisa kipya kipya, je nikiendeleze.


WAZO LA LEO: Masikini wapo, kama walivyo matajiri, haya yote sio kwa ujanja wetu, walijaliwa wengi wanaona labda kuwa hivyo ni kwa ujanja wao, wangapi wangapi wanajitahidi hawafanikiwi, au waliojaliwa wanakuja kukosa kabisa.., mola peke yake ndiye anayejua ni kwanini akaweka hizi hali mbili. Ilivyo, kama alivyotuagiza mwenyezimungu matajiri wanatakiwa wawasaidie masikini, na wawasaidia bila kuwanyanyapaa, wawasaidie wakijua ni wajibu wao, na masikini wasiwaonee wivu matajiri, kwani riziki zetu zimepangwa hivyo, muhimu ni kujitahidi, tusijipweteke, kwani vyote hivyo vinapatikana kwa jitihada,..na kumtegemea mungu!
Ni mimi: emu-three

No comments :