Mimi nikakimbilia nje, kwa muda huo nilikuwa sijajitambua
vyema, akili ipo kwenye ile hali kuwa baba mwenyenyumba alikuwa na dhamira
mbaya dhidi yangu, ndivyo nilivyokuwa nafikiria hivyo, kwa wakati huo, lakini
pia nilishaingiwa na woga kuwa mama mwenyenyumba hatanielewa,..atafikiria na
mimi nilikuwa nina nia mbaya, kwa hali niliyokuwa nayo, nilianza kujilaumu
kwanini sikuwa nimevaa vizuri, lakini ni kawaida wakiondoka navaa hivyo
kwasababu ya joto, na kwa vile ninafahamu kipindi hicho huwa hakuna mtu.
Na nikamuona yule kijana akiingia getini, hapo nikaharakisha kukimbilia chumbani kwangu kabla hajaniona, niliona ajabu na yeye kwanini amewahi kurudi hivyo, ...baba karudi mapema, na halikadhalika mama, na sasa kijana, kuna nini leo, sikutaka kufikiria zaidi, nikakimbilia chumbani kwangu.
Kwakweli akili yangu ilikuwa imetekwa na mawazo hayo sikuwa
nimefikiria jambo jingine, sikuwa na kumbukumbu za nyuma, hadi nilipofika huko
nje, nikatulia kidogo, nikajikagua, ooh, hali niliyokuwa nayo, nilivyovaa, sio
ya kuonekana na mtu, kwa haraka sasa nikageuka kuelekea ndani, hapo bado akili
imeganda kwa tukio hilo.
Nilipofika ndani, nikavaa nguo zangu za heshima, na wakati navaa,ndio
akili ikaanza kurejea mahali pale, na hapo ndio nikakumbuka ile barua, kwanza
sikuamini, nikahisi labda ilikuwa ni ndoto, nilitaka iwe hivyo, iwe ni ndoto
sio kweli,…unajua huwezi kuamini, kufiwa ni kitu kingine jamani, …
‘Haiwezekani, …kwanini , kwanini lakini, kwanini sisi,
kwanini jamani, sisi tumewakosea nini hawa watu jamani, na umasikini huu tena,
bado, mama yangu kawakosea nini jamani…’ hapo sikuweza kuvumilia tena nikaanza
kuangusha kilio, kilio cha kwikwi,….nililia hadi kichwa kikaanza kuniuma, na
sijui ilitokeaje, maana nilihisi giza usoni, na kulala sakafuni.
Nilizindukana mtu akinishika shika..nikakurupuka, na
kusimama nikitaka kukimbia, lakini nikajikuta nikishikwa na mshangao, kwani
aliyekuwa kasimama mbele yangu alikuwa ni mtu mgeni kwangu, ni mdada …mdada
aliyekuwa kavalia vizuri tu, akaniangalia usoni, akatikisa kichwa kama
kusitikia, akasema;
‘Oh, pole, sana…’ akasema akiniangalia kwa macho ya huruma,
sikuweza kumjibu, machozi yakaanza kunitoka kama maji, akili haitaki kukubali,
na japokuwa sikujua ananipa pole ya nini…lakini akilini nilihisi labda ananipa pole ya msiba, kama ni
hivyo kajuaje…nikataka kumuuliza ila yeye akaanza kuongea;
‘Mimi nilikuwa mfanyakazi wa humu kipindi cha nyuma, najua
nikwanini upo hivyo, ila mimi kwasasa nimekuja kuchukua mizigo yangu niliyoacha
humu ndani natumai mama mwenye nyumba amekuambia …’akasema.
‘Kawaulize wenye nyumba, mimi sijui, naondoka
zangu…’nikasema, sasa nikitaka kuanza kuchukua nguo zangu na kuondoka mbali
kabisa na hiyo nyumba, sikujua nataka kwenda wapi.
‘Unaondoka,….!! Unataka kwenda wapi bibi wewe,…hahaha, naona
umeshaanza kuionja joto ya jiwe au….! Nikuambie kitu, pambana na haki yako,
…usikubali kushindwa, mimi niliondoka hapa kwa vile nilipata sehemu nyingine,
vinginevyo, wangelinitambua mimi ni nani…’akasema akitikisa kichwa kwa
majigambo.
‘Sasa kwanini uliamua kuondoka..?’ nikamuuliza hivyo,
japokuwa sikutaka kuongea sana.
‘Kuna mengi yalitokea humu, ….nilivumilia sana, lakini
ikafika muda, nikaona haina haja, hata hivyo, nilikuwa nimepata kazi sehemu
nyingine,…ila kuishi humu inataka moyo,…kuna mambo mabaya sana humu ndani,…utajionea
wewe mwenyewe…’akasema.
‘Kuna mambo gani…?’ nikamuuliza kwa mshangao, japokuwa
nimekutana na mambo mambo..lakini kwangu mimi bado nilikuwa naamini ni ndoto
tu.
‘Sijui mashetani, sijui….aah, utajionea wewe
mwenyewe…’akasema na hapo nikakumbuka kale kakijitabu, nikajua huenda ni yeye
alikiacha hicho kijitabu kidogo.
‘Kwani hayo mashetani yapoje, mimi siyajui………’nikamuuliza na
yeye akaniangalia kwa macho ya kushangaa, halafu akaniuliza;
‘Kwani wewe umefika muda gani kwenye hii nyumba na je tangia
uje humu huwa unalala kwa amani …?’ akaniuliza;
‘Mhh…sina amani kwakweli, lakini kwani hayo ni mashetani
yapoje, yanaonakena, au…maana mimi nahisi kama naota tu, mtu ananikaba,
ananifanyia mambo mabaya, ni hivyo tu…’nikasema.
‘Hahaha, wewe wa wapi,….mmh,… hayo ni majinamizi, na
majinamizi kwa uelewa wako ni nini…na
baya zaidi, yanavyokufanyia vitu vibaya au sio…, si ukiamuka unajiona ni kweli
umafanyiwa vitu vibaya, vibya kwa vipi,…?’ akaniuliza.
‘Aaah kwakweli mimi sijui kitu….’nikasema sikutaka kusema
lolote, kwangu mimi bado niliamini ni ndoto, sikuwa na wazo jingine.
‘Hahaha, hujui kitu eeh…., ngoja ubebe mimba ndio hapo
utajua kuwa sio ndoto..ni kweli, na ukibeba huo mzigo, utaanza kuina dunia,
imeibeba wewe ….’akasema.
‘Mimba itaingiaje wewe, kupitia kwenye ndoto…’nikasema kwa
mshangao.
‘Hahaha, ..hebu niondoke zangu naona naongea na mtu
asiye-elewa, siku ukielewa utanitafuta….’akasema.
‘Mimi hata sijui…ni mtihani gani huu jamani, nimetoka kwetu
nikijua nakuja kupata ahueni ya maisha, sasa tena nakutana na mambo haya,..sasa
tena, mama yangu wamemuua…nitakwenda wapi mimi jamani , binti masikini…’nikasema.
‘Eti nini….!!!, wamemuua mama yako, akina nani hao…?’ akauliza
kumbe alikuwa hajajua kwanini nipo na hali hiyo.
‘Nilikuwa sijui, walinificha, nimegundua baada ya kuona
barua waliyoandikiwa, kutoka huko kijini..sijui kwanini walifanya hivyo…wangeniambia
tu, angalau nihudhurie msiba wa mama yangu….nitawalaumu sana kwa hiki kitendo, ….ndio
maana nataka niondoke kabisa humu ndani…’nikasema na kuendelea kulia.
‘Unajua hawa matajiri hawana moyo wa huruma kwa watu kama
sisi,…wao kwa wao wanaoneana huruma kwa vile wanaweza kusaidiana, sasa wewe
utamsaidia nini…., ndio wanaweza wakawa na huruma ya kujionyesha,…kwa vile…unanielewa
hapo…., lakini kwa maswala yasiyowahusu, au kwa kuogopa sheria tu…ila kiukweli,
kwa watu kama sisi, hawawezi kukutilia maanani hisia zako, kwao wao uwatimizie
kazi zao tu, ..na ukiumwa, utaona watakavyokuchukia….’akasema.
‘Lakini kwani wao hawafiwi, hawaumwi…?’ nikamuuliza.
‘Wanafiwa, wanaumwa ten asana…, lakini wao si wao,…hisia zao
kwao ni kwao, na kwa wengine hasa watu kama sisi, hawazijali sana, wanaju
ukipewa ruhusa ya kwenda kwenu, utakaa huko mwezi, na nani atawafanyia kazi zao,
na ukienda utwatia gharama, na gharama kwao, ni hasara, wewe utakuja kujionea
tu….’akasema.
‘Lakini hawa watu hapa wanaonekana ni wema, wamekuwa wema kwangu, wamekuwa wakimtumia mama vyakula ....kiukweli mimi sijawahi kuona ubaya wao....kuachilia
mbali haya yaliyotokea, na haya yametokea kwa bahati mbaya tu, mimi sikukusudia iwe hivyo…’nikasema.
'Yapi yaliyotokea...?' akaniuliza
'Aaah, ....'nikasema hivyo tu na yeye akasema;
‘Wema wanao, lakini …wema wao ni wa kumpatia ng’ombe majani
ili upate maziwa, …chunga sana, humu ndani, utakutana na mambo mengi tu,…mimi
niliondoka, ila…ipo siku, watanikumbuka…’akasema
‘Kwanini unasema hivyo…?’
‘Mimi nimetoka kwetu, nimeaga, walichonifanyia,…watakuja
kunitafuta, …huo ni ujumbe kwao, kama utawaambia haya,…na umbea wako,… kama
hutawaambia, yaache kama yalivyo, nimekuja kuchukua vitu vyangu, na kama
hujaanza kupatwa na matatizo, basi, labda mwenzetu upo tofauti, lakini ..mimi
….nimekuja tu hapa kwa vile niliacha nguo zangu, vinginevyo, nisingelikanyaga
tena hapa, mpaka wao wanitafute, najua watanitafuta tu….’akasema sasa akipanga
vitu vyake vyema.
‘Utawafanya nini….?’ Nikauliza
‘Hahaha, nitawafanya nini, kama walivyonifanyia mimi, na wao
nitawafanyia hivyo hivyo, na yoyote atakayekuwa upande wao, atakiona cha moto….’akasema.
'Kwani wao walikufanyia nini...maana ...?' nikauliza
'Mimi kwasasa sitaki kujiuliza uliza, humu kutawaka moto, yoyote aliye humu ndani atauonja ubaya wangu...sitakuwa na huruma na mtu ....mpaka moyo wangu ufurahi....'akasema
‘Ina maana….hata mimi…?’ nikauliza kwa mashaka.
‘Sikiliza ….nikuambie kitu, hapa kuna tatizo kubwa sana, siwezi
kukuambia ni nani yupo nyuma ya haya matatizo, awali nilimshuku sana baba mwenye
nyumba,…nilimtegea siku moja,…maana walijua mimi ni hivi hivi tu, baadae nikajiukuta nina mimba...aah, …lakini
tuyaache kwanza, sitaki nikusimulie kwa hivi sasa kila kitu, muda utafika nitakusimulia, lakini sio kwa sasa hivi….’akatulia.
‘Lakini si umesema ni mashetani au…?’ nikauliza
‘Ndio ni mashetani, hujanielewa nikuambia mara ngapi….’akasema akiniangalia machoni.
‘Sasa hao watu, baba mwenyenyumba wanakujaje hapo?’
nikamuuliza.
‘Inawezekana wao wanayatumia, au wao wanajivika huo ushetani,
au …hata sijui,ila mimi sijali kama ni wao au kuna mtu mwingine, hapa hapa
nitapambana nao, nilipatia matatizo humu nikaharibiwa usichana wangu humu, nika...we aha tu, sitaki hata kusimulia tena, nashukuru kuwa leo nimefika na nimepaona vyema...'akaangalia huku na kule, na mimi sikusema neno, yeye akaendelea kuongea.
'Siku ..., nilipoondoka hapa....niliondoka na giza
usoni,..nalia, nasononeka.....hakuna aliyenionea huruma,.... sasa nimekuja na macho yangu mawili, macho yenye nuru ya ukatili, unasikia, unyama unyama..…’akasema akiangalia huku na kule
kama kukagua.
‘Oh….mungu wangu, sasa nitaishije humu ndani, mbona unaanza
kunitisha…, kwanza mimi naondoka, mama yangu, kafa…mmh, mama yangu hayupo tena
duniani masikini mie..nitakua mgeni wa nani…ooh, mama umeamua kuniacha mama…’hapo
nikaanza kulia tena, hadi huyo msichana akanionea huruma.
‘Kwani mama yako alifarikije..?’ akaniuliza akiniangalia na
machoni nilimuona na yeye akilengwa lengwa na machozi.
Nikamuelezea kama barua ilivyosema, halafu yeye akasema;
‘Nilisikia taarifa kama hiyo….mmh, kuna mtu mmoja alitokea huko kijijini, sijui
itakuwa ndio hiyo au la…, lakini mbona ilitokea siku nyingi, labda sio hiyo
taarifa niliyoisikia mimi…ni mud asana…’akasema.
‘Sijui ilitokea lini,… mimi ndio niliona hiyo barua,
sijaangalia iliandikwa lini…’nikasema.
‘Hiyo barua ipo wapi…?’ akaniuliza
‘Aaah, …..hata sitaki kuiona tena…nilitoka humo ndani kwa
haraka, sijui ..itakuwa huko huko ndani…’nikasema.
‘Sasa utajuaje mama yako alifariki lini, maana huenda wasikuambie,...nikushauri kitu, ..jaribu kuwa mjanja,..uwe makini kwa kila
jambo, usipoteze ushahidi,..unajua kuna kitu nataka wewe unisaidie, kama
unataka uwe na amani..vinginevyo, na wewe yatakukuta hayo ninayotaka kuyafanya,
…mmh, naona muda umekwenda,..siwezi kukuambia kwa leo….’akasema.
‘Oh, wala sitaki kukaa tena humu ndani….’nikasema.
‘Sikiliza mama yako ameshafariki, huwezi kumrejesha tena
hapa duniani, hata ukienda huko kijijini, na kama ulivyonisimulia maisha ya
huko kwenu, ina maana huna ndugu huna jirani atakuekuthamini tena, ina maana
sasa wewe ni wewe, huna baba, huna mama, wewe ni yatima, masikini…unanielewa…’akasema.
‘Mungu mwenyewe anajua…’nikasema hivyo.
‘Sio mungu mwenyewe anajua,..... wewe kwa hivi sasa unatakiwa
upambane kivyako….au hebu niambie ukienda huko kijijini eeh,, utafanya nini, sana
sana watakuonyesha kaburi la mama yako, halafu,..niambie hilo kaburi
litakusaidia nini… utafanya nini, …muhimu kwasasa ni kuanza mapambano, kwanza
jitahidi upate chako, pili hakikisha haki inatendeka, hao waliomfanyia hivyo mama
yako, na wao uje kuwafanyia hivyo hivyo…kwa udi na uvumba…’akasema kwa
kujiamini.
‘Nitawajuaje mimi…wewe unakijua kijiji chetu kilivyo..huko
kuna watu watemi, wanafanya watakavyo…viongozi wa kijiji wenyewe wanawaogopa…..’nikasema.
‘Kwanini usiwajue, watakuwa ni wanakijiji au ni wageni, …sikiliza
nikuambie kitu, hakuna kinachoshindikana chini ya hii dunia, ukiwa bado
unapumua,…na ukiamua, lakini ukibakia kulia lia, haya lia, mpaka machozi ya
damu labda yatakusaidia, ni kweli hata mimi nililia sana, lakini baadae
nikazindukana, …wao kama wamekufanyia unyama, na wewe walipizie kwa unyama, kwa
njia yoyote ile usijali ni njia gani…’akasema.
‘Sijui, …hata sielewi, hapa kichwa changu hakipo sawa..unayoniambia
mimi sielewi…na sitaki kulipiza kisasi, mimi namuachia mungu tu…’nikasema.
‘Hahaha, haya muachie mungu, mungu humsaidia
anyejisaidia…haya muachie mungu, siku yako nayo ifike, huko mbele utalipiziwa
na mungu ..maana hao watu wakijua kuwa upo, na wakahisi unaweza kuwafuatilia na
wewe watakuua..sasa kabla hawajaanza kufanya hivyo,wewe wawahi…mapema….’akasema
kwa kujiamini.
‘Hapana mimi sitaki kufanya lolote baya…nitamuomba mungu tu
inatosha….’nikasema.
‘Hahaha, toka lini duwa la kuku likampata mwewe, haya omba,
omba usiku na mchana, tuone kama watakuja wakuambia ni sisi tumeua….hahaha,
wewe vipi wewe….pambana nao, wapige kiini macho na wao wataabike…’akasema
‘Hapana…, mama yangu alinipa usia, kuwa..nisipende kulipiza
kisasi, na pili, nisishndane na wenye pesa, kwani wao wameshikilia mpini,…na
…aah, basi mimi sina nguvu tena, ..waache waje waniue na mimi, ni heri tu
niende huko mbeleni, nikakutane na mama yangu..mimi sioni kama kuna umuhimu wa
kuishi tena kwenye hii dunia, nimezaliwa masikini, nimekulia masikini, na…sizani
kama kuna lolote nitafanya linisaidie….’nikasema.
‘Sikiliza wewe, usiwe mjinga,…mimi nitakusaidia kitu,… huyo
mtu aliyenisimulia anasema kuna watu anawahisi na wamekimbilia huku huku dar,
sasa kwa hivi sasa huwezi kufanya kitu huna mbele wala nyuma, hujaweza hata
kuweka mtaji, ili ufanye kitu, unatakiwa uwe na pesa..kuna hata kusafiri, hadi
huko kwetu, unakufahamu huko kwetu…kama unataka nikusaidie mimi…’akaniuliza.
‘Nitakujuaje huko kwenu na mimi ni mara ya kwanza kuonana na
wewe…’nikasema
‘Kwetu ni ufipa, lyamba liya mfipa,..huko ndani ndani,
ukitoka huko kwetu kuja huku, huagi, ..ila mimi sikukulia sana huko,…baada ya
kupatwa na matatizo humu ndani, nilikutana na ndugu yangu mmoja, nikamsimulia
wee, akaniambia hiyo ni kazi ndogo tu…, twende kijijini….haaah, nilipofika huko
nikawekwa sawa, na bado, kazi haijaanza, hawa watu humu watanitafuta…’akasema.
‘Wewe jamani kwanini unataka kufanya hivyo, kwanza huna uhakika kuwa ni wao, umesema ni mashetani, je kama sio wao,..mimi niliona jambo jema ni kuwasamehe tu….’nikasema.
‘Wasamehe tu eeh….haaha….!, unajua walichonifanyia,…wewe unasema
tu, niwasamehe tu, niwasamehe, kwanini wao hawakuliona hilo, wakanionea huruma, mimi nimepatwa na matatizo ndio niwasamehe, unajua sasa hivi sina kizazi….’akasema akishika
tumbo.
‘Kwanini…?’ nikauliza nikionyesha mshangao.
‘Yatakuja kukuta na wewe…haina haja ya kukusimulia…kwasasa
kaza buti, nakuonea huruma sana, lakini vita havina huruma, ama uwe upande
wangu au uwe nao, na ukiwa nao, wewe ni adui yangu, kwaheri….’akasema sasa
akiwa kachukua mzigo wake wa nguo zake.
‘Mimi hata sielewi kitu, hivi sasa akili yangu haipo sawa,
natamani ninywe sumu tu..nimfuate mama yangu, …’ nikasema.
‘Utaelewa tu, dunia itakufunda, ….kama wataka kujiua kajiue…utamkomesha
nani….’akasema akikagua humo ndani, kwa macho, halafu akatema mate chini, na
kusema;
‘Humu, ilikuwa jela yangu, humu niliteseka, humu, nililia,. ….mpaka
machozi ya damu, hakuna aliyenionea huruma, huyo kijana wao, anajifanya ana huruma,
lakini moyoni kama baba yake….sasa tutapambana…na wao…’akaanza kuondoka.
‘Sasa mbona unaondoka…’nikasema nilipoona nabakia peke
yangu.
‘Nitakufundisha kitu, lakini sio leo, …..ngoja niondoke
wasije kunikuta humu ndani…’akasema.
Mara nikakumbuka kitu,…
‘Wewe uliacha kijitabu kidogo hivi…?’ nikauliza
‘Ndio eeh kweli,….nimekitafuta wewe…yaani hicho ndio
kumbukumbu zangu zote, nakiomba tafadhali..humu kuna mambo nilifundishwa huko
kijijini, …sasa ok…nipe nipe…’akasema .
Basi nikampa kijitabu chake, na kwa haraka akachukua mzigo
wa nguo zake na kuondoka, na haikupita muda, mara mama mwenye nyumba akaingia,
akiwa kaiva, kakunja uso, ..sijawahi kumuona akiwa katika sura hiyo kabla,…akashika
kiuoni, ananiangalia machoni…macho yaliyojaa hasira…mkononi kashika mfuko wa
zawadi.
Na kwa nje, nikasikia gari liondoka kuonyesha kuwa baba
mwenye nyumba anaondoka !
**************
NB : Ndio ilikuwa hivyo, je itakuwaje baadae
WAZO LA LEO: Ukitendewa
ubaya, usikimbilie kulipiza kisasi, kwani hujui ni kwanini ikatokea hivyo, mola
wako hajakuacha, na huenda karuhusu huo ubaya ili upate fundisho fulani lenye
heri mbele yake. Muhimu ni kuvuta subira, na kuelekeza maombo yako kwa mungu.
Hakuna jambo lenye herii kama kusameheana. Kusamehe huvuta heri, na kulipiza
kisasi huzaa kisasi kingine.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
story poa, but sad, ...
lini watuma tena
Post a Comment