Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, June 29, 2017

DUWA LA KUKU....3


'Baba kanipa pesa nikakununulie dawa....'akasema na mimi kwa haraka nikauliza.

‘Dawa gani kwani mimi naumwa nini…?’ nikamuuliza yule kijana mwenzangu.

‘Kaniambie dawa za maumivu…kasema leo wakati unafagia ulikuwa kama umechanganyikiwa, ulikuwa unapiga makelele ovyo,…sasa kama hali hiyo itaendelea atarudi kazini aje akupeleka hospitalini, anahisi una malaria, kama yale uliyopimwa wakati ule wakasema malaria yako imependa kichwani…’akasema.

‘Lakini , mimi siumwi, najisikia vibaya tu, kwasababu usiku silali, napata shida sana…’nikasema.

‘Ndio…nakuonaga ukihangaika,…unapiga kelele sana usiku, kwani ukilala, huwezi kuamuka, ukaona kuna kitu gani karibu yako …’akasema.

‘Kuamuka kwa vipi wakati hayo yanatendelea nikiwa usingizini,..yaani ni kama mtu anakuja ananikaba, ananiifanyia mambo mabaya..yaani nashindwa hata kuelewa…’nikasema.

'Anakufanyia mambo mabaya, mambo gani hayo...?' akaniuliza

'Hata siwezi kusema,..mungu mwenyewe anajua...'nikasema.

‘Mhh…pole sana, baba kaondoka akiwa na wasiwasi sana….’akasema.

‘Lakini mimi  …..nina uhakika alitaka kunishika…’nikasema na ndio hapo mama akatokea

'Kukushika, kwa vipi, ..si ndio hivyo alitaka kukushika usikimbie, wewe hujijui tu, ukiachiwa hapo ukiwa kwenye hiyo hali unaweza kukimbia, ukapotea....

'Hapana sio hivyo....hisia zangu zinatuma vingine kabisa...'nikasema

'Unataka kusema nini, ...kuwa baba,...'akakatisha

'Wewe hujui tu,..tuyaache hayo, ila ..kiukweli, sijaota, sijachanganyikiwa, alitaka kunishika kwa..nguvu..au sijui alitaka nini, ila alikuja nyuma yangu wakati nimeinama, akataka kunishika...kwa..kwa nguvu....'nikasema na niliona kijana akitoa macho akiangalia mbele .

Kumbe alimuona mama akiingia,..

Tuendelee na kisa chetu..

*************

‘Nani alitaka kukushika…kwa nguvu,..’mama akasema kwa ukali, mimi nikakaa kimia, sikutaka kusema lolote kuhusu hayo yaliyotokea, huko chumbani kati yangu na baba mwenye nyumba,  kwanza kama kweli alikuwa na nia mbaya, hakufanikiwa, na pili nikisema ninaweza kuleta kutokuelewana kwa wanandoa hao na ikawa mimi ndiye sababu, na hapo inaweza kuwa ndio mwisho wa kazi hapo nyumbani.

'Jitahidi binti yangu, ujue dunia hii ina mitihani mingi, ukipatwa na shida, usikate tamaa, pambana na mikakati yako mpaka ufanikiwe...'nikakumbuka maneno ya mama.

Huyo kijana yeye akatangulia kujibu kwa haraka haraka, kwa kusema;

‘Mama, naona huyu mdada apalekwe hospitalini, usiku anapiga kelele sana, humsikiagi mama, yaani mimi nakosa usingizi, … sijui anaota nini, na leo kapiga kelele kamsumbua sana baba, baba akahangaika kumshika, maana alionekana kama anataka kukimbia…’akasema

‘Oh,…sasa ni hayo malaria yamerudi tena..au kuna tatizo gani, najua pia inachanganyikana na mawazo uliyo nayo,…sasa nikuulize wewe kama unataka kwenda kumuona mama yake, oh...mama yako huwezi kumuona,…’akasema na ghafla akakatisha ni kama lijigundua kuwa kasema neno ambalo hakutakiwa kulisema.

‘Kwanini siwezi kumuona mama yangu…?’ nikauliza nikionyesha mashaka usoni, nikimuangalia moja kwa moja usoni, na yeye akaangalia pembeni na kusema;

‘Kwasababu hali ya huko ni mbaya…kuna njaa sana huko kijijini, watu wanaishia kula mizizi, sasa hebu fikiria kwa ujumla kupo hivyo, je mama yako na ile hali atakuwaje…yeye pale alipo, anahitajia misaada kutoka kwa wasamaria wema,…na …mimi sasa hivi nimetoka kupeleka misaada ya chakula , nimeagiza kwenye mabasi, lakini kikifika huko ni cha kugombea maana wengi wana hali mbaya..unanielewa..’akasema.

‘Oh, kumbe, ulimpelekea mama yangu chakula…oh ahsante sana mungu, ahsante sana mama, umemfaa sana mama yangu, mungu atakulipa zaidi….kwahiyo ulipata nafasi ya kuongea na mama?’ nikamuuliza, sas anikionyesha furaha.

‘Nilishakuambia mimi namjali sana mama yako, muhimu utulie, ufanye kazi, kilichokuleta hapa ni kazi, na kazi ndio itamfanya mama yako …awe….asiwe na shida,… na mwisho wa mwezi huu nitamtumia pesa, nitakata kiasi kwenye mshahara wako, na mimi nitaongezea za kwangu kidogo, sawa…’akasema.

‘Sawa mama za kwangu mtumie zote tu….’nikasema

‘Usijali, naona sasa umepona…’akasema, akimuangalia kijana wake, na kijana wake naye akawa anatabasamu aliponiona nipo na furaha.

Kijana wake alionekana mwenye huruma sana, na unaweza kusema labda ndio huko kunipenda, japokuwa mimi sikuwa na uelewa huo, ….hata hivyo mimi sikumuamini, yeye na baba yake niliwaona kama wana tabia zinazofanana, hata hivyo sikuwa na mashaka na wao, zaidi ya kujitahidi kuwa mbali na wao.

‘Haya kafanye kazi,…au bado unajisikia vibaya,…kama unajisikia vibaya kapumzike  nitamalizia mwenyewe kazi zilizobakia,…usijali kuhusu huko kijijini,  nitajitahidi kadri niwezavyo kuwasaidia…’akasema huyo mama.

Kauli hiyo ilinifanya niingiwe na faraja kidogo, lakini moyoni nilihisi kama kuna jambo, kuna kitu , sijui kwanini nafsi yangu ilikuwa inanituma  hivyo, kiukweli mimi nilimpenda sana mama yangu, wakati mwingine najuta kwanini niliamua kuja huku, na kuwa mbali na mama yangu, lakininingelifanyaje..niliona kuja huku kutafungua sura mpya ya maisha yetu,..huenda ningelijaliwa niweze hata kumchukua mama yangu…ndio ilikuwa ndoto zangu hizo.

Siku hiyo ikapita hivyo…japokuwa usiku nilisikia mama na baba wakizozana kuhusu jambo, nahisi walikuwa hawaelewani, nikasikia mama akisema;

‘Na siki nikigundua kuwa ni kweli,…itakuwa mwisho wa ndoa yetu,..nakuambia hilo, yule binti wa kwanza ulijitetea, nikakusamehe, lakini huyi, hivi wewe una nini, binti wa watu masikini, hana mbele wala nyuma, ni nini umekikosa kwangu,…’

 Kauli hiyo ilinifanya nijua wananizungumzia, mimi, nikataka kutega sikio, lakini mara akatokea kijana wao, na yeye yaonekana alisikia, huo mzozani, kwani usoni alionekana hana raha..kiukweli, sikupenda kuingilia mambo yao. Na hilililitokea kwa bahati mbaya..

‘Kuna nini..?’ nikamuuliza

‘Hayakuhusu, hayo ni mambo ya wakubwa,…’akasema akinipita kuelekea nje.

Niliamua kumfuata huko nje…, kwani nilikuwa na maswali mengi ya kumuuliza, kuna mambo mengi yalikuwa yakiendelea kichwani mwangu.

‘Eti samahani, nikuulize kitu….’nikasema

‘Uniulize nini, kama ni maswala ya baba na mama, usiniulize….’akasema

‘Hapana, nauliza hivi, …hapa nyumbani, …kulikuwa na mfanyakazi wa ndani kama mimi….?’ nikamuuliza.

‘Kwanini unauliza hivyo, umesikiliza maneno ya wakubwa au..? ni tabia gani hiyo mbaya…’akasema kwa hasira, kwa mara ya kwanza nilimuona akinikunjia uso.

‘Nauliza tu, maana ndani ninapolala, nimekuta nguo nyingi ndani, niliwahi kumuuliza mama, akasema zilikuwa za mfanyakazi aliyepita…’nikasema.

‘Sasa kama unajua hilo, kwanini unaniuliza tena…’akasema akionyesha kukerwa, nikajua ni hayo yanayoendelea kati ya wazazi wake, niliona ajabu sana, watu hawa wana maisha mazuri, kwanini wasiwe na furaha, kwanini inaonekana kama wana msigashano fulani…hiyo sio mara ya kwanza kusikia wakizozana.

Naona huna raha, unajua wewe ni rafiki yangu, na nikikwazika najua wewe ndiye wa kunisaidia, sasa kama nakuuliza swali unakuwa mkali, basi, ngoja niondoke tu…’nikasema na yeye hapo akabadilika na kusema;

‘Haya uliza, unajua kun akitu kinanisumbua, nilitaka kuongea na mama, au baba, sasa naona hawapo vizuri,..aah, tuyaache hayo, ..niuliza, usijali…’akasema.

‘Nataka kukuuliza kuhusu huyo mfanyakazi,  aliondokaje hapa…?’

‘Aliamua tu mwenyewe, …’akasema sasa akiwa katulia, na mimi nikaona huo ndio wakati wakumdadisi mambo ninayoyaona humo nyumbani, sikupenda kumuuliza lakini kwa jinsi yanavyozidi nikaona kuna umuhimu kuyajua.

‘Mhh, hata sielewi…nahisi hakuondoka kwa kupenda, …’nikasema.

‘Ni uamuzi wa mtu, hata wewe ukijiskia kuondoka si unaondoka tu, hujalazimishwa, au sio, ..mimi ndivyo nijuavyo hivyo…’akasema.

‘Ndani kule chumbani, niliona kijitabu hiki  kidogo,…nahisi kilikuwa cha huyo msichana, na alipenda kuandika andika mambo, kuna sehemu nimesoma mpaka nahisi huenda kuna tatizo kwenye hii nyumba, nahisi …maana hata mimi sijielewi…’nikasema.

‘Aliandika nini…?’ akaniuliza akionyesha kushtuka.

‘Humu ndani kuna mashetani……’nikasema

‘Weee, nani kasema hayo, hakuna mashetani humu ndani…’akasema.

‘Ndivyo alivyoandia yeye…’akasema

‘Huyo muongo, alimzulia sana baba, na hata mimi, …unaona kumbe aliandika kuwa humu kuna mashetani, ole wake, …baba na mama wangelijua hilo, …’akasema

‘Lakini kwanini hata mimi sipati usingizi usiku,..kuna mambo yanitokea, ndio maana nahisi huenda nay eye yalimtokea hivyo hivyo…’nikasema

‘Wewe si malaria tu.. .sikiliza hayo aliyoandika ni uwongo, kama yapo mashetani mbona mimi hayajanigusa au wazazi, huoni kuna uwongo hapo…’akasema

‘Labda yapo kwa ajili ya wageni tu…’nikasema

‘Kwahiyo unaamini hayo maneno?' akaniuliza.

‘Sijasema nimeamini…ila nakuuliza maana yeye kaandika kuwa ikifika usiku akiwa amelala huwa anashikwa na majinamizi, yanamkaba, na sio kumkaba tu, yanafikia kumdhalilisha…’akasema na kijana akabakia kimia kama anawaza jambo.

‘Mbona hakusema…alikuwa analalamika tu, na kudhalilishwa kwa vipi, ni muongo huyo….’akasema

‘Kaandika kuwa aliwahi kumuuliza mama, mama akamfokea, na kumuambia anazusha mambo , na akiendelea na tabia hiyo atafukuzwa kazi,...na siku kadhaa akamuuliza baba, baba akasema hivyo hivyo,..ila baba alisema atafuatilia kuona kama maneno yake ni ya ukweli, mkamuita mtu wa dini, kweli si kweli…?’ akauliza

‘Kwanini aliandika hayo, ….hebu nipe hicho kijitabu….’akasema

‘Hapana siwezi kukupa hiki kitabu sio chako, nitamtafuta huyo msichana nimpe kijitabu chake..ila kwasasa nataka nikisome chote nikimalize…..’nikasema

‘Ole wako baba au mama wakiyasikia hayo maneno..., maana sisi hatuamini hayo mambo ya mashetani….’akasema

‘Hamuamini ndio , kwa vile nyie hayawasumbui….mimi usiku nalala kwa shida sana,..kama mama angelikuwepo, najua angelisaidia, lakini hapa nitamuambia nani anielewe….lakini kiukweli humu ndani kuna matatizo…’nikasema.

‘Huyo aliyeandika humo ni muongo…nimini mimi, alikuwa na yake , huenda alikuwa na mashetani yake, ndio yakawa yanamsumbua...kwanini huyo mtu wa dini alipokuja kuomba hakukuwa na tatizo lolote...’akasema,

'Hamna shida, mimi nilikuuliza tu....'nikasema

'Sasa kama wewe huamini ninayokuambia, basi itabidi yafike kwa baba na mama, na wakigundua kuwa una hicho kitabu kilichoandikwa uwongo, sijui kama watakuelewa, watakuona wewe ni mfitinishaji, watakufukuza..bora unipe hicho kitabu tukiharibu,….’akasema.

'Hapana hiki kitabu kitarejea kwa mwenyewe..'nikasema

'Utampata wapi..?' akauliza

'Atakuja kuchukua vitu vyake...'nikasema

'Mliongea naye...?' akaniuliza

'Nilisikia akiongea na mama, kwenye simu, akasema atakuja, ndio mama akaniambia vivipange vitu vyake vizuri, akija asikae humu ndani muda mrefu...'nikasema

'Sitaki hata kumuona....'akasema

'Kwanini...?' nikauliza

'Sio mkweli, muongo, mfitinishaji,..alitaka kuvuruga ndoa ya wazazi wangu...mtu anayewafany wazazi wangu wasiwe na raha, ni adui yangu...'akasema na mimi nikamuoangalia kwa jicho la pembeni, nilitaka kumuambia jambo, lakini nikasikia nikiitwa ndani.


********

Siku moja wakati nafanya usafi chumbani kwa mabosi wangu hawa, baba alikuwa hayupo, kurudi kwake najua ni usiku,.. halikadhalika mama naye alikuwa hayupo yeye, hurudi saa kumi jioni,  na kijana wao, alikuwa kaenda chuo , huwa anasoma chuo cha ufundi, lakini anawahi kurudi, kama kwenye saa nane hivi…, 

Basi mimi nikawa nafagia ndani kwenye chumba cha waheshimiwa hao, nikiwa huru kabisa, nipo peke yangu, nafanya kazi kwa nafasi,..najua nina muda, nikimaliza kufagia napanga panga vitu…baadae naenda kuosha vyombo.

Kawaida muda kama huo nina uhuru, nipo peke yangu, na wafanyakazi hawawezi kuingi ndani, huwa muda kama huo wafanyakazi, hawaruhusiwi kuingia ndani, mpaka nimalize usafi, kama wana jambo muhimu la kufuatilia ndani, inabidi wasubirie....ni amri waliyopewa na wenye nyumba,  na kwa vile kulikuwa na joto, nikawa nimejifunga khanga moja tu..,

Mara wakati nainua kitabu, kuvuta mavumbi, kukadondoka karatasi, ilikuwa ni barua,…sina kawaida ya kupekua vitu vya watu…, huwa navipanga kama vilivyo, ila sijui ilikuwaje, wakati nataka kuirudisha hiyo barua, ikadondoka tena chini, na sasa ikafunguka,..Sijawahi kusoma vitu vya watu humo ndani,…mungu mwenyewe anajua ni kwanini, ila ile barua ilipofunguka, nikaona neno kijijini, moyo ukanilipuka, paah,…nikaacha kupanga vitu, na kuanza kuisoma hiyo barua, mungu nisamehe tu, kwa kosa hilo.

Kumbe barua hiyo ilikuwa inatokea kijijini kwetu, kutoka kwa rafiki na jamaa ambaye ndio mama mwenye nyumba humtumia, kwa mawasiliano na huko kijijini. Mara nyingi wanawasaliana kwa simu, lakini nilishangaa kuwa kumbe wanaandikiana na barua.

‘Shoga, nimeona nikuandikie barua, ili iwe kumbukumbu kwak, huku kijijini hali ni mbaya sana, njaa, hali ngumu za kiuchumi, na zaidi, hivi sasa kumezuka tabia ya watu kuiba, na kufanya mauji, sijui dunia hii imekuwaje.

Hutaamini, kuwa watu hawa hawajali wanyemfanyia hivyo ni nani, najua ni kutokana na hali ngumu za maisha,…kama nilivyokupigia simu, tukio lile la moto, kumbe lilitokana na kile chakula ulichomuachia yule mama masikini..inasikitisha sana.

Vijana hao majambazi, sijui walijuaje kuwa umemuachia huyo mama chakula, na pesa, walimvamia usiku, na aheri wangeliiba tu hicho chakula, na pesa, kwani  hawakuishia hapo wakachoma na hicho kibanda cha huyo mama, na kuteketeza kila kitu.

Mama wa watu hakuweza kuokolewa, aliungua vibaya sana, na alipofikishwa hopitalini akafariki dunia,..na kutokana na hali aliyokuwa nayo, hakucheleweshwa kuzikwa, inasikitsha sana…  sasa sijui mtamu….
Binti hakuweza kumalizia kusoma hiyo barua akadondoka chini na kupoteza fahamu.

Siku hiyo baba mwenye nyumba aliwahi kurudi nyumbani, akiwa na furaha zake anapiga mrudi, akapiga hodi, akaona kimia.

‘Hawa watu wamehama…’akasema na kwanza akaingia chumba anacholala huyo binti, akijua labda huyo binti kajipumzisha, hakupiga hodi, akafungua mlango, huyo binti alikuwa hayupo chumbani, akaweka zawadi fulani juu ya kitanda cha huyo binti, halafu kwa haraka akaelekea chumbani kwake.

Alipofika chumbani kwake, akakuta mlango upo wazi, akajua labda ni mkewe naye karudi kwa dharura, hapo akili ikamcheza, kwa haraka akageuka na kurudi kule chumba cha huyo mfanyakazi , nia ni kuichukua ile zawadi, isije ikaleta matatizo, lakini sasa alipofika kule chumbani akakuta ile zawadi haipo.

‘Huyu binti kaingia huku saa ngapi….’akasema hakutaka kuita, akijua mkewe atasikia, basi akageuka na kurudi kule chumbani kwake, ili akaongee na mkewe, huenda naye karudi hajisikii vyema.

Alipofungua mlango, anashangaa, mtu kalala chini, ni yule binti, akiwa ka khanga moja,..na alivyolala,..sehemu kubwa na mapaja yapo wazi…kwanza ibilisi akamteka jamaa, lakini moyoni akahisi huyo binti hayupo sawa….

Kwanza ikabidi amkague huyo binti kwa kugusa mapigo ya moyo, kama kuna uhai,…na alipoona kuna uhai, akaona ni vyema akaribu huduma ya kwanza, anayoifahamu yeye, …akamgeuka na kumlaza chali, akaweka mikono kifuani, kuminya taratibu, anajua mambo hayo…binti hakuamuka.

‘Oh,…sasa hili ni tatizo….’akasema.

‘Ngoja nifanye huduma nyingine, akasema, sasa akachuchumaa, nia ni kupanua mdomo wa huyo binti na kufanya huduma ya mdomoni, hapo, sasa….

Ile anainama, na kushusha mdomo wake kukutanisha na mdomo wa huyo binti,  mlango wa chumbani kwake, ukafunguliwa, mama mwenye nyumba huyo akaingia…., jamaa akajikuta kanasa, kuinuka hawezi kuendeela na huduma hiyo hawezi, na binti alivyovaa , khanga moja, na sehemu kubwa ya mwili ipo wazi.

Mama mwenye nyumba akabakia mlangoni haamini anachokiona jicho limemtoka, na alichosema baada ya muda kidogo;

‘Kumbe ni kweli…..’ilikuwa kauli ya mama.

‘Huyu binti nimemkuta kazimia,..ndio nataka kumpatia huduma ya kwanza…’akasema.

‘Kazimia, humu chumbani kwangu, na …akiwa hivyo, uchi…..hahaha, sikuelewi….’mama akawa kama anacheka na kwa muda huo, huyo binti akawa kazindukana,…

‘Nilipozindukana, niliona nipo chumbani kwa watu, nikakumbuka nilivyokuwa nimevaa, na juu yangu yupo baba mwenye nyumba, kaniinamia… akili za kwanza zikanituma vibaya, nikajua huyu baba anataka kunifanyia kitu kibaya, nikakurupuka, na kuanza kupiga ukelele, nikisema;

‘Sitaki, sitaki…..’ na waki nakurupuka, nakimbilia nje,..ndio  nikakutana na mama mwenye nyumba kasimama mlangoni,… uso, kwa uso…na hilo jicho nililoangaliwa nikajua sasa kumeharibika, hata hivyo sikusimama, mbio mbio, nikakimbilia nje…na wazo langu la haraka ni kuondoka kabisa kwenye hiyo nyumba.

NB: Kisa hicho kinaanza kasi yake.


WAZO LA LEO: Ikitokea jambo baya, mfano kwenye mahusiano, au tukio baya katika jamii, …Kwanza tusikimbilie kuchukua hatua,..kulaumu, au kuhukumu, kwa kuhitimisha na kuhalalisha ubaya huo. Kwanza ni vyema kufanya uchunguzi kutegemeana na ukubwa wa jambo lenyewe, na kuona sababu za jambo hilo, huenda jambo hilo limetokea kwa bahati mbaya tu, au kuna sababu za msingi za kutokea jambo hilo. 

Wengi wetu , tunapenda kuchukulia mambo kwa pupa na hasira, na matokea yake, ndoa huyumba, au hata kuharibika, au mahusiano kati ya mtu na mtu au jamii, huja kuvurugika, na baya zaidi wengine hukataa hata kukaa mezani kuyaongelea matatizo hayo,  au kutafuta ni kwanini… Tukumbuke kuwa kila jambo hutokea kwasababu fulani, nahiyo sababu inaweza ikawa ni fundiasho kwetu, basi tulitafute hilo jambo kwa hekima ili tufundishike.
Ni mimi: emu-three

No comments :