Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, June 28, 2017

DUWA LA KUKU....2


Kiukweli njiani kilichonifanya nimsahau mama yangu kwa muda ni kule kuona vitu vya kunishangaza, nilizoea maisha ya kijijini, ngedere, tumbili, ngombe na watu, sikuzoea kukutana na magari,  na nyumba za kisasa, ilikuwa mimi na watu, kunyanyapaliwa ndio ilikuwa maisha yangu mimi na mama yangu,…sasa naelekea mjini, kwangu mimi kila kitu nilichokiona ilikuwa ni kushangaa tu, mpaka nafika mjini,….sasa nikaingia kwenye jumba. Kwangu ilikuwa ni jumba.

‘Nililiona kama jumba ya mfalme, mnaingia kwenye geti mnakutana na walinzi, walinzi wanamnyenyekea bosi wao, na mimi nakajihisi ni miongoni mwa ..hahaha familia hiyo, lakini kwa mbali nikamuona yule mlinzi akiniangalia kwa jicho la dharau.

‘Hapa ni kama ulaya…’nikajikuta nakijisemea hivyo…huku nikizungusha macho huku na kule kuona mandhari ya nyumba.

Hayo ya kushangaa yalikuwa ni mengi sana.., na siku baada ya siku nikaanza kuzoea, kwani pia pamoja na ushamba wangu, nilikuwa mwepesi sana wa kujifunza na kuelewa mambo, na nilijitahidi sana kutekeleza kila nilichoelekezwa, na kwa tabia hiyo, wenyeji wangu wakanipenda sana.

Pale nyumba walikuwa wakiishi baba na mama, na alikuwepo kijana wao wakiume, kuachilia mbali wafanyakazi,..nilikuja kufahamu kuwa familia hiyo ilikuwa na watoto wengine lakini wao walikuwa nje ya nchi, wakisoma, kwahiyo muda mwingi nilikuwa na huyo kijana wa umri wangu…, lakini yeye alikuwa ni mwanaume.

Alianza kunizoe kwa vile muda mwingi alikuwepo hapo nyumbani, na yeye ndiye alikuwa karibu kwa kunielekeza na kunifundisha kile nisichokijua, kwahiyo akawa ni mtu wangu wa karibu, japokuwa nilikumbuka usia wa mama.

‘Usipende kuwa karibu na wanaume, hawa watu wakiingiwa na hamasa, wakatawalia na matamanio yao ya nafsi huwa hawajali huyu ni nani, jichunge sana binti yangu…,na kaa mbali na  na wanaume…’mama aliniambia hivyo. Kwahiyo japokuwa kijana huyu alikuwa akinisaidia bado nilikuwa najaribu kuwa mbali na yeye kwa kadri nilivyoweza, mpaka yeye akaligundua hilo.

‘Mbona nakuona kama unaniogopa…?’ akaniuliza.

‘Ni kawaida ..sio kwamba nakuogopa natimiza wajibu wangu kama mwanamke..’nikamwambia hivyo.

‘Usiwe mshamba wewe…huoni nakusaidia ili ujue mambo mengi, ..ukiniogopa mimi, hutajua mambo mengi ambayo hujawahi kuyaona, au kuyasikia…’akaniambia.

‘Oh,…muda ukifika nitayaona na kujifunza kama ni ya lazima kujifunza…’nikasema na kuondoka.

Lakini sikuwa na raha, maana nilianza kufululiza ndoto mbaya mbaya, na nyingi zilimlenga mama yangu,...ikawa hainipi raha, nikamuomba mama mwenye nyumba ajaribu kutafuta mawasiliano ya huko, yeye akasema;

'Usiwe na wasiwasi, tulimuachia chakula cha kutosha, yeye peke yake kinaweza hata kumaliza mwezi...'akasema

'Lakini alikuwa anaumwa...'nikasema

'Kwahiyo unataka kwenda kumtibia...?' akaniuliza

'Aaah, nataka kujua hali yake tu....'akasema

'Nitatafuta mawasiliano ya huko,..nitakuambia...'akasema

Hakuniambia kitu wiki, mwezi..nikamuulizia tena, na sasa akawa mkali, hataki kulizungumzia hilo, mpaka nikawa na mashaka, kuna nini, kwanini nikimuulizia maswala ya mama yangu yeye anakuwa mkali sana,..

 Siku zikawa zinakwenda, na kwa vile mimi nilitokea sehemu ya umasikini, na sasa nimeingia seheme ya matajiri, mwili wangu ulianza kubadilika, kunawiri, na ule uzuri wa usiichana wangu ukaanza kuonekana, na hata wenyeji wangu wakaanza kunitania;

‘Kumbe maskini na yeye mnzuri….’ Alisema baba mwenye nyumba na mama mwenye nyumba akacheka...lakini akaniangalia kwa jicho lenye ujumbe fulani, kwani baba alipoondoka, aliniita pembeni akasema;

'Unasikia,...usijione umependeza ukakiuka mikataba yetu, hapa umekuja kufanya kazi, jichunge sana, wanaume watakuhadaa, ukiharibikiwa ujue ndio tiketi yako ya kurudi huko kwenu na sijui utakwenda kuishi nani huko...'

'Nitakwenda kuishi na nani....'nilijiuliza hivyo, sikumuelewa huyo mama ana maana gani, kauli hiyo ilinizidisha mawazo, lakini sikuwa na la kufanya, aliyekuwa karibu wa kumuuliza ni kijana wao, na nilipomuuliza akasema;

'Mimi sijui,...mama ndiye anawasiliana na watu wa huko, ningelijua namba za huko tungeliwapigia,...ngoja nitamuomba mama namba za huko utaongea nao...'akasema

Siki ya pili yake nikamuuliza kama kaipta hiyo namba, akasema 

'Mama kasema haipatikani, ...tuachane na hilo swala...'akasema

'Mimi nahisi kuna jambo wananificha...'nikasema

'Hakuna, kwani wewe una wasiwasi gani, hapa unaishi vyema, unakula unashiba, una wasiwasi gani...'akasema

'Mama yangu nampenda sana,..yeye ndiye tegemeo langu, sitaki nimkose,..kaniagiza nifanye kazi nimsaidia, tupate dawa, sasa ...siwezi nikawa na raha, kama sijui anaendeleaje..'nikasema

'Sasa amua moja, urudi huko kwenu au uendelee kufanya kazi.....'akasema

'Sawa ..nitafanyaje , mimi binti masikini nina nini tena,..ndivyo tulivyojaliwa tuwe hivyo, lakini naumia sana...'nikasema.

Huko kijijini walizoea kuniita jina hilo ‘masikini,..’ kwahiyo likawa limezoeleka, hivyo sikukasirika, nilijionea sawa tu, maana ni kweli hali yetu ilikuwa hivyo!

**************
'Masikini mbona upo hivyo...'nilishtuka sauti ya kiume, alikuwa ni baba mwenye nyumba.

'Hapana baba , hakuna kitu...'nikasema na kwa haraka nikakurupuka kwenda kuendelea na shughuli zangu.

Baba mwenye nyumba alikuwa mara nyingi hashindi hapo nyumbani anarudi usiku labda siku za wikiendi ndio tunakuwa naye, na sikuzoeana naye sana, na hakuwa muongeaji, zaidi ya kunituma kile cha ulazima, kama mkewe hayupo vinginevyo, hakuzoea kunituma zaidi ya kupitia kwa mkewe au kijana wake.

Muda ukapita nikaanza kuona mabadiliko fulani…., hasa kwa huyu kijana,…kwasababu nilikuwa naye muda wote, hata kwa baba mwenye nyumba, lakini kwa vile alikuwa anaonekana mara moja au mbili kwa wiki, sikuweza kumjali sana, tatizo ilikuwa kwa huyu kijana.

Huyu kijana … nikaona ananiangalia kwa jicho lisilo kuwa la kawaida, na kuna muda nilimfuma akinichungulia, nikiwa labda chumbani kwangu, au hata nikioga, ananichungulia kwenye tundu za milango.

‘Wewe vipi mbona umekuwa hivi siku hizi,,,,?’ nikamuuliza.

‘Hahaha, wewe hujioni, umekuwa mnzuri, nashindwa kuvumilia….’akaniambia.

‘Acha ujinga huo, wewe ni ndugu yangu…hujasikia mama akituambia, sisi ni ndugu, tuheshimiane kama ndugu….’nikasema.

‘Hahaha mimi ndugu yako mimi, acha ushamba huo…hayo ni mambo ya kizamani, mama hawezi kusema tusipendane, mimi na wewe tunaweza kuwa wapenzi bila ya mama kujua, unajua mimi nakupenda sana…’akasema

'Eti nini..unanipenda umejifunzia wapi hayo mambo ya kikubwa, ...'nikasema

'Hahaha, eti ya kikubwa, kwani wakubwa walianzia wapi...'akasema

'Sikiliza mimi siyataki hayo maneno yako, siyapendi, kama unataka tukosane endelea na hayo mambo yako...'nikasema.

'Utajifunza tu, usijali...'akasema , uzuri wake, huyu kijana alikuwa hakasiriki, anaweza ukakuuzii , ukamsema vibaya, yeye anatabasamu tu,...lakini kwa mabadiliko hayo, nikaanza kumuogopa zaidi, nikikumbuka usia wa mama.

 Huyu kijana hakuacha kunisumbua, kuna wakati mwingine antaka nione anavyoangalia kwenye simu yake au laptop yake, nikiangalia na kuta kaweka mapicha mabaya, basi, mimi huondoka hapo yeye anaishi kunicheka na kuniita mimi ni mshamba,…na ikafikia muda akawa sasa hafichi dhamira yake, alisema ananitaka, na atajitahidi mpaka anipate.

‘Unanitaka nini,...nimeshakuambia, mimi itaki upuuzi, huo na ukiendelea hivyo sasa nitamuambia mama yako…’nikasema.

‘Ukimuambia mama yangu, nimjuavyo, basi ujiandae kurudi kwenu, mimi na wazazi wangu tunapendana sana, na lolote nikisema wataniamini, je wewe watakuamini zaidi yangu….’akasema.

‘Hata kama …ila mimi nimeshakuambua mimi sitaki huo ujinga wako…’nikasema.

‘Utautaka tu, upende usipende…’akasema na sikumuelewa ana maana gani.

'Unataka kunifanya nini..?' nikamuuliza na yeye akacheka tu, na kusema;

'Wewe mshamba,..mimi mtoto wa mjini, najua jinsi gani ya kukupata...'akasema.

Basi nikaogopa, sikutaka kumtishia hivyo tena, ila nikajitahidi kuwa mbali na huyo kijana lakini huyo kijana hakuwa na raha bila ya kuja karibu yangu maana alishazoea kuwa name karibu kama mwalimu wangu.

************

Ilikuwa siku ya wikiendi, nilibakia na baba mwenye nyumba, nikafanya usafi sehemu zote, lakini sikuweza kufanya usafi ndani kwa wenye nyumba, kwa vile baba mwenye nyumba yupo, na akiwepo mama huwa anafanya usafi peke yake huko chumbani kwao..., lakini leo mama alikuwa hayupo, …na kijana alikuwa katoka.

Nikawa nimemaliza kazi ya usafi, na sasa nataka kwenda kuosha vyombo, mara nikasikia baba mwenye nyumba akiniita,…cha ajabu alikuwa akiniitia chumbani, nikashangaa sio kawaida yake.

'Binti masikini....'akaniita, nikaitika...

‘Mbona huku chumbani hujafika kufanya usafi…’akasema.

'Mama hayupo...'nikasema

'Ina maana mpaka mama awepo ndio unaingia kufanya usafi huku ndani...'akasema

'Nilikuwa nasubiria utoke...nisikusumbue umelalala...'nikasema.

'Wewe ingia ufanye usafi...' akasema.

 Nikawa najiuliza nitaingiaje kufanya usafi huko ndani, na wakati baba mwenye nyumba yupo, na aliposisitiza hivyo, na kwa vile nilimuona yeye kama baba yangu, nikatii amri,  nikaingia ndani, ….

Mungu wangu nilimkuta kavaa taulo tu kifua nje..na kakaa kitandani, sijawahi kumuona mwanaume katika hiyo hali, niliona kama nimemuona akiwa uchi...,..nikataka kutoka nje nihisi nimeingia kabla hajavaa shati, labda...akasema.

‘Fanya usafi, usijali, …kipi kigeni kwako hapa….’akasema yeye akiwa anaangalia lapotop yake aliyokuwa kaiweka, mapajani.

Nikaanza kufanya kazi kwa haraka haraka sio kama ile inavyotakiwa ilimradi nitoke humo ndani, sijui ilikuwaje, nilikuwa nimeinama nakusanya uchafu, mara nikahisi mtu ananikamata, kwa nyuma, yaani ilitokea haraka.

Nilipiga ukelele, unajua kupiga ukelele,..nahisi ulikwenda mbali sana, na huo ukelele ukamfanya jamaa aniachie kwa haraka,...na alipjaribu kunishia tena, kwa kuniziba mdomo...nikapiga tena ukelele na kwa haraka nikamtoka na kuanza kukimbilia nje....mbio,…mbio…

Wakati natoka mbio…, nakutana na yule kijana akiwa katokea dukani, akaniangalia kwa macho ya kujiuliza, maana nilikuwa nahema, ninatetemeka kwa uwoga.

‘Vipi wewe umeanza mashetani yako…’akasema.

‘Baba..baba…’nikawa nasema hivyo tu..na yeye, kwa haraka akakimbilia ndani akijua labda kuna kitu kibaya kimetokea kwa baba yake, baadae akarudi na kusema;

‘Mbona baba kalala kitandani..tena fofo, yaonekana alikuwa kalala muda mrefu, mimi nahisi ni hayo majinamizi yako unayoota kila siku..?’ akasema, lakini sikusema kitu tena zaidi ya hapo, ila nina imani, mtu alinishika kwa nyuma, tena akiwa uchi…sizani kama nilichanganyikiwa,..labda, lakini..hapana…alinishika, mimi sijachanganyikiwa.

‘Hapana…sijaota ni kweli…’nikasema.

'Ni kweli kwa vipi, kwani ilikuwaje,...?' akaniuliza, lakini sikumuambia kitu, nikabakia kimia tu.

‘Unajua wewe una tabia ya kuota na kupiga makelele, hasa usiku na hata mchana ukilala unakuwaga hivyo, sikujua kuwa hata ukiwa macho unapandwa na maruhani yako …’akasema.

Ni kweli nimekuwa na tabia hiyo, huwa naota sana, na  kuna siku niliota ndoto mabaya sana haijawahi kutokea,……sitaweza kuisahau…

*************

Mama alikuwa kanituma dawa, yeye alikuwa kalala ndani, anaumwa hajiwezi, na tuliomba omba tukapata vijisent vya kununulia dawa..., mama akanipa pesa, na mimi nikakimbilia dukani kumnunula hizo dawa,..

'Usichelewe mwanangu maana ukichelewa hutanikuta...'akasema hivyo.

'Mama sichelewi, kwanini nisikukute utakwenda wapi, wakati unaumwa....'nikasema

'Haya,..hujui mungu kapanga nini, nenda haraka, ....'akasema na mimi nikatoka kwa haraka nikakimbilia duka la dawa, lilikuwa mbali  kidogo, nikanunua, na  wakati narudi, nakaribia nyumbani, niona mosho umetanda juu, kama kuna kitu kinaungua, na hapo nikasema;

'Mungu wangu huo moto sio nyumba imeungua, isije ikatokea kwetu..'nikasema na kuongeza mwendao, na nilipokaribia nyumbani kwetu, ndio naona moto, unatokea kwenye nyumba yetu,..moto umewaka, nakwa muda huo unatokea  dirishani na mlangoni..unaanza kushika na paa...

'Mungu wangu ni mkosi gani huu...'nikasema nikikimbilia kutaka kujaribu kuzima, ..kitu ambacho hakiwezekani, moto ulishashika hatamu..

 Nikaanza kupiga kelele,..

'Mama, mamaaa, toka nje nyumba inaungua..'

 Lakini mama hakutoka, moto ulikuwa mkali kweli kweli…, na pale mlangoni ukawa ni makali kupitliza, mtu huwezi kupita, kuingia ndani….na sikuwa na njia ya kuingia ndani , ili niweze kumsaidia mama, na mama hali yake sio nzuri.

 Nikawapigia majirani makelele ya kuomba msaada, … ili waje kusaidia kuzima moto lakini hakuna hata mmoja aliyejitokeza , ni kama vile tulikuwa tunaishie peke yetu.

'Oh, mama yangu jamani,…’nikawa nalia, na sasa nikawa najaribu njia yoyote ili niweze kuuzima ule moto, nikaokota ndoo mbovu mbovu,  nikajaribu kutafuta maji, lakini hakukuwa na maji yoyote karibuni, maeneo ya kwetu maji ni shida, tunayafuatilia mbali sana, ..sikuweza kupata maji hata yale machafu, ...

 Moto sasa ulikuwa umezingira nyumba nzima, hakuna anayeweza kufanya lolote…na kwa maana hiyo mama atakuwa kaungua, na sizani kama angeliweza kupona kwa jinis moto ulivyo mkali.

  Kwa bahatio upande mmoja wa nyuma, nikaona sehemu hakujashika moto, naweza kupenya, nikajaribu kupaendea, japokuwa ni joto kweli, nilipokaribia tu, nikahisi mtu ananishika kwa nyuma,..kama kunizuia nisiende,…

'Niache niache nikamuokoe mama yangu...'nikasema lakini huyo mtu akawa haniachii.

 Nikawa nasumbuana naye, aniachie lakini hakuniachia, na alivyonishika, ni kama ananikaba, nikawa najiuliza iweje badala ya kunisaidia, kuuzima moto yeye  ananikaba, anataka nini huyu anataka mama yangu ateketekee na moto…

 Sasa ikawa napambana na huyu mtu, huku moto unazidi kuwaka, nyumba sasa inazidi kuteketea!

'Mama yangu jamani…’nikasema na huyu mtu akawa anaendelea kunikaba, na ..hata sijui alikuwa akinifanya nini…ila nilichohisi ni maumivu makali chini ya kitomvu,makali kama mtu aliyechomwa na kisu, hapo nguvu zikaniishia, sikuweza kupambana tena na huyo mtu, nikahisi kupoteza fahamu.

Mara…...

'Wewe vipi, mbona leo umelala kama gogo..’ ilikuwa sauti ya mama mwenye nyumba na mimi nikakurupuka kwa haraka kutoka kitandani, lakini mwili haukuwa na nguvu..

‘Nahisi vibaya mama,…’nikasema.

‘Wewe siku hizi umeanza uvivu, kila siku ukiamuka asubuhi hujisiki vizuri, una nini wewe..?’akaniuliza akiniangalia kwa mashaka.

‘Hata sijui mama, nimeota ndoto mbaya..mama yangu sijui …’nikasema na huyo mama akatulia kidogo halafu akasema;

‘Mama yako,…anakutegemea wewe ufanye kazi upate pesa umtumie, lakini kwa mtindo huu, sijui kamaa utaweza kufanya hivyo…’akasema.

‘Kwanini mama, najitahid, ila usiku inakuwa nishida kwangu,..naota ndoto mbaya,…sijui …nahisi mama hayupo sawa…’nikasema.

‘Kama hayupo sawa utafanya nini…bila ya kuwa na pesa, au unataka nikurudishe huko kwenu kijijini…’akasema.

‘Mama hapana…ila nataka kujua hali zao tu, sijawahi kuongea na mama yangu, tangia nije huku sasa sijui …oh, mama yangu jamani, sijui yupoje…’nikasema nikihis kulia.

‘Hebu amka kule, ukafanye usafi…’akasema huyo mama, na mimi nikajikakamua kuamuka, lakini mwili wote haukuwa na nguvu, nikawa nahisi joto la homa,…na nikahisi maumivu makali tumboni  mara...nasikia kama kutapika,…

'Nini hii tena jamani…’nikasema na kuhisi kichwa kikiniuma kweli kweli…tumbo, kichwa, na maumivu makali sehemu za siri…na hapo hapo, nikajiwa na kizunguzungu, na kupoteza fahamu.
 nilipozindukana nikajikuta nipo hosp nimelazwa….

Nililazwa wiki, nikatoka, sasa leo nakutana na tukio jingine la aina yake, na baba mwenye nyumba !

*********

‘Unajua wewe una tabia ya kuota na kupiga makelele, …’akasema yule kijana na mimi nikasema

‘Na nikiota kawaida ndoto zangu huwa kweli,….nahisi mama yangu hayupo sawa

‘Kwani hawajakuambia…’akasema huyo kijana

‘Kuniambia nini…?’ nikamuuliza na mara baba akatokea akiwa kavalia, …hakusema neno, akaelekea kwenye gari lake, na kijana akasema;

‘Kama unaumwa mwambie baba akupeleke hospitali

‘Niambia kwanza umesema kwani hawajaniambia , hawajaniambia nini..?’ nikauliza na baba akasikia, na kusema

‘Wewe nanihii..njoo…’akamuita kijana wake, wakawa wanateta, na baadae akarudi na kusema

‘Baba kanipa pesa nikakununulie dawa….’akasema

‘Dawa gani kwani anjua nina umwa nini…?’ akauliza.

‘Za maumivu…kasema unakuwa kama umechanganyikiwa,..unapiaga piga kelele ovyo...kasema akija atakupeleka hospitalini, anahisi una malaria, kama yale uliyopimwa kipindi kila ikaonekana malaria yako imepanda kichwani…’akasema.

‘Lakini , …..nina uhakika alitaka kunishika…’nikasema na mara mama akatokea

‘Ndio alitaka kukushika alipokuona ukipiga ukelele...alijua utaanza kukimbia ovyo,..usijali baba ni mtu mwema sana, atakusaidia sana, nilisikia akisema atakupeleka VETA kusomea ufundi,...ila usije kumuuzi baba.., ukimuizi baba,..ana hasira kali sana, na hawezi kusamehe, utarudi kijijini tu upende usipende..yaani mimi nasema ni bora ukosane na mama, kuliko kukosana na baba, mwenyewe si unamuona hana muda wa kuongea mara mbili…’akasema.

'Lakini nina uhakika, alitaka kunishika  kwa-kwa nguvu..kwa nia mba-a.....'nikasema na nikakatisha maneno, kwani mama alishafika, na akasikia nikisema hivyo, na hapo hapo mama akauliza

'Ni nani alitaka kukushika.....?' akauliza mama.

NB: Mambo yalianza hivyo..


WAZO LA LEO: Tuweni makini sana na wafanyakazi wa ndani, kuna visa vingi vinatokea, vingine ni wao wanakuja na tabia ambazo, zinakuja kuwaathiri watoto wetu,…kabla ya kumuachia mwanao jitahidi kuwa naye karibu, mchunguze kwa makini. Lakini pia kuna visa vingine vya wenye nyumba kuwazalilisha hawa wafanyakazi wa ndani,…haya ni madhaifu yapo na yanatokea, ewe baba, ewe mama, huyu ni mwanao kama watoto wako ana wazazi kama ulivyo wewe kwa watoto wako, mthamini kama mwanao…kwani ukimtendea mabaya, na wewe watoto wako watakuja kutendew hivyo hivyo, dhambi hizi hulipiziwa hapa hapa duniani.
Ni mimi: emu-three

No comments :