Kitendo kile cha kudondoka mzee na kupoteza fahamu,
kilitokea pia, upande mwingine, kwa kile mtu aliyekuwa kawekezewa kwenye huo
mtandao ambao kwa muda huo ulikuwa kwenye mikono ya docta, ilibidi ahakikishe
kuwa kila mtu kafunguliwa kwenye kifungo hicho cha kishetani.
Na ukumbuke yote
hayo alikuwa akiyaona docta, akiwa huko kituo cha polisi, na watu waliotekwa na
mambo hayo walikuwa sehemu tofauti tofauti…mimi nilikuwa kwenye jengo la mzee,
Mpelelezi alikuwa kwenye nyumba ya kibiashara mtakuja kuiona ni numba gani
hiyo. Kuna wanawake watatu, …’ katulia docta akiwa ananihadithia matukio hayo,
ambayo mimi sikuwahi kuyaona,
Na pale mzee, alipodondoka na kupoteza fahamu, na mimi
ilitokea kwangu hivyo hivyo, na kwa mpelelezi, na kwa hao wanawake…ni kwanini
ikatokea hivyo?
‘Ni kwasababu watu wote hao walipandikiziwa mazindiko
ya kishetani na uchawi, na walishakuwa watumwa wa hao watu wabaya, na akili zao
zilitegewa kwenye mtandao, ..na docta alipomaliza kuondoa hayo mauchafu kwenye
vichwa vya haoo watu, ndio kila mmoja akaanza kudondoka kwa wakati wake
‘Ni utaalamu wa aina yeka wa kutumia mitandao…’akasema
docta, akinihadithia
‘Lakini ni ujuzi wa kuchanganya mambo ya giza, na
utaalamu wa digitali…kama hawa watu wangewekeza utaalamu huo kwenye mambo mema,
kama kutibu na madawa wangelikuwa mbali, lakini wao, kama wao, wanasema hivyo
haiwezekani….kutokana na masharti ya mambo hayo ya giza…mimi sikuwaelewa…’akaendelea
kuelezea docta, kipindi hicho nipo kitandani, mgonjwa.
Ngoja sasa niwarejeshe ilivyotokea kwa upande wangu,
baada ya kuondolewa hay mazinduko ilikuwaje,..
Basi ngoja niwarudishe siku hiyo ambayo, nilichukuliwa
mimi nikiwa sijiwezi, sijijui,..nikitolewa kwenye hilo jumba la mzee, baada ya
matukio hayo ya kutisha…
Tuendelee na kisa chetu.
***********
Mimi nikiwa
ndani ya jumba hili la mzee , ambalo liligeuka kuwa jumba la matambiko la hao
watu, nilishuhudia mambo haya ya ajabu….
Kwanza ilifika muda, nikahisi kama masikio yangu
yamezibuliwa, ni kama vile mtu masikio
yaliingia maji, na yale maji yakatoka, unahisi hali tofauti..ndivyo naweza
kuelezea hivyo kwa upande wa masikio, na akilini..ilikuwa kama mtu aliyetoka
kwenye usingizi mzito wenye ndoto za kutisha...
Na wakati hali
hiyo ikiendelea kichwani mwangu, bado nilihisi mwili wangu ukiniisha nguvu,,,viungo
vinalegea…lakini sikutaka kuzidiwa na kulala, nilihisi nikifanya hivyo , hao
watu watanikuta humo na kunimaliza..kwahiyo nikawa napigana na akili…na kuna
muda nikawa nahisi pumzi inabana, …nashindwa
hata kupumua vizuri, nikawa sasa natafuta sehemu yenye hewa.
Kwa hali kama hiyo ikanibidi nitoke mle kwenye kile
chumba, na kutembea hadi kwenye ukumbi, ambao muda mfupi uligeuka na kuwa uwanja
wa mapambano…wote mle waliwekwa chini ya ulinzi, wamelala sakafuni, wengine ni
wameshakufa.
Nilipowaona hao watu wamelala, wengine ni maiti, hali
ikazidi kuwa mbaya, nikwa nahisi vibaya zaidi, nikaona ni heri nirudi tu kule
nilipokuwa awali,….na nilifanya hivyo, nikikumbuka kuwa yule kiongozi wao,
alikuwa bado kapoteza fahamu kule nilipokuwa mimi…lakini kuna mtu mwingine
nilikuwa sijamuona…
Niliporudi pale nilipokuwa nikaangalia pale alipokuwa
kalala yule kiongozi wao. Sikumuona…na askari aliyekuwa akilinda pale naye
hayupo…sijui yupo wapi…
‘Hawa watu vipi…?’ nikauliza nikiangalia huku na kule
‘Ina maana hawa
watu wamemuachia huyo mtu…muuaji,…, haiwezekani..’nikasema na nikiwa natembea kwa
shida, nikaelekea kwenye chumba kingine, kilichokuwa jirani yake, na hapo ndio
nikawaona, kumbe wao wawili, waliwekwa chumba kingine, na askari aliponiona
nataka kuingia huko akanizuia…
‘Afande nataka kumuona huyo kiongozi, wao, ….nina
majukumu naye, …’nikasema na yule askari alishanifahamu kuwa mimi ni
nani,..akasema;
‘Una majukumu naye kwa vipi…?’ akauliza
‘Ungemuuliza afande wako angekuambia…’nikasema
‘Haya kama unataka kukaa nao humo ndani, haya ingia,
lakini usije kuleta vurugu huko ndani, …maana nyote nasikia mumechanganyikiwa
na mashetani ha hao watu..’akasema na nikafunguliwa mlango na kuingia ndani.
Mlango ulipofunguliwa tu, nikasikia zogo,
nikamuangalia huyo askari, na yeye wala hakujali, akaniashiria niingie.
‘Wewe si unataka kuingia,..ingia, ukakutane na hao
vichaa huko ndani…’akasema na kwanza nikahisi huenda sio yule kiongozi wao,
nikasema kwa huyo mlinzi.
‘Yule anayeonekana kuwa ni kiongozi wao yupo wapi..?’
nikamuuliza
‘Ndio yupo humo ndani…’akasema na kufunga mlango kwa
nyuma yangu…hapo nikajiuliza itakuwaje iwapo ni kweli, hao watu
wamechanganyikiwa na kwanini wawaweke wawili, mke na mume…’nikasema nikisikia
sauti ya kike na kiume wakibishana kuhusu jambo fulani.
Kwanza sikuingia moja kwa moja,…uzuri wa chumba hicho
unaingia sehemu kama ya mapokezi vile…halafu
unakata kulia ndio uingie kwenye chumba chenyewe…nahisi walitaka
kupafanya hapo kama sehemu ya kujisomea. Kuna kabati kubwa linazuia, huwezi
kuona kwa ndani.
'Unataka kwenda wapi?..’nikasikia mwanamke akiuliza,
nilijua ni mimi naulizwa kuwa, lakini kumbe walikuwa wakiongea wenyewe huko ndani.
'Dada sikiliza,…jinsi muda unavyozidi kupotea hapa
ndivyo tunavyozidi kuingia matatani,…sijajua kinachoendelea…ni lazima nipambane
hadi damu yangu ya mwisho…hawa watu hawajanijua kuwa mimi ni nani..’akasema
‘Upambane na nani…?’ akaulizwa
‘Dada wewe peke yako ndiye unayenifahamu …sitaki
kusikia ukisema lolote,,…najua nikitoka hapa hakuna atakayenitambua
tena..tatizo nipo mbali na mitambo yangu…’akasema nikajiuliza ni kwanini
anasema hivyo.
‘Unajidanganya, wamegunduaje kuwa umevaa hiyo ngozi,
watashindwaje kukugundua kuwa….’akataka kusema, na ghafla akanyamaza.
Nikahisi kuna kitu…au kanyamazishwa au wameona kitu….mimi
nikajabanza vizuri nyuma ya kabati, na nikasikia wakisema.
‘Nilisikia kama mlango umefunguliwa,…’akasema mwanaume.
‘Ni huyo askari, alikuwa akijaribu kuona tupo salama,
wanajua wewe ni tahira wa mashetani….’akasema huyo mwanamke.
‘Unatafuta nini…?’ mwanamke akauliza.
‘Mimi ni mpiginaji, najua nini nitakachokifanya, ….’akasema
na akawa kapata kitu kama chuma, akaenda kwenye dirisha na kuanza kujaribu
kupindisha nondo za dirisha, ikawa haiwezekani…
‘Hebu tulia kule…’ilikuwa suti ya huyo mwanamke, …nilishindwa
kujua kwanini anasema hivyo kwa kujiamini, nikageuza shingo kumuangalia huyo
mwanamke…nikaona ooh, kashikilia bastola.
‘Hahahaha….kumbe unayo hiyo silaha…sasa dada hapo…eeh
umecheza, umewezaje kuificha wasikugundue,…unajua wakati mwingine mimi
nakuvulia kofia,…, tunaweza kujihami, nipe hiyo kitu, mimi najua vyema jinsi ya
kuitumia kuliko wewe…’akasema huyo mwanaume.
‘Nikupe nini…hahaha, ili uniue, nakujua sana wewe,
rudi pale ulipokuwa,..na ukae chini…, unajua nataka nini, ninataka wakukute wewe
ni maiti, kama ulivyofanya kwa binti yangu…’akasema huyo mwanamke.
‘Sikiliza dada, acha kunielekezea hiyo kitu, kama ndio
yenyewe, haikwepeshi labda uwe na dhamira ya kuni…jeruhi tu,..lakini ukiwa na
dhamira ya kuniua, kama ndio yenyewe, ni lazima itafanya hivyo, hata kama huna
shabaha..acha na nayo, geuza kule,..ujue dada mimi nakupenda sana,… hayo niliyoyafanya
, nilifanya kwa ajili yetu, …na kuhusu binti yako, mbona ipo wazi, alijiua
mwenyewe, …’akasema.
‘Hahaha..wadanganye wengine…siku zote nilikuwa
natafuta uhakika, je kweli binti yangu alijiua mwenyewe au la,..nimekuja
kugundua kuwa ni wewe ,…uliyemuua, kwa ujanja ujanja wako, wa kupandikiza
ushetani kwenye miili ya watu,…leo nimedhihirisha kuwa ni wewe na mambo yako…na
kwahiyo kama nilivyoahidi, kuwa aliyemua binti yangu na yeye ni lazima afe., ….’akatulia
sijui ni kwanini.
‘Dada unakumbuka tukiwa wadogo, nilikuahidi nini,…kuwa,
japo hatukuzaliwa tumbo moja, lakini sisi tumeungwanishwa kwa babu ni bibi ndio....
na wazee wale walitaka,kutupatia huo urithi, wewe ukakataa......'ilionekana kama
anahisi maumivu au anaigiza kuhisi
maumivu…pengine , ili huyo mwanake amuonee huruma.
'Lakini wazee wale hawakutulazimisha kuchukuo huo
mkoba,…walituasa ubaya wa hayo mambo,na kama hatutaweza ni bora, wakaharibu,
wewe ukasema nini kwa tamaa zako…tamaa za mali tokea ukiwa mdogo,..ukataka kurithi
huo ushetani , na baya zaidi mungu akakulaani, ukawa huna kizazi. Sijui ungekuwa
nacho ungefanya hivyo hayo mashetani yanavyotaka, …ukaona unigeukie mimi na
familia yangu…’akasema huyo mwanamke.
'Dada, sio kweli…mimi nawajali wewe na familia yako,
ndio maana nikawa nahangaika kutafuta mbadala wake,…najua walichotaka hao
wahenga,…lakini niliomba nipate mbadala wake,… na mbadala wake ni gharama
kubwa, damu nyingi ilihitajika..kutafuta watu wenye nyota kama za….’akatulia.
‘Kama za familia yangu, kama za damu yako…hiyo sio
damu yako…ni ushetani wako tu,…’akasema huyo mwanamke kwa hasira.
‘Sio ushetani wangu dada…ni masharti yao magumu….ilifikia
ikawa mimi au wewe, au watoto..lakini nikawa nakwepesha..ndio maana nilitaka
yule …mchumba wa binti yako..yeye ana nyota, …yeye angelifaa, sana, lakini….aah,
dada hebu tuyaache hayo, …nipe hiyo silaha…’akasema
'Mimi sikuelewi wewe…, pamoja na kusoma kote huko, una
kazi, una heshima, lakini bado, unashiriki kwenye huu uchafu wa ushirikina,
mimi sitakusamehe.
'Dada, sio kazi rahisi kama unavyofikiria wewe…hujui
jinsi gani nilivyoteseka,..huko chuoni,…ilifika mahali nikawa kama punguani,
kisa nimepuuza maagizo ya wale wazee,…hebu niambie, kwa hali hiyo, ulitaka mimi
niwe…hapana, ….sikupendelea ..nilijuta kukubali, lakini imeshapita, wewe
ulitaka mini nifanyeje…niteseke,..niharibikiwe kabisa, au…?’
'Ungefanyaje, wakati ulijitakia wewe mwenyewe kwanini
ulikubali….kwanini hukukataa kama mimi,…?’ akauliza
'Hilo lilishapita,…. haya ilikuwa upumbavu na tamaa
zangu, kukubali,…sasa … siwezi tena kujirejesha huko nyuma, huoni adhabu
niliyopewa,…kwanza sizai...sina raha, mke..oh, akanikimbia, kisa ni nini…nimekuwa
nikiishi kwa taabu, nateseka, usiku ukifika naadibiwa, mchana , nipo kama
tahira,,, ..aah..'akawa kama anataka kuanguka..kwa pale nilivyomuona.
Yule mwanamke
huruma ikamjia, akalegeza mkono, bastola ikawa inataka kudondoka mkononi….niliona
jinsi gani huyo jamaa alivyoinua jicho, nikajua kuna kitu kitafuatia….
Ilikuwa kama
mshale, yule mtu alivyojirusha, mateke mawili, yakampata yule mama kifuani..yule
mama akarushwa na kudondoka chini kama gunia, bastola ikadondokea upande
mwingine.
Nilisikia yule
mama, akitoa sauti ya kukugumia na yule mtu naye halikadhalika, kajitonesha, …lakini
kwa vile lengo lake ni bastola,…akajitutumua, na kwa haraka akajirusha kuifuata
ile bastola, lakini alipotua alitanguliza miguu, na mguu wake mmoja,, ukawa
umeipiga teke, ile bastola ikaserereka hadi pale nilipo….akawa anagugumia
maumivu damu zinamtoka begani, naona aliumizwa na risasi..walipokuwa kwenye
mapambano.
Ilibidi kwanza
atulia kusubiria maumivu kutulia,..na baadae sasa akili ya kuiangalia hiyo
bastola ikamjia,…hakujua imeenda wapi alivyoigonga na mguu…ilikuwa karibu name,
ni kiasi cha kunyosha mkono kuichukua, lakini nikifanya hivyo wataniona,…na
mimi kwa muda huo, ilahali ya kujisikia vibaya ikawa inakuja kwa kasi, nikawa
sasa nahisi mwili mzima, unaniishia nguvu,
sijui ni kwann.
Jamaa sasa
akawa kapiga magoti akiitafuta hiyo silaha, na yule mwanamke alionekana kukata
tamaa, bado alikuwa kalala pale sakafuni, , na jamaa akawa hajaiona ile silaha,
akamgeukia yule mwanamke.
'Hii bastola, ina mashetani,… nimeamini…kama ndio
yenyewe..basi …ipo wapi….’akawa sasa anataka kusimama.
‘Hutaipata kamwe…’akasema huyo mwanamke.
‘Unajua wewe sikuelewi…, kwa ujuha wako siku zote nimekuwa
nikikuambia umuibie mumeo hiyo bastola na vile viatu,..uniletee mimi, wewe unaogopa,
sasa leo, naichukua hiyo bastola, na ikiingia mikononi mwangu, hakuna atakaye
niweza tena…na hapo hata hivyo viatu nitavipata…’akasema akionyesha macho ya
kikatili.
‘Si mpaka…’akasema huyo mwanamke.
‘Hiyo bastola ipo wapi, unajua hiyo bastola ina
umuhimu gani, hata mumeo hajui..kwanza shabaha, haikosi ila ukifyatua uweke
dhamira, pili, unaweza ukapambana na jeshi kubwa tu…na….siwezi hata
kukuambia..hiyo silaha, imetembea nch nyingi duniani…kama ingelifika kwa yule
jamaa…’akatulia
‘Jamaa gani….?’ Akaulizwa
‘Wa dunia yangu…sasa hivi angelikuwa kama nani
vile..hahaha, sasa leo ni lazima niipate,..na viatu , unajua dada vina umuhimu
gani..vile ukivivaa, usiku unaweza ukuruka kama kangaroo…unajua kangaroo anavyoruka
na kukimbia…ni kama unapaa…hahaha, sasa natumai ndoto yangu itatimia, ..unajua
dada nilipoipata ile pete ya mtandao..inaitwa ufunguoa, nikajua sasa nitakuwa
mwana mitandao,..anayeweza kudhibiti, au kuingie kwenye aina yoyote ya
mitandao, huhitaji namba ya siri, hiyo ni nama ya siri, ya kuingia popote pale…nimeipata..lakini…haijakamilika…’akatulia
‘Unataka nini tena, tamaa zako hizo, ndizo
zitakuangamiza…na najua mwisho wako umefika,…’akasema huyo mwanamke sasa
akijitahidi kukaa. Na yule jamaa akawa anamuangalia kwa makini huyo mwanamke,
machoni..alijua kama huyo mwanamke kaiona hiyo bastola macho yake yataelekea
huko..lakini kumbe hata huyo mwanamke hakuona wapi hiyo bastola ipo…
Mimi pale nilipo macho yalishaanza kuwa manzito, mwili
wote umelegea na wakati wowote ningeliweza kulala chini…na kupoteza fahamu,
lakini nilijua ile bastola ni muhimu sana, …kuhakikisha haifiki mikononi mwa
huyo shetani,…
Mara yule mwanamke akaiona,…alitupia jicho paaa,
akaiona na kujivunga kuangalia upande mwingine, lakini hakuweza kumvunga huyo
jamaa , na yule jamaa akatupia jicho upande ule, akaiona….
NB: Ilikuwaje....
WAZO LA
LEO: Usipojenga tabia ya kuridhika, ukipata kidogo unataka kingi,
hata kama sio halali yako, ukiona mwenzako anacho unataka na wewe ukipate tena
sio kwa halali..ujue moyo wangu umetawalia na shetani,..tamaa hiyo ni mbaya, na
wengi wenye tamaa hiyo ndio wale hata wakiwa na madaraka, hata wakiwa matajiri,
bado hawatosheki..wapo tayari hata kuua..wapo tayari hata kujiunga kwenye
makundi ya kishetani..lakini wakumbuke kuwa mwisho wake ni wapi…wangapi wangapi
walikuwa hivyo na sasa wapo wapi!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment