Mpelelezi, alipoona
dereva kakiuka maagizo yake akaingiwa na shaka, hakuelewa ni kwanini mtu mdogo
kama yule asitii maagizo yake, na haijawahi kutokea, na baya zaidi alipompigia
simu akawa hapokei,
‘Ni kwanini huyu mtu
anafanya hivi…au..?’ akajiuliza na hii ilimpa dalili mbili, kuwa kuna tatizo la
kiutendaji , na anatakiwa kuchukua hatua za kinidhamu, lakini kinamna fulani
alihisi hatari, au kuna mkuu zaidi yake katoa amri,na kama ni hivyo, basi..huenda
kuna jambo nyuma ya pazia kwahiyo inabidi achukue hatua ya haraka, na akilini
mwake, alitekwa na ile kauli nyingine ambayo hakupenda kuisikia,..
‘Hakikisha hao watu
hawafungui mdomo, wakifungua mdomo wao, basi ujue wa kwako utafungwa..’
hakupenda kauli hii , hakupenda kauli za vitisho, lakini alijua huyu mtu
aliyemuambia hivi hatanii….na hapo akahisi mwili ukimsisimuka.
Mpelelezi aliyekuwa
akilifuatilia hilo gari kwa nyuma…alikuwa ameliacha nyuma kwa kukingwa na
magari matatu mbele yake.., akaona ni
lazima asitishe mikakati mingine yote, kwani ikiendelea itakuwa ni
hatari,..ndio hapo akachukua simu na kusema maneno haya;
‘Mission abort turn back now …’akasema na kukata simu.
Akiwa na hasira, akamwambia dereva wa boda
boda aongeze mwendo,..kulifuatilia hilo gari kwa karibu sasa… lakini kwao
haikuwa rahisi maana mbele yao
wakakutana na ajali ya gari, kukawa na folen kuwa, hapo akasema;
‘Unaona hawa watu
niliwaambia wasingie njia kuu, sasa unaona kitu kama hiki, nashindwa hata
kuchukua hatua, ngoja nione …’akasema na mwenye boda boda akasema
‘Lakini hii ajali ni
magari yalikuwa yakiingia njia kuu, na inaoenkana jingine lilikuwa likitoka,…
kwa haraka, utafikiri watu wamepanga haiwezekani mtu mwenye leseni akafanya
hivyo….’akasema dereva wa boda boda, na mpelelezi hakupendezewa na maneno yake
akasema
‘Vyovyote iwavyo amri zetu
hazipigwi, maana sisi wakubwa tunajua ni kwanini tunatoa amri fulani, sasa
sijui kama wameweza kupita eneo hili, maana siwani huko mbele na dereva hataki
kupokea simu yangu,..’akasema akikagua kwa macho kulitafuta lile gari, lakini
hakuliona
‘Walishapita mkuu,
niliwaona pale tuklipokuwa tunapishana na lile gari kubwa la mizigo…’akasema
dereva wa hiyo boda boda
‘Ok, sasa fanya haraka
tulifikie,…sitakiwi kuwa mbali na hilo gari…na huyo dereva huko kituoni,
atanitambua kuwa mimi ni nani…’akasema na mara akipigiwa simu na sasa akawa anaongea
na watu wake wengine, mara akasikia taarifa iliyomfanya ashtuke kidogo,
akasema;
‘Hebu simama kidogo,…’akasema
na kutoka nje, akawa sasa anaipokea simu, akasikiliza kwa muda halafu akasema;
‘Usijali..nitalifanyia
kazi…’akasema na kurudi kwenye boda boda, baadae wakafika kituoni.
Tuendelee na kisa chetu…
**********
Walipofika kituoni, alikuta
wale watu wawili wameshapelekwa mbele ya mkuu maalumu wa kesi za ndani, na yeye
akafuatilia, kahakikisha taratibu muhimu zimefuatwa, huku akiwapigia badhi ya
watendaji wake kuendelea kumsaka binti..
‘Na huyu binti atakuwa
sehemu muhimu ya kulimaliza hili, najua kila kitu nitakiweka sawa,na
nitahikikisha huyi mtu anayenifanya nisiwe na raha, …namweka sawa, hanijui
mimi..’akasema kwa sauti ndogo sasa akielekea kwa mkuu wake wa
‘Nimeshawaleta mkuu,
inabidi baadae niweze kuongea nao kiundani, nimeona kwanza niwafikishe huku,
halafu mengine yatafuata baadae…’akasema
‘Vizuri, nilishaambiwa
wameshafika…’akasema mkuu wake
‘Na nani na mimi ndiye
nilikuwa naifanya hii kazi,…’akasema
‘Unajua…nahisi kuna watu
walikuwa na mpango dhidi ya hawa watu wawili…’akasema mkuu
‘Mpango gani mkuu,
haiwezekani, ni nani kakupa hiyo taarifa mkuu...?’ akauliza mpelelezi kwa
mashaka.
‘Kuna mpango wa
kuwamaliza hao askari wawili, kwa vile wakiendelea kuwepo watasema kwanini
waliachia binti akapita, nina imani kuwa huyo binti hakupita hivi hivi bila ya
wao kuhususishwa, kwahiyo hawa askari wanajua mengi, …’akasema mkuu
‘Mhh…sijui kama kuna
ukweli wa hilo mkuu…mimi ndiye nastahili kusema lolote maana ni askari wetu
nawafahamu sana,, …na kama labda kuna watu wa nje ni akina nani hao,ngoja
nitalishughulikia mara moja mkuu na ukweli utafahamika…’akasema
‘Hao watu ni wajanja
sana,,,, walipanga kutengeneza ajali, ili magari yote yakwame…’aliposema hivyo
mpelelezi akawa kama kashtuka, na kusema;
‘Mkuu hizo habari
umezipatia wapi…?’ akauliza.
‘Ni jambo lisilo na
mantiki,..na haya yote ni kuonyesha kuwa kuna watu ndani yetu wapo sambamba na
hili kundi haramu, lakini, nitahakikisha
hili kundi na hao vibaraka wanafikishwa mbele ya sheria.…’akasema mkuu
akionyesha dhamira ya kweli, na mpelelezi hapo akanywea na kusema;
‘Mkuu mimi nipo na wewe,
tatizo ni huu utendaji wa kugawa makundi, wengine wanafanya hivi wengine vile
huu utendaji unanipa wakati mgumu sana…’akasema mpelelezi akionyesha wasiwasi
‘Tumewakamata hao watu waliotaka kuwamaliza hao askari, na wao
wataingia chumba maalumu , najua humo watataja kila kitu ni nani kawatuma
kufanya hivyo, na hiyo ni awali tu, nitahakikisha wote na huyo mkuu wao
wamekamatwa…’akasema huyo mkuu, sasa akimtupia jicho la kujiiba kumuangalia
mpelelezi
‘Mkuu mimi nitalisimamia
hilo zoezi..’akasema mpelelezi
‘Hapana wewe endelea na
kazi yako,…najua wewe una majukumu mengi,kwanza kwa hivi sasa nataka tuwe
pamoja hapa kituoni, kazi za kuzunguka, nataka msaidizi wako azifanye
yeye..nina mambo nataka tushuirikiane,…’akasema mkuu.
‘Kwanini mkuu, unajua
kazi zangu zilivyo, kukaa ofisini sio fani yangu…nataka niwe mstari wa mbele
kwenye mapambano…’akasema mpelelezi.
‘Najua..ni swala la muda
mfupi tu..baadae utendelea na shughuli zako kama kawaida, ni leo tu, baada ya
leo kazi zitakuw rahisi..tutamaliza kazi…’akasema mkuu,
Maneno haya ‘ni leo tu..’
aliyasikia kwingine, na sasa kayasikia hapa tena, je ni masikio yake au kuna
namna ya taarifa zinavuja, alikumbuka kuambiwa hivyo kabla.
‘Leo tunataka kumaliza kazi, baada ya leo,…kazi yetu itakuwa
kiuingiza..ni leo tu, baada ya leo hakuna kazi nzito….’aliambiwa maneno
hayo kabla.
Mpelelezi alihisi mwili
ukimsisimuka, akaanza kuwazia mbali, alijua mikakati yake itafanikiwa na mwisho
wa siku ataweza kuonekana shujaa, wa kuweza kulizima kundi hilo , lakini kumbe
njia yake imekuwa na ngumu, na amejikuta yupo kwenye mtihani mkubwa wakuamua
lipi lifanyike kwanza…
‘Oh..nahisi muda umefika…’akasema
akilini.
‘Sasa ni hivi ninataka
mimi na wewe tuelekeza nguvu zetu kwenye kumpata huyo binti kwanza, najua wapi
alipo, lakini hatuwezi kwenda moja kwa moja, mpaka tujue ni kwanini kafanya
hivyo, na …yupo nyuma ya nani,…umenielewa mikakati yangu, huu sio muda wa kutumia
nguvu, umenielewa..?’akasema mkuu wake
‘Bila shaka
mkuu,,,;akasema na kugeuka kuelekea ofisini kwake.
Na mkuu huyo akawa kasimama akimuangalia huyo mpelelezi
akitembea kuelekea ofisini kwake, aliona kuyumba kwa hatua za askari huyo
shupavu, alimuamini sna, na alijua kuna kitu kimemsukuma kufanya hivyo
anavyofanya, lakini hakuwa na muda wa kubembeleza tena, wakati sasa umefika.
Alichukua simu yake na kutoa amri kuwa mtu yoyote asitoke bila ya kibali chake.
Mkuu akarudi ofisini
kwake,..baadae akaona aende seehmu alipo docta, ili aone kama anaweza kupata
lolote, na ikibidi amuelezee baadhi ya mipango yake, na alipofika chumba
ambachp docta alikuwa anakaa, akakuta hayupo…
‘Docta kaenda wapi..?’
akauliza
‘Docta kasema wewe
umemruhusu kuondoka..kwenda kwa mgonjwa, anasema binti yupo kwenye hali mbaya
anahitajika kwenda kumuhudumia,, ..’akasema askari aliyekuwa akimlinda docta.
‘Nani kamruhusu huyu
mtu, mimi sijamruhusu kuondoka, kwanini anasema hivyo, ni lazima kuna jambo…ni
kwanini ukafanya hivyo, nilikuambia nini…?’akasema kwa hasira na sasa akawa akimpigia
simu docta.., lakini simu yake ikawa
inaita tu haipokelewi.
‘Huyu mtu anataka
kufanya nini….?’ Akawa anajiuliza bila jibu, na kwa haraka akaenda ofisini kwake kuangalia mitamabo yake maalumu,
hakuweza kupata kitu cha kumsaidia, hapo akaamua kwenda ofisini kwa mpelelezi, akakuta naye hayupo
‘Na huyu naye kaenda
wapi..?’ akauliza mkuu kumuuliza muhutasi wa ofisi ya upelelezi
‘Kasema kaenda huko
ulipomtuma…’akasema katibu muhutasi wa idara ya upelelezi.
‘Nilipomtuma mimi!…hapa
kuna tatizo, ofisi hii mnanishangaza sana, kwanini hamtii amri za viongozi
wenu, nitaawajibisha ofisi nzima…’akasema akitoka nje kwa hasira, na kuingia
ndani ya gari lake..
‘Twende makaburini….’akasema
akimuamrisha dereva wake
*************
Docta akawa sasa
keshafika kwenye nyumba ya mzee ambayo sasa yaonekana kama imetelekezwa,kwani
mpangaji aliyekuwepo hapo awali keshafariki…na katika hisia zake, alijua kabisa
mpelelezi atakuwa kaja eneo hilo, hakuweza kumfuatilia kwa karibu lakini kwa jinsi
alivyomuona akitoka pale getini , alijua kabisa safari hii itaishia hapa..
Ilikuwa ni bahati tu,
wakati alipoamua kutoka nje kupata hewa safi, akawa kasimama kwenye mti, na
akiwa kaangalia ofisi ya mpelelezi, mara akamuona mpelelezi akitoke kwenye hiyo
ofisi, na akawa anaongea na askari mmojawapo,…na haikupita muda akaja bajaji,
na mpelelezi huyo akaingia kwenye bajaji, na kundoka nayo..
‘Nilisikia mkuu akisema
mpelelezi leo hatakiwi kutoka, mbona kaondoka , tena anaonekana ana haraka,…’ docta
alijiuliza na hakupoteza muda, akaingiwa na maamuzi ya haraka, alitaka kumpigia
mkuu, lakini akaona anapoteza muda, na yeye akaingia ndani na kuvalia vazi lake
la udakitari, na kubeba mkoba wake, akaelekea getini
‘Unakwenda wapi docta..?’
akaulizwa
‘Nimeambiwa kuna mgonjwa
mahututi, natakiwa kumuwahi,…’akasema na ilikuwa ni bahati walinzi walikuwa
wakikabidhiana, ..huyu anayeingia alikuwa hajapata maagizo kamili kuwa watu
hawatakiwi kutoka leo bila idhini ya mkuu, na huyo mlinzi mpya, akajua docta ni
mtu muhimu hawezi kudanganya akageuka kumuuliza mwenzake..Docta hakupoteza
muda, akatumia mwanya huo, na kutoka nje na kwa haraka akaiwahi bajaji
iliyokuwa ikisuburiwa.
‘Hapa nacheza pata
potea,..huenda huyu mpelelezi anakwenda kumaliza kazi,…’ akawaza hivyo docta
huku akijua kafanya kosa kuondoka bila kibali cha mkuu wa kituo.
‘Inabidi nilifanye hili,
maana huyu mkuu, hata yeye sasa simuamini , ni kwanini ananishikilia mimi hapa
kituoni, kama mfungwa, hajui kuwa nina wajibu mkubwa kwa familia ya mzee…hao
wazee hawatanielewaje kama lolote litatokea kwa binti yao…’akasema.
‘Mpaka wapi
mzee..docta..?’ akauliza dereva wa boda boda
‘Wewe nishushie karibu na
yale makaburi…’akasema akimuelekeza dereva wa boda boda.
Docta akafika sehemu
aliyoona ni sahihi, hakutaka kuikaribia moja kwa moja nyumba ya mzee, akavua
koti lake la udakitari, na kulikunja, na kuanza kutembea sasa kuelekea kwenye
hiyo nyumba iliyotekelezwa ya mzee, akipitia kwa nyuma, ili kukwepa macho ya
watu…kila alipokuwa akiikaribia hiyo nyumba ndivyo alivyohisi mwili ukimsisimuka,…
‘Hii ni dalili mbaya…’akasema
lakini hakuweza kurudi nyuma, alijua akichelewa tu atamkuta binti wa mzee, ni
marehemu na hapo itakuwa mwisho wa uaminifu kati yake na hiyo familia ya mzee na mkewe!
‘Kwanini mkuu huyu
hakuchukua hatua za haraka za kufika huku, najua anafahamu kabisa kuwa huyu
binti atakuwa katorokea huku…na kuwepo haap peke yake ina maanisha nini,…kuw
ahuyu binti kwa hivi sasa sio yeye, anatembea kama roboti tu, na huenda mkuu
anamtumia huyu binti kama chambo, lakini ni hatari kubwa sana…’akasema sasa
akiwa kasimama nyumba ya ukuta wa hiyo nyumba, akaangalia huku na kule kwa
haraka akaruka ukuta na kudondokea ndani.
Alipohakikisha kuwa
hakuna walinzi kwa ndani, akatembea hadi kwenye mlangow a nyuma…
Akachukua ufungua wake
Malaya, akaweka kwenye kitasa baada ya kuhakikisha mikono yake imevaa kinga,
akafungua kwa kutumia ufungua huo bandia, haikualika mlio wa kufunguka, ina
maana mlango ulikuwa haukufungwa kwa ufunguo…akasita kidogo, lakini baadae
akazungusha kitasa cha mlango, na mlango ukafunguka.
Ina maana mpelelezi naye
alitumia mlango huu…akawaza hivyo, na hakupoteza muda akaingia ndani!
Docta akajua sasa yupo
uwanja wa vita, hisia zote zilionyeha yupo kwenye hatari, lakini hakujali,
alichojali ni kumuokoa huyo binti, na ..kwa hali ilivyojitokeza hakuamuamini
kabisa mpelelezi, ndio inawezekana alijua wapi binti alipo, na sasa alitaka
kuonyesha kuwa anafanya kazi yake vyema, atamchukua huyo binti hadi kwa mkuu
wake na kusema;
‘Huyu hapa nimempata…’
atasema akimkabidhi huyo binti kwa mkuu wake, na ataonekana mtendaji mwema, na
makosa yake yatafijichika, na kuendelea kufanya akzi zake kama mtu mbili…lakini
pia anaweza akawa katumwa, kummaliza huyo binti kwani yawezekana ndio kafara
lao la mwisho kama alivyoipata taarifa hiyo kutoka kwa mtu wake wa karibu.
‘Wanajiandaa kufanya
kafara la mwisho, na ina maana kuna damu itamwagwa, kwa wingi, be careful…’alitumiwa ujumbe na mtu wake
kutoka nje ambaye analifuatilia tukio hilo kwa karibu sana.
Alihisi mwili
ukimsisimuka, kwa hali kama hiyo inaashiria kuna mashetani, na kwa jumba kama
hilo ambalo halitumiki kwa muda, basi wadudu hao watakuwa wamefanya masikani
yao humo na watu wabaya hasa..hasa hilo kundi huenda wanalitumia hilo kama
makao yao ya usiki,…
‘Na huyu binti atakuwa
ndondocha tayari…hajitambui, sizani kama anajijua…’akasema docta.
Akaingia ndani , na pale varandani au chumba cha maongezi
hakukuwa na kitu chochote ni kama palivyoachwa,..chumba kilikuwa kimia, na hali
fulani inayofanya mwili uhisi baridi,..ilikuwa kama ni kwenye giza watu
wamejificha wanakuangalia,..alihisi hivyo, alijua ni hao wadudu…hakujali,
aliweka mbele ujasiri, kutokuogopa,…alijua ni wapi aelekee,… chumba cha
mabinti..
Kwa tahadhari akaelekea
huko, na alipofika, alikuta mlango upo nusu wazi, akatumia ule upenyo kuangalia
ndani, hakuweza kuona kitu, kwa mguu akausukuma mlango taratibu, ukawa wazi, na
kwa kasi ya ajabu akajirusha na kudondokea ndani,….akiwa tayari kupambana na
lolote japokuwa alikuwa mikono mitupu!
Alivyoruka na
kujizungusha kwa haraka, na pale chini akawa kama kachuchumaa, mtindo wa watu
wakianza mbioa wanavyokaa, huku macho yakicheza huku na kule..ni mazoezi yake
ya muda mrefu, na wakati huo huo hisia zake za mwili zikawa zinafanya kazi, pua
ikanasa harufu isiyo ya kawaida,…harufu ya maiti..
‘Oh, maiti…kuna dalili
kabisa ya maiti..’akili ikasema hivyo.
Chumba kilikuwa kimia,
japokuwa hisia ziligundua kuwa kuna hiyo dalili ya maiti,na damu, huenda maiti
hiyo imekufa kwa kumwagwa damu…docta anaijua sana harufu hiyo, na sio ya
kubahatisha, hapo mwili ulimuishia nguvu, ni maiti ya nani, na humo chumbani, kama
alivyoona kwenye video mbashara yake aliyekuwemo humo alikuwa mdada…na ambaye
angeliweza kuingia kwa muda huo ni mpelelezi, huo sasa ni mtego!
‘Hawezi awe ameshainga
na kuifanya hiyo kazi na kuondoka…’akawaza hivyo
‘Au alikuta binti
keshauwawa, akaamua kuondoka, maana kuja kwake hapo sio rasmi…vinginevyo kuna
mtego humo ndani…’akawaza hivyo docta, lakini mawazo hayo yalikuwa kwa muda
mfupi sana, kabla hajaangza macho kitandani ..na macho yake yalipotua
kitandani, akamuona,…mdada!.
Akiwa kwenye tahadhari,
akawa sasa anachungulia kitandani, binti alikuwa kalala chali, sehemu ya miguu
yake imening’inia, kalala akiangalia juu, mdomo wazi, inaashiria nini..ooh, sio
yeye, haiwezekani wameshamuua huyu binti wa watu….na alipotizama vizuri akaona
damu, sehemu ya kushoto, kwenye bega, au kwapani au sehemu ya titi la kushoto…..
‘Oh wameshamuua…’akasema
Ni kitendo cha haraka na
macho yalishaangaza kona za chumba, na ndipo akagundua kitu,…pembeni ya mlango,
kulikuwa na mtu kachuchumaa, karibu na mlango, bastola mkononi… ina maana
alipofungua mlango huyo mtu alikuwa nyuma ya mlango…lakini ile hali ya
kuchuchumaa ilikuwa sio ya kawaida, ni kama kaegeshwa …huyo mtu alikuwa tayari
maiti! Paji la uso lilikuwa na tundu la risasi…
‘Oh, maiti wa wawili…’akasema
docta sasa mwili ukianza kufanya kazi ya hali halisi na kabla hajakaa sawa
mlango ukafunguliwa kwa kasi.
‘Polisi…MIKONO JUU’
ilikuwa sauti kali
NB: Jamani sehemu hii
mniwie radhi kidogo nimeandika KWA HARAKA KIDOGO, ili twende na wakati,
tumechelewa sana kukimaliza kisa hiki!
WAZO LA LEO:
Unapopata kitu, iwe madaraka au kipato, ni kawaida kwa uanadamu wetu kujiona ni
zaidi au hata kufikia kuzarau wengine, na kuwaona wengine abda ni wazembe. Ni
kweli umepata, mshukuru mola wako, na moyoni uitakidi kuwa hayo yote sio kwa
ujanja wako, mpaji ni mola pekee. Yeye ndiye kakupa na kumfanya mwingine akose
kwa madhumuni maalumu, anayejua sababu ni mola peke yake,..tusifikie hatua ya
kukufuru na kuwazarau wengine kuwa labda wao ni wajinga, cha muhimu ni kusaidia
pale inapowezekana, na kuzidi kuwaombea wengine wapate kama ulivyopata wewe,
huo ndio wema wa muungwana, kwani leo kwako kesho kwa mwingine!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment