Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, May 3, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-21
Binti akasema:

‘Sawa,…mimi nipo tayari, kushirikiana na nyie,  mkiwa tayari mniambie, nipo chumbani kwangu mara moja..’binti akasema akiondoka kuelekea chumbani, na mimi na docta tukabakia pale, na docta akaninong'oneza akisema;

‘Binti anajua jambo…na hivi sasa huenda anawasiliana na hao watu, najua kwanini anafanya hivyo, lakini tumpe muda, hata hiyo ya kusema atashirikiana na sisi, sio kweli anachofanya ni kuvuta muda,…sasa sijui kwanini, kuna hii namba walimpigia, nataka tuipige , tujue ni nani kabla hajawasiliana nao..mimi natoka kidogo,...’akaniambia kwa sauti ya chini, na kuanza kutoka nje, mimi nikabakia

Haikupita muda, mara binti akaja akiwa  katokea chumbani kwake, alionekana mwenye haraka, na akatuangalia, akagundua kuwa docta hayupo, akasema;

‘Docta kaenda wapi…?’ akauliza akionyesha wasiwasi mkubwa

‘Yupo kaenda kujisaidia…’nikasema

‘Hapana nimeshamjua,….kachukua namba ya simu anataka kupiga, kumpigia..hapana asifanye hivyo, ataharibu…’akasema sasa akitaka kutoka nje

Baba alieyekuwa kimia akasema;

‘Wewe binti niambie kuna nini unaficha…’baba yake akasema kwa ukali, binti alishafika mlangoni akasema kwa sauti ya huzuni

‘Baba usiwe na wasiwasi, hakuna kitu ninaficha, usinielewe vibaya baba, ili uelewe kuwa, nayafanya haya kwa ajili yenu, nawalinda nyie…baba hawa watu sasa ni hatari kwetu., …’akasema huku akikimbilia nje, baba akamuangalia mkewe, kama anataka kumuuliza kitu.

Mkewe akawa kamuangalia mumewe kama anasubiria kuulizwa kitu, na alipoona mumewe hasemi neno, hakupoteza muda tena..huyoo..., mbio akamkimbilia mtoto wake kwa kutoka nje…..

Baba naye kuona hivyo, akaijiinua, na haraka akawafuata huko nje..nikabakia peke yangu...

Tuendelee na kisa chetu..


***************Hata mimi sikuweza kuvumilia, ikabidi na mimi niwafuatilie huko nje, na niliwakuta wote wamesimama, binti akionekana mwingi wa mashaka, akiwa bado anaangalia huku na kule akimtafuta docta,… na wazazi sasa walishamkaribia, na kuanza kumsihi arudi ndani, atulie, na mimi nilipofika pale waliposimama, nikamuuliza huyo binti;

‘Kwani wewe una mashaka gani,…sisi tunachotaka ni kuutafuta ukweli, na kama ni madhara tutayapata sisi, docta keshakuhakikishia kuwa mambo atayamaliza unawasiwasi gani, au kuna jambo unalolifahamu, ..’nikasema

Yule binti akatulia tu hasemi jambo, zaidi ya kuendelea kuangalia huku na kule na alipohakikisha kuwa doct ahayupo karibu akageuka kunikabili…akaniangalia kwa macho yenye hasira, hakusema neno.

‘Haya twendeni ndani…’akasema baba mtu, yule binti kwanza akawa katulia, sasa akiwa kageuka upande wa barabarani,…akawa kama hataki kurudi ndani.

‘Kwani unataka nini sasa…?’ akauliza mama yake

‘Nimesema twendeni ndani, …’akasema baba sasa kwa sauti ya ukali, na mdada akawa anageuka kama kuelekea ndani, na mama yake akasema akimuangali abinti yake..

‘Twende ndani unamjua baba yako keshabadilika hapo, unataka adondoke chini kwa hasira, …twende ndani…’akasema mama.

‘Mama nakuja wala usiwe na shaka na mimi, na wala baba hatadondoka,…ila ni muhimi ningelijua huyo docta anataka kufanya nini, …’akasema sasa wakawa wanatembea hatua ndogo ndogo kuelekea ndani, lakini mwendo wa pole.
‘Hebu niambie kuna tatizo gani..?’ akauliza mama.

‘Mama hakuna tatizo…..usiwe na shaka na mimi…’akasema na mama yake akasema;

‘Usinidanganye binti yangu ninakufahamu zaidi ya unavyojifahamu wewe, ukijiigiza ukiwa sawa, mimi nakufahamu, una tatizo, una kitu kinakusumbua, sasa usipotuambi asisi wazazi wako, unafikiri,  ..’akasema mama yake na kabla mama hajamaliza binti yake akasema sasa akiwa kasimama;

‘Kwahiyo mama wewe ulitakaje, maana mimi sio kwamba napenda haya, …ila ni kwa ajili yenu nawapenda sana wazazi wangu…siwezi nikakaa kimia wakati kuna watu wana nia mbaya,…mimi ni mkubwa sasa, ni wajaibu wangu kuhakikisha kuwa familai yetu ipo salama, haya yaliyotokea kwenye familia yetu yananitia uchungu sana, kwanini sisi, kwani tumewakosea nini hao watu…’akasema kwa sauti kubwa halafu akashusha na kuongea kwa.

‘Sasa kwanini hutuambii tatizo ni nini…ili tusaidiane…?’ akauliza mama.

‘Mama hakuna tatizo,…la mimi .  ila nahisi nyie mnalitafuta tatizo, na mimi siwezi kukaa kimia, hawa watu wawili watatuingiza kwenye matatizo makubwa sana…, nimefurahi kuwa wametusaidia tumepona, lakini huko wanapotaka kwenda, naogopa..’akasema.


‘Kwenda wapi sasa..wao wanachokifanya ni kile ambacho tulikuwa tukikihangaikia kwa muda mrefu,…mnakumbuka mimi niliwaambia nini, haya yaliyotokea tumuachie mungu, wewe na baba yako mkasema ni lazima tuutafute ukweli…mnaona sasa, ..kwahiyo matatizo mliyaanza nyie, wewe na baba yako…’akasema mama.

‘Lakini mama, tusingeliweza kukaa kimia,…ilikuwa ni wajibu wetu kufanya hivyo…na hata hivyo …hatuwezi kutulia, nilikuwa na mpango wangu wa amani, wa taratibu, lakini hawa watu wawili wamekuja kuharibu…’akasema akiniangalia kwa jicho moja.

‘Lakini kwa vipi, wao wamekuja kusaidia kumtafuta yule ambaye alisababisha binti yetu ajiue, sasa njia ya kufika huko ndio hii imetufikisha hapa binti yangu, je wewe unataka tuliachie hivi hivi, na wakati limeshafikia hapa,..’akasema mama.

‘Sasa kwa vile inazidi kutupeleka kubaya, basi tuachane nayo, kwani mwisho wa siku tutakaoumia ni sisi,hawa watu watakuwa hawapo,…wao wanachotafuta ni pesa,…unasikia mama, …mimi najua, lolote tutakalo fanya halitasaidia dada arudi,…hawezi kurudi, tumeshaombeleza vya kutosha, tumeshateseka vya kutosha, basi ….lakini hivi wanavyotaka hawa, mama kuna hatari huko mbele wewe hulioni hili..’akasema

‘Sawa twendeni ndani, tusiwape watu faida…’akasema baba ambaye alirudi na kumsikia binti yake akiongea, na aliposema hivyo akarudi ndani tena, na sasa mama naye akaelekea ndani, mimi nikabakia na huyo binti…na nilipona tupo peke yangu, nikamuuliza huyo binti swali;-

‘Nikuulize swali, hivi wewe unakubali kuwa dada yako alijiua mwenyewe..?’ nikamuuliza.

‘Si ndivyo ilivyoonekana, ..’ akasema kwa sauti ya ghadhabu kama vile ninamsumbua.

‘Nyie mlikubaliana na hilo..?’ nikamuuliza na sasa akainu auso na kuniangalia kwa macho yaliyojaa hasira, akasema;

‘Haya wewe niambie alikufaje,..nyie si madakitari, au labda nyie ni wanajimu au waganga wa kienyeji, tuambieni… mumegunduaje kuwa kama alinyweshwa sumu, ni nani alimnywesha, au hiyo sumu iliyonekana kwenye vipimo ni ipi, ..ni nani angelimuewekea maana siku nzimi nilikuwa mimi na yeye, alipokwenda huko chumbani kwake, ndio yakatokea hayo..’akasema.

‘Nikuulize kitu, nyie mnalalaje,…yeye ana chumba chake na wewe una chumba chako au sio?’ nikamuliza, kwanza alitulia kama vile hataki kujibu swali lakini baadae akasema;

‘Awali…tulikuwa tunachangia chumba kimoja..nyumba ina nafasi ya kila mtu kuwa na chumba chake,…lakini mara nyingi tulikuwa na wageni, wanandugu, kwahiyo tukawa hivyo, kulala chumba kimoja, tukazoea hivyo… lakini vinginevyo, kila mtu ana chumba chake..’akasema.

‘Siku ya tukio, hakukuwa na wageni, kwahiyo kila mtu alikuwa akitumia chumba chake au sio…?’ nikauliza.

‘Ndio…’akasema sasa akijibu kwa sauti ya kawaida.

‘Na ilipotokea tatizo, wewe ndiye uliambiwa uonyeshe dawa mlizonunua madukani…?’ nikamuuliza.

‘Ndio…’akasema.

‘Ukawapa polisi karatasi ambayo sio yenyewe…’akasema.

‘Sikugundua kwa wakati ule, maana vikaratasi vyote viliandikiwa hiyo dawa, kulikuwa na vibahasa viwili mle kwenye kabati,.. vinafanana..’akasema.

‘Ulikuja kugundua baadae au sio..?’ nikauliza

‘Ndio…’akasema

‘Iilikuwaje mpaka ukaligundua hilo…?’ nikamuuliza
‘Nilikuwa natafuta dawa, mara nikakiona hicho kibahasha,…nikagundua ndicho kile dada alipewa, nikajiuliza imekuwaje,…sikuwa na la kufanya..’akasema

‘Kwanini hukuwaambia polisi kuwa uligundua kuwa karatsi uliyowapa sio sahihi..?’ akaulizwa.

‘Sikuona umuhimu wake maana vikaratasi vyote vilikuwa sawa sawa…na nilishaona kuwa polisi hawana msaada wowote kwetu…’akasema.

‘Wewe si unahitajia dada yako apatiwe haki yake, sioni ni kwanini usiwaambie polisi maana inawezekana hizo dawa zikawa na kasoro. Labda ziliisha muda wake, ndio maana zikageuka kuwa sumu..’nikasema.

‘Hazina kasoro ni zile zile,..mimi nilizikagua..’akasema.

‘Docta anasema alipoangalia kwenye kabati, alikuta karatasi nyingine ya dawa hizo hizo, hiyo nyingine ilitoka wapi..?’ akaulizwa

‘Mimi sijui…kwani ilikuwa na nini ndani, na kwanini. mbona hakuniuliza alipoiona, sijamuona akiwa na bahasha nyingine ilikuwaje…hapana hakukuwa na bahasha nyingine sio kweli…’akasema akionyesha mashaka hapo

‘Naona una mashaka..naona kama unajua kitu kwa hilo, kwanini hutuambii ukweli tu…’nikasema

‘Ukweli upi,..uliza swali mimi nitakujibu, ili nafsi yako itulie, ..mridhike, muondoke zenu…’akasema

‘Sio kwamba hiyo nyingine ililetwa kuficha ushahidi na ile yenye sumu, ikachukuliwa..?’ nikauliza na yeye kwanza akashtuka, na kusema;

‘Mimi sijui hayo yanatoka wapi… na usitunge stori kwa jambo kama hili, nikuonye kwa hilo, …unanielewa, uwe makini sana,..umenielewa?’ akasema.

‘Nakuuliza wewe…unijibu, hilo halikupangwa ili kuvuruga ushahidi….?’nikasema na kumuuliza.

‘Kwanza sikiliza usinichanganye, wewe, au nyie ndio tatizo..hasa wewe unayejifanya dakitari wakati huna hiyo fani…, unajifanya mwema,eti unajua kuombea wakati sio kweli,..ok, labda yawezekana, lakini wewe sio mtibabu, wewe unatumia mgongo wa docta wako, nimeshakugundua wewe ni nani, sasa endelea kuchonga-chonga kama sitakuweka sawa..’akasema.

Kwanza nilishikwa na namna ya kutahayari, kwa maneno yake hayo, yanaonyesha keshanifahamu mimi na nani, na sijui kafahamu vipi, lakini nikajifanya kama sijali, nikasema;

‘Kwahiyo unanizuia nisiseme ukweli,..hupendi sisi kutafuta ukweli wa kifo cha dada yako ina maana wewe huna haja ya kuutafuta huo ukweli tena, bali wewe nawe una ajenda yako ya  siri, au.?’ Nikamuuliza.

‘Nauhitajia sana huo ukweli…, lakini sio kwa mtindo huo mnaokwenda nao, unaohatarisha maisha ya wazazi wangu, nimeapa kuwalinda wazazi wangu kwa nguvu zote..limetokea hilola dada, nisingelipenda litokee tena, labda kwa mapenzi ya mungu…’akatulia.

‘Kwahiyo unataka sisi tufanyeje, maana lengo letu ni kusaidia…hatuna cha zaidi..’nikasema

‘Kutusaidia au kujisaidia wewe mwenyewe…’akasema na kabla sijasema neno jingine akasema;

‘Mimi nitautafuta ukweli kwa njia yangu, nimeshagundua mengi,…, nina uhakika wanaohusika nitawang’amua hivi karibuni.., pamoja na vitisho vyao, nimeshajua hao watu wanahitaji namna gani ya kuja kuwanasa..lakini sivyo kama mnavyotaka nyie, mtaitia familia yetu matatani,,, unanielewa, kwahiyo take care ..’akasema.

‘Huko kuwalinda wazazi wako kwa njia hiyo ni kwa muda tu, sisi tunataka kuwalinda nyote kwenye njia sahihi ya kudumu,..na kuhakikisha kundi hilo limesambaratika,.. na hilo unalosema kuwa umeshanifahamu, sawa kwanini husemi ukweli kuwa mimi ni nani, …mimi siogopi kwa hilo…’nikasema.

‘Sitaki kusema huo ukweli, kwasababu wewe na huyo mwenzako mnaujua, sasa kwanini niuseme…na naikisema …nina uhakika utaharibu mambo mengi,.. maana najua muda wake utafika, na ukweli huo utabainika…unielewe hapo…’akasema kwa kujiamini.

‘Muda gani huo, na mambo yanazidi kuwa mabaya..’nikasema

‘Yanakuwa mabaya kwasababu yenu…vinginevyo, nilishaanza kuyaweka sawa…’akasema

‘Kwa vipi na wewe ulikuwa unaumwa…?’ nikamuuliza

‘Kuumwa kwangu..kunatokana na nyie..hamlijui tu, aah, tuyaache hayo,ila..nakuhakikishia muda ukifika utaumbuka, nitahakikisha unakwenda jela,…unasikia hilo nimeahidi…’akasema akiniangali kwa macho makali.

‘Kwanini niumbuke..wakati muda huo ukifika kila kitu kitakuwa wazi, kuwa mimi sihusiki kwa hivyo mnavyofikiria nyie,…ni kweli labda, nahusika kwa namna ambayo, sikuwa na lengo baya..lakini sio kihivyo, mnavyofikiria nyie,kwanza unajua wazi kuwa dadayako hakujiua, au hilo hujaligundua…’nikasema.

‘Hebu tuyaache hayo..maana kama nyie mnavyochunguza yenu , hata mimi nachunguza kivyangu, …sema mimi baada ya kuugundua ukweli, ndio nikaanza kuchanganyikiwa…sijui ni wao au ni kwanini,…nitaligundua tu…ila nilikuja kupata onyo kuwa hiyo ni mwanzo tu,..nikicheza baba anaondoke…keshaanza, …’akatulia

‘Akina nani hao, mbona huwataji..?’ nikauliza

‘Siwezi kuwataja maana sijawajua ni akina nani, na kiukweli …uonavyo kwa nje sivyo ilivyo kwa ndani, mtawakisia watu wengine kabisa, ambao hawahusiki kabisa, watu ambao ni njaa zao tu wamenaswa huko…,lakini wenyewe haswa, ni ndoto kuwapata, ..sijui…labda kama mnamiujiza…’akasema

‘Unajua unanishangaza, kwanini hutaki kushirikiani na sisi ili tuje kuupata ukweli pamoja,hili ni kwa manufaaa ya familia yako, sio kwangu, au kwa docta..’nikasema

‘Hahaha, eti sio kwa faida yenu, una uhakika na hilo….ila nawaonya tena hivyo mnavyokwenda, haiwezi kuwa na manufaa kwa hii familia abadani, mnachotaka kukifanya kitaiangamiza hii familia,..’akasema

‘Kwa vipi, ndio maana naanza kuwaogopa,hamuwajui hao watu walivyo, kuuaa kwao ni kama kuua mbu..hawajali, na wanaju awatauaje kiasi kwamba hata uchunguzi ufanyike je hakuna wakuweza kuwagundua…’akasema

‘Kwahiyo wewe unawafahamu..?’ nikamuuliza

‘Sio kwa moja kwa moja…lakini wapo,…watu wanaongea, hata kwenye mitandao wapo,…ila kumnyoshea kidole kuwa ni huyu, inakuwa ni vigumu, na kama mwenyewe ukafanya hivyo,..utaingia matatani, wana wanasheria, wana-ulinzi, wana kila namna ya kujilinda, na ole wako uingie kwenye anga zao…’akasema

‘Wanaitwaje hao watu kwa jinsi watu wanavyowasema, ni lazima watakuwa na jina, mahali nk..au..?’ nikamuuliza

‘Huko siwezi kujua maana hata mimi najiuliza hivyo, nimefanya uchunguzi wangu na kugundua kuwa watu kama hao wapo kweli..lakini kwenye kificho, ni ni…ndio maana wanaitwa mashetani, unajua…kwasababu ukiatafuta kwa njia halisi huwezi kuwapata,ila wapo wanafanya kazi, wanazalisha vyovyote iwavyo, kwa mbinu zao..na wakikuona unafaa watakuchukua, …’akasema

‘Unafaa kwa vipi…?’ nikamuuliza

‘Oh, unajua unaniuliza maswali ambayo hata mimi nahangaika nayo, kwanini wanamchukua huyu awe mtu wao, kwanini, wanaua, kwanini…hayo ndio hata mimi najiuliza…sasa siwezi kukujibu kihivyo,…ila nijuavyo, kama wakikuona ni tishio kwao, kama wakikuona …basi hawasiti kukumaliza, lakini kingine wanahitajia wanachama kutokana na sifa wanazozihitajia wao…urembo, mvuto, akili, kipaji..wanajua wenyewe wakikuona unafaa, na….watakujaribu, na ikishindikana, wanajua cha kukufanya, ndio hivyo siwezi kusema zaidi..’akasema.

‘Umewezaje kuyafahamu hayo…?’ nikamuuliza

‘Kwenye mitandao….humo wanatumia sana,…na zaidi ni kulinganisha matukio, ..na ujanja ujanja…likikukuta ndio utajua, lakini kama halijakukuta, huwezi, …haya mambo yapo, na yapo…na …chunga sana…’akasema

‘Nikuulize kitu, wewe una mpenzi kwenye facebook..?’ nikamuuliza akaniangalia huku uso umesawajika, kama anatabasamu lakini ile tabasamu ya dharau, na huku  ananikagua nina maana gani…mjanja sana huyu binti.

‘Mpenzi kwenye facebook ndio nani…una maana gani mpenzi wa facebook, maana hilo neno tata, kila mtu anayejiunga na facebook, anakuwa na mpenzi, au ukimuadd mtu anakuwa ni mpenzi wako wa facebook, au sio…sasa ukiniuliza hivyo nashindwa kukuelewa….’akasema.

‘Wewe umesema umechunguza na upo mbali kwenye uchunguzi wako, na kama ungelikuwa mbali kihivyo ungelikuwa umeshaligundua hilo,…kuwa watu hawa wanatumia mitandao kupata wapenzi wao, au sio….sasa mimi ndio nikakuuliza je unaye mpenzi wako kwenye facebook..?’ nikamuuliza

‘Sina kama ndivyo nilivyokuelewa, sina na sina haja naye, wa nini kwanza, wa kunitia kwenye matatizo..’akasema akikunja uso

‘Ina maana sio wewe…’nikasema halafu akacheka kuzarau fulani hivyo

‘Hahaha..eti sio mimi,….lakini una maana gani, sijakuelewa, sijui una maana gani, sio mimi kwa vipi, ni kweli sio mimi kama ulikuwa na maana yoyote kunihusu mimi, sina mpenzi yoyote,maisha yangu ndivyo yalivyo…’akasema

‘Basi usijali…utakuja kunifahamu nina maana gani, siku ukikamilisha uchunguzi wako…ila nina uhakika, una jambo kuhusu hilo…ama unatumiwa, ama …unafanya kwa vile unajua ufanyavyo hivyo, ndio unaisaidia familia, lakini sivyo hivyo…nikuambie ukweli…’nikasema

‘Huna swali jingine la kuniuliza..’akasema akiniangalia moja kwa moja usoni

‘’Huyo anayemiliki super market, mumeanza lini kufahamiana na yeye..?’ nikamuuliza

‘Mhh..kwanza nikuweke sawa, kama ni mawazo yak ohayo…wanaume mnapenda sana kukimbilia huko…, mimi huyo mtu sina mazoea na yeye ya kimapenzi,…zaidi y akuwa awali alikuwa akinifua fuata, kwa ajili ya kumtaka dada, baadae akanitaka na mimi, nikampiga fully stop…. na ikafikia sehem akasalimu amri,..unanielewa, kwahiyo dhana yako, kama ndio hivyo, ifute,…, sio kweli, ..zaidi ya ninavyomsikia kuwa yupo hivyo, ni hivyo tu sio zaidi....’akasema

‘Unamsikiaje kuwa ni nani..?’nikamuuliza hapo akakaa kimia kama anawaza jambo, hakusema neno, nikaona niachane naye huko, nikamuuliza swali jingine

‘Sasa mbona umekubali kuwa utashirikiana nasi ili uweze kukutana na huyo jamaa, au si ndivyo ulivyokubali hivyo..?’ nikamuuliza

‘Kwasababau hata mimi nilikuwa natafuta mwanya huo, ninajua kwa hivi sasa nitaweza kulifanya lile nililolikusidia nikijua kuna watu wapo nyuma yangu,tutasaidiana nao,..lakini baadae itakuwa kwa masilahi yangu na familia yangu, siwezi kwenda zaidi kama mnavyotaka nyie, kwasababu hamjui hicho mnachotaka kukiingia…’akasema

‘Sijakuelewa masilahi una maana gani..?’ nikamuuliza

‘Nitakuwa nimepata ushahdi wa kukuweka wewe ndani,..hilo ulielewe, ninajua baada ya hapo kila mtu atakuwa kakufahamu wewe ni nani..na wewe uliifanyia nini hii familia… na ikibidi hata huyo docta maana nimeshawajua nyie ni akina nani, kwahiyo huko najua nitawafahamu mahusiano yenu na hao watu,…’akasema

‘Oh, tunarudi kule kule…kwahiyo wewe unatushuku kuwa labda tumetumwa kuwachunguza, kwa manufaa ya hao watu au sio…’nikasema

‘Ndio hivyo, sina zaidi cha kukuambia kuhusiana na hayo, sijagundua mengine, muhimu nawaombeni, achaneni na hayo mambo …msije kui-ingiza hii familia yangu kwenye matatizo, tumeshachoka jamani, hebu na sisi mtuache tuwe kama binadamu wengine,..ndio ombi langu kwenu, pleaseee!…’akasema

‘Labda wewe ndio uwe umetumwa na hao watu, au labda, unaogopa tu..kuwa tukiendelea wanaweza kuidhuru familia yako,lakini vinginevyo,..sisi hatuna nia mbaya, nia ni kukusaidia, wewe na familia yako..’nikasema

‘Hahaha, eti kunisaidia mimi na familia yangu, baba alijaribu kwa njia hiyo unaona kilichompata, yeye hanielewi,..hata mimi nahis ndio hivyo,… sasa nyie…mtawezaje, ndio maana niliamua kujitolea kwa namna nijuavyo ni sahihi, na nina uhakika nitawashinda tu,ila sio kwa msaada wenu , …’mara simu yake ikalia mlio nahisi ilikuwa mlio wa ujumbe wa maneno, maana aliichukua simu yake na kuanza kuiangalia,

‘Sasa unaona nilijua tu, hivi jamani, hamunielewi, angalia sasa, …nimetumiwa ujumbe huu, hebu uusome..’akasema akinionyesha kwenye simu yake, kuna picha ya…yule mlinzi akiwa kalala kitandani, inaonyesha ni hospitali, na maandishi yenye rangi nyeusi chini yake, yakisema;

Waonye hao vikaragosi wako…, kati yao kuna atakamfuata huyu..keshatuambia yote wanayotaka kuyafanya…, na wewe kama hutaweza kuwafukuza hao watu kwenye familia yako, usije kutulaumu kwa hilo litakalotokea…’

**********
 Wakati nausoma huo ujumbe, ….

 Na mara akaja docta, alionekana na huzuni sana usoni, akamuangalia mdada, na kusema;

‘Vipi, mbona mpo nje..ni muhimu twendeni ndani maana polisi wanakuja,…’akasema

‘Wanakuja kufanya nini..?’ nikauliza kabla docta hajajibu mdada akasema;

‘Mnajua nyie mnatuletea sasa matatizo, haya huo ujumbe una maana gani,..na sasa unasema polisi,…ndio hayo tulikuwa tunayakwepa, wazazi wangu wanahitaji kupumzika, baba ndio huyo katokea hospitali hajapata muda wa kupumzika, ….sasa mnazidi kunichanganya, polisi wanakuja kufuata nini tena..’akasema akimuangalia docta.

‘Ni wajibu wao,…wanafuatilia kuhusu hiyo kadhia ya hivyo viungo vya binadamu, na wanatushuku sisi, wanasema au wanataka tukaisaidie polisi, unajua wakisema hivyo wana maana gani..nisingelipenda hilo , maana tutapoteza muda mwingi kituo cha polisi, na hatutakuwa na muda wa kuyafuatilia haya mambo,…’akatulia

‘Kwahiyo una maana tunaweza kuwekwa ndani…?’ nikauliza

‘Ndio maana yake, jiandae kwa hilo,…na nilijua…tu, ule ni mtego,…lakini hata hivyo, hawana mshiko…ushahidi wao hauna nguvu, …ila nahisi kuna nguvu nyuma yao, ..si bure, pesa inafanya kazi…’akasema docta.

 ‘Kuchanganyikiwa kwangu kumenifanya nirudi nyuma sana,  kiukweli
nawashukuru sana kuwa mlikuja kwenye wakati muafaka, kipindi ambacho nilishakata tamaa…sasa hayo ya huko polisi mumejitajia nyie wenyewe ..sitaki waje kumgusa baba yangu, wawachukue nyie…’akatulia kama anawaza jambo halafu akasema;

‘Hata hivyo, kunisaidia kupona sio sababu ya kunifanya nishindwe kutimiza wajibu wangu,… nawashukuru sana, ila sasa nawaomba muondoke,  kabla hamjaiingiza hii familia yangu kwenye matatizo, hamjui tu…’akasema na sasa akaanza kutembea kuelekea ndani..

Kabla hata hajaingia ndani….gari la polisi likawa linakuja kwa kasi…;

‘Polisi hao wanakuja,…’ alisema docta,  na mdada akakimbilia ndani, …

NB: Polisi wanakuja kumata nani…


WAZO LA LEO: Haki inapogubikwa na dhuluma, ikawa wenye mali, na uwezo wanaaangaliwa kwa jicho la kulia, huku walala hoi, wananchi wa kawaida wanaangaliwa kwa jicho la kushoto, na haki ikawa inapindishwa kutegemea na mueleo wa jicho, ujue hapo amani itakuwa kitendawili. …
Ni mimi: emu-three

No comments :