Nilipoona siwezi kumuona au kumuacha, nikatafuta njia nyingine, kama nilivyosema moyoni mwangu nimejijengea tabia ya kutokuogopa kirahisi, hapo mimi nikatafuta ujanja, nikaanza kutembea kuelekea kule walipokuwa wamekaa watu wengine.
Na hilo zoezi likafanya kazi,…nilipowakaribia watu nikahisi huyo jamaa hayupo tena, nikasema ngoja nirudi nielekee sehemu nyingine , sehemu ya mapokezi, nikahisi huyo mtu akiwa karibu name tena…,
'Hivi wewe nani..?’ nikauliza
Sikupata jibu, nikaona narudi muelekeo ule wa awali, pale walipokaa watu, ilikuwa eneo la wodini,… nikagundua, nikielekea muelekeo huo, huyo mtu, au au huo mwangwi wa mtu unapotea.
Basi nikaona nielekea huko eneo la wodini, hadi sehemu watu wanaposubiria kuingia kuona wagonjwa nikaa kwenye benchi, na pale walikuwepo watu kadhaa, sikuweza kuhisi mtu kuwa karibu nami, basi nikatulia hapo, na wale watu waliokuwa wakisubiria kuingia kuona wagonjwa, nikasikia wakiongea jambo…
'Huyo mama wa ajabu kweli, ….kachanganyikiwa lakini akikuelekeza jambo, ufanye unafanikiwa na ukiwa na tatizo lako anakulekeza…na kila mtu aliyeagizwa afanye hivyo, akifanya hufanikiwa ….yaani imekuwa ni ajabu ya mwaka…’akasema mtu mmojawapo.
'Unajua hata mimi jana nilikuwa nabisha , nikaenda kumuona akaniambia shida yangu, sijui alijuaje..basi nikafanya alivyosema nifanye nikaitatua, sasa leo nina shida nyingine nataka nimuone nione kama atasemaje…’akasema.
'Kwani inakuwaje…unatakiw ufanyeje…?’ nikawauliza.
'Wewe unaingia hapo kwenye hicho chumba, kuna mdada kachanganyikiwa lakini cha ajabu, yeye ana sijui miujiza gani, hao manesi wanamtumia kama mradi maana ili umuone ukiingia unaweza pesa mezani,..halafu wewe ukimsogelea tu anakutajia shida yako na jinsi gani ya kuitatua…’akasema jamaa.
'Ni mganga wa kienyeji?’ nikauliza
'Wala, huyo kaleta hapa akiwa kachanganyikiwa tu, ila ndio hivyo, kama una tatizo, ingia, na weka mia tano mbele yake, ndio ushuru wake, utashangaa atakachokuambia.
'Una matatizo yako ya kuchanganyikiwa, ukitaka kupona, nenda ukamuoe huyo mpenzi wako wa facebook, shida zako zitakwisha….’akasema
Huyu m-mama, kajuaje hilo,… mpenzi wangu wa facebook…lakini cha ajabu zaidi eti ili niondokane,na tatizo langu inabidi nimuoe huyo mpenzi wa facebook, nitamuoje wakati sijawahi kumuona..
'Mna uhakika na hayo maneno ya huyo mama aliyechanganyikiwa,…’ nikauliza.
'Ndio… hakuna aliyewahi kuambiwa akashindwa kufanikiwa…’akasema huyo jamaa
'Hata akikuagiza umuoe shetani…?’ nikauliza.
'Hawezi kukuagiza kitu ambacho hakiwezekani..’akasema huyo jamaa.
'Hahaha, hawezi , mbona mimi kaniagiza nikamuoe mtu ambaye sijawahi kumuona na watu wanasema huyo mtu ni shetani..’nikasema na watu wakabakia kuduwaa, na mmojawapo akasema;
‘Hebu rudi ena huenda hukusikia vyema,…’akasema na mimi nikaamua kurudi tena ndani.
'Wewe nimekuambiaje, nenda kamtafute huyo mpenzi wa facebook, umuoe, si una mpenzi wako wa facebook, au…’, akasema kwa sauti ya ukali.
'Huyo mpenzi wa facebook, hayupo, wengine wanasema huyo ni shetani, wengine wanasema ameshakufa, na sijui niamini kipi…’nikasema.
'Na wewe unasemaje, ..?' akaniuliza kwa sauti ya ukali, kabla sijajibu akasema
Basi nikatoka mle ndani nikiwa sina shauku tena na hayo mambo niliona ni mambo y akunichanganya tu kichwa changu,..isitoshe huyo mama kachanganyikiwa anaweza kuongea lolote tu.
'Ulikuwa wapi wewe…?’ akaniuliza docta.
'Nilinyosha miguu kidogo nikaenda wodi zile kuangalia wagonjwa..’nikasema.
'Sasa,sikiliza, nimeshapata kibali cha kumuhudumia huyo binti, na nimeweza kumuona, japokuwa sikuweza kuongea naye.. hatikisiki, yupoyupo tu, na dawa ninayoijua kwa hivi sasa ni wewe uende ukaongee naye…’akasema.
'Docta, kama wewe umeshindwa kuongea naye, huyu mwanafunzi wako atawezaje kuongea naye, …?’ akauliza huyo mzee.
'Hilo niachie mimi na mwanafunzi wangu,…huyu mwanafunzi ana kipaji,..ndio maana nikamchukua, akikutana na huyo binti, ataweza kufanya maajabu, wewe subiria tu…’akasema docta, na kiukweli sikumuelewa huyo docta ana maana gani, maana mimi sina kipaji kama hicho.
Mara docta akanisogelea na kuninong'oneza jambo sikioni, sikuamini alichoniambia, nikabaki nimeduwaa…nashindwa kukataa au kusema lolote, na mara docta akasema;
'Nakupa nusu saa nitakuja kuona matokea yake, usichelewe ni nusu saa tu ukichelewe utaharibu, …, uwanja ni wako, na ole walo uniangushe…’akasema docta.
Nikabakia nimeduwaa, na mara akilini nikaanza kusikia sauti ikiniambia, ni ile sauti ya yule mwanamama aliyechanganyikiwa, ilikuwa ikisema;
'Unakwenda wapi sasa, hutaki kumuoa huyo mpenzi wako wa facebook, hutaki matatizo yako yaishe, ukumbuke, na wewe unaumwa…wewe unajali wenzako zaidi ya kujijali wewe, kwanza fuatilia matatizo yako…, na kupona kwako ni kumuoa huyo mpenzi wako wa facebook,...'nikasikia sauti hizo zikinighasi kichwani.
Nikaanza kutembea kuelekea kwenye mlango wa hiyo wodi aliyolazwa huyo binti..wa sasa ni hatua ya mwisho, kuamua nimuoe nani, mpenzi wa facebook au huyo binti, kilema, aliyechanganyikiwa…
Nikashika mlango, nataka kuusukuma na mara nikahisi kitu, au mtu ananishika begani, nikageuka nyuma simuoni mtu…
Ni mimi: emu-three
No comments :
Post a Comment