Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, April 17, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-7 Mpenzi wa facebook, kazua mambo,...kafukua dhuluma iliyokuwa imejificha, ni kisa kinaendelea, na docta kaamua kulifuatilia hili tatizo, je ni kwanini docta aamue, kulifuatilia, badala ya kutoa tiba, ni kwanini aamue waende mguu kwa mguu hatua kwa hatua, hadi kwenye chimbuko la tukio,..hebu tuone sehemu hii muhimu uone wenye kujua taaluma yao wanavyofanya kazi,

                                                ************

‘Siku moja nikaamuuliza baba  yake huyo binti, kwanini binti yake hataki kuolewa, na ana bahati ya kupata wachumba wazuri tu…?’

Baba yake hakuwa na jibu zaidi ya kusema, hajui….mimi nikasema moyoni, huenda bado wanachuja, ili wampate mwenye nazo zaidi…lakini muda ulishapita, makamo ya huyo binti wengi walishaolewa.

‘Sasa baadae ndio nasikia, msiba, kwa bwana mashauri, nauliza msiba wa nani, wanasema msimba wa mtoto wa kwanza wa huyo bwana…mimi mbio mbio nikafika kwake,…kilio, kila mtu kataharuki, namuuliza baba mtu ni nini, hana la kusema.

Basi nilisubiria hali ikatulia, nikamdadisi vyema, ndio akanitonya kuwa binti yake kazidiwa, na dalili za mwanzo zaonyesha kama kanywa sumu, lakini bado hana uhakika, …nilishikwa na butwaa, kwanini binti mrembo kama huyo mpole, ..afikie hatua hiyo…

‘Kwanini amejiua..?’ nikamuuliza

‘Sijui…aheri ningelijua ingekuwa bora…’akasema

Sasa wakati anachunguzwa na madocta nilikuwepo, na ripoti inakuja kwa baba mtu na mimi nipo nyuma, akaambiwa binti yake kanywa sumu…,

‘Na zaidi alikuwa na mimba, bado change…’akaongeza docta.

Baba mtu alinywea, aligeuza uso huku na huku, hasira, chuki, kutahayari, maana alikuwa mtu kajijenga heshima zake, watoto wake ni watoto wa geti kali, …na zaidi huzuni kwa kufikiwa mtoto kipenzi chake.., baadae ndio nikamuuliza baba mtu.

‘Ulikuwa unajua kuwa huyo binti yako ana mimba, akasema alikuwa hajui, …labda mama yake, na mama yake alipoulizwa naye akasema alikuwa hajui,…

‘Basi iwe siri yenu, msije kulisema hilo…’nikawashauri..na kweli ikawa siri ya familia, na mimi kwa mara ya kwanza ndio nawaambia nyie…’akasema huyo mzee

‘Ahsante sana mzee, umetusaidia sana…’nikasema

‘Lakini hiyo kauli yake ilinitisha,….’akasema.

‘Kauli gani…?’akauliza docta.

‘Kuwa siku akimpata huyo aliyemfanyia hivyo huyo binti yake, atakachokifanya anakijua yeye mwenyewe, ama zake ama za huyo mtu…alitamka hayo mbele yangu…na jamaa anajulikana kwa hasira, tokea enzi akiwa jeshini…mimi namfahamu sana, akidhamiria jambo ukae mbali na yeye’’akasema huyo mzee.

‘Mhh…’mimi niliguna nikajua huko hakuendeki tena, nikamtupia jicho docta, na docta akaendelea kumdadisi akitaka kujua mengi, mimi kwangu niliona haina umuhimu tena, muhimu ni kurudi huko tulipotokea…

‘Kwani huyo marehemu alizikwa wapi…’nikamsikia docta akiendelea kumdadisi huyo mzee, hapo na mimi akili ikafunguka, nikatega sikio kusikia jibu..,

‘Amezikiwa sehemu inayojulikana kama ‘Makaburini ‘

 Hapo utasemaje tena…kama huamini tena basi ujue una uhimili wa ina yako..

Tuendelee na kisa chetu..

***********

‘Siulisema wewe huna hulka ya kuogopa, au sio,  sasa unasemaje…twende tukakabiliane na hiyo familia, au unasemaje?’ nikaulizwa na docta, muda huo tulishaachana na yule mzee mwenye nyumba maana alikuwa na safari zake nyingine, tulifanya hivyo baada ya kubadilishana namba za simu.

‘Mhh, docta, hapa sio swala la kuogopa,….  ni kwamba nikienda huko nitaenda kutonesha kidonda, na na nakwenda kufanya nini, hebu niambie hapo na wewe,…unielewapo hapo docta, sio kwamba naogopa, haya,..fikiria mwenyewe kwa makini utaona ni kwanini nachelea kwenda huko!..’nikasema na docta akaniangalia huku anatabasamu, hakusema neno na mimi nikaendelea kujitetea.

‘Kumbuka docta, tatizo hili lilitokea siku nyingi,  na hao watu watakuwa angalau wameshaanza kuzoea, japokuwa sio kusahau…kiukweli inasikitisha sana, na inaniumiza ikizingatiwa kuwa tatizo na chanzo cha hayo yote kimeelekezwa kwangu,…lakini, mimi sikujua hayo yote…’nikasema.

‘Kwahiyo unasemaje?’ docta hatimaye akaniuliza akiniangalia usoni.

‘Tuachane kabisa na hili jambo…huo ndio uamuzi wangu…’nikasema na docta akatulia kimia kama anawaza jambo fulani halafu akasema.

‘Kwahiyo wewe upo tayari kuendelea na huyo mpenzi wako wa facebook, au sio..upo tayari kuendelea na matatizo yako hayo ya kuchanganyikiwa au umeshapona baada ya kusikia haya…?’ akaniuliza.

‘Mhh…mimi sijawa na uhakika kuwa huyo mpenzi wa facebook ndio huyo marehemu, je wewe una uhakika na hilo docta,..?’ nikamuuliza docta na docta hakunijibu hapo hapo, na mimi nikaendelea kusema;

‘Kama ni swala la kuachana na huyo mpenzi wa facebook, kwani kuna tatizo mzee…, naweza kuachana naye, tu, si najitoa facebook, au nabadilisha akaunti, … ‘nikasema.

‘Na hizo njozi, na huko kupagawa, …unaongea peke yako, au uniambie huko kuongea peke yako labda kuna mtu unaongea naye, ni nani huyo…., mbona husemi,…au hujioni kuwa haupo sawa..hebu jiangalie ulivyo, ndivyo ulivyokuwa siku za nyuma, usharobaro wote kwishinie…, sasa hivi upo kama muokota makopo barabarani, hivi hujioni…’akasema na mimi nikajikagua na kusema.

‘Docta ndio maana nipo kwako, …mimi kiukweli sijijui kabisa…kuna muda nakuwa kama sio mimi….sielewi,…kama nimewakosea, basi wanisamehe….mimi sijijui docta…’nikasema sasa nikitaka kama kulia.

‘Kama unahitajia msaada wangu inabidi ufuate yale ninayokuambia, …’akasema docta.

‘Lakini docta hayo mengine mbona utanitia kwenye kuamini mambo hayo, wakati mimi sitaki kuyaamini, na kwa mfano, mimi ninaamua kumuuliza huyo mpenzi wa facebook, kuwa nimegundua kuwa yeye sio mtu, huni kuwa atanicheka sana…’nikasema

‘Kwanini akucheke…?’ akaniuliza docta

‘Unajua docta katika maongezi yetu mimi na yeye huko nyuma, mambo tuliyokubaliana ni kutokujishirikisha a mambo ya kishirikiana, yeye alisema mambo hayo hayaamini na hajishirikishi nayo, na nikaona ni mtu tunaendana, leo hii nimwambie kuwa nimegundua kuwa yeye sio mtu….’nikasema.

‘Nani kakuambia mwambie hivyo…..au hayo anayokuambia wewe umeshaniambia yote, au mengine unaficha…’akasema docta

‘Docta kiukweli mimi sina imani ya kishirikina ndivyo nilivyo,…kama nikuota, ni ndoto tu, hata nikukuambia itasaidia nini..ina maana nikikuambia nitakuwa nayaamini mambo hayo, mimi sio mshirikina docta…’nikasema

‘Kwahiyo haya mambo tunayoyafanya sasa hivi ni mambo ya kishirikina…?’ akauliza docta.

‘Kama itakuwa mambo ya kuamini uchawi, mashetani, ..hakuna jina mbadala na hilo, mimi siwezi kuwa mnafiki, …docta mimi nazungumza ukweli kutoka moyoni mwangu, kwa jinsi ninavyoamini, kama ninakosea basi unisamehe….,huko tunakoelekea tutajiingiza kwenye mambo yakishirikina,…. au nimekosea,..tunakuwa tumejiingiza kwenye imani za giza…mimi docta nashauri tuachane kabisa na mambo haya…’nikasema.

‘Kijana, ujue hili sio swala la  jinsi unavyofikiria wewe, na safari yetu hadi kufika hapa ni kuhakiki, je huyo mpenzi wako wa facebook, yupo hai,…. anaishi, na kama yupo tutampataje, haya tumefika hapo kwa huyo mzee, tumeambiwa alishafariki, hapo unataka kusema nini….’akasema docta.

‘Basi sio yeye,…huyo wa facebook ni mwingine,…huyu na huyo marehemu hawaendani kabisa ….docta, mimi kitu kinachonilinda nisiamini hilo ni sura…na kwasababu hii, kwangu mimi ninaona huyu tumtoe katika kufuatili kwetu,….labda tuanze kumtafuta mwingine…’nikasema.

‘Ni nani mwingine mwenye hulka na tukio kama hilo, kuwa uliachana naye kwenye mazingira kama hayo, ulimtenda,…ulimdhulumu…. na ukaja kuachana naye, bila ya masikilizano, ni nani, nitajie mwingine…?’ akauliza docta akinikagua usoni.

‘Mwingine mwenye tabia kama huyo marehemu au huyo mpenzi wa facebook….maana hapo unanichanganya,…?’ akauliza.

‘Kama huyu marehemu…’akasema docta.

‘Mhh, kama huyo marehemu hakuna..., na nilishakuambia hao wengine walikuwa ni wa kupita ti, sina kumbukumbu nao,…sasa labda hao wawili, lakini haoo wawili wengine walishaolewa, na nakutana nao, tunaongea vizuri tu…, sijui hata nikumbukeje, inakuwa kazi kubwa, muhimu docta tuachana na hili zoezi, unasemaje docta…’nikasema

‘No…unajua nikuambie kitu, sisi kuja kuonana na hii familia ni sehemu muhimu ya tiba yako, sio kwamba najifanyia tu kama mshenga….na kwa jinsi jambo lilivyo, hutaweza kupona mpaka uonane na hiyo familia,ili  kupatikane suluhu fulani, na itapatikanaje kama usipokutana na wazazi wa marehemu..ulitenda kosa, unakubali hukubali…?’ akauliza docta.

‘Ndio nakubali, kuwa nilitenda kosa, na kipindi hicho nilikuwa sijatulia,….na nilitenda bila kukusudia…sikujua….mbona wengi wanapitia huko docta...ni kipindi tu cha ujinga...’nikajitetea.

‘Bila kukusudia, wakati ulisema ulifanya juhudi za kila namna ili umpate huyo binti wa watu, na ukafikia kununua pete ya dhahabu badnia, ukaitisha shughuli, ukamvika pete,..baada ya hapo sijui ulimfanyaaje mpaka akakubali, ukatembea naye, kweli si kweli..je hiyo ni bahati mbaya…?’ akauliza docta.

‘Ni ujana tu…’nikasema

‘Ni ujana, ulikuwa na umri gani…?’ docta akauliza

‘Aah, ..unajua docta umri unaweza ukawa mkubwa lakini akili bado ikawa haijatulia, hujasiki wazee wanafanya mambo ya ajabu….’nikajitetea.

‘Muhimu ni jinsi gani ya ….tunachokifanya sasa kwenye sehemu ya tiba yako, ni kutafuta jinsi ya kuliondoa hilo kosa, sio jinsi y akutafuta visingizio vya kukwepa kosa, je unajua jinsi gani ya kuliondoa kosa ulilomfanyia mwenzako…?’ akauliza docta.

‘Ni kutubu, ni kuomba msamaha, hilo nalitambua sana docta, I wish angelikuwa hai ningelimuendea na kumpigia magoti mpaka anisamehe…’nikasema

‘Sasa utakwenda kutubu na kuomba msamaha kwa nani,..?’ akaniuliza

‘Si ndio hapo sasa docta…, huyo ambaye nilimkosea hayupo duniani…basi mimi nitamlilia mola wangu ninajua mungu ni mwema, atanisamehe tu…’nikasema

‘Ni rahisi hivyo, kwa vile sio wewe uliyendewa au sio…’akasema docta.

‘Sasa docta nitafanya nini , maana hao waliobakia, hawawezi kunisaidia kwa hilo…na nikiwaendea wao, inaweza ikawa chanzo cha kuzua uhasama na chuki nyingine dhidi yangu, unamfahamu huyo mzee au unamsikia, mzee Mashauri alishawahi kutuchapa mimi na mtoto wake mbele ya wenzetu, sitasahau, mpaka nikikutana naye nanywea, hapana siwezi kwenda kuonana naye…’akasema

‘Ili tiba yako ikamilike, inabidi kufukia haya madhambi uliyoWAHI kuyafanya, na hatua ya kwanza ndio hiyo,….kuhakiki kama kweli kitu kama hicho kilikuwepo…’akasema

‘Sawa hata mimi nimelikubali hilo, nakiri nilifanya kosa…’nikasema

‘Na kama tumegundua ukweli kuwa ulitenda kosa, na katika kutenda kosa, kosa likizaa makosa mengine, haya tusema kosa la kwanza, kama ulivyodai utamuomba mungu akusamehe, au sio…kwa vile uliyemtenda hayupo tena duniani, lakini ukumbuke, kama alivyosema mzee pale, kuna mlolongo wa makosa mengine yamekuja kujitokeza kutokana na kosa la awali, nikuulize je hayo makosa mengine, utayafanyaje, na je unahisi hayataendelea kuzaa makosa mengine…?’ akauliza docta.

‘Sasa docta unatia chumvi, unakuza haya mambo,….maana hayo mengine sihusiki tena mimi..ina maana ukitenda kosa, wengine wakaendeleza kosa kutokana na hilo kosa , mimi nakuwa lawamani, ndio kinaitwa kizalia, au….?’ Nikauliza

‘Unaniuliza tena mimi swali….’akasema docta.

‘Ndio …..maana hayo mangine sikuwepo kabisa… na kwanini yazae makosa mengine,…kwanini iwe ni kwangu tu, kwani ni mimi wa kwanza kuanza kuyafanya hayo, hapana, hata mungu anaona, atanisamehe, maana sikuwepo, sijawaambie wafanye hivyo …’nikajitetea,

‘Sio wewe kwa vipi, wakati sababu ya makosa haya mengine tatizo ni wewe,, chanzo ni wewe, usikwepe kosa, hilo, ndio maana tunaambiwa kuwa dhuluma ni mbaya inaweza kumea, na kuhatarisha maisha mengine, ikazua dhuluma nyingine,..sasa ni bora kuikwepa hiyo au kutafuta njia ya kuisimamisha hiyo dhuluma isiendelee…’akasema docta

‘Hata sikuelewi docta…’nikasema

‘Unajua wewe ulimtenda mtoto wa watu, alichokifanya ni nini, …?’ akauliza

‘Sikumwambia anywe sumu, na wala sikujua kuwa ana mimba…’nikasema

‘Jibu swali…’akasema na mimi nikawaza kidogo na baadae nikasema;

‘Alijiua..wanadai alikunywa sumu…’nikasema

‘Akajiua, yule ni mtoto wa nani..?’ akauliza

‘Wa wazazi wake…au sio’nikasema

‘Wazazi wake walifurahia…?’ akaniuliza.

'Aaah, hawawezi kufurahia, nalijua hilo...'nikasema

‘Mfano wewe ungelikuwa ni mzazi wa huyo binti ungelifurahia hilo tukio..je unajua ni kiasi gani mzazi alivyoumia,..kutokana na tendo hilo kwa mtoto wake, binti yake aliyempenda sana... huenda mama au baba alipatwa na shock kubwa…kuna athari zilitokea ndani ya miili yao, unaweza kuhisi ni ukubwa gani wa athar hizo,...kisa ni nani, ni wewe…hujui ni kiasi gani mwanadamu anavyoathirika kwa mshituko, na ukumbuke ni wazee, sio kijana, kuna tofauti ya kuhimili mshtuko kwenye mishipa ya fahamu kati ya kijana na mzee, unalijua hilo…’akasema

‘Wanisamehe sana wazee hao, sijui , sikujua jamani…’nikasema.

‘Tuache hayo....., mzee pale kasema kuna matatizo mengine makubwa,…mdogo wake alipatwa na nini..?’ akaniuliza.

‘Mhh..lakini…hilo halihusu au...'nikasema.

‘Nakuelezea kuhusu madhara mengine yaliyotokea kutokana an hiyo dhuluma, mdogo wake hatujui kadhurika kiasi gani, na hayo madhara mengine hatujui yapo kiasi gani mpaka wanaikimbia nyumba yao wenyewe..., na je huko walipo wanaishije,….na huyo mdogo mtu anapata taabu gani je itaishia hapo, je akifariki na yeye?’ akauliza na mim hapo nikaa kimia.

‘Sasa kabla haijafikia huko, ni bora kwenda kutubu, kabla hata hao waliopo duniani hawajaondoka, maana wakiondoka, ujue una msiba mkubwa una mzigo usiobebeka, mmoja keshaondoka hukuweza kutubu kwake, lakini wengine bado wapo, tuwawahi kabla hawajaondoka, na kabla hajatkea mpenzi mwingine wa facebook,…’akasema docta.

‘Mhh, hapo docta …unanitia mtegoni..’nikasema

‘Unajua kijana ,…tunapodhulumu awali, tunajiona ni wajanja, ni jambo la kawaida tu, lakini je, tunajua athari zake za baadae, ni nani na nani wataumia kutokana na hiyo dhuluma, kama ni mtoto umemfanyia hivyo ujue ana baba, ana mama ana ndugu…angalia hilo tatizo lako lilivyo, limekuwa chanzo cha mikosi kwenye hiyo familia, umesikia mwenyewe huyo mzee akisema, sio mimi….’akasema docta

‘Sasa unataka mimi nifanyeje,…mimi utetezi wangu ni sikujua…maana sio yeye peke yake, niliyewahi kumfanyia hivyo,..nigelijua hayo yatatokea, ningelijihami, ningeenda kumsihi asifanye hivyo,..na kiukweli awali niliwahi kupendana na wengi, tukaachana kwa maridhiano tu…sasa kwanini kwake iwe ni tofauti…’nikajitetea

‘Kuna ambaye kati ya hao, mlifikia kuwekeana kiapo cha uchumba, unakumbuka huyo ulimvika hadi pete mbele ya kadamnasi,..si ndio mnavyofanya hivyo vijana mnaiga eeh…sasa hao walikuwepo uliwaita ili iweje, si ili wawe mashahidi, kuthibitisha,na tendo hilo lilimpa faraja huyo mdada, na kuhakiki kuwa kweli unampenda..kweli si kweli…?’ akauliza docta.

‘Mhh…sasa docta…’nikawa nalalamika

‘Huyo binti alikupenda kweli kweli…, na ndio maana akawakataa wachumba wengine wote, alikuwa binti wa watu,  mpole, hana…uhusiano na mtu mwingine zaidi yako..ulimkatili maisha yake…unasema kwanini yeye iwe tofauti, bado hujaliona hilo kosa lilivyo kubwa…ndio maana nataka tufike huko kwa wazazi wake ili uone tofauti yake…’akasema docta

‘Kwahiyo nifanyeje, niende nikajitoe mhanga,..ndivyo unavyotaka docta…’nikasema

‘Ufanyeje, cha kufanya ndio hivii tumeanza, hatua ya kwanza imeshapita sasa ni hatua ya pili,  ni lazima ufike kwa wazazi wa huyo marehemu, ukajieleze,… vinginevyo, ndugu yangu, ipo siku utakwenda kuungana na huyo mpenzi wako wa facebook, huku ukiwa na mzigo mkubwa wa madhambi, na hutapata msamaha tena, maana mlango wa toba ulishafungwa….’akasema docta

‘Docta, kufa ni siku zako zikifika kama ndivyo nimepangiwa, siwezi kuwa na mjadala wa hilo,…au sio, siwezi kuogopa kufa kwasababu hiyo, ila…nisaidie tu jinsi ya kulitatua hili tatizo bila kuzua tatizo jingine, maana nionavyo mimi kwenda kwa huyo mzee, ni kuzua tatizo jingine…’nikasema

‘Je unakubali kuwa huyo mpenzi wako wa facebook, ndio huyo marehemu..?’ akaniuliza

‘Kiukweli hilo nalipinga, ..na..na docta  mimi sijui, maana hao watu wawili hawafanani, ngoja, …kama nitakuwa na picha ya huyo mdada, kipindi hicho, utalinganisha mwenyewe na picha za huyu mpenzi wa facebook, utakubali mwenyewe kuwa hawafanani kabisa…’akasema

‘Una hakika na hilo..?’ akaniuliza docta

‘Kwanini nisiwe na uhakika nalo wakati wote wawili nina mahusiano nao…, docta mimi vitu vya kuangalia na kumbukumbu sisahau, …nikipita njia mara moja au ukinielekeza jambo, linakaa kichwani, ni nadra sana kusahau,…au…picha za watu, kumbukumbu za watu, nikikutana na wewe kukusahau ni nadra, sina udhaifu huo wa ubongo..’nikasema

‘Mbona huyu umemsahau…’akasema docta

‘Sio yeye docta, kama unabisha turudi kwa yule mzee tumuonyeshe hii picha asema ni huyo binti au la….’akasema

‘Kesho tunakwenda kuonana na familia ya huyo binti…’akasema docta sasa kitaka kufunga mjadala.

‘Huko- mzee, hapana, huko-utakwenda-wewe-peke yako docta…nisaidie kwa hilo...’ nikasema kwa msisitizo nikitamka neno moja moja, na mara nikahisi kichwa kikima, ni kama sindano imedungwa kichwani, nikashikilia kichwa kwa muda, nikawa nimetulia, na docta akaniangalia kwa makini, sikusema neno.

Kitambo kikapita, halafu hiyo hali ikatulia na docta akaniuliza;

‘Kwahiyo umeshaanza kuogopa,….umeanza kukhalifu hulka yako wewe mwenyewe, mwanzoni ulisema wewe huogopi, …sasa kipo wapi, kwahiyo unasemaje, tutakwenda au mimi nirudi kazini kwangu,…?’ akauliza docta. Na kabla sijamjibu docta, mara simu ya docta ikaita,...

Na  docta akaiangalia simu yake, akawa kama anasita kuipokea baadae akaipokea na kuuliza;

‘Halooh, ni nani mwenzangu…?’ akauliza docta na akawa anjibiwa kwenye simu, halafu akauliza

‘Umesema nani, imekuwaje…?’ akauliza docta huku akiniangalia mimi kwa mashaka. Halafu akasema.

‘Mungu wangu imekuwa hayo….oh, ....’akasema na akawa anasikiliza…..

NB: Kwa leo naishi hapa


WAZO LA LEO: Usiogope changamoto pale unapotaka kuutafuta haki na ukweli, wakati mwingine haki na ukweli haviwezi kupatikana kirahisi, na changamoto zitakazojitokeza mbele yako ni namna njema ya kuuweka huo ukweli katika uwazi unaokubalika kwa kila mtu, ukiyumba, ukarudi nyuma basi utaungana na hao wenye kupotisha huo ukweli.
Ni mimi: emu-three

No comments :