Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, April 14, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-5
Ni kisa cha mpenzi niliyempata ndani ya facebook, …nilimpenda sana, na hatimaye nikapanga nikajitambulishe kwao, lakini kabla ya kitendo hicho tuliona ni bora tukutane mimi na yeye..kiukweli, nilishajipanga kwa vyovyote iwavyo huyo ndiye mwenza wangu wa maisha,..tatizo ikawa jinsi gani ya kukutana naye,

Alinielekeza njia, nikajikuta natokea MAKABURINI, je ni kwa bahati mbaya au kuna jambo

Safari ya pili, akanieleekza vizuri tu, GARI LIKAPATA AJALI, ajali ya namna yake, na aliyeumia ni mimi peke yangu, kwani ile breaki ilinifanya nirushwe na kugonga kwenye kiyoo cha mbele …nikaponea chupu chupu…lakini kutokana na athari ya kichwa,…nikawa kama nimepagawa, nilitibiwa nikaonekana nimepona , lakini akili yangu haikuwa sawa…

Na hatimaye nikakutana na docta...mwenye fani hiyo, ambaye alisomea udakitari wa kisayansi na kienyeji, yeye ndiye akaamua kulitatua hilo tatizo, haikuwa kazi rahisi…

Docta alisema tatizo langu haliwezi kumalizwa kwa tiba , kwa dawa, au kwa kusomewa, au …..inahitajia kwanza kujua kiini cha tatizo, kwani tatizo langu sio la kubahatisha, lina mguso wa jambo nililowahi kulifanya mimi au familia yangu….mimi sikumbuki kabisa jambo kama hilo na wazazi wangu hawana mambo hayo ya …kwangu mimi niliyaaita ya kishirikina,…sasa nitaponaje,…

‘Inabidi tuanze kazi mimi na wewe twende huko tatizo lilipoanzia…’akasema docta

Tuendelee na kisa chetu…...

****************

Kesho yake nikamuota tena huyo mdada,…na sasa hivi alionekana mnyonge hana raha, na hakuweza kuniangalia usoni kama ilivyokuwa kawaida yake, alikuwa tukikutana naye ananiangalia moja kwa moja usoni…

Na kitu cha ajabu nilichokuwa nikikiona kwa huyu mdada huwa akiniangalia machoni simuoni yeye tena, bali,…ninakuwa kama ninazama ndani ya macho yake, na kujikuta kwenye dunia nyingine…inakuwa na raha fulani hivi…kiukweli sikufurahia kumuona hana raha.., kwani pamoja na mengine mengi, tabasamu la mdada huyu lilikuwa ni furaha kubwa sana kwangu,…sikupenda kulikosa,… mwishowe nikamuuliza;

‘Mbona upo hivi mpenzi wangu…?’ nikamuuliza

‘Kweli bado unaniita mpenzi wako…?’ akaniuliza hivyo na mimi nikashtuka kidogo, halafu nikasema.

‘Kwanini unasema hivyo..my sweetie?’ nikamuuliza.

‘Haaah, kwanini nasema hivyo, nilikuambia nini na unafanya nini….nyie si mnataka kunimaliza, wewe na familia yako…au unafikiri mimi sijui mnachotaka kukifanya…’akasema.

‘Mhh, hapana mpenzi wangu siwezi kukufanyia kitu chochote kibaya, na nilishakuambia mimi nipo tayari kuja kukuoa, kwanini huniamini, kitu gani tunataka kukufanyia wewe, na wazazi wangu hawakujui bado, niliwaambia tu nina mpenzi, siku ikifika nitawafahamisha, …’nikasema.

‘Sio kweli..sizani kama nafsi yako inadhamiria hiyo kauli yako…usinidanganye, nimezoa uwongo wako…’akasema.

‘Kwa vipi mbona sikuelewi mpenzi mbona kama unakuwa na mambo ambayo mimi siyajui,….hebu kwanza, niambie nimekufanyia nini kibaya, mimi nimejitahidi kadri ya uwezo wangu , nikataka kufika kwenu, lakini kwanza nikapotea njia, su hukunielekeza vyema, na safari ya pili ndio nikapata ajali, unataka nifanye nini mimi ili uone kuwa nakupenda..?’ nikamuuliza.

‘Nataka uje kwangu, kama kweli unanipenda…na kama kweli unanipenda ninataka kukutana kwetu huku, kama hivi tunavyokutana …usije ukamwambia mtu yoyote, na siku nikikuambia uje kwangu, nataka uje kwa siri, iwe kati yangu mimi na wewe, na ukifanya kinyume chake, nitajua hunipendi, na huenda ikawa mwisho wangu wa mimi na wewe, hutaniona tena…pili nilikumbia uandike kwenye kumbukumbu zako, yale niliyokuwa nakutamkia, hukuweza kuyaandika, ukakimbia….’akasema.

‘Lakini mimi nilianza kuandika mara nika….sijui, litokeaje, lakini nikuambie mpenzi naona nipo huku mbali kijijini nitafanyaje nifike huko kwenu..?’ nikamuuliza.

‘Ukiwa tayari wewe niambie tu…lakini la muhimu uchunge siri yangu ya mimi na wewe, wapenzi tunatakiwa tuwe na siri, ukivunja sirio ya mpenzi wako ujue humpendi..unanielewa..’akasema.

‘Mhh….tatizo mimi sasa nashindwa kukuelewa, hebu kwanza niambie kiukweli wewe ni nani…’nikasema nahapo akanitupia jicho la mashaka, halafu akaangalia pembeni na kusema;

‘Leo hiii hunielewi …hahaha umeona eeh, leo hii unaniuliza mimi ni nani unakumbuka tulianzia wapi mahusiano yetu, umesahau eeh, na ulisema mara nyingi …unanipenda na vyovyote vile hutaniacha, unakumbuka..?, 'akasema

'Ulisema mimi ni wako wa kufa na kuzikana..unakumbuka, na siku moja…unakumbuka, ulitafuta pete ya dhahabu bandia ukanivalisha unakumbuka, na siku ile ndio ukaweza kunichezea, unakumbuka,…nikawaacha wapenzi wangu wengi tu, unakumbuka, na pete hii hapa mimi sijaachana nayo….’akasema.

‘Mhh…pete ipi hiyo,mbona sikumbuki kukuvalisha mimi kukuvalisha pete hapana umekosea mpenzi, sijawahi kukufanyia hivyo….maana mimi ndio natafuta mwanzo wa kukuona, na hiyo pete ndio nataka kuja kukuvika, …sijawahi kukutana na wewe kabla…’nikasema.

‘Hahaha, una uhakika na hilo, hebu angalia kule…’akasema na mara nikajiona sehemu nyingine, yaliyotokea huko sikuweza kuyakumbuka baadae tukarudi sehemu ile ya awali…

‘Umekumbuka eeh…?’ akaniuliza.

‘Mhh….’nikaguna tu.

Na ghafla nikazindukana kwenye usingizi, na nilijikuta nikihema sana, kama mtu aliyekuwa akikimbizwa, baadaye wazo likanijia, nikaichukua simu yangu na kufungua facebook, na mara nikamuona mdada yupo hewani,…picha ile ile msichana mrembo kakalia kaburi….

‘Usije kuchat tena na huyo mdada ukifanya hivyo, unampa nafasi ya kuingia kwenye ubongo wako na kusoma akili yako yote….’nikakumbuka kauli ya Docta, na bila kufikiria zaidi nikazima simu, huku mkono ukiwashwa, ukiwa na hamu ya kuchat na huyo mdada…

‘Oh….’nikaguna, na nikawa nataka kuishika ile simu…huku akilini nikisema; mimi siamini hayo mambo kwanini nisichat tu…hakuna kitu kama hicho,….ngoja nione, mimi siogopi, nikaishika ile simu na mara sauti ya simu kuingia ikalia,…unajua kilichotokea niliitupa ile simu kama nimeshika nyoka, au kugusa umeme….!

**********

Kiukweli mimi siamini mambo ya kishirikina au mambo kama haya ya kusikika tu,…sikupenda imani hiyo initeke akili yangu, na moyoni nilishataka nifanye uchunguzi hadi hatua ya mwisho, nijitoe mhanga hadi nifike huko anaposema huyu binti anaishi kama ni makaburini au wapi..

Nakumbuka wakati naongea na docta nilimwambia wazo hilo, akasema;

‘Unajua nilikuambia kuna mambo mengine huwezi kulazimisha, ukisema unataka kwenda kuonana na huyo binti, una maana gani, yeye keshafariki, …na huyo ni shetani tu, kajigeuza kwa umbo lake, lengo hasa ni kukuvuruga wewe akili…yawezekana, na ndivyo inavyoonekana kuna mambo ulikosana na huyo mdada, na shetani anatumia mwanya huo kukuvuruga,..niamini ninachokuambia..’akasema docta.

‘Lakini kama ni huyo mdada , ambaye nimemfikiria , hakuwa mrembo hivyo,…na kama ni yeye mbona nisiikumbuke sura yake, sio yeye docta,…huyu ni mwingine mrembo,…sio shetani docta, huyu anatumia mbinu tu za kunizihaki…’nikasema.

‘Kijana, najua una hamasa sana ya kulihakiki hili, unataka uwe na uhakika, na najua bila hata kusema, kinachokusumbua ni mapenzi, umeshampenda huyo binti, lakini kumbuka, sio vyote ving’aavyo ni dhahabu..huyo sio mtu, huyo ni shetani, na wapo wengi tu kwenye hizo facebook, muwe makini, sana, wapo wengi mitaani, …wana yao, …unasikia…mimi ni docta na nimefanya uchunguzi mwingi sana….’akatulia, na kunionyesha kile kitabu chake.

‘Hiki kitabu nimetunga mwenyewe, nimekuwa nikichukua kumbukumbu nyingi sana za matukio, nikakusanya maandiko mbali mbali, huku kuna uchunguzi wangu wa madawa, tiba, na historia za wagonjwa wangu….sasa hivi umekuwa miongoni wa wahusika kwenye hiki kitabu…’akasema akifungua sehemu mpya ya hicho kitabu.

‘Ninataka tuliendee hilo jambo mimi na wewe , mguu kwa mguu,…utaona ninachokuambia, muhimu, ujiandae, kwani huenda tukakutana na mambo ya kutisha,…na uhakikishe unafuata yale ninayokuambia, nikisema hiki usifanye, kweli usifanye,..unanisikia,….’akasema.

‘Sawa docta nitafurahi sana, nina hamu yakukutana na huyo mtu, hata kama ni shetani kama unavyodai, au …sijui..na docta ni kwanini tusiondoke hata kesho..’nikasema

‘Ngoja upone, tutalifanya hilo, tutafika hadi huko, ..nataka kulimaliza hilo tatizo kabisa…lakini kama nilivyokuambia safari hii inahitajia maandalizi, inahitajia uwe na nguvu, kiakili na kimwili,…na mimi hapa ninaacha udakitari halisi naingia kwenye mambo ya giza….hamna shida, kwani hata mimi nataka kuhakiki jambo…’akasema docta.

‘Docta mimi naona kama nipo sawa, japokuwa naota, na naona mambo ya kiajabi ajabu bado…

‘Umewahi kuota hivi karibuni, jana.. uliota nini…umeona mambo gani , je umeshamuota huyo mdada tena…mbona hujanambia nilikuambia ukimuota uniambie,…?’ akaniuliza na mimi nikasema

‘Sijaota kitu…sija..sijamuota..sikumbuki…’nikamdanganya.

Docta akatabasamu tu na kutikisa kichwa...

********
Siku kadhaa baadae tukafunga safari hadi Dar, tulipofika tulikaa siku mbili , bila kuanza kazi hiyo ya kufuatilia, docta alisema kuna mambo anayaweka sawa, …na ana dawa zake anazitengeneza, na kuzifuatulia sehemu mbali mbali, na alipokuwa tayari, tukafunga safari;

‘Safari yetu ni kwa huyo binti ambaye uliwahi kuwa na mahusiano naye ….ukamtekeleza, unakumbuka nyumbani kwao…?’ akaniuliza

‘Docta mimi sihitaji kukutana na huyo binti,..kwanza siku nyingi sana, na sina mapenzi naye tulishaachana,.... mimi nataka kukutana na huyu mpenzi wangu wa facebook…’nikasema.

‘Hahaha, kijana,…huyo binti wa face book, huwezi kukutana naye kirahisi hivyo, kinachotakiwa kwanza ni kufuatilia njia zake…na nishakuambia, usije kuchat naye, na ukimuota uniambie,…la sivyo sivyo tutakuwa hatufanikiwi…’akasema na mara akilini nikasikia kama mtu ananing’oneza.

‘Kama kweli unanipenda ninataka kukutana kwetu huku, hivi…usije kumwambie mtu yoyote,…ukimwambia mtu hutaniona tena, ….’sauti ikasema kama inaninong’oneza.

‘Sawa docta, nimekuelewa…’nikasema hivyo tu.

'Kwahiyo safari yetu ya kwanza ni huko kwa huyo mpenzi wako wa awali, sijui kama alikuwa wa awali au vipi lakini maagizo yangu yananituma huko,…huko ndio tutafungua njia ya kwenda kuonana na huyo mpenzi wako wa facebook…unielewe, huyo mpenzi wako wa facebook, sio mtu…nataka hilo uliweke akilini,….usidanganyike, ukaghilibika, kwani hao viumbe ni wajanja wanatufahamu udhaifi wetu, lakini wanatuogopa, sis hatujui tu…’akasema.

‘Sasa kama wanatuogopa kwanini wanawaingia watu , kwanini wanaweza kufanya mambo makubwa ambayo sisi hatuwezi kuyafanya…’akasema.

‘Kama yapi, …?’ akauliza docta.

‘Kama kaweza kuingie kwenye mtandao akajibadili, kama kaweza kusababisha ajali…kama anaweza kujibadili sura,…huoni ni mambo makubwa sana hayo docta…’akasema.

‘Sisi tuna mambo makubwa zaidi ya hao viumbe, tatizo la sisi wanadamu, wengi wetu hatutaki kuutumia ubongo wetu vyema,…tumejawa na hofu,…sisi wanadamu tuna akili nyingi sana, na mola wetu katupatia uongozi wa kutawala dunia, lakini hatulijui hili…hao vimbe ni dhaifi kwetu, …

wanatuogopa, lakini kutoka na uwoga tulio nao, hatutaki kutumia akili zetu…ndio maana wanatufanya watakavyo…unanielewa hapo…’akasema

‘Mhh, lakini sio kwa mtu kama mimi…’nikasema.

‘Hahaha, lakini sio wewe, mbona umezama kwenye penzi na huyo mtu, usiyemfahamu…una akili kweli hapo…hujatumia akili yako vyema, maana mapenzi sio kupenda tu, mapenzi yana mambo mengi ya msingi,…unapopenda ina maana umetoa nafsi yako kwa mwenza wako,…sawa si sawa..?' akauli na mimi nikatabasamu tu.

'Hebu jiuliza hepo, unakubalije kutoa nafsi yako, kwa mtu usiye na uhakika naye..humjui,…hujakutana naye, hajui maisha yake, hujui familia yake, hujui historia ya familia hiyo, hujui hatari alizo nazo mwilini…kuna magonjwa, kuna matatizo ya kurithiana…..umenielewa….fikiria kabla ya kuingia kwenye mahusiano,...'akasema.

'Docta,…docta…kwani wewe ulipomuoa mke wako uliangalia hayo yote kwanza, sema ukweli..., mengine unajifunza ukiwa naye, huwezi kumchunguza samaki, utashindwa kumla docta…’nikasema

‘Tunarudi pale pale kuwa tuna akili, tuna ubongo, lakini tumejilemaza, kama tungeliweza kuutumia ubongo wetu vyema, maisha kwetu yangelikuwa rahisi sana… sasa tuyaache hayo, jiandae tuondoke safari ya kwanza kwa huyo binti, umenielewa, na tatizo lako, umeshaanza kunidanganya…’akasema docta.

‘Kukudanganya…kwa vipi docta…?’ nikamuuliza.

‘Unajua kwanini…tumia akili yako vyema, tafakari,…hili tunalokwenda kulifanya ni kwa ajili yako, hili tukikose,a ujue na maisha yako yanaweza kuharibika kabisa, unaweza ukachanganyikiwa kabisa, uwe makini, na unielewe vyema, hayo unayayaona unayoyata, yanaweza yakakuvuruiga akili yako, huyo unayemuota anaweza kukuambia ukamuue mzazi wako….’akasema.

‘Siwezi kufanya hivyo docta..hata siku moja, kumuua mzazi wangu hahaha…’nikacheka.

‘Tatizo lako hujui dunia, huwajui hao viumbe,…kuna watu matajiri, wana mali, lakini hawana raha, unajua ni kwanini…?’ akauliza docta

‘Sijui, na haiji akilini mtu tajiri halafu hana raha…’nikasema

‘Kwasababu utajiri wake kaupata kwa njia ya hivyo viumbe, mashetani,…kaambiwa fanye kadha wa kadhaa, mtoto wake kamfanya zezeta,…kaua,…kazindikwa na masharti kibao, unatarajia huyu mtu atakuwa na raha,….hana raha na kifo chake kitakuwa cha mateso, tatizo, watu kama hao waka akili, wana ubongo lakini hawakutaka kuituma neema ya mungu aliyotujalia nayo…’akasema docta.

‘Ni uzembe wako…’nikasema

‘Hata wewe ni mzembe…’akasema docta

‘Kwanini, mimi siwezi kudanganyika, kiukweli docta , sio kwamba najisifia, lakini, siwezi…niamnini docta …’nikasema

‘Haya niambie umemuota huyo mdada wa face book au hujamuota, na kama ulimuota , alikuambia nini kwa mara ya mwisho…?’ akaniuliza docta na hapo hapo sauti ikaninong’oneza

‘Ole wako useme, ukiseme hutaniona tena, na ..nitajua hunipendi, na….yatakayokupata usije kunilamu..docta atakuwa hayupo, … hayo ni kati yako mimi na wewe..mpenzi wako, I love you.’

‘I love you too…’nikajikuta nimesema hivyo bila kutegemea, na docta akacheka sana, na kusema;

‘Twende…’

NB: Ijumaa njema

WAZO LA LEO: Kiukweli moja ya neema aliyotujalia sisi viumbe vyake ni akili, akili ya kutambua jema na baya, akili inayoweza kutafakari mema na maovu. Lakini je tunafahamu umuhimu wa neema hii, ..je tunaitumia vyema neema hii, ..tujiulize vyema, ili mwisho wa siku tusije kujijutia, wakati muda utakuwa haupo tena. Tumuombe mola wetu atujalie tuwe na maono sahihi, kwa ktumia vyema akili zetu kwa mambo aliyoyaridhia yeye, AMIN

Ni mimi: emu-three


No comments :