Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, April 13, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-4


Nilikuwa mpenzi sana wa facebook, na kiukweli niliona hapo ndio sehemu ya ulevi wangu baada ya kuachana na ulevi nyingine kama uhuni, nk...humo kwenye face book, nikawa na marafiki wengi tu, wengi wao walikuwa wasichana.
Kati ya hao, nikatokea kumpenda mdada mmoja,.. kiukweli mdada huyo alinivutia sana,  kisura, kiumbile ..na hata tulivyokuwa tunaongea nikaona huyo ndiye tunaweza kuishi pamoja, na moyoni nikpanga nikikutana naye tu, sina zaidi ya kufunga naye ndoa, ...
Tatizo kubwa likawa jinsi gani ya kukutana naye, kwani kila safari tuliyopanga ilifikia kukatishwa na jambo fulani,...na jambo hilo linatokea kwenye mazingira yenye utata,... safari ya kwanza alinielekeza njia nikatokea makaburini,..je alikosea .

Safari ya pili nikapata ajali, na ni ajali ya aina yake....hata walioshudia walisema mengi, japokuw amimi sikuyaamini, na hata kupona kwangu, hata mdocta hawakuamini....walijua nitakuwa na athari kwenye ubongo, lakini baadae waligundua kuwa sina tatizo kwenye ubongo, ,,,nikatibiwa nikapona.

Kupona kwa hospitalini hakukunisaidia, kwani baadae nilianza kuona mambo ya ajabu ajabu, hayaelezeki,, mambo hayo yalinifanya niwe kama nimechanganyikiwa, ...hali hiyo ikafanya wazee waamue kunipeleka huko kijijini.

Nilitibiwa sana huko, na hatimaye nikakutana na docta...mwenye fani hiyo, aliyisomea kitaalamu zaidi...docta aliyeamua kuchanganya hizo fani, kiasili na kitaalamu.

 Tuendelee na kisa chetu.....
                            ****************
Ukumbuke sasa nipo kijijini na nilipelekwa kwa mtaalamu mmoja, huyu awali alikuwa dakitari wa wa hospitalini,lakini baadae akaanzisha hospitali yake, na kama alivyonihadithia, alimua kuchanganya tiba, za kawaida na mitishamba, lakini pia alikuwa na kipaji cha kurithi, cha kupambana na wagonjwa wenye mashetani..sasa utaona jinsi gani mtu huyo alivyobobea kwenye kazi yake, na zaidi aliniambia kuwa amesomea mambo ya saikolojia….

‘Mimi nilipoamua kufanya haya watu walinishangaa sana, msomi, dakitari, tena dakitari bingwa, unaamua kufanya haya mambo, lakini wameshindwa kunielewa, kuwa mimi ni dakitari bingwa wa nini..hapa sasa mimi naonyesha ubingwa wa udakitari wangu…’akasema.

‘Oh, nimefurahi sana docta, maana nilipoambiwa napelekwa kwa mtaalamu wa magonjwa ya mashetani nilipinga sana, mimi sina mashetani, na…hata sijui kwanini wanafikiria hivyo…hawaelewi hawa watu...’nikamwambia.

‘Sawa kabisa,...usijali, kama unayo au huna, tutakuja kuyafahamu hayo baade ..muhimu uwe muwazi kwangu, maana mimi situmii ramli, mimi natumia elimu yangu, vipimo vya kisayansi, na kipaji changu na mwenyezimungu ndiye anayeniongoza, sitaki kujiingiza kwenye shiriki…’akasema.

‘Hapo docta tupo pamoja….’nikasema

'Hebu niambie matatizo yako ilikuwaje...?' akaniuliza na mimi ndio nikaanza kumuelezea ilivyotokea hadi nikaja kupatwa na ajali, na nilipomaliza kumuelezea hayo docta, akawa tayari na vipimo mbali mbali vya kitaalamu . Maana ukifika hapo unapimwa kila kitu damu, mkojo nk.. na zaidi ya hayo  alikuwa na kitabu kikubwa mbele yake, sijui ni kitabu cha nini….akaanza kuongea;

‘ Hili tatizo lako kijana wangu, ni tatizo lenye utata, mimi nimekuwa nikiwatibu watu wengi tu, kwa dawa, lakini pia nawaondolea matatizo haya ya mashetani…kwa duwa na maombi, na maelekezo kama ninavyoongozwa baada ya kumuomba mola wangu…’akatulia

‘Mola wako…ina maana wewe una mungu wako?’ nikamuuliza

‘Huo ni usemi tu…mungu wangu ni mungu wetu sote….’akasema.

'Sasa docta mimi nina tatizo gani hasa...?' nikamuuliza

‘Nataka nijue ilivyotekea zaidi, kabla sijafikia , kukuambia tatizo ni nini hasa...'akasema

'Lakini nimeshakuambia kila kitu au...'nikasema

'Unayafahamu mashetani...au ulishawahi kusikia kitu kama hicho au kuona mtu aliyepagawa kutokana na matatizo hayo ya mashetani..?' akaniuliza


************

'Lakini mimi sina mashetani docta…, na wala siamini mambo hayo…’nikamwambia.

'Najua..na huwezi kuamini hivyo, kukumbana na hayo madude sio lazima uchanganyikiwe sana, inategemeana na udhibiti wako wa kiakili...kuna namna nyingi tu unaweza ukakumbana na haya madude, ukaanza kupata shida …’akasema

‘Ukweli docta mimi sipendi kujiingiza kwenye mambo ya uchawi, sijui kulogwa,..au mashetani, mimi sitaki kabisa kujiingiza huko... lakini wazee bwana, wanasema tatizo hilo linahitajia tiba hizi..lakini nimefurahi kuwa wewe ni docta wa ukweli..’nikasema.

‘Unajua wewe huamini, na huna uwoga, na una imani ya dini, japokuwa sio sana…kama ungelikuwa na imani haba,..unajifanya unamtii mungu, unajifanya una dini lakini ndani ya nafsi una mashaka,  sasa hivi ungekuwa umeharibikiwa,… siwezi kusema ungelikuwa maiti...maana kufa ni kwa miadi ya mungu…’akasema.

'Sasa docta unaposema mimi nimekumbwa na shetani,..kwa vipi, na huyo shetani yupoje, kwasababu kama ni huyo mdada wa facebook, yeye ni binadamu tu hata ukiangalia picha yake, kama nilivyokuonyesha hana tofauti na binadamu ni mrembo, ana maneno mazuri ya kuvutia, anaonekana ana adabu, na anafaa sana kuwa mke mwema…’nikamwambia.

'Una uhakika gani kuwa ni binadamu, ujue nikuambie kitu, hayo mashetani mungu kayajalia uwezo wa kujigeuza maumbile tofauti tofauti, ..yanaweza kujigeuza nyoka, yakitaka kukutisha, au umbo la namna yoyote ile, kwasababu ili yakupate silaha yake kubwa ni kukuogofya,..ukitishika tu ndio yanakuingia mwilini mwako….’akasema

'Una maana kusema huyo mdada ni shetani? Docta mimi siwezi kuamini hilo..wewe ni docta msomi, …umeiona picha yake lakini, …ni binadamu kabisa...’nikasema.

'Pamoja na yote yaliyokutokea…kuelekezwa makaburini, na ajali,… bado huamini kuwa huyo mpenzi wako sio mtu wa kawaida, ..hujiulizi ni kwanini hayo yanatokea ….’akasema docta.

'Mzee…samahani docta,…, kupotea njia ni kawaida, japokuwa mimi sijawahi kupotea kabla..naelewa sana ramani…, maana nina akili sana ya kujua mambo…, ukinielekeza njia au jambo,lolote, siwezi kukosea, sasa sijui kama huyo mdada alinielekeza vyema nahisi alikosea....au alifanya maksusidi tu kunibabaisha..lakini ananipenda na mimi nampenda...’nikasema.

'Huyo mdada hakukosea kabisa, alikuelekeza sahihi, ila wewe kinachokulinda ni ujasiri ulio nao, huna uwoga, na huamini mambo hayo ya giza, lakini hayo mambo sio ya giza na ufahamu tu mdogo, hayo mambo yapo...'akatulia akifunua funua kitabu chake.

'Na kitu kingine kilichokulinda ni kuwa una iman ya dini,..kutoka moyoni, kuna tofauti ya kuijua dini kwa maneno tu na kujionyesha kwa watu kuwa wewe ni mcha mungu,..na imani sahihi ya kutoka moyoni, wewe dini yako ipo moyoni, hilo ndilo limekusaidia sana, ..pamoja na hayo bado una madhaifu yako machache….’akasema

‘Madhaifu gani docta hayo docta…?’ nikamuuliza

‘Hayo ndio tutayatafuta yanaweza yakawa ndio sababu ya haya yote,..na hasa kama madhaifu hayo yana muelekeo wa dhuluma…dhuluma ni adui wa imani, dhuluma haidumu, na mwenye kudhuluma anaweza kupatilizwa humu humu duniani…..na huenda ndio sababu ya kuingiliwa na huyo shetani.

‘Lakini docta mimi ni muadilifu sana…kazini ninasifika kwa hilo, hata kwenye shughuli zangu sipendi kabisa kumdhulumu mtu, sina maadui kabisa, sasa sijui kwanini useme dhuluma yaweza kuwa sababu ya tukio hili..hapo siamini docta…’nikasema.

‘Tuakwenda hatua kwa hatua…usijali…sisi wanadamu tuna mitihani mingi tu, tunaweza kudhulumu watu kwa namna nyingi, unaweza kufanya jambo likamumiza sana mwenzako, na wewe usijali, maana umefanikiwa , kufanikiwa kwako, umejiona ni mjanja,..na mwenzako akaumia, …lakini kihali halisi yaonekana ni mambo ya kawaida, huwezi kujua athari gani za ile dhuluma..dhuluma ni pana sana..’akasema docta.

'Mzee,..oh docta, mimi sijakuelewa, shetani anawezaje kutumia mitandao, akaweza kuingia huko, na  ...hapana mzee, na tukio la pili ni ajali tu, nakubali kuwa ni kosa langu maana sikufunga mkanda, ila ule mrusho ni wa,ajabu sana…hapa sasa kama una imani hapa ndio unaweza kuamini mambo hayo, lakini mimi najua ni ajali tu, na huku kuchanganyikiwa ni kwasababu ya kuguswa kwenye ubongo….hakuna zaidi…au sio docta?’nikasema.

‘Kwahiyo ulikaa kwenye kiti , gari likafunga breaki, ukarushwa kuelekea mbele ukagonga kwenye kiyoo cha gari,…..ulirushwaje…?’ akaniuliza

‘Ni kweli …mimi naendesha gari, najua ….kama hukufunga mkanda, unaweza kurushwa …ila ule mrusho na janisi nilivyokuwa nimekaa, ni kama kuna nguvu fulani zilitumika kunirusha…sasa hayo labda ndio ukiwa na imani haba unaweza kuhisi hivyo..lakini yawezekana tu….’nikasema.

'Umeonaeeh,…kuna nguvu za ziada, ni nguvu gani hizo… na ni kwanini huyo mdada uliambiwa ukae kiti cha mbele, ni kwanini uliona damu...na ulisema wakati unarushwa ulimuona huyo bint akikupokea, huoni bado kuna jambo jingine hapo.. na mara kwa mara umekuwa ukimuota huyo mdada na unaiona hiyo hali kama kawaida, yaani kumuota kwake, ni kama tukio la kweli au sio..?’ akauliza docta.

'Kihalisia sioni tatizo hapo docta, labda uniambie wewe…yule mdada aliniambia nikae kiti cha mbele  sawa, nia yake ni ili anione nikifika,…ni namna ya mapenzi au sio… na swala la damu, ukumbuke, nilikuambia wakati naingia kuna mdada alikuwa kakaa kwenye kiti hicho, sijui kwanini, baadaye yeye aliamua kushuka kwenye hilo basi na mimi ndio nikapata hiyo nafasi…’nikasema.

"Ulimuona huyo mdada sura yake?’ akaniuliza.

'Hapana, sikuwahi kumuona na..kiukweli nilipoona ile damu niliingiwa na hamasa za kumuangalia, ili kuona kama kalowana damu…au kaumia,…lakini hata nilivyojitahidi kuangalia kule nje kwa kupitia dirishani sikuweza kumuona tena ni kama alitoweka, au labda alikuwa kaingia kwenye gari jingine…’nikasema.

'Dereva alisemaje kuhusu huyo mdada..jinsi alivyoingia, alivyotoka muonekano wake….?’ Akaniuliza.

'Alisema huyo mdada alikuwa wa kwanza kuingia kwenye gari, wakati huo yeye alikuwa kasimama nje ya mlango wa sehemu yake ya dereva, ila hakumuona akiingia, ....na...unajua tena watu na imani zao, eti alipomtizama usoni, alihisi mwili ukimsisimuka, akahisi sio mtu wa kawaida…’akasema

'Alisema hivyo huyo dereva…na huyo dereva ni mtu mzima au kijana..?’ akauliza

‘Ni mtu mzima, halafu anasema eti hiyo damu ni ishara mbaya kwake,..yaonekana ana tabia za kishirikina kishirikina,….’nikasema

‘Unajua haya mambo yana uwanja wake mpana, huyo dereva ana uzoefu na kazi yake, na hilo tukio linaweza likawa ni sababu ya huyo mdada,  aliyekuwa akikutafutia njia ya kukutana na wewe kwenye mazingira ambayo anaweza kutimiliza haja yake...’akasema docta.

'Docta hapana, …unaamini mambo hayo, ….hapana, Ina maana ndio huyo mdada…mbona asiniambie kuwa ndio yeye, na alionekana kabisa ana haraka zake na hata dereva alimuona….’ Nikasema.

'Wakati anakupita , ukiwa unaingia kwenye gari, na yeye anatoka, ulihisi nini ..hakuna jambo la ajabu ulihisi mwilini mwako…?’ akaniuliza.

'Mhh docta, hayo ndio mambo mimi siaminigi, eti jicho likicheza, eti, ukiuma mdomo, watu wanapenda kujijengea imani dhaifu,...haya yanatokea tu, si hivyo docta?…’nikasema

‘Aaah, wewe niambie ulihisije, hakuna kitu kilitokea mwilini mwako…?’ akauliza

‘Unajua kwa muda ule sikuwa na mawazo yoyote mabaya, ndio nilihisi mwili kunisisimuka, nywele zikawa kama zinachanua, nalikumbuka sana hilo, lakini sio mara ya kwanza, mbona inanitokea hivyo mara kwa mara tu...sioni kama hapo kuna tatizo…’nikasema.

'Tatizo ni kuwa ulikutana na kitu kisichokuwa cha kawaida,… miili yetu huhisi, maana wao wana dunia yao, wanapojitokeza kimaumbile ya kuonekana, miili yetu huhisi,....lakini akilini kwa vile hatujwahi kukutana na vitu kama hivyo, tunakuwa hatuna kumbukumbu nazo... kwa watambuzi wanajua...’akasema.

'Kwahiyo ina maana, siku zote ninapohisi hivyo, mwili kunisisimuka, nywele kusimama, basi ndio nipo karibu na hayo madude...mzee usitake kunitisha, mimi sitishiki kirahisi hivyo…’nikasema.

'Sio swala la kukutisha, ninakuelezea upande mwingine wa maisha yetu, mimi katika kazi hii nimeona mengi, nimeweza kuingia kwenye hiyo dunia nyingine, ya hayo mashetani...nina kipaji alichonijalia mungu, sikupenda kukiacha licha ya kuwa nimesomea udakitari wa kisayansi, nia yangu ni kuwasaidia watu kama nyie, sitaki kutumia kipaji hicho kuwasumbua watu,maana wengine hutumia vibaya elimu hii...hao ndio wachawi….’akasema

'Kwahiyo unataka kusema mimi nina tatizo gani....maana nimeshatibiwa hospitalini wanasema nimepona, lakini akilini bado nahisi matuwe ruwe, naona mambo ya ajabu ajabu...ni kama nimechanganyikiwa hivi...?' nikauliza

'Bila kukuficha wewe umekumbana na shetani....'akasema

'What..are sure docta,,,,?' nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukubali.

'Ok mzee, sasa niambie, nifanyaje ili niondokane na tatizo hilo, maana kiukweli, siamini, na sijui utafanya nini ili niamini mambo hayo…mimi ninachotaka kama ipo dawa wewe nipe tu ninywe, yaishe, maana naona kama unaweza kuniingiza kwenye mitihani ya kuamini mambo hayo na mimi sitaki…’nikasema

‘Hilo sio shida….lakini dawa za mambo hayo zinahitajia wewe mwenyewe….maana chimbuko la tatizo ni wewe mwenyewe au kutoka kwa wazazi wako….’akasema

‘Yale yale…ndio maana sipendi mambo haya, utataka kusema natakiwa kupewa uchawi, …au nimerithi, mimi hayo sitaki docta….’nikasema

‘Na jingine docta, …. Kwanini nisikutane na huyo mdada…nimuone , kama anaonekana, kama aliweza kuingia kwenye gari, akaonekana,..si umesema ndio yeye,…, kama ni kweli, maana docta mimi siwezi kuamini, huyo mtu kaonekana kaingia kwenye gari halafu unasema ni shetani,..haiwezekani,… kama unaweza mimi nataka nikutane naye uso kwa uso..

'Nimependa sana ujasiri wako kijana, lakini kuna jambo nataka kukutahadharisha, haya mambo yapo, na yanawatesa sana watu, hawajui kuwa wanateseka na mambo kama hayo, tatizo kubwa ni ufahamu mdogo, na uduni wa elimu..na imani ndogo ya dini.

Wengi wetu hatutaki kuelimika, ujue kila jambo lina elimu yake, na ili ufanikiwe inabidi ulijue hilo jambo kwa sili yake na kwanin likawa hivyo au sio..na kwanini limetokea, sasa kwa haya mambo hayatokei tu..wengi wakikutana na matatizo kama haya wanakimbilia tiba, …sawa tiba zipo , hasa kidini na kienyeji…lakini kwangu mimi nipo tofauti….’akatulia akifungua kitabu chake.

‘Pamoja na utaalamu wangu wa tiba, pamoja na kipaji changu, …maana yakija mambo kama haya kwanza namuelekea mola wangu, na kutokana na yeye napata maelekezo fulani, kama ni dawa za kawaida au ni dawa za kienyeji au ….sasa hayo siwezi kuyapata bila ushirikiano wa wewe na asili , au hitoaria ya hilo jambo..

Jambo ninalotaka kukutahadharisha ni kuwa sio kila jambo linahitajia ujasiri wa kihivyo, kuwa ngoja nikutane nalo, nitapambana nalo, ngoja nionane naye…sio hivyo, ujasiri wa hali ya kawaida unaweza kubadilika kutegemeana na tukio…hayo madude yakiwa kwenye hali halisi yanatisha,..ndio maana mtu akikutana nayo anapagawa…

‘Docta, mimi sijisifu…lakini ina asili ya uwoga, ..sio kwamba nataka kuonana naye kwa vile nimezama kwenye pendo, hapana, lakini nataka kuurizisha moyo wangu, …nataka niwe na uhakika, maana mfano kaam sio kweli, huyo mdada yupo, huoni kama nitakuwa nimefanya dhuluma…’nikasema

‘Nikuulize ni nini maisha yako ya nyuma…je ulikuwa una wapenzi, ..?’ akaniuliza swali ambalo sikutegemea

‘Kwani hayo yanahusianaje na hili tukio…?’ nikauliza

‘Yaweza kuwa…katika kulichunguza hili, tatizo lako limegwanyika sehemu mbili, kwanza umekumbana na huyo shetani,..hilo linaweza kutatuliwa tu, kwa vile moyo wako ni jasiri, ujasiri, imani tahibit ya dini, ndiyo itakufanya uyashinde hayo mashetani, kwasababu yenyewe yanajua,…mwanadamu kapewa mamlaka, ..na hayawezi kukuingia mpaka yakutie hofu, hofu ya kukutenganisha wewe na imani yako ya kumtegemea mola wako….hofu,…ndio tatizo kubwa!

‘ Lakini la pili ni dhuluma, matatizo mengine hutokea kwasababu ya dhuluma, ndio maana kwenye kuomba la kwanza na la msingi ni kuomba toba, kutubu dhambi zako, na ingelikuwa ni bora sana ukaenda kumuomba uliyemkosea akusamehe…'akasema

'Ni rahisi kihivyo, utawakumbukaje....'nikasema

'Awali nimekuambiwa dhuluma haidumu, dhuluma inatakiwa ipatilizwe, ilipizwe, huweze ukafanya dhuluma ukajiona upo huru, mpaka uliyemkosea akusamehe., sasa ukimfanyia mwenzako ukajiona mjanja wakati mwenzako anaumia, ujue. ipo siku utalipizwa kwako mwenyewe au kupitia kwa familia yako…ndio maana dhuluma ni mbaya sana…ndio maana nataka kujua je huko nyuma ya maisha yako ulikuwaje…?’

‘Mhh..docta, unajua mimi sina historia ya mahusiano mabaya na watu..., hasa nilipoanza kujitambua,….’nikatulia

‘Una maana gani kujitambua..?’ akaulizwa

‘Awali, kiukweli nilikuwa mtu wa kujirusha, umbile langu, ushombe shombe huu ulidanganya, ni kweli nilikuwa napagawa sana na akina dada wakijigonga gonga kwangu,..kwahiyo nikawa na huyu na yule..lakini sikuwa na urafiki wa kudumu…sikutaka kujiingiza kwenye mahusiano ya moja kwa moja…ili nipate muda wa kujijenga kwanza…’nikasema

‘Katika hao wa kujirusha nao, hakuna uliyewahi kuahidiana naye kuwa atakuwa ..ukijaliwa awe mke wako..hukuwahi hata kudanganya hivyo..?’ akaulizwa

‘Hahaha, docta, unajua tena maisha hayo…,kauli kama hizo ni nyingi tu, nakupenda sana, utakuwa wangu wa milele..hizo zilikuwa sana..lakini ikafika muda nikajirudi, nikasema basi, najipa muda , ikifika muda muafaka nitamtafuta anayenifaa…’akasema

‘Kwahiyo uliwahi kudanganya, …ukawafanya wengine wakakuamini hivyo, kuwa wewe ni mtarajiwa…?’ nikaulizwa

‘Docta, docta..docta..hayo yalishapita, sitaki hata kuyakumbuka inakuwa kama najirudisha kwenye matope, sitaki hata kuyakumbuka maisha hayo, ..na kiukweli baada ya kukutana na huyu mpenzi wa facebook, niliona kuwa huyo ndiye ananifaa..basi…japokuwa kuna wengu humo ndani niliwahi kuahidiana nao pia, kuwa nawapenda, lakini ni lugha tu…baadae nikakutana na huyo mmoja …nikaamua awe wangu…’nikasema

‘Hujajibu swali langu…inaonekana kwako, kudanganya kuhusu mapenzi ni kitu cha kawaida sana, hujui kuwa ni jambo linagusa hisia ya ndani ya mtu, na hii mitandao wengine mnajikaribishia maovu, mnadanganya, mnajenga chuki..sio vizuri, maana hata mashetani wameshagundua kuwa huo ni uwanja mnzuri wa kupatia wateja wao….’akasema docta

‘Kiukweli docta niliwahi kudanganya sana..lakini sikuwa na upeo mpana hivyo…nilijua ndio maisha yalivyo, bila kuwadanganya hawa akina dada huwezi kuwapata…nilifanya hivyo, na …ikafika muda nikaona hawanifai,…wengine hawaendani na mimi tena, si unajua tena….basi nikatulia…’akasema

‘Sasa nikuambie jambo, kati ya hao uliowadanyanya,..kuna mmojawapo ulimdhulumu sana, alijua wewe ndiye mtarajiwa wake,..alikupenda zaidi ya maelezo…ukaja kumuumiza sana, huenda ulimtamkia wazi wazi kuwa humtaki, au ulifanya matendo ya kumuumiza, na huenda kutokana na hilo….ikawa ndio sababu ya umauti wake….’akasema docta

‘What…..sijawahi kuua docta..sijawahi kufanya jambo la kusababisha umauti kwa mtu hapana mimi sina roho mbaya kihivyo…na mimi docta sikuwa na lugha ya …..mmh,….hamna mbona sijawahi kusikia kitu kama hicho…sio kweli docta… ’nikasema na kutulia

‘Mapenzi ni kitu hatari sana…kinatesa..na sio wote wanaoweza kuvumilia kutelekezwa, na hujui sababu ya kuachana kwenu ilikuwaje, na lugha uliyotumia , awali ulisema nakupenda nk..baadae unakuja kusema maneno mabaya kiasi kwamba yule mtu anajihisi vibaya , anaumia…anajiona hana thamani tena mbele ya watu…na wakati huo ulishamchezea mwili wake..na huenda ulishampa hata uja uzito….hujui huko kwenye familia yake kupoje.’akasemaa docta

‘Uja uzito..oh,…’alipotamka hayo nikahisi kitu kimegusa kumbukumbu zangu

‘Umeonaeeh…sasa anza kukumbuka huenda tukaweza kulimaliza hili tatizo, kuliko kukimbilia tiba tu, tiba ya haya mambo mengine , hasa kupitia kwangu, inaanzia kwenye asili ya tatizo, ..vinginevyo itakuwa kama kukata mti matawi, baadae kesho unachipua..ninataka tulimalize hili tatizo kabisa..sasa hebu kumbuka vyema….’akasema docta.

‘Docta….mmmh…umenikumbusha jambo….lakini sijui, mbona siku nyingi sana,na mimi nilijua kuwa alikuwa akinidanganya, na hajafa lakini, sina uhakika, maana baada ya pale sikuwahi kuonana naye tena wala familia yake..…’ nikatulia nikijaribu kukumbuka ni tukio la siku nyingi sana….lakini sina uhakika kama linahusiana na hilo.

NB: Tuishie hapa kwa leo

WAZO LA LEO: Kuna matatizo mengine hutukumba sisi wanadamu kutokana na dhuluma, kuna magonjwa unaweza kutibiwa usionekane tatizo, lakini kumbe sababu yake kubwa ni dhuluma,…na dhuluma sio lazima kuiba, dhuluma zipo za namna nyingi..kila jambo unalomtendea mwenzako isivyo haki, ukamdhulumu nafsi yake, akaumia,..ni dhuluma,… sasa hatujui umbali wa kuumia huko. Tumuombe mola atusaidie tuweze kutendeana haki na tukikoseana tukumbuke kuombeana msamaha, na iwe ni toba ya kweli
Ni mimi: emu-three

No comments :