Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, April 11, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-2


 Nikiwa ndani ya facebook, nilibahatika kupendana na msichana mmoja, ...tuliwasiliana naye sana, tukajuana lakini kwa kupitia mtandao, tukawa tunatumiana picha, mpaka ikafikia mahali nikataka nikutane naye uso kwa uso...

Hakupendelea hilo wazo, nikajua ni taratibu tu za mwanamke anayejiheshimu, mimi nikamwambia sio kumuona tu, nataka nionane na wazazi wake, ili ikibidi tufunge ndoa..bado aliendelea kusita, lakini hatimaye akaakubali, na ndio nikafunga safari ya kwenda kwao kukutana na wazazi wake.

Kabla ya kukutana na wazazi wake tulipanga kuwa nikutane mimi naye yeye, nyumbani kwake, kwahiyo akanielekeza na cha ajabu ramani aliyonipa, au maelekezo yake aliniyonipa yalinifikisha makaburini...

‘Ohh, huyu honey, kakosea nini, mbona natokea huku makaburini, nahisi kakosea....'nikasema

'Mimi hapo nikajaribu kumpigia simu kwa namba ile ile tunayowasiliana naye siku zote,.., lakini kwa muda huo hakuweza kupatikana..., sio kawaida yake, haijawahi kutokea, huwa tukipigiana simu muda wote tunakuwa hewani.

Nilihangaika kutafuta huku na kule kama kuna nyumba mahali hap , au karibu na hapo, lakini sikuona nyumba kama hiyo,...nyumba nyeupe, ina maru maru kuzunguka...nikauliza watu hakuna aliyeitambua nyumba hiyo

Basi baadae nikiwa nimekata tamaa, nikaamua kurejea nyumbani

Hapo ndio nikaota ndoto ya ajabu,...hata hivyo sikuwa na wasiwasi wowote, akili yangu ilikuwa kwa mrembo, nikapanga nionane naye siku nyingine, baada ya kuomba sana, ndio akanikubalia...

Tuendelee na kisa chetu...

*************

‘Mbona hunielewi baby,..i love you so much…but,…eeh, mimi nahisi ulikosea kuniekeleza…au sio, hapo uliponielekeza barabara inapitia makaburini, na huko mbele, au hata pembeni hakuna sehemu za nyumba za watu…, zaidi ya kupita juu ya makaburi ya watu, …’akasema.

‘Mhh, kumbe ulivyokuwa unanisihi hivyo hukuwa na mapenzi na mimi, nakumbuka mashari yako ya mapenzi ulisemaje, utanitafuta hata kama makaburini…utanifuata hata kama ni kuzumuni, utanipenda hadi siku kiamani, au sio…, si ulisema utafika kwetu hata kama ni ndani ya pango, ili unioe, tuwe pamoja, kweli si kweli…? akauliza.

‘Lakini hiyo ni misemo ya kimapenzi….au …nakupenda sana honey wangu, na niliyasema hayo nikimaaanisha jinsi gani nikupendavyo, na ya kuwa nitajitahidi nifike pale ulipo kwa vyovyote vile lakini sasa hujaniekeleza vyema,…nikuambie kitu honye, tusipoteze muda, wewe nieleekeze tena, naona ulikosea tu, au sio…’nikamwambia.

‘Hapana…naona muda wako wa kukutana na mimi haujafika, ukifika tutaonana tu…usijali sana mpenzi wangu, …poa, wewe jiandae taratibu, na hilo halitaki haraka, unasikia..’akaambiwa

‘Hapana mimi nimeshajiandaa sina shaka na hilo….’akasema

‘Usilazimishe jambo ukaja kujijutia baadae…huku unapotaka kuja kuniona sio njia rahisi, unasikia, …’akasema

‘Basi nitakodi hata ndege…’nikasema nijua ni mzaha wake tu, unajua hadi hapo sikuwa na mawazo mengine zaidi ya kumpenda huyo binti wa facebook.

‘Basi kama umedhamiria kweli, ....jiandae ipo siku nitakuambia, ...'akasema

'Sawa honey, usinifane nikasubiri sana....'nikasema

'Basi kesho nitakuelekeza vyema, na safari hii usiogope, njia ni hiyo hiyo, ukifika hapo, nitakupokea mimi mwenyewe…’akasema na mimi kabla sijamjibu ndio  nikazindukana…kumbe alikuwa anaota.

Basi nikajiandaa kwenda kuwajibika kazini kwangu, huku nikitizama kwenye simu kama nitapata meseji yoyote mpya kutoka kwa huyo mpenzi wangu, lakini hakutokea kama ilivyokuwa kawaida yetu, nikampigia simu ikawa haipatikani.

Siku hiyo nilifika ofisini nikiwa kama mgonjwa, kisa sijawasiliana na mpenzi wangu,..baadae mcha mchana hivi ikaingia meseji na ujumbe na picha, nikaifuingua, mara naona mtu kasimama juu ya kaburi, na ujumbe unasema;

Anaye yakimbia mauti, mwisho wake, ni hapa, jiandae, na utamkuta umpendaye anakusubiria, yeye hana haraka, anafika hata kwenye pango,…gizani hata ndani ya maji,…muhimu jiandae…’

 Mimi niliyachukulia maneno hayo kama maneno ya kufurahishana tu kwenye mtandao, sikuwa na wazo lolote baya kwa huyo binti basi mimi nikaweka maua, na sura za kimapenzi, na kusema;

‘Baby, mbona wanitisha, …mimi kwa ajili yako siogopi kufa, kwani inzi kufa kidondani ni kawaida tu…' na hakunijibu, nikajaribu kumpigia hakupatikana, na jioni akanitumia meseji kuwa kaongea na wazazi wake, wamesema wanahitajia muda wa kunichunguza kwanza.

‘Umesikia, kwa vile umeshatambuliwa kwetu kama mchumba, inabidi tusiwe kama zamani, kuchat nk..inatakiwa uniheshimu kama mtu wako, sio hawara au …mpenzi wa kupita, kwahiyo nakuomba tupunguze mawasiliano…’akasema hivyo.

Kiukweli nilikubali kishingo upande, nikamajibu sawa kama uonavyo ni sahihi, lakini mimi sitaweza kulala, hata kula kwa ajili yako…

Ilipitia wiki nikawa kama mgonjwa, mpaka watu wakanishangaa, wakiniuliza nawaambia nyie acheni tu, nampenda sana mpenzi wangu wa facebook…na siku moja huyo mpenzi wangu wa facebook, akanitumia ujumbe na kuniambia;

‘Sasa wazazi wangu wapo tayari kukutana na wewe…lakini siku hiyo unatakiwa ufanye yafuatayo...kwanza utakuja tuonane mimi na wewe uso kwa uso, baada ya hapo nitakupeleka kwa wazazi wangu,...

'Sawa itakuwa vizuri sana, nikuone ulivyo, sura yako..tuongee, unijue na mimi nikujue au sio...'nikasema

'Lakini jingine la muhimu, usija na gari lako,...nataka uje na daladala,..wewe wahi asubuhi na mapema, ukifika kituoni utaliona gari linasubiria abiria,  na ukae kiti cha mbele…’akasema.

‘Kwanini cha mbele, kama kina mtu je..?’ nikamuuliza

‘Kitakuwa hakina mtu…na itakuwa ni rahisi kwa mimi kukuona ukija, na nafsi yangu itafurahi sana...’akasema.

'Hamna shida upendavyo sweetie...'nikasema.

                                       ***************.
Basi siki hiyo nikajiandaa vyema kabisa…cha ajabu kila nguo niliyokuwa nikivaa niliikuta ina kasoro hii na ile,…sikupenda nguo yenye kasoro, na mimi nilipendelea siku hiyo nivae nguo yenye rangi nyekundu maana siku hiyo ilikuwa siku ya wapendanao...kweli ilinitoa kinamna nitakavyo.

‘Kweli siku muhimu sana, nashangaa amekubali tukutane siku muhimu kama hii...'nikasema huku nikicheza cheza na kujikagua kwa kupitia kwenye kiyoo kikubwa nilichoweka ukutani. Kiukweli mimi ni mtanashati sana, najipenda , na kupenda kuvaa nguo nzuri

Nilipoona nipo tayari, nikaingia barabarani, …ilikuwa asubuhi na mapema tu, sikupenda kuchelewa, na haraka nikaelekea kituoni,..kuna mwenzo kidogo wa kutembea na cha ajabu , njiani nilikutana na vikwazo vingi, mara nikutane na mtu ninayemfahamu anataka tuongee kuhusu jambo fulani, na utakuta jambo hilo ni muhimu sana…, mara nikutane na mtu anataka nimsaidia jambo, mwingine anataka nimuelekeze njia…yaani ni vitu vidodgo vidogo, vya kunifanya nichelewe

Ikafika muda sasa sijali mtu, anayeniita nakausha , nikajifanya sijamsikia,..kiukweli nilikuwa najulikana sana, na mimi ni mcheshi kwa watu…lakini kwa muda huo nikajifanya sina masikio…;.
Na mbele nikakutana na rafiki yangu akaniuliza gari langu lipo wapi, nikamwambia leo nataka kusafiri na basi, nina sehemu naelekea.

‘Basi subiria kuna dereva wangu anakuja na gari nitakusogeza mbele…’akasema

‘Hapana, leo sitaki kupanda gari jingine nataka kupanda daladala tu…’nikasema

‘Kwani unakwenda wapi mpaka uwe na masharti magumu hivyo, …usije ukawa unadaiwa hutaki kuonekana..’akasema kiutani

‘Hapana, mimi leo nina miadi na mrembo wangu….’nikasema

‘Kuwa makini rafiki yangu, nakuona siku hizi upo bize na simu,…nimekugundua sana, kama ni marafiki wa mitandao, uwe makini nao sana… , hujasikia kuwa warembo wengine ni viini macho…’akaniambia nikageuka kumuangalia, akacheka na kusema;

‘Hasa warembo wa mitandao, wanaweka picha nzuri lakini kumbe sio wao, ni watu wengine kabisa…na…na’akasema.

‘Lakini sio huyo wa kwangu mkuu…, wewe hujamuona tu…’nikasema.

‘Hebu nimuone…’akasema na mimi kwa furaha nikamuonyesha,..alipoiona ile picha akawa kama anashtuka,…na kurudi nyuma, mpaka nikashikwa na butwaa.

‘Vipi…umeonaeeh, urembo wake tu umekufanya ushtuke hivyo, je ukimuona uso kwa uso itakuwaje…’nikasema.

‘Uliwahi kuonana naye uso kwa uso…?’ akaniuliza.

‘Hapana ndio mara ya kwanza, nakwenda kuonana naye…’nikasema.

‘Ndugu yangu mimi nina kipaji, nimezaliwa hivyo…mimi sitaki kujizoesha sana mambo hayo, sipendi, japokuwa wengi wameniomba nikitumie hicho kipaji,..huwa naweza kuwatambua watu wabaya,…wenye mapepo na wachawi…sasa huyo mrembo wako nahisi sio mtu….’akasema.

‘Kwanini…?’ niliuliza hivyo, mara ukaja upepo, wa kutia mchanga, tukawa tunahangaika kujizuia, na badae huyo jamaa yangu akapata usafiri wake na kuondoka kabla sijaongea naye zaidi.

Huyu mrembo wako nahisi sio mtu…mijitu mingine bwana, wivu tu,..halafu hizo imani za kishirikina mimi sizipendi,… eti sio mtu, huyu ni nani…hahaha, watasema sana?’ nikasema nikiiangalia ile picha na tabsamu la mrembo huyo likanifanya nifarijike, nikaendelea kutembea hadi kituoni.

Nilipofika kwa bahati, nikakuta gari halina watu, wanapiga debe kuita watu, nikaingia kiti cha mbele kilikuwa na mdada mmoja, nilipoingia mlangoni mdada huyo akasimama na kushuka,..

Mimi sikumuangalia vyema, nikijua ni abiria tu, nikasogea hadi kwenye kile kiti..nikataka kukaa, lakini kabla sijakalia hicho hiti, nikaona alama za damu…damu mbichi kabisa…nikasita kukaa, nikasema;

‘Dereva mbona kiti chako kina damu…?’ nikauliza na dereva akashtuka na kuangalia ile sehemu, akasema;

‘Huyu dada aliyekaa hapa …..naona kapitiwa, nashangaa kateremka, nilimuona hayupo sawa, hata ukimuangalia macho yake, unahisi mwili unasisimuka…’akasema dereva

‘Nilimuona akiteremka kwa haraka…’nikasema

‘Oh, na damu ni ishara ya balaa…’akasema huyo dereva, sasa akawa amechukua kitambaa na kuifuta huku akilalamika baadae mimi nikaweza kukaa kwenye hicho kiti, maana nilitaka nisije kumuuzi honey wangu,..na kwa muda huo sikuwa na mawazo mabaya hata chembe , hapo akili yangu ilikuwa ni namna gani ya kukutana na huyo mdada.

Gari lilichelewa kidogo mpaka abairia wakawa wanalalamika,..hata mimi ilibidi nipaze sauti, maana hawakujua nina miadi muhimu, na badae ndio gari likaondoka,…abiria wakiwa wameshonana kweli
 Kila kituo watu wanateremka, mimi nahesabu vituo,… nilishangaa mbona kumekuwa mbali hivyo, sio kama siku ile, mpaka ikafika sehemu nikashikwa na usingizi..

Ndani ya usingizi nikawa naota nipo na huyo mdada kaja kunipokea, na sasa akawa ananipeleka nyumbani kwao, na ajabu iliyoje, tulifika sehemu ya makaburi akawa sasa ananionyesha …

‘Unaona pale ndipo nyumbani kwangu…’akasema

‘Wapi mbona sioni nyumba..?’ nikamuuliza

‘Hahaha, ina maana huoni…ile pale…’akasema

Na mimi nikakaza macho kuangalia mbele, sikuona kitu, nilichoona zaidi ni kaburi

‘Kaburi..?’ nikamuuliza.

‘Hahahaha….welcome my honey….’akasema na kucheka saana,..

‘Ndugu unakwenda wapi…?’ akaniuliza konda, na kunikatiza ndoto , nilizinduka nikiwa nahema,..na sikutaka hata kuikumbuka hiyo ndoto,.

‘Kituo cha makaburini…’nikasema

‘Oh, ni kituo kinachofuata…nasikia huko siku hizo kuna mauza uza…’akasema konda

‘Mauza uza gani…?’ nikauliza.

‘Mhh, watu wanaogopa hata kuongea maana ….nasikia hata kwenye mitandao kuna namba za ajabu ukitumiwa ukaipokea ..basi hukatizi siku…mitandao hii ina mambo, mimi sitaki kujiunga na mambo haya, mtu humjui, mnawekeana urafiki…ni ajabu kabisa…’akasema na mimi nikawa nimetulia.

Basi konda akawa anaongea mambo mengi kuhusu hayo mauza uza,….lakini mimi akili yangu haikuwa kwenye hayo mauza uza, akili yangu ilikuwa jinsi gani nitakutana na huyo honye wangu, unajua kupagawa ..mimi nilipagawa kwa huyo mtoto…nilihisi kausingizinikawa najitahidi nisilale nikaja e kupitishwa, …sijui ilitokeaje, maana mbele alionekana paka mkubwa mweusi anakatisha njia, dereva sijuii  kwa uwoga, akafunga breki,…nilirushwa kichwa kichwa  kutokea kwenye kiti na kwenda kugonga kwenye kiyoo cha mbele…

Ajabu sasa wakati tendo hili linatendeka, yaani wakati narushwa kuelekea dirisha, ..mbele yangu nilimuona huyo mdada, mpenzi wa facebook, akionyesha mikono ya kunipokea, tabasamu tele mdomoni, huku akisema ‘mpenz wangu karibu…karibu nyumbani kwetu…’giza likatanda usoni, sikujua kilichotokea baadae.

NB: Haya tusome sehemu hiyo ndogo, ili tuende sawa, akili bado haijatulia lkn nimeona nisiwavunje nguvu wapendwa wangu.

WAZO LA LEO:Kuna mambo mengine ni ya kufikirika, yapo, lakini hayana uyakinifu halisia, kuna mambo ya mashetani, uchawi nk…haya hayana sayansi kamili…lakini yapo, na watu wanaathirika na mambo hayo, na wengine wanafikia hata kuyanunua mambo hayo…mimi najiuliza iweje…kwanini ujishirikieha na mambo ambayo mwisho wake unaweza kupata shida nayo. Kitu kama mashetani yana maisha yake, kwanini utake kuyaingilia,huo unakuwa ni ushirikina!


Muhimu ndugu zanguni, tujue kuwa dunia hii ni mapito tu..ufanye ufanyalo itafika siku utaachana nayo, kwanini tujihilikishe na mambo makubwa kupita uwezo wetu.., sisi tunachotakiwa nacho ni kumjua mola wetu na kumuabudu, tufuate aliyotuamrisha tufanye na tukatazike na yake aliyotukataza, hiyo ndio njia sahihi nyinginezo ni kujitakia matatizo.
Ni mimi: emu-three

No comments :