Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, April 29, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-18


‘Nani huyoo atakuja…?’ ilikuwa sauti ya mke wa mzee Majaliwa, na kutufanya sote tugeukie huko upande sauti lipotokea, na mimi pale moyo ukaanza kudunda dunda, nikajua sasa kumekucha, sasa hali itabadilika , wote walio-niona mimi ni mwema, mtu mzuri, mwenye adabu, watakuja kuniona mimi ni mtu mbaya, muuaji..

Tuendelee na kisa chetu…
                              **************
Baba hakupenda hicho walichokuwa wakizungumza kizungumzwe kwa binti yake, hakupenda hilo jambo liendelee kuisumbua familia yake, moyoni, zaidi ya kutaka kumpata huyo aliyemsababishia binti yake hadi ajiue, hakupendelea hilo jambo liendelee kuwasumbua maana mola keshamchukua mja wake, wanataka nini tena,..

Hata kila hatua, anajikuta tatizo hilo likiendelea kumtafuna, likiendelea kumuathiri, yeye na familia yake, sasa wametokea hawa watu, anahisi wanaweza kumsaidia, lakini pia hataki familia yake isumbuliwe zaidi,.. saa je atafanyaje, …

Akageuka na kumuangalia binti yake, ambaye kwa muda huo alikuwa akimuangalia huyo dakitari msaidizi, moyoni akahisi labda binti yake keshampenda huyo dakitari, lakini ule uangaliaji sio wa kupenda ni uangaliaji  uliojaa chuki ndani yake, usoni kulionyesha kila kitu,..akajiuliza ni kwanini binti yake akawa anamuangalia huyo msaidizi wa docta kwa namna ile,…, lakini hakuweza kusema neno.

‘Nimeuliza ni nani huyo mnamsubiria kwa hamu, nimesikia baadhi ya mazungumzo yenu, naona yanahusu husu mambo ya waganga wa kienyeji, mimi sitaki mambo haya kwenye hii nyumba, sitaki tena hayo mambo ya kumtafuta mchawi yarejee kwenye hii nyumba, kwani hata akipatikana huyo mtu ataweza kumrejesha binti yetu, ni miaka mingapi imepita, iwe leo…’akasema mama.

‘Lakini mama je akipatikana huyo aliyesababisha dada ajiue, hutafurahi, ili haki iweze kutendeka..na yeye aadhibiwe?’ akauliza binti yake na kunifanya nianze kukumbuka ile ndoto,..nilijua tu…ndoto zangu huwa hazisemi uongo, nikikumbuka,…nikawa sasa naanza kutafuta namna ya kujiokoa hapo!

‘Yupo wapi, kama polisi walihangaika muda wote huo, hawakuweza kumpata huyo mtu,…ni nani sasa mwenye uwezo zaidi ya polisi kwenye kutafuta wahalifu, tuyaache hayo mambo jamani, tuyaache kama yalivyo, tumuombe mungu tu,…yeye anajua ni nini cha kufanya, atamuadhibu kwa jinsi anavyoona yeye mimi najua duwa ya mwenye kudhulumiwa haipitilizi…’akasema mama, na moyoni nilijihis vibaya kweli.

Baba mwenye nyumba akatugeukia na kusema;

‘Mke wangu hawa unawafahamu ndio wanaotusaidia kuhakikisha familia yetu inarejea kwenye msimamo wake tena, na zaidi wamesema wanaweza kutusaidia hata ile nyumba yetu tuliyoihama ikawa salama tu lakini kwa uwezo wa mungu, sio kwa madogori..unielewe hapo mke wangu,…hata tukitaka kurejea kule tutaweza au hata tukitaka kuiuza hewala,  itawezekana..’akasema mzee.

‘Mhh, kwa vipi, maana unanitia hamasa tu… ila kiukweli mimi hawa watu nimeshaanza kuwaamini , kiukweli,…sina shaka na nyie, kwa vile mnafanya mambo kwa utaalamu na kumtegemea mungu, nimeipenda hiyo…’akasema mama akitukagua mmoja mmoja, na aliponitupia mimi jicho, akasita, ni kama alitaka kusema neno lakini akasita.

'Mama usimwamini kila mtu, ndio ni madocta,lakini ....'akasema binti akitilia shaka, na baba akamkatiza na kusema;

‘Ndio hivyo,… lakini kwa namna yao wanataka kujua chanzo cha tatizo, wapi tatizo lilianzia,..unaona kama ni hivyo ina maana wanaturudisha kule kwenye majonzi,..sizani kama hilo litakufanya ubadili nia, au sio…’akasema na hapo mkewe akabakia kimia.

‘Na wamesema wanahitajia kumuhoji mtu mmoja mmoja, maana tukiongea kwa pamoja inawezekana kwasababu fulani mtu akaogopa kuzungumza jambo,..anataka kila mtu awe na uhuru wa kuongea kila kitu, hata kile cha sirini moyoni mwake,.. sasa walitaka kuongea na wewe peke yako na binti peke yake..mnaonaje…’akasema baba.

‘Sawa, kama imekuwa ni mambo ya kipolisi tena…, sawa, ila naombeni, hatutaki kurejesha msiba hapa nyumbani, ulishapita, sasa…kwanini tena, sipendi, ila kama itasaidia kumpata huyo aliyesababisha binti yetu akajiua hewala, ..itakuwa vyema ili haki iweze kutendeka..’akasema mama.

‘Je akipatikana ulitaka afanyweje..?’ akauliza binti yake.

‘Najua mwenyewe, hata kufungwa afungwe tu, hata kunyongwa, anyongwe tu, na sizani kama hiyo itatosha, na sijui kama nitaweza kumsamehe…’akasema mama.

‘Mama jamani, kama atapewa adhabu zote hizo, bado humsamehi,…mwenyewe umesema tujifunze kusamahe, sasa mbona umesema kinyume chake..?’ akauliza binti yake.

‘Sijui, kwakweli mimi sijui, kwanza ni apatikane, najua haya ni maneno tuu, kama ilivyokuwa kwa polisi, ….sasa jamani karibuni, mlitaka muanze kuongea na nani, na mimi au binti, maana binti alikuwa nahamu sana ya kuongea na nyie, hususani …msaidizi, sijui kwanini, …’akasema mama akicheka kwa utani.

‘Mamaah…, sijasema hivyo, nilitaka kujua tu, kama ni yeye au la, nahisi nimeshamuona mahali, …’akasema, na kabla mama hajasema neno, baba akasimama na kumshika mkewe mkono huku akisema;

‘Sawa, sisi tunakwenda jikoni, leo nataka kumsaidia mke wangu kupika, sasa sijui mtaongea hapa au mnahitajia sehemu ya faradha zaidi, huko chumbani kwake, kuna nafsi kubwa tu, mnaweza kwenda kuongea huko…sisi, hatutasikiliza mazungumo yenu…ila kwa mke wangu, mmh, mtaongea hapa hapa, ….’akasema baba na kumshika mkono mkewe wakaondoka..

‘Babaaah..’akasema binti yake akiwaangalia kwa makini huku tabasamu likiwa tel mdomoni lakini alipohisi yupo na wageni, akabadilika, uso ukawa hauna raha…

*************

‘Mimi nimeshakuona mahali, huwezi kunidanganya tena…’akasema binti akiniangalia mimi usoni moja kwa moja.

‘Yawezekana maana kama nilivyomuambia mama, kuna kipindi nilipatwa na matatizo, nikawa kama nimechanganyikiwa, ilianzia kwenye ajali ya gari, …baada ya hapo kumbukumbu zikawa mbovu, unajua tena,..kiukweli nimapata shida sana namshukuru huyu dakitari amefanya kazi ya ziada…’nikasema.

‘Kwahiyo mambo ya nyuma huyakumbuki..kama ulikuwa na rafiki, ukamufanyia mabaya, kama ulikuwa na mke, au mtoto…hukumbuki..?’ akauliza.

‘Baadhi , ni kama akitokea mtu aliyenifahamu akanisimulia, tulikuwa hivi na vile basi inafikia sehemu nakumbuka kidogo kidogo…, ndio maana ya safari yetu hadi tukafika huku, sikutegemea kuwa tungefika huku,..sijui, kama unavyosema uliwahi kuniona, labda unikumbushe…’nikasema.

‘Wewe hukuwahi kuwa na mchumba..?’ akaniuliza akiniangalia lakini alipogundua kuwa docta yupo anatusikiliza,akawa kama katahayari fulani hivi, mimi nikasema;

‘Mchumba,..hahaha, hapana,… labda wewe ulikuwa mchumba wangu, unikumbushe, nahisi kama hivyo, lakini sina uhakika, unajua kumbukumbu bado…wewe ulikuwa mcumba wangu au..?’ nikauliza.

‘Hapana sio mimi, mimi sio mchumba wako, mimi sina mchumba,…na wala sijawahi kuwa na urafiki na wewe, na sikujui,..lakini nahisi nilishakuona , ndio maana ninakuuliza wewe hujawahi kuwa na mchumba ukamuacha, kwani hivi sasa una mke..?’akauliza maswali hayo kwa pamoja.

‘Sijui labda,…lakini nina uhakika sina mke,… ila la kuwahi kuwa na mchumba yawezekana, sijui...hebu nifafanulie vyema..labda nina machumba mahali, unamfahamu nisaidie, nionane naye kama sio wewe…’nikasema na yeye akatulia kidogo, na hapo docta akaingilia kati na kusema;

‘Binti, uniamini,najua nyote kumbukumbu zenu hazipo sawa, sasa nataka tupambane na hizo hali, ili wote muweze kukumbuka vyema, hayo tutakuja kuyaongea baadae…’akasema
‘Docta, lakini mimi nipo ok, kumbukumbu zangu zimesharudi, labda huyu…’akasema.

‘Sawa kama wewe kumbukumbu zipo safi, basi nataka nikuulize mambo, kuhusiana na mambo yaliyopita, si utakuwa unayakumbuka yote..?’ akauliza docta.

‘Nazani, ndio nitakuwa nakumbuka, nipo safi docta…’akasema.

‘Safi kabisa,… mimi ni docta wako, kuna mambo nataka kukuuliza, hasa yanayohusiana na dada yako ni muhimu sana kwako,..na kwa familia yako kwa ujumla…, kuna kitu nimegundua…nataka usipaniki…dada yako hakujiua mwenyewe, nataka wewe unisaidie kwa hilo..’akasema.

‘Eti nini, docta,…unapingana na polisi,…kwanini, wakati inaonekana wazi, unataka kumficha huyo mbaya wetu au sio, nahisi nyie lenu moja….’akasema.

‘Tulia,…una maana huniamini tena,…kuwa mimi ni docta wenu…ina maana hutaki kujua ukweli wa kifo cha dada yako…sema kama hutaki sawa, au kama hutaki kuyareesha maisha yenu kama zamani, basi sisi tuondoke zetu…’akasema docta.

‘Haya unataka kuniuliza nini..nimekasirika, maana nahsi huyu mtu anaweza kuwa ndio yeye, na huenda anajifanya tu…’akasema akinionyeshea kidole, na mimi nikaonyesha uso wa kushangaa.

‘Kifo cha dada yako, kilipangiliwa, …lakini haikujulikana lini kitakamilika, lakini yaonekana walivyotaka wao ndivyo ilivyokuwa…maana hata wewe, familia yenu, wote mumekubaliana na hiyo dhana kuwa dada yenu alijiua…kweli si kweli?’ akauliza docta.

‘Ni kweli, kwani uwongo…lakini ungelimuuliza baba na mama, kama huniamini mimi…’akasema sasa kwa hamaki.

‘Siku kabla ya tukio hilo mlikuwa wapi..wewe na dada yako, twende taratibu usiwe na wasiwasi, nina yetu ni kuwasaidia, hatuna jipya, hatuna jambo la kukukwanza wewe, au una wasiwasi gani…?’ akaulizwa.

‘Nakumbuka siku ile, tulitoka kidogo,..si ndio unataka kujua hivyo, au,,,?’ akauliza binti.

‘Mlitoka, mlikwenda wapi wewe na dada yako,…?’ akuliza docta.

‘Sokoni,…na tukapitia dukani, na pia dada alipanga kupitia sehemu, ..’akasema.

‘Alikuambia anataka kupitia wapi, useme ukweli usinifiche, niamini , usiwe na shaka ,maana ukweli wote utasaidia mambo mengi sana….maana kuna tatizo limejificha hapo…’akasema.

‘Alisema anakwenda kumpa taarifa mchumba wake, anahisi kapoteza siku zake, kwahiyo huenda ana mimba, kwahiyo anataka waongozane akapime, wakiwa pamoja, mimi sikuamini maana dada hakuwa na tabia na wanaume…mmh, sikuamini..’akasema.

‘Kwahiyo akaenda kuonana na huyo mtu, ..wakati huo wewe ulikuwa wapi, alikuacha wapi..?’ akauliza.

‘Kwenye duka moja la ..soda, nikawa nakunywa soda pole pole kupoteza muda nikiwa naangalia runinga iliyokuwemo humo dukani...’akasema.

‘Wakati upo hapo unakunywa soda kuna mtu yoyote alikuja kukuona, mkaongea, akakuuliza hiki na kile..?’akaulizwa.

‘Mhh..ndio alikuja jamaa mmoja, msumbufu sana yule..anapenda kutufuatilia fuatilia, sijui alijuaje tupo hapo, aliegesha gari lake, akanifuata pale nilipokuwa nimekaa akaanza kuniongelesha, sikupenda, spendi kukaa hivyo na wanaume,…’akasema.

‘Alikuongelesha nini..?’ akaulizwa.

‘Yeye alizidi kunisisitiza kuwa anampenda sana dada yangu na anataka kumuoa, ananitaka mimi nimsaidie kumshawishi dada,…, lakini kiukweli, dada alikuwa hampendi,na huyu mtu alishawahi kuleta posa kwa wazazi, lakini dada kama ajilikanavyo, aliikataa, mimi sikujua kwanini awali, lakini baadae aliniambia kuwa anye mtu keshampenda, hakutaka kuniambia ni nani, alisema mpaka siku muafaka..’akasema.

‘Je akaja kukuambia ni nani..?’ akaulizwa.

‘Ndio, ipo siku moja alinitambulisha, lakini ilikuwa haraka haraka, maana mama alikuwa anakuja kutuchukua, na kweli ..mama alikuja kutufuma tukiongea na huyo jamaa, na jamaa akaondoka kwa haraka…’akasema.

‘Kwahiyo wewe ukawa umemtambua huyo mtu, kwa sura nk…?’ akaulizwa.

‘Ndio..ndio maana,..n….’akataka kusema kitu na docta akamkatisha kwa kuuliza swali jingine.

‘Huyo mtu aliyekuja wakati ukinywa soda ni nani,…?’ akaulizwa.

‘Ni lazima nimtaje..?’ akauliza.

‘Ndio ni muhimu sana…’akasema.

‘Ni …aah, anadai kuwa yeye ni ndugu yake na yule mpangaji,..anayelinda nyumba yetu, lakini simuamini, nahsi alisema hivyo ili awe anapata muda wa kufika nyumbani, na kuongea na dada, lakini dada hakukubali kabisa kuongea naye….’akasema.

‘Kwahiyo mara kwa mara alikuwa akifika nyumbani..?’ akaulizwa.

‘Ndio hasa wakati wazazi hawapo, sijui alikuwa anajuaje,…’akasema

‘Yeye anaishi wapi…?’ akaulizwa

‘Yeye ana makazi yake huko Mbezi, ana uwezo fulani hivi…’akasema

‘Ok, ana kazi gani, anajishughulisha na kazi gani..?’ akauliza.

‘Yeye …anadai alishawahi kwenda nje na kuishi huko kwa muda, baadae ndio akarudi hapa nchini, na aliporudi hapa nchini, akawa kaajiriwa hapa na pale, akaja kufungua studio,…anatengeza matangazo..ni mbunifu wa matangazo,,anavyodai yey, ila kwa sasa hivi ana duka kubwa sana, kama super market….kiukweli ana uwezo, ila hajaoa, alitaka kumuoa dada…, sijui kwasasa, labda kama keshaoa, mimi sijui taarifa zake zaidi…’akasema.

‘Kiukweli unavyoona, je alikuwa akimtaka dada yako au likuwa akikutaka wewe?’ akaulizwa

‘Yeye alimtaka dada…si ndio mpaka akaleta posa…’akasema.

‘Ndio alimtaka dada, lakini wewe alikuwa hakuoni mara kwa mara ana alipokuona wewe akawa kama kakupenda wewe zaidi, kweli si kweli..?’ akaulizwa.

‘Hahaha..sina habari na yeye kabisa, wala simpendi, ..sipendagi wanaume, yeye ananisumbua tu kuwa,…kama dada hamtaki, basi anioe mimi,…nilimkatalai kabisa nahisi kuna kitu ambacho sio cha kawaida kwake…’akasema.

‘Kwanini…unahisi nini?’ nikamuuliza mimi.

‘Muongeaji sana, halafu, kama ni tapeli fulani hivi, anajua sana mambo ya nje, wengine wanahisi anauza unga, madawa ya kulevya, wengine…mmh, wanasema huenda ni…ni..’sema tu.

‘Ni friimasoni, ..kitu kama hicho…’akasema.

‘Nini, ..ni nani alikuambia hayo..?’ nikamuuliza sasa nikihisi hatari, maana hao watu nimesikia sifa zao, na sitaki kuwafuatilia zaidi.

‘Watu wanasema tu mimi sijui, unajua siku hizi mtu akiibuka na mali,..akatajirika kwa muda mfupi,  basi watu husema mengi, hukimbilia kusema huyo mtu ni friimason..sasa sijui, ..ila watu wanasema hivyo..’akasema

‘Kwahiyo baada ya hapo dada yako akarudi, aliporudi ilikuwaje..?’ akauliza

‘Alikuwa analia tu…, hakutaka hata kusema, au kuongea chochote, mimi namfahamu sana dada yangu akiwa kwenye hali kama hiyo, inatakiwa umpe muda, basi tukaondoka naye,…tukiwa njiani ndio tukakumbuka kuwa alikuwa na mpango wa kununua dawa, tangia awali tulikuwa na mpango huo, kwani alikuwa anajisikia vibaya , ..basi tukapitia duka la dawa akanunua hizo dawa..’akasema

‘Unakumbuka ni dawa gani alinunua,…?’ akauliza docta

‘Ni dawa za maumivu tu,  maana alikuwa hajapima kuwa ana tatizo gani, na hata yeye alihisi ni mauchomvu tu, kichwa kinamuuma, basi, ndio hivyo…?’ akauliza

 ‘Una uhakika alinunua dawa hizo..?’ akaulizwa

‘Kwanini unaniuliza hivyo, ndio…wakati ananunua nilikuwepo, aliagiza dawa za maumivu, na akapewa,….nakumbuka kabisa hilo.., hata leo, nimeziona kwenye kabati, nilishangaa kuziona, kumbe polisi niliwapa zingine,..kulikuwa na kipaketi kingine cha dawa za maumivu, sijui kwanini hatukuziona mapema, tukakimbilia kununua nyingine..’akasema

‘Zipo wapi hizo dawa, , ..’akasema

‘Kwenye kabati lake…’akasema

‘Kwahiyo polisi waliulizia dawa gani, ukasema ni za maumivu, wakazichukua kwa ajili ya uchunguzi, au sio..?’ akauliza

‘Ndio…lakini nimegundua kuwa sio zenyewe walizochukua, nilikuja kugundua kuwa nilichowapa sio chenyewe, lakini zote zimeandikiwa jina hilo hilo..dawa ya maumivu…’akasema.

‘Hebu twende ukanionyeshe..’akasema na docta wakaingia ndani , kwenye chumba caha mabinti, maana walikuwa wakichangia chumba, mimi nikabakia peke yangu hapo kwenye chumba cha maongezi, haikupita muda mara mlango ukagongwa…nikajiuliza nifanyeje , maana wenyeji hawapo, kabla sijasema kitu mara mlango ukafunguliwa.

Jamaa alikuwa kasimama mlangoni, akiwa na macho yaliyovimba, utafikiri hajalala, uso ulikuwa umekunjamana, kama ana hasira fulani, macho yamemtoka, aliponiona tu akasogea kunijia, lakini akasimama …akageuka huku na kule kama anahakikisha jambo, halafu akasema;.

‘Oh,… nyie mlifanya nini kule…?’ akauliza

‘Wapi mbona sikuelewi…’nikasema.

‘Nyie....mliingia ndani na kuniharibia mambo yangu, hivi ni tabia gani hiyo, mnaingie kwenye majumba ya watu, na kuanza kuharibu …na kuiba,… mnajua nilikuwa nafanya nini pale, mumeharibu kila kitu, mumeni..weka pabaya,…sasa halafu kwanini mumechukua dhamana yangu..’akatikisa kichwa kama kuhisi kitu, akahema kwa nguvu, alikuwa hayupo sawa kwa ujumla.

‘Dhamana yako, ndio nini,….na hakuna aliyeingia nyumbani kwako, kwani wewe unaishi wapi, mbona sikuelewi…’nikasema.

‘Ooh,..nyie watu nyie watu….kwanini… nipeni haraka, mnanitesa,..hiyo..sio mali yenu kwanza naweza kuwaitia polisi kuwa mumeingia kwenye nyumba na kuiba, …’akasema sasa akinikodolea macho.

‘Itakuwa vizuri ili polisi wajue unachokifanya..’nikajisemea tu hivyo na kweli niliona imefanya kazi.

‘Kitu gani nimefanya, nimefanya nini, nipeni ..kwani mwenzako yupo wapi, halafu, …wewe bwana mdogo usiinichezee unanijua mimi ni nani..?..., unajua naweza kukuharibu ,…kwanza bahati yako..’akasema.

‘Bahati yangu nini..ulitaka kuniua sio kama ulivyomuua, …’kabla sijamaliza, mara docta akarudi na yule binti, jamaa huyu alipomuona docta, na huyo binti, akanywea, akajifanya mpole, akawa anajitahidi kuficha ile hali aliyo nayo, mara akaanza kutikisika, halafu akasema maneno hayaeleweki, na kumalizia hivi…

‘Vuuuuuuuh, haya haya…nipeni habari, mnataka nini, sio mimi jamani, …’akasema akawa anatikisa kichwa, huku anaitikie, ‘Taire..taire..taire…’ halafu akasema;

‘Sio mimi wahenga, sio mimi, nilitaka kukamilisha kazi, watu wakaniingilia, wakaharibu, sijui ….nimewaona, …lakini sijakipata….’akatulia, huku anaitikia ‘taire, taire..taire, ..’ halafu akasema;

‘Hapana wahenga sio mimi, sijaharibu,…nilikuwa mbioni kukamilisha,….na, niwapeleke wale watu, lakini kabla, ndio,…oh,… nisaidieni,…’akatulia, na mara akawa kama anahisi maumivu, anajinyonga nyonga, na kulia kama mtu anayeteswa, baadae akasema…

‘Wahenga jamani nisaidieni jamani, sio mimi sio mimi…nitaongea na hao watu, nitaambia, hapana msiniue,..’ ghafla akalalala akadondoka, sakafuni…

Sisi pale tukabakia tumetulia tu, baadae akina mama na baba wakafika, huku wanauliza;

‘Kuna nini mbona tumesikia kelele, za mtu kama ana….omba msaada, kuna nini, tulijua mambo yameharibika..’akasema baba, na mara wakamuona huyo jamaa kalala sakafuni, ..
‘Vipi tena huyu mtu karudi mbona kalala hapo, ana nini..?’ akauliza mzee

‘Hata hatujui kaja,...maana kaingia na kuanza kupandisha , anaomba sijui wahenga wake wamsaidie….na ghafla huyo kadondoka chini…hatuelewi ana nini…’akasema docta.

‘Mhh…sasa hili si balaa kweli, hivi, akitufia humu ndani itakuwaje..’akasema mama

‘Atazindukana tu, msiwe na wasiwasi..mimi niliwaambia huyu mtu atakuja, kuna kitu chake muhimu anakitafuta, ndio mambo yao wanayopewa huko, sasa sijui ni cha mababu zake au kuna watu wamempa,….’akasema docta.

‘Kitu gani mnacho nyie….?’ Akauliza mzee.

‘Ndio tunacho…tulikichukua, yeye anajua umuhimu wake,  sasa ndio huyu keshakuja…atazungumza yote..yaonekana huyu mtu ana mambo makubwa sana, ambayo yanaweza kuhusiana na matatizo mnayoyapata,...na huyu ndiye atakuwa njia yetu, …’akasema docta.

Na mara simu ya huyo jamaa ikawa inaita…ilikuwa mkononi mwake.., docta akasogea pale kwenye hiyo simu na kuichukua, kwanza akawa anasita kuipokea, baadae, akasema, kuniuliza mimi…

‘Simu yako si inaweza kurekodi,…nataka urekodi sauti ya huyu jamaa akiongea,  sina uhakika ni nani anampigia, hapa imeandika jina moja tu,  ‘mkuu’ haya naiweka hewni weka chambo cha kurekodia

‘Docta akaiweka hewani, na mara sauti ikasikika ikisema;

‘Sasa umefanya nini..mbona hajaonekana huku, na…umefanya nini mbona umeharibu, hatukuoni huku,…upo gizani,…na ile kazi imeishia wapi,…unakumbuka…ni lazima ikamilike kabla ya siku tano , zimebakia siku mbili, vinginevyo, utageukiwa wewe mwenyewe..unasikia, mbona hujibu kitu…wewe…sema …shhht...’mara akakata simu.

Tukabaki tumeangaliana, na docta akasema,…

‘Mkuu…huyu mtuni nani,…sasa chukua hii namba yake uweke kwako ufanye kama unamtumia pesa, itataja jina lake…’akasema docta, na mimi nikafanya hivyo, na mara jina likatokea…

NB: Kuna nini hapa, kumbuka haya yote yalianzia kwenye facebook, nikampata rafiki, rafiki ndiye kanivuta hadi nimefika hapa, je ni bahati mbaya, au kuna nini zaidi..tuzidi kuwemo


WAZO LA LEO: Kutokana na shida, hali za maisha kuwa ngumu, watu wengine hutegeka na kujiingiza kwenye mambo wasiyoyafahamu ilimradi tu wapate kipato. Shida na nakama za maisha sinawafanya watu wanakosa subira, wanaacha maamurisho ya mungu , ya kutenda mema, na badala yake wanakuwa tayari kutenda maovu, mambo ya kishetani, ..lengo likiwa ni utajiri, hivi ni kweli shetani anaweza kukupatia utajiri hivi hivi…tuweni makini, tusidanganyike,…Tumuombe mungu atulinde na kutuongoza kwenye njia sahihi,…Aaamin.
Ni mimi: emu-three

No comments :