Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, April 27, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-16‘Unasema wewe ni mpenzi wake wa facebook, kwanini hujampigia yeye mwenyewe kwenye simu yake,..?’ akauliza docta

‘Hayupo hewani, lakini simu…’akasema akiniangalia mimi, ni kweli simu yangu ilikuwa imezimika.

‘Umeipataje namba ya simu yangu..?’ akauliza

‘Oh,…kwahiyo wewe upo wapi..nyumbani kwako wapi…ok, kwahiyo wewe unataka nini sasa,..aje au tuje, wapi sasa..nyumbani kwenu wapi..?’

‘Makaburini..?’ akauliza docta kwa mshangao

‘Unajua usituchezee akili, sema wewe ni nani..?’ akauliza docta kwa sauti kali, halafu akawa anasikiliza.

‘Ok tunakuja, …na nasema sitaki kusumbuana, kama wewe ni mpenzi wake kweli, basi ujitokeze, na tusiwe tunafika hapo,  halafu hakuna mtu, mimi sio mtu wa kuchezewa, unasikia,…sawa, tunakuja..’akasema na kukata simu

Docta akaniangalia kwa makini , halafu akasema;

‘Unajua kuna kitu kipo nyuma ya haya yote…, na inabidi twende huko makaburini anapodai huyo mpenzi wako wa facebook yupo na tutakutana naye huko.., lakini ..hebu fungua mtandao wako wa facebook..’akasema docta na mimi nikafungua mtandao wangu na kwenye page yangu, sasa nikamuona huyo menzi wangu wa facebook, sasa akiwa hewani.

‘Hebu chat naye…’akasema na mimi nikaanza kuchat naye, na huyo mpenzi wa facebook, akaandika ujumbe kuwa mimi nimemsahau sitaki hata kuwasiliana naye..yaonekana simpendi tena…

‘Lakini wewe ulikuwa umefunga akaunti yako ya facebook, ningewezaje kuwasiliana naye…’nikamwandikia hivyo.

‘Samahani line yangu ilipotea, na sasa nimeirudisha tena, ila siku kadhaa nilipojiunga tena, sikukuona ukiwa hewani ndio nikajua hunitaki tena..’akaandika hivyo.

‘Sasa kwanini umempigia simu docta, …unataka sasa hata yeye akufahamu kwanza umemfahamuje, na namba yake..?’ nikamuuliza

‘Ndio najua huyo ndie mshirika wako wa karibu…yeye anajulikana sana, hata namba zake kazitoa, zipo hewani kwasababu ya utaalamu wake,…sasa nilikuambia awali sitaki nijulikane na watu, sitaki urafiki wetu ujulikane na watu, kabla wazazi wangu hawajafahamu, mbona umeshamjulisha huyo docta wako...’akauliza

‘Lakini yeye ni dakitari wangu , na hajui kuwa mimi na wewe ni marafiki ndio maana nashangaa wewe kumpigia simu yeye…’nikasema

‘Kwahiyo sasa umeshaanza kunidanganya, hivi kweli unania ya kunioa mimi, ..wakati unanidanganya,…wakati mpo na huyo docta, kila kitu anakifahamu,…’akasema

‘Sasa unataka tufanyeje ili uweze kuniamini, ..nilishakuambia nataka kuja kwako kujitambulisha, ukanielekeza vibaya, sasa unataka mimi nifanye nini..’nikaandika

‘Kama umeshajiandaa haya wewe njoo, itakuwa vyema zaidi, …nataka uje eeh, ok, njoo tu…’akaandika hivyo.

‘Nije wapi sasa..’nikauliza

‘Kule kule nilipokuelekeza kipindi kile…, utanikuta nakusubiria, ..’akasema

‘Unauhakika maana safari zote nikija unakuwa haupo, kiukweli nina hamu sana ya kukutana na wewe..’nikasema

‘Usijali utanikuta…ukitaka unaweza kuja na huyo docta wako…baadae kuna kazi nafanya..’akasema na kutoweka hewani.

Docta akasema twende…na tukaondoka naye hadi huko maeneo ya makaburini, na tulipofika hatukukuta mtu, kama alivyodai yeye, tukazunguka wee, mpaka tukachoka, tukapiga simu ikawa haipatikani.

‘Umeona eeh, huyu mtu kuna kitu anakitaka kwako…’akasema docta

‘Kitu gani docta…una maana huyu mpenzi wa facebook,?’ nikauliza , lakini docta hakunijibu alikuwa kama anachunguza jambo, akawa anaangalia huku na kule kwa makini, hlafu akasema;

‘Hebu twende kwenye hilo kaburi, alilozikiwa huyo mpenzi uliyemuasi,..akajiua..’akasema

‘Mimi silijui, …sijawahi kufika eneo hili nikaingia ndani kwenye maeneo ya makaburi,, safari ile ya kwanza niliishia hapa…’nikasema

‘Litakuwa lile pale,..walisema limejengewa vizuri, lile pale,…huoni hata jina lake..’akasema na kuanza kutembea kuelekea huko, sikupenda kwenda huko lakini ikabidi, nikawa namfuatilia nyumna docta hadi tukafika.

Lilikuwa limejengewa vizuri tu,..ila kuna sehemu inaonekana kama ilibomoka, au kubomolewa kwa pembeni, na kukarudishwa tofali kama kuegeshewa tu,…docta akapachunguza, baadae akasema;

‘Hapa nahisi kama kuna mtu kabomoa,kwa makusudi, …hebu kwanza,akajaribu kuinua lile tofauti kuliondoka, lakini likawa limekaza halitoki..baadae akaghari na kucha kama lilivyo.

‘Kuna mtu anatuchezea akili..’akasema docta akiangalia huku na kule

‘Kwa vipi..?’ nikauliza

‘Wewe huoni hapa,…ni kama kuna mtu alipabomoa hapa kwa makusudi halafu akaja kulirejesha hili tofali , kwa kulichimbi, hapa hapajajengwa zamani, ni karibuni, unaona hii sementi sio y asiku nyingi…, angalia hapo, kuna mguu uliokanyaga hapo, na kuacha nyayo za cement..’akaonyesha,..

‘Ina maana kuna maiti ..inatoka kaburini..na kuja duniania..?’ nikmuuliza

‘Maiti haiwezi kutoka kaburni…huyu ni mtu anafanya usanii, lakini ngoja tuone kwanza, unajua kuna kitu tunatakiwa tukifanye kisayansi ili kuondoa sintofahamu kwenye vichwa vya watu…kama ingeliwezekana , wenyewe wakaturuhusu tungelilibomoa hili kaburi tuone huko ndani kupoje, inaonekana kabisa kuna uwazi ndani, …’akasema

‘Oh, haiwezekani, maana kaburi linashushiwa udongo mwingi sana, na kujazwa, iweje kuwe na uwazi..?’ nikauliza

‘Ndio maana hata mimi ninashangaa…’akasema , akawa anachunguza,kulizunguka hilo kaburi, mpaka akaona kuna sehemu kuna uwazi, akachukua kijiti na kukizamisha kwenye huo uwazi, kijiti kikazama chote..

‘Unaona…kuna uwazi kwa ndani, sijui kuna nini humo ndani, lakini hatuwezi kufanya lolote kwa sasa, …’akasema

‘Sasa..?’ nikauliza nikichunguza ule uwazi, na kuhakikisha kuwa kweli kuna uwazi fulani kwa ndani.

‘Inabidi , ikibidi tuongee na wahusika, ili tuje kubomoa,lakini hata hivyo..kwanini kwenye hili kaburi, kuna kitu hapa,...’akasema docta

‘Labda tuwaambie kuna uchunguzi unafanya wa kidakitari, lakini havyo docta, ili iweje, tunataka kuhakiki nini,…’nikasema

‘Ok,..tuachane na hilo,.. ukumbuke tuna safari ya kwenda  nyumbani kwa Mashauri, nataka wewe ukaongee na huyo binti yake, uone kama anakukumbuka, au ana nini anachokitaka kwako,je yupo tayari umuoe, maana kiukweli ni lazima umuoe,..hiyo ni sehemu muhimu kwako, na kwa hiyo familia..’akasema

‘Lakini docta, yawezekana huyo binti ndiye anatuchezea,… huenda ndio yeye kajiingiza kwenye facebook akatafuta picha ya kihivyo..inayofanana fanana na yeye au sio, na dio huyu ana…kaja huku kutuchezea akili, hulioni hilo..?’ nikauliza

‘Sizani, maana yeye anaumwa kweli, hawezi kutembea,ndio anaweza kuchuku bajaji akaja akafanya hivyo, lakini jiulize ili iweje, anataka nini…haiji akilini,…labda awe anashikirikiana na mtu mwingine, swali bado ili iweje,…nahisi kuna mtu mwingine, yupo nyuma ya hili jambo, ana utaalamu wa mitandao, na…ni mtaalamu wa nguvu za giza, yawezekana huyo huyo ana mawakala, au yeye huyo huyo anajianya  mpenzi wako wa facebook…’akasema

‘Lakini awali ulisema huyo mtu ni shetani..’nikasema

‘Yawezekana ni shetani kweli…lakini uelewe shetan pia anaweza akawa binadamu kutokana na matendo yake kuna watu mashetani, wanakula nyama za wafu, ..wanakunywa damu za watu, tunaishi nao….dunia hii ina mambo..’akasema

‘Docta..unaamini hayo mambo kuwa yapo kweli, mtu ale nyama za wafu, ni mtu kweli huyo, hapana docta..’nikasema

‘Tutaona huko mbele, mimi sio mganga wa kienyeji, natumia sayansi kuhakiki mambo, ila hisia zangu zinaona kuwa kuna mtu yupo nyuma ya hili jambo sijui dhamira yake ni nini,…na pia yawezekana ni shetani, au ana tabia za kishetani, kama nilivyokuambia kuna watu kwa sura na maumbile lakini kitabia sio wenzetu...’akasema

‘Ohh, docta naona unanichanganya ok, uonavyo,,..sasa..’nikasema

‘Subiri…unaona ile karatasi pale, yaonekana imepeperushwa, ilikuwa pale juu ya kaburi…,unaona alama ya kubanduka,…hebu, usiguze kwanza…’akasema na kuchukua kijiti, akaigeuza ile karatasi,…na ndipo tukaona maandishi, kulikuwa na maandishi yaliyoandikwa kwa rangi nyekundu, ni kama damu iliyotumika kuandika; maneno haya;

‘Karibu mpenzi wangu wa facebook, hapa ndio nyumbani kwangu, najua siku si chache tutaungana pamoja..mimi nikupendaye ..mpenze wa facebook.

Docta akawa anatumia kijiti kukwangua kwangua yale maandishi…, ni kama bado yalikuwa hayajakauka, kwani kila kikwangua na kile kijiti, inajichora..…akaacha kile alichokuwa akikifanya akawa anaangalia huku na kule

‘Kuna mtu kaweka, huu ujumbe na hayupo mbali, mhh, huyu mtu ni hatari….’akasema akichunguza huku na kule, lakini hakukuwepo na mtu karibu, ila yeye ni kama naona kitu ambacho mimi sikuoni..

‘Hata maandishi hayajakauka vyema..’akasema, na kuchukua kifaa chake kwenye vitu vyake, ni kidarubini kidogo, akawa anachunguza yale maandishi,..na kusema

‘Hii damu kabisa..ya mnyama au mtu..’akasema na akachukua kichupa na kuanza kukwangua ili kupata sample akaweka kwenye chombo, na kusema;

‘Nitaenda kupima kwenye maabara…’akaweka kwenye nailoni, halafu akaichukua ile karatasi na kuiweka kwenye nailoni alikuwa kavaa kinga kwenye mikono yake, na alipomaliza kuziweka hizo kumbukumbu, akasema;

‘Unajua hili jambo sasa linaanza kuleta sura nyingine tofauti na nilivyodhania,..kuna hatari kubwa, nahisi kuna dalili za mauji….’akasema

‘Kwanini..?’ nikauliza sasa nikimuangalia docta kwa mashaka.

‘Inabidi tumtafute huyo mpenzi wako wa facebook au huyo anayejiigiza kuwa ndio yeye, nahisi kuna mtu anakuchora,..anayekujua wewe na mahusiano yenu ya nyuma, kuna mtu…sizani kama ni mtu kweli…’akasema

‘Oh, kwanini unafikiria hivyo, unahisi labda ni shetani..?’ nikauliza

‘Wewe huoni, kwanza jinsi gani alivyoweza kukulaghai, hadi ukaingia kwenye mtego wake,… halafu akakuvuta hadi ukaja kukutana na hiyo familia, na sasa kuna jambo anataka kulifanya,…usiogope, ila nahisi anataka kukutendea jambo baya, lakini anataka kujenga hoja ya visingizio,..hoja ambayo hata familia yako haitaweza kuigundua…’akasema

‘Una maana gani docta, kuwa ataniloga, au , doctaaa…, usijifanye unaamini mambo hayo, hakuna mtu wa kuniloga mimi, kwanza siamini mambo hayo..’ nikasema kwa kujiamini.

‘Unajua mimi nina uzoefu sana na haya mambo ya watu na tabia zako, …kuna watu wanaweza kutumia mshetani, au viini macho wakiwa na malengo yao binafsi, kuna wengine wanayatumia mambo hayo kutaka utajiri, japokuwa hao wa hivyo na utajiri wao,..hakuna hata mmoja anyeweza kuishi kwa raha, ni utajiri machoni mwa watu ila kwao wao,… hawana amani, na kifo chao huwa kibaya sana…’akasema docta

‘Mimi sijui..’nikasema.

‘Lakini wapo hao wenzangu na mimi…ushirikina, na uchawi, hawana mbele wala nyuma, kazi yao kubwa, ni kughilibu vichwa vya watu, kuwasumbua watu wamelala, na kuwachezea, hawana lolote, ujinga na wao,..na nikuambie kitu,..sio wote wanaosema wana mashetani, kuwa wana mashetani, wengine ni ghiliba tu, ili kutamiza malengo yao..sasa uwe makini sana…’akasema docta

‘Kwahiyo docta ndio kusema hayo mambo yapo, na wewe unayaamini , na kama unayaamini, unataka tufanyeje sasa, mtu kama mimi ambaye siyaamini kabisa.., kwanini tusiwaambie polisi,kama una imani kuwa kuna maafa dhidi ya watu kwa kupitia njia hiyo, si tuna ushahidi, na wewe unayafahamu hayo mambo, au..’nikasema

‘Polisi hawawezi kuingilia mambo kama haya yasiyo na ushahidi unaoshikika, kwa hili, kwa sasa hivi, sijui huko mbeleni, itakuwaje..ila kuanzia sasa, kutokana na hili, sisi ni polisi , wapelelezi, … muhimu kwa hili, unisikilize, na unifuate nitakachokuambia, narudia tena, ukiwasiliana na huyo mtu, usinifiche jambo, kwa angalizo, sio nakutisha, wewe upo hatarini..’akasema

‘Nipo hatarini kwa vipi docta,…usinitishe….na unasema nichati na huyo mdada, maana nimemumisi kweli.?’ nikauliza

‘Sawa…nakuona bado unalichukulia jambo hili ki mzahamzaha.., huu sio mzaha, unawafahamu watu wanaoitwa freemasoni..?’ akaniuliza

‘Nawasikia tu…wapo kwenye mitandao, wana mpaka mtandao wao..unajua mimi siamini mambo hayo ya kutaka utajiri, sijui …siamini, sasa wengi wanajiingiza huko eti wakitaka utajiri, mimi sina tabia yangu…’nikasema

‘Sasa haya mambo yana fanana fanana hivyo, uwe makini sana, ..hii mitandao kuna wengine wanaitumia kwa namna yao, wameshajua huku kuna watu wanaingia lakini hawajui kabisa wakitendacho, kazi yao ni bendera fuata upepo, wanaweka mapicha yao, wanaweka kumbukumbu zao za simu, ni hatari,..kuna watu watalizwa humu, na..na hebu ngoja kwanza, kwenye ndoto yako uliota upo maeneo gani ..?’akaniuliza

‘Hata sikumbuki…ila kweli…nilikuwa maeneo kama makaburini, au..unajua unaota kama umelala, lakini upo mahali fulani hivi, ndio nakumbuka nilikuwa sehemu tulivu, kuna miti miti…baadae tukajikuta tupo na hiyo familia, kama vile tupo mahakamani, mimi nimesimamishwa kuhukumiwa,…mengine ni kama nilivyokuambia...’nikasema

‘Kwanza nataka twende kwenye hilo jengo walipokuwa wanaishi hiyo familia, na tukitoka huko tunaweza kwenda kuonana na wagonjwa wetu..’akasema

‘Ina maana huyo aliyekupigia simu alikuwa nani, mimi nilijua ni huyo mgonjwa wetu, binti..?’ nikauliza

‘Sio yeye, ..nilidhania hivyo awali , lakini wakati tunakuja huku niliwapigia simu, nikaongea na mama yake, anasema mgonjwa bado hajaweza kutembea vizuri, na siku nzima ya leo alikuwa naye…sasa angeliwezaje kuja huku…’akasema docta.

‘Kwahiyo ina maana uliyeongea naye,huuenda ni…ni huyo mpenzi wa facebook..docta hapo mimi sijakuelewa, nahisi kama unachanganya mambo..?’ nikauliza

‘Wewe unasemaje…, je huyo mpenzi wa facebook, yawezekana akawa nani, unahisi labda ni huyo dada mgonjwa au, hebu rudidha kumbukumbu zako…maana mlikuwa mnatumiana picha,unasema picha zote alizifuta, lakini unamkumbuka vyema, au sio…na sasa umeshamuona huyo binti mgonjwa,  je wanafana ..?’ akauliza docta

‘Unajua nikimuangalia huyo binti, inakuja taswira machoni mwangu, kama zile picha za huyo mpenzi wa facebook, lakini nikimuangalia sana, sura ile inaondoka…na nikimchunguza sana huyu binti, ndio kuna kufanana fulani hivi…, lakini sio yeye,  maana, huyo mgonjwa, macho yake yamezidi ukubwa na uzuri zaidi…na kwa upande wa huku usoni yule wa facebook ni mnzuri zaidi, unaona, ,…kuna utofauti fulani, lakini mmh, utafikiri ndio yeye…’nikasema

‘Hapo sasa,.huoni kuwa kuna jambo limejificha,..ndio maana nataka twende huko kwenye hilo jengo lao walilolitelekeza, kuna kitu kinanivuta twende huko,..nataka kuliona na kuingia ndani, …na sijui huyo mwenyeji wao kama yupo au keshaondoka…’akasema

‘Aondoke kwenda wapi wakati yeye ndio mlinzi au..?’ nikauliza.

‘Sio mlinzi yule, ..alikuwa mpangaji wao..na walipohama wenye nyumba, yeye akaendelea kubakia humo..’akasema

‘Kwanini sasa,…?’ nikauliza

‘Ndio swali langu hata mimi, hebu twende huko…nataka kuliona hilo jengo, ila subiria kwanza tuombe ulinzi maana huko tunakwenda kwenye miliki za watu..na kama hayupo itakuwa vyema,..nahisi hayupo,…’akasema

‘Unajuaje…?’ nikauliza, lakini docta hakunijibu yaonekana alikuwa kwenye maombi, au anawaza jambo, huku tunatembea…

Tukatembea, ilikuwa sio mbali sana na hapo makaburini, tulipofika, docta akaniambia niwe namfuata nyuma …nisitembea mbali na yeye, sikumulewa, alikuwa kama anaona jambo, lakini hataki kuniambia.

‘Yaonekana hakuna mtu, ndani ya nyumba, ila kuna dalili za harufu na moshi, huuoni …’akasema

‘Mhh, mimi siuoni, hata harufu bado….…’nikasema.

‘Hebu subiria,…’akachukua gloves za mikono, akavaa, akashika kitasa cha mlango, akazungiusha kitasa, mlango ukafunguka,..akaniashiria tuingie ndani,..nilihisi mwili ukinisisimuka…nikasita kuingia lakini kwa hali kama hiyo nikaona nisicheze mbali na huyu mtu.

‘Sasa na mimi.., puani kulipenye harufu kali ya manukato ya kufukiza, ..nilihisi hata kichwa kinaanza kuniuma, docta akawa anatembea taratibu huku mimi namfuata nyuma, ni kama tunanyata…alikuwa na tahadhari kweli, ni kama anaona kitu ambacho mimi sikioni,, …tukafika sehemu ya mapokezi..kati kati ya sehemu hiyo ya mapokezi,..kulikuwa na chungu, kinafuka moshi, na juu kimening’inizwa kitu kama vibuyu, kina shanga za rangi mbali mbali…

Docta akawa anavichunguza vitu hivyo kwa macho, chini sakafuni, nikaona karatasi,..kama ile ya kule kaburini, na maandishi yale yale… na pemben kuna kuna picha, ..picha ya msichana,..niliitizama kwa makini…mmh, sio picha ya …marehemu…ndio ni picha yake!…oh..na kabla sijasema kitu kwa docta mara nikaona picha yangu.

‘Picha yangu docta na ya marehemu...!’ nikasema.

‘Docta akaniashiria kwa kidole kuwa nisiongee, akasogea hadi kwenye ile picha, akazisogeza mbali na kile chungu, hakuziokota kwanza…, akachukua kijiti na kuchokonoa chokonoa kwenye kile chungu, ..yalikuwa makaa ya moto, na yalikuwa na moto… na mafukizofukizo….

Docta akaangalia kushoto na kulia, …akawa kama anatafuta kitu, akaona alichokitaka..maji,..kumba alikuwa akitafuta maji, akayaendeea, akayachukua yale maji, kwenye chombo, akawa anayasomea kitu, halafu akafika kwenye kile chetezo,..chungu akaanza kumwagia maji mle kwenye chetezo huku akiweweseka maneno mdomoni,, na moshi ukawa unatoka, ,,kama vile ukizima makaa ya moto inavyokuwa, lakini cha ajabu, ule moshi ulikuwa kama unakwenda juu na kuzama kwenye kile kibuyu kilichokuwa kimening’inizwa.

Baadae akahakikisha kuwa ule mkaa umezimika wote, taratibu akisogeza mkono na kukichukua kile kibuyu chenye uchanga, akakivuta, kwa vile kilifungwa na kamba kutoka juu kikawa kimening’inia,..kwahiyo akakivuta hadi ile kamba ikakatika akakichukua kile kibuyu, akawa anakikagua, halafu akatikisa kichwa kama kukubali jambo.

Sikumuelewa,..ila alionyesha uso kama kutabasamu hivi …

‘Sasa basi kaisha..’akasema akawa anahakikisha kifuniko cha kile kibuyu kimefunikwa vyema…

‘Nani…kaisha?’ nikauliza.

‘Atakuja mwenyewe, twende zetu…’akasema na mimi bila kusema neno nikamfuata nyuma, nilikuwa sijisikii nyema humo ndani, maana pumzi likuwa ndogo,..na kabla hatujatoka, docta alihakikisha amechukua zile picha na kuhakikisha kuwa hakuna moto tena…

Tukatoka nje ya lile jengo, docta akatoa kitu kama mafuta akawa anasoma soma soma huku anayarushia mafuta hiyo nyumba,..halafu akasema;

Kwa uwezo wa mungu,..mabaya yote, mashetani yote, na viini macho vyote viteketee, na nyumbahii iwe salama na amani, kwa uwezo wako ewe muumba, mungu mwenyezi, weka ulinzi kwenye nyumba hii na mabaya yote yaangamia, na kupotea…’akarusha hayo mafuta, na kukawa kama kitu kama upepo ukavuma halafu kukawa kimia.

‘Ok, sasa tumemaliza, twende…’akasema na mimi nikamfuata nyuma, sikuwa na neno, nilihisi kabisa sehemu hiyo sio salama, harufu, mwili unasisimuka, pumzi inakuwa ndogo..

‘Unajua ..kuna watu wabaya sana kwenye hii dunia, ..’akasema.

‘Nani hao..?’ nikamuuliza.

‘Bado sijajua,… mimi sio mganga wa kienyeji wa ramli, mimi nafanya mambo kwa kumuomba mungu,..ndio napata njozi, napata maelekezo, lakini huwa sifanyi jambo mpaka niwe na uhakika nalo..nilihis kuna jambo,..sasa naanza kugundua,kweli lipo jambo,…lakini sina uhakika huyo mtu ni nani na ana mantiki gani, na lengo lake hasa ni nini,..lakini atakuja mwenyewe..’akasema.

‘Docta sijakuelewa..’nikasema.

‘Ulikuwa unasema kuwa unahisi kuwa kuna mtu anakufuatilia mara kwa mara ila humuoni…na kila unapokwenda, anakuw akaribu yako, …na ulipofika hospitalini, ukaenda kwa mama mmoja,..unakumbuka..’akasema.

‘Ndio…nakumbuka docta nilikuambia hivyo…’nikasema.

‘Hawa watu wajanja sana,…wanataka kutawala kila mahali,..sasa wameingilia hata mitandao,..na wana mawakala wao, wengine wameingia kwenye majumba ya ibada wanajifanya watu wa dini, wanatoa mapepo, wanafanya miujiza mbali mbali,..kuweni makini sana, sio wote wanaofanya hivyo, wana maana hiyo, wengine ni mawakala wa shetani, wanamtumia shetani huyo huyo shetani kwa ajili ya kutoa shetani…nia yao hao watu ni masilahi…’akasema.

‘Utajuaje sasa…maana kama ni hivyo wapo wanafanya mambo ya ukweli, wanatoa mapepo, wanasaidia watu nk..nimewahi kuwaona ila mimi siwaamini…’nikasema

‘Muhimu kama wewe unamjua mungu wako, unaijua dini yako, fuata maagizo ya dini yako ukiona mtu anafanya mambo kinyume na dini yako jiulize ni kwanini,…hebu jiulize mungu katuambiaje, shetani ni adui yake, tumlaani na tuachane naye, kwanini huyo mtu awe anatumia mashetani, kwanini..jiulize..kwanini awe na ajenda za kishetani,..kuna tatizo hapo, kuweni makini sana..’akasema

‘Oh, lakini docta ngoja nikuulize kitu, wewe umejuaje haya…kuwa huku kwenye jengo kuna tatizo…?’ nikamuuliza

‘Ndoto yako..imenisaidia sana..’akasema

‘Kwa vipi…?’ nikauliza

‘Huyo sheteni, huyo mbaya wenu, anataka kukugombanisha wewe na mimi,..ndio maana akakuvika viini macho uone kuwa mimi nataka kukuangamiza,..nikajua kuna mtu yupo nyuma yako na keshagundua kuwa nitamgundua..sasa ujanja wake nimeunasa..’akasema

‘Oh,…docta unataka kunifanya nianza kuogopa..’nikasema

‘Mambo bado, utagundua mambo ambayo huwezi kuamini, ila usiamini, endelea na imani yako hiyo ya kutokuamini haya mambo, hiyo ndio inakusaidia,..vinginevyo, ..picha hizo mbili zina maana ya kafara,..kulikuwa na kitu kinatakiwa kufanywe dhidi yako…ulikuwa unaitwa taratibu uingie kwenye mitego yao,…mungu anakulinda, imani yako, ushujaa wako wa kutokuogoa vimekusaidia sana…, na ni mungu tu…wa kumshukuru, na siku zako hazijafika,..’akasema

Mara simu ya docta ikaita…docta akaitizama hakupokea, akakata simu..

‘Mbona hupokei simu..?’ nikamuuliza.

‘Bado wakati muafaka…’akasema, na tukachukua usafiri hadi nyumbani kwa familia ya Mzee majaliwa, tulipofika tulimkuta mzee Majaliwa yupo na mtu mwingine wanaongea, yule mtu alipotuona tu, akasimama, akaoenakana hana raha, akawa ananiangalia sana mimi kama haamini jambo,..

‘Karibuni..’akasema mzee Majaliwa

‘Asante…’tukakaa kwenye viti, na mara yule mtu akawa anaanza kuondoka

‘Mbona unaondoka bila kuaga,..ndugu yangu subiri nikutambulishe..kwa madocteri wangu,..’akasema Mzee majaliwa.

‘Hapana sikai, nahisi ..sijafunga mlango, ..’akasema huyo mtu sasa akiondoka kwa haraka hadi mzee Majaliwa akabakia anamshangaa.

‘Hujafunga mlango wapi…kule makaoni kwako,… , kwani kuna nini cha kuibiwa kule, na kwanini uondoke bila kufunga milango, unahatari wewe..?’ akauliza mzee majaliwa.

‘Hapana, sikutegemea kuwa nitafika huku,..…baadae …, nitakupigia simu, kwaherini, sikai, …’akawa sasa kama anakimbia.

'Huyu mtu vipi...?' akauliza mzee Majaliwa akimuangalia huyo jamaa akiwa kama anakimbia, na kutuangalia sisi kwa macho ya mshangao, kama anataka tumpatie jibu

‘Atarudi tu…’akasema docta, akimuangalia kwa macho ya aina yake, mimi nikabakia kuduwaa tu,siku hiyo ilikuwa ni ya maajabu, na kumbe bado maajabu zaidi yanakuja!
NB: Ni nini hiki, hebu ..hata mimi naanza kuchanganyikiwa.

WAZO LA LEO:Katika hii dunia, kuna watu wanajifanya wajanja, kila kitu akifanya ukimuuliza utasikia,’… unanijua mimi nani, au..nitakuonyesha cha mtema kuni, au…’ wanakuwa na kiburi, cha kujiona wao ni zaidi, ni watalawa, ni matajiri, wana nguvu..utawaambia nini…


Jamani jamani, katika dunia hii hatutakiwi tuwe na kiburi , hatutakiwi tutembee kwa kujigamba, maana hii dunia sii yetu, sisi ni wapiti njia tu,..yupo mwenye kiburi, mwenye mamlaka ya hii dunia, akisema kiwe kinakuwa, akisema wewe siku yako imefika hakuna majadala, huyo ndiye anastahiki kuwa na kiburi,… sisi wanadamu hatuna kitu, si lolote si chochote,..Tumuombe mola tuwe wenye kumtii yeye, na kufuata maagizo yake, na kuyaacha yale yote aliyotukataza ..Aamin
Ni mimi: emu-three

No comments :