Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, April 25, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-14'Usiogope bwana mdogo, ..ujue wewe ulifanya makosa kwenye hiyo familia, unastahiki kuadhibiwa na wao ndio wa kuamua adhabu gani upewe..kwahiyo, ili kuweka mizania nzuri kati yako na hiyo familia, basi  muhimu na sahihi ni wewe kumuoa huyo binti,..

'Kwa vipi wakati wote wanamchukia huyo mbaya wao, na hawajamfahamu kuwa ni nani, je siku hiyo wakinigundua huoni ndio itageuka kuwa chuki, hasira chuki visasi vitageukia kangu..?' nikauliza

'Ndio hivyo hakuna jinsi lakini wema hufuta madhambi au sio, muhimu tumeshaanza kutenda wema, najua mara nyingi madhambi huonekana zaidi...lakini ukumbuke kuwa,..hayo madhambi yalifanyika zamani, siku baada ya siku hasira za hao watu zilishaanza kufifia,...sasa basi, ili tuliweze hili, endelea kuitendea wema hiyo familia...'akasema docta

'Kwa vbipi docta..?' akauliza

'Kwanza ni kubainisha ukweli...kwa vipi,..tutaanzia hapa hapa, kwa namna ya kipekee kabisa, unapotaka kubaisnisha jambo nzito, anza kwa namna ya kupunguza makali, hilo niachie mimi,

‘Haya twende wanatusubiria,

Tuendelee na kisa chetu....

                                          **************

‘Docta karibu,…karibuni madakitari wangu,… au tukipisheni maana naona mumesimama hapo mkishauriana jambo, kwa muda sasa, halafu mnaongea kwa kunong’ona, na msaidizi wako, mnaogopa kusema tuwapishe nini, msijali mimi narudi kwenye wodi yangu au binti yangu unasemaje…maana tumejisahau na kujiona kama tupo nyumbani…’akasema mzee Mashauri akimuangalia bint yake.

‘Usijali baba, mimi nipo na mama, lakini sitaki uondoke, ….eti mama, unataka baba aondoke..?’ akamuuliza mama yake.

‘Ngoja baba yako akapumzike,…anahitajika huko wodini kwake, hairuhusiwi , alipewa muda kidogo tu, lakini wewe umemganda baba yako kama ruba,.. hata hivyo kajitahidi sikutegemea, hii sasa inanipa faraja kuwa mtapona…ila sijui kama utaweza kurudi peke yako,…?’ akauliza mama.

‘Nipo na mkwe wangu hapa..’akasema.

‘Mkwe kwa nani..?’ akauliza binti yake kwa hamaki.

‘Usijali binti yangu, mbona unakuwa mkali hivyo, unafikiri mimi baba yako naweza kukutafitia mtu mbaya,…hilo sahau, ..nitahakikisha umempata unayempenda lakini pia awe na sifa za mume mwema,…na tulishakubaliana kuwa tutaongea wawili ili mama yako asisikie au sio ngoja niondoke maana hapa tatakesha..’akasema baba.

‘Aaah, baba, sasa naona unakwenda mbali, ..kwanza mimi sitaki kuolewa, sitaki yaje kunikuta kama yaliyomkuta dada, sitaki sitaki…..na sitakii niwe mbali na nyie wazazi wangu nyie ni kila kitu kwangu.., mnajua kuwa mimi ndiye mtoto wenu pekee….’akasema binti.

‘Lakini ni lazima uolewe au sio,..huwezi kukhalifu amri ya mungu, kama watu wangeliamua kuishi watakavyo, dunia hii ingekuwaje, ni lazima tufuata taratibu njema za muumba wetu, au sio..na hata ukiolewa, bado tutakuwa karibu..’akasema baba.

‘Baba bwana usitake kuiharibu siku yetu hii muhimu…’akasema binti.

‘Lakini kwani nimekosea nini,..,kwani wewe ulitakaje, kuwa uolewe uzunguzni au marekeni au ughaibuni, hapana utaolewa hapa hapa,…na huenda tukaishi pamoja wewe na mume wako,..hiyo yawezekana au sio… lakini hilo tutaongea baadae, ngoja, nikajipumzishe kidogo, au docta unasemaje..?’ akauliza.

‘Ndio maana nimekuja, ..kwanza nataka kumuhudumia mgonjwa wangu, na wewe unahitajika wodini kwako, docta anakusubiria, na muda sasa umepita,  …kama hutojali lakini, ni muhimu uwahi kurudi wodini kwako….’akasema docta.

‘Haya docta msaidizi njoo unipe mkono maana ooh, huu uzee jamani, mmh, nautamani ujana urudi,…aah..’akasema akitahidi kusimama, alionyesha kuhisi maumivu, lakini akawa anajitahid kuficha ili binti yake asihisi kitu.

‘Unajua mimi bado,… lakini haya yoye ni sababu ya huyo mtu, nilikuwa bado na nguvu zangu,..unajua yule …eeh, aliyewaleta hapa, yeye ni mkubwa kwangu kiumri, lakini mnamuona bado anaokana kijana kuliko mimi,..ni haya matatizo tu..’akasema na muda huo nilikuwa nimeshafika kumsaidia kuinuka.

‘Mzee usijali, mimi nitajitahidi kuwa karibu na wewe mpaka upone nataka uzisahau shida zako zote.., japokuwa na mimi matatizo yamenifanya nifike hapa, lakini nina imani, hali yangu itarudi kama zamani …nipo na mwalimu wangu atanisaidia..’nikasema.

‘Na wewe docta msaidizi una matatizo, wakati wewe unaombea watu wanapoa..?’ akauliza mama akimuangalia kidogo halafu akaendelea na shughuli zake.

‘Mganga hajigangi, kila mtu ana shida zake hata docta bingwa wa magonjwa fulani anaweza kusumbuliwa na magonjwa hayohayo anayoyatibia, ..ni mipangilio ya mungu, sisi kama wanadamu hatuna mamlaka nayo…’akasema docta.

‘Ni kweli…, lakini niulize jambo kabla baba hajaondoka, na huyo msaidizi wake..…’akasema binti akiniangalia mimi usoni.

‘Lakini lisije kumkwaza baba yako, ..huu ni muda wake wa kupumzika, na kinachotakiwa sasa ni yeye kufurahi, ulitaka kuuliza kitu gani..?’ akasema mama yake.

‘Basi mama, naona umejihami…baba usiwe na shaka na mimi, nitajitahidi kesho nifike wodini kwako nikuchukue turudi nyumbani…mimi sitakikukaa hapa hospitalini tena..’akasema huyo binti, bado akiendelea kuniangalia mimi machoni, na mimi nikawa najitahidi kumkwepa kumuangalia machoni.

‘Oh, nitapona haraka, yaani kesho ukitembea na kuja wodini kwangu, sijui nitasemaje…na mimi nitasimama tufanye mazoezi pamoja…na mama yako akiwa nyma yetu , tuone ni nani atashindwa..au atachoka haraka..’akasema baba mtu.

‘Basi baba usijali, tumuombe mungu tu…na wewe docta msaidizi samahani lakini ukimfikisha baba urudi nina maongezi na wewe…samahani lakini…’akasema na mimi moyo ukawa unadunda dunda, nikijua sasa wakati umefika ukweli kubainika.

‘Na wewe ina maana aliyosema baba yako umeshayachukulia uzito, hutaniwi acha hizo, huo ulikuwa ni utani tu, si unamfahamu baba yako alivyo…’akasema mama yake.

‘Mama kuna kitu nahisi …na kila nikiwaza nashindwa, huyo docta msaidizi nahis nilishamuona mahali,…mama kwani huyo aliyekuwa akiongea na mimi nikiwa..sijui ni ndoto au ni kweli, nilikuwa na wewe …ulikuwa na mimi hapa sio, na huyo hapana lakini sio hapa, nilishawahi kumuona kabla, mmh, sijui..nahisi kichwa kama hakikumbuki mambo, atakuwa ndio yeye tu mama…’akasema na muda huo mimi na mzee Mashauri tunatembea kutoka nje.

‘Umemsikia binti yangu, anasema anahisi amewahi kukuona mahali ..nahisi ni kwa vile, ulikuwa unamtibia, na ukiwa umezimia, au kupoteza fahamu unaweza ukayachukua matendo ya watu wanaofika kukuguza kukuongelesha kama njozi, si ndio hivyo…nakumbuka wakati nilipofanyiwa upasuaji..ilikwua hivyo hivyo…’akasema.

‘Ni kweli kabisa mzee, inatokea hivyo,.na kwa vile mimi nilikuwa nafika kumuona kumuuguza, ..basi akili yake inajua kuwa alishaniona mahali…au labda katika mihangaiko aliwahi kuniona mahali, yawezekana siwezi kukataaa…’nikasema.

‘Lakini hata hivyo, unajua hata mimi nahisi sura yako sio ngeni kwangu, hebu niambie kuhusu wazazi wako?’ mzee akawa kama ninizaba kibao shavuni, sikutaka kuongea na huyu mzee chochote kwanza, nilitaka kwanza nielewane na bint yake ili niweze kupata msaada. Kama binti yake atanisamehe, akawa karibu yangu nina uhakika baba hawezi kumuuzi binti yake..lakini sasa nitamdanganyaje huyu mzee.

‘Wazazi wangu walihama muda mrefu kutoka maeneo ya kule kijiji cha..eeh, (nikamtajia) ,..wakaenda kuishi maeneo mengine, na mimi sikuwa naishi na wazazi wangu sana,nilikuwa naishi na baba zangu wengine, kwahiyo sio rahisi watu wa huko kunifahamu, labda nilikuwa nakuja mara moja moja..’nikasema.

‘Ndio maana nakumbuka sura yako, yawezekana sio wewe, ila mnafanana na watu ninaowafahamu, …kuna jamaa mmoja alikuwa akiishi maeneo sio mbali na mahali nilipokuwa nimepanga, ambapo nilianzia maisha, alikuwa mweupe sana , na tena akaoa mke mweupe,….si ndio wazazi wako..?’ mmh mzee huyu ana kumbukumbu.

‘Ndio yawezekana ndio hao…’nikaitikia kwa mashaka, na mara nesi akaja kwa haraka, akasema mzee anahitajika haraka wodini kwake, kwahiyo inabidi amchukua na kigari cha wagonjwa.

‘Oh, nataka kuchukua zoezi la kutembea, ..’akalalamika mzee.

‘Najua , hilo ni muhimu sana, lakini kila kitu kina muda wake, docta wako anataka kuondoka na anataka kuhakikisha keshakufanyia matibabu yanayostahiki…samahani mzee..’akasema sasa akielekezwa kukaa kwenye hicho kigari.

‘Na mimi nirudi au..?’ nikauliza

‘Aaa, wewe rudi tu kaongee na binti yangu, kasema ana maongezi na wewe ila uwe makini, usije kumuhadaa binti yangu, tutakosana, na ukija, kama bado nipo hospitalini au nyumbani ninataka kuongea na wewe kwa kirefu, hatujajuana vyema..’akasema.

‘Mzee, acha waoane…’akasema nesi.

‘Waoane nani na nani,..hata wakioana mimi nina shida, ila kwa utaratibu uliokubalika, sio kihuni huni…, mimi sina shaka, na huyo eeh, ..hata akisema leo anataka kumuoa binti yangu ninampa tu…, lakini kwa utaratibu unaokubalika au sio,..hata hivyo lazima nijue historia yake ya nyuma..’akawa anaongea na huyo nesi huku wanaondoka.

‘Siku hizi mzee, hayo yamepitwa na wakati,..kuwa mpaka wazazi wamkubali wafanye uchunguzi, familia zipoje, mmh, hayo yalikuwa kwenu, siku hizi wakikutana wawili wakapendana, ya huko nyuma ni ya wazee na uzee wao…

'Siku hizi tunakwenda kidigitali, kwenye facebook unapata mchumba hamjui hakujui, ukipenda sura yake na maneno yake matamu, haya, uchumba, …na hata kuoana humo kwa humo, na inaweza ikafikia hata talaka, watu hamjakutana ..kuna mambo huko mzee wangu we acha tu..’akasema nesi.

‘Na mimi nitakuoa wewe…’akasema mzee akitaniana na huyo nesi, na mimi nikatabasamu, huku nikigeuka kurudi kwa huyo binti…nikikumbuka kauli yake;

‘….Na wewe docta msaidizi samahani lakini ukimfikisha baba urudi nina maongezi na wewe..’ hiyo ilikuwa sauti ya huyo binti, ikirudia rudia kichwani mwangu.

*************

Nilirudi wodini kwa binti, nikakuta docta, mwalimu wangu akiendelea kumfanyia masaji huyo mgonjwa wakishirikiana na mama, na baadae walipomaliza, akatoa dawa na kumuambia mgonjwa azinywe, haikupita muda huyo binti akalala…

‘Keshalala, sasa mama unaweza ukaenda nyumbani, ukirudi atakuwa kasha-amuka, mnaweza kuendelea na mazoezi, cha muhimu sasa ni mazoezi tu..na kumpa faraja, maneno yenye kumjenga, na kwa vile bado nipo nipo nitakuwa nakuja tu…’akasema docta.

‘Nitajitahidi sana kwa hilo,…lakini muda mwingi wanakuwa na baba yake, tatizo la baba yake ni mtu wa hasira, unakuta wanaongea ghafla wamekosana, baba kakasirik,ainabid mimi niingilie kati…ndio hivyo, lakin kiukweli hatuna jambo baya kwa huyo binti wetu..’akasema mama.

‘Pamoja na hayo mama, baba anahitajia kubembelezwa, kurekebishwa, ili aondokane na tabia yake ya hasira, unajua mume kwa mke ni kama mtoto, unatakiwa umlee, umbembeleze na hivyo hivyo mke kwa mume, ndio raha ya ndoa, au sio, ..najua mumeo ana mafundo moyoni mwake, jaribu sana kumfanya hayo mafundo, ya visasi hasira yaondoke..bila hayo kuondoka ..hataweza kupona …’akasema docta.

‘Mhh, kwa mzee, hapo sijui nifanyeje, nitajitahidi..si unajua tena… lakini siwezi kukuahidi kwa hilo, maana nimeishi naye miaka mingi, namfahamu sana, ubishi, hasira, visasi,..ooh, hapo usimwambie kitu, lakini umri unavyokwenda na yeye anabadilika…’akasema

‘Na kiukweli mume wangu ,kabadilika sana mume wangu sio yule niliyekuwa namfahamu, enzi hizo, akirudi unakunyata, unajiangalia mara mbili tatu usije kufanya kosa, lakini sasa mmh, mume wangu kawa mwingine kabisa…ana mapenzo, ananyenyekea, yaani, unatamani hayo yangelikuwa enzi hizo.. ..kilichomkorofisha ni baada ya huyo binti yake kufarikia…’akatulia.

‘Poleni sana, lakini hayo ni mapenzi ya mungu, je unafikiri nyie kama wanadamu mungeliweza kulizuia hilo…?’ akauliza docta.

‘Najua ni mapenzi ya mungu, lakini..hata wewe fikiria, mtu aliyefanya hivyo, halafu hata kujitokeza, angalau angelifika basi, akaomba msamaha,..hakuwahi hata kujitokeza, hatumjui hadi hii leo, hebu fikiria, ni lazima utafikiria vibaya,..si mlaumu mume wangu kwa hilo maana hata mimi ..aah, hata sijui…’akasema.

‘Mama sisi tunakutarajia wewe, maana mama, au mke kwenye familia ni nguzo muhimu sana..ndani ya familia, yeye ndiye anajenga daraja kutoka kwa baba na watoto, kutoka kwenye familia na jamii ya nje,unaona umhimu wake ulivyo ..mke mwema ndiye anaifanya familia ijengeke vyema, mume awe na furaha, akirudi nyumbani ajihisi yupo peponi, sio jahanamu, ..najua mume ni kichwa cha familia, lakini mume sio mlezi, mlezi ni mama, unanielewa hapo..’akasema.

‘Nakuelewa sana…’akasema mama.

‘Kwahiyo kubadilika kwa baba, kutoka kwenye hasira, kutaka kulipiza visasi,..na mafundo moyoni kunategemea sana juhudi zako..na ndio tiba yake muhimu, vinginevyo hiyo stroke ikirejea tena,sijui itakuwaje,…nakuomba sana, jitahidi. Kila iwezekenavyo mumeo ajirudi, aachane na tabia na hulka za asili, najua hilo ni gumu, lakini jitahidi sana sana mama…’akasema docta.

‘Lakini sasa, …unajua mimi nionavyo, bila ya huyo mtu kupatikana, sijui kama mzee ataweza kutulia,..huyo ndiye anampa shida sana mzee, mzee anasema kuwa akifa kabla hajakutana na huyo mtu itakuwa ni deni kubwa sana mbele ya mungu,..unajua siku ile ya mazishi,  aliapa kwenye kaburi la binti yake, kuwa ni lazima huyo aliyefanya hadi binti yake akajiua,ampate na kulipiza kisasi…sasa hapo unafikiri nitafanya nini mimi…’akasema.

‘Unaweza, na utaweza…kumbuka jambo moja, anachotaka kufanya mume wako ni kulipiza kisasi, je anafahamu makosa ya huyo mtu, je anajua ni kwanini mpaka ilifikia hapo,… lakini hata hivyo hebu jiulizeni na nyie, je hamjawahi kuwakosea watu wengine, mkasamehewa..au nyie ni watakatifu sana, hamkosei..makosa ni mengi tuantendeana aus io…muhimu na lililo bora ni kusameheana..’akasema docta.

‘Unajua mtu akipatwa na jambo, ndio anajua uchungu na maumivu ya hilo jambo, na ni nadra sana mtu kukumbuka machungu hayo kwa wengine kila mtu anaangalia nafsi yake,..sisi yametukuta hayo, tunajua uchungu na shida gani tumepitia, tulifikia kujiona ni wafu tu hatuna maana..mpaka jamii inatukimbia,…' akasema.

'Yaani we acha tu,  yaliyokuwa yakitokea ndani ya nyumba…we acha tu,…sasa kwa hali kama hiyo, huwezi kusema je kwa wengine, walio na matatizo kama hayo,..inakuwa vigumu kibinadamu, lakini..mimi nitajitahidi sana…kusahau, kumuomba mungu, …lakini moyoni nimeumua sana,na huyo mtu akijitokeza akaelezea ukweli, huenda,..sijui..maana nafsi ndio itajua hayo…’akasema mama.

‘Mama, nikisema nitakuja na huyo mtu utasemaje..’akasema docta na mama akashtuka na kumuangalia docta, halafu akasema;

‘Utakuja naye,ina maana unamfahamu huyo mtu..?’ akauliza mama kwa mshangao.

‘Nitawasaidia kumtafuta huyo mtu kwa juhudi zangu zote.., ila akipatiakana nataka dhamana yako, nataka wewe unihakikishie usalama wake…maana sio kwamba hakutaka kuja, ila anaogopa..anawafahamu hasira mlizo nazo, na amejaribu mara nyingi kuja kwenu lakini kila akija anakuta mpo kwenye hali ambayo mtu hawezi kuongea na nyie..’akasema docta.

‘Oh, sijui, kama utamleta huyo mtu, ..kiukweli sijui nitakupa zawadi gani, najua unatudai gharama nyingi sana,..hizo gharama zako tutazilipa tu wala usiwe na shaka,,…hilo na wala usiogope kuweka gharama zako zote, nimeshaongea na watu wangu, pesa yako ipo…’akasema mama.

‘Usijali mama hilo la gharama lisiwape shida, tutaona itakavyokuwa…’akasema docta.

‘Najua  na wewe unahitajia kula, una familia, umeacha shughuli zako huko, ..na ni nani atashindwa kulipa fadhila kama hizi, …siwezi na mtu kama huyo yupo, basi hastahiki kufanyiwa wema,…wema wako ni mkubwa sana, ..ni lazima tulipe, japokuwa nina uhakika hata tulipe shilingi ngapi hatuwezi kufidia huo wema wenu…’akasema huyo mama.

‘ Sasa mama, mkiwa tayari mimi nitamleta huyo mtu...lakini mkiwa tayari, ninaomba sana, hii ichukulieni kama sehemu muhimu sana, katika maisha yenu, muombeni mungu sana, safisheni mioyo yenu,...kwangu mimi niliposikia tatizo lenu kwa haraka nikaanza uchunguzi, nikagundua kuwa huyo ni sehemu muhimu sana katika matatizo yenu,..kwahiyo ikanibid nianze kufany auchunguzu wa haraka, nishaanza kuwasiliana naye, kwa mawasiliano tu....lakini sasa....'akatulia.

‘Ongea tu baba…’akasema mama akimuangalia docta halafu binti yake pale kitandani.

‘Ni hivi mama, nyie kwa hivi sasa, mnahitajia muda wa kujiweka sawa, mlitafakari hilo jambo maana nyie ni wazazi, na huyo pia mtoto wa wazazi wenzenu, wanakosa na wakikosa wanaadhibiwa au wanasamehewa, mimi nitachukua dhamana kwa huyo kijana au mwanaume, maana atakuwa mkubwa au sio...'akasema docta

'Sawa tutakutana na hao wazazi wake ikibidi ili tuone ..lakini mmh, hata sijui...'akasema mama

'Mimi nawaomba tena sana,…tumieni hekima zeni katika kuhukumu makosa ya wengine waliowatendea ubaya, najua dhuluma ni mbaya na matokea yake ni kama haya, lakini tusihukumu na sisi tukaja kuhukumiwa kwa kutokuwa waadilifu,.., utaona kwa vile sio mtoto wenu basi mje kumkomoa, itakuwa sio busara…unanielewa hapo..’akasema docta.

‘Nimekuelewa sana, ila yaonekana kama kweli unamfahamu sana huyo mtu, kwanini unamtetea kihivyo,...hujaangalia kwa upande wetu, je ni haki alichokifanya,...uangalie pande zote, au sio...nikuulize tena, kweli unamfahamu huyo mtu..?’ akauliza mama, akimuangalia docta.

‘Mama usijali hiyo kazi nitaifanya maana ni sehemu ya matibabu ya wagonjwa, ninajua bila kupatikana kwa huyo mtu mzee hawezi kutuliza akili yake, nafsi yake imeshasadikisha kuwa hiyo ni dhima kwake, sasa ili matatibabu yangu yakamilike, basi,..hilo kwangu ni muhimu sana…’akasema.

‘Na huyu msaidizi wako naye anamfahamu huyo mtu.?’ akauliza akiniangalia usoni.

‘Hapana, yeye ndio ikibidi, nitampa kazi ya kumfuata huyo mtu akaja naye, unajua mimi nafanyia kazi mikoani, sasa sijui lini mtakuwa tayari , kama bado ..maana yote inategemea hawa wagonjwa, ..ni sehemu ya matibabu lakini je wapo tayari kuhimili, ..sasa mwenznagu hapa ndiye nitamtumia zaidi, atapatikana tu usijali mama.’akasema docta.

Mama sasa akawa ananiangalia kwa makini mimi, baadae akasema;

‘Lakini hii sura sio ngeni kwangu..’akasema mama akiendelea kuniangalia kwa makini

‘Wengi wanasema hivyo, sijui kwanini, hata baba alisema hivyo hivyo, sura yangu yaonekana ni...tofauti au…’nikasema nikijihami.

‘Usijali, kinachonifurahisha na kunipendeza kwako, unaonekana wewe ni mtu mwenye tabia nzuri,..na ukichanganya na kipaji chako, hakuna mzazi ambaye hatafurahi kuwa na mtoto kama wewe…’akasema mama.

‘Na wengi wangelipenda awe mkwe wao..’akaongezea docta huku akicheka.

‘Hahaha, docta hayo ya ukwe, ni wao wenyewe wakikubaliana wakapendana, sisi wazazi ni kutoa ushauri tu kuwa anafaa au hafai..ndio mambo ya siku hizi, kama mzazi inabidi ukubali wakati au sio…’akasema.

‘Ni kweli, ndio mtihani wa wakati huo mama kila mabadiliko huja na changamoto zake…’akasema docta.

‘Lakini sasa docta mbona hamjaniambia vizuri, huyu msaidizi wako ni nani, ..nahisi namfahamu, nahisi nimeshawahi kumuona mahali, nahisi nahisi, mmh, ni nani wewe, tumeonana wapi…?’akasema mama akijaribu kukumbuka.

NB: Mama huyoooh


WAZO LA LEO:Tunapotaka kuhuku jambo, kwa wengine tujiulize kwanza kuhusu sisi wenyewe, je hatujakosea hivyo, au kama hivyo…wengi wetu tunakosea sana, lakini mara nyingi tunaona makosa ya wengine zaidi ya makosa yetu..kwa kufanya hivyo, tunajenga uadui badala ya kusaidia kuondoa matatizo. Tumuombe mungu atujaze hekima ya kuhukumu sawa, kwa haki na uadilifu.
Ni mimi: emu-three

No comments :