Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, April 24, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-13


'Nimesikia sifa zako kutoka kwa mwalimu wako, huyo docta,  kuwa wewe una kipaji cha kuombea watu, wakapona kwa uwezo wa mola wetu,..sijui unafanyaje, mungu mwenyewe ndiye anajua,  …'akasema mzee Mashauri na moyoni nikawa najiuliza kwanini docta akanipakazia  sifa kama hizo, wakati mimi sijui kama ninazo.

'Na pia nimesikia kuwa wewe ndiye uliyemuombea binti yangu, unataka kusema kuwa keshapona kabisa, niambie kijana, maana sijaamini mpaka nimuone kwa macho yangu..'akasema

'Ndio ukweli mzee, kazindukana na sasa nimekuacha anaongea na mama yake na docta mwalimu wangu...'nikasema

'Oh, mimi kwanza nimshukuru mola wetu, kwa kuwezesha nyie kuwepo, kuja kwenu imekuwa ni faraja kubwa, na ni neema zake mola , maana haya yote ni kwa uwezo wake mungu,nyie ni kama njia tu au sio…’akasema mzee

‘Ni kweli mzee..’nikasema

‘Sasa ninaomba nikuulize kitu,..., wewe umeshaoa, una watoto wangapi?’ akaniuliza swali lililonifanya nihisi kama mtu kanizaba kofi usoni, japokuwa hapo alishanifungulia njia ya kuelezea matarajio yangu...lakini nikashikwa na kigugumizi, na kichwa, nikakumbuka jinsi binti huyo alivyoniambia;

‘…Sawa nimekuelewa, lakini nenda kwa baba kwanza umwambie kuwa nimeshapona na ikibidi kama ni kweli basi uanze kumuambia,..mimi nakumbuka uliniambaia upo tayari au,…’

Haya ninekutana na baba yake, na tulikuwa na nafasi ya kuliongelea hilo wakati namtembeza naye kutoka wodini alipokuwa kalazwa huyo mzee hadi wodini alipolazwa huyo binti yake, ..lakini sikuweza kumwambia lolote,…na sasa tumeshafika wodini alipolazwa binti yake, binti anasubiria kauli ya baba yake kuwa, sasa itakuwaje,…

Tuendelee na kisa chetu…

************


Kiukweli furaha kwangu ilikuwa imeanza kugeuka kuwa sintofahamu nyingine maana docta kanitwika mzigo mkubwa kuliko uwezo wangu, mimi na kipaji hicho cha kuombea ni wapi wapi,mwenyewe nina matatizo kibao , nimeshindwa kujiombea. hili sasa ni tatizo, nitakuja kuonekana tapeli huko mbele.

Tukawa tumeshaingia ndani ya wodi, mzee macho yake kwa binti yake aliyekuwa kakaa kitandani, ..na mimi nikawa nimesimama pale mlangoni japokuwa mzee huyo aliniambia niwe naye sambamba ili akizidiwa asije akadonoka, mimi nikajipa moyo kuwa huyo mzee sasa hawezi kudondoka keshapona, nikabakia pale mlangoni nimesimama, lakini akili ilikuwa mbali kimawazo.

Baba huyo akawa anatembea mdogo mdogo, mwendo wa kujitahidi, alijitahidi kweli, hadi akafika pale kitandani alipokaa binti yake..., na binti akawa anajikakamua angalau inuke kidogogo, angalau asimame ili aweze kumkumbatia baba yake, lakini alionekana kushindwa, na baba akamfuata pale pale kitandani akapitisha mkono wake mmoja mgongoni kwa binti..

Binti akajiegemeza kifuani kwa baba yake huku analia, analia kilio cha furaha,snslis kumuona baba yake rafiki yake mpenzi, na hapo nikasikia akisema;

‘Siwezi kuielezea furaha ya leo binti yangu mpenzi,,…anayejua tu ni mungu, siwezi kusema kitu cha kukuonyesha binti yangu kuwa nakupenda sana, na kupona kwako ni sehemu ya kunipa mimi nguvu ya kupona, ..ninajua nimechoka, na uzee huu tena, na mitihani hii ya maisha lakini mungu atanijali niweze kukupigani, kukusaidia uweze kupona kabisa..’akasema

‘Baba usiwe na shaka tena, mimi nimeshapona, sasa hivi macho yangu yanaona sio kama mwanzoni nilikuwa naanza kuona kitu kama ukungu ukungu, na baadae ikawa sioni, niliogopa sana siku ile ndio maana nililia kwa uchungu, kumbe kwa kufanya vile nilikuababishia na wewe ukadondoka, na kupoteza fahamu kaniambia mama...akasema binti..

'Oh, niliogopa sana binti yangu, nilijua tena sina binti, maana huku huwezi kutembea huko tena macho hayaoni,..nikaona hayo yote kama yapo mwilini mwangu, na ghafla nikakuone umpoteza fahamu, ...sikujijua tena, ..nimezindukana nipo hospialini…’akasema baba mtu

'Pole sana baba, sasa hivi nitajitahisi sana nipone, nitaanza kusahau machungu ya dada, japokuwa sio rahisi, nilikuwa nampenda sana dada yangu kuondoka kwake, ilikuwa kama nkanivunja mwili wote...sijui kama nitaweza kumsahau...'akasema kwa huzuni.

‘Pole sana binti yangu, najua mengi yametokea huenda ni kwasababu ya madhambi yangu, sijui..mungu mwenyewe ndiye anayajua mabaya gani nilifanya,..na haya ni namna ya kutuadhibu, lakini kubwa ya hayo, ni huyo aliyemtendea ubaya huyo dada yako, sitaki kukumbusha hilo,ila nakuahidi kuwa , mimi baba yako ilimradi bado napumua, nitajitahid nimtafute huyo mtu, kokote lipo, ili aipate hiyo adabu yake, na hasira zangu zote zitaishia kwake....’akasema.

‘Baba usiwe na shaka na hilo, huyo mtu atajileta mwenyewe…maana nijuavyo mimi mungu humlipiza kila anayedhulumu wengine kwa namna aionayo yeye mola kuwa ni sahihi kwake,.unajua baba , japokuwa mimi bado mdogo lakini nimejifunza kitu, adhabu ya mungu, haina kipimo kama sisi tunavyotaka,…'akasema binti.

'Mimi ninajua jinsigani ya kumuadhibu, wewe utaona, jicho kwa jicho....sifanyi kosa hilo mwanangu, na yeye aende huko alipolala binti yangu ..haniambi mtu hapo..unasikia binti yangu, ninajua bado nitakuwa sijalipiza ...kisasi...'akasema baba akionyesha hasira zake.

'Lakini baba kisasi sio kizuri, au...maana ukifanya hivyo mungu wetu atazidi kutufany atusipone..'akasema binti.

'Ngoja apatikane kwanza, hayo mengine niachie mimi, ...sasa huwezi hata kuinuka...'akasema

'Baba unajua, huyo mtu hayupo mbali na wewe...ila muhimu haitakiwi kujichukulia sheria mikononi mwetu, huyo ana adhabu yake tayari, mimi nalijua hilo, …’akasema huku akionyesha kutaka kuniangalia.

Pale nilipo nilihisi mwili ukiniisha nguvu, ina maana huyu bint kaamua kunichomelea kwa baba yake, hajataka hata kunipa muda wa kujitetea,..hapo ndio nikageuka nyuma tayari kwa kukimbia..

Usijali binti yangu nitampata, hilo nakuahidi, awe karibu au mbali, unajua mwanzoni niliwaachia polisi wafanye kazi yao, lakini nimegundua kuwa polisi hawana maana, wanalichukulia tatizo hili ki..namna yao, sasa mimi nitalichukulia kinamna yangu, nitatumia kila njia,....'akasema

'Baba, kwanini wataka kujipa mizigo mingine mikubwa, unajua baba mimi nimeshamgundua huyo mbaya wetu, ila ...nipe muda kwanza..'akasema huyo binti.

'Usijali binti yangu, mimi nitampata tu..hilo amini.....cha muhimu sasa ni wewe kuweza kusimama, na ukianza kutembea mimi nitakupatia zawadi kubwa sana,ukiweza kufanikiwa ukatembea tena kama zamani…’akasema baba mtu sasa akibadili maneno.

‘Zawadi gani baba…mimi nikiwaona nyie wawili mna furaha kwangu ni zawadi kubwa sana..?’ akauliza na kusema

‘Zawadi hiyo ni mume, mimi nimeshakutafutia mume sahihi anayefaa kukuoa wewe..’akasema baba yake.

‘Mume ...baba ndio zawadi hiyo,....baba naye bwana, umemtafuta wapi huyo mume wakati wewe ulikuwa unaumwa..?’ akauliza

‘Mungu ana miujiza yake,…keshanionyesha kwenye njozi zangu, kuwa ni nani stahiki yako mume anayeweza kukuoa wewe sio hao wahuni wengine, wahuni walimdanganya dada yako na baadae wakamuacha kwenye mataa, …hilo niachie mimi, je upo tayari.. mimi nikutafutie hiyo ya zawadi ya kumpata mume mwema stahiki yako..?’ akaulizwa baba.

‘Baba bwana, hilo liache kwanza, siku hizi mume unajitafutia mwenyewe, sio kama nyie enzi zenu,..ni lazima nimpate ninayependa, wewe baba, subiria kwa hilo, nikiweza kusimama,na kuanza kutembea nitakuambia,..tutaongea ..unataka mama naye asikie mambo yetu …’akasema na mama yako akiwa na furaha akasema.

‘Nyie wawili nyie, isingelikuwa ni mtu na binti yake, ningeliwashuku vibaya, mnapendana utafikiri mtu na mpenzi wake…’akasema mama.

‘Wivu huo sasa…’akasema baba, na wakawa wanacheka kwa furaha,

************

Walishanisahau kuwa mimi nipo….furaha iliwafanya waisahau dunia nyingine, na kweli furaha ina nguvu sana,..mateso na machungu ya matatizo ya dunia yanaweza kusahaulika, kwa furaha moja tu,..hasa  pale nafsi inapokipata kile ikitakacho..

Kwa vyovyote iwavyo, familia hii itautambua ukweli hivi karibuni, inavyoonyesha huyo binti atautumbua huo ukweli,…kwa vile huyo binti keshanifahamu, kuwa mimi ndiye huyo mbaya wao…na sijui kama kweli anayo hiyo hisia ya kutaka mimi nimuoe,…sijaiona hiyo hisia bado..

Hapo mimi nikawa nikajiuliza ni nguvu gani iliyomfanya huyo binti hadi aweze kuzindukana, je ni hiyo kauli yangu kuwa mimi ninataka kumuoa,…hilo sizani, labda ni kwa vile nimetamka kuwa mimi ndiye niliyemfanyia dada yake hivyo, …kwahiyo alijitahidi azindukane anione mimi uso kwa uso

Ndio maana na yeye kajiunga kwenye nguvu moja ya kutaka mimi nipatikane na nguvu ya sheria ichukue mkondo wake, lakini mzee haitaki hiyo nguvu ya sheria, yeye anataka kuchukua sheria mikononi mwake, sijui kadhamiria kunifanya nini mimi, 

Nilipoliwazia hilo, hapo hapo nikageza kichwa changu kutizama nyuma, nikitaka kuhakiki kama hakuna mtu mwingine anayeweza kunizuia, nikitaka kukimbia. Hakuna …nikawa na uhakika,..kuwa sasa naweza kutoka nje, kama sio taratibu, basi nitimue mbio..

Nikageuka kuangalia kule kitandani, nikawaona,  mzee sasa akiwa amekaa vizuri pale kitandani pembeni mwa bint yake, akiwa bado kamzungushia bint yake mkono kupitia mgongoni, mama akiwa kakaa kwenye kiti karibu yao,wakizidi kuongea kwa furaha..huku mama akimkanda kanda binti yao miguuni..binti pekee aliyebakia!

Nilijua baadae wote watageuka kuniangalia mimi..,na wakifanya hivyo hapo ndio nitajua ni mwisho wangu, uso uliojaaa furaha utageuka kuwa chuki dhidi yangu,..na watageuka pindi huyo binti akianza kuufichua ukweli, na ninahisi haitachukua muda…ilimradi wameshaanza kuliongelea swala la kumtafuta huyo muhusika, huyo aliyewawezesha kupata hiyo shida yote, …

Niliiona hiyo dalili ya huyo binti kunitaja lakini kila alipotaka kulisema hilo neno, baba matu alikuwa akiingilia kwa hija nyingine,..hapo nikajua labda siku zangu hazijafika muda ukifika baba ataambiwa na hapo sizni kama atakumbuka hayo tuliyafanya kwa binti yake..

‘Sasa unasubiria nini..kimbia…’nikahisi kitu kikiniambia akilini, sasa hivi sio zile hisia za mtu kuniambia, bali ni nafsi yangu mwenyewe ndio inanishauri hivyo.

‘Kimbia kabla mambo hayajaharibika kwanza pale walipo wameshakusahau, unaweza kutoka taratibu wasikuone...’nikahisi nafsi ikinishauri hivyo.

 Baadae hapo ndio nikamkumbuka docta, docta kaenda wapi, mbona simuoni humo ndani, niliangalia chumba kizima, labda alikuwa kakaa pembeni, hakuwepo kabisa humo ndani, hata kule kwenye chumba cha mapumziko cha wahudumu kulikuwa hakuna mtu.

Huyu mtu atakuwa kaenda wapi, hapo nikazidi kuingiwa na wasiwasi,…huenda kaamua kuondoka na kuniachia msala,..kama nilivyosema mimi huwa sina tabia ya uwoga, lakini kuhusu jambo hili, nilianza kuingiwa na wasiwasi, uwoga ukaanza kunitanda kwenye nafsi yangu, sio uwoga wa kuja kupigwa au kuuliwa na huyo mzee…

Uwoga ulioanza kunitawala sasa hivi ilikuwa uwoga mwingine tofauti, ni uwoga wa kuwa huyo bint, pindi mzazi wake akimkatalia kuwa huyo unayemtaka awe mume wako ni adui yangu, na mimi nilishaapa kuwa nitamfanya kitu mbaya..inaweza ikaleta balaa jingine.

‘Lakini haya yakija kutokea mimi sitaki niwepo tena, ni bora nikimbize shingo yangu kwanza, mengine nitakuja kujua huko baadae..’nikasema, nikawatupia macho nikawaona bado wanaongea huku wakijaribu kumuinua inua huyo mgonjwa kitandani.


' Sasa hapa ndio nafasi ya kuondoka....'nikajisemea huku nageuka nikianza kuinua mguu, kama mtu ananyata.

'Unataka kwenda wapi..’ sauti ilinisthua nakunifanya ninywee..

*************

Kumbe alikuwa ni docta, alikuwa katoka kidogo, na sasa kesharudi ndio akanifuma nikinyata kutaka kutoa nje ili nikimbie mbali kabisa na hiyo familia, mkononi alikuwa na dawa, mbali mbali..

‘Oh, nilikuwa nakutafuta, nikajua umenikimbia,..’nikasema

‘Nikukimbie wewe kwanini,...hapana, siwezi kufanya hivyo …ila nahisi wewe ndio unataka kukimbi,unajua wewe ulitakiwa uwe karibu na hiyo familia, ili waanza kukuzoea..’akasema

' Kwani docta sisi tunasubiria nini,mimi naona tumeshaimaliza kazi yetu au sio,..’nikasema

'Nani kasema tumemaliza kazi, wewe unahisi kazi imekwisha, bado, hiyo ni sehem tu ya matibabu, bado kuna hatua muhimu sana, najua hatua hiyo inaweza kuwa ngumu lakini nia ni kuhakikisha tunaliondoa hili tatizo kutoka kwenye chimbuko…’akasema docta

'Hatua gani tena hiyo docta, mimi nijuavyo, kwa mgonjwa ikishagundilikana tatizo iliyobakia ni kupewa dawa, na kwa yule binti muhimu ni mazoezi au sio…’nikasema

'Dawa ni kitu kidogo tu, ..lakini kinga, kuharibu kabisa kiini cha tatizo, ..ni muhimu sana, unaweza ukapewa dawa ukapona leo, kesho ukaumwa, maana hukujali kinga, hukuondoa kiini cha taizo hilo..unanielewa hapo…’akasema

'Kwahiyo unataka sisi tufanye nini docta..., basi najua mengine ni ushauri nasaha, na mimi sina ujuzi wa mambo hayo, nahisi hatua hiyo mimi sihitajiki sana, basi ngoja mimi niondoka docta..’nikasma

'Wewe naona umshaanza kuogopa…’akasema

'Sio swala la kuogopa docta mimi unanifahamu sana, sina hulka ya kuogopa, , ila naogopa kuja kuwaharibia hawa watu furaha yao, je wakigundua kuwa mimi ndiye chanzo cha matatizo yao nitasemaje mimi…’nikasema sasa nikiwatupia macho, bado walikuwa wakijaribu kumuinua yule binti kwa mazoezi.

'Ndio maana ninasema sehem ya matibabu iliyobakia inaweza ikawa ngumu kidogo,..na hiyo ni muhimu sana, kwani bila hiyo, bado tutaicha familia hiyo kwenye sintofahamu…’akasema

'Docta, mimi kwa maoni yangu, tumejitolea vya kutosha,..najua wewe kuna malipo yako unahitajia, lakini mimi ninajitolea tu, kwa hilo kwangu inatosha,..,mimi kwa ushauri wangu docta, kwanza kiukweli sizani kama wanaweza kukulipia gharama zote hizo, na unavyozidi kuwatibia unazidi kutumia gharama kubwa zaidi,…waambia kiasi gani hivi sasa unadai ili wao wakulipe, halafu utafute njia ya kulipotozea hilo, na uwape moyo, basi tutafute mwanya isis tuondoke zetu,,'nikasema

'Sio rahisi kihivyo, mimi nikiikubali kazi, na nikiianza kazi yangu, sijali gharama kwanza, hilo napenda ulielewe, na swala la gharama asilimia kubwa utalipa wewe…’akasema

‘Docta mimi kazi sina,…nitakulipaje gharama kubwa hivyo..., ninaweza kukulipia gharama zangu lakini sio kwa hao watu,…sina uwezo huo…’nikasema

‘Usijali, gharama zangu zitapatikana tu, hilo lisikuumize kichwa,..na mimi siwezi kufanya kazi nusu nusu.., maana hiyo tunayotaka kuikimbia ndio sehemu muhim ya matibabu yenyewe, sio kwa wao tu, bali pia ni pamoja na wewe

'Na mimi docta kwa vipi, maama mimi sina tatizo kubwa, muhimu ni wao, na nionavyo mimi , hata wao sasa hawana tatizo kubwa, au..?

'Tatizo bado bwana mdogo,  kama nilivyowahi kukuambia awali, mimi sitibii kama kukata matawi kwenye mti, ukisema nimeuua mti, mimi natibia kutoka shinani na kwenye mizizi, tatizo hilo lina chanzo chake , tusipotibia chanzo chake, hali hii itarejea tena, chuki visasi vitaendelea kuwatafuna wanafamilia hao...sasa hilo mimi kama docta siwezi kuliachia kihivyo..’

'Kwahiyo,…?’ nikauliza

'Kwahiyo sasa ni muda wa kuufichua huo ukweli…’akasema

'Docta unataka tufanye nini, unataka  mimi nikafungwe, unakufahamu jela lakini... hujasikia walivyokuwa wakiongea…wananitafuta mimi ili nikafungwe, kama mzee atanibakisha hai…’nikasema

'Usiogope bwana mdogo, ..ujue wewe ulifanya makosa kwahiyo wakitaka wewe ufungwe ni sahihi, lakini sizani kama itafikia huko,..na hili tatizo kwa hivi sasa haitakiwi kupoteza muda, maana furaha ni seheme ya kufuta machungu, na ukitumbukiza chungu kwenye furaha, inaweza ikalizamisha kabisa hilo chungu, hata lisionekane ni chungu tena.

'Docta mimi siwezi kukuelewa, mimi naondoka, ni lazima niondoke, kwanza nina mambo mengi ya kufanya…’nikasema.

‘Huendi popote..wewe mwenyewe umesema family hiyo ina majeraha, sasa ni nani  atayaponyeha hayo majeraha, kama sio wewe..’akasema docta.

'Kwa vipi..?’ nikauliza.

'Kama nilivyokuelezea awali ni wewe kuoa ndani ya hiyo familia, wewe umuoe huyo binti mgonjwa, wewe mwenyewe  umemuona binti alivyo, pamoja na kuumwa, lakini huo urembo wake ulikutia wewe kiwewe..’akasema docta.

'Docta naona wewe ulihisi vibaya,ila nilipoona huyo mdada amejifunua uso , na kubakia uso wazi, nikamtizama, sikuona sura yake kamili, nilichoona ni kingine kabisa..’nikasema

'Uliona nini..?’ akaniuliza huku akionyesha uso wa tabasamu la kejeli.

'Docta huwezi kuliamini hili, sasa sijui kama ni macho yangu tu yalinizuzua,.., sijui kama ni hiyo taswira bado inanitawala kichwani, sijui..kiukweli docta mpaka sasa sijawa na uhakika huo, haiwezekani…oh..’nikasema

'Sikiliza,… sasa ni muda wa kuangalia ukweli, huu sio muda wa taswira, hayo mauza uza ya kichwani, yanatakiwa yaondoke, na kuondoka kwake, ni wewe kuukubali ukweli, hakuna maswala ya giza hapa, sasa ni kuukubali ukweli na kukabiliana nao, ondoa hofu, wekeza kwenye hali halisi,..unajua ni kwann nilikuambia twende makaburini..?’ akaniuliza.

'Sijui..’nikasema

‘Nilitaka ukakutane na hilo shetani,…’akasema

‘Eti nini..?’ nikauliza

‘Nilitaka ukaione hali halisi, uonane na huyo shetani, na makao yake…’akasema

‘Oh, docta, unaamini hayo..?’ akauliza

‘Kama wewe huamini hayo... kwanini unaogopa kuukabili ukweli,..unajua ukweli upo wapi, wewe unataka kuukwepa, huoni kuwa kwa kufanya hivyo, wewe utakuwa unachezewa na shetani,…sasa inabidi ukubali kuukabili ukweli, tupambane na hali halisi, na hili tunalianzia hapa hapa, ..twende tukaungane na hiyo familia…’akasema

Na muda ule niliwaona wanafamilia wale wakigeuza kichwa kututizama sisi, nikajua ehee, yule binti atakuwa keshamuelezea huyo mzee ukweli, hapo sasa nikagueza kichwa kuangalia nje, docta akasema

‘Haya twende wanatusubiria,...huu ndio wakati muafaka...'akasema docta akianza kutembea kuelekea kwa kwa ile familia pale kitandani.

NB: Leo nimekuwa na wakati mgumu, sehemu hii nimeiandika kwa kujiiba, yaweza ikawa na marekebisho, mengi lakini nahis ipo pouwa,

WAZO LA LEO: TUsijifanye wajanja kwa kuukwepa ukweli, au kuliahirisha tatizo, kwa visngizio mbali mbali, huku tukisema tutafanya kesho, au hili tuliache …au kunywa ulevi ili kusahau matatizo, hiyo haisaidii kitu,  maana hatujui ya kesho anayeyajua ya kesho yetu ni mola peke yake.
Ni mimi: emu-three

No comments :