Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, April 22, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-12


 Nikawa namuomba mungu, na maombi yangu kwa wakati huo yalitoka moyoni, kauli ya mama ilinigusa sana, nilimuonea huruma mzazi huyo, nilimuona kama mama yangu kwahiyo wakati natamka haya, ilinitoka kutoka maoyoni japokuwa …kinamna nyingine sikuwa tayari kwa hilo, kwa vile nilishampenda mpenzi wangu wa facebook.

‘Nakushika kiganja chako cha mkono,kama ishara ya mshikamano ,kuwa mimi na wewe kuanzia sas tu wapenzi wa kweli..’nikasema na huku moyoni kidogo natamani kusita, lakini kuna nguvu ilinivuta nizidi kusema mengi zaidi.

‘Na kwa uwezo wa muumba wetu, ewe mola wetu, ninakuomba kwa rehema zako, umponye mja wako huyu, aondokane na hicho kifungo cha umauti, na mateso ya maradhi anayopambana nayo, .. nakuomba mola wetu umjalie mja wako huyu azindukane kutoka kwenye usingizi mnzito alio nao, azindukane ili tuweze kutimiza wajibu huo muhimu wa mimi na yeye kuwa kitu kimoja..’ nikatulia kidogo halafu nikaongezea,

‘Ili mimi nay eye tuje kufunga ndoa…na ili dada yake huko huko alipo atulie, roho yake itulie,  na awe na makazi mema peponi!...’ nikatulia na kabla sijaendelea ndio nikasikia

‘Aamin….’

Hiyo Amini sikuitamka mimi,..hapo nikashtuka, …

 Kiukweli nilisikia sauti ya kuitikia hivyo, Aamin, na ilikuwa ni sauti ya kike..sauti ambao haikuwa tofauti na sauti ninayoifahamu mimi,

‘Oh,…’hapo nikasita kuendelea na maombi yangu, huenda ningeliendelea ningeligundua ni sauti ya nani, kitu kikanivuta kuchunguz kwanza hilo, ni nani kaitikia aamin, na,..humo ndani hakukuwa na mtu mwingine wa kike zaidi ya mgonjwa.

Awali kwa akili za haraka nilijua labda ni yule mtu, au kivuli cha mtu, kinachonifuata fuata, mtu ambaye haonekani, lakini kama ingelikuwa ni huyo mtu ningemuhisi, maana huyo mu akiwa karibu yangu huwa ninamuhisi,sikuwa na naihisi hiyo hali, …basi kama hakuna mtu mwingine aliyeitikia hiyo aamni, atakuwa ni nani mwingine..

Tuendelee na kisa chetu.

**********

Ndio ikabidi badala ya kuendelea kuomba duwa, ikanibidi nigeuza kichwa kuangalia huku na kule, …sikumuona mtu, hakukuwa na mtu wala ishara kuwa huyo mtu anayenifuata yupo karibu yangu

Baada ya kuhakikisha kuwa hakuna mtu mwingine ndio nikageuka kumuangalia mgonjwa wangu, nilihis joto, nilihis mwili kufanya kazi kwenye mkono niliokuw animeushika, lakini kwa awali akili hiyo haikuwepo, akili ilikuwa inamtafuta huyo aliyeitikia Aamin.
Ndio nikageuka kumangalia huyo mgonjwa aliyekuwa kalala kitanani, macho yangu yalitua kichwani mwa huyo mgonjwa, uso ulikuwa wazi, kitambaa alichokuwa kajifunika huyo mgonjwa sasa hakipo tena…

Nikakumbuka mama akiondoka, huyo mgonjwa alikuwa kafunika uso wake,..ila sio kwa kitambaa kile cha kufnga moja kwa moja nyuma ya kichwa, ilikuwa ni leso ndogo tu.., sasa hiyo leso haikuwepo usoni…uso ulikuwa wazi, na sasa ninachoona ni macho…

Macho yaliyofunguka,…macho yaliyokuwa yakiniangalia mimi, macho makuwa yaliyojaa nyusii nyingi, kama yamepakwa wanja, …mmh, …lakini sio macho tu, bali pia na uhai kuwa hayo macho yanaona,..sina uhakika na hilo, ila macho yalikuwa ymefunguka.

Sikuamini….akili ilikuwa haiamini hicho inachokiona, ni kama vile ulitaka upate pesa, na sasa unapata dhahabu…, japokuwa ndivyo nilikuwa naomba, moyoni nilikuwa naomba hivyo, mama wa huyo binti ndio alikuwa anomba hivyo, baba ..na wengine wanaompenda huyo binti walikuwa wanatamani iwe hivyo…

Lakini kilichonivutia zaidi ni …..macho, eeh, macho, …ya huyo mdada mgonjwa, yalinivutia sana,..kiasi kwamba nilihisi moyo ukiganda, nikawa namuangalia tu…na nilichoweza kukisema kwa wakati ule …ni..ni…ni ….

‘Ni ni…ni…’nilijikuta nikisema hivyo,..na kabla sijasema zaidi ndio mlango ukafunguliwa akaingia docta akiandamana na mama wa huyo binti..

Kiukweli sio kwamba niliathirika na umbile , macho, na uzzuri wa huyo binti , bali kulikuwa na jingine kubwa, lakini kabla sijaweza kuliweka wazi, kiakili na…mara ndio wakaingia docta na mama yake huyo mgonjwa.

‘Vipi kuna nini kimetokea mbona upo kama umeona mzuka..?’ aliyeuliza alikuwa ni docta na huku mama akiwa na hamasa, hakuacha kuendelea kuangalia pale kitandani, na ukumbuke huyo binti alikuwa katulia vile vile, ila…macho,….na mama alipomuona vile sijui nisema nini..

‘Mungu mkubwa….mwanangu umeamuka, mwanangu umezindukana, mungu mkubwa namshukuru mungu, namshukuru mungu siamini…’akasema mama akiinua mikono juu, na wakati huo docta alikuwa akiniongelesha mimi hakuwa na habari ya kumuangalia huyo binti kwanza, ila aliposikia kauli ya mama ya kumshukuru mungu, ndio na  yeye macho na akili yake ikaenda kule kitandani

Kwa haraka docta alimfuata huyo mgonjwa kitandani na kuanza kumpima pima, na alipomaliza, akasema;

‘Mgonjwa yupo kwenye hali nzuri, muhimu kwasasa ni zoezi la kuinuka, …mazoezi ya viungo na mengine, maana alikuwa kalala muda mrefu na viungo vinakuwa kama vimekakamaa, lakini yupo safi na muda tu anaweza hata kutembea,…’akasema

‘Nimepona mama….’ilikuwa sauti ya mgonjwa na hpo ndio nikajua ndio yeye aliyetamka yale maneno ya Aamin…nikageuka kumuangalia na yeye huku akiwa kakumbatiwa na mama yake pale kitandani akanitupia tena jicho…tukaangaaliana, na hapo hapo nikajua ndio yeye..

‘Umepona mwanangu , siamini, siamini, natamani nikuone ukiinuka ukitembea, unipe faraja nijisikie na mimi ni mama, nina mtoto, amuka basi mwanangua…’akasema mama yake akijaribu kumuinua mama yake, lakini binti akatamka neno lililowafanya wote watulie kidogo.

‘Baba yupo wapi..?’ akauliza huyo binti akiangalia huku na kule...

‘Baba yako yupo, alikuwepo, katoka kidogo, na tukimpatia taarifa, kuwa umeshapona, atafurahi sana..’akasema mama yake

‘Nataka nimuone baba yangu kwanza…’akasema binti na hapo watu wakaangaliana.

‘Atakuja kwani una haraka gani na baba yako, naye kachoka anahitajia kupumzika, alikuwa hapa muda mfupi uliopita….’akasema mama

‘Nataka nimuone baba yangu, yupo wapi, naona kama mnanificha jambo, najua baba kapatwa na kitu , nataka kuhakikisha, nataka nimuone baba yangu kwanza, la sivyo mniambie ukweli, babayangu yupo wapi…’akasema hivyo huyo binti, na aliyeweza kuufunua ukweli alikuwa ni docta, docta akasema;

‘Baba yupo, usijali, .. ila kutokana na hali yako ilivyokuwa, hali ya baba yako ilibadilika ,akazidiwa ana kuanza kuumwa, na hivi sasa yupo kwenye hospitali hii hii kalazwa, akipatiwa matibabu, anaendelea vizuri, na nikuembie kitu, kupona kwako ndio itakuw afaraja ya kumfanya yeye apone haraka, …’akaambiwa na docta.

‘Basi kamwambieni nimepona, nataka na yeye apone, aje anione, yawezekana likafanyia leo, sasa hivi…’akasema na docta akasema,

‘Usijali mimi mwenyewe nitakwenda huko, mguu kwa mguu nikampe hiyo taarifa kuwa umeshapona na unaongea, na hivi karibuni tu utaanza kutembea..’akasema docta

‘Hapana usiende wewe,…wewe ni docta bado nakuhitajia hapa, mimi ninataka huyu, masaidizi wako ndio aende, si docta wako msaidizi au nilikuwa naota..nataka yeye akamwambie baba kuwa nimepona na pia ili aweze kumpa baba hizo taarifa zingine alizokuwa kiniambia, nataka baba akija hapa alitambue hilo…’akasema binti.

‘Atambue nini..?’ akauliza mama yake akimuangalia binti yake kwa mashaka.

‘Kwani hujui mama, hajakuambia tu..?’ akauliza binti, akimuangalia mama halafu mimi, halafu docta, na kabla docta hajasema kitu mimi nikasema;

‘Sijamwambia mama, unajua ilikuwa sehemu ya matibabu yako, na mama hajui hayo matibabu, na mengine nitamwambia, …subiri kwanza…si unajua tena kila kitu kin autaratibu wake,…umenielewa..’nikasema

‘Sawa nimekuelewa, lakini nenda kwa baba kwanza umwambie kuwa nimeshapona na ikibid kama ni kweli basi uanze kumuambia, au hilo ni haraka sana,..mimi nakumbuka uliniambaia upo tayari au, haya sawa mimi nitakaa kimia, …mengine utajua wewe mwenyewe, ila ninataka baba yangu awe afurahi , ili naye apone haraka, mwambie asipopona haraka na mimi nitashindwa kupona haraka..’akasema.

‘Utapona haraka binti yangu, kwanza ninataka mimi mwenyewe nianze kukupa zoezi la kuinuka hapo ulipolala, uanze kutembea,…’akasema mama akiwa na haraka ya kumuinua na docta akasema

‘Mama, bado..subiri, kuna mafuta ya kumkanda..nitakuelekeza jinsi ya kufanya, inabidi viungo vyote vichuliwe, kabla ya kuanza zoezi la kusimama, ..ni hatua kwa hatua, ..na wewe nenda ufanye ulivyoagizwa..’akasema docta docta alipoona bado nimesimama nikimkodolea macho huyo binti..

‘Sawa bosi,..’ nikasema huku natembea , huku naangalia nyuma nikajikuta nagongana na ukuta…docta aliyekuwa akiniangalia akaangua kicheko, na wengine wakageuka kuniangalia lakini nilikuwa nimeshatoka nje.

**********

Wakati natoka mle ndani akili sasa ilishatulia, nikawa nikiwazia jinsi gani ya kukutana na huyo mzee, …ukumbuke hasira za huyo mzee dhidi yangu, japokuwa mpaka sasa hajanitambua kuwa mimi ni nani,..na sina uhakika kama ananifahamu pili, je akija kugundua kuwa mimi ndiye niliyefanya mabaya kwa binti yake mpaka akajiua, itakuwaje wakati alishasema mara nyingi kuwa huyo mtu atakuwa halalii yangu, ama zake ama zangu..

‘Oh, sasa naingie kwenye mtihani mwingine, nakuomba mungi wangu unipe wepesi, niweze kupambana na mtihani huu, ninajua nimekosa, na nia na lengo langu ni kutubu, lakini kwa hali ilivyo siwezi kukiri ukweli mbele ya hawa watu, nahisi itaweza kuleta shida, sasa nifanyeje..

Nikawa nawaza huku natembea huku namuomba mungu wangu..

‘Sasa nifanye nini..nitoroke, lakini siwezi kutoroka maana nimegundua kitu muhimu sana katika maisha yangu, mpaka sasa hivi siamini…huyu ni mrembo wa nama gani, huyu..oh, haiwezekani..na nikajikuta nimeshafika chumba alicholazwa Mzee..na nilipofika mlangoni, maana kitanda cha huyo mzee kilikuwa karibu sana na mlango nikasikia sauti ikisema;

‘Yaani Docta, siku nikikutana na huyo mtu, ..sizani kama polisi au nani ataweza kunizuia, ..yaani mpaka nihakikishe na yeye hayupo hapa duniani tena..’ilikuwa sauti ya huyo mzee .

‘Usiseme hivyo mzee, unajua kauli kama hizo zinaweza kukufunga, inaweza ikatoke ala kutokea huyo mtu akazurika na jambo jingine watu wakavumisha kuwa wewe ulisema utafanya hivyo, chunga ulimi wako mzee…’yawezekana ikawa sauti ya docta.

‘Hilo mimi sijali nimeshatamka hivyo, kama yeye alijiona kidume basi nitauona huo udume wake,…ngoja nijiweke vyema, sijachoka kumtafuta, ila nahisi ipo siku atajitokeza tu..’akasema huyoo mzee.

Na mimi nikawa nipo mlangoni, kumbe docta aliweza kuniona nikiwa nimesimama kule mlangoni akasema;

‘Ni nani wewe upo hapo mlangoni, sio muda wa kuona wagonjwa sa hizi..’akasema na mimi moyoni nikasema,

‘Sasa kumbe ndio mwanya wa kuondoka hapa  na kukimbia moja kwa moja..na kabla sijachuku maamuzi hayo mara nesi mmoja akaja kwa nyuma na kusema;

‘Mbona huingii, wenzako wanasubiria taarifa yako …wana furaha kweli, usiwacheleweshe ingia, …’akasema nesi

‘Ni nani huyo …?’ akauliza docta kwa ndani

‘Si huyu msaidizi wa docta rafiki yako…’akasema nesi

‘Vipi lakini huko kuna taarifa nzuri, vipi huyo mgonjwa,…?’akasema docta na mimi sasa nikawa nimeshaingia ndani hapo alipolazwa Mzee Mashauri.

‘Mambo mazuri kabisa, huwezi amini mgonjwa sasa anaongea, nimemuacha akiongea na mama yake…’nikasema

‘Kweli eeh, mungu mkubwa, ..ooh, unaniafanya na mimi nitamani kuinuka hapa, ooh, lakini mwili bado mnzito....’baba akasema akionyesha furaha;

‘Ni kweli baba na hivyo nimekuja kukuchukua, binti yako anasema asipokuona wewe hataweza kupona vizuri, anataka kuhakikisha kuwa upo salama..’nikasema.

‘Oh..docta,..inabidi niende,fanya ufanyavo ili niende huko nikamuona huyo binti yangu,…siwezi kuzuia hiyo furaha, nahisi kupona,..ooh, mwili bado mnzito, nisaidie docta nisimame…’akasema na docta akataka kusita lakini baadae akawa anamsaidia huyo mzee na mzee akaweza kusimama.

‘Docta nimepona, nitajikongoja mpaka nifike huko, nataka bint yangu apone haraka…anione nikiembea mwenyewe na kufika hapo alipo…’akasema na kweli akaanza kujikongoja, hatua kwa hatua, na kila hatua ikawa inaleta maendeleo ya hatua nyingine mpaka akaanza kujichanganya.

‘Sasa safi..’akasema docta.

‘Lakini ..naona..’ halafu nikatembea hadi pale nikawa namsaidia huyo mzee, huku moyoni nikiomba, na kumbe nilikuwa naongea kwa sauti…

‘Ewe mola wangu nakuomba umuwezeshe huyu mzee, baba wa binti, ili aweze kupona ili aweze kumuwezesha bint yake apone haraka, na wote wapone haraka, ili iwe furaha kwetu sote, na furaha iweze kufuta yaliyopita..oh, mola tusaidie kwa maombi yatu…’nikawa naomba hivyo, mara baba akasema

‘Aamini..’ nikashtuka, na kushtuka kule nikawa nimemuachia huyo mzee, akayumba akataka kudondoka, lakini akajikaza na kuanza kuvuta hatua, moja mbili tatu…akaanza kutembea vyema, huyoo…hatua kwa hatua, sasa yupo peke yake bila kushikiliwa.

‘Oh, kijana kweli wewe una kipaji, maombi na duwa zako zimefnaya kazi, nahisi nguvu ya ajabu, nahisi kupona,..twende mimi nipo tayari…’akasema na docta muda huo yupo nyuma yetu akitufuata nyuma kwa karibu..

‘Safi kabisa, naona sasa mzee umeshapona, ..jitahidi..’akasema docta

‘Kama umechoka mzee nikusaidie..’’nikasema

‘Hapana wewe mwenyewe  umesema bint yangu anataka kuniona, nikikitembea peke yangu mnzima ili aweze kupona haraka, …usinishike kabisa, twende, hatua kwa hatua hakikisha huchezi mbali, ila usiniguse…’akasema sasa kitembea vyema na huku akinitupia macho na kuniangalia kwa macho yenye udadisi, akasema

‘Na wewe….sijui nitakupa nini, nimesikia sifa zako kutoka kwa mwalimu wako, docta kuwa una kipaji cha kuombea watu, …na ninauhakika ndio wewe umeweza kumuomba binti yangu, sasa anapona au sio, namshukuru sana mungu kuwezesha nyie kuwepo, maana haya yote ni kwa uwezo wa mungu,…na nikuulize kitu, wewe umeshaoa, una watoto wangapi?’ akaniuliza

‘Bado mzee, …mimi bado sijaoa, ndio natafuta mke…’nikasema

‘Usiogope kuoa, maana ndoa ni wajibu, na maisha, riziki,  mungu mwenyewe atajalia tu kwa neema zake, na kuoa haraka kuna baraka zake, unapata watoto mapema, na unakuja kufaidi matunda ya watoto wako ukiwa bado una nguvu…sasa oh, natamani wewe sasa uwe mkwe wangu, unasemaje…’akasema

Moyoni nikasema;

‘Imejipa, lakinni..mtihani huu…’nilijikuta nikisema

‘Mtihani kwa vipi, humpendi bint yangu kwa vile hajiwezi, wewe sio ndio utamtibia,.usije kusema nakutupia mzigo, atapona huyo binti…lakini sikulazimishi, ila nimekupenda sana, sio kama hiyo mihuni mingine inadanganya, ilimpa binti yangu mimba, na ikaja kumtelekeza hao sio watu., ni wanyama..’akasema kwa hasira.

‘Mzee, cha muhimu sana ni kusamehe, ili upone vyema, usiposamehe ukaweka mafundo ya hasira, visasi, kupona inakua vigumu sana, samehe na wewe utasamehewa..’nikasema nikifuatilia maneno aliyowahi kutamka docta.

‘Ni kweli eeh..sawa, kwa ajili ya binti yangu kama inabidi kufanya hivyo nitasamehe..lakini huyo mtu lazima nimfanye kitu kibaya…oh, kusamehe vigumu kijana wangu, tunakaribia, sasa uniache, ila usicheze mbali ukiniona nayumba tu , usogee..haya fungua mlango..

NB: Naishia hapa


WAZO LA LEO: Tujihaidi sana kuweka nyoyo zetu mbali na shetani, shiriki ni namna mojawapo ya kumpokea shetani, matendo mabaya kama wizi, uwongo, nk,..ni namna nyingine ya kumpokea shetani kwenye maisha yetu...

Kuna watu wanamkaribisha shetani kwenye maisha yao bila wenyewe kujijua, ukifanya shiriki, ukawa na chuki na wenzako, ukawa muongo, mwizi, mdhulumaji, na madhambi mengine mbali mbali, ujue wewe umemkaribisha shetani kuwa rafiki yako..tumkwepe shetani maana shetani ni adui wa mungu, naadui wa mungu ni adui wetu…shetani kazi yake ni kufarakanisha ndoa, ndugu kwa ndugu, wazazi na watoto,..marafiki na marafiki, ili wasipatane..tumkwepe na tumuondoe shetani katika maisha yetu… 

Ni mimi: emu-three

No comments :