Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, April 21, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-11

                           
 Mpenzi wa facebook kaniingiza kwenye mitihani mikubwa na sasa imefikia hatua naambiwa nimuoe mdada mgonjwa, asiyejiweza, ndugu yake na marehemu, ...huku kwa upande mwingine nilishaambiwa ili niondakane na mataizo niliyo natakiw nimuoe mpenzi wangu wa facebook, lakini swali kuwa huyo mpenzi wa facebook yupo wapi....

Mimi docta tukaamua kwenda makaburini, kuhakiki kaburi la yule mdada aliyefariki baada ya mimi kumkataa, alijiua kwa ajili yangu, sijui docta alitaka twende huko kwasababu gani, sasa angalia kilichotukuta,...

Tuendelee na kisa chetu..

************

Niliposikia docta anaitwa huko kwa huyo mzee nikajua sasa mambo yamesharibika, labda mzee wa watu yupo kwenye hali mbaya sana na kuna kitu anataka kuacha kama usia,…lakini mbona kasema;

‘Unaitwa na Mashauri…kwahiyo huyo mashauri ndiye anamuiita,…kama anamuita sizani kama ana hali mbaya kiasi hichoo…’nikajipa moyo hivyo, nikawa nasubiria pale nje, na baadae docta akaja, huku akionekana mwingi wa mawazo, hakusema lolote kuitwa kwake kwa muda huo.

‘Unajua,..nataka twende kwenye hilo kaburi alipozikwa huyo marehemu…’akasema

‘Kufuata nini huko..?’ nikauliza kwa mshangao

‘Hujiulizi ni kwanini kila ukitaka kwenda huko, huwezi kufika, awali ulisema huyo mpenzi wako alikuelekeza huko, ni kwanini… hajajiuliza hilo swali, sasa mimi ninachotaka kufanya ili kuondoa vitu kwenye mioyo yetu, na kuhakiki hilo kaburi,.na mengine yatafuata baada ya hapo …’akasema

‘Lakini nakumbuka awali ulisema kuwa mpenzi wangu wa face book sio mtu, ukasema ni shetani, mimi nilikukatali hilo kabisa mpaka sasa siamini hivyo najua huyo mtu yupo ila ananichezea tu…’nikasema

‘Kwanini akuchezee hivyo, na mpaka akuvute uje kwenye hii familia, ina maana na yeye anahusika kwa namna moja au nyingine..’akasema docta.

‘Hata mimi hapo sielewi, ....lakini docta nikuulize huko kaburini unataka tukafanye nini..,?’ nikamuuliza.

‘Wewe twende tu huko..na kingine ninataka unionyeshe ile picha aliyokutumia huyo mpenzi wako , ulisema alikuwa kakaa juu ya kaburi, au sio..’akasema.

‘Hapo tena,..nimejaribu hata kutafuta sehemu ya picha, haipo imefutika na kila kitu chake hakionekani tena...’nikasema.

‘Kwahiyo ulijaribu kuchat naye ukawa humuoni..?’ akauliza.

‘Kuna muda nilitaka kumuangalia, ndio nikakuta hayupo hewani na account yake hapo tena, nikama kajifuta, kaiondoa kabisa…’nikasema.

‘Ulikuwa muda gani huo, ni kabla hatujafika huku hospitalini..?’ akauliza docta

‘Ndio ni muda ule tulipotoka kuongea na yule mzee tuliyekwenda kwake kwa ajili ya kuulizia familia ya huyo mzee Mashauri…’nikasema.

‘Ok, nishaanza kuelewa,… lakini muhimu hebu kwanza tufike huko makaburini kuna kitu nataka kuhakiki..’akasema.

‘Kitu gani docta, docta wewe kila kitu unataka kuchunguza mengine hayana maana docta,..lakini kama unataka twende sawa,… twende tu… lakini mimi sioni umuhimu wa kwenda huko…’nikasema.

‘Kuna umuhimu, utaona tu..’akasema docta.

********
Ili kufika huko kwa haraka tukachukua piki piki ya kubeba watu wawili na safari ikaanza, kulikuwa na mwendo kidogo kabla ya kuweza kuingia barabara hiyo ya mtaa wa makaburini, sasa tulipoingia mtaa huo, ndio ghafla, dereva akaongeza mwendo.

‘Vipi..dereva mbona unakimbiza piki piki hivyo, ni hatari?’ akauliza docta, dereva wa hiyo piki piki hakusema neno, na ghafla likaja roli likitokea mtaa mwingine kwenye baraka zinazoungana na hiyo barabara tunayokwenda nayo...akashindwa kufunga break.., tukaavaana na hilo roli..., sikujua, nilichogundua baadae nipo kwenye mtaro wa maji machafu.

‘Upo sawa, ilikuwa sauti ya docta…akinifuata pale nilipo, alionekana kuchechemea,

‘Oh hata sijui, kwanini huyu dereva akafanya hivi..’nikalalamika.

‘Nimemuuliza anasema aliona kitu cha ajabu kikitufuata..ndio akawa anakikimbia…’akasema docta

‘Kwa vipi wakati yeye alikuwa kaangalia mbele....yale yale nisiyoyataka mimi..’nikasema

‘Yapi hayo..?’ akauliza docta

‘Hizo imani imani, atasema aliona uchawi au shetani..’nikasema

‘Lakini kuna tatizo..sio bure, nahisi mwenyezimungu anazuia jambo fulani,…sasa tufanyeje maana dereva kaumia,…dereva vipi upo sawa…?’ akauliza docta akimuendea huyo dereva kwa muda huo alikuwa bado kakaa chini, akishikilia mguu wake, yaonekana kweli kaumia.

‘Ina maana mnataka tuendelee na safari..?’ akauliza

‘Ndio kwani si ajali tu, kama hujaumia sana twende kazini…’akasema docta

‘Huko siende tena..., nendeni wenyewe, hata kama ni pesa hiyo mimi siitaki..’akasema huyo dereva.

‘Kwanini..?’ nikauliza

‘Hicho nilichokiona, siwezi hata kukiongelea, ....huku ndio maana sitaki kuja kuna mauza uza sijui kwanini…’akasema

‘Mauza uza gani, au unavuta kidogo..?’ nikauliza.

‘Hata sijui…’akasema sasa akikagua piki piki yake, kiujumla hatukupata majeraha makubwa, na piki piki yake ilikuwa na hitilafu chache, akajaribu kuzirekebisha, na huyo akageuza kurudi huko alipotoka.

‘Sasa mbona unatuacha hapa…’akasema docta

‘Tafuteni usafiri mwingine mimi huko siende..’akasema na mimi nikamuangalia docta na docta akasema;

‘Hebu tujaribu kutembea, sizani kama kuna umbali mrefu umebakia hadi makaburini…’akasema.

‘Sawa twende..’nikasema

Hutamini tulitembea tukatembea,..mwishowe tunajikuta upande mwingine wa bara bara…

‘Tumepotea docta..’nikasema

‘Haiwezekani..’akasema docta, baadae tukaamua kuulizia watu, na watu wakatushangaa, wakisema;

‘Mbona makaburini mumepaacha mbali kabisa huko nyuma…’akasema, na muda ulikuwa umekwenda sana, na docta akasema;

'Tumeshachelewa, haina haja ya kwenda leo huko tena, tutakwenda siku nyingine

Baadae tukaamua kurudi nyumbani , tukatafuta usafiri wa kurudi, na usafiri wa kurudi nyumbani wala haukusumbua…

*********
 Tukiwa tumefika nyumbani hoi, kila mmoja akiafuta njia za kujimwagia maji na kujipumzisha mara simu ikaita, ilikuwa simu ya docta.

‘Haloh, ..’akasema docta akiwa hana hamu ya kuongea na mtu lakini alichokisikiliza kilimfanya ajiweke vizuri na kusikiliza.

‘Kaanza kuongea..?’ akauliza

‘Ok, sasa tunakuja…ingawaje, mmh..ok tunakuja..’akasema docta na kukata simu

Mimi nilikuwa nimechoka na nimeshaanza kuutafuta usingizi..

‘Docta kama ni kwenda uende peke yako, mimi nimechoka kwanza hapa kwenye nyonga nahisi maumivu isije ikawa nimeumia ndani kwa ndani..’nikaanza kulalamika.

‘Bint anakuulizia ..’akasema

‘Binti, binti gani huyo..?’ nikauliza

‘Binti wa mashauri…nasikia alipata fahamu kidogo, na kuanza kuongea kukuhusu wewe, ila hawajui kuwa alikua akiongea kukuhusu wewe, ila mimi nimeelewa hivyo…’akasema.

‘Kwa vipi maana hanijui,na niliongea akiwa kafumba macho, na sikumbuki kumuambia jina langu…’nikasema

‘Katamka, maneno machache kuashiria ni wewe…halafu akapoteza fahamu hajaweza kuzindukana tena,…mama alikuwepo muda huo, anasema yeye alitoka na aliporudi nesi akamuambia kuwa binti yake alizindukana kidogo,na kuongea maneno hayo...'akasema docta.

‘Oh…sasa huu mtihani, unaona docta, umenitia kwenye matatizo, sasa itakuwaje, …’nikauliza.

‘Huyo binti ni lazima ufunge naye ndoa,…’akasema docta

'Docta haiwezekani, mimi najua tunafanya hivyo ili tu aweze kuzindukana..'nikasema

'Ni lazima uje kufunga naye ndoa...'akasema

*************
‘Docta,..hivi unanitakia mema kweli, mimi mwenyewe hali yangu sasa mbaya, sina mbele wala nyuma ndio nimchukue huyo binti …tutaishije..?’ nikauliza.

‘Huyo ndiye atakufanya ubadilike, na ukumbuke hayo wanayopambana nayo , matatizio ni sababu yako, kwahiyo unatakiwa uwasaidie sana, fany aufanyavyo hiyo familia irejee kwenye msimamo, vinginevyo..’akasema docta.

‘Oh..docta, kuna kitu sijakuambia wakati nipo pale hospitalini, kuna mama mmoja sijui tumuite mtabiri au …yeye kifupi ukifika kwake anakuelezea tatizo lako hata kabla hujamwambia, na kukuelekeza jinsi gani ya kulitatua, ana karama na kipaji hicho, na nilipofika kwake, akaniambia kuwa ili matatizo yangu yaishe ninatakiwa nimuoe mpenzi wangu wa facebook..’nikasema.

‘Ukamwamini, kwanini mpaka ukaenda kwake, ina maana bado una shaka na huyo mpenzi wako wa facebook..?’ akauliza.

‘Sikuenda kwa nia ya kuenda,..labda nina shida hiyo, ilitokea tu, nimefika pale nikaona nipoteze muda na mimi nisikie hicho wanachofanyiwa wengine maana wanaamini na wanadai kweli wamefanikiwa,.., na sio kwamba mimi niliamini hayo,  la khasha, mimi nina msimamo wangu, ila kiukweli hata kabla ya kauli yake hiyo, mimi bado naamini kuwa huyo mpenzi wangu wa facebook, yupo…na ipo siku nitakutana naye..’ nikasema.

‘Yupo wapi huyo mpenzi wako wa facebook, maana ufanye mambo yenye uhakika..kama unakufahamu huko nyumbani kwake, tukitoka hapa twende huko na mimi nitakusaidia kuwa mshenga wako unajua anapoishi..?’akauliza docta.

‘Ndio tumtafute docta..unisaidia kwa hilo ili tumpate…’nikasema

‘Nilikuambiaje awali..kuwa mtu huyo hayupo, sio mtu…hukuniamini au..?’ akasema docta

‘Docta najua umesemea tu,… nina uhakika hiyo kauli yako kuwa huyo ni shetani, uliisema tu, kama watu wanavyosema ila wewe mwenyewe huamini hayo.., docta nikuambie kitu mimi nitahakikisha namtafuta huyo mpenzi mpaka ninampata, huyo ndiye chaguo langu..’nikasema

‘Huyo sio chaguo lako, maana huyo mpenzi wako ni wa ndoto hayupo….utakuja kuliona mwenyewe, mpenzo wako wa ukweli ni huyo bint mgonjwa,…na ni muhimu ili utokane na matatizo ya huko mbele, uhakikishe huyo binti mgonjwa amepona, na kupona kwake ni mpaka wewe ufunge naye ndoa..’akasema docta

‘Huo sasa ni mtihani docta, kwanini mnafanya hivyo, kwanini unataka maisha yangu yawe kwenye dhiki na mawazo, unajua jinsi mapenzi yalivyo, ukimpenda mtu unakuwaje, ….nielewe docta..’nikasema

‘Nakuelewa sana ndio maana nakusisitizia kuwa chaguo lako kwa hivi sasa ni huyo binti kwa sababu kwanza unatakiwa ulipie mateso yote uliyoisababishia hiyo famlia, na huna jinsi ya kulipia hilo maana huwezi, ila kwa kupitia huyo binti unaweza angalau kifuta jasho…’ akasema docta

‘Oh….’nikaguna hivyo tu.

‘Na huna jinsi ya kuiliwaza hiyo familia, mpaka upitie kwa huyo binti, ujue kupona kwa huyo binti, ndio faraja kwa yule mama na kwa baba yao, nimeongea na huyo mzee, kiukweli anateseka sana ndani kwa ndani…sasa kama huna huruma kiasi hicho, kama bado unataka kuendelea kubeba madhambi na misuko suko,endelea na huyo binti wako wa facebook…’akasema docta.

‘Mhh, docta hapo umenitega,…unanifanya nisiwe na jinsi nyingine, lakini huyo binti mgonjwa akipona tu, nitamuambia ukweli, kuwa yupo niliyempenda, ila yeye nimeamua kwa vile ilitakiwa apone, na kwahiyo anisaidie, kama atakubali, najua atanielewa tu mimi nitamuambia ukweli, na,..’nikasita

‘Kwahiyo unataka na yeye ajiue kama alivyojiua dada yake, ndio unataka hivyo…usije kuthubutu kuongea kauli kama hiyo mbele yake, …huyo hahitajii kauli yoyote ya kumvunja nguvu,..han uwezo wa kubeba mateso mengine,.. utamua…’akasema docta kwa ukali.

‘Lakini docta..ok, ok…sawa nitajua jinsi gani ya kuongea naye, ..ila nahitaji kwanza niwasiliane na huyo mpenzi wangu wa facebook, namuhitaji sana, nataka anielewe asije akafikiria nimtenda, unajua tumeshaahidiana mengi, sasa ..ni muhimu nimueleze kinachoendelea…’nikasema

‘Wasiliana naye kabla hatujafika huko hospitalini…, ingia kwenye mtandao mtafute, au kuna jinsi gani nyingine ya kuwasiliana naye, sema nikusaidie…’akasema docta

‘Hakuna njia nyingine njia ni hii tu ya kupitia mtandao…’nikasema

‘Umeona eeh, nikuwa huyo mtu hayupo…cha muhimu kuanzia sasa weka akili yako kwenye vitu halisi, ..usitekwe na mambo ya mtandao, huyo mchumba wa facebook hayupo ni kiini macho tu,..ndio maana nakuambia  ni shetani, ..huyo sio mtu, nielewe nikisema hivyo, kama ni mtu kweli mwambie ajitokeze, muonane naye….’akasema docta.

‘Oh….nitamfuta docta, na nitakuja kukuonyesha…’nikasema

‘Ukimpata nitakupa zawadi..’akasema docta

‘Docta…’nikasema

‘Nitakuozesha hapo hapo bila kupingwa,…’akaongeza kuongea docta

‘Oh…ngoja utaona…nitamfuta na docta ujue ahadi ni deni..’nikasema

‘Najua hivyo, ndio maana nimekuahidi hilo…’ tukaongea mpaka tukafika hospitalini na tulipofika tu, nikaambiwa nielekee chumba alichokuwa kalazwa huyo mdada, na nikaelekea huko na wakati huo docta akaelekea chumba alicholazwa mzee Mashauri,.

Nilipofika kwenye hicho chumba alicholazwa huyo mdada,..nikafungua mlango, na mle ndani zaidi ya mgonjwa alikuwepo huyo mama yake kama kawaida, hataki kuachana na binti yake, safari hii alionekana kuwa na huzuni zaidi ya awali.

‘Vipi mama anaendeleaje mgonjwa..?’ nikauliza

‘Hali inazidi kuwa mbaya, alizindukana mara moja mimi sikuwepo wakati anazindukana, nesi anasema alipozindukana aliongea maneno fulani…’akasema

‘Maneno gani?’ nikauliza

‘Eti alisema, aliongea hivi,…namtaka mchumba wangu,..aliyeniahidi kuwa atanioa, mchumba wangu ndiye aliyesababisha kifo cha dada yangu, nataka anioe ili kuwezesha dada yangu atulie…alisema hivyo na nesi akawa kayaandika hayo maneno kwenye karatasi…hii hapa..’akasema mama akinionyesha hiyo karatasi

‘Nini…mama, ina maana kaweza kusema hivyo..oh,..?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Ndivyo alivyoniambia nesi, mimi sikubahatika kumsikia, maana tokea hapo, hajaweza hata kutikisika tena, yaani mimi naanza kukata tamaa, sijui kama ataweza kuzindukana tena, hata docta anasema ikifikia kesho inabidi waondoe hayo mashine ya kupumulia,…ina maana nitampoteza binti yangu tena, hata sijui nifanye nini, kwanini mimi jamani…’akaanza kulia

‘Mama usilie, amini mungu, na kwa uwezo wa mungu,… sio mimi , nitajitahidi nifanye niwezavyo, ili binti wetu azindukane, nitajitahidi tena kuongea, eeh, kumuombea, maana hata mimi linanigusa, nitafanya juhudi zote hata kama….nitafanya mama…’nikataka kusema ‘kumuoa, ‘ lakini nikakumbuka kuwa hilo halitakiwi kusemwa

‘Sawa…sina jinsi, nitafanya nini mimi tena, sina la kufanya nimeshakata tamaa,.. haya mimi nakuachia bint yangu, ila ninakuomba usije kuongea mambo ya kumuumiza, nataka utakachoongea, sijui unafanyaje…unaomba au unafanya nini, uombe kwa maneno ya kumsaidia, sitaki tena…kuja kumpoteza binti yangu, ni heri mimi nife na binti yangu apone…’akasema huyo mama

‘Nitajitahidi mama, kwa uwezo wa mola wetu..’nikasema na huyo mama akaondoka nikabakia na huyo binti…nikasogeza kiti karibu na kile kitanda. Na kusogeza mkono wangu kushika viganja vyake…

‘Mpenzi  nimerudi tena.., nahitajia kauli yako , jibu lako kuwa kweli upo tayari nikuoe, upo tayari kuchukua nafasi ya dada yako, ukumbuke, dada yako anakutokea akitaka ulipize kisasi, na kulipiza kisasi haisaidii kitu.., kinachotakiwa ni wewe kuchukua nafasi yake na mimi nipo tayari kwa hilo, na kwa vile mimi ninakupenda, basi upone haraka, ufungue macho yako haraka, uweze kuwa kama zamani ukiwa na afya yako…kumbuka ninakupenda sana mpenzi wangu..’ mkono ukaanza kutikisika…kule kutikisika nikajikuta nimemuachia,..

Nikatulia, na nikanyosha mkono wangu tena na kushika kiganja cha huyo mdada, nikaulazimisha ikawa kama tunasalimiana hivi,  viganja vimefumbata..

‘Nakushika kiganja chako cha mkono,kama ishara ya mshikamano ,kuwa mimi na wewe tu wapenzi wa kweli kwa uwezo wa muumba wetu, ewe mola wetu, ninakuomba kwa rehema zako, umponye mja wako huyu, aondokane na hicho kifungo cha umauti, nakuomba mola umjalie mja wako huyu azindukane ili tuweze kutimiza wajibu huo muhimu wa mimi na yeye kuwa kitu kimoja..tufunge ndoa…na ili dada yake huko alipo atulie na awe na makazi mema peponi!

‘A-a-miin…’ hiyo kauli sikutamka mimi,…

Hiyo amini sikutamka mimi nikajua labda na ya yule mtu anayenifuata fuata, nimesikia kwa masikio yangu, sio hisia,…niliinua macho yangu na kutizama wapi sauti hiyo imetoka…

Nikgeuza kichwa kuangalia nyuma hakuna mtu, nikageuza macho na kuangalia kitandani, na nilichoona kilinifanya nivute mkono wangu kutoka kwa huyo binti na kutaka kusimama, sasa sijui nilikuwa nataka kukimbia au kufanya nini..macho yalitoka kama mtu aliyeona kitu cha kutisha, …

‘Ni..ni..ni……’ na mara mlango ukafunguliwa.


WAZO LA LEO, Duwa na maombi kwa watu kuelekeza kwa mola mwingi wa rehema, mwenye kurehemu ni tiba kubwa kuliko tiba zote, tunapofikwa na maradhi, majanga, shida na mitihani mbali mbali, tusichoke kuomba, kumuomba mola wetu, kwani mola akisema liwe litakuwa bila pingamizi yoyote.
Ni mimi: emu-three

No comments :