Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, April 20, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-10 Nilishaambiwa ili matatizo yangu binafsi yaishe natakiwa nimtafute mpenzi wangu wa face book..nimuoe..., huyo mpenzi hajulikani wapi alipo, wengine wanadai kuwa huyo sio mtu, huyo ni shetani, wengine wanasema huo ni mzimu wa binti niliyemtenda akajiua,...

'Ukitaka matatizo yako yaishe umuoe huyo mpenzi wako wa facebook,...' ndivyo nilivyoambiwa na huyo mama, ambaye wanadai ukifuata hayo atakayokuambia ujue matatizo yako yatakwisha, wengi wameambiwa wakafanya waliyoelekezwa na wamefanikiwa ..

Lakini sasa ndio nakutana na docta, docta naye ananiagiza mambo mengine ambayo yananiweka njia panda, je nifuate ya huyo mama ili nipone matatizo yangu au nifuate ya docta ili nibebe mzigo wa madhambi yangu mwenyewe

Niende nikakutane na huyo binti mgonjwa, binti ambaye kapoteza fahamu, ..muda sasa hajiwezi hata kuinua mwili, binti ambaye kafanya baba yake adondoke na kupoteza fahamu, sasa mimi naambiwa niende nikamtamkie maneno, maneno ya kujifunga, ....na sio maneno, tu,... inatakia iwe hivyo, je ni adhabu kwangu, kwa hayo niliyowafanyia hao watu, na docta anataka niadhibiwe kwa njia hiyo, au kuna nini kitatokea..

Tuendelee na kisa chetu

**********

 Hii hali ya kuhisi mtu anakushika au unaona watu wakati watu wengine hawawaoni ilinitesa sana,…hali hii ilinianza kipindi kile nilipopata ajali, …wakati mwingine unakuwa kama upo kwenye dunia yako,..unaweza ukawa unaongea na watu , watu weneywe unawaone peke yako..

Nikaangalia saa nikakuta muda umekwenda sana, na nilitakiwa kuingia ndani nionane na huyo binti, na nisema hayo niliyoagizwa na docta , na docta alisisitiza swala la muda,…nilipoona nimepoteza muda mwingi kwa kuwaza tu,nikaamua kuchukua hatua kwahiyo bila kupoteza wakati sikujali tena zile sauti au huyo mtu anayenifuata fuata na wakati haonekani.

Nikasukuma mlango na kuingia ndani….Nilipokuwa kwa ndani, sikusogea mbali na mlango nikasimama, nikakagua mazingira ya mle ndani, na wakati huo nilihisi masikio yangu kama yananguruma, sijui ni kutokana na hali ya hewa ya humo ndani au ni kichwani kwangu tu.

Kwa mbele yangu niliweza kukiona kitanda, na mle kitandani alikuwa kalala mgonjwa, nahisi ni huyo binti, kawekewa mipira ya kuongeza maji au dawa, na…pembeni yake alikuwa kakaa mama mtu mnzima, mama huyo alikuwa kaegemeza kichwa kwenye kitanda, na alionekana kalala, nahisi alikuwa ni mama wa huyo binti..,..masikini alikuwa kachoka, huenda katingwa na usingizi wa kukesha.

Pamoja na kulala vile mkono wake mmoja ulikuwa umeshika kiganja cha bintie,…nani kama mama, kiukweli moyo wa huruma uliniingia nafsini mwangu,..nilimuonea huruma sana yule mama, nilimuona kama mama yangu, nakuichukulia ile hali kama vile ndio mimi nimelala pale kitandani, na mama yangu yupo hapo kitandani pembeni akisubiria kuwa nitaamuka...

Ilichukua kama dakika moja, nikiwa nimesimama pale mlangoni, nashindwa kuingia, niliogopa, kuwasumbua, niliogopa huenda huyo mama atanitambua, na kama nilivyosikia, wazazi hao walikuwa na hasira na mimi, lakini sikuwa na uhakika kama huyo mama ataweza kunitambua

Baadae …ndio nikakumbuka swala la muda,…

Kwa haraka ndio nikasogea hadi pale kitandani  , na mara yule mama akainua kichwa na kuangalia kitandani, nahisi alihisi ni binti yake kazindukana, na alipogundua sio hivyo, ndio akageuza kichwa kuniangalia..akaniona, na alionekana kama kushtuka, nahisi alijua ni docta, ...

‘Shikamoo mama ..?’ nikamsalimia.

‘Wewe ni nani na unafuata nini humu ndani hawaruhusu mtu kuingia kwa hivi sasa wamesema tumuache mgonjwa alale kwanza..’akasema huyo mama akinikagua kwa macho.

‘Mimi nimetumwa na docta, nije  niongee na mgonjwa naomba dakika chache tu..’ nikasema.

‘Uongee na mgonjwa, utaongea vipi na mgonjwa wakati hawezi kuongea, au kujiinua hajaweza hata kufungua macho, alivyolala ndio hivyo hivyo kama maiti...na awali kabla hajapatwa na hayo matatizo alikuwa anasema mwanga unamuumiza macho, haya keshakuwa kiwete ...na sasa upofu unamnyemelea..., ndio maana tumefunika usoni hivyo…’akasema.

‘Usijali mama yangu , hili ninalolitaka kulifanya ni moja ya tiba zake, sio lazima afungue macho, sina haja ya kumuamusha, mimi kuna mambo natakiwa kumfanyia hata bila ya kumgusa…’nikasema.

‘Kwahiyo wewe ni nani…?’ akaniuliza akiniangalia kwa mashaka,..nilihisi huenda kaanza kunitambua, maana kipindi kile alishawahi kuniona, lakini hakuwahi kutambulishwa kuwa mimi ni nani kwa bintie...ni kipindi kirefu cha nyuma,...kiukweli mimi na binti yake tulikuwa tunakutana kwa kificho, ila siku moja ndio huyo mama aliwahi kunifuma nikiwa na bintie, siku hiyo binti yake aliogopa sana, alisema kama mama yake atamuambia baba, basi sijui itakuwaje....
.
‘Mhh..nahisi nilishawahi kukuona mahali…’akasema huyo mama akiendelea kunikagua usoni na mimi nikaukwepesha uso wangu na kuangalia pembeni.

‘Mama, mimi ni msaidizi wa yule dakitari kutoka mikoani..na hili ninalotakiwa kumfanyia binti yako linahitajia muda maalumu na hivi sasa nimeshaanza kuchelewa, samahani kidogo mama,..kama unaweza kutupisha…’nikasema na yule mama akasimama na kusema.

‘Kuwapisha ina maana nikuache wewe peke yako na binti yangu, ndio kasema docta hivyo,... unataka mimi nitoke nje kabisa..?’ akauliza akionyesha mashaka.

‘Ndio mama kama hutojali, tafadhali ..muda unakwisha...’nikasema na huyo mama alionekana kuwa na wasiwasi lakini atafanyaje, akaanza kutembea kuelekea nje, huku anaangalia angalia nyuma..na mimi nikatikisa kichwa kumuashiria kuwa asiwe na wasiwasi. 

Akatoka nje na kufunga mlango,..nikabakia mimi na huyo binti, sasa….

Nikasogea pale kitandani, na kumtizama huyo binti, alikuwa kafunikwa sehemu ya kubwa ya usoni, ila pua na mdomo upo wazi,…usingeliweza kujua sura yake katika hiyo hali, nilitamani nisogeze ile nguo iliyofunika usoni, lakini ilionekana ni kama kitambaa ambacho kimefungwa kwa nyuma.

Hata hivyo sio vizuri, kwanini nimfunue, ila shauku ya kumfahamu ilinijaa, sana,…alikuwa kafumba mdomo, na yupo kimia, alivyolala utafikiri hana uhai tena lakini mapigo ya moyo yalikuwa yakionekana kwenye chombo kilichokuwa ukutani, kuashiria kuwa bado yupo hai…,

‘Sasa ni kazi moja mpendwa…’nikasema huku nikikaa ile sehemu aliyokuwa amekaa huyo mama, kwenye kiti, ..nikasogeza mikono yangu na kukaribia kama kutaka  kukishika kile kiiganya cha huyo mgonjwa, lakini nikasita,...kiganja kilionekana cheupe, na ule weupe ulionyesha kama vile hana damu, au yawezekana ni maumbile yake..nilimgusa kidogo, mkono ulikuwa wa baridi sana.

‘Bado dakika ngapi…’nikajiuliza nikiangalia saa.

‘Bado dakika kumi…’nikasema nikiangalia saa

‘Mungu wangu nisaidie… ’nikasema na kuanza kufikiria cha kuongea, docta kasemaje…oh, huu mtihani sasa..na ndipo nikaanza kuongea haya maneno kwa sauti ndogo lakini kama huyo binti anasikia angeliweza kuyasikia…

‘Mpendwa, sijui nikuite, mdogo wangu..lakini hapana mimi ningelipenda nikuite mpenzi,..ndio mpenzi, natamani nikuite hivyo, kwani moyo wangu unataka iwe hivyo, nimekuwa nikikuwaza tokea siku nilipoambiwa, tokea siku ile nilipokutana na wewe ukiwa na dada yako, sijui kama unanikumbuka.

Ni kweli siku moja wakiwa na dada yake niliwahi kukutana nao, lakini hatukuweza kuongea, kwani walikuwa na wasiwasi walitokea madukani, wakawa wamechelewa, na walijua huenda baba yao atakuwa amerudi, niliwasalimia juu kwa juu.

Mpenzi, tokea siku ile moyo wangu umekuwa ukikuwaza sana wewe,…na kila siku moyo wangu umekuwa ukiumia, ni lini nitakuona tena.., na leo nimeipata bahati hiyo, mpenzi, samahani kwa kutumia neno hilo, lakini nalitamka kwa vile ninataka iwe hivyo..nakupenda sana…’ nikasema nikahisi kidole kikitikisika.

Nikaangalia, kweli kidole kilikuwa kinatikisika…ni ajabu, maana wanasema tangia afikishwe hapo hajaweza kutikisika hata kidole..nikaona niongeze dozi..moyoni nikahisi raha,…unajua tena, japokuwa nayafanya haya kwa vile docta kasema.

‘Nakupenda sana mpenzi..na natamani uamuke mara moja ili niyaone macho yako yakirembua na kunitizama mimi, natamani uamuke ili , uweze kutembea tena, uweze kuwa kama zamani, …a tujuane, na hatimaye ije ile siku niliyokuwa nikiiombea, siku ya mimi na wewe tufunge ndoa…’nikasema na sasa kidole na hata kiganja cha mkono kikawa kinacheza.

‘Nazungumza haya kutoka moyoni mwangu,..niliwahi kupenda, nikaacha, …lakini sijui ni kwanini,…nilitaka nimuoe dada yako, lakini sheteni akaingilia katina kiukweli kama isingelikuwa hivyo dada yako angelikuwa mke wangu…nilimpenda, lakini sheteni akafany aliyoyafanya na siku alipofika kwangu..ikatokea ilivyotokea, nikatamka niliyotamka,….sijui ni kwanini, najuata sana…’nikasema

Sasa mkono ukawa unacheza, hata mwili, lakini hakuweza kusogea, jinsi alivyolala, nikasogeza kiganja changu cha mkono na kukishikiza na kiganja chake, nilihis kama mwili umegusa kitu kama umeme, kwani hata mimi nilihisi mtikisiko fulani mwilini mwangu, sijui kwanini…na mkono wa huyo mdada sasa ulikuwa sio baridi tena!

‘Dada yako akachukulia hasira..na kwenda kufanya jambo ambalo limekuwa likinitesa hadi leo,...na ndio sababu ya mateso mnayokumbana nayo hata nyie,  lakini labda ndivyo mungu alivyopanga,...sikujua hayo yatafikia huko,..sikujue, kama ....oh labda tusema hayo yalikuwa ni mapenzi ya mungu.

'Leo nimekuja kukutana na wewe nasikitika kukuona katika hiyo hali..nimekuja ili niweze kutimiza dhamira yangu, kama mungu kamchukua dada yako, basi...labda ndio kapanga mimi na wewe tutumize yale yaliyotakiwa yafanyike...…natamka tena, nakupenda sana, nataka mimi na wewe tufunge ndoa….’nikatulia,

Nilitulia maana mkono wa huyo binti, ulivutwa kutoka kwenye mikono yangu , na mara huyo mdada akaanza kutikisika…

Unajua kutikisika, hadi kitanda kinacheza cheza, nilipoiona ile hali, nikasimama,  nikiwa na wasiwasi, nikaangalia huku na kule, hakuna docta au ...

‘Docta…docta…’mbio nikawa natoka nje, ili kuwaita madakitari, maana ile hali sio y akawaida, na mlangoni nikakutana na docta jamaa yangu akiwa anataka kufungua mlango, na pembeni yake yupo mama wa huyo binti,..

‘Docta mgonjwa anatikisika sana, nahisi anahitajia msaada..’nikasema na wote mbio mbio hadi kitandani, na wakamkuta anatikisika lakini sio sana kama awali, na akaendelea hivyo na baadae akatulia.

‘Nusu saa tayari…’akasema docta

‘Nimeweza kufanya ulivyosema docta..’nikasema

‘Ikawaje…’akauliza

‘Awali alianza kutikisa kidole, na nilipoendelea …ndio akaanza kutikisika kwa nguvu..’nikasema.

‘Ulimwambia nini mwanangu, ulimfanya nini binti yangu.?’ akauliza mama, na docta akaingilia kati na kusema;

‘Kuna maneno nilimwambia amsomee,..ni seehmu ya dawa, huyu kijana ana karama nyingi sana,ni msaidizi wangu usijali mama  …’akasema docta.

‘Sasa ndio kusema, tumuite docta wake au sio..’akasema mama.

‘Hapana mama…kwa hivi sasa mimi ndio nitakuwa docta wake,..hiyo ni dalili nzuri, na anahitajia muda, inahitajika muda mwingine abakie yeye tena na huyo msaidizi wangu, lakini ngoja kwanza…’akasema docta akitoa kipimo chake na kumpima huyo mgonjwa kwenye mapigo ya moyo..

‘Mhh, sasa yupo safi..’akasema huyo docta.

‘Kwahiyo…?’ akauliza mama

‘Hata hivyo bado anahitajia muda, wa pumzika kidogo..ila mama, usiwe na shaka, hutaamini, mwili uliokuwa mekufa ganzi, sasa umeanza kusisimuka kuashiria kuwa sasa damu , mishipa ya fahamu imeanza kufanya kazi,…akili inakwenda sawa na mwili,…kazi nzuri kijana wangu..’akasema akinipiga piga mgongoni.

‘Ina maana ni kweli..?’ nikamuuliza docta, na docta akaniashiria kwa kidole kuwa nisiseme kitu.

‘Ni kweli ndio,..hamna shaka, itabidi ufanye hivyo, tutaongea baadae..na hii hatua inaonyesha kuwa duwa zako zimefanya kazi, inatakiwa uzikazanie, lakini sio leo  sio leo muda umekwisha....’akasema docta akiendelea kumkagua-kagua huyo mgonjwa, baadae akamgeukia mama na kusema;

‘Sasa mama ngoja sisi tuondoke, tukijaliwa kesho, au kama kuna lolote litatokea basi wewe utupigia simu haraka iwezekanavyo, ningeliendelea kuwepo hapa, lakini kuna mambo mengine inabidi yakafanyike, kuna dawa natakiwa nizitafue, na huyo msaidizi wangu kuna kazi anatakiwa akaifanye hii leo, ili hili zoezo liweze kukamilika…’akasema.

‘Sawa nashukuru sana docta, sijui kama isingelikuwa wewe leo ingelikuwaje,..umekuja wakati muafaka maneno yako uliyoniambia awali yaliniingia vyema kichwani...oh, unajua docta mimi nilishapanga na mimi niishie tu…'akasema

'Hapana usfikie hapo mama, wanakutegemea sana mama...'akasema docta.

'Hivi hata nikiishi mimi nina thamani gani tena kwenye hii dunia, …kama kifungua mimba keshaondoka,...unajua najuta kile nilichokifanya, kufunga kizazi..sijui kwanini ..tulifanya hivyo,...sasa mungu ananiadhibu kwa kosa hilo,..maana  na huyu tena..sijui ...'akaguka kumuangalia binti yake kitandani.

'Hayo ulifanya kwasababu ya ushauri wa docta..na ingelikuwa ni hatari kama ungelibeaba mimba tena, hilo sio kosa lako...'akasema docta.

'Lakini haikutakiwa nifunge kizazi au sio...'akasema

'Hilo halihusiani kabisa na haya matatizo mama, wala usiumize kichwa chako...'akasema docta.

'Lakini docta, mimi nitakuwa na thamani gani tena, ni nani ataniita mama,sina kizazi tena, sina mtoto…mume ndio huyo hajiwezi, jamani,  …’akaanza kulia.

'Mama usikate tamaa mtoto unaye, huyu binti yako atapona tu...'akasema docta

'Aaah, sijui..nateseka sana,..mpaka lini jamani...'akawa analia

‘Mama usilie na wala usijilaumu sana, ..hakuna kitaharibika kwa uwezo wa mungu, kila kitu ni kwa mapenzi ya mungu, usilie sana ukafikia kukufuru, sasa hivi wewe ndio tegemeo la mtoto na mumeo, ukikata tamaa utawavunja nguvu wagonjwa wako..’akasema docta.

‘Nashukuru sana, najua huyu binti yangu akipona, baba yake pia atapona, baba yake anawapenda sana watoto wake, alipoondoka huyo wa kwanza baba yao alisema sehemu ya mwili wake imekufa..alilia sana..hata mimi sikulia kama alivyolia yeye, alimpenda sana binti yake…’akatulia.

‘Na mungu anisamehe tu, ila huyo mtu aliyetufanyia hivi,..huyo mtu aliyemfanya binti yangu hadi afikie maamuzi ya kujiua,..sijui nitamfanya nini nikimuona, sijui kama ningelikuwa na uwezo, sijui…’akatikisa kichwa.

‘Unajua baba yake amesema siku akikutana naye, sijui kama kuna kitu cha kumzuia kukifanya hicho alichodhamiria…naogopa sana, ni bora huyo mtu atokomee huko huko,….’akatulia

‘Najiuliza alikosa wapi wanawake wengine mpaka aje kwa binti yangu, anajua jinsi gani nilivyojifungua hawa watoto kwa shida, ilikuwa mimi nife, watoto wapone, nikapambana hadi ..oh… halafu hivi yeye anahisi hatazaa, au kama ana watoto anahisi watoto wake wameumbwa na jiwe…kiukweli sijui kama nitaweza kumsamehe…sijui..’akasema huyo mama kwa uchungu.

‘Mama nisikilize kwanza, maneno mengine hayafai kusema ..maana hujui ni kwanini hayo yalitokea, na mtu siku zake zikifika mengine yanakuwa ni kisingizio tu,…mama, siku ukikutana na huyo mtu cha muhimu sana ni kumsamehe..’akasema.

‘Unasema nini…hilo sikuelewi, kwanini kwanza unasema hivyo, unajua haya mateso tunayoyapata , docta, hata kama angelikuwa ni ndugu yako, mimi..siwezi kumsamehe kamwe,…’akasema

‘Mama utamsamehe tu… unajua mama ili ufanikiwe kwenye toba zako, na ili uweze kupona kwenye matatizo yako,..ukimuomba mungu pamoja na kutubu madhambi yako, lakini pia moyo wako unatakiwa uwe huru, ukubali kusamehe, na kusamehewa,…jifunze sana hilo mama yangu…’akasema docta.

‘Wewe unasema tu kwa vila hayajakukuta machungu niliyokutana nayo..hujui jinsi gani tulivyotaabika, tangia mtoto atutoke sisi tumekuwa watu wa kuteseka tu, imebidi tukimbie nyumba yetu, kwanini, nimewakosea nini hao watu jamani..basi watumalize wote ili waweze kuishi kwamani, binti yetu alikuwa hataki kabisa kukaa kwenye hiyo nyumba, anamuona dada yake kila kona ya nyumba…’akasema

‘Kwani unahisi kuna watu wanawafuatilia mama yangu, hakuna watu, hiyo ni mitihani tu ya mungu….’akasema docta.

‘Ni mitihani ndio…lakini kwanini waje kwangu, hatujawahi kuwasumbua watu, kuingilia familia zao,…na wanangu wamekuwa watu wa getini,..walikuwa hawana ubaya na watu, sasa huyo aliyejiona kidume mpaka akazama ndani ya geti langu yeye ni nani…'akasema kwa hasira.

'Ina maana alitaka kutonyesha kuwa anaweza kukifanya kile tulichokuwa tukikizuia, kutokomesha,…na sijui alifanyaje hadi, akaweza kumshawishi binti yangu, binti ambaye hakuwa na ugomvi na mtu yoyote…haya sasa kafa, lakini mbona mabalaa yanazidi kutuandama tu tumekosa nini, ndio maana nasema kuna watu hawatutaki, mpaka tufe wote…’akasema huyo mama.

‘Nikuambie kitu mama yangu, baada ya dhiki ni faraja,…mungu humpenda mja wake anayekutana na mitihani aliymkadria na bado akaendelea kusubiri, na akawa anamtegemea yeye tu, na kawem haingii kwenye shirki..

‘Mama ukipatwa na mitihani ukakimbilia kuwazania watu kuwa ndio sababu, labda wanakuloga sijui wanakufanya nini, unakuwa umeshindwa na mitihani hiyo, jua kuwa mitihani hiyo ni sehemu ya kukupima imani yako,..’akasema docta.

‘Sijasema kuwa kuna mtu anatuloga, sina imani hiyo, ila huyo aliyemfanya binti yangu akajiua, ndiye naweza hta kumuita mchawi..’akasema kwa hasira.

‘Mama nakushauri tena, achana na imani hizo,nikuambie kitu, kuanzia sasa inua mikono yako muomba mungu wako , atakusaidia,… ila kumbuka ili mola wako aweze kukusikiliza maombi yako, kwanza tanguliza toba, kwani sote sisi wanadamu ni wakosaji, hujui ni kwanini mola akakupatia mitihani yote hiyo,kwahiyo tubia kwake,.. na safisha moyo wako uwe mbali na mafunzo ya visasi,..samehe na wewe utasamehewa….’akasema docta na mama kweli akainua mikono juu.

‘EWE mola wangu nisamehe, ni mitihani tu hii, mimi ni mdhaifu tu , najua nimekosea, kwa kauli zangu nakuomba ukubali toba zangu, na unujalie binti yangu pekee aliyebakia apone, na mume wangu ..yeye ndio mimi, ukimuondoa tena duniani nitaishi na nani,..nakuomba umponyeshe mardhi yake,..tuwe naye pamoja, mimi yeye na bint yetu…aamini…’akasema

‘Hapo sasa mama tupo pamoja endelea kuomba hivyo hivyo na utakuja kuyaona maajabu ya mungu, mimi ni docta, lakini naamini sana kuwa mungu ndiye docta wa madocta, hata ufanye nini kama hutamtegemea yeye, unaweza usipone kabisa…sasa mama turuhusu tuondoke, tutarudi, na tukirudii tuna kuja kamalizia kazi kwa uwe wake mola…sawa..’akasema

‘Aamin, kwa uwezo wake mola, …’akasema huyo mama

Hapo nilipokuwa nimesimama, nikahisi kupumua kidogo, na nilipotupia macho kule
kitandani nikaona mdada akichezesha kiganja cha mkono, nikataka kumuonyesha docta, lakini docta akanishika mkono na kunivutia nje..na tulipofika nje, doctawa hapo akawa anakuja kwa haraka, na kusema;

‘Docta mzee Mashauri anakuhitajia kwa haraka…’akasema

'Mimi..kuna nini kwani...?' akauliza docta

'Twende, twende utajulia huko huko...'akasema docta akimshikilia docta mwenzake mkono.

NB: Bado tupo hospitalini, kwasababu hapo ndio kila kitu kilikuja kuwekwa sawa, na tukitoka hapo tunamaliza hiki kisa


WAZO LA LEO: Tujifunze kusamehe tukikosewa, kwani tukiwa na tabia hiyo ya kusamehe na sisi tunasamehewa tukiwakosea wenzetu na mbele ya mungu tutakuwa kwenye daraja kubwa sana la wacha mungu.
Ni mimi: emu-three

No comments :