Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, March 3, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-8


 Baba yake Soldier, akaonekana kushangaa, huku akiangalia mlangoni, na alibakia hivyo hivyo mpaka wawili hao walipoingia na kukaa kwenye kiti…

‘Oh, imekuwaje tena…?’ akauliza baba akiwaangalia wageni hao wawili…

‘Mama amekuja mwenyewe, najua sasa mambo mengi ataweza kuyaongea yeye mwenyewe yanayomuhusu, na yale yanayonihusu mimi mwenyewe nipo tayari kusema au kujibu kama ni stahiki yangu,….’akasema Dereva.

Baba mwenyenyumba, akasema ;

‘Hamuwezi kufika kwenye kikao cha watu na kuanza kuomba kuongea, hamjui kwanini tumewaita hapa, mnasikia, kwanza tulieni ili twende kiutaratibu wetu…, tulikuwa tunakuhitajia wewe dereva, kwa vile tulijua mama yako hatakuwepo…. sasa amefika…..’akasema na kumgeukia Soldier

‘Naona mwanangu wewe ndiye ulisema una maswali dhidi yake, au mama yako, tuanze na nani..kuwauliza maswali hawa wageni…?’ akauliza

‘Kwa vile mama yake dereva yupo, sioni kwanini tusimpe hiyo nafasi yeye kwanza, kwasababu hayo yaliyofikia hadi kuitwa dereva muhusika wake mkuu ni mama yake, au sio…?’ aliyeongea sasa ni yule mzee aliyekuwa kimia muda wote.

‘Haya..mama , mama..eeh, mjane, samahani kwa kulitumia jina hilo, kuna maswali tunataka kukuuliza kuhusu mwanao ,…dereva,..hebu soldier muulize swali hilo huyo mama..’alikuwa huyo mzee.

‘Ni hivi, mama, samahani lakin, usije kujiskia vibaya, kuna utata hapa, mwanao anasadikiwa, kama watu wanavyoongea kuwa huenda ana damu ya …baba hapa, nafikiri unanielewa nikisema hivyo, kuwa huenda ni ndugu yangu, sasa sisi tulitaka kusikia kauli yako wewe mwenyewe je ni kweli kuwa ni ndugu yangu au ni maneno ya watu tu ….’akasema Soldier

‘Kwahiyo mnataka kusema nini….?’ Akauliza huyo mama kwa kudakia haraka haraka

‘Tunataka uhakika, je huyu ni mtoto wa baba au ni maneno ya watu tu..kuna maana hapa, kma ni ndugu yangu, basi sisi tutamtambua hivyo, lakini kama ni maneno ya watu …tutayapuuza, lakini ni wewe unayeweza kututhibitishia hilo, ili kuondoa huo utata’akasema Soldier

‘Kwanza humo kwenye swali lako kuna shutuma,…kuwa nilitembea na baba yako…sio kweli. Huwezi kusema kuwa hujanishutumu, maana mtoto hawezi kupatikana bila ya matendo hayo, labda tusema baba yako alinibaka, haiwezekani,…kwahiyo mnanishutumu mimi kuwa ni mzinifu, kuwa nimemuiba baba yanu, na hata dada yangu hapa, ambaye tulikuwa kitu kimoja kipindi cha nyuma anakuja kunigeuka, kwakweli simini….’akasema akitikisa kichwa.

‘Unakumbuka enzi mume wangu akiwa hai, tulikuwa kama mapacha, akiondoka mume wako, basi tunakaaa pamoja, wakati mwingine tunatamani wasirudi tukae peke yetu, umeyasahau yote hayo, au ni kwa vile mimi nimekuwa mjane…jamani mimi sikuomba iwe hivyo, kwanini tusirejee hiyo hali, ..ina maana maneo ya watu yanatufanya tutengane, tusiaminiane tena, siamini ….’alipofikia hapo baba mtu akaingilia kwa kusema;

 ‘Unajua….ukweli wote nimeshawaambia hawa watu,..kuwa hayo ni maneno ya watu,..ukisikia kila neno ukaliamini unaweza kuharibu mambo mengi tu,..ujirani, urafiki wa muda mrefu, ndio hivi mnavyoona, watu walishibana sasa wanaonana maadui, kisa ni nini..majungu…..na inaumiza sana kushukiwa kitu ambacho hujakifanya, sioni kwanini turejee nyuma tena…’akasema baba

‘Lakini baba mbona unamsema shahidi, ni nini lengo la kuwaita hawa watu hapa, ni kutoa ushahidi,....au sio baba, au sio mama?’ akauliza Soldier

‘Tutapoteza muda mwingi hapa, na haya mambo yanaumiza, mnamkumbusha mwenzenu mbali..mimi sipendi, kwa hekima zangu naona tuliepushe hilo na ninajua jinsi gani ya kulimaliza hili bila kuumizana mioyo…ngoja,…’akageuka kumuangalia docta.

‘Docta..kazi yako sasa imefikia sehemu yake,..naona tusipoteze muda, tulimalize hili kitaalamu, maana docta anaweza akaondoka wakati wowote…, hawa watu wanahitajika sana, mimi nataka utusaidie jambo moja …’akasema baba

‘Kwa vipi…?’ akauliza Soldier.

‘Docta hebu waonyeshe huo ushahidi na uwaelezee ni nini maana yake…’akasema baba mtu, na docta aliyekuwa kimia, akakohoa kidogo kulainisha koo, na baadae akasema;

‘Hapa nina karatasi,…aliyonipa mzee hapa, … karatasi hii ina vipimo vya DNA, DNA, ni utaalamu wa kumtambua mzazi wa mtoto, kwa kupitia vipimo maalumu, vipimo hivi ni vya kitaalamu zaidi kwani vinatambulikana kisheria, na ukiviwakilisha mahakamani ni ushahidi tosha…’akasema akiikunjua hicho karatasi.

‘Kwanini hayo yote,  ni yanini hayo…, na nitakuwaje na uhakika na vitu kma hivyo, mtu si anaweza akajitengenezea tu…hiyo si karatasi tu jamani.’akasema mama.

‘Kwenye vipimo hivi kunakuwa na docta aliyeshughulia vipimo hivyo, kuna sahihi yake na ukitaka uhakika unaweza kumpigia simu..na kwa vile inatambulikana kisheri, docta hawezi kugushi,au kudanganya, maana upimaji wake unatoka kwenye chombo maalumu…na kama itatokea docta kagushi kitu kama hiki, anaweza kufutiwa udakitari wake, kufungwa na faini…kwahiyo hakuna mtu anaweza kugushi..kitu kama hiki…’akasema docta.

‘Waambie sasa ukweli…huyu ni docta, msomi , mtaalamu, docta bingwa,… pili huyu ni upande wenu huko,…kwa wajomba zako, hawezi kukusaliti, …nilitaka hili lifanyike ili kusiwe na dukuduku,…na hawa mnaowaita mashahidi wenu, wamekuja tu, ili kutimiza muito, lakini hivi vipimo vilitosheleza kila kitu,….sasa sijui mnataka kuwauliza nini hawa watu wawili zaidi..?’ akauliza baba.

‘Docta, una uhakika kuwa vipimo hivyo ni sahihi,..ok vinaweza kuwa ni sahihi, lakini..watu wanaweza kucukua vipimo sahihi, wakavitengeneza, sasa je una uhakika na hilo..?’ akauliza Soldier sasa akinyosha mkono kuichukua hiyo karatasi

‘Kama vinavyoonekana ….siwezi kusema moja kwa moja au kukujibu swali lako hilo, maana ni kweli, kutokana na mitandao mtu anaweza akachukua vipimo sahihi akavitengeneza na kubadili jina nk..lakini kwanini mtu afanye hivyo..na nyie ni familia moja..na lengo kubwa ni kuhakikisha kama kweli huyo ni ndugu yenu,….mimi naona ifikie mahali muaminiane, …’akasema docta.

‘Docta nakuuliza hivyo, maana hatujui, haya mambo yanaweza kubadilika huko mbele, kukatokea tatizo ikabidi tusimame mahakamani, na wewe hapa uwe ni shahidi wetu,…si unajua mambo ya sheri, wewe utasimama kama shahidi aliyethibitisha kuwa hivyo vipimo ni sahihi…’akasema Soldier.

‘Kwanini unafikia kusema hivyo, nani atasimama mahakamani, kuhusu nini,..usikuze mambo, haya mambo ni ya kifamilia tu ni madogo tu..na kama kuna lolote jingine liongelewe…., na sijui tatizo hapo ni nini, lengo ni….si nyiemlitaka kuthibitishiwa,…kuwa hayo mnayemdhania kuwa ni mwanangu je kweli ni mwanangu,..sasa huo ni utaalamu usio na shaka..kuwa huyo dereva sio mtoto wangu baba yake alishafariki….na hayo yanayoongewa na watu ni uzushi…..’akasema sasa akimuangalia mkewe.

‘Sasa docta hivyo vipimo vinasemaje..?’ akauliza yule mzee aliyekuwa kimia.

‘Vinaonyesha kuwa Dereva sio mtoto wa mzee hapa,..maana hapa inaonekana ilichukuliwa damu ya baba yake Soldier na damu ya dereva, vikaoanishwa, ikaonakena hazina nasaba…kwahiyo kutokana na vipimo hivi hapa, hilo swala la dereva, kuwa labda…linatatuliwa kwa ushahidi huu hapa…na mimi naliona hilo mlimalize kihivyo, sijui kama kuna jingine…’akasema docta.

‘Hahahaha…Docta, mimi sikupingi,..utasema labda mimi sijasoma,…lakini mimi ni mwanamke, na mke wa huyo unayemuita mzee,…nimeishi naye miaka mingi, na urafiki wetu ulianzia mbali, namfahamu kama kiganja changu cha mkononi, hanidanganyi mtu, hawa wawili wana mahusioano, hilo naliweka wazi kwenu..muamini msiamini, na huyo dereva ni mtoto wa ..…’akatulia akiashiria kwa kichwa kwa muewe.

‘Kwani, ..dada, tatizo ni nini..mimi sitaki kuingilia huko, kazi yangu ilikuwa kuelezea hivi vipimo, kama kuna mengine,…vipimo vinaonyesa wazi kuwa sio mtoto wake, ..sasa dada huwezi kupinga utaalamu,..kama wana mahusiano hilo ni jingine, ila kwa hili …..mmh, na kama kuna matatizo yenu mengine,dada mimi nawashauri mtafute njia ya kuyamaliza….ukiyaweka sana kichwani utaumia, hali yako itaathirika,….mimi naomba ruhusu niondoke..’akasema docta.

‘Ruhusa..ahsante sana..umenisaidia vya kutosha…’akasema baba yake Soldier

‘Kabla hujaondoka,..wewe upo upande wangu, kama hutojali, naomba usibirie kwanza,maana huenda tukaondoka wote…’akasema mama

‘Kwanini mama…?’ akauliza Soldier

‘Ukweli, kuhusu ukweli!…..ukweli nilioutaka haujawekwa bayana…mimi sitaamini hivyo vipimo kamwe…, nilitaka mimi watu hawa, wakubali, wakiri kosa, watubu, ..tuombeane msamaha,..mimi nilikuwa tayari tuyamalize kihivyo…..lakini sasa naona mambo yanapindishwa, kwa vile mimi sitaaminika tena, nitaonekaan mzushi,…ina haja gani ya mimi kukaa hapa..najua haya…yatakuja kuwasumbua huko mbeleni…’akasema mama

‘Sasa mama unatakaje..?’ akauliza Soldier

‘Nataka nimuulize kwanza dada yangu hapo, je una uhakika kweli hujawahi kutembea na mume wangu, nataka unijibu kutoka moyoni mwako na mungu akusikie….’akasema mama soldier akimuangalia mama yake dereva

‘Dada hayo yanakujaje, kwanini huniamini, tulishayaongea hay asana, nikakuthibitishia sasa unataka nisema nini tena, huaniamini….’akasema mama yake Dereva.

‘Jibu swali kama alivyouliza…’akasema yule mzee, na huyu mama akageuka kumuangalia mwanae, halafu akamuangalia kwa haraka baba yake Soldier, …akawa kama anasita, na baba yake Soldier akasema;

‘Sikilizeni, maswali mengine hayana maana, kutembea na mimi, ….najua una maana gani, lakini mtu hawezi kujijibia tu, kumbe ulikuwa na maana yako nyingine..ni hivi,…mimi ni binadamu, na inatokea, ..tamaa zipo nk,..unajua tena… lakini sio kwa huyu mjane, yaani mume wake kafariki na mimi nianze kuchombeza,..hapana tuombe radhi mke wangu kwa dhana hiyo mbaya…’akasema baba mtu.

‘Narudia swali langu kwa dada, je hujawahi kutembea na mume wangu..?’ akauliza mama mtu.

‘Nami nikuulize hukuwahi kutembea na mume wangu, maana kuna kipindi niliwashuku vibaya unakumbuka mpaka nikakuliza, ….’akasema na baadhi ya watu wakacheka.

‘Hebu tulimaze hilo, wewe mama Dereva jibu hilo swali…’akasema baba yake Soldier akiwa hamuangalii usoni mama yake dereva, na mama yake dereva kwa haraka akasema;

‘Sijatembea naye…’akasema huyo mama

‘Basi mimi nilitaka kusikia kauli yako hiyo,…lakini nakuuliza tena unijibu , nataka unijibu mara tatu…’akasema na kuuliza hilo swali tena, na jibu likawa ni hilo…hajatembea naye,..na mwishowe mama yake Soldier akasimama na kusema;

‘Nilijua haya mambo yatakwisha kwa amani, nilijua wenzangu watakuwa waadilifu tuyamalize kwa kuombeana samahani, maana binadamu huteleza..na mbora wa haya, ukitenda kosa ukatubu huyo ndiye muadilifu na mbele ya mungu ana daraja kubwa tu…, lakini nimegundua wenzangu sio waadilifu hawamuogopi hata mungu..kauli hiii ya kukatata mara tatu, imenifanya nifikie maamuzi magumu..naipenda sana familia yangu, lakini siwezi tena kuvumilia…..mimi naondoka zangu, narudi kwetu…’akasema

‘Mama , unasema nini tena, kwanini mama…?’ aliyesema hivyo, alikuwa mke wa Soldier akionyesha uso wa mashaka, …

‘Siwaamini tena hawa watu, nilijua watajirudi, watatubu, yaishe, lakini kama bado wanaendelea 
kunidanganya, basi, …najua yataendelea haya kisiri,…mkweli ni yule anayemuogopa mungu, sasa kama mtu hamuogopi mungu, anakubali kusema uwongo mara tatu,..hapana, hapa kuna jambo,..na mimi siwezi kuwa mjinga kihivyo, imetosha, ….kwaherini…’akasimama na kuanza kuondoka.

Mama wa dereva akawa, anatikisa kichwa kama kusikitika,…na mtoto wake alikuwa kaaingalia juu, kama anahesabu paa, huwezi kujua anawaza nini…

‘Mama kama wewe unandoka hata mimi ninaondoka..tulikubaliana mimi nivumilie haya mambo, ..tulikubaliana kuwa hili niletu sote, nikakubali yote mama,nikakubali kuyabeba yote kwa moyo mmoja, japokuwa ni mazito sana, kwa kukupenda wewe mama yangu, ….sasa kama unaondoka, mimi ninafanya nini hapa tena,…na mimi lazima niondoke tu..’akasema mke wa Soldier

‘Na wewe unaondoka kwenda wapi, hatujaongea lolote kukuhusu wewe,hayo ya baba na mama yanakuhusu nini,…na kwanini uondoke, na hata hivyo mama hataondoka, …’akasema Soldier akimuangalia mke wake.

‘Haina maana kuongea, maana kauli hizo za kutokusema ukweli, zitanirudia na mimi…watu ni wale wale, na tabia ni zile zile….kama mama anaondoka na mimi ninaondoka,..hilo halina mjadala..’akasimama mke wa Soldier kuondoka.

‘Hahaha..ajabu kabisa, mke unamkimbia mume wake…, kisa nini, maneno ya kusikia, kisa eti unahisi mimi nimetembea na mume wako…mimi, kwanini mimi, kwani hawapo wanaume wengine, na kwanini nijizalilishe hivyo,..…hahaha,…dada kuna siku nilikuambia, jitahidi kuwa jasiri, linda ndoa yako, ijenge ndoa yako, mwanamke jasiri huisimamia ndoa yake akaijenga na sio kuikimbia,…’akasema akimuangalia mwenzake.

‘Wewe unasema tu…kwa vile hayajakukuta…’akasema mama yake Soldier.

‘Mimi sasa….naamini, wewe huwezi kazi, kwanza jiulize ni kwanini mume wako atembee nje, huoni hapo kuna tatizo, kama unamshuku mume wako anatembea nje, ujue wewe mwenyewe hujiamini, una tatizo na kwa vile una tatizo unajishuku....sasa dada nakuambia hivi,…ikimbie ndoa yako na wengine wataichukua…’akasema kwa sauti ya kama kutania.

‘Wache wachukue,..kama wamechukua nikiwemo,..itawashinda nini…’akasema mama Soldier.

‘Lakini hebu jiulize, utakuwa umepata faida gani kwa kuondoka kwako, unakwenda kujitesa kwa mawazo…acha hayo dada yangu hebu rudisha moyo wako nyuma, ishi na mumeo, kumbuka tulipotoka,…’akasema mama wa Dereva na kauli hiyo ikamfanya mama wa Soldier kusimama….akageuza uso, ..machozi yalikuwa yakimtoka.

‘Baba mimi naona hapa kuna tatizo kubwa,…na, kama kuna ukweli umejificha, naomba baba uufichue, la sivyo, mimi ni mtoto wako wa kwanza, …ninaweza kuamua kufanya uchunguzi wangu, na kama nitagundua kuwa kuna jambo….’akatulia

‘Utafanya nini..?’ baba yake akamuliza akiwa kamkunjia uso.

‘Baba mimi siwezi kuona ndoa yenu ikivunjika,..na hizi kauli hapa zinanipa mashaka,…nahisi kuna tatizo, na anayejua chanzo cha tatizo hili ni wewe,…sasa kama mnataka kuishi na …’akageuza uso kumuangalia mama yake Soldier, …

‘Ehe, wewe mtoto wewe, usitake nikasema nisiyoyataka kuyasema…unasikia…wewe hujui dunia hii…unafikiri nayapenda haya…we ngoja tu…’baba mtu akawa anamnyoshea mtoto wake kidole kwa hasira na mama mtu akaona aingilie kati

‘Mwanangu acha hiyo kauli yako mkasigishana na baba yako..usifikie huko..wewe bakia na baba yako, anakuhitajia sana,…na kuhusu swala la mkeo…’ mama akawa anaongea lakini akiwa amekipa mgongo kikao…

‘Labda nisubiri tuliongelee hilo kabla sijaondoka, maana siwezi kuvumilia haya yote tena, tulikubaliana haya mambo yawe siri mimi na baba yako… nikaja kuliongea hili , mimi na mkeo, tukakubaliana naye,…iwe siri, lakini sasa siwezi kuweka siri hii tena moyoni mwangu na mtu nisiyemuamini,..baba yako simuamini tena….’akatulia.

‘Mama siri gani hiyo..ni kuhusu mtoto au,…?’ akauliza Soldier akigeuza kichwa kumuangalia mkewe, mtoto, halafu baba yake….

NB: MAMBO YALIKWENDA HIVYO


WAZO LA LEO: Suluhu ya mambo inawezekana sana kama kila mmmoja atakiri kosa lake, ili kuondoa sintofahamu ya nyuma, makosa madhambi yakitubiwa kwa ukweli na dhati, ni rahisi sana kujenga mahusiono yaliyotaka kuvunjika,..na suluhu ya kweli itapatikana, lakini kama kila mmoja atakuwa mjanja kuficha madhambi yake,..hata suluhu ikipatikana itakuwa ni ya muda tu. Tumuombe mungu atupe ujasiri wa kutoa toba ya kweli.
Ni mimi: emu-three

No comments :