Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, March 2, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-7


Soldier aliposikia mama yake akisema;

‘…sijawahi kukufumania wewe na mjane, au unataka niongee kila kitu mbele ya watoto…?
Kwa mshangao wenye kukereka, Soldier, akamkazia baba yake macho, na kumuuliza swali la haraka;

‘Ina maana baba kweli uliwahi kufaminiwa…?’ akauliza Soldier…

Baba yake akiwa na tabasamu mdomo la dharau…, akiwa hajali, akamuashiria mtoto wake kwa mkono kuwa atulie,..na Soldier akiwa katahayari akamgeukia mama yake, akitamani kusikia zaidi kuhusu hiyo kauli,..lakini mama yake alibakia kimia, na baadae baba akasema;

‘Umemaliza mpenzi…?’ mumewe akamuuliza.

Tuendelee na kisa chetu….

**************

‘Unataka nisema kila kitu …naogopa kuwa nikiongea zaidi nitaharibu mambo mengii, hata watoto hawatanielewa,…sasa ni wewe, …useme ukweli, kiri mbele ya watoto wako kuwa umefanya madhambi, kiri na mtambulishe huyo mwanao wa nje ya ndoa, na baada ya hapo mimi nitajua ni nini cha kufanya maana mimi nimevumilia na sasa naona ni bora nichukue maamuzi, najua nitaumia, nitaumiza wengi, lakini nitafanyaje….’akasema

‘Umemaliza…?’ baba akauliza sasa akiwa kakunja uso.

‘Nimemaliza nini...kama unataka nisema zaidi ..haya,…’akasema mkewe.

‘Sema, si umetaka kuongea, ongea kila kitu kilichopo moyoni mwako, sema kila mtu asikie,…uwanja ni wako sasa…’akasema akijiegemeza kwenye kitu akiweka mikono nyuma kama anaigemea.

‘Inatosha…’akasema mkewe, na baba mtu akasubiria kwa muda, halafu akasema;

‘Kwanza kabisa nakupa hongera, maana ni kwa mara ya kwanza kukusikia ukitoa siri za mumeo, ..sio kwamba nakubali kuwa hayo uliyosema ni ya ukweli,..kuwa labda ilikuwa siri yetu mimi na wewe.. hapana, ila ki kawaida mke ni msiri wa mumewe kama alivyo mume kuwa msiri kwa mkewe…najua una mengi moyoni na ndio maana leo nataka uyaongee yote, ili moyo wake uwe huru…’akageuka kwa mzee mualikwa na mzee alikuwa akitikisa kichwa kama kukubali.

‘Mke wangu, najua hayo yote yametokea wapi,…na mimi ni mtu mwenye subira sana, ule ukali wangu wa ujana, sasa haupo tena…, ndio maana nimekuwa kimia kwa muda wote huo, watu wakisema hiki na kile…wakaanza kukuambia kwa uwazi sasa na wewe ukiyapokea tu kama pakacha la taka, bila hata kufikiria, unazidi kuumia ndani kwa ndani..…lakini kila jambo lina mwisho wake….’akatulia

‘Lao nataka hiki kikao kugeuka mahakama tuulizane maswali…ukweli uwe bayana, tuyamalize haya mambo, na kile mwenye maamuzi yake, ayachukue, mimi siwezi kumzuia mtu afanye atakavyo….sasa mke wangu, nataka nikuulize maswali unijibu mbele ya kadamnasi, nilitaka hili alifanye mzee wangu hapo, lakini hapana, yeye abakie tu kama shahidi….’akasema na kumgeukia mke wake.

‘Wewe unasema uliwahi kunifumania, mimi na mke wa marehemu,…una uhakika kweli ulitukuta tukizini..sema ukweli wako, ulipofika uliniona nikitenda hilo tenda,..nataka usema kinaga ubaga ulivyonikuta…usifiche kitu….?’akasema akiuliza na mkewe akawa kama anacheka, na kutikisa kichwa akasema;.

‘Najua utajitetea, kuwa sikukuta mkiwa mnatenda hilo tendo…, lakini dalili zote za dhambi hiyo zilikuwepo,…kuzini kuna dalili zake..kukaribia zinaa ni dalili mojawapo…kiukweli mimi niliwakuta mkiwa kitandani, haya nikuulize kitanda cha watu na mke ambaye sio mkeo ..mlikuwa mkifanya nini..na ile hali uliyoonekana nayo,..jasho linakutoka,…mimi sio mtoto mdogo…’akasema mama.

‘Sawa kabisa mke wangu, ni kweli ulinikuta nikiwa kitandani, kitanda cha watu..ni kweli kabisa mtu kama mimi niingie kwenye kitanda cha watu, na mke …wa watu,…sio sahihi, ni lazima kulikuwa na jambo, ama huko kuwa na dhamira ya kuzini…au kulikuwa na jambo jingine, sasa.. wewe hujataka nikuelezee ukweli, kuhusu mimi kuwepo pale kitandani, hutaki kunipa nafasi hiyo,….’akatulia.

‘Hivi ..kweli jamani… upo kitandani na mwanamke, mnataka kufanya nini, au mlifanya nini…na mwanamke yupo…nusu uchi, ndio alikuwa kavaa khanga moja…chui na mbuzi wake zizi moja…,kwa hali kama ile..huniambii kitu…yaonyesha kabisa mlikuwa…jasho lilikuwa la nini….muda kama ule..hebu niambie..’akasema mkewe.

‘Nikuulize tena,..kunifumania huko, ni kwa kuhisi kuwa kwa vile uliniona kwenye kitanda cha watu, na mwanamke asie mke wangu,…basi wewe ukahitimisha kuwa nimetenda hilo kosa, sio kwamba ulinikuta natenda hilo kosa, nataka hapa uwe muwazi…uliniona nikizini au ni hisia zako tu…’akasema.

‘Kwahiyo wewe unataka nitamke maneno yasiyofaa mbele ya watoto, hayo niliyooangea kwangu yanatosha kuelewa jinsi gani ulivyokuwa…muhimu uwe mkweli, …maana hiyo sio mara ya kwanza, kama unataka niendelee kuongea, kuna siku..nilikutafuta ukanidanganya kuwa upo kikaoni, nikapitia kwa ..huyo …mke wa marehemu nikakuta..hapo ndio kikaoni…na hali niliyowakuta nayo.., mpo mumekaa kiti kimoja mumeshikana…kimahaba..si ndio unataka niongee hivyo…je huo mkumbatio…aah, usitake kunichefuke...’akasema mkewe akikunja uso kwa huzuni.

‘Nataka uongee kila kitu, dalili, ushahidi,..kila kitu, …ongea na jingine,..na kingine, nataka ushahidi sio kukisia,…’akasema baba na Soldier akaona aingilie kati na kusema;.

‘Baba lakini mimi sioni kuwa kuna haja ya mama kuongea yote,..hayo aliyoelezea yanatosha tu,sisi tumeshaelewa,…’akasema Soldier.

‘Umeelewa nini hapo wewe mtoto…, kuwa baba yako ni mnzizi kuwa kweli mimi natembea na huyo mama mjane,…usiparamie haya mambo kwa pupa, acha mama yako aongee kwanza, au unataka kusema nini..?’ akamuuliza mwanae.

‘Siwezi kusema hivyo baba, lakini kwa jinsi mama alivyoongea yaonyesha kuwa kuna mahusiano kati yako na mama mjane…ndivyo anavyoona yeye, sasa mimi nionavyo, kama kweli yapo, au hayapo, basi tuyamalize,..sioni haja ya kuingia kwa undani zaidi…’akasema Soldier.

‘Huna akili kabisa wewe....usikubali kuhitimisha maneno ya akina mama hivi hivi,..hawa wanapenda kuhitimisha mambo kwa haraka sana, …nikuulize wewe, huko kazini, mkiwa na sherehe, haitokeo siku ukakaa na wanawake, na hata kukumbatiana, kwa…kufurahishana tu, sio kwa mapenzi..haijatokea hivyo..utani utani tu, lakini akilini unajua wewe ni mume wa mtu unajua mipaka yako…haipo hiyo?’ baba akauliza

‘Hapana baba, sio kwa kiasi cha kuvunja miiko ya ndoa, mimi nijuavyo,….ukishaoa, kuna mambo unatakiwa uwe makini nayo…mojawapo ni hilo..kuwa mbali na yale yatakayohatarisha miiko ya ndoa…sasa mama anasema alikuona ukiwa kwenye kitanda na mke asiyekuwa wako, huo ni ushahidi mkubwa sana baba…., lakini mimi naona tusiende huko zaidi…’akasema mwanae.

‘Una uhakika na hilo unalolisema mwanangu, maana hiki kibao kitakugeukia wewe, na utatafuta sehemu ya kukimbilia usiione,..mimi ni mtu mnzima, nina akili zangu, na kwa utu uzima huu ninaweza kufanya jambo kwa minajili fulani..kihekima tu,…naweza kufanya mambo kwa ajili ya kumliwaza mtu…na kumfanya aondokane na huzuni,..na ndivyo nilivyofanya kwa mke wa marehemu…’akasema

‘Labda nikiri kuwa ucheshi wangu wa kupindukia,..kuliwaza huko, kwa kupitiliza, labda ndio mnaona ni kosa, lakini hayo nimekuwaq nikiyafanya hata hapa nyumbani…, wanakuja shemeji zangu tunataniana na tunafika sehemu tunakumbatiana kimzaha, mke wangu,… my love…, ni jambo tu la kufurahishana lakini mimi nina akili zangu timamu,….siwezi kuvuka mipaka ya ndoa..’akasema

‘Kwahiyo kwa kauli yako hiyo baba, unamuhakikishia mama kuwa hukuwahi kwenda zaidi ya hayo ya kukumbatiana,…ni ucheshi wako tu...tunakuonaga hata hapa nyumbani,..ndio, lakini ..baba hilo la kuingia hadi kukaa kitanda cha mke wa mtu, asiye kuwa mke wako, hata kama ingelikuwa ni wewe baba, ungelimuona mama kakaa na mwanaume mwingine kitandani, sidhani kama ungelifurahia, ni lazima ungelihisi vibaya najua huenda hukuwahi kufanya tendo, labda ulikuwa na sababu ya msingi, sasa mimi nionavyo, tuyaache hayo….’akasema na baba yake akawa kakunja uso kwa hasira.

‘Unasema tuyaache wakati hata nyie mumeshanihisi vibaya, haya hayaachwi, mpaka ukweli ubainike, nataka…ushahidi, nataka ukweli…unasikia, mama yako abainishe..kwanini nisingiziwe,…kwanini, sasa mwambie mama yako atoe ushahidi,….vinginevyo…’mzee sasa akawa anakuja juu.

‘Samahani baba nakuuliza haya nikitaka usahihi…, ili mama asiendelee kuteseka, ajue kuwa ulikosea na hutarudia tena, …kwanini baba usikiri tu kuwa hapo ulivuka mpaka na umekosea..,..au hata kama hukufanya, ukisema nimekosa samahani mke wangu sitarudia, tena,..yaishe, ….si ndio hivyo mama…?’ akauliza.

‘Hata kama hakufanya..hahaha…mungu hamfichi mnafiki…alifanya kwa siri lakini ukweli umemuanika…ukweli upo ….sasa sijui anataka kusema nini…’akasema mkewe

‘Hahaha, wewe mtoto wewe…ngoja ya kwako yanakuja….na nikuambie kitu ili mtu moyo wake uwe na amani , inahitajika ayaonge yote yanayomkera….asifiche, mimi nipo tayari, kama kweli nimekosea nitasema ..lakini hilo la kusingiziwa,..sipo tayari…na umemsikia, kasema anao ukweli bayana, nataka usikiwe mbele ya hadhara hii….’akasema.

‘Lakini mama kasema kakuona ukiwa kitandani..hiyo hali inamtesa, huo ni ushaidi au sio baba, au sio mama, narudia baba kukuuliza jemfano ungemkuta mama yupo na mwanaume kama alivyokukuta wewe, ungelifikiriaje,...hebu chukulia hapo baba..inauma kwa kweli baba….’akasema Soldier

‘Nakuelewa sana..ila nikuambia ukweli mwanangu..maana mimi nimekuwa jeshini, hunidanganyi kitu, nimekuwa kiongozi, na unafahamu kabisa jeshini kulivyo, …wakati mwingine inabidi utende jambo kwa nia ya kumaliza tatizo....haya ya kwangu ninayoshukiwa nayo hapa ni dhana tu,  ni madogo…hunidanganyi kitu mwanangu, kuwa huko ulipokuwa ulikuwa humgusi mwanamke, huchezi mziki, hamkumbatiani…hamfikii hata hatua ya labda ukaenda ukakaa kitandani kwa wanawake, kwasababu fulani, mwanamke anaumwa, ana tatizo, je huwezi kwenda kukaa kitandani kwake….wewe usitake nikuumbue...’akasema baba

‘Baba..huko ni kambini, na mnapokuwa huko mnakuwa wakati mwingine kama wanafunzi, mnaweza mkafanya hivyo,…lakini hayo ni ya huko, yanaishia huko huko…. sasa hivi…tunazungumzia mambo ya uraiani…mazingira ya kule ni tofauti na ya hapa baba, tukitaka tufanye yale ya kule huku,..tutakosana na familia zetu, ndoa zitalega lega, …na kama ulivyosema awali, nia hapa ni kuliweka hili bayana, halafu tuombeane msamaha yaishe,…mimi ndivyo nionavyo, …’akasema

‘Niombe msamaha kwa kosa gani…sasa nasema hivi mimi ninataka mama yako abainishe hayo makosa yangu awe muwazi..anaogopa nini sasa?’ akauliza akimuangalia mzee aliyekuwepo hapo, huyo mzee alikuwa kimia tu.

‘Baba …mimi naona tusiende mbali zaidi, mkachafuana zaidi na zaidi, tusiende huko,…mama keshaeleza ni kwanini anakushuku ni kwanini hali imefikia hapo,..najua kwa umri mliofikia hayo yaliyowahi kutokea huko hayawezi kutokea tena, au sio, tuombeane msamaha yaishe….’akasema Soldier.

‘Mwanangu.., utakuja kuona kuwa sijafanya kitu..nakuelezea unielewe…mimi sijafanya kitu cha kuharibu ndoa yangu, mimi ninafahamu maana ya ndoa kuliko wewe,..mimi ni kiongozi najua jinsi gani ya kusuluhisha haya mambo, ninakutana na kesi hizi kila siku….ninajua, …nianze vipi na nitamaliza vipi, hii ni kesi yangu,niachie …’ akasema

‘Baba nakuelewa, lakini tupo hapa ili tusaidiane kama familia, mimi ni mtoto wenu mkubwa, haya niliyoyakuta hapa yamenipa wakati mgumu sana,..kwanza kuhusu nyie wazazi wangu, ..imefikia hatua mama sasa anaathirika, shinikizo la damu…ni hatari, kisa ni hayo mambo, tufike mahali sasa tymalize, mama awe huru, asiwe na mashaka tena, yeye ni binadamu atasamehe yaishe au sio mama…’akasema

‘Wewe tulia, haya yataisha yote hii leo….mimi ni askari nimeanzia chini hadi juu…sio kwa kupewa pewa cheo tu, ujue, mimi nilisota ile mbaya, najua watu,..naufahamu vyema uongozi wa kuongoza watu,..nafahamu tabia za watu, …. ..ndio maana nataka mama yako anailewe, twende hatua kwa hatua, athibitishe kwa ushahidi,….’akatulia

‘Aaah, mimi sitaki kuongea tena….basi inatosha,…basi..’akasema mkewe akitaka kuondoka.

‘Mke wangu,..unataka kwenda wapi, hapa ndio sehemu ya kuyamaliza haya,… mimi ninachotaka ni wewe utoe ushahidi ulivyonifumania, na kufumaniwa maana yake umenikuta natenda….tendo…sio kudhania dhania tu…haya hilo la kutenda tendo, halipo,…aseme ukweli wake..hilo halipo na halikufanyka…ni dhana tu…au ..sema mwenyewe, je aliwahi kuniona nikizini....’akasema.

‘Nimeshakuambia…sitaki kuongea mambo mengine mabaya mbele ya watoto, nilichoelezea hapa kila mtu anaweza kuona ulivyo, kamwe sikupenda kuyaongea haya unanifahamu nilivyo,…na kuzini unakofikiria wewe…ni kupi, sio lazima mkutwe mpo kwenye tendo,..dhamira,…kukaribia, kushikana yote hayo ni kuzini tu….’akatulia na mumewe akawa anamuangalia, na mkewe alipoona bado anasikilizwa akaendelea kusema;

‘Unaonaeeh….kwahiyo wacheza mziki wote, wanacheza jukwaani wanashikana, au waigizaji wote, wanaigiza …wanazini…..kifupi huna hoja hapo, hujawahi na hutwahi kuniona ni kizini….nataka hili libanikie na liwe wazi kwenu, hizo shutuma za mama yenu sio kweli….’akasema

‘Haingeliwezekana, mimi nije nikukute bayana, …maana sikujua,..na sikuwa na lengo la kukufuatilia, hiyo ilitokea mimi nimefika tu, kwa jambo jingine nikwafuma,…sasa ukijitetea, ukapindisha maneno, ni upendavyo wewe, ila kwa kifupi .wewe ulivuka mipaka ya ndoa, lakini hata hivyo mimi nilikuvumilia,…kwa vile unajifanya mcheshi, ushike-shike wanawake za watu , tena wakati mwingine mbele yangu,mimi nikuangalie tu, je mimi nikifanya hivyo utafurahi…mbona mimi unanikataza hata kukaa karibu na mwanume….hivi nyie mnafikiria sisi wanawake tuna miyo ya chuma, hatuumii….’akasema mama kwa huzuni.

‘Pole sana mke wangu..sikujua kuwa nakumiza, lakini ndivyo nilivyo..ila nasema tena, hilo la kuzini , hilo la kufamaniwa halipo, sijawahi kufanya hivyo..na mama yenu hana uhakika na hilo kama ana ushahidi mwingine aseme nataka kwanza hilo liwe bayana, ana ushahid gani kuwa mimi nimezini na huyo mjane, autoe, na akiutoa, hapo nitaweza kukiri kosa langu…’akasema

‘Unataka ushaidi wa vipi, kwanza hilo ulilofanya hujakiri kuwa ni kosa, wewe unaona ni jambo la kawaida tu…, …au wewe unataka tuonyeshe matokea ya dhambi zako,....na huyo mtoto wa nje sio ushahidi, kila mtu anafahamu kuwa huyo mtoto ni wako ..au utamkana kuwa sio mtoto wako…’akasema mkewe

‘Mtoto yupi huyo ?,….huyo dereva..? Lakini hilo si nimeshalieliezea,..huyo sio mtoto wangu, anafanana na mimi kwa vile baba yake alikuwa akifanana na mimi…hilo lipo wazi,…. Sawa…sasa ni hivi, maana tulikuwa tunakwenda huko,…, kwa vile umelitaja hilo, sasa mimi nataka kukuthibitishia kuwa huyo sio mtoto wangu, nitamuita hapa huyo kijana,..na kama mama yake angelikuja pia ingelikuwa ni bora, nilitaka wote wawili waje watamke hapa bayana je huyo mtoto ni wangu...’ akasema

‘Hata wakija si umeshaongea nao, umeshawapanga wasema hivi…maana wote mpo kitu kimoja, huyo dereva awali alikuwa anakubali….,sasa ulivyomuweka sawa anakataa..na huyo mwanamke wako akija hapa hawezi kusema ukweli, kwasababu ni mpenzi wako…atakusaliti vipi…na nijuavyo mimi, mwongo ataumbuka tu,…anajua hilo ndio maana kaogopa kuja..’akasema mkewe.

‘Kama ni mtoto wangu kwanini anikane, …atajiharibia yeye mwenyewe, ngoja aje, tumuulize, asema ukweli wake,..je mimi ni baba yake, je   mama yake anasemaje kuhusu hilo,..au unaogopa uongo wako utakuumbua wewe mwenyewe,..tatizo lako ni upole na wivu, hakuna jingine…muiteni hapa huypoo dereva yupo nje, aingie…’akasema baba

‘Haina haja….umeshamkataza asisema, …kasema yeye mwenyewe kuwa wewe umemkataza ….sasa hata akija atasema nini , na mama yake niliwahi kumuuliza, majibu yake ya dharau tu..ananidharau kwa vile mnajuana…..’akasema mkewe, na Soldier akaingilia kati na kusema;

‘Mama tafadhali, mimi naona huyo dereva aje hapa, tumuhoji, tusikie na yeye kauli yake, anavyosikia, na je kweli yeye anakubali kuwa huyu ni baba yake au la, na mama yake anasemaje, na tutamwambia hapa ndio suluhu…, akikataa kuwa huyu sio baba yake, ndio imetoka hivyo…, isije ikatokea …hatuombei mabaya, aje tena akisema mimi ni mtoto wa familia hii…hilo tuliweke hapa bayana , mbele ya baba..na hata hivyo hata mimi nina maswali ya kumuuliza huyo mtu…’akasema Soldier,

‘Sawa …muiteni dereva aje, …’akasema baba mtu kwa sauti ya mashaka mashaka.

Dereva akaingia…na ajabu akawa kafuatana na mtu mwingine,…..!

NB: Haya tuendelee kidogo, au…


WAZO LA LEO: Unapofanya jambo, ambalo huenda linaweza kumuathiri mwingine, kabla ya kulifanya hebu kwanza jiulize je nikifanyiwa mimi nitalipokeaje..je nio tayari kuliona , au kulipokea akinifanyia mwingine, kama utaona haupo tayari, basi liache…ukumbuke akiumiza mwenzako moyoni na wewe utakuja kuumizwa hivyo hivyo,.. 
Ni mimi: emu-three

No comments :