Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, March 1, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-6

  

 Soldier alizindukana kutoka kwenye usingizi baada ya kusikia kilio, kilikuwa kilia cha mtoto, kwa haraka akainuka kitandani, na pembeni yake akamuona mtoto kalazwa karibu yake, akajua huyo ni mkewe kafanya hivyo, akamsogelea mtoto na kumweka vyema, alikuwa kajisaidia kwa hiyo alihitajika kubadlishwa nepi…, akawa anataka kumbadili lakini nguo za kumbadili zilikuwa hazipo, akataka kumuita mkewe kwa sauti, lakini akaona amchukue mtoto atoke naye nje.

Akambeba vyema huku anamkagua,..anamuangalia usoni,… mtoto alikuwa kanyamaza kimia,..alikuwa mtoto mnzuri mwenye afya tele tu.., na kila akimuangalia usoni, anaiona sura ya dereva,…na …ndio yawezekana kuwa anafanana na baba yake, hapana…ndio…akawa anajiuliza huku anatembea na kila akijiuliza anahisii mwili unamchemka…damu insisimuka, hasira…, kwa haraka akafungua mlango kutoka nje ya chumba cha kulala, na mara akamuona mtu kasimama mlangoni, alikuwa ni yule binti Yaya, akiwa amesimama, hapo malngoni kama anasubiria…

‘Oh, kumbe upo hapa, mtoto analia na mama yake hayupo, kaenda wapi,..?’ akauliza na yule Yaya, akaonyeshea kwa kidole, kuelekea jikoni.

‘Kwani wewe huwezi kuongea?’ akamuliza huyo binti, kwa mshangao, na huyo binti hakusema kitu akawa anataka kumchukua mtoto, huku kainamisha kichwa chini, na Soldier akamkabidhi huyo yaya mtoto na huyo yaya kwa haraka akaondoka, na muda wote alikuwa anatizama chini.

‘Huyu binti vipi, sijui hawezi kuongea na ana aibu kupitiliza,…’ akasema sasa akitembea kuelekea mlango wa kutokea nje, alitaka akapate upepo wa nje kidogo na ikibidi achukue na mazoezi, …alipofika nje, akaona gari likiingia hapo eneo la nyumba…, alikuwa ni yule dereva.

Moyoni akasema, sasa nitaongea na huyu jamaa nipate ukweli fulani,…akawa analisogelea gari na kwa muda huo dereva naye alikuwa akifungua mlango wa gari na kutoka nje..

‘Za asubuhi mkuu, naona kidogo umelala, hivi huko kweli mlikuwa mnapata muda wa kulala..?’ akauliza

‘Kuna muda unapata , kuna muda unalala kwa kimang’amu ng’amu..ndio hivyo..vipi umefika asubuhi hii kuna abiria hapa anatoka..?’ akauliza

‘Aaah,…nimeitikia wito wa baba yako, alinipigia simu kuwa leo niwepo hapa nyumbani ana mazungumzo na mimi….na alitaka nije na mama, lakini mama kasema hajisikii vyema….kwahiyo, nimetii wito, nitamuwakilisha na mama, sijui kuna nini la zaidi…’akasema.

‘Ok..karibu,…lakini bado naona kama hawajaandaa vyema huko ndani, tunaweza kuongea kidogo..?’ akasema.

‘Bila shaka,..’dereva akasema na wakasogea kwenye benchi lililopo chini ya miti, wakakaa, na aliyeanza kuongea alikuwa ni dereva.

‘Unajua kazi zangu hizi ni za kuitwa itwa…sasa sijui mzee kaniitia nini, na muda huu natakiwa kuwachukua wanafunzi fulani, si unajua tena kazi zangu hizi,…au labda anataka kutoka, lakini alisema ana mazungumzo na mimi,…..’akasema.

‘Ok, mtaongea tu, hamna shida, ila mimi kitu nataka kukuuliza… kidogo, hebu niambie…wewe na baba yangu, mpoje, maana nimesikia watu wakiongea, hili na lile…. hata kwenye kikao..nilisiki amzeee akiligusia japokuwa hakuweza kusema ukweli…, kuna ukweli wowote kuwa labda wewe na mimi  ni ndugu moja..?’ akauliza.

‘Mhh…mtu wa kukujibu hilo ni baba yako,..ila labda, nikuambie jambo,…hivi hujawahi kuona watu wanafanana lakini hawana hata damu ya udugu…?’akauliza.

‘Wapo, lakini usikwepe ukweli, kama upo ukweli huo..na mimi nastahiki kufahamu au sio, kuna leo na kesho, baba yupo ..na…unajua tena…sasa kama upo niambie tu, hakuna shida, au sio..?’ akauliza.

‘Sijui lolote kwakweli,..na ….unajua nikuambie kitu, kuna mengi yanasemwa,..hata kuhusu mtoto wako, …wengine wanasem nafanana na yeye, haya …hilo la mimi kufanana na baba yako ndio limeenea sana, lakini ….mimi siwezi kusema lolote kuhus hilo, ili hali msemajei yupo…. muulize baba yako…’akasema.

‘Kwanini wewe hutaki kuniambia ukweli?’ akauliza.

‘Kwasababu baba yako …na hata mama yako wamesema hivyo…’akasema.

‘Kuwa usiniambie ukweli..kwanini?’ akauliza akimuangalia dereva na dereva akawa anatabasamu tu, halafu akasema;

‘Sikiliza Soldier, …kwani kwa mfano…mimi nikiwa,… nasemea kwa mfano tu maana …atakuambia baba yako yote, kwa mfano,…,  mimi nikiwa ni  ndugu yako kuna ubaya..?’ akauliza.

‘Swali langu hujalijibu,..je wewe ni ndugu yangu, kama watu wanavyosema au la…?’ akauliza, sasa kwa ukali, na kabla dereva hajasema kitu, mara sauti ya kuitwa ndani ikasikika,..

‘Mnaitwa ndani, mzee anawasubiria…’ilikuwa suti ya ndugu yao na mazungumzo yakakatizwa..

‘Ngoja niwahi maana hapa nitachelewa..’dereva akasimama na kuanza kuondoka kwa haraka, na Soldier akamfuatia kwa kwa nyuma akiongea…

‘Nitaongea na wewe baadae, kwani sio swali hilo tu, nina maswali mengine muhimu dhidi yako…, nataka unijibu wewe kwa kinywa chako, maana nafahamu unaufahamu ukweli ulivyo,…nitamuuliza baba, lakini kauli yako itanifanya niwe na amani zaidi, na umesema wewe mwenyewe kwa kauli yako, kuwa unafanana na mtoto, iweje ufanane na mtoto wangu..., sasa nataka ukweli kutoka kwako, la sivyo…sitaogopa kunyongwa unielewe, sitanii…?’akasema Soldiera wakitembea kwenda ndani.

‘Usijali…hilo…hahaha, ina maana na wewe unaamini hayo,…acha hizo bro,….ngoja, naona mzee huyo, ......’akasema na mara baba wa Soldier akatokea na kumuita Dereva waongee pembeni, na Soldier yeye akaingia ndani.

********
Chumba cha maongezi kilikuwa kimeshachangamka,…Soldier alipitisha macho kwa haraka, …yupo mama, anakunywa chai akiwa kimia, yupo mke wake, anacheza na mtoto wapo ndugu zake wengine wa familia,..na alikuwepo mzee mwingine, ambaye ni mwanafamilia pia, na ….yupo mgeni , anamfahamu ni docta. Baba alikuwa bado nje akiongea na dereva.

Soldier, alisalimiana na wengine akamsogelea mama yake wakasalimiana na akamuuliza vipi khli yake, mama yake akamuambia leo hajambo, hana shida..na akasogea kwenye kiti na kukaa, alikaa karibu na docta, akawa anaongea naye;

‘Ulikuja kwa ajili ya mama..?’ akamuuliza

‘Hapana mzee wako aliniita tu,..kasema kuna jambo anataka nimsaidie... na kwa vile nimefika hapa, nikasikia mama yako anaumwa, kwahiyo nikajaribu kumsikiliza ili nijue tatizo nini hasa,….na..mama haumwi kihivyo..ila mawazo,..unajua mawazo yanaweza kukufanya ukawa mgonjwa, nimemwambia ajaribu kulikwepa hilo, kwani athari zake zinaweza kuwa kubwa zaidi..’akasema.

‘Docta nikuambie ukweli, mimi sijui kabisa kinacheondelea hapa nyumbani.., lakini kwa vile nimefika…, nina imani tutayamaliza tu, ..na…’kabla hajaendelea baba yake akaingia…dereva hakuonekana, na Soldier akawa na wasiwasi kuwa huyo jamaa anaweza kuondoka. Akataka kusimama ili akamzuie lakini baba yake akaanza kuongea…

‘Jamani tuna maongezi kidogo..tulia bwana mdogo unataka kwenda wapi…..’akasema akimnyoshea mkono Soldier.

‘Mimi nimeona…, ni muhimu sana tuyaongee haya kama familia,..mtaona kuna watu wengine wasio kuwa wanafamilia kwa ukaribu wake…, lakini wana udugu fulani …mnamuona docta hapo, huyo ni mtoto wa wajomba, anatokea familia ya mke wangu, kwahiyo ni ndugu kwa namna fulani, ila yeye nimemuita hapa kwa jambo moja muhimu sana…’akatulia.

‘Kuna tatizo lipo hapa nyumbani,…lilikuwa tatizo dogo tu, la mimi na ..mke wangu, lakini sasa naona limekwenda mbali, eeh, ni sawa, lakini kwanini iwe hivyo,..’akatulia akiinama kidogo.

‘Sitaki kumlaumu mtu,..na ..sio kwamba nashitaki, mimi siwezi kushitakia jambo kama hili kwa watoto,..ila nataka niweke wazi, atakayeumia aumie..., mimi ni askari nimepambana na matatizo makubwa sana tu,…ila mimi ni mtu mnzima na ufahamu wangu na umri wangu unanifanya nijishushe,..na najua nifanye nini ili kuyaweka haya mambo sawa kwa wakati muafaka!’

‘Mama yako Soldier,  sasa hivi anaumwa, hajijui tu,..na tatizo lake kubwa kutokuniamni…sijui kwanini haniamini na umri huu…mimi sio kijana tena, haya anasema nilikuw amsiri amekuja kugundua mwenyewe madhambi niliyoyafanya huko nyuma,…lakini madhambi gani..hana ushahidi, anahisi tu,…sasa mimi sitaki haya mambo yazidi kukua, maana mwisho wa siku nitakuja kulaumiwa mimi….nataka niliweke hili wazo mbele yenu wote...’akatulia

‘Soldier, wewe ni mtoto wa kiume, mambo kama haya yapo na yaweza kutokea kwenye familia yako, nataka ujue kuwa,…mwanaume sio kuvaa suruwali tu,mwanaume ni kupambana na mambo kama haya,..najua wewe umeiva na sina shaka na wewe..ila ulivyofika kutoka huko …naona ulitaka kuingia kichwa kichwa,..tulia...bwana mdogo, nilkuambia mapema kila kitu nitakiweka sawa, huniamini mimi baba yako..?’ akawa anauliza ,na alipoona mwanae anataka kuongea.

‘Baba sijasema sikuamini…ila....’akajitetea.

‘Ninajua ni kwanini…mama ni mama tu,..kila mtoto atamuonea mama yake huruma…si unajua tena, hapo baba anaonekana hana maana,..lakini mnashindwa kufahamu dhima ya baba, baba wa kweli ni yule anayeangalia mambo, bila kujali maneno ya watu,..muhimu kwake ni kuhakikisha haki inatendeka, msimamo wa familia yake unakuwa hauyumbi, ushirikiane wake na majirani pia nao una umuhimu wake, ubinadamu nk...sasa niwaambie ukweli, maana mimi siwezi kudekeza mtu hata siku moja hiyo ndio silka yangu…’akakunja uso.

Kuna tatizo lilianza zamani kidogo,…kabla baba yake dereva hajafariki, baba yake dereva alikuwa rafiki yangu mkubwa sana…na urafiki wetu ulifikia mbali, kusaidiana kifamilia…ilikuwa mimi nikisafiri au yeye, mmoja anachukua jukumu la kulea familia ya mwenzake..kweli si kweli..?’ akauliza akimgeukia mkewe.

‘Ongea tatizo…’akasema mkewe

‘Ndio nalifichua hivyo,..lazima wanafamalia wafahamu chanzo ni nini,  choko choko, ya kutoakuaminiana imetokea wapi…

'Sawa ongea na mimi uje unipe nafasi hiyo nieleze ni kwanini sikuamini...'akasema mkewe.

'Sijamaliza lakini kuongea, na wala sijakupa nafasi ya kuongea...'akasema baba

'Samahani endelea..'akasema mkewe

'Mambo yalianza kuharibika pale rafiki yangu alipofarikia,…hebu niwaulize kwa hali kama hiyo mimi kama rafiki yake marehemu ningefanya nini…nimuache yule mjane ateseke tu, hebu fikrieni hata ingelitokea jwangu angemuacha mke wangu ateseke tu, asiwe karibu naye, sis tulishakuwa ndugu, wa shida na raha...kwahiyo ilikuwa ni wajibu wangu kumsaidia yule mama, kwa kumliwaza, kumfanya ajione bado yupo na sisi, sasa mwenzangu hilo halitaki, kwanini nakuwa karibu sana na mke wa marehemu, kwanini..ikazaa menginena kusahau ukweli halisi,…’ akasema

‘Hujasema tatizo bado hapo, …’akasema mkewe.

‘Tatizo kwako eti ni kwa vile dereva anafanana na mimi, au sio, na kwa vile mimi nilikuwa karibu na mke wa marehemu kwahiyo huenda nilitembea naye au sio, kwahiyo kuzaliwa mtoto anayefanana na mimi ndio ushahidi wako kuwa mimi nina madhambi, ni msaliti wa ndoa yangu, au sio..ushahidi wako ni huyo mtoto, au sio....?' akauliza

'Elezea bayana, usizunguke ...maana utapoteza muda na ukweli...'akasema mama

'Si ndio hivyo naelezea,..kuwa ni kwanini nimekuwa karibu na mke wa marehemu,.na unakumbuka kabisa mimi na marehemu tulikuwa tunafanana sana,...kama mapacha..sasa kuzaa mtoto anayefanana na mimi sio ajabu…’akasema.

‘Kwahiyo unapinga kuwa dereva sio mtoto wako uliyezaa na huyo mjane...unaikataa damu yako, mimi nilishakuambia ukubali ukweli, na umtambulishe huyo mtoto kwa familia kuwa huyu ni damu yako, basi...lakini hutaki, ...kwanini, ...?' akauliza mkewe

'Huko tutafika...usiwe na shaka...'akasema mkewe

'Nijibu kwanza hilo swali langu je dereva sio mwanao wa nje ya ndoa...?' akauliza mkewe

'Kwanini unishuku hivyo, ..huniamini mimi, haya hata kama huniamini mimi je humuamini mke wa marehemu...mke wa marehemu alikuambia nini...?' akauliza baba,

'Ndio sikuamini,..kama sikuamini wewe, hata yeye nitamuaminije,...wakati nina ushahidi kamili kuwa hauaminiki ukiwa na yeye, lenu ni moja...'akasema mama.

'Kwa vipi?' akauliza baba

'Kwasbabu  niliwahi kuwafumania ..wewe na mjane, au unataka niongee kila kitu mbele ya watoto…?’ akauliza mkewe, na Soldier aliposikia hivyo akatoa macho kumuangalia baba yae, akauliza

‘Ni kweli baba kuwa uliwahi kufumania na mke wa marehemu…?’ akauliza Soldier, na baba yake akaashiria kwa mkono kumwambia mwanae atulie..

NB: Tutaendelea…


WAZO LA LEO: Uongozi mnzuri huanzia ndani ya familia yako. Kama ilivyo jamii, jamii nzuri huanzia ndani ya familia, jinsi familia zitakavyojengwa na kulelewa vyema ndivyo jamii itakavyoweza kuwa na masikilizano mema na maendeleo mazuri. Ndio maana ni muhimu sana kuangalia familia kwanza ili kuweza kuwa na jamii njema , na familia njema huanzia kwa baba na mama, kama wana ndoa hawa hawatakuwa wema, wenye maadili mema,..muelekeo wake ni kujenga familia mbovu ambayo itaunda jamii mbovu na hata uongozi wake utakuwa mbovu…ni hayo kwa leo.Ni mimi: emu-three

No comments :