Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, March 30, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-30

                          
Wakati anaongea hivyo Soldier akachukua simu yake na kupiga namba, akasogea pembeni kidogo halafu akiwa anaongea na simu, na baadaye akarudi na kusema;

‘Haya elezea…tusipoteze muda, nimeshapiga simu polisi, wakati wowote polisi wanaweza kufika hapa…’akasema Soldier

‘Polisi wa nini, Soldier sasa unataka kuharibu…?’ akauliza shemeji sasa akiangalia mlangoni, yaonyesha huyu jamaa alikuwa na mashaka fulani.

‘Waache waje….’akasema huyo mdada aliyekuwa kajifunika usoni, na kuwa tayari kuanza kuelezea kisa cha maisha yake ambacho ndio chanzo cha kupata huyo mtoto ambaye hajulikani baba yake ni nani

Tuendelee na kisa chetu ….

*****************


 ‘Mimi nimezaliwa hapa hapa nchini, na mapacha mwenzangu huyu hapa mnayemuita Yaya,  mama yetu ni mzaliwa wa nchi hiyo yenye machafuko, machafuko yanayotokana na kundi la Waasi ambao wanapingana na serikali kwa kutafuta matakwa yao yasikilizwe…ni mambo ya kisiasa zaidi.

Baba yeye ni Mtanzania halisi, ila hutaamini hana ndugu, sijui ilikuwaje, au ni yeye tu hajapenda kuonyesha ndugu zake hadi leo sijawahi kukutana nao.., sijawahi kumsikia baba akisema ana ndugu zake mahali, hata ukimuuliza anasema yeye hana ndugu ,anasema wazazi wake walifariki wote akabakia yeye mwenyewe akilelewa kama mtoto wa mitaani

'Siwezi kuwahadithia kisa cha maisha yangu maana kinasikitisha sana, nashukuru sana nilikuja kukutana na mama yenu, na ikawa mwanzo wa kubadilisha maisha yangu yakawa kama hivi...'alisema baba yangu siku moja tukimuuliza wapi asili yetu.

Wazazi wangu walihamia kwenye hiyo nchi katika kutafuta maisha yao binafsi , kama nilivyosema awali, baba alisema hakuwa na ndugu, kwahiyo mke ndiye aliyemvuta baba kwenda kuishi huko anapotokea mama, na kipindi hicho ilikuwa hakuna machafuko, watu walikuwa wakiishi kwa furaha na amani, sisi kipindi hicho tukiwa wadogo sana….’ Mdada akawa anaendelea kuelezea.

Wote walikuwa kimia, wakitaka kujua huyu mdada ni nani katokea wapi na huyo mtoto alimzaa na nani,na kwanini iwe siri kiasi hicho...!

Maisha ya huko awali yalikuwa mazuri tu, kwani tulikuwa miongoni mwa familia zilizobarikiwa, nyumba nzuri na wazazi wangu walikuwa na gari lao..., tulikuwa watoto wa getini,…na kwa umaarufu huo, baba alijulikana haraka kwa watu…japokuwa kujulikana huko pia kulizaa maadui, hakuna aliyependa maendeleo ya wengine, kwani wengi wa wakazi wa kule walikuwa na maisha duni sana!

Machafuko yalipoanza, wakwanza kupata athari hizo ni wale wenye uwezo, waasi hao walikuwa wanakuja kuiba, kuharibu mali za watu, na hawakusita hata kuvunja nyumba za watu, na kwa kitendo hicho walitufanya na sisi tubakie hatuna nyumba, wala maisha mazuri tena….

Baba alipanga turudi huku nchini, lakini angelipitia wapi,na ukumbuke kuwa huku nyumbani hakuwa na ndugu hana makazi halisi, na huko anapotokea mama ndipo walipokuwa wamewekeza kila kitu chao,...na kutokana na machafuko hayo, kupata hasara, wananchi wengi waliilalamikia serikali, wakahitajia namna ya kufidiwa na serikali , waliahidiwa hivyo, kwahiyo ule muda wa kusubiria ndio yakatukuta makubwa zaidi.

Kipindi machafuko yanaanza mimi nilishamaliza masomo yangu ya unesi, nikawa natumikia taifa, kwani niliajiriwa kwenye moja ya hospitali za serikali, nilikuwa nalipwa mshahara mdogo tu, lakini nilirizika nao, maana kazi yenye niliipenda kutoka moyoni , kusaidia watu hasa wagonjwa na akina mama.

Sasa machafuko yalipoanza familia ikasambaratika, maana ilitokea siku moja tukavamiwa, na watu wakatekwa, wengine waka uwawa, kubakwa, na mateso mbali mbali, mpaka serikali ilipokuja kugomboa eneo hilo, athari kubwa ilishatokea,..tukawa hatujuani kila mtu aliyeweza kuokoa roho yake alikimbilia kivyake.

Mdogo wangu yeye alichukuliwa na gari la msaada tu, akajikuta yupo nchi ya jirani, ambapo wengi walikimbilia huko kama wakimbizi, wazazi wangu walichukuliwa sehemu nyingine hata hatukuelewa ni wapi, tulikuja kujua baadae kabisa, nikiwa na mimi nipo kambi ya wakimbizi.

Mimi kwa vile nilikuwa nesi, nilichukuliwa na serikali kuhudumia walioathirika na machafuko hayo, tukawa tunatembezwa huku na kule, hadi walipofika vikosi vya kusaidia, kutoka nchi mbali mbali. Na kuna muda kulikuwa  na amani, kwani waasi hao walikimbilia maporini.

Ikawa wanajitokeza mara moja moja, na kuvamia kijiji hiki na kile, na wakati mwingine wanaingia kwenye mapambano na askari wa serikali, na baadaye ndio wakaja maaskari wa umoja wa mataifa, au umoja wa afrika,…na kiukweli mimi nikawa kama miongoni mwa wapiganaji.

Siku isiyotarajiwa ikanikuta mimi, nikiwa nahudumia wagonjwa, ilikuwa ni kambi ambapo wagonjwa waliwekwa wakihudumiwa, na mimi siku hiyo nilikuwa kwenye zamu,..nikatoka kidogo kufuatilia vifaa, njiani ndio tukakumbana na hao waasi wakatuteka nyara, na kutupeleka huko msituni kwenye kambi zao.

 Ndio nikaanza maisha ya kulazimishwa kuwahudumia watu, kuwatibia maaskari wao waliojeruhiwa na watu mbali mbali waliotekwa ambao walikuwa wakilazimishwa kuishi huko, na vijana waliotekewa ambao walilazimishwa kujiunga na kundi hilo.

Ilikuwa ni kazi nzito sana, ikizingatiwa kuwa mimi nafanya kazi hapo kama mtumwa, kama mateka,kwahiyo kuna kupigwa, kuna kunyanyaswa…nashukuru mungu haikunitokea tatizo kubwa kama la kubakwa kwa kipindi hicho..na nashukuru mungu hao walioniteka walifahamu umuhimu wa mtu kama mimi…kwahiyo pamoja na shurti, kufanya kazi muda mwingi bila kupumzika lakini waliniheshimu kama mtu muhimu wa afya zao.

Siku moja nikachukuliwa kwenye kambi ya mbali kidogo, humo kulikuwa na mateka waliofikishwa humo majeruhi, na wengine walikuwa wakiteswa, mpaka wanapoteza fahamu, na hata kufa..Ilikuwa ni sehemu ya kutisha sana,…nikawa nawahudumia hao watu na kuwatibia majeruhi,..Ilikuwa ni kazi nzito sana, humo nilikaa muda mrefu…

Kuna wengine waliofika hapo, wakawa wanateswa, mpaka wengine wanapoteza maisha, ni mateso makali sana..na wakifikishwa hapo wanavuliwa nguo, wanavalishwa nguo maalumu za huko…kama matambara, yaliyounga

Ni kila baada ya mteso mimi naambiwa niwahudumie, na unawahudumia watu waliovurugwa, unawatibia bila ya sindano ya gazi, wana vidonda unaambiwa uwanyoshe hivyo hivyo….inatisha, kweli kweli..

Na siku moja nikiwa nimechoka kweli kweli ndio nikavamiwa na mtu,…kiukweli sikumuona sura  wakati ananifanya kitendo hicho,…alinikaba kama anataka kuniua, na nikajitahidi kujitetea, na haikuwa kazi rahisi, na alinikaba mpka nikapoteza fahamu…sijui ilikuwaje, maana nilipozindukana nilijikuta sehemu nyingine.

‘Samahani kwa kiendo hiki…nilitaka nitoroke na wewe…na hakukuwa na jinsi nyingine ila kufanya hivi…’akasema akiwa kajifunika uso.

‘Kwani wewe ni nani…?’ nikamuuliza

‘Mimi ni mmoja wa watu waliotekwa humu, lakini nikiwa kazini, inabidi wakati mwingine mfanye hivi ili muweze kupata tarifa za ndani na wamenigundua…’akasema

‘Kwahiyo wewe ni askari…?’ nikamuuliza

‘Hapana mimi sio askari…ila sisi ni watu tunaojitolea kusaidia…’ akasema

 Basi tukawa tunatafuta sehemu ya kutoroka, askari waasi wakawa wanatutafuta, na siku moja, wakatuona wakiwa na mbwa, haikuwezekana maana walikuwa ni wengi sana, japokuwa huyo mtu alipambana nao, akapigana nao kadri alivyoweza wakamzidi nguvu, na kukata kata na mapanga…walimuumiza vibaya sana..

Baadaye ndio tukarudishwa kwenye kambo hiyo ya mateso, na huyo mtu,..sasa kilichotokea hapo, ndio siwezi hata kusimulia;

‘Nyie mlitoroka wewe na hawara wako sio…’akasema huyo mkuu wao

‘Mimi nilitoroka peke yangu , huyo alikuja kunisaida tu, maana nilikuwa naumwa..’akajitetea, na kuongea kwake kulimponza, akateswa, ..kupigwa shoti na umeme, wakitaka kumfahamu yeye ni nani,…na hatimaye ikaja hilo tukio..

‘Huyu afande ni kidume, yeye si hawara wa huyo mdada, sasa watuonyeshe walichokuwa wakifanya huko…’akasema mmojawapo, na wengine wakashabikia, sawa watuonyeshe mkuu, hapo ikawa kulazimishwa kufanya hicho wlichokitaka wao kifanyike, …ooh,…siwezi kuelezea, …hapana…

Sijui walipata nini….maana japokuwa jamaa alitaka kukataa lakini mateso yalimzidi ikabidi afanye wanavyotaka wao, huku bado wanamtesa,..mpaka akapoteza fahamu…ikawa kila siku mateso ni hayo hayo…mpaka jamaa akachanganyikiwa, akawa hana kumbukumbu…ikawa hawezi kusimama wala kujiinua hapo alipo

‘Sasa kazi yako ni kumuhudumia huyu bwana wako mpaka apone..tunamuhitajia sana huyu mtu, tumegundua kuwa ni mtu muhimu sana kwetu…’wakasema na ningafanya nini, nikajitahidi kumtibia huyu jamaa, alikuwa kwenye hali mbaya sana, na...ukumbuke hayo yalifanyika kwa muda,..sio kipindi cha siku mbili tatu, miezi ikapita..

Baadaye wakachoka,…jamaa akawa huru maana alikuwa kama zezeta tena,..hajitambui, sijui kama alikuwa anajiigiza au vipi,…yaani mate yamatoka mdomoni, unahisi tu kutokana na kile kitambaa walichomfunika usoni, unakuta muda wote kimelowana, siruhusisi kumfunua,…basi ikawa kazi yangu kumuhudumia.

Baadae , wakaturuhusu mimi nikarudishwa sehemu ya wanawake, na huyo jamaa akawa kwenye sehemu maalumu wakiendelea kumuhoji …lakini alionekana hana kitu tena, keshakuwa tahira, kama walivyokuwa wakimuita,..’wewe tahira…’

Ilikuwa kazi yangu kuitwa kumkagua, kuhakikisha yupo salama, unamkuta kajichafua, kajisaidia ovyo..kwa hali hiyo, akatengwa na kuwekwa sehemu nyingine.

Na muda huo nilishajigundua kuwa ni mimba….lakini sikutaka nijulikane, nikawa najikausha tu tu..na siku moja nikiwa namuhudumia huyu mtu kabla hajapotza fahamu na kumbukumbu,….
Nilitaka nimfahamu maana hiyo mimba ni yake,…

‘Wewe ni nani…?’ nikamuuliza siku moja.

‘Hahaha, wou, wou….hoooo, yayayayaya..’akawa anasema hivyo, anabweka kama mbwa, halafu baadae analia kama anahisi maumivu,..walishamuharibu akili,..basi nikawa namtibia , wakawa sasa, wanampatia madawa ya kulevya, ili awe analala tu, kumuua hawataki bado wanasema yeye ni mtu muhimu sana kwao,…sikujua kwanini hawakutaka kumuachia, nilijua tu mwisho wa siku watamuua….

Huruma ilinishika nikijua sasa nina kiumbe chake tumboni, nikawa najaribu kuona jinsi gani ya kumsaidia,….

Ilishapita kama miezi mitano hivi, mimba ilishaanza kuonekana na wakawa wameshafahamu kuwa mimi ni mja mnzito, na hawakutaka shida, walitaka kuniachia,..ila waliogopa kuwa nimefahamu siri zao nyingine, kukawa na kutokuelewana kwa mabosi wao wawili, mmoja alitaka niuliwe, mwingine hakutaka…….

Nilipoiona hiyo hali,.. nikaanza kubuni mbinu za kutoroka, niligundua kuwa kuna magari yao hutoka kila siku usiku, wanakwenda kuiba au kufanya uvamilizi nikaona nafasi ndio hiyo hiyo, na kwa vile mimi nilikuwa na nafasi ya kutoka kwenda kwa wanaume, kama kuna dharura, na kurudi, wakati mwingine nasaidia kubeba vifaaa vya upishi, nikaona nitumie mwanya huo,..

Basi siku moja, usiku nikamchukua huyo jamaa nikamweka kwenye mkokoteni, kama vile nimebeba mizigo, nilikuwa nafanya kazi za kuingiza mizigo ndani , kama vifaa mbali mbali au kusafisha vyoo,nk..kwahiyo hakuna aliyenishuku…nikaweza kumfikisha kwenye moja ya gari niliokuwa nafahamu litaondoka usiku…ilikuwa jioni jioni na wao walikuwa kwenye doria kuna hali tete ilishatangazwa, wanapigana sasa kufa na kupona..

Nilimuomba mungu huyo jamaa asizindukane, mpaka hilo zoezi lifanikiwa angalau yeye ondoke hapo kambini maana watamuharibu kabisa akili,…kama hatapata msaada wa haraka..ilifikia mahali akiamuka, anakuwa kama mbogo, anajipiga piga, kichwani, alikuwa kama anahisi maumivi fulani au kero fulani kichwani..

Na kweli usiku ikafika nikafike eneo hilo nikiwa nimevalia kiaskari..kama mwanaume, huwa usiku walinzi wanavaa nguo fulani zimevalishwa majani,…kwahiyo nilifanya hivyo kama wao,…na misheni ikakamilika, tukaondoka, tulipofika sehemu gari likanasa kwenye matope, na mimi nikaona ndio sehemu ya kumshusha huyo jamaa ilimradi aondoke maeneo hayo.

Basi nikamtoa kwenye ile sehemu nimkasukumia nje, na wakati huo hao jamaa wanashughuli na kazi ya kulikwamua gari, mara tukasikia milio ya risasi, bomu…mimi kwa haraka nikamsukumia jamaa sehemu ya porini kuna kama mteremko, akaserereka kwenda bondeni,  na mara mvua ikaanza kunyesha, nikasikia gari huko linaondoka, huku wanaitana,…mimi nikajificha mpaka wakaondoka.

 Nilipohakikisha kupo kimia, nikateremka hadi pale alipokuwa na ikawa kazi ya kumzindua jamaa, nilikuwa na dawa za kusaidia, nikampa , na baadae akazindukana, na ghafla akaanza kukimbia, nilijaribu kumfuatilia, hadi tukajikuta tumetokea karibu na mtu,…jamaa akawa kasimama hapo, kazubaa tu…hapo nilitaka nimuondoe ile nguo usoni, ili nimuone vyema, lakini hakutaka nimguse usoni, …

Nikawa sasa namsaidia maana mguuni aliumia sana anavuja damu, nikawa namsaida tuondoke eneo hilo maana kuna sauti kama za watu zilikuwa zinakuja, mara milio ya bunduki, mabomu, niliposikia hivyo nikaanza kukimbia, hapo sikujali tena nina mgonjwa,.. yeye alibakia kasimama pale pale, wakati nakimbia, mara nikakanya kitu..mungu wangu, ilikuwa kama mtego, yaani haikuchukua muda,..ilikuwa ni mlipuko, sijawahi kusikia masikioni mwangu…

Mimi sikujua kilichoendelea,…, ila kwa mara ya mwisho nilihisi kama narushwa hewani, na fahamu zikanipotea,…nilipozindukana najikuta nipo pembezoni mwa mto…mwili mzima unauma, na akili ilipokaa sawa, ndio nikagundua kuwa nina majeraha ya kuungua…

Nikajaribu kujizoa zoa, na nikagundua kuwa nipo pembeni ya mto, nikajaribu kujisogeza kwenye maji nijionyeshe hayo majeraha, unajua mimi ni nesi, naujua odocta, kutokana na uzoefu wa kazi yangu ya kuwahudumia wagonjwa,..kuangalia pale kwenye mto nikaona kitu kama mamba, …binadamu waoga, nilipohisi hivyo,..kuwa ni mamba, , nilipata nguvu za ajabu..nikaanza kukimbia, kukimbia kwenyewe kwa shida ni kama unajiburuza..hadi mbali kidogo na huo mto.

Niliweza kutoka sehemu ya hatari, kutokana na majeraha, maumivu, nilihisi kupoteza fahamu nikawa napigana na hiyo hali lakini ikafika muda nikazidiwa,..nikapoteza fahamu , na nilipozindukana tena nikajikuta sipo peke yangu, kuna mtu ananikagua nilijuwa ndio hao jamaa, nikataka kujitutumia nisimame….nikimbie…

‘Tulia,…kuna watu huko,…’akasema huyo mtu

‘Kwani wewe ni nani, …alikuwa kajifunika kama wanavyofunikwa watu huiko matekani.?’ nikamuuliza

‘Nimtoroka kambi ya waasi nilitekwa nyara huko…’akasema.

 Aliposema hivyo nikawa na matumaini, kuwa huyo sasa ni mwenzangu, na akili yangu kwanza ilitaka kuhakikisha, labda ni yule jamaa niliyetoroka naye, lakini maumbile hawafanani kabisa,.., nikamuuliza

‘Hukumuona mtu kama vile kachanganyikiwa huko, kavaa ovyo ovyo....?’

‘Sijaona, ila kuna mapigano makali waasi wamesambaratishwa,…nahisi sasa kutakuwa na amani…’akasema.

‘Oh sijui kama atakuwa mnzima…’nikasema sasa nikiwa na matumaini kuwa angalau niliyejitahidi kumuokoa huenda akawa mikono salama, japokuwa mimi imenigharimu maisha yangu.

‘Ila nimeona mtu kabebwa kwenye machela ya wagonjwa sijui kama ni huyo…’akasema

‘Labda yupoje…?’ nikamuuliza

‘Kavaa matambaratambara kama mwenda wazimu…usoni bado alikuwa kafunikwa kama hivi, si unaua taratibu za hawa waasi…’akasema

‘Ndio yeye, lakini ina maana waliomchukua ni waasi, au…?’nikasema

‘Sio waasi , hao ni maaskari wa usalama,…nimewaona, yeye ni nani wako…?’ akaniuliza

‘Hata simjui vyema, ila nilikuwa namuona hapo kambini… ila kachanganyikiwa sema ya kuteswa sana…’nikasema

‘Basi tuondoke hapa..kwa hali uliyo nayo huwezi kutembea mimi nitakubeba…’akasema na kweli alinibeba hivyo hivyo mpaka tukatoka eneo hilo,…..na mengine ni kama nilivyowahadithia awali….’akasema

Akaishia hapo na kukaa kimia, Soldier akawa anamuangalia sana huyo mdada, na dereva akasema;

‘Umesikia bro, sasa hujaamini kuwa huyo mtoto ni wako….’akasema

‘Kwanini wewe asiwe wako, wewe ulisema uliwahi kutekwa na hao jamaa, …’akasema Soldier.

‘Lakini mimi sikuwahi kuteswa,…waliponigundua kuwa ni mfanyakazi wa kusaidia watu, wakaniachia…je wewe hukuwahi kuteswa, hukuwahi kutekwa,…sema ukweli bro…?’ akauliza Dereva.

‘Usijifanye mjanja, hii ni hadithi yenu mumetunga wewe na huyu mdada, nitaihakikisha pindi wakija polisi, …hakuna mtu kuondoka hapa…’akasema Soldier sasa akionekana yupo kazini.

Wakati polisi wanakuja nikuulize swali wewe mdada;

‘Uliza tu…’akasema kwa sauti ya kinyonge…

‘Ina maana kweli kwa muda wote huo ulipokuwa ukiwauguza hao watu, na kumuuguza huyo mtu, hukuwahi kumuona huyo mtu usoni, hata mara moja, …maana mliweza kukaa naye kwa muda mrefu, kama ulivyodai, inawezekanaje hivyo , ni lazima uliwahi kumuona sura huyo mtu…au sema, sema ukweli ...’akauliza baba.

‘Hutaamini baba,...maisha ya huko yalikuwa ya mashaka, kuogopa,, kosa dogo linaweza kukugharimu maisha yako, kwahiyo tulikuwa tukitii amri..., wanaume wote humo walikuwa wamefunikuwa uso na walikuwa na sehemu yao tofauti na sehemu ya wanawake, na hakuna ruhusa wanawake au wanaume kufika sehemu za wengine..kuna ulinzi mkali sana, wanawake kazi yao kubwa kupika, kufua,..na kazi za kutafuta kuni.

Mimi nilikuwa nakwenda sehemu waliyoitenga kama hospitali, na huko wanaume wamefunika usoni, hata kama kaumia usoni, huruhusiwi kumtizama, unaulizwa, na askari umuelezee cha kufanya kwa huyo mgonjwa, kwanza walikuwa hawajali sana , watu wanatibiwa kiharaka haraka..kama sio binadamu, labda kama unamtibu askari wao.

Kiukweli, ilikuwa ngumu sana kumfahamu mwanaume huyu ni nani,……lakini huyo katika kumtibia niliwahi kumuona sura kidogo tu…..ni kundi la ajabu sana, sijui kwanini hawakutaka watu wawafahamu hao wanaume sura zao…’akasema

‘Kama ulimuona kidogo tu, ni nani sasa , je ni Soldier au Dereva…?’akaulizwa, na kabla hajasema kitu polisi wakafika wakiwa na viongozi wa jeshi…ilikuwa ni ajabu ni kwanini walifika hivyo, kama vile wanakuja kumkamata mtu hatari…

Shemeji mtu kuiona hiyo hali akamgeukia, Soldier na kusema;

‘Utajuta kwa hili….dada umeona mtu wako,....’akasema akimuangalia Soldier, na dada mtu akamgeukia mumewe na kumuangalia kwa macho ya chuki...

NB: Tunaishia hapa na tukijaliwa tutaingia kwenye hitimisho la kisa hiki

WAZO LA LEO: Sio vizuri, watu kutafuta mambo ya ndani ya wengine ambayo huenda ni siri ya mtu na kuanza kuzitangaza hadharani kwa njia ya kuzalilishana, au madhaifu ya kimaumbile, wengine huona raha kuyatangaza kwa wengine, unaona kuwa mungu aliyefanya hivyo kafanya makosa au sio!


Tukumbuke kuwa kutangaza mambo ya wengine kwa nia ya kudhalilishana, kudhhofishana, inamfanya mtu aumie kisaikolojia, na kujiona hafai, na uvumilivu hutofautiana kati ya mtu kwa mtu, wengine wanaamua, kulipiza kisasi, na matokeo yake ni chuki za mtu mmoja mmoja, na baadaye wanahusishwa mashabiki, na matokea yake ni vurugu za makundi. Tuweni makini na chuki hizi ambazo chanzo chake ni vitu vidogo vidogo tu.
Ni mimi: emu-three

No comments :