Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, March 25, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-27



Hebu fikiria, mume ni askari, kaenda kwenye kazi za kivita za kimataifa , huko alikaa miaka mitatu....huko kakutana na majaribu mengi tu, akiwa huko alijua kuwa yeye ana mke nyumbani na anamapenda sana, kwahiyo alijitahidi kulinda miiko ya ndoa yake!

Miaka mitatu ikapita, kwa shida, ...maana vita ni vita, na ukiondoka salama huko unamshukuru mungu, sasa anarudi nyumbani, na anapokelewa na mkewe, mara mkewe anamuonyesha mtoto wa miezi minne, anasema;

'Mume wangu huyu ni mtoto wako...' huamini, huelewi, siku zinakwenda unajaribu kuutafuta ukweli, mke hataki kukuambia yeye anakuambia huyu ni mtoto wako, humuoni mnafanana naye,...unashindwa kuelewa maana mtoto hafanani nawe tu, pia anafanana na ndugu yao dereva, pia anafanana na baba yako...mengi yanapita hapo...mara mtoto ni wa baba yako, mara mtoto ni wa dereva...

Aikili inakuchanganya...huwezi kukosana na baba yako, lakini nahisi kuwa huenda huyo mtoto ni wa dereva, ila huna ushahidi, dereva mwenyewe ni tapeli, ni muongo...lakini una ushahidi gani...imefikia hatua sasa mke anakuambia, niambie ukweli, mtoto ni wa ko au sio wako, na ukitoa jibu mimi nitajua cha kufanya, ila mimi mtoto huyu ni wangu...

Tuendelee na kisa chetu…

                                                             *******************

 ‘Kwanza niwaombe radhi, au niseme msamaha kwa kuwaingilia kwenye mambo yenu ya kifamilia, mungu ni mwema, mwenye rehema,..anaweza kukuongoza kwenda sehemu usiyotegemea, mpaka ukajiuliza huku nafuata nini, lakini kumbe anakuelekeza  kwenye maombi yako…sikujua kama itakuwa hivi kabisa kabisa,…’akaanza kusema huyo mdada.

‘Wengi nilipokuwa napita njiani wamekuwa wakiniangalia mpaka najisikia vibaya, nahisi kama nisingelijifunika hivi, wangeniangalia zaidi na hivyo, na huenda ningelijisikia vibaya zaidi , maana sisi wanadamu, hisi zetu ni karibu sana, na zinaweza kutusukuma na kutenda jambo lisilo la kawaida, wengine wanafikia hadi kujiua,…ni hatari…’akasema

‘Siwezi kuamini kuwa leo nipo hai, lakini mungu ni mwingi wa rehema, na jamani ukiamuka asubuhi na ukaweza kupumua mshukuru sana mungu, wako, mkiwa na amani kwenye nchi yenu, hakuna vita,  mshukuruni sana mungu, japokuwa huenda miyoni, huenda maisha mnapigana vita na ugumu wa maisha, hali ngumu, ambavyo ungeliweza kuviweka wazi ingelikuwa ni vita ya aina nyingine, lakini ogopeni vita hii ya waza….’akatulia

Kabla sijajieleza mimi ni nani, maana katika haya kila ninapopata nafasi nageuka kuwa mtoa ushauri, hotuba, mawaida, mahubiri..si ndio hivyo, nimeona nifanye hivyo maana mimi ni miongoni mwa waathirika wa machafuko ya vita….

Nianze kwa kujibu hisia za mzee wetu hapo , baba yetu , unaumwa na mtu akiumwa kitu kikubwa zaidi ni maombo, kukirimiwa, kuonewa huruma, haya tunayoyafanya hapa basi yaendane na huruma tusije tukavuka mipaka tukamuathiri mgonjwa, tufanye yale yatakayompa faraja, ili aweze kupambana na hayo maradhi…maradhi ni vita, ni mtihani….’akatikisa kichwa

‘Mimi ni nesi, na katika ghasia hizo zinazoendelea huko kwetu, nimepata bahati ya kuwa mmoja wa manesi wanaosadia mejeruhi…ni kazi ya hatari sana, na nimpeponea chupu chupu mara tatu,..na hii ya tatu ndio iliyonifikisha huku, na hiyo ya tatu,..nilijua ni njia ya kwenda ahera…

‘Baba samahani kwa hayo niliyokusababishia mimi, maana nimesikia ukisema umepata mabaya , kutokana na mimi na sasa umeshampata mbaya wako ambaye ndio sababu ya matatizo yako, mimi sijui ni kwanini hayo yaliyotokea yafanye mpaka ufikie hapo kitandani,..kwakweli mimi sijui….labda nitakuja kupata maelezo baadae, ila ninachotaka kuelezea ni jinsi ilivyotokea ikawa hivyo…

Nilifanya hivyo kwa minajili ya kukiokoa hicho kiumbe kisicho na hatia,…kama nilivyosema mimi ni nesi, na moja ya kazi zetu ni kuwahudumia wagonjwa, …na kuangalia mazingira bora ya watu, kutoa nasaha, na matibabu kwa maelekezo ya dakitari…na wateja wetu wakubwa ni  wagonjwa, na mimi licha ya kuwa baadae ilibidi niwahudimie watu wote, lakini mimi hasa hasa nimesomea unesi wa watoto..na huyo mtoto alihitajia mazingira bora, kuliko huko alipokuwepo mwanzoni.

‘Wengi wetu mnasikia mtoto katupwa, mtoto kaokotwa,, wengine hawaamini kama kweli mzazi, mwanamke, anaweza kufanya vitu kama hivyo,…lakini ndivyo ilivyotokea kwa mtoto huyo, je mzee ningelimuacha huyo mtoto huko alipokuwa ukasikia, kadhurika ukakutana na mimi ungelinielwaje, na labda ndio ugundue kuwa ni damu yenu..hebu niambie mzee ungelijisikiaje,..maana utasema kwanini sikufanya nilichokifanya, na ndio maana nimefanya hivyo, au mfano ningeamua kuondoka naye huko kwetu kwenye vurugu, au kambi ya wakimbizi, ukaja kugundua kuwa ni damu yenu, ungalijisikiaje,..jamani msifikiri kambi za wakimbizi kuna raha, hakuna raha huko, huko ni mateso,..ni kifungo cha aina yake…

************

Siku kadhaa nyuma, nilifika eneo nikasikia mtoto analia, na hapo hapo nikakumbuka, moja ya kazi yangu, sikusita… haraka nikamuendea yule mtoto na kumbemba, nilimuonea huruma sana, maana ni mtoto mnzuri mwenye afya, nikajua huyu anastahiki kufika kwa wazazi wake stahiki…, nifanye juu chini afike kwa mzazi wake..na ndivyo nilivyofanya…’akageuka kumuangalia dereva, halafu Soldier. Kama vile anatafuta ni nani baba yake, Soldier alikuwa kamkazia macho tu, Dereva akatabasamu kidogo na kuangalia chini

Wanaume nyie mnajua kutunga mimba tu, mnaona raha, lakini mfahamu wanawake wanapata matatizo makubwa, kubeba mimba, ile adhabu ya miezi tisa, nyie mnaijua nyie…mtasema mnaijua lakini hamuweze kuelezea ile hisia, mateso, anayejua hayo ni mzazi peke yake…

Na bado hujafika kwenye tundu la …kaburi, maana muda wa kujifungua ni kucheza na umauti, wengine wanapitia kipindi kigumu sana, hilo hamlielewi, ndio maana hamtuonei huruma, mimi kama nesi nimeyaona hayo sana, na kama mzazi nimepitia kipindi kigumu, siwezi hata kuelezea

‘Kwahiyo nilipokiona kile kiumbe kinalia,…mlio ule kwa mzazi wa kike anajua mtoto analilia nini, mlio kama ule kwa mzazi unagusa hisia za ndani za machungu ya uzazi, nani kama mama, hebu niambieni,…kwa mzazi hasa ni lazima huruma itakushika hata uwe na roho mbaya gani, sasa ni kwanini inafikia mzazi wa kike anaamua kuwa mnyama, anaamua kumtupa mtoto wake aliyemzaa kwa shida, kutoka mimba hadi uzazi..sababu kubwa ni nyie wanaume..na mzigo huu mtaubeba nyie, ndio maana sikusita kulifanya hilo..kuufikisha huo mzigo kwa walengwa…

‘Baba ni kweli mtoto yule anafanana na wewe, ..na awali nilipomfikisha kwa huyo anaitwa….dereva, nilijua nimefikisha kwa mwenyewe, na sikuwa na shaka hiyo..lakini baadaye akaanza kunipa mipango yake, kuwa..nifanye hivyo nilivyofanya, sikuona ni shida kwangu, nilichotaka hicho kiumbe kifike kwa walengwa..wasiwasi wangu ukawa je ni kweli huyo mtu niliyeambia kweli ni damu ya huyo mtoto..

 Pale hotelini nilisubiria sana, nilikiliwazia hilo…, huku moyoni nateseka, je kama sio yeye, je kama huyo mtu aliyenielekeza nifanye hivyo ana nia mbaya tu, na wakati nilimuona yeye ndiye mtu sahihi, ..yeye ndiye baba wa mtoto, hebu iangalieni sura ya huyo mtoto, na huyo dereva , kiukweli nilipomuona huyo dereva nikajua huyo mtoto ni wa kwake, na ndiye anayestahiki kuubeba huo mzigo..nilitamani hata nimshitakie.

‘Baba nimehangaika sana na huyo mtoto…siku nzima nazunguka huku na kule na kipindi kama hicho na maeneo kama hayo, na hali kama hiyo hakuna aliyejali, …nashangaa hata mtoto alipopatikana ametupwa, wengi walisikitika mara moja, lakini ni nani alihangaika kuona huyo mtoto ataishije, atafikaje kwa wazazi wake, hakuna,maana hao watu wa pale wametoka kwenye shida, wametoka sehemu wanaruka maiti, wanaruka, hata kukanyaga watu walioumia wakiwa wanaomba msaada, wengine wapo mahututi..lakini hakuna cha kujali, kila mtu anakimbiza roho yake…

‘Nikuambie kitu huyu mtoto anafanana na watu ninaowafahamu…’akaniambia huyo dereva alipomuangalia huyo mtoto vizuri.

‘Lakini mbona anafanana na wewe…’nikamwambia

‘Mimi nafanana na hao watu pia, kuna mzee mmoja, …namfahamu tena bahati nzuri yupo hapa,..huyo nina imani kuwa ndiye anajua au anahusika na huyo mtoto..’akasema

‘Ni kweli kuna mdada mmoja..anaishi huko, nimuelezea huyu ….’akasema jamaa mmoja niliyekuja naye hapo.

‘Huyo mdada anaitwaje…?’ akauliza na huyo jamaa akasema alisikia akiitwa kwa jina hilo la shemeji.

‘Unasema anaitwa nani…?’ akauliza mara ya pili.

‘Nikamtajia jina, na kuna watu wengine niliokuja nao, wakathibitisha hilo, ni kweli huyo mdada alikuwepo, akiwa na mtoto maeneo ya uraiani, karibu na kambi, baadaye akaonekana hana mtoto, ….kwahiyo moja kwa moja ikajulikana kuwa mtoto huyo alitupwa na huyo mdada, saa ni nini kifanyike, hilo jukumu niliachiwa mimi niliyemuokota huyo mtoto.

Siku ya kwanza, ya pili ndio nikapata mwanya wa kufika kwenye hicho kituo ch akuwahudumia wakimbizi, sikuweza kufika siku ile ya kwanza maana kulikuwa ghasia watu wanagombea huduma, nk…na hata hapo kituoni hakukuwa na watu , kulikuwa na vikao, na shughuli nyingi tu

 Siku ya pili yake ndio nikafika hapo kituoni...nafungua mlango nakutana na hiyo sura, nilipomuona tu,…sijui, lakini…ilibidi nisimame nimeshikwa na butwaa, nahisi hata yeye mwenyewe alishangaa, kwanza nikaamua kumkagua mtoto tena na tena unajua kufanana,…huyu dereva na huyo mtoto ni kila kitu.

‘Unauua kabla ya siku hiyo, nilikuwa nazunguka na huyo mtoto nikiwauliza watu, ni nani alimuona mdada au m-mama mwenye mimba, aaliyezaa hivi karibuni…niligangaika huku na kule, na ndipo nikakutana na watu wakaniambia kuhusu huyo mdada..

‘Mdada gani…?’ akauliza mama

‘Huyo mdada walisema alifika hapo akiwa na mtoto mchanga, akawa anaishi kwa mama yake, lakini baadae mama yake akaondoka, akabakia yeye na mtoto, na baadae huyo mdada akaonekana akiwa hana mtoto,….’akasema.

‘Sasa huyo mdada yupo wapi..?’ nikawauliza na wao wakanielekeza, nilipofika hapo nikaambiwa huyo mdada alishaondoka hayupo tena eneo hilo, na nikawauliza wenyeji waliokuwepo wapo je huyo mdada kweli alikuwa na mtoto mchanga, wakasema ndio..nikajua ehee, ni kweli..

Basi kesho yake ndio nikafika hapo ofisini, na mara kuangalia bosi wa hapo, ohh…anafanana na mtoto, oooh, nikajua sasa nimeshampata muhusika , huyo ndiye baba wa huyo mtoto hakuna kukataa, nikashukuru mungu, na bila ajizi mimi nikamwambia;

‘Nimekuletea mtoto wako..’nikamwambia, akashikwa na mshtuko, na kuniangalia kwa wasiwasi

‘Mtoto wangu!!!’ akasema kwa mshangao

‘Ndio huyu hapa, huoni mnafanana na yeye…’nikamwambia na yeye akamchunguza huyo mtoto akawa kama anashangaa, uso unaonyesha kabisa kushangaa, halafu akaniangalia na kuniuliza;

‘Huyu mtoto ni wako…?’ akaniuliza na mimi nikamwambia

‘Ndio,… umesahau eeh, najua umesahau, maana unatembea na wanawake wengi, sasa huyu ni mtoto wako nakuachia…’nikamwambia

‘Sikiliza wewe mdada, mimi sina mtoto, na sijawahi kutembea na mwanamke yoyote hapa, mimi ni mgeni, nimefika hapa kituoni sina hata zaidi ya mwezi , je mwezi mmoja ningeliweza kumpa mwanamke uja uzito, na kuzaa….’akasema

‘Usijetete, ina maana mimi hunifahamu..?’ nikamuuliza

‘Kiukweli mimi sikujui, kwani wewe ndiye mama wa huyo mtoto..?’ akaniuliza

‘Huyo mtoto tumemuokota na aliyemtupa hatujamuona, lakini wewe unafanana na huyo mtoto, hebu angalieni jamani…’nikasema nikiwaonyesha watu waliokuwepo hapo, na kila mtu akasema kweli.

‘Sikilizeni niwaulize nyie watu mliwahi kuniona maeneo haya kabla?’ akawauliza na wengi wao wakasema hawajawahi kumuona, na akajitetea sana,..baadae mtu mmoja akamuuliza

‘Kuna mdada mmoja alikuwa anaishi maeneo nje ya kambi alikuja na mtoto sasa hayupo, na niliwahi kusikia wakimtaja kwa jina hilo…’akalitaja hilo jina

‘Wanatokea wapi..?’ akauliza

‘Nilisikia wanatokea nchi ya jirani …’akasema

Basi akasema tusubiri akachukua simu akapiga kwa watu mbali mbali baadae akasema;

‘Nimeshawapata wazazi wa huyo mtoto, na bahati nzuri muhusika mkuu mwenyewew yupo hapa nchini, ni bahati sana, sasa sikiliza, nyie wengine ondokeni, mimi nitabakia na huyo mdada, nitamfahamisha cha kufanya..

‘Kiukweli, mimi huyu mtoto sio wangu, ila kuna watu ambao nafanana nao, nimeambiwa kuwa ndio wenye huyu mtoto, mimi nitasaidia mpaka umfikishe kwa wenyewe..’akasema

Hapo mimi nikashukuru mungu, nilijua ni mbinu za huyu jamaa nia yake ni ili watu wasijue kuwa yeye ndiye aliyembebesha msichana wa watu labda akamtelekeza, hakujua kuwa damu yake itamfuatili hadi hapo. Niliwazia hivyo kuw labda anafanya hivyo kwa vile yeye yupo kwenye sehemu ya kuhudumia watu, na kufanya jambo kama hilo inaweza kumchafulia hadhi yake, kuwa hafai kazi kaam hiyo..

‘Ndio akanielekeza jinsi gani ya kufanya,…na ndivyo nilivyofanya…

Sasa mzee siku ile ulipofika pale nikakuangalia, nikajua kweli huenda anayosema huyo mkaka, ni kweli,..na ni kweli mzee mnafanana sana na huyo mtoto hata uzeeni kwako huwezi kuficha sura yako na huyo mtoto.,…lakini akili yangu haikukubali, nilijua huyo dereva ni mtoto wako na huenda nyote mna mbinu moja, ya kuificha hiyo kashfa,..mimi nikaona nikubaliane na hilo wazo lake.

Kwahiyo kwangu mimi nilijua yeye ndiye baba wa mtoto…mtoto anafanana na yeye mengine hayo anayofanya eti nimpeleke mtoto kule kwenye hoteli kuna jamaa atakuja, basi hapo nimuachie yeye, niliona labda ni mbinu zake tu za kujipatia pesa, au kulinda hadhi yake ya kazi, mimi sikujali,…

Kwangu mimi mpaka hapo nikawa nimepumua, kuwa angalau sasa mtoto kafika kwa baba yake, na mimi nitaweza kuendelea na kazi zangu..sikuwa na kazi lakini nisingeliweza kupata kazi hasa kazi yangu, nikiwa na mtoto au sio, ningemuachia nani na mimi nipo kambini, na kiukweli nilikuwa sina mbele wala nyuma…na kutokana na matatizo niliyokutana nayo sikupenda kujionyesha kwa watu..

Hata hivyo akili yangu haikutulia,…nilitaka kuwa na uhakika kuwa kweli mtoto huyo amefika mahali salama, na ni wapi, hapo akili ikanicheza. Kabla hata sijafika kwenye hiyo hoteli, alipofikia huyo mzee, nikamuelezea huyo dereva kuwa mimi nina ndugu yangu yeye kasomea uyaya, kwahiyo huyo mtoto kama atakuwa kafika kwa wazazi wake, basi huyo mdada anaweza kusaidia, hasa kutoka hapo hotelini hadi huko, na kama wataona hafai yeye atarejea huku.

Kwa haraka huyo dereva akakubali, na hapo nikawa na uhakika kuwa huyo jamaa ndio baba wa mtoto,,,,kwanini akubali harakaharaka hivyo, na cha achabu,akasema anataka atafute na nauli ya huyo yaya, ili isimpe shida huyo muhusika ambaye nitamfikisha huyo mtoto, kwahiyo kwa muda huo akawa anawasiliana na watu anaowafahamu wa huko kituoa cha ndege, na tiketi zikawa hazina shida.

Na mimi kwa haraka nikafika kwa ndugu yangu nikamuelezea kuwa kuna kazi imepatikana kwahiyo ajiandae kwa haraka,.. na yeye bila shida akakubali, maana kuondoka  hapo kambini ni furaha, na anaenda kufanya kazi , na tena anakwenda kufanya kazi nchi yenye amani, nchi ambayo hata yeye alikuwa akitamani kwenda kuishi.

Hayo yakafanyika vizuri tu, na mtoto akafikishwa kwa walengwa, na mimi huko kambini , nikapumua, japokuwa akilini nilikuwa sina amani,……sikuwa na amani kabisa..’akatulia

Hakuna kipindi nilichoteseka kama kipindi hicho, …ilifikia sehemu nachanganyikiwa, kuna muda nasikia mtoto akilia kichwani mwangu, mama, mama..mbona unaniacha…kwakweli nilipata taabu sana, na baadae ndugu yangu ananipigia simu na kuniambia taarifa ya ajabu kabisa,..kwakweli sikuweza kuvumilia, nikaanza kufauta nauli,….kuja huku…

‘ Sasa kwanini usiwe na amani, wakati mtoto keshafikishwa kwa wenyewe…?’ akauliza mama

‘Mama, hivi kweli kuna mzazi anaweza kumuacha mtoto wake kwa watu baki..sawa mtoto kafikiswa kwa watu ambao unajua ni damu yao, lakini je mtoto wa hali hiyo, anaweza kuishi salama mbali na mama yake , na mtoto huyo ni mchanga,..hivi kweli mzazi, mama, anaweze kutuliza akili yake…?’ akauliza

‘Kiukweli hakuna, lakini mbona hatukuelewi….?’akasema mama

‘Mama mimi..nimelifikiria sana hili na nikafikia uamuzi, siwezi tena kuendelea na mpango huo, nimeamua kuifichua siri,…mama mimi ndiye mama halisi wa mtoto huyo….’akasema na kuanza kufungua uso wake na kubakia wazi, na watu wakabakia mdomo wazi.

‘Wewe….’aliyesema hivyo alikuwa dereva

‘Haiwezekani…’akasema Soldier

‘Unafanya nini sasa…’alisema Shemeji akimkodolea macho huyo mdada


‘Dada….mbona unaharibu tena…’akasema Yaya

NB: Oh..., hapa hata mimi nachanganyikiwa ngoja kwanza niishie hapa...

WAZO LA LEO: Mzazi uliyebahatika kuwa na mtoto, ukazaa kwa shida, ukaibeba mimba miezi tisa iweje sasa unakitupa kiumbe cha mwenyezimungu, unakitesa,..unakitelekeza, Ewe mwanaume uliyembebesha mwenzako mimba kwanini sasa unakimbia majuku yako,…Nyote wawili mjue, nyie ni njia tu, mwenyezimungu aliamua kukileta kiumbe chako kupitia kwenu, sasa kwanini mnakana mwenyezimungu, mnakana maagizo ya muumba wako. Kama yamekukuta matatizo, usikate tamaa, mlee huyo mtoto na mola wako atakubariki, atakujalia, na huenda huyo mtoto ikawa ndio sababu ya mafanikio, hapa duniani na kesho Akhera.
Ni mimi: emu-three

No comments :