Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, March 24, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-26


‘Jamani naona mimi nianze  kuongea…..’aliyesema sasa alikuwa mke wa Soldier. Soldier hakutarajia kuwa mkewe ataanza kuongea, yeye alitaka aupate ukweli kupitia kwa watu wengine…

‘Maana kama nilimuuliza mara kadhaa akanificha, sasa kwanini nisumbuke naye…’akilini alikuwa akiwaza hivyo.

‘Nitaupata huo ukweli hata kama hutaniambia wewe…’aliwahi kumwambia mkewe hivyo, sasa mkewe huyu hapa anataka kuusema ukweli mbele ya watu, je ukweli huo hautamuathiri baba yake,…ngoja ausikie, hapa akajikuta akimkazia macho mkewe, lakini cha ajabu mkewe alikuwa anatizama upande upande kama anamkwepe kumuangalia mumewe usoni.

Tuendelee na kisa chetu…

‘Wazazi wangu, na ndugu na jamaa zangu (hakumtaja mumewe)….naongea hili kutoka undani wa moyo wangu…’akaanza kuongea. Na alipoanza kuongea hivyo, baba mkwe alijishusha kitandani na kujilaza, maana muda wote huo alikuwa amekaa, baada ya kuweza kujiinua kwa miujiza na kitendo kile kiliwafanya waliokuwepo humo ndani kugeuka kumuangalia mzee..kama kazidiwa nini.., na Soldier akamuuliza baba kwa ishara kuwa yupo ok, baba yake akaonyesha dole gumba kuwa yupo ok..

‘Najinyosha kidogo tu…’akasema na huku mkewe akiendelea kuongea;

‘Mimi nilimpenda sana mume wangu, na nilijitahidi sana kuwa mke mwema, na niliahidi nitafanya hivyo kwa kadri mola alivyotujalia uhai wetu, ilimradi tupo kwenye ndoa, na mungu alisaidia kwa imani hiyo, kwani kiukweli nimepitia majaribu mengi …’akatulia.

‘Mume wangu alipoondoka, walinijia watu wengi tu, wakiniambia hili na lile, na wengine wakaja kunisingizia kuwa mume wangu huko alipo ana mke mwingine, hapo nilikuwa sijapata taarifa nyingine iliyonivunja nguvu kabisa, japokuwa nilijitahidi nisiiamini…’akatulia

‘Mimi….?’ Akauliza Soldier akishika kifua, Soldier akatabasamu kwa dharau, na shemeji mtu ndio akacheka kabisa.

‘Lakini mimi sikuwahi kukubaliana na hayo maneno, na hayo maneno yalivuka yakaenda hadi kwenye familia yangu, na familia yangu iliniita na kuniuliza kama nina habari kama hiyo, kiukweli niliwakatalia, lakini bado walinisisitizia kuwa niwe makini, kwani hao wanaoongea hivyo wanatokea nchi ya jirani.

‘Haya yalienda , mpaka ikaja hiyo ya baba, baba mkwe, akawa analewa, nilijua ni sababu labda za ndoa yake, lakini mimi nilijitahidi sana kumuheshimu baba, kama ninavyomuheshimu baba yangu mzazi, hadi pale alipoanza kikiuka mpaka,…alikuwa analewa kupita kiasi mpaka anakuja kutaka kulala chumbani kwangu.

‘Oh…’ulikuwa mguno wa Soldier

‘Mwanzoni nilijua ni pombe tu, lakini ..aah, sikuweza kuvumilia, na siku moja ndio nikasema basi ngoja niondoke tu….alikuja na kuanza kuongea akiwa kalewa, anaongea kuwa amesikia mtoto wake amekufa…sasa kama mtoto amekufa, na mke kamkimbia, kwanini mimi nisiwe mke wake,…’akatulia

‘Sikupenda kuyaongea haya mambo, maana yalikuwa ni maneno ya kilevi, nayaongea kwasababu ya haya yanayojitokeza, na inavyoonekana nisipoongea, naweza kuonekana mimi ni mkorofi,sina adabu…matendo hayo ya kilevi, samahani natumia kauli hiyo baba, yalijirudia tena na tena, mpka kwangu ikawa ni shida,…uvumilivu ukanishinda,  ndio nikaamua kuondoka…’akatulia.

‘Umemaliza…?’ akaulizwa na mama mkwe

‘Kwa upande huo nimemaliza, labda huko nilipoelekea kulitokea nini, maana naona kuna mengi nimehusishwa nayo hata sijui ilikujaje…’akasema

‘Je katika huko kulewa kwa baba mkwe wako, ..je aliwahi kukushurutisha kufanya lolote, na je ilitokea akakushika kwa nguvu na tendo likafanyika..?’ akaulizwa

‘Mama haikuwahi kutokea hivyo maana nilishafahamu kuwa sio akili yake, na nisipokuwa makini yanaweza kutokea mabaya, kwahiyo nilijitahidi kuwa mbali naye kadri ilivyowezekana,  kero zilipozidi,nikaona njia nzuri ni kuondoka, na nahisi kama ningeendelea kubakia humo, huenda ningezidiwa nguvu,,…kuna siku niliamua nimpige hata chupa,…nasema haya kutoka ndani ya moyo wangu,..’akasema

‘Hebu angalieni, unamvumilia mtu kama baba yako na bado anakukera, unafanya yale hata yasiyofa, maana ukilewa unaweza kupitiwa na haja, mimi ilibidi niifanye hiyo kazi,..na bado anakukasirikia, kuwa simjali nk…unajua ilifikia muda ananifokea kama mkewe, ila heshima ya ukwe ikawa haipo…’akasema

‘Nilivumilia nikimuona yeye ni baba yangu , nilivumilia kwasababu ya mama, kwani mama aliniambia anaondoka, lakini nimsaidie mume wake, kwani anajua hayo yanampitia ni shetani tu,,lkn ili mume wake aweze kujitambua ni lazima yeye achukue hatua, mimi..nilitii sana kauli ya mama, zaidi ya kauli hiyo, kuwa huyo ni sawa na baba yangu…maana kama yeye angejitambua kuwa ni baba yangu asingeliweza kufanya hivyo…’akatulia.

‘Sasa ndio napata taarifa kutoka huko, alipokuwa mumewangu,… kwanza nilisikia amekufa, baadae nasikia ana mke mwingine na baadae eti wameshazaa mtoto…, huku baba ndio huyo haeleweki, huku familia yangu inanisakama na ilishafikia sehemu imesema kama sitaki kurudi kwetu, basi litakalonipata ni juu yangu,…kwa hali kama hiyo mlitaka mimi nifanye nini..

‘Ni kweli nafahamu nilivunja miiko ya ndoa, nikaondoka kwetu, sehemu nilipopewa kama kwangu, ..nilikiuka miiko ya ndoa nikakimbia sehemu ya mume wangu, nakiri hilo ni kosa, lakini nililifanya hili kwa makusudi..ili nijiokoe..na sikwenda kwetu, nilikwenda kuishi kwa shangazi yangu.

‘Huko kwa shangazi yangu, binamu yangu alikuwa amejifungua mtoto mchanga, na akawa anasoma,..kwahiyo nikawa mimi ndio mlezi wake,..ndio maana nikawa sipati muda, kulea mtoto sio mchezo, na..sijui labda, hao walioniona na mtoto ndio walichukulia hivyo, labda…mimi sijui..kwani binamu yangu alikuja akachukua mtoto wake wakaenda kuishi Dar na mumewe…’akasema

‘Kumbee….’akasema dereva, na kukawa na ukimia kidogo na aliyeongea sasa alikuwa baba …


‘Pole sana mkwe wangu, nikuombe radhi, nimekosa na sikuwa nimejijua kipindi hicho, nasikitikika sana, kwa hayo niliyokutenda, nataka niitoe hii kauli haraka, maana ya mungu mengi,.. ndio maana hata nilipoumwa, nilitamana nife tu….ila nilipomuona mtu wangu, ambaye ninajua atakuja kuusema ukweli, na kunisafisha,… nilijua hilo litakuja kufanyika, lakini  kwa vipi, niliongea na mke wangu kuwa ili hilo liweze kusubiriwa hadi wakati muafaka mke wangu amshawishi mkwe, ili aubebe mzigo, anyamaze na kutokusema lolote, nashukuru kuwa aliweza kulifanya hilo…’ilikuwa kauili ya baba mkwe pale kitandani.

‘Hebu nyamaza huko, huoni umenitia aibu…’akasema mkewe.

‘Lazima nitubu mke wangu, usione hivyo ukafikiri nilipenda, mke wangu nilikupenda sana, kuondoka kwako ilikuwa kama nimekatwa sehemu ya mwili wangu,..kila nikiwaza najikuta naumia, na nikaona pombe ndio dawa , kumbe ndio najiumiza, nasema hayo kiukweli, mnisamehe sana…samahani kwa kukukatiza ila liweke moyoni kuwa nahitaji msamaha wenu wewe na mke wangu..’akasema akimuangalia mkwewe na mke wake.

‘Baba mimi nilishakusamehe, nilijua sio wewe, ni udhaifu wa kibinadamu na pombe..sipendi kabisa pombe, lakini niliamua kukuvumilia,..na isingelikuwa hivyo, ningelishaondoka..isingelikuwa ni mama, kuonyesha mapenzi yake kwako, kuwa pamoja na hayo alikuwa tayari kukusamehe, ila alitaka ukweli,…alitaka kuhakikisha familia haitaumia baadae, ila ilimuuma sana ulipoamua kutembea na rafiki yake, na nimejua ukweli huo kupitia kwangu…’akatulia.

‘Sikuweza kuja kuusema ukweli mwingine kwa mama, japokuwa aliniomba sana nisema, lakini nilijua nikisema je ikiwa sio kweli…lakini watu walishasema wapo tayari kunipeleka kunihakikishia kuwa mume wangu ana mke mwingine na wameshazaa naye…’akatulia

‘Sikutaka kulisema hilo kwa mama japokuwa mama aliniomba sana,…aliniona nilivyokuwa sina raha, ..lakini nilisubiria wakati muafaka, ili niweze kuupata ukweli, na ushahidi kamili…’akatulia.

‘Na ghafla siku ya siku naletewa mtoto, mtoto anafanana uso kwa uso na mume wangu,kama nilivyoambiwa kuwa mtoto huyo anafanana na mume wangu…hebu niambieni hapo unaweza kusema nini….ni kuwa kumbe kweli mume wangu alikuwa ana mke mwingine…’ akasema akimuangalia mama . Mama mkwe akawa kainama chini tu.

‘Sasa nichotaka ni ukweli kutoka kwa mume wangu,,…autamke ukweli mbele yenu kuwa hayo yanayosemwa ni kweli au si kweli..na huyo mtoto aliyeletwa kwangu ni wake, na kama ni wake, huyo mke wake yupo wapi…na kwanini asiwe wake na ushahidi upo, unajionyesha, huyo mtoto anafanana na nani…’akatulia na kugeuza uso , sasa kumuangalia Soldier.

Soldier alikuwa kanyamaza…yaonekana alikuwa akiwaza….akatikisa kichwa kukataa na akasema;

‘Mimi sielewi kitu….dereva, kama upo nyuma ya haya, utaniona mbaya…..’akasema na dereva akacheka kwa dharau. Na mke wa Soldier akaendelea kuongea;

‘Kinachoniuma zaidi ni kuwa mume wangu aliporudi akaanza kunisakama mimi kuwa sikuwa muaminifu kwake, nimefanya madhambi na mungu kanidhihirisha kwa kupata mtoto, akaniuliza je huyu mtoto ni wanani,..kama kweli ni wa baba yeye ataondoka kabisa kijiji hiki ili aniachie nafasi, kama ni mtoto wa …dereva basi, ajua jinsi gani y akufanya, kwani na yeye ana mke kama mimi..sasa sijui hapo alikuwa na maana gani….’akatulia.

‘Mimi namuuliza sasa huyu mtoto akiwa ni wake,..mimi nifanyeje…asema, kama yeye alishatoa maamuzi kama hayo, na mimi nitoe maamuzi gani ikiw huyu mtoto ni wa kwake….?’

Soldier kwanza alishikwa na kitu kama ganzi, akabakia ameduwaa, akajaribu kufikiria, hayo yametoka wapi…mbona haelewi kitu,…mbona anazushiwa kitu ambacho hakifahamu…. baadaye akasema;

‘Umemaliza mke wangu…?’ akauliza

‘Sijamaliza, nitamaliza pindi ukinijibu swali langu ili niweze kuendelea na kutoa maamuzi yangu...’akasema.

‘Mke wangu, kwanza hebu rejea maswala ya baba, baba ameshutumiwa na mambo mengi tu, na mengi  ya hayo ni uzushi mtupu,…yamedhihirika hapa, na utaona mengi hutungwa na wanadamu na wengi wao ni ndugu wa karibu tu,…ukisema mtoto kufanana na mimi bado kuna dereva anafanana na huyo mtoto mbona yeye humshiki shati…

‘Dereva nilishaongea naye, na nikafuatilia nyendo zake, ..kuna watu walimchunguza kama yeye kama kweli huyo mtoto ni wake, na la kujiuliza ni kwanini amkatae mtoto wake, kama ni wake…kiukweli inaniuma sana, kwani nyie wanaume mpoje, kama umezaa umeshazaa, iliyobaki ni kusema ukweli tu.., jinsi unavyoficha huo ukweli ndio jinsi mnavyotutesa sisi wanawake pindi tukigundua ukweli.

‘Au unaogopa kuhusu huyo mwanamke uliyezaa naye, itakuwaje kama unaliogopa hilo kwanini, ulitembea naye, ulipopanda mbegu ulitegemea nini, na hayo ni maswala ya kukubaliana, maana ni wewe mwanaume ndiye mwenye maamuzi, kidume, au sio…hahaha’ akasema akijilazimsiha kucheka.

‘Kama ni mtoto wako, mtambulishe, mimi sina wasiwasi, hata hivyo nimeshachukua maamuzi yangu,nasubiria nikusikie utakavyojitetea,…nilikupa muda wa kuniambia ukweli, na muda huo umeshapita, na sasa nakupatia muda wa mwisho, ….’akasema akimuangalia Soldier.

Soldier alitikisa kichwa kama kusikitika, akainama kidogo chini, halafu akainua uso na kumkabili mkewe, akasema;

‘Mke wangu sijui nikuambieje, kiukweli mimi sijui hayo yametokea wapi..mimi nilikuwa vitani, nilikuwa maeneo mbali na raia, sasa sijui hilo la mtoto, la mke,limetokea wapi…na sijui kwanini unakuwa kama unamtetea Dereva,..jamani kama mtoto huyu sio wa kwangu, basi ni wa dereva,..’akasema akimgeukia baba yake.

‘Mini sijui kwanini namuhisi vibaya huyu ndugu yangu wa kufikia, yawezekana ni mbinu zake chafu,,,na niwaulize jamani..hivi mnafahamu maana ya vita,..ndio kuna muda mnapata nafasi ya kutoka nje…, inatokea mnaweza mkatembea tembea lakini ni muda mfupi tu, sisi tupo kwenye mikataba ya kimataifa kuna masharti yake…hebu nikuulize hao watu waliokuambia hivyo walisema waliniona wapi…?’ akauliza

‘Hilo kuwa wewe walikuona wapi, kwangu, sizani kama lina mantiki, mimi ninachotaka ni jibu lako la ukweli, Je huyo mtoto ni wako au sio wako, kama si wako sawa, basi huyu mtoto hana baba, ila mimi nitakuwa mama yake, hilo nimeshaamua hivyo, na atakuwa mtoto wangu wa kwanza, nitamlea, na tutaishi naye, nimeshaanza maisha yangu, najua nikiwa naye atanipa faraja, je ni mtoto wako au sio wako…?’ akauliza

‘Mke wangu huyo mtoto sio wa kwangu, unataka nisemeje ….atakuwaje wangu, ningezaaje, na nani…?’ akauliza sasa kwa sauti ya hasira.

‘Kwahiyo unamkana mtoto wako mwenyewe…’akasema mkewe akitabasamu ile ya kusikitika

‘Aaah, sasa hapo sikuelewi, hebu niambie wewe unataka nisemeje, maana huyu mtoto awali alifikiriwa ni mtoto wa baba,…ikaonekana ni uzushi,…. haya akaja kufikiriwa ni wa dereva, na wengi walijua kuwa huenda mumeshirikiana naye, lakini wewe umelikana hilo, haya mimi unataka nikubali tu wakati mtoto sio wangu…’akatulia, halafu akamgeukia dereva

‘Dereva,  hebu ndugu yangu..,sema ukweli tuondokane na shutuma hii tuendelee na mambo mengine, unajua ukitaka nitumie nguvu nitatumia, na ukifika wakati huo, hutaamini kuwa mimi kweli ni ndugi yako…’akasema Soldier akimuangalia Dereva.

‘Hahaha, bro bwana..mimi hapo sina usemi,…hayo ni yako wewe na mkeo, na nikuambie ukweli bro, kama sio baba kama walivyosema watu, basi huyo mtoto ni wa kwako, angalia mnavyofanana na wewe, …’akasema akicheka kama mdhaha, hakuonyesha wasiwasi wowote.

‘Hahaha, lakini pia anafanana na wewe…sasa mumebakia nyie wawili, ni nani mwenye huyu mtoto, mtuambie ukweli…kama baba yenu keshatoka hapo, sasa ni nyie wawili, au labda mna ndugu mwingine anayefanana na nyie, maana bab zenu hawaaminiki…’aliyesema ni mama

‘Mama,..kama angelikuwa huyo ni mtoto wa kwangu, ningemchukua mara moja,  mama, ni mwaka sasa, tunatafuta mtoto mimi na mke wangu..tunataka mtoto hatujampata…unakumbuka mimi nilioa mapema kabla ya bro…lakini sijachelewa, tutampata mtoto muda haujafika tu, sasa kama ingelikuwa ni mimi nimezaa nje, mbona ingekuwa poa tu, maana ningeenda kumringishia mke wangu kuwa mimi nina mtoto, yeye ndiye ana tatizo..lakini …’akatulia

‘Kwahiyo wewe huwezi kuzaa..?’ akauliza na Shemeji, kaka yake mke wa Soldier.

‘Nani kasema siwezi kuzaa wewe, mimi nimepima kila kitu kipo sahihi, ila muda muafaka bado, tutampata mtoto tu mungu akipenda, na…kama huyo angelikuwa ni wa kwangu, ningelishamchukua,..mke wangu anapenda sana watoto…’akasema

‘Wawili chini..bado mmoja…’ akasema baba akiwa kitandani, na wote wakawa wanajiuliza ana maana gani.

‘Hahaha baba kama mtoto, familia hii puuuh,  haya sasa Soldier, ongea, si unataka kutupeleka polisi sisi, unatuona sisi ni wahalifu, je hilo ulilofanya sio uhalifu,..  kumbe wewe ni kiwembe kama baba yako, ..simba mwenda pole, nilijua tu…sasa hilo, …ukicheza tu umempoteza mke,…na uking’ang’ania na dhamira yako, ya kunifikisha polisi, …nitakuumbua ukweli wa kukuumbua…’akasema Shemeji yake.

Soldier akamuangalia shemeji yake huyo, halafu akatabasamu, na kutikisa kichwa kama kusikitika,… akageuka kumuangalia mkewe kwa muda tu, halafu akageuka kumuangalia mama yake, …akatikisa kichwa, hakusema hivyo ila akilini alijikuta akisema, `hata mama… haniamini..’

Akili haikuelewa chochote, ni kwanini wamemshuku yeye, haelewi….na mara kikohozi kidogo kikatoka kwa yule mdada mgeni, kuonyesha kuwa anataka kuongea…

‘Na mimi naweza kuongea kidogo…’akasema huyo mdada, lakini alionekana akisitasita, kama anaogopa. Dereva, akamuangalia kwa mashaka, na aliyeonyesha kushtuka zaidi ni shemeji, alikunja uso akimtizama huyo mdada….

Yule mdada kwanza akamtizana sana dereva, halafu Soldier, kabla hajaanza kuongea…

NB: Mhh, naona imekuwa ndefu sana


WAZO LA LEO: Uongozi ni dhamana, na dhamana hiyo ni deni kubwa, wengi wetu tunapopewa dhamana hiyo tunachofikiria zaidi ni masilahi yetu binafsi kabla ya kulipa gharama ya dhamana hiyo. Uongozi wa kuongoza watu ni dhamana kubwa zaidi, yahitajia hekima, busara, na kujitolea kwingi, na wakati mwingine inahatarisha hata maisha ya mtu. Wenye uelewi mkubwa hawapendi kuibeba dhamana hii, hata kama ina malipo kiasi gani, lakini inabidi, kama mungu kakujalia kipaji hicho na uwezo unao inabidi, basi kama tumeamua hivyo, kuibeba dhamana hiyo, tujitahidi kutimiza masharti na miiko ya uongozi la sivyo, tutakuwa tunajibebea mizigo mizito ya madhambi, na adhabu yake inaweza ikakutesa kuanzia hapa hapa duniani.
Ni mimi: emu-three

No comments :