Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, March 23, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-25


 ‘Unajua hii familia naichukia sana, nilimuonya sana dada yangu asiolewe kwenye hii familia, lakini akaleta ubishi,…unaona sasa, wamefikia hatua hiyo, eti….umezaa na nani na huyu tapeli, ….hivi kweli mumekosa la kusema..’ akasema huyo jamaa akimuangalia Soldier.

‘Lakini hakuna aliyesema kuwa dada yako kazaa na dereva,…kama nimesikia sawa..’akasema Yaya.

‘Haya kazaa na nani…?’huyo jamaa akauliza akimgeukia Soldier.

‘Sikiliza shemu, wewe umekurupuka tu, na jaziba zako…, ngoja nikuambie ilivyo, huyu dereva, kwa maelezo yake anasema dada yako kabeba mimba akatupa mtoto…kweli sikweli….?’ akamuuliza dereva.

‘Kweli kutokana na taarifa nilizozipata ..’akasema dereva

‘Kutoka kwa nani..?’ akauliza Soldier

‘Kutoka kwa raia wema ambao walimuokota huyo mtoto, na mmojawapo ni huyo dada hapo mgeni …’akasema dereva, na watu wakageuka kumuangalia huyo mdada aliyejifunika uso.

‘Mlikutana naye wapi, akakuambia hayo…?’ akaulizwa

‘Nikiwa kazini, mimi ni mmoja wa watu wanaoshughulikia, kusaidia wakimbizi, na nilichaguliwa kiongozi wa kundi lililopelekwa huko ncho ya jirani…’akasema

‘Hao raia walithibitishaje kuwa huyo aliyemtupa mtoto ni mke wangu…?’ akauliza Soldier

‘Raia wengi tu, akiwemo kiongozi wa eneo lile,…walisema kuna mdada mmoja alikuja na mtoto, akawa anazunguka zunguka naye, baadae huyo mdada akatoweka…baadae wakapata taarifa kuwa kuna mtoto ameokotwa, akaletwa pale ofisini …’akasema na kabla hajamaliza, Soldier akadakia kwa swali jingine.

‘Ndio ulijiridhishaje kuwa kweli huyo aliyemtupa mtoto ni mke wangu…?’ akaulizwa.

‘Walivyomuelezea sifa zake, mpaka jina,…sura , umbile,…nikasema huyo mtu namfahamu mimi, sikusema pale palekuwa namfahamu nilitafuta njia ya kuhakikisha hiyo damu inarejea kwa wenyewe..na hata hivyo nikiwa pale bado nilikuwa sina mawazo hayo maana majina yanafanana..mpaka nilipofanya uchunguzi ….’akasema.

‘Uchunguzi gani ulifanya..?’ akaulizwa.

‘Nilipotulia, niliamua kupiga simu huku, kwa watu ninao wafahamu, nikawauliza, kuhakikisha jina, kama ni sahihi..ndio nikaambiwa mambo yaliyonihakikishia kuwa ni kweli…’akasema

‘Hapo bado hukutakiwa kuhitimisha kuwa mke wangu ndiye kafanya hivyo, maana hapo kikubwa umefuat ushahidi wa kimaumbile, …hivi wewe ukifanya kosa mimi nitahukumiwa kwa kosa lako, maana sura na maumbile yetu yanafanana…?’ akaulizwa

‘Mimi nilipomuona huyo mtoto anafanana na na mzee, nikawa na uwezo wa kufikiria hivyo, ukiunganisha, hayo niliyoambiwa,..na ni kweli mtoto anafanana na nyie..na kwa vile wamemtaja mke wako kwa jina…, na niliambiwa shemeji hapa alitoroka nyumbani kwake, ..karibu mwaka sasa…nikauliza uliza habari za huku…nikajua ni mke wako…’akasema, halafu akamgeukia kaka yake Soldier.

‘Unabisha kuwa dada yako hukuwahi kufika kwako...akiwa na mtoto mchanga, yule mtoto aliyekuja naye yupo wapi, alikuwa wa nani,...je hukuwa unaishi naye huko…nchi ya jirani..?’ akauliza na jamaa akawa kimia, jamaa alionekana ana hasira zake tayari.

‘Usiniulize maswali ya kijinga mimi,... ndio dada yangu huwa mara kwa mara anakuja kwangu, na kama alikuja na mtoto au yeye mwenyewe haijalishi , yeye ni ndugu yangu, kuna ubaya gani hapo…’akasema kwa hasira

‘Uliwahi kukutana na mke wangu kabla..?’ akaulizwa dereva na Soldier. Soldier, hakutaka kumuuliza swali shemeji yake,  alijua huo sio wakati muafaka.

‘Zamani sana…kabla ya hapo,…’akasema na kabla hajatoa maelezo, akaulizwa swali jingine.

‘Kwahiyo hukuwahi kumuona mke wangu akiwa mja mnzito..?’ akaulizwa

‘Sikuwahi…mimi nina muda mrefu sijaonana na mke wako, huwa nilikuwa nafika huku lakini sikuwahi kukutana naye…kama nilivyosema yote hayo niliyasikia kutoka kwa watu..na nikapiga simu kuulizia watu wahuku, nikaambiwa huyo mdada alitoroka nyumbani kwao, kwa visa vya baba mkwe wake…nanukuu walivyosema…’hapo akatulia.

‘Walikuambia alitoroka akiwa mja mnzito..?’ akaulizwa

‘Hapana,..sikuwahi kuuliza hilo swali, ukweli ni kuwa mke wako aliondoka nyumbani kwao muda…sijui kama alikuwa akirudi rudi au vipi, watu wengi wanahisi alipoondoka alikuwa mja mnzito, …’akasema na mara akaingilia shemeji yake Soldier akicheka;

‘Hahaha, baba mkwe, hahaha, mumesikia jamani, baba mkwe, anafanya uchafu huo, dada kama ni kweli niambie...au kama huyu muhuni anakusingizia niambie...'akasema shemeji. halafu akamgeukia dereva

‘Haya wewe dereva elezea, hivi visa vya baba mkwe, baba yenu vilikuwaje, maana nataka kukusanya data…, ili huyu anayejifanya mtu wa usalama, achukue hatua...'akasema akimgeukia Soldier

‘Ndio maana nimesema sitaki kuliongea hili maana litazidi kumuathiri baba, na naona mnaongezea mambo mengine ya kuharibu ajenda yetu, mimi nakuomba ndugu tuende kwa utaratibu, wewe sijui mna nini na bro, lakini…’akasema dereva na Soldier akaingilia kati kwa kusema.

‘Kwanini limuathiri baba, wakati unafahamu fika kuwa wewe ndiye muhusika mkuu wa haya yote, najua hilo litakuwa wazi, wewe ndiye mchonganishi ….wewe unatumia ujanja ujanja wako kuwarubuni watu, kugonganisha familia…, na sasa umejaribu kukwepesha makosa yako yaende kwa mtu mwingine…’akasema Soldier.

‘Nisikilizeni jamani, kwanza sio kwamba naingilia kauli yako mwanangu maana hayo ni mambo ya usalama, lakini nakuomba mwanangu achana na hisia zako kwa ndugu yako,...mimi ninataka tuyamalize haya matatizo ndani ya familia, nataka ukweli wote leo ubainishwe, tuoambeane msamaha…’akasema baba mtu.

‘Baba usijali,…haya tutayamaliza tu…ila kama kuna wakosaji ni lazima sheria ifuate mkondo wake, hilo siwezi kulipinga baba..lipo juu ya uwezo wangu...’akasema Soldier.

‘Sawa Soldier, nimeshakukabidhi kijiti endelea, na ajenda yetu, mimi nipo sawa, naweza kuhimili lolote lile, kwahiyo, ongeeni tu, ila mimi nitakuwa msikilizaji tu …msiwe na wasiwasi na mimi…mimi nina uhakika mhalifu wa haya yote yupo hapa, nimeshamuona ni nani, sasa kama familia tutajua tutamfanyaje sio lazima sheria za kimahakama..’akasema baba yao..

‘Baba mimi nilisikia tu, usinisakame bure mimi, sikuwa na haja ya kukuharibia hadhi yako , ila niliongea kutokana na watu walivyosema na ni baada ya uchunguzi, na haya mengine ni kwa manufaa ya familia, je mngelikubali damu yenu ipotee, mshukuru mtoto wenu sasa yupo mikononi mwenu…’akasema dereva

‘Dereva, wewe muda wote huo,ulikuwa wapi..?’ akaulizwa

‘Muda upi , kama ni kabla ya kufika huko nchi ya jirani kwenye kambi ya wakimbizi, mimi nilikuwa nasoma, nilikuwa nje ..huko kwa wenzetu, tulikuwa na mafunzo ya jinsi ya kuhudumia wakimbizi..na mambo mengine kama hayo…’akasema.

‘Na mlikuwa mnapata nafasi ya kurudi rudi kutembelea wakimbizi..?’ akaulizwa.

‘Ndio, lakini sikuwahi kupangiwa maeneo ya kanda za huko, mpaka ilipofikia muda huo wa tukio, unielewe hapo… sikuwahi kufika huko kabla’akasema dereva.

‘Una ushahidi na hilo, kuhusu ratiba yako….maana nitaagiza watu wafuatilie,…?’ akasema Soldier.

‘Ndio ninayo,… ratiba zetu hazina usiri, na , …hahaha bro, unafikiri mimi ndiye baba wa huyo mtoto..hapana bro… nisingeliweza kufanya hivyo, napenda sana watoto, kama angelikuwa ni wa kwangu nisingelimkataa….na muulizeni huyo mdada aliyemleta huyo mtoto, kama niliwahi kukutana naye kabla,…’akasema dereva.

‘Kwasababu ni uwongo…wewe umekuwa unafanya kazi za utapeli, kuhadaa watu ili kupata mali, ilimradi tu upate pesa na mali, ndio maana hakuna anayekuamini…’akasema baba yake.

‘Lakini baba ngoja kwanini tunazunguka, wahusika wakuu wa hii ajenda wapo hapa, mimi nahisi tumpatie nafasi huyo mdada mgeni aongee aseme ukweli, pia yupo shemeji hapa aongee kama kweli huyo mtoto sio wa kwake, na kama ni kwake je alizaa na nani…?’’akasema dereva akimuonyeshea mke wa Soldier, na wote wakageuka kumuangalia mke was Soldier.

Soldier akasema, bado hatujafikia huko, sijamalizana na wewe…’akasema Soldier , lakini watu wengi walikuwa wamemgeukia mke wa Soldier.

Mke wa Soldier alikuwa kimia, akiwa kaangalia upande mwingine , baadae alipoona kama vile watu wanamsubiria aongee, akamgeukia mama mkwe wake…alimuangalia mama mkwe wake kwa muda bila kusema neno na mama mkwe akasema;

‘Jamani haya mambo naona yanatakiwa yamalizike, …hatuwezi kuzunguka, na kupotezeana muda, wengi naona mnamnyoshea kidole mkwe wangu, kuwa sijui kazaa,, halafu akatupa mtoto, swali alizaa na nani, wakati mume wake alikuwa hayupo..au sio?’akauliza mama

‘Ndipo hapo tunautafuta huo ukweli…kama alizaa , alizaa na nani, maana ukweli wa kuzaa upo wazi, yeye kama sio kweli aupinge, watu walimuona, sasa ataupingaje, kama anasingizwa basi aseme, …’akasema dereva

‘Dereva wakati nilipokuuliza kuhusu wewe, kuwa watu wanasema kuwa wewe ni mtoto wa mume wangu ulisemaje..?’ mama akamuuliza.

‘Nilikuambia mimi sijui..maana mimi ni mtoto tu na mengine yawezekana ni kusingiziwa tu, ila tuache ukweli utasema wenyewe…, na wakubwa ndio wakuulizwa sio mimi, nilikuambia hivyo au nimekosea…’akasema dereva.

‘Hayo uliyasikia watu wakisema na hukuyachukulia kuwa ni kweli au sio,…Sasa kwa hili, acheni ukweli useme, na waulizeni wakubwa, msimsakame mwanangu, huyu binti hapo alipo amefungwa na masharti, sasa labda nimuulize mume wangu, ..je upo tayari kwa lolote lile…?’ mke akamuuliza mumewe.

‘Nimeshasema, kwani kuna tataizo gani, mimi nipo ok…nafahamu mke wangu mpaka sasa hujaniamini, unahisi labda kweli yanayosemwa na watu yana ukweli…mke wangu ni kweli nilikuwa nalewa, ni kweli nilikuwa napitiliza, naweza kukosea chumba na kwenda kulala kwa eeh, mkwe,..lakini nalala sakafuni, nilizidiwa kipindi kile, lakini nisingeliweza kufanya tendo kama hilo,..nina uhakika na hilo …’akasema.

‘Hahaha mzee umejileta mwenyewe, umesikia mdogo wangu..?’ akasema Shemeji akimuangalia dada yake.

‘Huyo ni baba mkwe wako anakiri mwenyewe kuwa ni mlevi, analewe anapitiliza anakuja chumbani kwako, anakuja kufanya nini, halafu bado unataka ….kung’ang’ania ndoa,..unataka uchangie mume pamoja na baba yake…hahaha, mimi hilo sitalikubali kamwe, kuanzia sasa wewe …’akashindwa kumalizia.

 Mama akawa kamgeukia mumewe, akisubiria kama mume wake ana maelezo ya ziada, na lipoona mume wake yupo kimia akasema…

‘Mume wangu mimi nimekuuliza je upo tayari kuyasiki hayo atakayoyaongea mkwe wako, yaani mke wa mwanetu, maana kuja kwake huku, kwanza ni kukuona , halafu ni kuhitimisha matatizo yake na mumewe..amesema leo anakuja kuusema ukweli wote,…mimi nilimuambia asubirie kwanza maana wewe hujawa sawa…’akatuliza

‘Mimi naona baba hayupo tayari…tunakimbilia mambo ambayo yaweza kumuathiri baba, kwanza niachieni mimi nifanye kazi yangu, mnivumilie tu,… nitawahitaji dereva na shemeji tukitoka hapa tupitie polisi, kuna maongezi na mahojiano,…ni utaratibu tu wa kawaida, na huko najua tunaweza kuupata ukweli wa haya yote bila kumsumbua baba…’akasema Soldier.

‘Kwanini unipeleke polisi, kwa kosa gani, …?’ akauliza shemeji mtu.

‘Nimesema ni maswala ya kawaida, mtahojiwa na mkimaliza mtaruhusiwa, kama hamna makosa mna wasiwasi gani…?’akasema Soldier kama kuwauliza.

‘Huko mimi siendi, …kwanza niambie nina kosa gani , naenda huko kuhojiwa kwa kosa gani, hiyo ni haki yangu kufahamu…kwanza mimi nina aleji na vituo vya polisi, unasikia , na pili wewe wewe kama nani wa kuniamrisha niende kituo cha polisi, wewe ni askari wa vita sio polisi, na kwasababu hiyo mimi siwezi kwenda huko…’akasema

‘Nina RB, ya kufanya hivyo, sio kwamba nakurupuka tu….utaratibu wote umefuatwa, mimi nimechukulia hivi kama ndugu, kuliko waje wawakamate wawatie pingu, nikasema mimi nitawachukueni kistaarabu tu…’akasema akitoa karatasi ya kuonyesha hiyo RBi.

‘Swali bado hajanijibu nimefanya kosa gani…?’ akauliza shemeji mtu.

‘Huna kosa,..unasikia, kosa ni mpaka lithibitishwe na ndicho hicho wanataka kufanya, sio nyie tu kuna wengi wanaitwa kwa kuhojiwa, ni mambo ya kawaida, ya ulinzi na usalama, na sijui kwanini uogope, sijui kwanini ukatae, ukikataa basi nitaiachia sheria ichukue mkondo wake…’akasema Soldier.

‘Jamani hayo ni yenu, hebu kwanza tumalizane na hili…’akasema mama akimuangalia mume wake.

‘Mke wangu hilo nalo ni kubwa, linahusu jamaa zetu, au sio ni muhimu kujua nini kifanyike, hata kama wataenda tuwe tumejipanga kwa lolote lile, ..mimi kama kiongozi wenu sina shaka, najua hayo ni mambo ya usalama tu, sioni kwanini mkatae kwenda huko…na mke wangu unasemaje, ….maana akili ilikuwa imeshutuka, unataka nifanye nini sasa, ok, tumalizane na hili letu au sio..?’ akauliza baba yake Soldier.

‘ Kwa hivi sasa tunahitajia kauli yako, kama kweli utaweza kuhimili hayo yanayotaka kufanyike, je kweli upo sawa kuhimili lolote, maana mkwe wako anaweza kuanza kuongea mambo ambayo yatakugusa, halafu ukadondoka kwe presha…’akasema mkewe.

‘Kitu gani cha kunidondosha mimi kwa presha…, mimi sina wasiwasi mke wangu, kwa vile muhusika wa haya yote yupo hapa, na yupo tayari kutoa ushirikiano,…hana ujanja ni lazima atoe ushirikiano,… mimi ni askari mstaafu, naweza kumuhisi muhalifu kwa kumuangalia tu…’akasema akimuangalia dereva, na dereva akatabasamu, na kusema;

‘Baba…tatizo labda unahisi bado nipo kwenye yale mambo yetu, hapana mzee, kule nimeachana nako kabisa nilikuwa na maana yangu na maana hiyo imeshakamilika, sina shaka tena, na nafahamu bro anataka niende polisi kwasabau gani, na hilo kwangu halina shaka, mimi siogopi kwenda huko, na itakuwa vyema kabisa maana sasa mambo yapo hadharani, na yale yangu na baba, tulishayamaliza, au sio baba,  yale yamepita maana ukweli sasa upo mezani, kwahiyo yanayofaa kuongewa yaongewe tu,…’akasema dereva.

‘Kwahiyo wewe unatuthibitishia kuwa huyo mtoto sio wa kwako…?’ akauliza mzee.

‘Huyo mtoto sio wa kwangu baba, maana sijawahi kutembea au kuja huku na kukutana na ..’akageuka kumuangalia mke wa Soldier,

‘Muulizeni…shemeji aseme ukweli,…na kwanini mzee, tunarudi nyuma, na labda mtasema kuhusu huyo binti mgeni, mimi sijawahi kukutana na huyo binti mkimbizi kabla, sikuwahi kumfahamu kabla kama unafikiri mimi nilikula njama na yeye,..unasikia na kulithibitishia hilo,, mpeni nafasi huyo binti aongee ukweli, aeleze alivyomuokota huyo mtoto, na jingine mnaweza kuwasiliana na uongozi wa huko , alipookotewa huyo mtoto…’akasema.

‘Mhh…hapa naona hatuwezi kufikia muafaka, maana mara mke wa Soldier aongee, sasa mnarudi kwa huyo mgeni, yupi na yupi mnataka awathibitishie lipi…?’ akauliza mama.

‘Soldier…ongoza kikao, mimi nitakuwa msikilizaji…’akasema mzee.

‘Jamani naona nianze  kuongea mimi…..’aliyesema sasa alikuwa mke wa Soldier, na Soldier mwenyewe akamkazia macho, kama kuonyesha mashaka fulani,  lakini mkewe hakutaka waangaliane, maana ukitaka kumuua nyani msiangaliane machoni.

‘Wazazi wangu, na ndugu na jamaa zangu….naongea hili kutoka undani wa moyo wangu…’akaanza kuongea.

NB: Hii sehemu nimejaribu kuweka mambo mengi kwa pamoja, ili tuharakishe kukimaliza hiki kisa, sijui kama nimekosea?


WAZO LA LEO: Mnapotaka kutoa hitimisho la jambo, iwe ni hukumu au uamuzi fulani, ni muhimu kuwe na mizania ya usawa, ya kuwahusisha wale wote wanaokisiwa kuwa watendaji au wakosaji. Tusipendelee kuangalia upande mmoja eti kwa vile ni ndugu, rafiki au chama au imani moja, haki itapatikana pale wewe msemaji au mtoa hukumu, utakapoweza kuwasikiliza wote bila kubagua, na ukaweza kupitia ushahidi, …uchunguzi na tafikiti yakinifu. Tusipende kuhukumu kwa kusikia tu.
Ni mimi: emu-three

No comments :