Nikiwa nimetokea kwenye mikutano, sasa nikawa natembea kuingia
hotelini mwangu, kama kawaida nilipitia ufungu wangu wa chumba, wakati sasa
naelekea kwenye eneo ambapo kuna chumba changu, ndio nikamuoana mdada mmoja
kakaa mlengo wa chumba changu, nikajua labda ni muhudumu tu, nikatembea kwa
tahadhari hadi pale mlangoni;
Wakati natembea kuelekea hapo mlangoni nikawa najiuliza maswali mengi,
iweje huyo mtu akae mlangoni mwangu, na kwanini kule mapokezi hawakunipatia
taarifa kuwa nina mgeni wangu ananisubiri, kama utaratibu wao ulivyo, machale
yakanicheza..…yawezekana ni mtego…hapo nikasimama kidogo..
Alikuwa mdada, kajifunika kitu kama shuka nyeupe, imechakaa,..na kuna
sehemu ya nyingine kwenye hiyo shuka ni kama imeungua,…na kuna alama za damu
damu, hapo mwili ukazizima, damu zimetokea wapi, na ule mkao ni wa masikitiko, mtu anakaa
miguu inakuja karibu na kichwa, kainama hataki kuniangalia… inatia huruma
kumuona, ..
Lakini kilichonivuta zaidi ni ..pembeni yake kulikuwa na mtoto
mchanga, kalazwa, ikiashiria huyo mama ni mzazi, ….sasa kafuata nini, na ni
nani huyo;-
*****************
Nilibaki nimeduwaa…
Nilipeleka macho yangu kumtizama yule mtoto…ni mtoto mchanga, anaweza
akawa na umri wa chini ya mwezi mmoja hivi,..au
mwezi mmoja kamilizi, ni sizani ni zaidi ya hapo. Kichanga kile kilikuwa
kimelala. Nikamgeukia huyo mzazi, nahisi atakuwa ni mama yake:
'Wewe ni nani, mbona upo hapa?'nikamuuliza nikimkagua vyema, kama
nilivyosema nguo zake zilikuwa kuu kuu..zimechanika, na alama za damu na
kuungua ungua!
Na huyo mwanamke aliinua kichwa
taratibu kama hana haraka, na kuniangalia, kwa mashaka, na yanyesha alikuwa
hataki nimuone, ila yeye alitaka kuniona mimi sura yangu, au kuhakikisha jambo,
maana aliinu uso taratibu lakini akaufunika kwa haraka.
Oh..nikahisi mshituka,..uso wa huyu mdada,…oh,… kafanya nini, au
kafanywa nini....oh ..hapana;
'Mbona uso wako upo hivyo,……
uliungua...?'nikajikuta namuuliza.
Hakusema kitu, nikahisi kama
analia...ni kweli analia, alitoa ile sauti ya kulia, moyo unakizizima kwa huruma.
Kwa muda huo mfupi, mandhari ya hiyo hali , mtoto mchanga, haya huyo mama ana
majeraha usoni, kama ya kuungua, vyote hivyo vikanifanya niingiwe na huruma,
nikimuangalia kwa makini, kuwa
yawezekana ni mtego, kama ni mtego, nilitaka niwe makini sana,..
Kiuharaka haraka akili yangu ikanituma kuwa huyo mzazi atakuwa ni mkimbizi,! Lakini alifanya nini mpaka
yamkute hayo madhila, huenda mumewe kauwawa, na kutokana na hali ya kivita akawa ametengena na familia yake..nikawa hivyo.
Jamani usiombe hiyo hali ya ukimbizi uwakute, watu wanapata shida,
wanakimbia majumbani kwao kuishi maporini, kama kuna ambao yaliwakuta kidogo, kumbukeni mabomu ya gongo la mboto, ilikuwaje, sasa hayo ni ya muda mfupi, hawa wenzetu mwaka, wanataabika,..
Inafikia muda…wengine wanapoteana, mke na mume,
wazazi na watoto, .. wanaacha nyumba zao na kukimbilia maporini, wanapokimbili napo hawajui usalama wao
utakuwaje…
Yaani inafikia muda watu wanawakimbia wanadamu wenzao, …wanadamu
wenzao wameshageuka kuwa wanyama,..watu wanauana ovyo, hawaogopi tena kumwaga damu ya wanadamu wenzao, …ni kwanini….watu wanaona ni heri wakutane na wanyama porini, kuliko kukutana na wanadamu wenzao, ndivyo ilivyowakuta wenzetu hawa,…vita sio kitu cha kuombea, na kama kuna watu wanafanya hayo, kwa masilahi yao, sijui mbele ya mungu watakuwa wapi,..
Sasa kama huyu ni mkimbizi,
sheria itanibana sana, hata kama nitataka kutumia ubinadamu , maana mtu kama
huyu anahitajia msaada wa kibinadamu, japokuwa huko kambini wanahudumiwa lakini
yawezekana kaona huko hapati huduma stahiki…hata hivyo, hakustahili kuja hapo,
nashangaa alipitaje kule mapokezi,..na kwanini aje mlangoni kwangu hapo
nikabakia na mashaka.
Mimi mwenyewe kwenye mikutano,
kama kiongozi, nililiongelea hilo, kuwaonya wakimbizi kuwa wafuate sheria, wakae
makambini mwao niliwaambia wakitoka uraiani wakakamatwa watashitakiwa kwa
kukiuka sheria,..
Na pia nilipowhutubia raia, niliwaonya wasije kuwachukua wakimbizi na
kwenda nao majumbani, kwa tahadhari, kwani huwezi kujua, unaweza ukafanya hivyo
kwa nia njema tu, kumbe huyo uliyemchukua akawa ni jambazi kutoka kwao akaja
kukugeukia wewe au majirani.
Nakumbuka niliwahi kuwatania,
japokuwa sio utani hayo yanatendeka kimakosa, niliwaasa hasa wanaume,wasije
kuingiwa na tamaa wakiwaona mabinti wazuri wakimbizi, wakawatamani, wakawachukua na kwenda nao mahotelini,
hairuhusiwi, hao wapo kambini kisheria...!
Sasa huyu yupo hapa kafikaje,
mlangoni mwangu tena mimi ni miongoni mwa viongozi? Au sio mkimbizi, na kama
sio mkimbizi ni nani?
Alionekana ni mnzuri kasoro hayo mabaka mabaka kama ya kuungua usoni,
hebu fikiria pamoja na kasoro hizo bado alionekana anavutia, ..mrembo! Sikuwa
na wazo la kufikiria hivyo kwa muda huo, ila nataka kuelezea hali halisi!
Niligeuza uso na kumuangalia
yule mtoto mchanga, alikuwa kalala na sehemu kubwa ya uso imefunikwa. Kiafya
ndivyo itakiwavyo, hata hivyo bado niliona udhaifu katika nguo alizomfunika huyo mtoto…, lakini atafanyeje
katika hali kama hiyo, ukimbizi ni umasikini. Nikawa na hamasa sana na yule
mtoto. Na utafikiri mtoto huyo alitaka nimuone, ghafla akajinyosha, na vimkono
vyake vikasukuma nguo alizofunikwa na kuacha uso wazi.
Najua mtoto mchanga hatakiwi
kuachwa wazi, kwa haraka nikataka kukimbilia kumfunika,..hata huyo mzazi
nilimuona akijitahidi kutaka kufanya hivyo, na tukajikuta sote twaelekeza
mikono yetu sehemu moja… lakini mimi kwa tahadhari, kama nilivyokuambia inaweza
ikawa ni mtego, kwahiyo jicho moja kwa mama yake na jicho jingine nilimuangalia
huyo mtoto, …na wakati nataka kuinama, sura ya huyo mtoto ikanivuta zaidi….
Watoto wachanga huwa wanafanana
sura zao, na wakati mwingine unaweza, usiweze kugundua kuwa mtoto huyo
anafanana na nani, katika wazazi wao mpaka atimize umri fulani …
Lakini sio kwa mtoto huyo, sura
na hata ile mienendo, ya kujinyosha, kubenua mdomo, kwa haraka sana, nikamkumbuka
mtoto wangu Soldier alipokuwa mchanga, wanafana, unajua kufanana, ….oh, nikajikuta
natabasamu na bila kujielewa, nikasema;..
'Soldier..'nilijikuta nimetamka tu hivyo.
Sijui kwanini, kwani nilivyotamka hivyo tu, ilikuwa kama
ishara kwa huyo binti, au sijui kwanini alishtuka na kusimama kwa haraka, usoni
akaonekana mwingi wa mashaka, japokuwa alijitahidi kuficha uso wake,...
'Soldaar...'alitamka hivyo, kwa
lafudhi ya kigeni, sijui ni mtu wa wapi, akageuka kuangalia huku na kule,
halafu akaniangalia mimi,..na bila kusema neno jingine…, akaanza kukimbia!
Nilishangaa, mwanamke gani huyu
anakimbia na kumuacha mtoto wake...tena mtoto mchanga!
'Hey you....'nikasema, lakini ilikuwa kama nimemchochea, aliongeza
speed, na mimi nikaamua kumkimbilia, lakini nilishachelewa, akawa keshatoka
mlango wa eneo la vyumba, na kupinda kulia, kwahiyo nikawa simuoni,
nilijitahidi kumkimbilia lakini sikumuona...
Wazo likanijia, nirudi haraka
nikamchukue huyo mtoto nije naye mapokezi, nikawakabidhi… maana hata
nikiwaambia hao watu wa mapokezi bila ushahidi haitasaidia kitu, kwanza
napoteza muda wangu wa kupumzika, maana mimi usiku kama tisa natakiwa kuwahi
ndege ya kurudi kwetu.
'Nitawapigia simu nikifika
chumbani kwangu, waje wamchukue huyo mtoto mchanga, sitaki kujiingiza kwenye
matatizo…’ nikasema na kuendelea kutembea, sasa nageuka kushoto, ili nielekee
upande wa chumba changu, huku bado nikiendelea kujiongelekesha.
‘Sijawahi kuona, mzazi amkimbie mtoto wake,..huyu ni mwanamke wa ajabu
kabisa, kwanini anafanya hivyo...'nikasema,
na kuanza kurudi kuelekea chumbani kwangu.
Wakati nimefika ile kona ya kugeuka
kuangalia kule usawa wa chumba changu, nikawa naangalia pale mtoto alipoachwa,
sasa nikaona mtu kasimama, huyu ni mwaname, na mwanaume kweli kwani kapanda juu
na pandikiza la mtu, hapo nikasimama kidogo,..hatari..!
Inawezekana ni mlinzi wa humu ndani…kama ni hivyo.., afadhali..atachukua
jukumu la huyo mtoto, mimi sina muda, nahitajika kumpumzika….nikajipa
moyo,..lakini bado nafsi inasita, natamani nigeuke nirudi mapokezi...
Nikakajipa moyo nikatembea kuelekea pale aliposimama huyo mtu, na
nilipomkaribia nikasema;
'Hey, huyo mtoto kaachwa na
mama mmoja..nahisi ni mama yake..sasa fanya mpango,…uwaarifu wahusika wa hotel wafuatilie,
je wewe ni mfanyakazi wa humu ndani…?’nikasema na kuuliza.
Yule jamaa akawa kasimama vile
vile akiwa hafanyi lolote, mpaka nikamkaribia kabisa, na alipohisi nipo karibu
yake, akanigeukia na kuniangalia,…
Alikuwa kavaa mawani meusi
makubwa, yameziba sehemu kubwa ya macho, kwa uvaaji huo,nikahisi kuna jambo, uvaaji
wa namna hiyo una maana ya kuficha jambo, nikaingiwa na mashaka, nikahisi kuna
hatari….au kuna jambo linakuja lisilo la kawaida!
‘Hey….’huyo jamaa akasema hivyo tu.
‘Hey,…Who are you…?’ nikamuuliza na yeye akageuza uso na kumtizama
yule mtoto halafu akasema.
'Mzee, I have
something for you, ..ni ujumbe wako...'akasema akichanganya Kiswahili na
kiingereza.
'Ujumbe gani, unahusu huyu.mtoto au...mimi sijui lolote,
unajua..'nikataka kuendelea kuongea, yeye akawa anatoa kitu kwenye mfuko wake
wa koti,..hapo machale yakanicheza, nikajua sasa...inawezekana jamaa anataka
kutoa bastola, ..
Nikarudi nyuma kidogo, na mkono
wangu ukaingia mfukoni, nikitaka kuishika simu yangu.
Kwenye simu yangu nimeegesha
namba tisa, inapiga namba ya hatar ,tulipewa namba ya hatari kuwa ikitokea
lolote uipige namba hiyo, na watu wa usalama watafika haraka kukuokoa,lakini
kabla mkono haujazama kwenye mfuko , jamaa akatoa karatasi….na sio bastola.
'Mzee, don’t worry, mimi ni mjumbe tu,...'akasema na sasa akawa
ananikabidhi ile karatasi.
'Ya nini...hii karatasi?'nikamuuliza.
'Imetoka kwa bosi...'akasema
'Bosi, who is the bos...?' nikamuuliza
'Ni mwanao..kama alivyosema nikuambia hivyo,....na mzee, bora umpigia mtaongea na yeye, mwenyewe...'akasema
'Mimi nina watoto wengi,...na na...'nikasema nikigeuka kumuangalia yule mtoto
'Mzee, wewe mpigie simu bosi,..., namba imo humo, nyuma ya
hiyo karatasi...amesema uiangalia hiyo karatasi kwa makini....'akasema , sasa kiongea Kiswahili vizuri, nikajua ni wenzetu , …
‘No...subiri kwanza, niambia huyo mwanangu ni yupi..?’ nikauliza sasa
nikianza kuwazia mbali.
‘Sijui...kwa vipi ni mwanao...unasikia mzee, usipoteze muda, mpigia mtaongea naye…’akasema.
'Na huyu mtoto...?'nikamuuliza huyo jamaa, lakini sasa hakunijibu akageuka na kuanza kuondoa.
'Hey..wewe...usiondoke kwanza....'nikamwambia lakini hakusimama kwa haraka akaanza kuondoka.
Hatari................
.
NB: Nimeona niandike kipande hiki kifupi kwa haraka , ili tu siku
isipite bure, mvua imenifanya nichelewe kufika ofisini ambapo ninapata komputa
ya kuadikia…tuwe pamoja na kamlisho la sehemu hii …
WAZO LA LEO: Tuwe
wepezi kusaidia wenye uhitaji, wapo watu wanakabiliwa na matatizo makubwa tu,
wazazi, watoto…masikini, wasiojiweza, na wengine yanawakuta matatizo na
inafikia hatua wanahitaji msaada wa kibinadamu. Tusikimbilie kuwanyanyapaa
kwanza hawa watu, tusaidie kwanza, halafu kama kuna la kuongea basi lifuate
baadae, wengine mpaka wanafikia hatua hiyo wamehangaika sana…Mola anajua ni
kwanini anatoa mitihani hiyo. Tumuombe mola wetu atupe moyo mwepesi wa
kusaidiana.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment