Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, March 9, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-13


‘Huyu ni nani…?’ mke wangu akauliza sasa akiwa kasimama, na macho yamemtoka akimuangalia huyo mgeni aliyeingia…alijitahidi kusimama lakini alionekana hana nguvu akawa anayumba yumba….nikataka kumshika lakini akaniashiria kwa mkono nisimsogelee..

Mgeni aliyeingia akawa ananiangalia mimi tu usoni, hakutaka hata kumuangalia huyo anayemuuliza huyu ni nani. Na alipoona ile hali ya mle ndani, watu wanamuangalia yeye tu, akasema;

‘M-m-mzee nina shida na-na-na wewe…’akasema kwa kigugumizi.
Watu wote mle ndani wakawa wanaendelea kumuangalia huyo mgeni aliyeingia, na mimi kwa haraka nikasimama na kumshika mkono huyo kijana na kumwambia;

‘Twende nje…’nikasema na yeye bila ubishi akanifuata …na tulipofika nje, yeye akawa wa kwanza kuongea;

‘Umemfanya nini mama yangu…?’ akauliza

‘Kwani kuna nini kimetokea…?’ nikamuuliza

‘Niliambiwa na baba kuwa ni kiwa na shida nije kukuona…wewe, natumai mliwahi kuongea naye, au sio….’akasema sasa akiwa kashika kiuono, hakuelewa kuwa sisi sheria za jeshi kushikiwa kiuno na mtoto mdogo kam huyu  ni dharau…nikamwangalia tu…

‘Sasa una shida gani…?’ nikamuuliza.

‘Kwanza nimefika nyumbani, nimekuta mama kalewa,…’akasema

‘Kalewa…?’ nikamuuliza

‘Yaani chakari…hajitambui…, anachoongea anakijua yeye mwenyewe…ananiogopesha sana mama huwa halewagi kwanini anafanya hivyo…’ akatulia akiniangalia.

‘Mhh..kuna tatizo…’nikasema

‘Na mzee,..katika kuongea kwake, akawa anakutaja wewe na kukulaani, kuna nini umemfanyia mama yangu…, nataka kujua hilo kwanza…’akasema akiniangalia kwa upande upande.

‘Kanitaja mimi kasema nini,kuwa mimi nimefanya nini..?’ nikamuuliza

‘Haeleweki…anaongea, kilevi levi…..mimi sipendi, mimi unaniona nilivyo, sinwi, kabisa, wengine wananihis kuwa ni muhuni, lakini mimi sina tabia hiyo, natumia akili tu….’akasema

‘Sasa sikiliza mimi nitakuja huko nyumbani, nitaongea na mama yako, kwa hivi sasa mke wangu anaumwa, unaona…sasa niambie una shida gani nyingine?’ nikamuuliza.

‘Nikuulize kwanza mzee, ni kwanini watu wanasema mimi nafanana na mtoto wako, ….’akasema na ilikuwa kama mtu kanipiga rungu kichwani, nikamuangalia huyu kijana na kusema

‘Nani umemsikia akisema hivyo…?’ nikamuuliza

‘Na huyo mtoto wako yupoje mbona mimi sijawahi kumuona..?’ Akaniuliza

‘Kwani kuna ubaya, wewe kufanana na mtoto wangu,  mbona mimi nafanana na baba yako…’nikasema

‘Mimi sijui… kama wewe unafanana na baba yangu...hayo ni yenu,...,labda mlipokuwa wadogo mlikuwa munafanana, mimi sijui…ila kiukweli nina mashaka, maneno aliyokuwa akiongea mama leo, yanaanza kunifungua akili,..nahisi kuna jambo, na…mimi sipendi kuvumilia, kitu kikiniingia akilini nataka nipate jawabu lake haraka…tena haraka kabla hali haikabadilika...'akashika kichwa.

'Mzee mimi nahisi kuna jambo..na usiponiambia wewe…, nitalitafuta na nitalijua tu.., na nikilijua kwa jitihada zangu….nitafanya jambo mtashangaa…hamtaamini, mimi sio mtu wa kawaida mzee, muulize mama...’akasema.

‘Unataka kujua nini sasa..?’ nikamuuliza nikiona ananipotezea muda wangu.

‘Kujua ukweli, kama watu wanavyosema…’akasema

‘Wanasema nini?’ nikamuuliza

‘Huenda wewe ni baba yangu wa damu…’akasema.

‘Baba yako wa damu, una maana gani,...wewe mtoto wewe…una akili kweli, unaamini maneno ya watu, watu wanaweza kusema maneno mengi, na lengo lao ni kubomoa tu, hebu niondokee huko na upumbavu wako, una nini wewe …ina maana umewaamini watu wa mitaani, na unataka kumkana hata baba yako,au kwa vile hayupo duniani, eeh, .’nikasema.

‘Mimi sijamkana baba yangu..na kama ningelisikia hivyo mapema ningelimuuliza baba yangu,..na hata kama angesema ni kweli, yeye ni baba yangu, angelibakia kuwa hivyo.. muhimu ni kujua tu ukweli, na kama ukweli unafichwa, basi kuna jambo,..na kama kuna jambo linafichwa,…hiyo ni dili…kwa watoto wa mjini…hiyo ni dili…unajua mzee, dili inalipa, dili ina gharama...’akasema akiangalia pembeni.

‘Dili!! dili gani, ?…Unataka kusema nini hapo..?’ nikamuuliza nikimuangalia kwa mashaka.

‘Mimi sijui..muhimu ni kujua ukweli…akili yangu inahisi kuna jambo, kichwa hakitulii..naogopa nitabadilika, nitafanya kitu mbaya...hata nashangaa,kwanini imepoa hivi, mtu amchezee mama yangu..haijawahi kutokea, nahisi nimeanza kuwa na mabadiliko..sijui....’akasema akiwa anahangaika hangaika, kama kuna kitu kinamsumbua kichwani.

‘Unajue uwe na akili ya kufikiri, ..hivi, kama hayo yangelikuwa ni ya ukweli kwanini baba yako asikuambie, kwani alikuwa na tatizo gani…, achana na maneno ya watu..rudi nyumbani ukakae na mama yako...’nikasema kwa ukali.

‘Ok…sawa, nitaachana na hayo..lakini sasa..mimi nimekuja nina matatizo, nahitajia kuendelea na masomo yangu, sina ada,…unaweza kunisaidia kwa hilo?’ akaniuliza sasa akiniangalia usoni moja kwa moja.

‘Shilingi ngapi..?’ nikauliza nikijua labda ni pesa ndogo tu.

‘Lakini saba kwa sasa..’akasema

‘Laki saba….ooh! mimi…sina pesa nyingi kiasi hicho si unajua maisha yetu yalivyo, labda niuze kiwanja…’nikasema

‘Inabidi ukakiuze…maana kama sitapata hizo pesa, ..nikasoma, sitatulia, na nataka niondoke kabisa maeneo haya, nikaishi mjini..lakini ...kama sitaipata hiyo pesa kirahisi,...nitaipata kwa nguvu, ...mzee na wewe si unataka kuwa kiongozi au sio…?’akaniuliza.

‘Unataka kusema nini..wewe mtoto, unasema nini, sijasikia vyema, uongozi na hayo yanahusikanaje..?’ nikamuuliza

‘Mimi ni mtoto wa mjini, masikio yangu yanasikia sana, na macho yangu yanaona sana..akili yangu inafanya kazi usiku na mchana….baba alikuwa ni askari wa silaha, mimi askari wa kalamu na karatasi, nimecheza sana na mitandao, nimejifunza mengi…..kwahiyo, ujue ya leo sio ya jana,..umenielewa mzee…?’akaniangalia kuonyesha kuwa ana dhamira ya kweli.

‘Sikuelewi…nahisi wewe una matatizo, mbona baba yako hakuniambia, upoje wewe…’nikasema sasa nikiwa nimekasirika.

‘Mzee….,nikuambie kitu siasa ni kitu rahisi ukiwa mjanja,..na wanaotaka kupanda juu, wanahitaji sapoti, kitu cha kushikilia, unajua..., na wengine nao wanatamani kupanda huko huko, ukumbuke mti ni mmoja, wengine wanaweza kukuvuta mguu, hasa wakiona udhaifu wako au sio…..sasa mimi nimesikia, na nipo mbioni kuona ukweli, kuna kitu nimekisikia…nikikithibitisha, mzee, nitakifanyia kazi, kama hatutaelewana,utaniona mbaya, ...'akasema

'Mbona mimi sikuelewi...unataka kusema nini..?' nikamuuliza

'Mzee mimi ninachotaka ni ada..laki saba tu,  …’akatulia akiniangalia machoni.

Nilimuangalia huyu mtoto bila kummaliza, haya..anayoyaongea nimeyaona kwenye sinema, nimesoma kwenye vitabu,…siamini kuwa huku kwetu kuna watu wenye tabia kama hizo…na huyu ana asili ya damu yangu, japokuwa nilishamtoa kwenye damu yangu kwa ahadi..kama kweli ni damu yangu…hata hivyo hiyo tabia ni aya ajabu kwangu, sisi hatuna hulka kama hizi,..hapana, hii sio damu yangu, haiwezekani…

‘Sikiliza wewe mtoto, unanifahamu kuwa mimi ni nani…nitakuchapa viboko na ukubwa wako huo ..siogopi kukuzaba vibao..na ukileta ubishi tutapigana ngumi...msijione mumekuwa mkafiria mna nguvu sana...baba yako alinikabidhi wewe kama mwanangu, sasa usione nimezeeka hivi, napiga, na nikipiga kweli..….’nikasema nikimkodolea macho ya ukali.

‘Baba,….usije ukaja kujutia baadae haya ninayokuambia, kwani mimi nitakosa nini, nikiusema huo ukweli, watu wakaujua jinsi ulivyo…mama kaanza kusema ovyo…na nimeunganisha maneno yake, nimegundua jambo, wewe una kitu na mama, na huenda kilianzia huko kwa baba….ni heri isiwe hivyo, lakini ikiwa ni hivyo, mzee, hutaamini, mzee kama hatutaelewana utakuja kuniona mtu wa ajabu sana,…’akaniangalia halafu akaangalia pembeni.

‘Kitu gani mimi na mama yako wewe, hebu acha huo uhuni, mtoto mdogo kama wewe unachunguza chunguza mambo ya wakubwa, umeyapatia wapi hayo maneno…unajua mimi na baba yako tulikuwaje..sikiliza hayo unayotaka kuyafanya sisi ndio askari wa kuyakomesha, sasa jifanya unajua uone utakachokipata…unataka kuwa nani wewe…huo ni ujambazi..unalifahamu hilo..?’ nikauliza

‘Ohh..ujambazi, au sio…mimi siibi, sivunji nyumba za watu, situmii silaha, natumia akili yangu, macho na masikio….sasa, kama unataka kunipima, ngoja niifanay kazi yangu..bado natafuta ukweli, nikija kuugundua,…sitojali mzee…unisikie, jambo muhimu,… sitaki mama yangu apate shida, nimejua wewe ndiye shida ya mama…sasa nilikuja mara moja kuona kama nitapata ada,…nakuuliza tena mzee, utanipa ada au hunipi….?’ Akauliza

‘Sina pesa nyingi hivyo, unafikiri mimi ni tajiri…’nikasema

‘Una shilingi ngapi .?’ akaniuliza akiniangalia machoni.

‘Sasa hivi sina pesa, subiria niuze mazao…’nikasema

‘Mzee, nakushauri, uza kiwanja,..nataka ada kwa haraka sana…’akasema kama anatoa amri

‘Siwezi kuuza kiwanja…kiwanja ni mali ya familia, …ni mpaka tukae na familia,tujadiliane , sio kitu rahisi kihivyo nitaongea na mama yako kama anaweza kuuza sehemu yake ya ardhi..mna maeneo ya kule chini, , …’nikasema

‘Ongea naye..lakini mimi nikirudi tena nataka pesa kutoka kwako sio kwa mama, vinginevyo, hutaamini nitakayoyafanya…bado nakusanya ‘data’….mzee mimi ni mtoto wa mjini, kwanza nataka kujua mimi na wewe tupoje, halafu wewe na mama mpoje..unanisikia,…nimemuona na mke wako ananiangalia kwa mshangao….ana hamu ya kujua mengi au sio…’akasema akitabasamu kwa dharau.

‘Kujua nini…?’ nikauliza.

Mzee…ngoja nikuambie kitu kimoja kunihusu mimi…siku muulize mama atakuambia…akakaa mkao wa kutaka kunihadithia jambo, na mimi nikatulia kumsikilia..alikuwa akinipotezea muda, lakini sikuwa na jinsi…

‘Ni hivi mzee…watu wanasema mimi ni hatari sana nikibadilika….mimi sijui, maana  huwa wananisimuliaga tu,  wakati mwingine siamini na sipendi initokee lakini sijui nina tatizo gani....

Mimi ni adui kwa yoyote yule anayemliza mama yangu, huyo kwangu ni adui, haijalishi ni nani, nikiwa mdogo, nilipambana na baba…nilikuwa kama paka, wanavyosema wao,…, walihisi nimechanganyikiwa, kisa baba alimzaba mama kibao mbele yangu, mama akawa analia.....baba ilibidi akimbie,...


Wakati nikiwa mdogo, shuleni kuna siku walinikorofisha, alikuwa ni mwalimu mmoja alipenda sana kutuchapa, na katika kuniadhibu, akaongea jambo la kumkashfu mama yangu….nasikia walivyonisimulia, nilitutumuka,..na nilichokifanya siku hiyo, niliacha historia…


Wanasema nilibadilika, na kuanza kumpiga huyo mwalimu na kila mwalimu aliyekuja kusaidia,niliweza kumuinua mnzima mnzima na kumbamiza jinni kama gunia…walikimbia walimu wote na wanafunzi….


Nikiwa chuoni, ilitokea hivyo hivyo mpaka wakaita polisi, na hata,polisi walipokuja hawakuweza kunizuia niliwarushia mbali, unajua ni kitu cha ajabu wanasema namrusha mtu kama mpira…


Ni hali inayoniingia mwilini na kuwa mtu tofauti na mimi, sijijui, na hata hali hiyo ikiisha siwezi kukumuka kama nilifanya hivyo..na hakuna anayeweza kunidhiti,..ndivyo wanavyoniambia…


Na ili hali hiyo iishe wanasema ni mpaka huyo mtu atimiza takwa langu, na aliyenikosea ajikate mahali ajitoe damu niione,....


Sijui kwann nimekuambia hayo,...

Mimi nilimsikiliza kama mtu anayetoa hadithi za kufikirika, nikatabasamu na kusema;

‘Kama una mashetani mimi najua jinsi gani ya kukabiliana nayo, usijaribu kunitolea vitisho visivyo na maana mimi ni askari, nimepambana vita..kuna kitu kinaua kama risasi…sasa mimi nilikabiliana na risasi ..kwahiyo usinitishe kijana, unasikia..’nikamwambia

‘Hahaha mzee hapo patamu, hapoo eeh, napenda namna hiyo…, unanipa changamoto, sawa mzee, kamliwaze mkeo, maana siku nikija inabidi anifahamu rasmi kuwa mimi ni nani, si hupendi anifahamu , sasa jitahidi asinifahamu maana namshukuru mungu, kanipa macho, akili na masikio…kwangu hivyo ni hazina kubwa sana….sifanyi makosa ….utaona…’akasema, halafu akaweka mikono mbele kama muombaji na kusema kwa sauti ya unyenyekevu..

‘Lakini mzee mimi sitaki shida, …sipendi mabaya yakukute, …tumalizane tu…, si unajua cha kufanya, ada tu…basi usisahau, samahani mzee kwa usumbufu, kwaheri, usisahau….’akageuka na kuanza kuondoka huku anaimba imba wimbo...

Nilibakia nimeishiwa nguvu….

‘Sasa hili ni tatizo…’Mzee mzima alishika kichwa, akatulia kwa muda akiwaza visivyowazika, akatamani aje kufanya jambo baya....na ghafla, akashtuka mtu anamshika bega, ..akajua ni yule kijana karudi, akasimama kwa hasira, ...

'Nimekuambia....' akatulia, na kunywea alipomuona mtu aliyemsimamia mbele yake.

NB:Niendelee....


WAZO LA LEO:  Usipoziba ufa utakuja kujenga ukuta kwa gharama kubwa sana, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo…tuwe makini kuyakabili matatizo yetu yakiwa machanga, kwa kuelezana, kushauriana, kusaidiana..kwani hatari ikianza kutokea huenda ikaharibu yote yale mliyokuwa mumeyafanya…
Ni mimi: emu-three

No comments :