Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, March 7, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-11
**************

Kiukweli, nilipomuona huyo kijana sikuamini kuwa sio mtoto wangu Soldier...!

Unajua kufanana, huyu kijana alifanana kabisa na mtoto wangu, …sema kwa vile huyo dereva ana masharafa na midevu mengi , lakini kwa kipindi hicho alikuwa kanyoa, inavyoonekana..na alikuwa bado kijana!

‘Huyu sio Soldier, huyo ni mwanangu, wanafanana sana na mtoto wako, ni kama mimi na wewe..’akasema rafiki yangu akijitahidi kutabasamu.

‘Ni kweli,..naona mungu karejesha historia…’nikamwambia huku nikiendelea kumchunguza huyo kijana, kama anakaribiana umri na mwanangu basi atakuwa kwenye miaka kumi na tisa hivi.

‘Na tatizo lake mindevu imemuandama mapema, kama babu yake, babu yake alikuwa na mindevu karibu uso mnzima,…akiyachia unaona macho tu ….na nimemuambia awe anayafuga hivyo hivyo hasa akiwa likizo, huko shuleni anapata shida sana…, nasikia huku walipomuona wamekuwa wakimsumbua sana, kwa kumuita jina la mtoto wako…’akasema.

‘Hata mimi nilijua ni yeye…’nikasema, nikiendelea kumkagua hadi kijana mwenyewe akajionea shida, na kutoka nje, akatuacha tukiwa wawili.

‘Rafiki yangu hebu niambie ukweli…!’ nikaanza kumdadisi rafiki yangu akaonekana hana furaha usoni, sijui ni kwasababu ya maumivi ya kuumwa kwake au ni sababu ya hilo swali, akasema;

‘Ukweli gani…naomba unipe maji, ...ooh, nahisi vibaya, ngoja nilale kidogo..’akasema na mimi nikawa sinabudu kuondoka.

Siku hiyo ilinifanya nikumbuke mbali, japokuwa sikuwa na uhakika na hilo lakini nilijikuta nikikumbuka siku ile ya tukio,..unajua akili ya binadamu ilivyo, jambo la aina hiyo litasumbua sana kichwa chako zaidi ya jambo jema..sijui ni mimi tu au la….tukio lile lilikuja kusahaulika baada ya muda mrefu, ...sasa nimetoneshwa kidonda...’akatulia.

‘Hilo tukio likawa linanirudia rudia kichwani mpaka najisikia vibaya, ..mimi huwa silewi, ila huwa nakunywa siku moja moja kiushabiki tu, na kutokana na hiyo hali nikaamua ninywe, niliogopa sana kuwa siri hiyo itaweza kugundulika na mimi nitakuwa nimevunja ahadi na rafiki yangu,..nitavunja ndaoa yangu na kipindi hicho ndio najitangaza kugombea uongozi wa udiwani.

Nikajifanya nakunywa na watu ili kujitangaza, unajua tena, kipindi hicho kilikuwa cha kampeni, na kosa dogo tu mwenzako analivalia njuga,..mimi nilionekana msafi kuliko wenzangu, sina madhambi, je wakija kuligundua hilo, itakuwaje.

Muda wote nilikuwa nikiombea mke wangu asije akakutana na huyo mtoto, na sijui mama yake anajisikiaje akimuona huyo mtoto anavyofanana na mwanangu,,…sikuwahi kukaa naye kwa karibu zaidi ya kusalimiana na baadae anakuwa akiongea na mwenzake,…na nilipomuona huyo mtoto nilijaribu kumchunguza shemeji kama ananiangalia kwa shuku fulani, sikumuona akionyesha dalili zozote za shauku.

Na siku kadhaa baadae rafiki yangu akatuita mimi na mke wangu...taarifa hiyo ilipokuja nikajua rafiki yangu ana hali mbaya, lakini nikajiuliza kwanini atuite mimi na mke wangu...nilipatwa na wakati mgumu, nilitamani nimuambie mke wangu nitangulia kwanza yeye aje baadaye..lakini tukaongozana tu.

Tulipofika, akaanza kusema ametuta ili atupatie usia....

'Usia...?' nikauliza

'Ndio usijali...'akasema

Kiukweli yaliyoongelewa siku ile, mke wangu anayafahamu sana, alianza kusema;

'Ndugu zangu, nimewasumbua kidogo, najua nyie siwasumbui..ni wajibu wenu ..na nikiongea na nyie napata faraja kubwa sana...

'Tukubali tusikubali, mtu akifikia hali niliyo nayo, anajua kabisa safari imefika,...hatuwezi kudanganyana tena...ila nimewaita nyie wawili, hata mke wangu sikutaka awepo hapa, maana ataanza kulia lia hapa.....nafahamu anavyonipenda, lakini yupo anayenipenda zaidi....'akatulia

‘Ninaondoka,...lakini moyoni nina imani kabisa, nikiondoka hapa duniani, najua kabisa familia yangu ipo kwenye mikono salama, ….rafiki yangu nakukabidhi familia yangu mke na mtoto, wazazi hawana shida,…nafahamu unajua umuhimu wao…walikuwa wakinitegemea mimi, lakini nimejaribu kuwawekea mazingira mazuri tu…hao wapo mikononi mwa ndugu zake…

‘Na kingine ….ni kuhusu mtoto…’hapo akatulia, nikahisi anataka kutoa siri, hapo moyo ukawa unanidunda kwa kasi,..nikawa namuangalia kwa makini ili akitaka kuongea hilo nimkanye, kwani ataniharibia ndoa yangu.

‘Mtoto ni huyo mmoja mungu aliyenijalia…angalau, nafariki nikiwa nimeacha mbegu…, namshukuru sana mungu kwa hilo, na najua ataweza kukiendeleza hiki kizazi, na..mengine mungu mwenyewe anajua’ akisema;

Halafu akanigeukia mimi….

‘Rafiki yangu..tumetoka mbali mimi na wewe, kutokea utotoni hadi uzeeni, na leo unahudhuria ....kuagana kwetu.., kama kuna kitu nikifa nitakikumbuka huko mbele, kama mungu anatupa nafasi hiyo..urafiki wetu wa kweli.

'Nakiri moyoni kuwa, …tumekuwa zaidi ya ndugu…sasa mimi nakuomba sana, uitunze familia yetu..nasema yetu, unafahamu zaidi …., na hakikisha kila tulichoahidiana unakitimiza, tumepanga mengi, tulipanga mengi kuwa tunashikiriana kuyafanya, lakini ya mungu mengi… sijui nitaishi muda gani,…lakini akili yangu inakuwa inasahau, nahisi muda wa kuishi tena haupo, na naombe ufike hamjui ninavyoteseka…’akatulia.

‘Sasa nikaona kabla sijasahau kabisa, na kabla sijasahaulika, kwenye huu uso wa dunia, basi niwaite nyie ndugu zangu wa kweli,…maana ni nani kwenye hali kama hii angeliendelea kuwa name karibu, mumekuwa nami, mnanisaidia, kwa kila hali..mpaka wakati mwingine ..nashindwa kusema, mungu mwenyewe anajua…ahsante sana, mungu awazidishie….’akasema.

‘Lakini rafiki yangu utapaona,..na haya yote ni kawaida, mimi na wewe hatuwezi kutupana kamwe,… usikate tamaa hivyo…’nikamwambia.

‘Mungu mwenyewe anajua hilo,..na kama bado nina pumzi kwanini nisiwaambie ndugu zangu,..najua itafika muda sitaweza kuwa nanyi tena, yote haya ni mapenzi ya mungu, siwezi kuyapinga,…nawapenda sana nyie ndugu zangu nanyi mpendane huku baadae..msije mkafarakana mkaitupa familia yetu,…’akasema na halafu akamgeukia mke wangu na kusema

‘Shemeji ..mfanye mwenzako kama dada yako…na mtoto wetu huyo, najua hatakuwa hapa, kutokana na masomo yake,..ameamua kuwa fundi wa magari, sawa, sikumkataza… na yeye anapendelea kuishi huko mjini, lakini huenda itafika muda atakuja kuishi huku na mama yake, ikibidi,… basi akija huku nawaombeni sana mumsaidie kwa hali na mali…’akasema

‘Sawa shemeji..usijali, na usikate tamaa shemeji utapona tu…’akasema mke wangu.

‘Maisha ni matamu, na kila mtu anapenda kuishi, ila kwa taabu ninayoipata nafikia mahali namuomba mungu tu aichukue roho yangu….na..zaidi mniombee tu huko niendako maana hakuna anayepafahamu, mengi tumayafanya ya kumuudhi mola,..lakini ndio maisha, tuombeane tu…basi ni hayo wapendwa…’akasema kwa sauti ndogo na kwakweli siku hiyo nililia.

Siku hiyo ilikuwa ya majonzi sana kwetu…ni kama kweli alikuwa akituaga, maana haikupita muda, taarifa ikafika kuwa keshatangulia mbele ya haki….hakuna mtu aliyeonekana kuzidiwa na msiba huo kama mimi, waulizeni wenzangu, nilijiona nimenyang’anywa sehemu ya mwili wangu…, kiukweli iliniuma sana…

Kipindi cha kuombeleza kikapita, mimi na mke wangu tukawa kwa asilimia kubwa tunafika hapo nyumbani tunakaa na jamaa, na mjane mpaka siku inaisha,..sisi tuliendelea hivyo mpaka tukaridhika kuwa sasa mjane yupo na hali nzuri, maana ilikuwa ni kazi,…kumliwaza, …alikuwa akipoteza fahamu kwa kulia, ….kwakweli alimpenda sana mume wake..kwa hali kama hiyo akama mgonjwa, hali..hanywi..akakonda sana…lakini baadae siku zilivyokwenda akaanza kuizoea hiyo hali.

Mimi nilikuwa na kawaida kila nikitoka kwenye shughuli zangu nampitia karibu kila siku,..nakuwa naye karibu sana, kwahiyo akanizoea, na kila akiwa na shida, ananiambia mimi kama alivyokuwa akimuambia mumewe…lakini siku moja, ilikuwa jioni hivi, nafika shemeji akaanza kulia, na kuniambia;

‘Niambie ukweli shemeji, niambie ukweli..ndio maana hata mimi kila nikikaa nilikuwa nawazia sana hili iweje mwanangu afanane na mwanao, afanane zaidi na wewe..ni kweli awali nilichukulia ni miujiza ya mungu tu…sasa niambie ukweli, usinifiche…….’akawa analia mpaka nachanganyikiwa sasa ni nini tena hii.

‘Shemeji hayo yote yametokea wapi?’ nikamuuliza

‘Usinifiche shemeji mume wangu alisema kila litakalonitatiza nikuone wewe, na hili limenipa wakati mgumu sana..nataka uniambie ukweli wote, ..la sivyo nitajiua…’akasema

‘Oh, imakuwa hayo tena shemeji hayo ya kujiua yametoka wapi…?’ nikauliza

‘Hilo nakuhakikishia, maana..nafahamu ipo siku ….nami siwezi kuvumilia,….’akasema akikatisha maneno kiasi kwamba huelewi anachokiongea ni kitu gani je ana tatizo gani.

‘Shemeji kwanini unasema hivyo, kuna tatizo gani…?’ nikamuuliza

Mara akatoka na kuingia chumbani mwake, na kurudi akiwa na boksi ndogo hivi, akasema;

‘Hivi ni vitu vilivyokuwa kwenye kabati la mume wangu sikuwahi kulifungua hilo kabati kwani alikuwa akihifadhi mambo yake ya kazini na vitu vyake ambavyo sio muhimu kwangu,…., na wakati nafanya usafi na kupekua pekua, nikaona cheti hiki cha dakitari, kikielezea matibabu yake na kichogunulikana, mengi yaliyoandikwa huku hakuwahi kuniambia ujue mimi nilisomea unesi, na nafahamu mambo mengi ya udakitari,…’akasema na kunikabidhi hicho cheti.

Nilikiangalia kile cheti, nilishakiona kabla ni cheti ambacho alipimwa na kuonekena, uti wa mgongo umeathirika, na kuna maelezo chini , na kitibabu kuwa hata weza kuzaa,…hawakuandika moja kwa moja.

‘Lakini hakuna ubaya wa kilichoandikwa hapo… alitibiwa wakagundua hilo, na akaendelea kutibiwa, kwahiyo mengine ni majaliwa ya mungu mungu…’nikasema

‘Shemeji nimekuambia mimi nilisomea unesi, na nilipokiona hiki cheti ili kujiridhisha nimempigia docta mmoja ninayemfahamu akanielezea tatizo hilo lilivyo, anasema mwenye tatizo kama hilo hawezi kuzaa…hawezi kuzaa…umenisikia shemeji hawezi kupata mtoto…..sasa niambie ilikuwaje, maana …..naanza kuhisi jambo, ….niambieni ukweli!

‘Shemji hakuna la kukuambia….zaidi alikuwa anafahamu mume wako,..mimi sijui zaidi ya hayo…’nikasema

‘Haya na hii diary yake hapa kaandika nini…hebu soma mwenyewe hapa…aliandika baadaye akafuta lakini maneno yanasomeka, kaandika nini hapo…hebu soma wewe mwenyewe,….nikaanza kuyasoma yale maneno..ooh…..

NB: Kuliandikwa nini….

WAZO LA LEO: Mtu akiwa mgonjwa, au mtu akiwa kwenye mitihani ya maisha,…au kapungukiwa na viuongo, au madhaifu mbali mbali….huwa anahitajia faraja nyingi kutoka kwa wenzake, hasa kutoka kwa wale watu wake wa karibu aliokuwa akisaidiana nao…Tujitahidi kuwasaidia watu kama hawa, kuwa nao karibu, kuwafariji, hata kwa simu. Kuna wengine wanafikia hatua ya kukata tamaa, lakini wakiona watu wanawajali, wanafika na kutoa ushauri, nasaha…ushauri huo au nasaha hizo, zinaweza kuwa ni moja ya tiba kwao…Tumuombe mungu atusaidie tuweze kupambana na kuishinda mitihani hii ya maisha na tusiwe wepesi wa kukata tamaa…
No comments :