‘Rafiki yangu mimi ninaumwa sana, sijui kama nitapona..’
akasema mgonjwa.
‘Utapona tu rafiki yangu kuumwa sio kufa..jipe moyo wewe ni
askari bwana, kufa ni kufa tu…’akamwambia.
‘Unajua rafiki yangu, nilikuwa nimedharau sana tatizo
hili….nilijua ni maumivu tu ya nyonga, lakini kumbe tatizo hilo limekwenda na
kuathiri uti wa mgongo, hapa nilipo kiuno chote hakifanyi kazi…ulishawahi
kuteguka nyonga, basi hiyo adhabu ndio inanipata mimi mara kwa mara...’akasema.
‘Pole sana, naelewa..lakini utapona tu…’nikampa matumaini.
‘Sawa, ni kweli imani yangu ni hiyo, nipone…’akasema
‘Oh, unajua wewe ni dharau zako nilikuambia mapema kamuone
dakitari bingwa, ukadharau sasa hali imefikia hapo ulipo, lakini usikate tamaa
rafiki yangu, utapona tu…’akamwambia rafiki yake, kipindi hicho bado wapo
kazini.
Miezi ikapita, na
siku moja, nikaitwa na rafiki yangu huyo, akiwa kitandani, huwa alikuwa anapona
anendelea, hali inarudia tena anakuwa ni wa kitandani, siku aliponiita ndio
anakaweza kuniambi jambo moja ambalo lilinifanya niwe na wakati mgumu…ndio
linanitesa hadi leo, sikutakiwa kuliongea, hadi kaburini, lakini nitafanyaje
kwa hali kama hii…’akasema.
‘Rafiki yangu, hizi kazi zetu bwana, ….niliumia nikiwa
vitani, lakini nani ataelewa,..ukiumia ni unaambiwa ni uzembe wako…sasa
nilichokuitia hapa ni kuwa, nimeenda kupima, kipimo kinachoaminika kabisa…’
akasema.
‘Ehe, umeambiwaje?’ akamuuliza
‘Uti wa mgongo umeathirika sana, wamenipa matumaini,…nitapona,
nitapona… lakini muhimu walichonishauri ni kuwa niachane na kazi ngumu,…na sana
sana kama inawezekana nichana na hii kazi yetu,… sasa sina jinsi inabidi
niandike barua ya kustaafu kabla ya muda wangu…’akasema.
‘Oh..unajua awali nikushauri usifanye hivyo, lakini kwa sasa
kama hali iimefikia hapo basi kapumzike tu….najua umuhimu wa kazi , lakini afya
yako ni bora kwanza,mambo mengine tutaendelea kusaidiana usijali rafiki yangu…’nikamwambia.
‘Sawa ila kuna jambo muhimu nataka kukuomba,..unielewe na
ulikubali, maana sina jinsi na ..nimefikiria sana nikaona wewe peke yake ndiye
unaweza kunisaidia…’akasema.
‘Rafiki yangu hivi mimi nikiwa na tatizo nahitaji kukuomba,
unanieleza tu, tunasaidiana, uniamini mimi, hakuna jambo linaloweza
kushikindikana kati yetu wawili, tumesaidiana mangapi, nashukuru kuwa hata wake
zetu ni kama tulivyo, wameivana hakuna mpaka watu wanatuonea wivu…niambie ni
tatizo gani…?’ nikamuuliza.
‘Oh…, rafiki unaweza kuniona mimi ni mtu wa ajabu sana…,
sijui kama nitakuwa nimekosea, lakini hapana, mimi naona tufanye hivyo,
nakuomba sana, unisaidie hili bila kusita,ni amri kama amri za kijeshi lakini,
lina masharti muhimu sana, unielewe na uyazingatie…..’akasema.
‘Wewe bwana, wewe…wewe sema, toa amri mimi nitatekeleza,
kwasababu kwanza kwa kuandikishwa jeshini ulinitangulia, japokuwa tuna cheo
sawa, lakini wewe ni senior kwangu lazima nikutii, afande, toa amri nitatii…’nikaongea
tukiwa tunatabasamu tu, lkn rafiki yangu hakuonekana mwenye furaha kama ilivyokuwa siku nyingine.
‘Rafiki yangu kutokana na tatizo hili sitawezi kuzaa tena…’akasema
hapo nilikuwa na chupa ya maji ikaniponyoka.
‘Unasema nini…?’ nikamuuliza
‘Hayo ni maneno ya dakitari bingwa, …, na hakuna jinsi hata
kama nitapona, ..ndivyo alivyoniambia huyo docta bingwa, umenielewa, ….’akasema
‘Hapana,…nawaamini sana madakitari lakini, kuzaa ni majaliwa
ya mungu..utapona utazaa tu..muhimu kwanza ni wewe kupona, mengina yatafuta,
tutahangaika pamoja usijali hilo kabisa….’nikamwambia.
‘Nisikilize kwa makini, hili ni siri kati yangu mimi na wewe, sitaki hata
shemeji yako afahamu..unasikia vyema, nataka tufanye jambo, angalau na mimi
nipate mrithi…’akasema.
‘Jambo gani…?’ nikamuuliza sasa kwa mashaka, moyoni nilihisi labda anataka mkewe akapandikizwe mbegu au kitu kama hicho, sikuwa nimewazia jambo kama hilo.
Ukumbuke wawili hawa walishibana sana, na ungeliwaona ungelifikiria
ni mapacha,…kwanza mungu kawajalia wanafanana ...utafikiri ndugu lakini sio ndugu wa baba na mama mmoja, na wakiwemo kazini hadi nyumbani
wapo wawili…,na usingeliwaambia kitu cha kuwatenganisha, watakuumbua. Na mmoja
wapo akiumwa, inakuwa kama na mwenzake anaumwa, asiyeumwa anakuwa hana raha
utafikiri ni yeye anaumwa.
Basi kukatokea maelezo marefu tu.....
‘Nimekusikia rafiki yangu,….lakini ujue hilo ni gumu sana,
kwanza kwa shemeji , pili kwa mke wangu, huoni tunakufuru, ni dhambi kubwa
sana…’nikamwambia, lakini akazidi kunisihi sana,..
'Kitanda hakizai haramu bwana...usiniangushe..'akasema lakini kwa sauti ya huzuni.
Ukumbuke kipindi hicho damu inachemka, na unajua tena sisi
maaskari tukiwa jeshini ni kama wanafunzi tu..watu wa mazoezi kwahiyo uimara wetu wa viwili wili unakua ni chachizo.... Nililichukulia kirahisi tu,
japokuwa sikupenda, japokuwa, nilielewa ni nini maana ya ndoa nilijua nima
kosa, lakini urafiki wetu niliuweka mbele,…si tunasaidiana, yeye na mimi ni
rafiki, lakini tatizo ni jinsi gani ya kulifanya hilo jambo.
‘Sikiliza kama nilivyokuambia hilo ni kati yangu, mimi na
wewe, asifahamu yoyote yule, hasa shemeji, na hata mke wangu hatafahamu,…..jinsi
gani ya kufanya niachie mimi, nitakuja kukuambia….’tukamalizana hapo
***********
Siku baadaye rafiki yangu akanitumia ujumbe nikiwa kwenye
lindo,kuwa nikitoka huko nipitia moja kwa moja nyumbani kwake,..tulikuwa maeneo
ya kambini, na kuna nyumba zimejengwa familia kwa familia, kutokana na kuumwa
kwa rafiki yangu yeye akahamishiwa sehemu tofauti, ni utaratibu tu wa kawaida,
lakini wake zetu, wanakuwa pamoja karibu mchana kutwa, …
Kwahiyo hiyo shughuli aliyonialika ilikuwa kwenye eneo lake…na
kwa ujumla muda huo alikuwa hajambo anavuta vuta muda kusikilizia barua yake ya
kustaafu kwasababu ya afya…, anafanya shughuli ndogo ndogo tu hapo kazini…barua
ikajibiwa kuwa anaweza kuondoka, kwahiyo aliamua afanye shughuli ya kuwaaga
marafiki zake..
Aliniambia mapema tu, lakini kutokana na kutingwa na kazi,
nikawa sipo kwenye kuitayarisha hiyo shughuli..basi nilipotoka lindoni,
nikaelekea nyumbani kwake, ..watu walikunywa, wanaokunywa, ..baadae
wakatawanyika..wakimpa mkono wa kwaheri kuelekea uraiani…
‘Rafiki yangu njoo, lile jambo linatafanyika leo…’akaniambia
watu wakiwa wameshaondoka, hata mke wangu alishaondoka.
‘Jambo gani..?’ nikamuuliza.
‘Aaah, bwana, ingia huko ndani shemeji yako kalewa chakari,
hajitambui..niliamua kumlewesha leo sasa kama nilivyokuambia, kila kitu kipo
tayari,..fanya ufanyavyo, mimi ninatoka, usiniangushe,..’akasema akiwa anatoa
machozi.
‘Lakini rafiki yangu…’nikajitetea
‘Nielewe, nalia, sio napenda, lakini sitaki kumuacha mke
wangu bila kumzalia mtoto, nampenda sana mke wangu, na nilimuahidi ni lazima
tutapata mtoto, sijamueleza kuwa siwezi kuzaa…nataka unielewe hilo , hilo ni
kati yangu mimi na wewe….nakuomba tafadhali, usipoteze muda, jitahidi, na mungu
atatusaidia…oh…hakikisha shemeji yako hakufahmu taa zimezimwa...’akaondoka huku anasikitika.
Nilijiuliza sana, na kabla sijatulia kulifikiria hilo jambo
mara sauti ikaita kutoka ndani
‘Wewe mume wangu mbona unaniacha hivi..njoo, bwana….’ilikuwa
sauti ya shemeji, bila ajizi mimi nikaingia ndani, namkuta oh…kama alivyozaliwa…hebu
fikiria na ujana wangu, damu inachemka, na jeshini usiniambie kitu,……siwezi
kuelezea hapo zaidi, lakini ..sitaweza kuisahau hiyo siku imenitesa.lakini
ungelifanyaje.., kweli pombeni ni shetani.
Masiku yakapita na rafiki yangu alishaondoka yupo kijijini,
tunawasiliana , tunajuana hali,..tunasaidiana, na miaka ikapita,.. lakini hatukuwahi
kuliongelea tena hilo jambo,kama alivyoniagiza tuwe hivyo…na hayo yalishapita,
na kuyasahau kabisa. Na mimi ikafikia muda wangu wa kustaafu,…ilikuwa tustaafu
naye, lakini yeye aliharakisha kutokana na afya yake.
Na mimi nikarudi kijijini,…yeye sasa alikuwa kijijini cha
pili, ila hapo kijijini , yaani hapa, yeye pia alikuwa na nyumba na makazi yake,
tulikuwa hatuachani, hata makazi, maeneo, mashamba tukinunua tunanunua pamoja..kwahiyo
huwa anafika na kuondoka, na mara nyingi hafiki na mkewe,..anasema mkewe ana
kazi nyingi, kukawa na kutengena kwa namna fulani,.
Kuna kipindi mke wangu anakwenda kusalimia, hata mimi mwenyewe…lakini uone
ilivyo ajabu kila tukifika huko tunawakuta wapo wao wawili, yeye na mkewe, wazazi wake wanakuwa hawapo
kwasababu mbali mbali..na mtoto anakuwa sheleni, alikuwa anasoema mbali, analala huko huko, tulishajua kuwa wamejaliwa kupata mtoto,….
‘Rafiki yangu nitahamia huku, ila
mtoto atabakia na bibi yake…’akaniambia siku moja alipokuja kunitembea akikagua nyumba yake, ambayo aliipangisha.
‘Mtoto..wako sijawahi kumuona...ni ajabu kabisa miaka yote hii ’ nikamwambia
‘Ndio…mara nyingi wanakuwa na bibi yao, si unajua tena…
namshukuru sana mungu, angalau nimepata mrithi, ni dume kweli la nguvu…’akasema.
‘Si nilikuambia, usiamini madocta,..unaona sasa..’nikasema
na kiukweli wakati tunaongea hayo sikuwa nafahamu kuwa huyo mtoto ni yule wa
mipango, nilijua kabisa ni mtoto wake,..muda ukafika wakahamia, tukawa tunaishi
pamoja, tunasaidiana, lakini huyo mtoto hakuwahi kufika huku, hadi amekuwa
kijana mkubwa tu..
Siku zikapita, rafiki yangu akawa na hali
mbaya,..tunashukuru kuwa aliweza kuishi muda huo wote tofauti na tulivyodhania,…tokea
astaafu, miaka kumi nane ikawa imepita..hebu fikiria, hatukwahi kumuona huyo
mtoto wao…jamaa kuna muda anateseka na maradhi, lakini afya haikuwa mbaya kama
kipindi hicho, alizidiwa kiasi kwamba tukajua safari imewadia, na siku hiyo
yupo kitandani, anagulia maumivu nipo naye,…mara akaja kijana mmoja.
‘Shikamoo, baba, unaendeleaje..?’ kijana akamsalimia baba
yake.
‘Sijambo kiasi, aheri umefika, ….nilijua hutaniwahi, leo umenyoa mindevu yako,...hahaha, na bibi
yako kakuruhusu ajabu kabisa…’akasema.
‘Kwanini baba unasema hivyo mara nyingi unaumwa kama hivi
unakuja unapona, usikate tamaa baba..’akasema mwanae.
‘Mwanangu, wewe ndiye mrithi wangu…na huyu hapa, ni yule
baba niliyekuambia, mimi sina ndugu wengine,ndugu wengine walishafariki,
aliyebakia ni huyu peke yake na huyu ni ndugu tu wa kufikia, lakini ni zaidi ya
ndugu, huyu ni baba yako muheshimu sana..’akamwambia mwanae
‘Sawa baba shikamoo baba…’akanisalimia na hapo akaniangalia
usoni, unajua,..nilishtuka,…hapo nilikuwa kama ninamuangalia mwanangu soldier,
nilishangaa nikasema hivi…
‘Soldier, umefuata nini huuku..?’ nikauliza kwa mshangao.
NB: Haya siri imekuwa sio siri tena, itakuwaje..
WAZO LA LEO: Urafiki
wa kweli unaonekana kipindi cha dhiki na shida. Inashangaza kweli pale mmoja
anapokutwa na mitihani ya maradhi au umasikini, wengi humkimbia…lakini akiwa
anajiweza watu hujaa tele. Jamani mpaji ni mungu, leo kwa huyu kesho inaweza
kuwa kwako, onyesheni upendo wa dhati kipindi cha shida. Tumuombe mungu atujali
kwa hili tupendani kwa dhati hata ikiwa kipindi cha shida.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment