Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, February 25, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-3


Keleee…vifijo…hoi hoi…shangwe nderemo…vikatanda, pale Soldier alipoingiza mguu wake ndani…’
‘Shujaa, shujaa, shujaa, shujaa…..’
Soldier hakuamini,..alishikwa na butwaa, akabakia kasimama pale mlangoni, ..hakuamini kuwa ndivyo ilivyopangwa hivyo, hakuamini kuwa sifa zake zimefika hadi huku kijijini..kiukweli alikuwa shujaa huko alipokuwa alifanya mambo mengo ya ushujaa…
Kwa kitendo hicho akili ya mawazo yake ya sintofahamu, yakatulia, sasa yakaendana na tukio hilo…sasa, faraja, upendo..vikatawala kwenye ubongo wake, kumbe wanandugu,wanafamilia, jamii kwa ujumla inampenda kihivyo, hakuamini…akabakia kutikisa kichwa tu, na tabasamu,..akazuia machozi yaliyoanza kumtoka,…akageuza kichwa huku na huku kuwatizama waliokuwepo,..

Wapo baba na mama wa pande zote,…yaani ukweni na kwake,… wapo pia wadogo zake, shemeji zake,…wapo majirani..wapo pia maaskari wenzake, ambao alikuwa nao huko kwenye misheni ya kimataifa ya kulinda amani…alishangaa kumbe na wao walialikwa hapo,…oh, akafarijika sana,…

Akainua mguu wa pili kuingia ndani, …na wa kwanza kuja kumkumbatia kwa bashasha alikuwa baba yake mzazi…,huyu ndiye aliyemlanda,wanasema nyoka huzaa nyoka, basi hapo ilitokea kweli, baba mtu aliwahi kuwa askari na mtoto naye sasa ni askari…, tabia na miendendo ni ile ile ya baba na mtoto, labda imetofautiona kidogo kutegemeana na nyakati….

Baba alimkumbatia mwanae akimpiga piga mgongoni, halafu akamshika mwanae mkono, wakaangaliana usoni, huku wote wakitabasamu, na baba mtu akamnongoneza kitu sikioni mwanae,..kwa kusema hivi:
‘Sasa umekuwa mwanangu, sasa nahisi faraja, …ila kabla ya yote uwe na subira…usije kuchukulia mambo kwa pupa…nitakuja kukuambia mwenyewe ni nini kinachoendelea, ..najua, na hata ingelikuwa mimi, ningechukua hatua kali sana, lakini …usije kumvunja mama yako moyo, yote hayo ni kwasababu ya mama yako…na hataki kuniambia ukweli, sasa..tuwe na subira….’halafu kwa haraka akamshika mkono na kuanza kumtambulisha kwa wageni.

‘Wanandugu,mimi ni baba yake, mimi ndiye mlezi wake, nikiwa humu mimi ndiye mwenye mamlaka,…nachukua nafasi hii kuwakaribisha wote, japokuwa tulishakaribishana..ila kwasasa nahisi watarajiwa wote wamefika…hasa wale waliokuwa pamoja na mwanangu huko walipokuwa..ni vita, ya kuwasaidia wenzetu,…kwahiyo kazi waliyokuwa wakiifanya ni ya kujitolea…

‘Huyu mwanangu pia na wenzake waliokuwa huko mstari wa mbele pamoja, tunashukuru sana kuwa wote wamerudi salama,..…sisi kama wanakijiji tuliona tulifanye hili kama familia ya kijiji..Nashukuru kama kiongozi wenu wa kijiji mliitikia hili tukashirikiana pamoja, na tumelifanikisha, hongereni sana na ahsanteni sana…’akawa anaongea na watu wakamshangilia.

Soldier pale akili yake ilikuwa mbali, akawa kila mara anatafakari maneno ya baba yake, hasa pale alipoambiwa;
‘..Najua, na hata ingelikuwa mimi, ningechukua hatua kali sana, lakini …usije kumvunja mama yako moyo, yote hayo ni kwasababu ya mama yako..

‘Ina mama anahusika na hili….haiwezekani, mama yangu mwenyewe…’ akawa anatikisa kichwa cha kutokukubaliana na hilo, na hapo akageuza kichwa upande ule walipokaa akina mama na akamuona mama yake akiwa amekaa mstari wa mbele na dada zake,..huku kashika shavu, mama yake hakuonekana mwenye raha kama walivyokuwa wengine. Anamfahamu sana mama yake,ni mpole,..na wakati mwingi sio mcheshi wa kuruka ruka, kuongea sana, japokuwa ni mkarimu sana, ataongea maneno machache tu…basi kamaliza

Soldier anampenda sana mama yake, anakumbuka kuna kipindi aliwahi kupigana na baba yake kwasababa baba yake huyo alikuwa akimpiga mama yake..na, kitendo hicho anakikumbuka hadi leo kwani kilimfanya yeye na baba yake wakae karibu wiki nzima hawaongei lakini baadaye yeye mweneywe akajua kafanya kosa akaenda kumpigi baba yake magoti.

Baba yake alipoona mwanae anafanya hivyo, akatikisa kichwa, …akamzuia mwanae asimama na kusema;

‘Haina haja ya kunipigia magoti…najua mimi ndiye niliyekosea, lakini wakati mwingine inabidi tufanye hivi,..sio kwamba napenda,..hulijui hili, ila ipo siku utalijua… hawa akina mama, hawa…..wanawake, wengine inafikia wanafanya mambo kama watoto, inatokea, hata sisi wanaume tunaweza kufanya mambo ya kitoto, inatokea,…sijui kwanini…lakini mwanangu utakuja kuoa, haya utakuja kuyaona,..ni kawaida, sio kosa lao,..sio kosa letu, ni ubinadamu, na akina mama, wengi  wanapenda kudekezwa…’akaambiwa.

‘Lakini baba mungeyaongea tu ndani…, sio kumpiga,..mama mwenyewe mpole..nasikitikka sana kufikia hali hii…’akasema

‘Najua sana,..mimi ninamfahamu sana mama yako, kuliko unavyofikiria wewe, na kama isingelikuwa ukali wangu, mamaa yako angelikuwa hata sijui nisemeje, ana huruma kupitiliza, ni mpole kupitiliza, na yupo tayari vitu viharibiwe, hapana mimi siwezi….anaonewa tu…inabidi nimkomaze,… niseme hivyo, upole umemzidi….ila unielewe kitu kimoja,…’akatulia

Mimi ni najua ni nini ninachokifanya, usipende kuniingilia pale ninapotimiza wajibu wangu, kama mume, … tutakosana, hii ni ndoa yangu na wewe utakuja kuwa na ndoa yako… hujui ni nini mama yako alichokifanya, na ameniomba msamaha sana..sina tatizo na yeye yaliyopita yamepita,..ila nakuonya sana mwanangu, uwe makini sana..hasa ukioa ..najua wewe una tabia kama yangu,… chunga sana mkono wako, usije ukawa kama mkono wangu…’baba yake alimuambia hivyo..

Alipokumbuka maneno hayo akageuza kichwa kumuangalia mama yake, na macho yao yakakutana, na mama akawa anamuangalia tu, bila kushusha macho yake, yeye, akashusha ya kakwe,..hakutaka waangaliane sana,…hataweza kuvumilia,… na sasa akageuza kichwa kuangalia walipokaa wakwe zake…baba mkwe, mzee Simba, jabari kuliko majabari, simba wa nyikani aliyewahi kupigana na simba na kumuua kwa mkono wake mwenyewe…ni simba ni kweli..mungu kamjalia minguvu,… akakumbuka kauli yake wakati anamposa binti yake;

‘Kijana nikuonavyo wewe ni sawa na baba yako,…baba yako ana hasira, hajui kuhimili, ila nampenda sana, anajua kuhudumia familia,..ndio maana akanishinda kwenye chaguzi za uongozi wa kijiji,.. yeye ni mfano hapa kijijini, kaunganisha wanakijiji, kwenye shida na njaa, baba yako alipoacha uanajeshi alikuja moja kwa moja hapa kijijini,..tukaungana naye pamoja…sasa umezidisha ujirani wetu na umoja wetu, kwani umekuja kumuoa binti yangu..ila nakuonya sana…’akakumbuka maneno hayo aliyoambiwa.

‘Mwanamke hapigwi kwa fimbo, mingumi,….kama unapigana na mwanaume mwenzako,..mwanamke hupigwa kwa kauli nzuri tu, mimi na miguvu yangu yote sijawahi kumpiga mke wangu, ananiogopa sana,…wanasema mwanamke hapigwi kwa fimbo anapigwa kwa nini vile, …upande wa khanga..sio hivyo…., kuna namna ya kumnyosha mke wako, maana yeye sio mtoto mdogo, ana akili timamu,..amelelewa na wazazi wake..ana heshima zake, sasa itunze ile heshma yake kwa maneno ya hekima…unanielewa…’aliambiwa.

‘Ole wako,..nikisikia umempiga mwanangu..najua yapo matatizo yatatokea kama familia, hilo lipo wazi,.., najua..kuna kukwaruzana, sasa sitaki nisikie umempiga mwanangu…kupiga, kwanza kwanini umpige kwa mingumi , fimbo..huyo sio mtoto mdogo…inawezakana ikatokea, akamzaba kibao kimoja..viwili ok.., hata yeye anaweza kufanya hivyo kwako....inatokea, lakini sio kumpiga unanielewa….kumpiga..unanielewa…’akaambiwa.

‘Narudia tena ole wako…nawafahamu sana tabia zenu,..huyo binti yangu mpendwa, ninayempenda sana…amamranda sana mama yake, nikimuona yeye namuona mama yake….sasa uharibu kiyoo changu uone niakavyokufanya, mimi ni simba simba wa nyika uliza watu watakuambia…..’halafu akampiga kwa ngumi begani ngumi yenye nguvu inauma,..jamaa anasema maumivi yake anayakumbuka mpaka leo. Baba mkwe alipoona mkewe anamuangalia akmuonyeshea ishara ya dole…kileo dole tupu!

Pembeni ya huyo yupo kaka mtu, ….huyo ni adui yake tokea utotoni, walikuwa kila siku wanapigana, mpaka walipofikia utu uzima ndio wakawa kidogo wanaheshimiana, anakumbuka kaka mtu huyo hakupenda yeye amuoe dada yake, kwani siku zote alimuona yeye kama adui yake..lakini wazee waliingilia kati ndio wakaja kufunga ndoa hata hivyo kaka mtu huyo hakuhudhuria hiyo harusi yao,..leo yupo kwenye shughuli, …

Soldier, aliwaangalia wengi wenye sifa hizi na zile, lakini baadaye uso wake ukarudi kwa mama yake, mama yake alikuwa bado amemtizama, mpaka soldier akaingiwa na mashaka…anamfahamu sana mama yake akiwa na jambo anataka kukuambia, inachukua sana muda kukuambia, huwa anliwazia sana, na hataki kukurupuka tu,, na jinsi alivyomuona akimuangalia,akahisi kuna jambo..akatamani atoke pale amuendee mama yake ,amuambie watoke nje, wakaongee, lakini hapo kuna utaratibu hauwezi kuuvunja…kwani mpaka muda huo alikuwa hajapewa nafasi ya kusamiliana na wengine akiwemo mama yake.

‘Sasa ndugu zanguni, najua wengi mna hamu ya kumsikia shujaa, awasalimie kidogo, leo ni kusalimiana kidogo tu,…najua mna hamu ya kusalimiana naye mkono kwa mkono, lakini kwasasa siwezi kumruhusu, mila zetu zinazingatiwa, atawasalimia kwa ujumla kwanza ataanza yeye kama mwenyeji wa nyumba hii, halafu atawaita wenzake mmoja mmoja..tunataka kusikia mikakati yao ya kuendeleza hiki kijiji, ndio maana ya kusoma, ndio maana ya kuwa kwenye nyadhif, kukumbuka kwenu na kujua ni vipi utaendeleza jamii ya kwenu …

‘Mke wake yupo..?’ akauliza na alipotaja hivyo Soldier alihisi damu ikimchemka,…na mara mkewe akatokea kwa nyuma akiwa amembaba mtoto..amakabidhi mtoto yaya wake na kuelekea pale mbele waliposimama baba mkwe wake na mumewe…

‘Njoo hapa maana wewe unadhima kubwa leo,…kuhakikisha mwanangu anapoteza mawazo yote ya kwenye vita, awe furaha zaidi ya ile ya fungate…’watu wakashangilia
‘Eeeh, mnielewe neongea kiutu uzima hapa..sio lugha za sasa hivi za kukera….au sio ..vinginevyo..eeh’akacheka akigeuka kumuangalia baba wa mkwewe.

‘Najua baba yako yupo hapo, simuogopi mimi, tumekuwa hivi, ngumi ngumi utotoni, hadi leo tunapambana kwenye uwanja wa siasa,..lakini ukweli ni ukweli tu....lazima watoto wetu walelewe kwenye maadili mema, ikibidi nguvu ..haya,…japokuwa siku hizi hizi weeeh, …’akasema na watu wakacheka.

‘Unajua mimi na mwenzangu pale tulikuwa kama simba na yanga…hata hivyo mwisho wa siku tunakula na kucheka, ndivyo maisha yalivyo, ni ajabu watu mnakuwa madui kwenye ushabiki hadi kwenye misha ya kila siku , huo ni ulimbukeni,…malizeni ushabiki , mnarudi mnanunuliana zawadi mshindi kashinda mpe haki yake,,..sasa mama mkwe ni hivi, kiutaratibu wetu, wewe unakwenda kwa mumeo unamshika mkono, msogee pamoja pale mbele, hicho ni kimila chetu....halafu kwa unyenyekevu unamkaribisha mumeo nyumbani, …ukimaliza hapo, yeye, ataomba kibali kwangu, ili aongee..jamani si ndio hivyo…eeh, sisi tunawaheshimu sana wanawake,..wanawake mbele..’akasema na akina mama wakaitikia mbelee, na vigelegele..

‘Bila wanawake sisi sio kitu, mwanamke ni shujaa, anajua kuihudumia familia yake, watoto na mumewe, anamfanya mwanaume aitwe mwanaume, bila mke mwanaume sio mwanaume, au sio..wanawake mbeleeee…’ akasema na wanawake wakashangilia na kucheka, kukachangamka kweli, vigelegele na wakati huo mke mtu akawa anafanya kama alivyoagizwa.  na kabla hajaendelea zaidi mtoto akawa analia..kilio kikubwa,..

Mtoto wao…. Mke mtu akageukia kule kilio kinapotoka, mumewe hali kadhalika,….

‘Mlete huyo mtoto huku mbele anataka kumuona baba yake…’akasema baba mkwe, na Yaya akawa anakuja na yule mtoto kuelekea pale waliposimama Soldier na mkewe,…

Na wakati huo huo… na kule mlangoni akawa anaingia yule dereva,..Soldier akamuona, na kugeuza kichwa kuelekea kule mlangoni, kitendo hicho kiliwafanya hata watu wengi wageukie kule mlangoni…

NB: Jamani simu haitaki niendelee..

WAZO LA LEO: Mke hapigwi kwa ngumi na fimbo..mke hupigwa kwa upande wa khanga, ni maneno yenye hekima sana,..nayapenda sana, na nawashangaa wale wanaopiga wake zao kama watoto wadogo..nasikia kuna wanawake pia wanawapiga waume zao! Halafu haya hufanyika mbele ya watoto au mbele ya watu wengine. Hayo ni makosa, tuchunge maadili ya ndoa zetu,..tukumbuke mke ni mzazi mwenzako, ni ubavu wako, ana heshima zake…unavyomtendea hivyo unawafunza watoto nini hapo, na wao waje kufanya hivyo hivyo au! Ukumbuke huyo ni mtu mnzima tendo kama hilo linamtesa..linamnyong’onyesha, unamuumiza mwenzako kisaikolojia,..njia njema, muite mwenzako chumbani, muongee, mpeane maadili mema, ya hekima, na hata kama kutakuwa na kusigishana, ikabidi,..maana binadamu wote sio sawa,muyamalize huko huko chumbani.
Ni mimi: emu-three

No comments :