Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, February 24, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-2


Bila ajizi japo kwa kusita Soldier akamchukua yule mtoto kutoka kwa yaya, alimtambua huyo binti kuwa ni yaya, kwa vile ndiye aliyekuwa muda mwingi kambeba huyo mtoto, na mkewe kuna muda alitamka maneno yakuashiria hivyo kuwa huyo ni yaya, lakini alikuwa hajamtambusliha rasmi,..

‘Ni yaya…yaya wa mtoto, …mtoto wetu…’akajikuta akisema hivyo huku akimuangalia mtoto usoni.
Mtoto mnzuri mwenye afya tu…

Kila alivyozidi kumkagua huyo mtoto alikuwa akihisi mwili ukimcheza, na hali hiyo ilimuanza pale mtoto alipofika mikononi mwake,..alishangaa…na kilichomshangaza zaidi ni …ni machozi, yeye.ni kawaida yake hasira zikimzidi sana hutoa machozi, na akitoa machozi kama ni adui yake atafute sehemu ya kujificha..na pia....hata furaha, akiwa na furaha sana huwa anajikuta akitoa machozi, sasa hapo hata yeye mwenyewe hakufahamu kuwa machozi hayo ni ya furaha au hasira.

Akawa kampakata yule mtoto vizuri, huku akimkagua,..sura…anafanana na nani huyu mtoto,....labda mama yake,..hakuweza kulithibitisha hilo, ndio mkewe anamfahamu sura yake,..lakini hakuweza kumfananisha na huyo mtoto…

Kitu kilichompa shikinikizo la damu ni….umri,…mmh, hata mtoto mdogo atatambua tu kuwa huyo mtoto ni kati ya miezi mitatu, au mitano…sasa hii ina maana gani,…

‘Huyu mtoto ana umri gani…?’ akajikuta anauliza, lakini hakuna aliyekuwa karibu yake kumsikiliza,…akawa anajizuia, maana alihisi machozi yakimjia kwa kasi..
‘Whats the problems…’akajiuliza mwenyewe

Wakati huo mtoto yupo mikononi mwake, akiendelea kumkagua,..mkewe na yaya, pamoja na dereva walikuwa kwenye shughulika za kuingiza mizigo kwenye gari....yeye hakujali tena, hakujali tena kuwa kuna zawadi nyingi tu kaja nazo na alitaka ahakikishe zimefika kwa walengwa hasa mkewe..kwa muda huo,..alichojali ni kuhusu huyu mtoto..

‘Mume wangu kuna mzigo mwingine, naona yote iliyoandikwa jina lako imeingia kwenye gari..?’ ilikuwa sauti ya mkewe

‘Ok, hakuna mingine ni hiyo tu,,…’akasema sasa akizungusha kichwa kukagua lile eneo alilokuwa ameweka mizigo yake, na alipona hakuna mzigo uliobakia, akahema kwa nguvu.

‘Haya twendeni…’mkewe akasema sasa akitaka kumpokea mumewe mtoto lakini mumewe akawa anatembea kuelekea kwenye garii, kama vila hamuoni, huku akiendelea kumkagua yule mtoto machoni, mtoto alikuwa kalala…kafumba macho.

 Wakati wanataka kuliingia kwenye gari, yule yaya, akataka kumchukua mtoto, yeye akasema;

‘No…hapana acha nikae naye…’akasema na kweli akaingia kiti cha mbele na kumweka mtoto vizuri mapajani kwake. Hapo sasa kuna muda akashindwa kujizuia, akawa analia, anatikisika mwili mnzima akijizuia hiyo hali isionekane.. …mpaka dereva akashangaa, …na bahati nzuri tendo hilo mkewe na Yaya hawakuliona maana walikuwa kiti cha nyuma wakihangaika kupanga vitu vizuri, …

‘Vipi bro, ni kawaida, mtu ukitoka vitani salama.. huwezi amini , ni jambo la kushukuru sana…, na naona una bahati sana kuwa umerudi na una zawadi ya mtoto..’akasema dereva

‘Mhh…’akaguna.

‘Huko ulikaa muda gani vile…?’ akauliza huyo dereva

‘Miaka mitatu….’akasema

‘Miaka mitatu!, Mingi sana….Oh, kwahiyo ulikuwa unarudi rudi hivi…na bahati, ukajaliwa kutengeneza mtoto,…maana huyo mtoto ni miezi mitatu au mine hivi au sio…, ulikuwa mjanja sana, hukutaka mkewe abakie mwenyewe, lakini uliwezaje kurudi rudi, kwani mlikuwa nchi gani..?’ yalikuwa maswali ya dereva ambayo hakutaka kuyasikia.

‘Usijali nitakuja kuwasimulia kila kitu, lakini sio sasa,…endesha gari….’akasema kwa sauti iliyomfanya dereva ashtuke, na sijui ni kama vile dereva alielewa au vipi…akatulia kimia akiendesha gari….mara huyo dereva akaanza kuimba huku anaendesha gari…

‘Kitanda hakizai haramu, hakizai haramu, pupupupu..titititi dindidi…kitanda hakizai haramu,  haramu haramu, …’

‘Wimbi gani tena huo dereva…?’ aliyeuliza swali hilo ni mke mtu.

‘Si unajua mambo zangu, nafanya mambo mengi, ilimradi riziki iende kinywani, wakati mwingine nashughulika pia, na eeeh, kuimba, nina kundi la ngoma za kienyeji,…sasa huo wimbo wa ‘kitanda hakizai haramu, ndio upo kwenye chati, na jana ulishika namba moja kwenye harusi ya jamaa mmoja, tukianza kuuimba, wakina mama wanasimama..…’akasema.
Kitanda hakizai haramu eeh, kitanda hakizai haramu..tinditindi..tititi…..’akawa anaimba huku akachezacheza kwenye kiti

  Kiukweli, huo wimbo na maneno yake ilikuwa kama kitu kimemgonga Soldier kichwani, ni kama vile alizinduliwa kutoka kwenye dimbwi la ubumbuwazi, mnzito, sasa akaanza kuelewa, …ina maana gani hii,  ina maana mke…kani…kafa..kani…ka, ..haiwezekani, sio mke wake,…
‘Hawezi kunifanyia hivyo, hapana…’akajikuta katoa sauti, na dereva akamgeukia na kusema;
‘Ni kweli…..’akasema dereva
‘Ni kweli nini..?’ akauliza Soldier
‘Ninaimba kwenye kikundi cha ngoma…waulize hata familia yako wananifahamu…’akasema dereva.

Hapo Soldier, akageuka nyuma kuwaangalia mkewe na yaya, wote walikuwa wakitabasamu kwa furaha hakuna aliyeonyesha mashaka yoyote…, hasa mkewe, mkewe alikuwa na furaha mpaka unaihisi.

‘Mume wangu samahani sijakutambulisha,…huyu ni yaya wetu…nilimchukua maalumu kwa ajili ya mtoto….’akasema mkewe.

‘Mhh…’jamaaa akaguna tu.

‘Utampenda sana, ni mchapakazi, anajua kulea, usafi…yaani nashukuru mungu, nina imani kuwa mtoto wetu yupo kwenye mikono salama…’akasema mkewe

‘Sawa kabisa…ni vizuri…’jamaa akajibu.

‘Anaitwa Switie…sijui kwanini walimchagulia jina hilo…’akasema mkewe

‘Labda ni mtamu sana…’akasema dereva na huyo yaya, akasema;

‘Mama yangu aliniambia kuwa jina hilo ni kwasababu kipindi akiwa mja mnzito alikuwa akipenda sana vitu vitamu, ndio akapenda kuniita jina hilo, kutokana na docta mzungu aliyemzalisha, alimuambia aniite jina hilo….’akasema.

‘Kitanda hakizai haramu eeh, kitanda hakizai haramueeh…tindi tindi tindi….’dereva akawa anaimba wimbo wake.

‘Sitaki huo wimbo..’ilikuwa sauti ya Soldier, na jinsi alivyotoa sauti  ilimfanya dereva ageuze kichwa kumuangalia huyo jamaaa kwa mashaka, halafu akatulia na baadaye akasema;

‘Sawa bosi,…sawa afande…’akasema akigeuza geuza kichwa kumuangalia Soldier, na huyu askari sasa alikuwa kajiegemeza kichwa kwenye kiti akiwa kazama kwenye mawazo…

***********

 Huyu mtoto ni damu yangu kweli…miezi mitatu..haiwezekani,…kama sio damu yangu, … ni nani kampa mimba mke wangu,…
Hapo akainua kichwa na kugeuka kumuangalia mkewe, na mkewe kwa muda huo walikuwa wakiongea kitu na yaya, wkawa wanacheka,…

‘Huyo mtu…kichwa chake ni halali yangu…tutkula sahani moja, mimi na yeye…., ile hasira ya kumkosa adui yangu mmoja vitani itarudia kwake, alikumbuka jinsi alivyomkosa adui yake kwenye vita, .ilikuwa ni ambush, waliianda vyema kabisa, wakawazingira maadui,…lakini kiongozi wao aliweza kutoroka, sasa hiyo hali ya kumkosa kiongozi wo ilimuuma, sana, akasema atafanya juu chini mpaka ampate huyo kiongozi wao..wa maadui.., lakini mpaka wanamaliza huo mkataba hakuweza kumpata.

‘Baba wa huyu mtoto atalipa….’akajikuta akisema kwa sauti, japo ni ndogo, lakini dereva alisikia,

‘Baba wa mtoto, nani huyo, kwani wewe sio baba wa huyu mtoto…?’ akauliza huyo dereva kwa sauti kama ya utani!

‘Nani kakumbia hivyo…?’ askari akauliza akiwa kakunja uso, na dereva alipokutana na hiyo sura, alitikisika, karibu ayumbishe gari

‘Oh..samahani nimesikia tu, ukisema ;’baba wa huyu mtoto atalipa…’akasema dereva.
‘Sawa, wewe endesha gari, …’akasema Soldier, na dereva akawa anaendesha gari kimia, na mara kwa mara anageuka kumuangalia huyo askari, na muda fulani wakakutanisha uso, kila mmoja akimuangalia mwenzake,…, na sijui ilikuwaje, Soldier akahisi jambo,.. kuna kitu kikamvuta, sura ya huyo dereva,..mbona..hapo kwa kuhakikasha akamtizama mtoto, kwa muda huo kitoto kilikuwa kimeamuka kimefungua macho…

‘Oh….’akaguna, na muda ule dereva alikuwa ameshafungua mlango kutoka nje ya gari…

‘Tumefika jamani….’ilikuwa sauti ya mkewe, na ikawa sasa ni shughuli ya kushusha mizigo na kuingiza mizigo ndani ya nyumba,

Soldier, akawa naye anateremka kwenye gari huku kambeba mtoto, hakutaka kumuachia, alikuwa kama kashikilia ushahidi, hataki umponyoke, lakini sasa alikuwa akitaka kumkagua usoni, dereva, kuna kitu kahisi, lakini ikawa sio rahisi maana watu walishafika kuwapokea,..wazazi, ndugu..na hatimaye mtoto akawa kachukuliwa na mkewe..

‘Ngoja mtoto akanyonye…’alisema mkewe akimchukua mtoto kwa mumewe, ambaye alikuwa hataki kumuachia,lakini hakuwa na jinsi, akageuka kumtafuta dereva,..alikuwa hayupo , akawa anageuka huku na kule,..alipoona hamuoni akamwambia mkewe…

‘Ok…na naomba dereva asiondoke…’akasema

‘Kwanini!!, mbona yupo kazini, …tumemkodi tu mara moja, ..’akasema mkewe akiwa anataka kuondoka na mtoto hakuonyesha wasi wasi wowote.

‘Nasema hivi, dereva asiondoke,…nataka awepo..si kuna sherehe, na yeye awepo basi, au,…?’akasema akiangalia jinsi kulivyopambwa kishughuli, na alijua ni kwa ajili yake, … shughuli ya kumkaribisha, na mkewe hakusema neno, akaondoka kuelekea ndani yeye na mtoto, pamoja na yaya.

Soldier akaangalia huku na kule hakumuona dereva, ila gari lake lilikuwa bado hapo nje,…akaanza kutembea kuelekea ndani, akili ilikuwa imeshawekwa kwenye uwanja wa vita, lakini hamjui adui yake ni nani….
‘Nitamjua tu…’akasema akiangalia huku na kule, akijaribu kumtafuta mtu wake, na mara akagongana na jamaa akiwa ametokea ndani,..akiwa na haraka.

‘Oh sory….’alikuwa ni dereva, na soldier alipogundua kuwa ni huyo dereva akasema;

‘Usiondoke,…ukaribie kwenye shughuli….’akasema askari

‘Bila shaka, hata kama nitaondoka, ..nitarudi tu, hapa ni nyumbani mkuu…’akasema huyo dereva akitabasamu, na haraka akawa anatembea kuelekea kwenye gari lake huku akiimba wimbo wake…
‘Kitanda hakizai….’akakatiza huo wimbo alipokumbuka kuwa aliambiwa asiuimbe,..akageuka kumuangalia askari ambaye kwa muda huo alikuwa akiingia mlangoni huku anatizama nyuma kumtizama huyo dereva…

NB: Jamani shida kutokuwa na chako,…jembe limeharibika

WAZO LA LEO: Hisia, au dhana, inaweza ikakufanya ukakufuru, hasa unapokuwa kwenye mitihani ya matatizo, inaweza kukufikia hali ya kumdhania kila mtu ni adui yako, kumbe sio…Muhimu tuwe na subira, tujitahidi kuchunguza kwanza, kujirizisha kwanza,…subira na kuhakikisha tunatenda yaliyo mema, tutafanikiwa.
Ni mimi: emu-three

No comments :