Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, February 17, 2017

FUPA LILILOMSHINDA FISI-5


  
  Ilikuwa ndani ya ofisi ya mpelelezi….

 Mpelelezi aliendelea kupitia mkabrasha , akisoma kumbukumbu za nyuma,…na sasa alikuwa kashika file la Mzee, mtu aliyekufa kwa kujinyonga, lakini kifo chake kina utata,..akawa anasoma maelezo yake,..,…akajikuna kichwa kwa haraka haraka.


‘Hiki sio kifo cha kujinyonga,…kuna namna….’akasema kwa sauti ndogo. Akumbuka jinsi alivyoambiwa na mkuu wake wa kazi.

‘Kuna kesi nataka uifuatilie wewe, … ninataka utafute ukweli halisi  wa kifo cha huyu mtu, anayeitwa mzee,…sijapata malalamika ya familia kibarua, au wanafamili kufika hapa kulalamika, lakini ni wajibu wetu, kuhakikisha haki inatendeka, nahisi kuna jambo zaidi lililofichika, nataka uligundue na ukweli ubainike ili haki familia ya marehemu huyo iridhike….’akaambiwa

‘Sawa mkuu….’akakubali hivyo.

Na siku hiyo alipopewa maagizo hayo aliamua kwanza kwenda kutembea eneo alipojinyongea huyo marehemu na kuongea na baadhi ya watu..lakini hakuweza kuongea na wanafamilia , kwani wanafamilia walikuwa kwenye sughuli za kumaliza msiba, …

‘Nitakuja siku nyingine…’akasema na kuondoka.

Leo asubuhi, akaanza hiyo kazi rasmi kwa kupitia nyaraka na kumbukumbu zilizokusanywa hapo ofisini kwao…kazi ilishaanza, akili za likizo zilitakiwa kuondoka akilini mwake,…wakati anapitia nyaraka za hicho kifo, akakumbuka jinsi watu walivyokuwa wakiongea,…

‘Kifo hiki ni cha aina yake, haiwezekani Mzee kujiua, lazima kuna jambo,…’akasema mtu mmoja.

‘Au ndio hayo mashetani ya mdudu mtu…’mwingine akasema.

‘Mdudu mtu! Mdudu mtu gani, acheni hayo jamani,..nani aliwahi kumuona huyo mdudu mtu, ..huo ni ujanja ujanja tu wa watu, wanatuhadaa ili watimize malengo yao, ingawaje siku ya mtu ikifika ya kufa, ni lazima kuwe na sababu, lakini hiyo sababu lazima itizamwe kwa uadilifu, msikimbilie imani hizo haba za kupandikizwa, tutafute kweli alijiua, na kwasababu gani…’akasema mtu mmoja wa imani ya dini.

Mdudu mtu….

Mpelelezi, akakumbuka, hiyo habari ya mdudu mtu, alikumbuka jinsi jina hilo lilivyotokea, ni kipindi alipokuwa akijiandaa kwenda likizo, kuna habari zilienea kuwa kuna uchawi, na huyu mchawi anajigeuza kuwa mdudu, anapenya kwenye ubongo, na kuharibu akili za watu…watu wanajikuta wanatoa kila walicho nacho,….!

Habari hizo zilienea sana hadi zikafikishwa kituo cha polisi, na wakati anaondoka likizo , aliacha wenzake wakilifanyia kazi hilo tatizo, hakufahamu zaidi kilichoendelea, …

‘Nitalifuatilia hilo baadae, kwanza ni hili la kifo cha Mzee…’akasema huku akizidi kupekua pekua!

 ‘Mimi namfahamu sana, mzee, sio mtu wa kufanya jambo kama hilo..hapo kuna mkono wa mtu, na kama polisi hawatagundua kitu, sisi tutafanya mambo yetu kimila,…tutahakikisha haki inatendeka,….’aliambiwa na mzee mmoja wa kijiji, alipoongea nayee.

***********

Kifo cha Mzee kina utata….

 Mpelelezi sasa akawa anapitia nyaraka ndani ya faili la marehemu Mzee, moja baada ya nyingine…alipofika sehemu ambayo inaelezea kuwa marehemu alifika hapo ofisini akiwa na taarifa…akaacha kuendelea kusoma kwanza,  yaliyoandikwa, akalichukua lile kabrasha (file)  na kutoka nalo nje ya ofisi yake alikwenda moja kwa moja hadi kwa katibu muhitasi wa mkuu wake wa kazi.

Amezoea kutaniana sana na huyo mwanadada, lakini  kwa muda huo hakutaka utani, alionyesha ule uso wake wa kikazi, na alipofike kwenye meza ya huyo mwanadada hakutaka kuangalia huyo mwanadada anafanyakazi gani, akasema;

‘Samahani dada,..kuna kitu nataka kukuuliza…’akamwambia huyo katibu muhutasi , ambaye humo ofisi wanamtambua kama KM…katibu muhutasi wa mkuu….

‘Nipo bize kidogo, ni kuhusu nini…?’ akauliza huyo dada akikunjua uso, uliokuwa umejikunja kutokana na kuzongwa na kazi, akatabasamu kujali miiko ya kazi yake, tabasamu anapokujia mteja,…aliendelea kuchapa barua, bila kumuangalia mpelelezi, na alipoona haambiwi kitu zaidi, akainua uso na kumuangalia mpelelezi, na uso aliouona akajua huyo mtu kaja kikazi zaidi.

‘Ni kuhusu kifo cha Mzee…’akasema , na alipotamka hilo neno, aliona yule mwanadada akiacha kuandika ile barua, akahema kidogo,  na uso wake ulionekana kubadilika rangi,…na japokuwa huyo mwanadada alijaribu kuificha ile ile, lakini mpelelezi alikuwa keshagundua.

Mpelelezi, alihisi huenda huyo mwanadada ni mtu wa karibu sana na marehemu, akasema;

‘Pole sana, sikujua kuwa wewe ni mtu wa karibu na huyo marehemu, ni nani wako…?’ akamuuliza

‘Hapana mimi sio mtu wa karibu na marehemu,..yeye nilimfahamia hapa hapa, ..mara ya kwanza kumuona na ya mwisho ilikuwa siku alipofika kutaka kuonana na bosi…’akasema

‘Mhh…mbona nilipokutajia jina lake, ukaonekana kama kuguswa sana,…?’akauliza mpelelezi

‘Ni kawaida yangu, mtu nikiwa nimemfahamu na nikasikia kafariki, najisikia vibaya sana…..Tafadhali..kidogo, hebu kwanza nimalize kazi za mkuu, maana naona utanichanganya…kuna kazi bosi anaisubiria…’akasema huyo mwanadada.

Mpelelezi akilini aliweka alama ya kuuliza, lakini hakuichukulia maanani,  akamtupia jicho tena mwanadada kwa haraka, akamuona mwanadada huyo akiendelea na kazi zake tu, mpelelezi akageuka kuondoka, akipanga kuja kuongea tena na mwanadada huyo, alihisi anaweza kupata  jambo  hapo….

‘Huyu lazima ana jambo….’akasema huku akitembea kurudi ofisini kwake, akageuza kichwa kumtizama mdada, alimuona akiendelea na kaze zake tu.

Alipofikia mlango wa ofisi yake,… akashtuka, anakumbuka alifunga mlango,ukajibana vyema, sasa upo nusu wazi, ina maana kuna mtu kaingia ndani…! Kaingia saa ngapi, na mbona hakumuona wakati anaongea na mdada akausukuma mlango kwa haraka, na tahadhari,

Tahadhari ni moja ya kazi zao, hata kama upo kwako….!

Mkuu wake wa kazi alikuwa kakaa kwenye kiti cha wageni na mkononi kashikilia faili kubwa la boksi..

‘Oh, bosi, sikujua kuwa umeingia huku…’akasema mpelelezi

‘Hamna shida, nilikuja kuulizia umefikia wapi kuhusu upelelezi wako kuhusu kifo cha mzee, maana hiki kifo cha huyu mtu kimenigusa sana,…nahisi kama nawajibika na hicho kifo…’akasema

‘Kwanini mkuu unasema hivyo…?’ akauliza mpelelezi.

‘Najuta kwanini sikuzifuata hisia zangu siku ile... Unajua,..siku ile nilitaka kumwambia asiondoke, abakie humu kituoni kwa ajili ya usalama wake…’akasema mkuu

‘Kwa ajili ya usalama wake,…! Mhh, kwahiyo mkuu unakubaliana na hayo wanayozungumza watu mitaani, kuwa huenda kifo chake sio kwamba kajinyonga mwenyewe…, kuna sababu nyingine zaidi…au?’akasema mpelelezi.

‘Siwezi kusema hivyo, mpaka tulithibitishe, unafahamu taratibu na fani ya kazi zilivyo au sio…lifanyie kazi,…’akasema mkuu.

‘Sawa mkuu, ninafahamu…, unajua nilipofika huko kijijini,mazungumzo yote ni kuwa marehemu hajajinyonga,…na hili linanipa mwongozo kuwa kuna jambo, na kauli yako inanifanya nihisi hivyo, kuwa marehemu atakuwa kauwawa, ……’akasema mpelelezi.

‘Kinachotakiwa wewe ni kuifanya kazi yako, na kama kuna cha kuniuliza uniulize haraka…nina dakika chache, nahitajika mkutanoni….’akasema mkuu wake.

‘Labda kwa kunisaidia tu mkuu, je marehemu alipofika hapa alikuwa na jambo gani muhimu, ushahidi nk…maana sijaona kitu kama hicho kwenye kumbukumbu zake, ni maelezo machache tu..…?’ akauliza mpelelezi

‘Umepitia faili zima hakuna chochote ulichogundua…?’ akaulizwa

‘Bado sijaliangalia kwa makini…ndio nilikuwa nimeanza, ….’akasema.

‘Usifanye mzaha na hii kazi, ni kazi inahitajia uharaka, na ni ya hatari…’akaambiwa.

‘Mkuu naelewa sana,…ndio nilikuwa kwenye harakati za kupitia kila kitu, unajua jinsi ninavyofanya kazi yangu, utapata kila mkuu…’akasema

‘Ok, una swali jingine…?’ akaulizwa

‘Nimezipitia kumbukumbu kadhaa…kwa vile una haraka…, unaweza ukanipata maelezo zaidi ambayo huenda hayapo kwenye kumbukumbu zake..nimesoma kuwa siku kabla ya kifo chake alifika hapa akiwa na taarifa za kutaka kusaidia…. kuwapata watu wanajihusisha na malegeza..na kuhusu  mdudu mtu…lakini hakuna kitu ….’akasema mpelelezi na mkuu akamkatisha kwa kusema;

‘Ndio hivyo…alifika tukaongea naye... niliongea naye mimi mwenyewe.., akanieleza anavyofahamu… yeye alikuja kutoa taarifa kuwa aliona tukio ambalo huenda likasaidia...., na akaelezea kuwa siku kadha nyuma, aliwahi kuliona  gari la serikali  lipo maeneo ya mitaani kwao…anasema yeye alijua lipo kwenye doria za kawaida za kikazi.

‘Sasa basi ghafla akawaona vijana wetu, wakitoa mzigo kwenye gari, baada ya kuja gari jingine, ambalo lilifika na kusimama sambamba karibu na gari la serikali, vijana wetu na vijana wengine wawili, waliotoka kwenye gari zao, wakabadilishana mzigo kwa mzigo…’akatulia

‘Mzigo gani…?’ akauliza mpelelezi.

NB: Kidogo kidogo tutafika.


WAZO LA LEO: Tusipende kuhitimisha jambo bila ya ushahidi, wengi wetu tunapenda kusema,..lazima..ni wewe, kafanya nk..na hata kutuhumu moja kwa moja bila ya ushahidi kamili. Hebu jiulize kama sio kweli…hebu fikiria kama ungelikuwa ni wewe ingekuwaje,..kuna vitu vinauma kama kweli hukutenda. Tuiachie sheria, na mamlaka yake ithibitishe kwanza!
Ni mimi: emu-three

Ni mimi: emu-three

No comments :