Ni kisa cha binti
Maringo, hilo sio jina lake halisi, jina lake halisi aliitwa Maua…alikuwa maua kweli,..kwa uzuri na umbile .... na kwa vile alijaliwa kuwa na wazazi wenye uwezo, basi alikuwa akijiona, akajawa na
dharau..kutoka utoto hadi usichanani..
Umri ulivyokwenda , ndivyo alivyozidi kunata, ..... Ikafikia hatua wanaume nao wakamdharau, ila kwa wale wenye nazo
hawakusita kumtaka. Na wengine wakataka kutumia pesa kumkomoa! Siunajua tena wanaume wengine, hawashindwi wakiamua..lakini kwa binti huyu wakagonga mwamba!
Pindi tukasikia kaolewa, na kila mmoja akawa na shauku ya
kufahamu ni nani kamuoa huyo binti Maringo,…mhh, kweli aliolewa na kibopa
mmoja,…ni tajiri wa uhakika,…lakini..mmh, kila mmoja aliposikia kuwa jamaa huyo
ndiye kamuoa huyo binti, aliishia kuguna tu.
Kiboba huyu hakujulikana wapi anapatia pesa zake, ilikuwa ni
siri yake kubwa hata familia yake ilikuwa haifahamu. Pesa kwake ilikuwa kama
makaratsi tu,…anabadili magari kama nguo, nyumba anajenga kama uyoga…
Hata hivyo za mwizi
ni arubain, siku kadhaa tukasikia jamaa, yaani huyo kibopa kakamatwa huko
Uchina, na madawa ya kulevya,…
‘Oooh, kumbe ndio ilikuwa kazi yake….’watu wakaanza kusema.
Siunajua tena Uchina hakukopeshwi, ukikamatwa huko na madawa
ya kulevya, adhabu yake ni kifo…tukasikia jamaa kanyongwa…na binti maringo
akawa mjane.
Siku zimepita binti maringo, kabakia mpweke, kila anayekuja
kutaka kumuoa, yeye hamtaki, kisa hana hadhi, …hana uwezo, ..na kauli za kejeri
kibao…mmh, akaja kuolewa na jamaa mmoja…Jamaa huyo anazo, lakini sasa , tatizo
lake ni ngumi mkononi,…Binti Maringo kavumilia vikamshinda, akamwaga manyanga, na
kurudi kwao, na jamaa akasema;
‘Hata mimi sikutaki…chukua talaka yako…, kwanza mtu mwenye
unanipa shida tu..’wakaachana kwa kashifa kihivyo.
**********
Ni kisa kirefu…mwishoni mwa mwaka 2016 nikakutana na binti
maringo, yupo maeneo ya kariakoo, anatembeza nguo za mikononi,..sikuamini, kwa
hali niliyomkuta nayo, ana makovu usoni, wakati awali uso wake ulikuwa mwororo
wa kuvutia....nikajiuliza kulikoni, kwa vile nilikuwa namfahamu na mara kwa
mara tulizoea kuongea,….nikamuuliza…
Binti huyu , akaishia kulia,…
‘Mhh…natamani nife tu, lkn siwezi, wadogo zangu wataishije,
wananitegemea mimi sasa..ila,hapa nilipo…natamani niende kwa wazazi wangu huko
walipo…’alilia na kuongea maneno ya kusikitisha sana.
Kiukweli nilimsikitikia binti huyu…., lakini ndio maisha,
mola ni mwingi wa rehema, mola humjalia mja wake kwa wakati fulani, na anaweza
akamnyang’anya kila kitu kwa wakati fulani,..yeye anajua ni kwanini,.
‘ Ila nimejifunza jambo moja,..kiburi cha neema za mungu, hatutakiwi
kukiringa , na dharau, ni tabia mbaya sana, mimi nilikuwa na tabia zote hizo,
kisa mali ya baba, mali ya wazazi wangu, sasa hawapo tena duniani….mola wangu
nisamehe….’akasema akilia.
Akilini niliwaza mbali sana, nikikumbukia maisha ya huyu
binti,..ama kweli, aliyekupa wewe leo, ndiye aliyeninyima mimi, na huyo huyo
anaweza kunipa mimi pia….tukipata kamwe tusimsahau mola wetu, kwani dharau,
kiburi, hulipizwa hapa hapa dunia..nasema hili sio kwasababu ya huyu binti ila
mengi tumeyaona, tunayaona…,….
**********
Kumbe binti maringo,
masikini, baba yake alikuja kufariki, ..na utajiri wa wazazi wake, aliouacha
baba yao, ulianza kupukutika kidogo kidogo, wakaja hata kuuza jumba lao la
kifahari, jumba ambalo binti huyu aliliita ‘KASIRI YA MFALME….’
‘Hii ni kasri ya kifalme,…’alikuwa akisema hivyo, maana
kweli ilikuwa kasri, kila kitu ndani,…
Ilifikia mahali, wakaamua waiuze hiyo nyumba, lengo lilikuwa
kumtibia mama yao ambaye alikuwa akiumwa kwa kipindi hicho, kwani zilihitajika
pesa za kwenda kumtibia mama yao nchi za nje…wakabakia na kibanda cha uani, ….
Mama yao alitibiwa kweli, akarejea akiwa na afadhali, lakini
hali yake iliendelea kuzorota na pesa walizokuwa nazo kama akiba walijaribu
kuziwekeza kwa biashara hii ni ile, lakini waliandamwa na mitihani mingi,
wakaja kuibiwa, kutapeliwa, na huku mama anaumwa hapo…, ikawa shida,
kumtibia,..
‘Mama alivumilia, kumbe alikuwa akiteseka kwa maumivu,
hakupenda kutuambia, akawa anajitahidi hivyo hivyo akijua yeye ndiye baba,
ndiye mama….’akatulia.
‘Siku nilipogundua, nikajua..sasa mama atatuacha…nilimuona
anavyoteseka, kwa maumivu, na huenda moyoni aliomba afe tu, ili akapumzike na
mume wake huko alipo, lakini akitufikiria sisi, …lakini hata hivyo ikafika muda
wake,…akatangulia mbele ya haki…akituacha hatuna mbele wala nyuma..nililia sana
siku hiyo,…hadi kupoteza fahamu siku tatu…’akazidi kunisimulia.
***********
Binti maringo alikuwa ndiye mkubwa kwenye familia, akabakia
na wadogo zake, wadogo zake walikuwa wakiwategemea wazazi wao, walisoma shule
za bei mbaya,..lakini hawakufanya vizuri, walikuwa wamelemaa na utajiri wa wazazi wao, sasa wazazi hawapo,
mali hazipo…hawana ndugu wa kuwasaidia, wamebakia mayatima na masikini….
Binti maringo, akaanza kuhangaika,…
‘Nilifikia hatua nikaanza kujiuza,…tusife njaa, wadogo zangu
wapate kula, wanaume wakatumia mwanya huo kunizalilisha, badala ya kunisaidia,
hawajui kuwa na wao ipo siku na wao yatawakuta, hata kama sio wao …inaweza
ikawkuta watoto wao, maana mimi sikuomba kadhia hiyo inikute..ndio mimi
nilikuwa naringia mali ya wazazi wangu, lakini sikujua, aliyekuwa anajua ni
mola peke yake, sikujua kuwa ipo siku na mimi nitakuwa omba omba, nizalilike
hivi…. …..’akakatisha akilia.
‘Nilifikia hatua nikauza bar..unakumbuka nilivyokuwa
nikiwazarau wanaofanya biashara hiyo nilikuwa nikisema bora nikalime …..lakini
nigelifanya nini mie…nilifanya hivyo sio kwa ajili yangu tu, ila kwa ajili
wadogo zangu, nawapenda sana wadogo zangu……’ akasema ….
Kwakweli kila hatua ya kisa hiki…alivyokuwa akinihadithia, ilikuwa
ni aheri ya jana, na alikuwa akinihadithia kisa cha maisha yake huku analia,…ni
kisa cha aina yake, lakini ….simu haiwezi kukiandika chote kwa marefu yake…,
tukijaliwa ipo siku nitakitohoa kwa mapana yake.
WAZO LA KISA HIKI KIFUPI: Katika maisha haya ya hii dunia, tukipata,
tusisahau kuwa kuna leo na kesho. Iwe tumepata kutoka kwa wazazi, tumepata cheo….tusiwadharau
wenza wetu, au kuwdhulumu, kuna mabosi, wanatumia vyeo kuwadhulumu wenza
wao..hii sio sahihi jamani maana hutujui ya kesho yatakuwaje,..
Pia, tusitegemee sana utajiri wa wazazi wetu, waume zetu,
wake zetu, ndugu zetu…tujaribu sana kujitahidi kusimama kwa miguu yetu wenyewe kwa kujaribu
kujifunza, kuwekeza, kusaidiana na wenzetu, au kufuata nyayo njema za wazazi
wetu, waume zetu au wake zetu walivyofanya wakafanikiwa.
Tumuombe mola wetu
atujalie tuweze kuishi kwenye njia sahihi, anazoziridhia yeye, atusaidie , atuongoze
maana mitihani ya dunia ni mingi sana, tunaweza kujiona tupo sahihi, kumbe
tunakengeuka na uwezo wetu wa kujua ghaibu ni mdogo. Aamiyn!
WATUMIE WENGI TUJIFUNZE NA TUKIO HILI.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment