Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, January 28, 2017

TUTAISOMA NAMBA.....


‘Hivi mbona mambo yanazidi kuwa magumu, maisha yanakuwa magumu sijawahi kuona, ina maana kumbe, ufisadi, dili, rushwa…ilikuwa na neema fulani, japokuwa ilikuwa ikitutafuna kama kansa…’ilikuwa kauli ya jamaa kwenye treni.

‘Kwanini unasema hivyo bro..?’ akauliza mwingine na wote tukatega sikio kusikia hoja hiyo.

‘Mimi nilikuwa nimeshanunua kiwanja, na kuanza kujenga, nilijua mwaka tu nitamaliza, na sio mimi tu, wenzengu wengi walishaanza azimio hilo,..lkn tangia kasi hii mpya ya sasa kazi tu, iingie tumekwama kabisa, majengo hayaendelei…., hakuna hata mmoja ameweza kusogea mbele..’akasema

‘Sasa kwanini ina maana mlikuwa mkijenga kwa pesa za dili..au?’ akaulizwa

‘Hamna bwana...ni kubangaiza huku huku tu, upo ofisi, lakini nje una vijimradi vya hapa na pale…lkn sasa utabangaiza wapi, wenye kampuni wenyewe wanafunga virago…, wenye biashara biashara haziendi tena, wanasema kodi zimewaziba pua,..haya hata vidili vidogo vidogo havikamatiki tena, mtu kati yupo wapi hakuna…sasa nitafanya nini…?’ akauliza

‘Oh..kumbe, sasa MTAISOMA NAMBA..’mama mmoja akasema, na kauli hiyo ikaanzisha mjadala mkali, kichwa cha habari, ni kwanini sasa, ambapo watu walitarajia neema, maana mafisadi wananyea ndoo, dili za rushwa, zimejificha chooni, …watu wanalipa kodi bila kupenda,..eeh, sasa kulikoni…ina maana hata watoto wetu wasisome shule za kulipia…haya warudie shule za kata, maziingira yapoje…kazi kweli kweli….

'Mliotegemea dili...maisha ya uchochoro chochoro, mtaukimbia mji sasa, hamkuelewa waliposema tutahamia Dodoma,...sio serikali tu,..ilikuwa na maana ndefu tu, kuwa hata sisi, tunatakiwa kuhamia wapi....makwetu...hahaha mtaisoma namba....'akaongeza mwingine

'Unajua ni kweli, kwenye dili, ..tulikuwa tunasaidiana, ukipata na ndugu naye kapata..kutoa mkono unakuwa mwepesi tu...., lkn kwenye dili serikali haipati,...inaumia kwa kubeba mzigo usiobebeka... ndio maana sasa serikali inabana, ili ipate haki yake..umeonaeeh, ...'akasema mzee mmoja

'Nakuunga mkono mzee,...., hivi hamkukaa mkajiuliza hili jambo, siasa ni sehemu nyeti..kuongoza watu sio mchezo, , lkn ilifikia hatua watu wanaacha biashara wanakimbilia huko, wanaacha kazi zao za maana wanakimbilia huko, siasa ikawa dili,...sasa hivi siasa imekuwa KITI MOTO, ...umeonaeeh, kiukweli madaraka sio 'dili' madaraka ni wajibu, ni wito...usipowajibika, utaulizwa, sasa ni zamu ya serikali kuwauliza viongozi, bado zamu yetu inakuja,..watu wataamuka, na kuanza kuhoji, kiongozi wetu anafanya nini, katufanyia nini....'akasema huyo mzee mwingine.

'Na kwanini watu wake tu wasifanye kazi, wale walale , waangalie tv,..wakavute bangi, madawa ya kulevya,..hivi sasa walevi, wabugia unga wanapungua, kidogo kidogo...maana pesa za dili zipo wapi...mtaona wenyewe , mdogo mdogo, tunahamia wapi....?' akauliza mzee

'Dodoma...'vijana fulani wakasema na kucheka


'Sio Dodoma,...kijijini....'mzee akasema na kikawa kicheko


‘Mimi nimeamua kuwafukuza ndugu zangu warudi kijijni, nitawalisha nini tena…, sasa hamuoni kuwa maisha kama haya, ubinadamu haupo tena, ndugu tutanuiana…ina maana tutaishi kila mtu na lake..ndio tunataka hivyo, hata ndugu yako akitoka kijijini kukutembelea asije bila taarifa na akija unampa mgeni siku tatu, ya nne arudi kwao…?’ mmoja akauliza swali kwenye mjadala wetu .

 Maisha sio mchezo, kila jambo awali yake huwa ni gumu sana, wengi tulizoe hivyo, maendeleo mpaka dili, ukifika ofisini, ili ufanikiwe inabidi usuke mpango wa kupata teni parcent, vochaa, vocha..sped up, mara hivi na vile,..usaidie kampuni kwenye zabuni fulani na humo unaweka dili yako…ukifanya biashara ili utoke, unakwepa kodi…nk…ikafikia mahali kila kitu mpaka kuwe na mtu kati, ..yaani madalali , hawa jamaa wakatajirika kweli, mdomo tu..,….hayo ndio yalikuwa maisha yetu, sasa yanabadilika, ….ugumu wa maisha mengine, umeanza..

Mtindo huu wa maisha ya sasa inabidi utafute upate na lazima ulipe kodi, kodi ni malipo kwa serikali kwa huduma inayokufanyia, kwa maana hiyo basi Mwenye nacho, atafanikiwa na hata kuongezewa, kama atawekeza kihalali na kujibidisha kwenye njia sahihi, ....anapata analipa kodi anabakiwa na faida...na asiyekuwa nacho,..ITAKUWAJE,... hata hicho kidogo alicho nacho atanyang’anywa, kwani wanasema; asiyefanya kazi na asile….na ukumbuke, utalipa kodi upende usipende…


Tumuombe mungu wetu, tuliombee taifa letu, tuwaombee viongozi wetu, tujiombee wenyewe, maana kiukweli sio kazi rahisi, sio jambo la mazaha kama watu wanavyofikiria, kujibadili kunahitajia ‘jasho’ , juhudi ya kweli na maarifa ya uoni wa mbele,..kama wengine kipindi hicho maisha bado yalikuwa magumu, je kipindi hiki itakuwaje,… ni kumuomba mungu tu, ili tuweze kulivusha jahazi hili kwa amani na salama, maana mafanikio ya taifa ni maendeleo yetu na vizazi vyetu.

Ni mimi: emu-three

No comments :