Ni siku ya naikumbuka sana, ni siku ambayo niliteguka
nyonga, si unajua tena hii shida yetu ya usafiri, na ilitokea usiku wakati
narudi kazini. Usiku sikulala, nilitamani kupambazuke haraka niwahi hospitali.
Lakini tatizo la ofisi yetu ili utibiwe ni mpaka upate sick sheet, na ni lazima
ufike kwanza ofisini uandike kuwa umefika, usipofanya hivyo siku hiyo inakatwa,
na unakatwa kwenye mshahara.
Basi kulipopambuka tu, saa kumi nikadamka, hata kutembea
shida, nanyata kama kinyonga, taratibu nikawahi kituo cha reli, maana nilijua
nikipanda dala dala nitaumia zaidi, japokuwa mbeleni nitahitajika kupanda hiyo
daladala, uwezo wa taxi au bajaji upo wapi!
Uzuri wa treni hainaga foleni nikafika Buguruni saa kumi na
mbili, kuna mwendo wa kutembea kutoka Tazara hadi buguruni sokoni ,
nilijikongoja hivyo hivyo, hadi nikafika kituoni,..Nilipofika hapo kituoni, niligwaya
kwani umati wa watu waliokuwepo hapo…, utafikiri magari yamegoma. Nami natakiwa
kwenda ofisi moja ipo kwenye jengo moja lipo njia panda ya kwenda Kawe.
Magari ya Kawe buguruni au Kawe masaki ni kama enzi zile za
magari ya kwenda mbagala, ni magari ya kugombea, watu wanarukia kwenye
madirisha, ukizubaa huwezi kupanda. Na mimi siwezi hata kusimama kwa muda
mrefu.
‘Jamaa yangu nakuomba unisaidie naumwa,…ugombee upate siti
ili unipatie nikae…?’ nikamwambia jamaa mmoja aliyekuwa akielekea njia hiyo.
‘Mimi mwenyewe sijui kama nitapata gari, hapa nilipo
najisikia vibaya…’jamaa akaniambia hivyo.
Kukuru kakara ikaja gari, ikasimama pale pale nilipokuwa
nimekaa, haraka nikajitahidi nikadondokea mlangoni, watu hawakujali,
wakaniparamia na kuanza kunikanyaga, hakuna aliyejali, hata nilipoweza
kusimama, nilikuwa nimechafuliwa nguo. Sikujali, nikasimama na kuingia ndani ya
gari.
Uzuri kondakita alikuwa kakaa kwenye kiti karibu na mlangoni,
akanipisha nami nikaweza kukaka kwenye kiti! Hapo nilikuwa na maumivu makali
sana, ..nijiuma meno….gari likaanza kuondoka, kwa mbele ulikuwa ni mnyororo,
foleni, gari halitembei. Mpaka tunafika Karume njia panda, dakika arubaini na
tano zimepita,..hapo natamani hata kulia,ni maumivu makali sana!
Nikamuomba mungu, angalau nipate usingizi, na duwa zangu
zikakubaliwa, nilipitiwa na kausingizi na nilipoamuka nikakuta tupo njia panda
ya magomeni, kumbe tulitumia saa moja kwenye hiyo foleni, ..hadi tunafika
Moroco, ni masaa mawili na nusu yamepita. Sasa kutoka hapo Moroco kuelekea huko
Kawe, hapo ilikuwa kazi, mpaka abiria wanadondoka na kuzimia, trafiki hana
habari na upande wetu.
Tukaondoka hapo saa jingine limepita,..tukafika sehemu
wanaita kwa Warioba, hapo kuna historia, bila nusu saa au saa nzima hamuwezi
kuruhusiwa kupita,..hapo abiria wengine waliamua kushuka na kutembea kwa miguu,
na wale wenye uwezo wakachukua pikipiki. Sijui kuna nini sehemu hiyo!
Nilifika ofisini saa tatu na nusu, na daftari la mahudhuria
limeshachukuliwa, sikujali, mimi umuhimu ni sick sheet tu..Bosi aliposikia
ninaumwa, akanijia na kuanza kunibwatukia;
‘Wewe kila siku inaumwa,..veye hutaki kazi,..sasa nenda
tibiwa na baki huko huko mpaka ponaeeh, ..’akasema bosi huyo.
‘Sawa bosi lakini sikuomba iwe hivi…’nikalamika.
‘Itajua mwenyewe….’akasema kwa dharau. Na kauli yake ni
moja,..ningefanya nini,..nikaondoka hapo ofisini nikiwa na mawazo mengi,
nitaishije. Basi nikajikongoja hadi kwenye kituo cha dala dala..nilichokikumbuka
ni kuwa nilikuwa nasimama, kwani nilikaa kwenye gogo lilikuwa limewekwa hapo
kituoni.
Wakati nasimama, nikahisi maumivu makali sana,…lakini
nikajitahidi hivyo hivyo….nikainua mguu , hautaki, nikajitahidi, nikaweza,
nikavuta hadi mlango mwa gari, unajua tena magari ya dala dala hayana
kuremba,..sijainua mguu likaanza kuondoka, nilihisi nikirushwa na kudondoka
chini, na kichwa kilikoswa koswa na gurudumu, na giza likatanda usoni.
Nilizindukana na kujikuta nipo hospitalini na bandeji kichwani…
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment