‘Ngoja nikusimulie
ilivyokuwa, maana ilikuwa harusi ya aina yake haijawahi kutokea…’akasema
msimuliaji.
‘Mhh..tuambie maana
watu tuna hamasa sana ya kusikia, ilikuwaje, na ulikuja kumuoa nani, mpka mkapata watoto, na huyo binti aliolewa na nani,….’nikasema
**********
Siku ya ndoa..., hapana usiku wake, ndio mambo yalianza kujitokeza. maana hayo nilikuja
kuambiwa .
Wanasema huyo bwana harusi, alionekana kwenye nyumba moja ya starehe akiwa na
kimwana, usiku huo ambapo kesho ndio anatakiwa kuoa...na huyo kimwana aliyekuwa naye, kumbe alikuwa mshikaji wake wa siku nyingi,…
Wanavyosema, eti huyo bwana
harusi alikuwa hajatulia, unajua tena watoto wa wakubwa wengine
walivyo..wanajua kutumia tu mali za wazazi wao,...hawana uchungu nazo, wanaringa, wanajidai kwa jasho la wazazi wao. Pesa ni mtihani, huyo kijana akawa,
huku anataka kule anataka, kwahiyo alikuwa na matatizo mengi, ni kama mimi enzi
zangu,..hahaha’ msimuliaji akasema na kucheka.
‘Kwahiyo ilikuwaje..ulikwenda kuweka pingamizi, na kuwaelezea kuhusu huyo kijana au...?’ nikauliza
‘Haikuwa hivyo
ndugu,..sikuwa na lengo hilo abadani,....'akasema
'Kwahiyo harusi ilifungwa, wewe ukashuhudia tu, au sio...?' nikauliza
‘Subiri kwanza
nikuelezee kuhusu huyo bwana harusi, hiyo kukutana huko na huyo mwanamke wake
wa siku nyingi ilikuwa namna ya kutafuta mbinu ya kuzimisha moto uliokuwa
umeshaanza kuwaka…kulikuwa kuna tatizo kubwa, na hilo tatizo lilitokea baada ya
huyo bwana harusi mtarajiwa alipotangaza ndoa.
Kumbe huyo mwanamke
mwingine alishapata ujauzito,lakini awali hakuwahi kumwambia bwana harusi, ndio
akaja kumwambia usiku huo wa ndoa, na huyo binti baba yake ni kigogo fulani, alijua asipomshinikiza huyo jamaa akaenda kwako kusema ukweli kuwa hiyo ni mimba yake, atakuja kupata shida!'
‘Nimeshasema huwezi
kumuoa huyo Malaya wako…’akaambiwa.
‘Lakini
nimeshatangaza ndoa…na huyo sio malaya kama wewe....’akalalamika muoaji
‘Mimi leo ni malaya sio...na kwani hukujua kuwa
mimi ndiye mwanamke wako… kwanini ukanisaliti, na wakati nina mimba yako…’akaambiwa.
‘Mimba…hapana, sio
kweli, huna mimba yangu wewe..usitake kuniharibia ndoa yangu…’akasema mtarajiwa.
‘Kama unabisha
twende tukapime,…nilikuwa natafuta muda wa kukuambia na mara ndio nikasikia
unataka kuoa,…sasa sikiliza, hiyo ndoa haipo tena, na kama utaifunga hiyo ndoa,
…utakachokipata utakuja kuniambia…nitaweka mauchafu yako yote hadharani,…’akaambiwa.
‘Usinitishe wewe…mapenzi
yetu yalikuwa ni ya starehe tu, sikuwa na mpango wa kukuoa wewe…’akasema bwana
harusi, kukatokea kujibishana maneno mpaka akotokea msuluhishaji.
Kilichoendelea baadaye hapo hakikujulikana,
maana kesho yake bwana harusi, akawa anasita kwenda kwenye harusi, lakini baba
wa huyo bwana harusi akatoa amri huyo kijana aende kufunga ndoa,…amri ya baba
ni baba, muoaji akajiandaa akaelekea kwenye harusi
************
Kama ilivyo ada, waowaji wakafika sehemu ya harusi,
wakiwa wameshajiandaa kwa kila kitu, wakiwa wameshaingia ndani sehemu ya
kufungia ndoa, sasa wamekaa wanaubiria amri , na taratibu za ndoa, mara bwana
harusi akadondoka…’
‘Vipi jamani….’watu
wanauliza, na wapambe wakawa wanamchunguza bwana harusi, wakasema bwana harusi
kupoteza fahamu, wakamuhudumia wakijua labda ni mfadhaiko tu wa ndoa..ilichukua
muda, mpaka akaitwa dakitari.
Baadaye bwana
harusi akazindukana….’akatulia
‘Alipoamuka
anauliza nipo wapi…akaambiwa, ‘upo kwenye harusi,..’
‘Ya nani…?’
akauliza na watu wakashangaa,
‘Ya kwako,…’
‘Ya kwangu, mimi
nilishawaambia simtaki kumuoa huyo binti..simtaki,s imtaki,..’akasema kwa
hasira .
‘Lakini … kwanini…?’
akaulizwa.
‘Kwanini,…
hayawahusu, kwani muoaji ni nani, si mimi, kama mnataka nyie fungeni ndoa,
lakini sio mimi,..nilishamuambia hata huyo binti harusi kuwa simtaki, wazazi tu
wananishinikiza, simtaki, nimeshaamua sasa… ‘akasema na sasa akitaka kuondoka.
Wanandugu
wakajaribu kumsihi, wakamwambia ni bora hiyo harusi iahirishwe ije kufungwa
siku nyingine kama anajisikia vibaya…, lakini bwana harusi akasema hataki na
hamtaki tena huyo binti harusi, na aliposema hivyo ….akaondoka, na ndoa ndio
ikavunjika hivyo…, sasa…hebu fikiria, wazazi, na huyo bibi harusi,
walivyojisikia.
Japokuwa binti
harusi alikuwa hakutaka hiyo ndoa awali…, lakini ilishafika hatua ikabidi
akubali tu, na kuna zile imani kuwa ndoa yako ikivunjika siku ya harusi ni
nuksi, hatakuja kuolewa tena.
Kwahiyo ilivyotokea
ivyo…binti, na wazazi wakajua ndio basi tena binti yao keshaharibikiwa,
kilichofuata baadaye, baada ya kutangazwa kuwa kuna tatizo bwana harusi
kaondoka, na ndoa haipo tena, wakina mama wakaanza kulia….ikawa sasa ni taharuki,
mama analia kwanini wamemfanyia hivyo binti yake, wanafamilia wakawa
wamechanganyikiwa, sasa kila mmoja anasema lake!…
***********
Wakati
hayo yanaendelea huko mimi sijui, nilikuwa kwenye mgahawa uliokuwa karibu,
kwani nilishakata tamaa,…nilisubiria nione magari yakitoka ya bwana na bibi
harusi,..nikaona kimia, baadae vilio…
‘Kilio cha nini…?’
nikajiuliza , ndio nikatoka pale mgahawani, na kuelekea kwenye hiyo nyumba, wazo la kwanza labda kumetokea ajali,….
Nilipofika hapo,
nikawauliza watu kumetokea nini, hakuna anayeongea , watu wameshika kichwa,
wengine wakisema;
‘Nuksi hiyo….haolewei
tena huyo….’
‘Kwanini….’hakuna
aliyenijibu, hapo sasa nikaona nisubirie nione mwisho wake itakuwaje.Kwa ujumla
mimi nilikuwa nasubiria tu kupoteza muda.., sikuwa na tumaini tena na huyo
binti, maana hata kama hiyo ndoa imevunjika kuna sababu, na sababu hizo
zinaweza kusawazishwa au sio.
‘Hiyo ndoa haipo
tena, nilijua, tu…yule kijana hajatulia…’nikasikia mtu mmoja akisema.
**********
Muda ukapita, baadaye
kitu kikanivuta, kwanini nisiingie huko ndani tu, ili nijue moja, halafu
niondoke zangu..ilikuwa wazo tu, na bila
hata kufikiria, nikatembea hadi mlangoni,…mlango ulikuwa wazi, nikaingia ndani, muda huo hakuna anayeshughulika na mtu,
kila mtu kainamisha kichwa chini,..ni aibu, fadhaa, kuchanganyikiwa,..
Mimi nikaingia hadi
ndani na kuwakuta wazee wamekaa,..ilikuwa ni wazee wa hiyo familia, wamekaa
lakini wote wamainama kama wanaombeleza…nikabakia nimeduwaa pale ndani, sikujua
sasa hata nifanye nini.
Nikaona kwanini
nisiende kumliwaza huyo baba, baba wa huyo binti ananifahamu, ila sikuzoeana
sana na yeye, nikasogea hadi pale alipokuwa amekaa…
‘Mzee poleni
sana..mimi naombeni msikate tamaa, hii ni mitihani tu itakwisha tu…na binti
yenu ataolewa, …’yule mzee, aliinua kichwa akiwa kakunja uso kwa hasira,
nikajua sasa naweza kupigwa ngumi.
‘Wewe ni nani….?’
Akaniuliza, na kabla sijamjibu akaiona sura yangu, kwa haraka akasimama na kunishika mkono na kunivuta sehemu
nyingine ya chumba , sikujua anataka kunifanya nini…ni kama vile alitaka kunipiga
au ..hata sielewi…tulipofike sehemu nyingine ya chumba, akaniangalia kwa hasira
huku akisema;
‘Haya niambie
umefuata nini wewe mtu..ndio umekuja kutusanifu au sio..?’ akaniuliza kwa
hasira.
‘Mzee sina nia
mbaya, nimesikia haya yaliyotokea, najua hali mliyo nayo..na najua nyie
hamunitaki nimuoe binti yenu,….mimi nimekubaliana na hali halisi, …lakini hili
limtokea mimi kama binadamu lazima nije kuwapa pole..’nikasema.
‘Kutupa pole, ili
iweje….sitaki tena kuwasikia hao watu, na kama akijitokeza mtu wao, sijui..
nitakwenda kufungwa tu kwa hicho nitakachowafanyia, siwezi kuabishwa kiasi
hiki….wewe subira nitakavyowafanya, haya ondoka hapa, sitaki kukuona mbele
yangu…’ Akanisema kwa hasira.
‘Mzee, labda nisema
neno moja tu, nawaombeni kama itashindikana kwa huyo mchumba wake,wala msiwe na
wasi wasi,,eti mkosi au nuksi,…, mimi bado nina dhamira ya kumuoa binti yenu, kama
ikishindikana kwa huyo basi niozesheni mimi…’nikasema
‘Eti nini, ndio
ulikuwa unaombea hilo litokee, una wazimu nini wewe..nimekuambia uondoke , na
nyie ndio mumeitia mkosi ndoa hii..sitaki hata kukuona, toka humu ndani kwangu….’akasema
kwa hasira, kumbe wazee wengine wamesikia , na mara akaja mzee mwingine huyu
ndiye mjomba mtu, na wakati anaingia ndio mimi najitetea.
‘Sio hivyo mzee,
yote ni mapenzi ya mungu….’nikajitetea
‘Jamani kuna tatizo
gani tena huku….’akauliza mjomba mtu.
‘Huyo …mtu sijui
kaja kufata nini hapa, hebu sikia eti kaja ili tumfikirie, kwa vile hii harusi
imevunjika, basi yeye atamuoa binti yetu, ….utafikiri mchawi,…’akasema baba wa
binti.
‘Oh… kwahiyo, yeye
anasema hivyo, kuwa , ..yupo tayari, kumuoa..baada ya haya yote, mimi naona
tumetatua tatizo mzee mwenzangu, haya
mambo yana imani zake ikifikia jioni ya leo tusipofanya jambo, binti yako
atakuozea humu ndani,..hataolewa tena, sasa muda wakulitatua tatizo hili ni
sasa…kabla muda haujaisha…’akasema mjomba mtu.
‘Kwahiyo unasemaje…?’
akauliza baba wa binti.
‘Njoo huku tuongee….’akachukuliwa
huyo baba wa binti na huyo mzee ambaye ni mjomba wa binti, wakaenda huko
walipokwenda, kuongea, baadae baba mtu akarudi, na kunikuta mimi bado nimesimama
hapo hapo, naogopa hata kuinua mguu!
‘Ulisema nini, …kuwa
upo tayari kumuoa binti yangu, …si ndio hivyo…, basi sawa, nitafanyaje sasa,,..sina
cha kufanya, sawa..si wewe unamtaka binti yangu haya, utamuoa leo hii,..sitaki hata mahari yako,
ninachotaka huu mkosi uondoke… unasikia utamuoa leo hii…. umenisikia leo hii,
sawa..?’ akaniuliza
‘Leo hii, lakini
mbona sijajiandaa…!’ nikasema
‘Hakuna cha lakini
tena hapa,… tusipoteze muda, …’akasema na kuondoka, akiniacha nimeduwaa
Baadaye akaja mtu mwingine
kuniita, nikapelekwa chumba kingine nikakuta nguo za kuvaaa, …nikaambiwa nizivae…
ni maalumu kwa ajili ya harusi,…nikawa sina la kufanya, nikafanya
nilivyoambiwa, … ..na huko nje ninasikia tangazo:.
*************
‘Nawaombeni watu
msiondoke, harusi ipo kama kawaida..’tangazo likarudiwa mara nyingi tu na
msemaji mkuu,…Na haikupita muda,watu wakarudi, sasa wakiwa wengi zaidi na hata
wale wasiokuwepo awali, kila mmoja na mihemuko yake,
Wengine walitaka kujua
ni nini kinaendelea, kwanini huyo bwana harusi kaamua kurudi tena, hakuna
aliyejua kuwa muoaji sio yule wa awali…
Hutaamini,
tukafungishwa ndoa, bwana kapata bibi,
bibi kapata bwana…harusi ikafana tena sana,..lakini nilkuja kutoa
mahari..usije kusema nilioa bila mahari,…hahaha..’akasema kwa furaha.
‘Oh
hongera…’nikajikuta nikisema mimi msimuliwaji na kusimama kumpa mkono
msimuliaji.
‘Hicho ndicho kisa changu
cha ukweli… toba ya kweli….nimemaliza…’
MWISHO
WAZO LA LEO: Lililopangwa na mungu litokee, litatokea tu, ..muhimu ni
kufanya subira, huku tukimtegemea mola. Tusifanye subira huku tukikufuru..tukalalamika,
tukalaani, hata kujenga chuki na hisa mbaya kwa watu wengine. Hiyo sio sahihi,
hujui ni kwanini mola wako analisubirisha hilo jambo, yeye anatujua zaidi ya
tunavyojijua weneywe, tusubirie, na.., muda muafaka utafika, na kwa kudra zake
maanani utapata ufumbuzi wa tatizo lako.
NB: Nawashukuruni
sana wote mliokuwa mkikifutilia kisa hiki, najua kuna wenye kusema hili na
lile, lakini nia na lengo langu ni kutoa visa vyenye mafundisho. NATOA visa
ambavyo hata watoto wangu wanaweza kuvisoma, iwe ni kwa manufaa ya jamii ya leo
na kesho. Ahsanteni sana.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment