Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, December 14, 2016

TOBA YA KWELI-21(Hitimisho -2)


Docta akiwa amepumzika mara simu yake ikaita, alipoangalia akaona ni simu ngeni kwenye simu yake…, akaipokea, akilini akijua ni mmoja wa wagonjwa wanaotaka kuwasiliana naye,…, au ni mtu anayehitajia huduma yake,..mara sauti ikatanda sikioni na hali kama kwikwi ya kilio.

‘Wewe ni nani, na unalia nini…?’ akauliza docta

Mpiga simu akajieleza, yeye ni binti aliyekuwa akiishi na jirani yake..aliposema hivyo ndio docta akamtambua, akashangaa ni kwanini huyo binti kaamua kumpigia simu tena anaonekana kama analia, akamuuliza kuna nini,ikabidi  huyo binti amsimulie ni nini kinachoendelea huko kijijini, na alipomaliza docta akamuuliza;

‘Kama wazee wako wamefikia hatua hiyo.. wewe unataka mimi nifanye nini,?’ docta akauliza.

‘Mimi ninachoomba kwako ni kitu kimoja tu…ninataka wewe uwapigie simu wazee wangu ili wapate ushahidi kuwa kweli marehemu ndiye alitaka mimi niolewe na huyo jirani yako, nataka nisije kuonekana kuwa mimi sikujitahidi, sina jinsi, siwezi kuwapinga wazazi wangu, lakini pia siwezi kupinga kauli ya marehemu, nilimpenda sana, na nilishakuwa tayari kuolewa na huyo aliyekuwa mume wake, lakini sasa....…’akasema binti na kukatiza kwa kwikwi , kama anataka kulia.

‘Je wewe ulikuwa tayari kuolewa na huyu jirani yangu, ni kweli kuwa unampenda, au ulitaka kuolewa naye tu, kwa vile marehemu alitaka iwe hivyo…?’ akaulizwa docta

‘Docta, mimi nimeishi na huyo mtu humo ndani, nimemzoea sana, kuna kitu anacho…kimenifanya nimpende, na najua nikiishi naye tutaishi kwa amani…huyo mtu ana utu, ana ubinadamu, ana hali ya kujali, siwezi kukuambia mpaka uishi naye..…japokuwa alikuwa na madhaifu yake ndio..lakini kwasasa kabadilika kabisa, hayo madhaifu yake hayapo tena, ..ni mtu mpya, mpendevu…’akasema binti.

‘Lakini mwanzoni alikuwa akikuchukia au sio, mpaka ukanilalamikia,..unakumbuka…?’ akauliza docta.

‘Ndio…awali alionyesha wazi kunichukia, ni kwa vile alikuwa na kumbukumbu ya mkewe..hata hivyo, kuna muda nilikuwa namfuma akiniangalia sana, kuashiria kitu fulani moyoni mwake..kuna wakati ananifananisha na mkewe….’akatulia kidogo.

‘Ni kweli alikuwa mtata awali, hata mimi  ilifikia wakati nikamchukia kwa matendo yake ya kunitukana..kunikashifu….., kwa jinsi alivyokuwa akinitendea..ilihitajia subira kwakweli…, lakini siku aliponitamkia kuwa anataka kunioa, kweli ananipenda, na nikakumbuka mkewe, alivyokuwa mpendwa wangu… nikawa tayari nimeshampenda, na hakuna cha kumlia mkewe zaidi ya kuolewa na ..na…’akasema kusita kumalizia.

‘Mhh, hebu niambie ukweli, ulikuwa unampenda huyu jamaa tokea lini, yaionyesha labda ulikuwa ukimpenda tangia awali, au sio…?’ docta akauliza

‘Hapana, hapana, docta…yaani nikuambie ukweli, kumpenda, imeanza siku za karibuni tu..sikuwa na wazo hilo kabla..mimi nilimpenda marehemu tu,kama dada yangu sio yeye,…., mimi siwezi kumpenda mume wa mtu..kamwe, sina tabia hiyo mbaya…, hata hivyo aah, tuyaache,….mimi ninachokuomba kwa sasa ni wewe uongee na wazazi wangu….’akasema

‘Lakini si umesikia kuwa huyo mtu ana matatizo, ….’akaambiwa

‘Matatizo gani…?’ akauliza huyo binti kwa mashaka

‘Ya kiafya….’akasema docta

‘Lakini mbona mwenyewe kasema ameshapona,..hana tena hayo matatizo…nina uhakika ameshapona, mungu keshamponyesha…’akasema huyo binti.

‘Mhh…sawa kama kweli umempenda, mimi sina kizuizi, nitajitahidi kuongea na wazazi wako, lakini kama wataendelea na dhamira yao hiyo…, basi …nikushauri kitu, ni kweli huyu jirani ni rafiki yangu, lakini nakuomba usiende kinyume sana na matakwa ya wazazi wako…lakini jitahidi kuwaelezea msimamo wako…hadi mwisho’akasema docta.

‘Kwahiyo, unataka kusema nini hapo docta….?’binti akauliza, na mara ikasikika sauti kama sauti ya kukemea, na simu ikakatika, yaonyesha huyo binti alikuwa akiongea kwa uficho na sasa keshafumwa akiongea na simu.

********
Docta hakuona shida, akawapigia simu hao wazazi wa huyo binti, na kuanza kuwaambia ukweli kuhusu huo usia wa marehemu...

‘Kwanza ni nani kakuambia utupigie simu, haya yanakuhusu nini wewe…?’ akaulizwa

‘Mimi nilitaka kuliweka hilo wazi kuwa ni kweli, marehemu alisema hivyo, isije kuonekana kuwa huyo binti kajitungia, lakini pia ni vyema na nyie mkalijua hilo, ili baadae msije mkasema , kwanini hatukusema hivyo….samahanini wazee wangu…’akasema docta

‘Lakini sasa atawezaje kumuo binti yetu wakati huyo mtu anafahamika kuwa sio kamilifu, mnataka binti yetu aende akawe majaribio au sio…au ndio ndoa za siku hizi, za kuangaliana tu, kama picha, ina maana wao hawataki watoto, au ndio mwanzo wa kubambikiwa watoto wasio halali, au unataka kumpandikiza mtoto wetu mbegu kama ng’ombe…?’ akaulizwa docta.

 Na kabla docta hajajibu baba akaingilia kati, maana sauti iliwekwa hewani kila mtu asikie anachoongea mjomba,…

‘Hebu tuambie wewe ni docta sio, je huyo mtu anaweza kuzaa…?’ baba akauliza

‘Kwani ni nani alisema kuwa huyo mtu hawezi kuzaa…?’akauliza docta

‘Tunakuuliza wewe sasa, utuambie…’akasema mzee

‘Mimi hilo kuwa hawezi kuzaa silijui…..’akasema docta

‘Docta,au ndio umeungana kutuangamizia binti yetu ujue wewe ndiye utabeba lawama zote…’akasema baba lakini mjomba akadakia na kusema

‘Hata hivyo sisi hatuwezi kukubaliana na hiyo kauli ya marehemu, ni kauli yake, lakini hakuwa na amri ya binti yetu, kwa mfano umeulizwa una uhakika kuwa kweli huyo jamaa kapona hana matatizo tena, umeshindwa kutupatia majibu ya uhakika, huna uhakika,..kama docta, inaashiria akuwa unaficha jambo..’akasema

‘Aaah, nisikilizeni…’akasema docta, lakini akakatishwa

‘Sisi sio watoto wadogo, kauli yako tu inaonyesha una mashaka,..na tukuambie ukweli, sisi tumeshapokea mahari,na kila kitu kimeshapangwa,…kwahiyo hayo na mengine kwetu kwasasa hayana nafasi tena…’akasema baba

 Docta alijaribu kunitetea, lakini haikusaidia kitu, ikabidi docta asalimu amri

Docta  alipomaliza kuongea na hao wazee, ikabidi atoke hapo nyumbani kwake,  kwenda kwa jirani yake,akijua huenda hajaondoka, alitaka kumwambia ukweli, na ilibidi amshauri aachane tu na huyo binti, lakini alipofika nyumbani kwa huyo jamaa akakuta mlango umefungwa, na alipouliza majirani wengine, akaambiwa jamaa kasafiri kwenda kijijini.

‘Mhhh, huyu rafiki yangu kafanya nini…’akasema lakini akawa hana jinsi ikabidi asubiria asikie kitakachoendelea huko Kijijini

**********

‘Kwahiyo wewe uliamua kwenda kijijini,.. ili iweje sasa, ili ukaizuie hiyo ndoa, au ….hebu tuelezee hapo vizuri…?’ nikamuuliza msimuliaji.

 ‘Ni kweli, wakati hayo yakiendelea, na mimi nilikuwa nafuatilia kwa namna yangu, ndio nikasikia kuwa huyo binti yupo karibu kuolewa,….

‘Ina maana binti ilifika sehemu akasalimu amri, akakubali kuolewa na huyo mchumba waliotaka wazazi wake…?’ nikamuuliza

‘Ndio…., unacheza na wazazi wewe,…binti wa watu alijitahidi mwishowe akasalimu amri,  na tarehe ikapangwa, na watu wakawa kwenye maandalizi ya ndoa…niliumwa  kwa muda mfupi, nikawa kama mtu aliyechanganyikiwa….…’akasema

‘Mhh kwahiyo sasa ikawaje…..’nikamuuliza na mimi nikivunjika nguvu, sikutarajia itakuwa hivyo.

‘Mhh, ninachoshukuru …sasa hivi nina mke na watoto,..mimba ya kwanza tu ilianza na mapacha....,hiyo ilikuwa ni mimba ya kwanza;  mapacha…watu hawakuamini..lakini utasema nini , kwani watoto waliozaliwa tunafanana kuanzia kichwa hadi vidole, sura na kila kitu…’akasema akitabasamu
‘Sasa…sijui labda tabia..na nisingelipenda waje kurithi tabia yangu ya awali….na na.., mimba ya pili ya kawaida tu….’akasema akizidi kutabasamu

‘Rafiki, …mimi nimeamini mungu ana maajabu yake maana wengine walishaanza kusema mke wangu kapandikizwa mbegu, hamna kitu kama hicho …weeeh, mnacheza na mungu,…hiyo ni siri ya toba,….lakini toba ya ukweli…’akawa anatikisa kichwa.

‘Sasa hebu tufafanulie hapo, ina maana wewe ulikuja kuoa mke mwingine tofauti na yule,..sio huyo binti tena, au ilikuwaje…maana kwa taarifa ya docta, wazee walishapitisha kuwa hataolewa na wewe, na ….hata wewe umesema hivyo, sasa ilikuwaje…?’ nikamuuliza

‘Sitaweza kumsahau marehemu mke wangu,  na kila nimuonapo mke wangu huyu mpya, naiona taswira ya mke wangu waziwazi…, kiukweli wawili hawa kumbe kweli wanafanana sana..’akasema msimuliaji.

‘Kwahiyo ina maana gani, huyo mke mpya uliyempata ni ndugu na na….’nikasema na yeye akatikisa kichwa kama kukataa na kusema;

‘Hapana sio ndugu….Unajua namuomba mungu sana,….namuomba mola wangu aiweke roho ya marehemu mke wangu  mahali pema peponi,…’akasema akiinua mikono juu.

‘Mhh, hapo mimi sijakuelewa…kwahiyo, unatubia kwake kuwa alichotaka yeye hakikuweza kufanyika au sio..?’nikamuuliza.

‘Unajua kilichotokea siku hiyo,…kama nilivyokuambia, mimi sikuweza kuvumilia, niliamua kwenda huko huko kijijini, nia ni kutata kuthibitisha mwenyewe huyo binti akifunga ndoa,…na kweli  hata siku hiyo ya ndoa nilikuwepo hapo kwenye eneo la harusi, huku moyoni ninalia…’akasema,

‘Mhh….sasa wewe ulishajua kuwa umeshindwa, kwanini sasa uliamua kwenda kujitesa hivyo..?’ nikamuuliza

‘Sikuamini kuwa maneno ya mke wangu yanaweza yasifanikiwe, sikuamini kuwa binti ambaye baadaye nilikuja kumpenda, ataolewa na mtu mwingine…sikuamini kuwa kauli ya wakuu wa imani yanaweza kwenda kinyume, sikuamini kuwa mungu anaweza kunikosesha, baada ya juhudi zote hizo..ndio maana nilitaka kuthibitisha kwa macho yangu mwenyewe…’akasema

‘Sasa ilikuwaje..?’nikamuuliza

‘Ngoja nikusimulie ilivyokuwa siku hiyo ya ndoa, maana  ilikuwa ndoa na harusi ya aina yake haijawahi kutokea…’akasema akijiweka sawa kusimulia.

NB: Nimeona niweke sehemu hiyo ndogo ya hitimisho, mtandao unasumbua sana,nitakuja kuweka sehemu iliyobakia, mungu akipenda…. mniwie radhi.


WAZO LA LEO: Mpende akupendaye, na asiyekupenda achana naye, maana huyo asiyekupenda ana wake anayempenda, ukilazimisha mapenzi, maisha yenu yatakuwa ya mashaka, kwanini uhangaike na huyo wakati wengine wapo, kwanini uumie na mtu mmoja, wakati wapo wengi wazuri tu.
Ni mimi: emu-three

No comments :