Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, December 6, 2016

TOBA YA KWELI-20(hitimisho-1)




 Kitendo cha docta kusita kunipa majibu yenye uhakika kilinifanya nihisi kuwa huenda kagundua kuwa mimi mimi bado nina matatizo, lakini imani niliyokuwa nayo ilinifanya niamini kuwa mimi nimepona…niliamini toba yangu, niliamini maneno ya yule kiongozi wa imani

‘Ehee sasa ikawaje…?’ nikamuuliza

‘Sasa ikawaje..subiria uone majibu yake sasa…’akatulia akiwa anaangalia mbele…

 ‘Unajua kabla sijahitimisha kisa hiki, nikuambie ukweli, mimi nimekuwa ni shuhuda kwa vitendo,..unajua mimi nilishajulikana kuwa siwezi kuzaa …tasa,…tasa,  na hata kamaa ningeweza kuzaa kwa vipi, maana nilishaandamwa  na maradhi mabaya yanayovunja nguvu za kiume, nilipatwa na gonjwa la kisukari, ugonjwa wa moyo…vidonda vya tumbo…ooh,


Sasa mtu kama miye ambaye nilishajulikana hata hospitali kuwa siwezi kazi, ..unajua kisukari kinavyotesa..hutakiwi ule vyakula vizuri vizuri..haya presha,..haya hata nguvu za kiumwa huisha kabisa…hebu katika hali kama hiyo ni nani atakubali umuoe binti yake,…hebu fikiria hapo hata ingelikuwa ni wewe, na hata huyo binti anakupenda vipi kweli atakubali umuoe tu, kwa lipi nililokuwa nalo tena…ili aje tu kuniangalia, sina mali, sina…nilishakwisha….’akatulia

‘Kwahiyo…?’ nikauliza

‘Ndio nakuuliza wewe….ili uone nguvu ya toba ilivyo…..’akasema

‘Sasa nikurejeshe nyuma kidogo,….’akaangalia saa yake halafu akaendelea kusimulia;

‘Ukumbuke docta alishachukua vipimo vyangu,…ipo siku tulikwenda na docta akachukua vipimo vyangu, lakini hakuweza kunipa majibu siku hiyo, ilihitajia muda wa kuvifanyia kazi…na ikawa kila nikimpigia simu anasema nisubirie..nikajua hakuna jipya.

 Na ndio yakaanza kutokea haya ya huyu binti, kuumwa, na hata kwenda kwao..nielewe hapo kidogo, kuwa haili ilivyo, hata docta asingeliweza kunitetea…’akatulia.

*************
Sasa huyu binti alipofika kwao ilikuwaje…!
Huyo binti alipofika kwao, akapokelewa kwa vigelegele..hata mwenyewe alishangaa, kumbe alishaandaliwa kama mtarajiwa wa kuolewa,

Kumbe wazee, akina….baba mama, mashangazi walishapitisha kuwa huyu binti anaolewa na nani,….kumbe watu walishaleta hadi mahari, uone ilivyo kuwa ngumu..ngombe nyingi tu, zilishapokelewa, na muoaji keshapitishwa ni nani..

Sasa ndio binti anafika nyumbani akiwa kebeba taarifa yangu, na taarifa yenyewe ya mikono mitupu,.. eti mie namtaka kumuoa binti yao, unajua hata binti mwenyewe awali, aliogoapa kabisa kuliongelea hilo…Ataanzaje..

Alipoanza kuelezewa kuhusu hizo posa na sifa za muaoji,…akataka kujitetea,  akasema yeye kwa hivi sasa hataki kuolewa..na hilo swala limekuwa kwake la kushitukiziwa, anahitajia muda wa kuliwazia, hata huyo bwana mwenyewe hajawahi kuongea naye….

‘Kwanini, ina maana hutuamini sisi wazazi wako….?’akauliza na hakusema moja kwa moja, kunihusu mimi,  

‘Au labda umeshapata mwanaume mwingine, maana nyie mabinti wa siku hizi, mnajiamulia tu,…na badala ya hata mwanaume kuja kujitambulisha nyie ndio mnajitambulisha wenyewe kuwa mna wachumba…’akasema mjomba.

‘Hawezi kutuangisha binti yetu, mimi ni imani hawezi kutukataliwa chaguo letu,….’akasema shangazi.

‘Haya mnataka apewe muda gani, eti binti tukupe muda gani kuamua…?’ akaulizwa.

‘Naombeni hata mwezi….’akasema.

‘Haiwezekani, tunataka kauli yako hii leo,..labda unaona aibu kutuambia hapa,haya nenda ukaonge na shangazi yako faraghani na mama yako …’akaambiwa

Kweli ikabidi watoke na shaangazi, na mama kwenda kuongea faragha, na huko binti akaanza kuonywa, na kwa maneno makali ,..kuwa asije kuikataa hiyo ndoa, maana ina umhyimu mkubwa.

Binti akaona autumie mwanya huo kujieleza.

‘Eti nini unasema nini,  wewe binti mbona una hatari, unataka kutuletea mtihani gani huo,..huyo mtu hatakiwi, na unakumbuka, alikuwa haelewani hata na mkewe, mpaka anafariki, sasa unakuja na hoja, hiyo,..sisi hilo hatuwezi kabisa kuliongelea….’wakasema lakini binti aliposisitiza, ikabidi akina mama hao kuja kutoa taarifa kwenye kikao.

Wazee waliposikia hilo, walipandisha zile mori za kiasili,….baadaye mjomba akatuliza kikao na kusema;

‘Tulijua tu…wewe umekaa na huyo muhuni huko mjini, kakughilibu akili yako...na nyie watu hivi kwanini mlimruhusu huyu binti  mwenye maadili yetu aende kuishi na huyo muhini huko mjini, mnaona madhara yake haya…’akasema mjomba

‘Au ni kwa vile nilisikia kuwa huyo mwanaume anaumwa, hawezi kazi…au…?’akauliza mjomba kwa hasira na baba akawa kainamisha kichwa chini tu kwa aibu…huku akitamani kumrarua binti yake mbele ya kikao.

‘Hivi nyie watu kwanini mkamruhusu….’wakaulizwa tena wazazi.

‘Lakini kaka, hebu kwanza tumsikilize mwanetu, unajua yeye ndiye anatarajia kuishi na mumewe..hatujui ni kwanini akafikia uamuzi huo…lazima ana sababu za msingi , mnamfahamu vyema huyu  binti yetu, hawezi kutuabisha…’akasema mama

‘Haya atuambie tumsikie..au labda keshapachika mimba ..tuambie sasa…’akasema baba sasa.

‘Atapachikwaje mimba, wakati tunasikia huyo mwanaume, jogoo haliwiki, au ilikuwa uwongo,e…hapo tena labda mumsingizie….’akasema shangazi kwa mdhaha.

‘Sasa huyu binti ana sababu gani, atuambie la sivyo, asubirie maamuzi yetu, msimbembeleze huyu, hawa mabinti mkiwaachia mwisho wa siku aibu ni zetu..haya tuambie…’akasema mjomba

Binti alikaa kimia, hakujua hata aanzie wapi, na baba akasema;

‘Mimi naona tuchukua uamuzi wetu,  maana huyu binti anataka kutuabisha, hapa kijijini wamekuwa wakituongelea vibaya, wanatudharau,yote haya ni sababu ya mama yake, eti anamuheshimu marehemu, marehemu hayupo, …’sasa akajitetea baba.

‘Usimlaumu mkeo, kama ni makosa haya ni yenu wote….’akasema mjomba.

‘Sasa sikiliza wewe binti…, sisi kwa pamoja, tumeamua utaolewa na huyo mtu wetu tuliyemuona anakufaa, nay eye anatoka kwenye familia tunayoifahamu sisi…’akasema baba, hapo binti akaamua kufungua mdomo, na kusema;

‘Baba,..na wazazi wangu kwa ujumla… naombeni sana, mnisikilize na mimi… wazazi wangu mimi sitaki kuwakatalia mawazo yenu na maamuzi yenu, nawajali sana wazazi wangu, lakini hebu rejeeni nyuma, mkumbuke mema mangapi aliyowahi kuwafanyia marehemu..mumeshasahau hayo jamani….ni nani aliwasaidia hata kufikia kuwajengea hiki kibanda, mumeshamsahau kwa vile hayupo duniani…’akasema binti

‘Hayo yana maana gani kwetu, yanahusiana nini na maamuzi yetu…?’ akauliza shangazi.

‘Ndio…yana maana kubwa sana…, ili mfahamu ni kwanini nikakubali huyo mwanaume anioe….’akasema binti.

‘Hakuna kitu kama hicho,..usituletee uhuni hapa,….haya elezea, inahusianaje na hili….?’ Akauliza mjomba.

‘Marehemu hatuna ubaya naye, sisi ubaya wetu ni kwa huyo mume wake, mume ambaye alimtenda sana mke wake, kila mtu anazifahamu sifa zake, japokuwa mkewe hakutaka kumtangaza ubaya wake....’akasema shangazi.

‘Na hata yeye mwenyewe unamafahamu sana,  umeshasahau alichotaka kukufanyia kipindi kile,..ukaapa kuwa hutarudi tena kwake..unakumbuka,..huyo kawafanyia mangapi mabinti wa wenzake..ni mume gani huyo, unataka kutuletea mbegu mbaya kwenye kizazi chetu…wewe hujui tu..tabia nyingine mbaya hurithiwa…’akasema baba.

‘Baba huyo mnaye mzungumzia nyie alikuwa mwingine, huyu wa sasa ni tofauti baba, huyu wa sasa ni mcha mungu wa kweli, kabadilika kabisa…, alichokifanya sio rahisi mtu wa kawaida kukifanya, …niulizeni mimi niliyeishi naye hapo nyumbani..wazazi wangu nilichotaka kuwaambia ni kuwa, marehemu ndiye yeye mwenyewe aliacha usia kuwa mimi nije kuolewe na huyu mtu…’hatimaye binti akapasua ukweli.

‘Eti nini…marehemu aliwahi kukuambia hivyo….hapana kama ni watu wamekuambia hivyo, wao wamekudanganya, yule mtoto haweze kumchuuza mwenzake, mfupa ulimshinda yeye kwanini amtupie mwenzake, hana tabia hiyo, usimsingizie …’akasema mama.

‘ Ni kweli mama, ..hakuwahi kuniambia mimi moja kwa moja..lakini aliacha usia huo kwa watu , na hao watu ni watu kuaminika, na wao ndio walionishawishi mimi, sasa je mnataka nimkane marehemu…., nikiuke usia wake, mtu tuliyemuona kama ndugu yetu, nilimpenda sana, na niliahsi kumfanyia chochote….’akasema binti kwa sauti ya kusikitika.

‘Oh…unaona ulivyoghilibiwa, yeye mwenyewe mfupa ulimshinda, au sio… sasa anataka na wewe ukautafune , wewe una meno gani, kwanza hebu tuulize sisi wazazi wako kwanini hatutaki wewe uolewe naye,…tuulize, tunasababu za msingi…’akasema mjomba akiwaangalia baba na mama.

‘Je una hakika gani kuwa marehemu alitoa kauli hiyo, kuwa yeye akifariki uje kuolewa na mumewe,,..?’ akauliza baba akionyesha kushitushwa sana na kauli hiyo, na ilionekana imemgusa.

‘Ndio baba…ushahidi na mashahidi wapo…mimi sikukubali tu …..’akasema binti

‘Lakini sasa utaolewaje na mtu mgonjwa, si unafahamu matatizo yeka, au unataka kwenda kuwa mfanyakazi wake tu..hutaki kizazi…au ndio mumeshapimana huko maana nyie vijana wa siku hizi ni hatari, mnajiingiza kwenye mambo makubwa kabla ya umri wenu…?’ akaulizwa shangazi.

‘Ngojeni kwanza…, unasema una ushahidi na mashahidi…eeh, hebu tumuache atupe huo ushahidi na mashahidi,… lakini hayo,  hayawezi kubadili msimamo wetu maana tulishakubali, unatuelewa, haya elezea huo upuuzi wako….’akasema baba.

NB: Naona hitimisho litakuwa na sehemu mbili, tuwe na subira, tuone sehemu ya pili itakuwaje, je binti atakubaliwa , …ukumbuke wazazi wameshapokea mahari….


WAZO LA LEO:  Wakati mwingine ni muhimu kuwasikiliza watoto wetu, hasa inapofikia sehemu ya kuchagua ni nani anayefaa kuwa mwenza wa maisha. Yawezekana, ikawa ni  heri kwa wawili hao, yawezekana mwenza aliyemuona yeye akawa ni mwenza mwema, lakini ni muhimu, wazee kufanya uchunguzi wa kina, tusikimbilie kuangalia mali, mahari, na utajiri tu wa mwenza wa watoto wetu, tuangalie yake  mambo ya msingi, maana, ndoa ndio chimbuko la kizazi chema, ndoa ni sababu ya jamii njema , tukiharibu hapo, tumeiharibu jamii.
Ni mimi: emu-three

No comments :