Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, December 30, 2016

KISA CHA BINTI YATIMA-4


 Baba alifariki akiwa kawaacha mama na bibi hawana kitu, ni kama vile alikufa baada ya kuhakikisha kile alichowahi kukichuma kwa mikono yake, kiwe hakipo tena duniani,…hata umaarufu wake ulishapotea, ilibakia historia ya kufaninishwa na mabaya yake tu.

Na ndio maana hata baba alipofariki, mazishi yake..licha ya kuwa aliwahi kuwa kiongozi mwenye nyadhifa, yalikuwa ni ya kawaida tu, walihudhuria watu wachache…hakuna viongozi wanaomfahamu waliwahi kufika….

Sasa maajabu ya walimwengu, yalitokea siku ya kutangaza mirathi,….

Tuendelee na kisa chetu…

*********

 Wakati baba anaumwa, watu hawakuonekana, lakini cha ajabu baba alipozikwa, ikawa na siku ya kutangaza mirathi, watu walipotokea huamini, kumbe baba alikuwa na watoto wa nje, hawakujulikana, walijulikana siku hiyo, na wao wanataka mirathi!

Watu wakaanza kupigana…maana walitarajia baba, kaacha mali nyingi, wanandugu wakaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe, ….baadaye wakamgeukia mama, na kuanza kumsakama kuwa eti kapeleka mali kwao, au kauza..yaani ikawa ni fujo mtindo mmoja..mama atasema nini, yeye analia tu!

Kwa bahati kulikuwa na baadhi ya maeneo yalibakia, viwanja na mashamba, hivyo ikabidi wanandugu waanze  kunyang’anyana, kila mmoja akidai apate sehemu, hapo hawakujali kuwa kuna mjane, au watoto hao wa nje…hawakuli kuwa mama mjane ana mtoto mchanga,…wakati huo mimi ni mtoto mchanga,, hayo alikuwa akinisimulia bibi ilivyokuwa,…bibi anasema mimi hata mwaka bado.

Basi wao bila hata kujali hayo wakaanza kugawana mali mashamba yote wakachukua, hata hicho kibanda, walichokuwa wakiishi bibi na mama walitaka kukichukua, lakini mzee wao mmoja akaingilia kati na kukataza, wao walisema wanawapa muda mama na bibi watafute sehemu, siku yoyote watakuja kuwafukuza….na waliokuwa wakiongoza hayo yote ni wanaume….usione ni kwanini nasema nawachukia…

Mama aliambiwa wazi wazi kuwa hana chake…maana yeye ndiye kamuua mumewe…akishirikiana na bibi,…shutuma zikaanzia hapo…maneno yakakuzwa, na mama akaanza kunyoshewa kidole,…, ilibidi hilo nalo wazee wengine na wakuu wa dini, waliingilie kati maana ilishafikia wakati mgumu, na mama na bibi wakabakia hapo kwenye kibanda wakiishi kwa mashaka, na..unafikiri kibanda chenyewe ni kibanda hasa..we acha tu. Baba alikuwa kauza nyumba zote nzuri.

Siku moja mama akiwa shambani , ..walikuwa na sehemu nyingine ya shamba, ilikuwa sio ya familia, mama alipewa tu na jamaa zake, wanandugu wakawa wakimfuatilia mama,…na siku hiyo walipogundua mama yupo peke yake shambani,  wanandugu wa mume wakamfuata huko huko shambani,..wakaanzisha fujo,, waanza kumpiga mama, walimpiga wee, mpaka hamu yao ikaisha, na mama akapoteza fahamu.

Bibi yeye siku hiyo alibakia nyumbani, alikuwa hajisikii vyema, ikafika jioni hamuoni mama akirudi, ikabidi aanze kufuatilia, ilishafika usiku sasa, bibi anaumwa, lakini mwanae haonekani atafanya nini, mimi kanibeba mgongoni,….akaanza kazi ya kumtafuta mama, akaelekea huko shambani,…na alipofika hakumuona mama, kumbe walimtupa kwenye bonde.

Wakati bibi kakata tamaa, mara akasikia mbwa akibweka,…ndio akafuatilia, na hapo akamkuta mama kalala, hajitambui, akapiga ukelele, watu wasamaria mwema wakafika,…ilikuwa ni bahati tu….vinginevyo mama angeliwa na fisi, kwani walishaanza kumsogelea.

Walimbeba hadi nyumbani akiwa hajitambui, bibi akawa anaomba watu wamsaidie wamfikishe hospitalini. Watu, walishajengewa fitina, hakuna aliyekubali, waondoka zao , bibi afanye nini, mgongoni ana mtoto, mwanae anaumwa, kumbeba hawezi, akabakia kulia.

Kwasabbabu ilikuwa usiku tena, bibi akatafuta majani ya miti shamba anayoyafahamu akamkanda kanda mwane, hadi asubuhi, na asubuhi na mapema, bibi akaenda kwa mjumbe, ili apate msaada, na hapo akapata msaada mama akapelekwa hospitalini. Huko akapimwa akaonekana kavunjika mbavu.

Haya matibabu yanahitajia pesa, bibi hana kitu...bibi hana pesa..., ikawa dana dana, mara inahitajika damu, na ni nani wa kutoa damu....Bibi akawa anatembea huku na kule kuomba, ..ni nani atamsikiliza, mama akawa anateseka tu, hakuna cha maana kinachofanyika,…

Siku zikawa zinakwenda mama  hali yake ikazidi kuwa mbaya, bibi anapita mitaani akiomba, akilia kama mtoto, na alikwua radhi hata kuuza hicho kibanda, ni nani atakinunua,,…basi tena, hapo apo hospitali, wakamtibia walivyoweza, lakini hali ya mama ikazidi kuwa mbaya, akawa sasa hata kuinuka kitandani hawazi…

Baadaye sana, hapo hospitalini wakashauri mama apelekwe hospiali kubwa zaidi..ikawa haina jinsi , na wao wenyewe walikuwa na gari la bosi wao, siku hiyo hiyo alikuwa akienda huko mjini, ndio wakamchukua na mama...sasa, huko ndio wakagundua makubwa,  kumbe mama pamoja na matatizo hayo pia alikuwa kaathirika…

‘Unaona..yote ni haya ni sababu ya nani…..ni baba, kumbe baba alimuachia mama ugonjwa huo...baba hakuwahi kusema,… na ilipogundulikana kuwa mama ameathirika, kibao kikageuzwa kuwa mama ndiye alimuambukiza baba,….’ akatikisa kichwa.

‘Nyie wanaume nyie,….’akasema msimuliaji.

‘Watu walisahau kabisa tabia aliyokuwa nayo baba…kuwa baba alikuwa hakimpiti, aliwabadilisha wanawake kama nguo, …na kumbe alikuwa keshapima, akajijua kuwa anao! Lakini hakuwahi kumwambia mtu, ilikuwa ni siri yake...

Sasa mama alipopimwa na kugundulikana kuwa kaathirika, mzigo wote anatupiwa yeye, sasa yeye ndiye anasingiziwa kuwa ndiye alimuambukiza baba..na haikuishia hapo watu wakaendelea na maneno yao ya fitina kuwa wao ndio walimloga baba, wakishirikiana na bibi....yote hayo ya ugonjwa ni njia tu…

'Huo ugonjwa ni visingizio tu...' wakawa wanasema.

Basi ikawa na shutuma nzito, fitina, uzushi...ukasambazwa hapo kijiji, mpaka watu wakaanza kuamini hivyo, na ikafikia hatua mama na bibi wakatengwa, hakuna mtu anayekuja kuwaona, na bibi akitoka kwenda sokoni, au dukani,  kununua kitu, wauzaji wengine wanakataa kumuuzia, inabidi waende mbali zaidi,…

Na hali ya mama ikawa inazidi kuwa mbaya sana, bibi anasema mama alikonda sana, wanasema alikuwa kama fito,..madonda yakawa yanamtokea mwilini,... akabadilika sura kabisa, na kila aliyefika akamuona kwa bahati mbaya, hawamuangalii mara mbili, muuguzaji wake ni bibi, nani kama mama, na walimwengu wanazidi kujenga fitina, wakisema,…

'Huyo anateseka kwasababu ya dhambi zake, si alimuua mumewe, ngoja na yeye aipate....'

Basi siku ya mama nayo ikafika, akafariki dunia…na siku hiyo anafariki bibi alikuwa kaenda kumtafutia dawa, ilikuwa dawa ya bei mbaya, bibi alitumia kila alivyoweza kuipata hiyo dawa, ndio anafika hospitalini, akiwa na hiyo dawa , anajua sasa mtoto wake atapona,...

Ile anafika kitandani anakuta kweupe...

'Binti yangu yupo wapi...?' akauliza

Ilibidi madocta watumie hekima kumwambia....na palikuwa hapatishi, bibi hakuamini, akawa anataka kumuona mwanae, ndio akapelekwa chumba cha maiti, akaonyeshwa....

Bibi alilia mpaka akazimia,...japokuwa mama alikuwa kaisha sana, ..lakini bibi alikuwa na matumaini ipo siku mwanae atapona, hakuwa amekata tamaa, na alisema  kuwepo kwa binti yake japokuwa anaumwa, lakini ilikuwa ni faraja, ...sasa ndio huyo bintii yake keshaondoka, kamuachia mtoto mdogo, hapo nilishafikisha miaka miwili hivi...

Ni ni nani wa kuja kumliwaza bibi...bibi anasema mimi japokuwa nilikuwa mdogo, lakini ndiye nilikuwa nikimliwaza,...najua nini hapo,...wakati mwingine namuuliza bibi unalia, nini...hapo bibi ndio anazidi kulia,..

 Haya msiba umekwisha….bibi hana mbele wa nyuma..shamba lile walilokuwa wakilima, mazao kumbe walikuja wakachoma moto...kulikuwa na migomba na mihogo, yote ikateketezwa...

Haikuishia hapo watu wakaanza kutoa vitisho kuwa ni lazima na bibi aiage dunia...

'Huyo ni mwanga lazima aondoke, ni lazima amalizwe....'vijana wakawa wanapita mitaani wakisema

Sasa bibi akawa anaishi kwa mashaka, anaogopa hata kutoka nje, watu wanamnyoshea kidole,..mwanga mwanga.... Haijapita muda, kukasikika minong'ono kuwa watu wamejipanga usiku huo kuja hapo nyumbani kuchoma nyumba moto…wamuangamize na bibi,

'Mungu wangu sasa nitafanya nini na hiki kiumba cha watu...'bibi akawa anahangaika, na wazo likamjia, bora ahame hapo usiku huo na mapema, Bibi alisema;

'Isingelikuwa ni wewe mjukuu wangu, nilikuwa radhi nibakie hapo wanieu tu, kwani nina thamani gani tena, lakini niliogopa watakuja kutuangamiza wote wawili, na mimi nilipata kuja kukulea hadi sikuyangu ya mwisho....ndio maana usiku huo nikaamua kuhama hicho kijiji na kwenda kuishi kijiji cha mbali...lakini haikuwa kazi rahisi...

 Bibi anasema wakati tunatoka huo usiku,.. kumbe kuna vijana walikuwa wakipita pita, walituona, wakaenda kutoa taarifa kwa hicho kikundi kilichokuwa kimejipanga kuja kutuangamiza na usiku huo wakaitana kwa haraka...

NB: Ngoja tuishie hapo kwa leo, ilikuwa nawashitua kidogo, kuwa kisa hiki bado kipo.

WAZO LA LEO: Fitina ni mbaya sana… na fitina hutokana na ulimi, watu hujenga hoja zisizokuwa na ukweli, nia ni kuangamiza wenzao. Ole wao, wanautumia ulimi wao mbaya, maana siku hiyo ya mwisho, kiwili wili hicho kitakuwa ni shahidi.

Tumuombe mola atusaidie, awasaidie wazee wetu wanaoteseka huko vijijini, wengine wanateseka kwasababu ya fitina mbaya tu…wengine wanateseka kwasababu ya hali mbaya za kiuchumi, au maradhi nk…yote hii ni mitihani. Tunakuomba uwasaidie wazee wetu hao, maana uzee nao ni mateso, hasa ukiwa huna msaada wowote.
Pia tunakuomba uwajalia makazi mema peponi wazee wetu na wale wote waliotangulia mbele za haki . AMYNI.


NB: Ni kutokana na maombi ya wengi, inabidi tukiendeleze kisa hiki, sio kirefu sana, tuwe pamoja.

Ni mimi: emu-three

No comments :